Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Selemani Jumanne Zedi

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri na moja kwa moja nitaanza na mitandao ya simu katika maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kubaini kwamba, makampuni ya simu za mikononi yamekuwa reluctant kujenga minara katika maeneo ya vijijini kwa sababu maeneo hayo hayana mvuto wa kibiashara Serikali kwa nia njema kabisa iliamua kuanzisha Mfuko Maalum wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili uweze kutumia fedha za mfuko huo kujenga minara katika maeneo ya vijijini. Lakini mpaka sasa nimeona kuna jitihada fulani zimefanyika, lakini bado maeneo mengi ya vijijini hayana huduma hii muhimu ya simu za mikononi. Mimi mwenyewe kwenye jimbo langu katika huu mfumo wa UCSAF ni kata za Isagehe na Semembela na Kamahalanga ndizo ambazo ujenzi wa minara ya simu umeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ombi langu kwa Serikali ni kwamba, kwa kuwa bado makampuni haya ya simu ya Airtel, Vodacom na Tigo tukiyaachia yenyewe yajenge minara kwenye maeneo ya vijijini hayataweza kufanya hivyo kwa sababu, hakuna mvuto wa kibishara. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwenye maeneo mengi ya Vijijini bado mfuko huu wa UCSAF utalazimika kujena minara hata kwa kutoa ruzuku kwa asilimia mia moja. Tukiyaachia haya makampuni ya simu hayataweza kujenga kwa sababu maeneo hayo mengi hayana mvuto wa kibiashara na makampuni haya motive yake kubwa ni faida tu hayataweza kwenda huko. Kwa hiyo, tunahitaji mfuko wa UCSAF ujenge minara maeneo ya vijijini, maeneo mengine uwe tayari kujenga hata kwa asilimia mia moja kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu tatizo la upelekaji wa fedha katika Halmashauri zetu za Wilaya hasa Mfuko wa Barabara na fedha za ruzuku (LGCDD), ili kuhudumia barabara ambazo zinahudumiwa na Halmashauri za Wilaya. Kuna tatizo kubwa sana la kwamba fedha tunazopanga kwenda kuhudumia barabara zetu za Halmashauri mwisho wa mwaka unapofika ni asilimia ndogo mno ya fedha inakuwa imekwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Nzega, mwaka 2014/2015 kwenye Mfuko wa Barabara tulitenga takribani milioni 700 kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Nzega inamtandao wa barabara wa karibu kilometa mia sita na kitu. Kwa hiyo, tulitenga na tulipanga shilingi milioni 700 ziende kuhudumia barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, lakini mpaka mwisho wa mwaka unafika ni shilingi milioni 300 tu zilikuwa zimekwenda na hivyo kufanya barabara nyingi kukosa huduma. Lakini hali ilikuwa mbaya sana kwenye mfuko wa LGCDD ambako tulipanga zipelekwe shilingi milioni 700, lakini mpaka mwaka unaisha ni shilingi milioni 49 tu zilikuwa zimekwenda kwa hiyo…
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono hoja na tulikubaliana na Mheshimiwa Mwakasaka atamalizia dakika tano nyingine, asante sana.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi jioni ya leo niweze kuchangia mjadala huu ambao uko mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza kwenye maeneo kadhaa ambayo ningependa nitoe mchango kuhusu hotuba ya mapendekezo ya bajeti iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango. Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua vizuri sana kwa kuja na nguvu sana katika eneo la kudhibiti ubadhirifu katika matumizi ya fedha za umma na mimi naunga mkono kabisa kwa sababu ni jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kupitia hotuba ya mapendekezo ya Waziri wa Fedha nimeona kuna contradiction ya ajabu. Kwa sababu huwezi kupambana na ubadhirifu wa matumizi ya fedha za umma kwa kauli tu za kisiasa. Ni lazima uwe na vitendo ambavyo kweli vitapelekea kupambana na ubadhirifu huu wa fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna taasisi muhimu ya kimkakati katika kupambana na ubadhirifu wa fedha za umma basi taasisi hiyo ni Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaani CAG. Contradiction ninayoisema ni kwamba kwa upande mwingine Serikali inasema tumedhamiria kupambana na ubadhirifu wa matumizi ya fedha za umma, lakini kwa upande mwingine taasisi ambayo ndiyo taasisi ya mkakati, ndiyo hasa kiini, ndiyo key institute katika kupambana na ubadhirifu ambayo ni CAG imepangiwa fedha ambayo kwa kweli haiwezi kabisa kutimiza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii tunayokwenda nayo ambayo inakwisha mwezi huu wa Sita ni bajeti ya shilingi trilioni 22. Katika bajeti hii CAG tumemtengea shilingi bilioni 74 ili kukagua shilingi trilioni 22. Bajeti hii ambayo tunaijadili sasa ni ya shilingi trilioni 29 lakini CAG tumempangia shilingi bilioni 44 tu. Huu ndiyo nauita mkanganyiko na contradiction ya ajabu kwa sababu kwenye bajeti ya shilingi trilioni 22 CAG tumempa shilingi bilioni 74 kwa ajili ya kukagua lakini kwenye bajeti ya shilingi trilioni 29 ambapo kuna ongezeko la shilingi trilioni saba tumepunguza hela ya kumwezesha kukagua sasa tunategemea nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwangu mimi hii ni contradiction na naona kabisa kama hatutafanya chochote, basi kauli za kusema tumejipanga kupambana na ubadhirifu ni kauli tu za kisiasa na ambazo hatutafikia matokeo tunayotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuchangia, nimeangalia katika hotuba Mheshimiwa Waziri wa Fedha amependekeza kufuta utaratibu wa retention kwenye taasisi za Serikali ambazo kimsingi zilikuwa zinaruhusiwa kubakiza fedha ambazo zinakusanywa ili ziweze kutekeleza majukumu yake. Mojawapo kati ya taasisi hizo ni Shirika la Maendeleo la Petrol (TPDC).
Mheshimiwa Naibu Spika, sipingani na wazo la kufuta retention, lakini angalizo ninalolitoa ni kwamba, kuna taasisi nyingine muhimu, ni taasisi za kimkakati kwa mfano TPDC. Najaribu ku-imagine endapo Wizara ya Fedha kupitia Hazina itakapotekeleza agizo la kutoruhusu TPDC kuwa na retention ikachukua fedha zote ambazo TPDC inakusanya ikazipeleka Mfuko Mkuu wa Serikali halafu ikashindwa au ikachelewesha kupeleka fedha TPDC kwa mujibu wa bajeti yake na ikaifanya TPDC ikashindwa kufanya baadhi ya majukumu, nakuhakikishia tutapoteza fedha nyingi kuliko ambazo tunadhani tutaziokoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TPDC ndiyo jicho la Serikali kwenye shughuli zote za gesi. Sasa hivi tumefanikiwa kugundua kiasi kikubwa sana cha gesi lakini walio kwenye biashara ya gesi wote ni wawekezaji binafsi na TPDC ndiyo mbia ambaye anasimamia kwa upande wa Serikali. Moja kati ya kazi zake ni kufanya ukaguzi wa shughuli zinazofanywa na wawekezaji wa gesi ili kujua mapato wanayopata na kujua mgao wa Serikali kama ni sahihi. Kwa hiyo, TPDC wasipokuwa na fedha za kufanya kazi hii, nakuhakikishia tutapigwa bao na hao wawekezaji wa gesi, fedha nyingi sana zitachukuliwa na lile lengo letu la kusema kwamba eti wasibaki na retention ili Serikali iweze kupata fedha nyingi halitafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuwe makini na angalizo langu hapa ni kwamba, tuhakikishe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kupitia Hazina upelekaji (disbursement) wa fedha kwenye taasisi kwa kweli ni jambo ambalo lisije likawa kama utaratibu ulivyo sasa kwa sababu tutaingia kwenye athari kubwa kuliko ambavyo tunatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda nichangie ni suala la value for money kwa miradi ambayo imekamilika. Kuna miradi mingi nchini kwetu ambayo imekamilika lakini haijaweza kuleta manufaa kwa wananchi kama ambavyo imetarajiwa. Kuna maeneo mengi utakuta madaraja, miradi ya umwagiliaji mabilioni yametumika lakini haifanyi kazi kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu mimi Serikali imetumia fedha nyingi sana kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika wameweza kujenga zahanati za kisasa katika Kata ya Itobo na Tarafa ya Bukene na wameweza kufunga vifaa vya kisasa vya upasuaji. Hata hivyo, sasa hivi ni karibu mwaka mzima umepita majengo ya kisasa yamekamilika, vifaa vya kisasa vya upasuaji vimefungwa huduma za upasuaji hazijaweza kuanza kufanyika. Kwa hiyo, mabilioni yametumika lakini wananchi hawanufaiki chochote na mabilioni hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna haja ya Serikali kujipanga kupitia Wizara ya Fedha na Wizara husika kuhakikisha kwamba pale ambako tumewekeza fedha nyingi na miradi imekamilika, ifanye kazi sasa wananchi waweze ku-enjoy matunda hayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kushirikiana na Mheshimiwa Waziri wa Afya na TAMISEMI, naomba kabisa kupata suluhisho kuhusu huduma za upasuaji katika vituo vya afya vya Itobo na Bukene ambapo fedha nyingi zimetumika, huduma hii ianze kutolewa, ni mwaka sasa. Vifaa vilivyofungwa vinakaribia kuanza kuota kutu na mabilioni ya fedha yametumika, hatuwezi kukubali hali kama hiyo. Hivyo, nashauri huduma ya upasuaji iweze kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa niliwekee mkazo ni suala la upelekaji wa umeme REA III. Hili ni muhimu sana, nimeona Serikali imetenga fedha za kutosha na nina imani kwa namna ambavyo Wizara ya Nishati na Madini imejipanga na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara kule maeneo ya kwetu na aliongozana na mkandarasi na kuhimiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika baadhi ya maeneo matunda yameanza kuonekana na nina uhakika miradi ambayo iko katika REA awamu ya III itatekelezeka na wananchi waweze kupata manufaa. Kama tunataka kukuza ajira hasa maeneo ya vijijini basi umeme vijijini ni lazima uwepo kwa ajili ya shughuli za kusindika mazao ya kilimo ili yaweze kuongezewa thamani na yaweze kuuzwa sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.

The Access to Information Bill, 2016

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwa na afya njema ili nami nipate nafasi ya kuchangia Muswada huu muhimu sana wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa (The Access to Information Act) ya 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imeshasemwa Ibara ya 18(d) ya Katiba yetu inatoa haki ya wananchi wote wa Tanzania kupata taarifa. Haki hii imekuwa haitekelezeki au haipatikani vizuri kwa sababu tumekuwa hatuna sheria ambayo kimsingi ndiyo inapaswa sasa kuwalazimisha watoa taarifa kuweza kutoa taarifa hizo kwa wananchi. Jamii yetu tumedhamiria kutengeneza jamii na nchi ambayo inaheshimu misingi ya uwazi na uwajibikaji.
Mheshimiwa mwenyekiti, huwezi kuwa na jamii inayoheshimu misingi ya uwazi na uwajibikaji kama ndani ya jamii hiyo upatikanaji wa taarifa unakuwa haupo. Kwa hiyo, muswada huu wa sheria ni muafaka kabisa, umekuja kwa wakati unaohitajika kabisa ili sasa upatikanaji wa taarifa uwe ni jambo ambalo ni la lazima. Kwa hiyo, itatupelekea sasa kutimiza azma yetu ya kujenga jamii na nchi ambayo inaheshimu misingi ya uwazi na uwajibikaji.Ukiangalia muswada huu katika kifungu cha 9(1)(b) ndiyo kifungu ambacho sasa kinatoa namna ambavyo sasa sheria hii itaanza kutekelezwa. Kifungu hiki kimetoa utaratibu ambao unamtaka mmiliki wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu kwamba tuna taasisi za umma nyingi; kuna Wizara, Mashirika, Halmashauri na hata taasisi binafsi ambazo zina maslahi ya umma. Tunafahamu kwamba majukumu ya taasisi hizi yamepishana na kwa hiyo, taarifa zitazopatikana kutoka kwenye taasisi moja na taasisi nyingine kwa vyovyote vile lazima zitatofautiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kifungu hiki cha muswada huu wa sheria kinamtaka mmiliki wa taarifa ambaye ni Mkuu wa Taasisi au Wizara au Shirika au Taasisi yoyote ndani ya miezi 36 baada ya kupitishwa kwa sheria hii kuandaa orodha ya taarifa ambazo zinaweza kupatikana ndani ya Taasisi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano zuri ni TAMISEMI - Makao Makuu ambao wameandaa Client Service Charter ambayo inaonyesha taarifa zote ambazo unaweza ukazipata ukienda kuziomba kutoka TAMISEMI - Makao Makuu na wamekwenda zaidi mpaka kutoa muda ambao taarifa fulani unaweza kuipata ndani ya wiki mbili, taarifa fulani ndani ya wiki moja, taarifa fulani ndani siku mbili na taarifa fulani ndani ya siku moja. Kwa hiyo, kifungu cha 9 cha muswada huu ndicho hasa kimetoa wajibu kwa wamiliki wa taarifa wote ndani ya miezi 36 tangu sheria kupitishwa kuandaa orodha ya taarifa zote zinazoweza kupatikana ndani ya taasisi zao ili mwomba taarifa sasa anapokwenda kwenye taasisi aweze clearly kabisa kusema nataka taarifa hii na hivyo atajua kwamba ataweza kuipata kwa muda gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kifungu cha 6, kimeorodhesha taarifa ambazo haziruhusiwi kutolewa. Mimi naungana kabisa na kifungu hiki kwa sababu haiwezekani tukaruhusu taarifa zote za aina yoyote ziweze kutolewa, litakuwa ni jambo ambalo ni hatarishi na hatuwezi kulikubalia. Kifungu hiki kimetoa orodha ya taarifa ambazo zinazuilika na zina mantiki. Kwa mfano, taarifa zote ambazo zikitoka zinapelekea kuhatarisha Usalama wa Taifa, hatuwezi kukubali taarifa hizi zitolewe.
Vilevile kuna taarifa ambazo kama zitatolewa, basi zitapelekea uchumi wa nchi yetu kuhujumiwa. Taarifa hizi zimezuiliwa na hatuwezi kukubali taarifa zinazohujumu uchumi ziweze kuruhusiwa kutolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kifungu hiki kimezuia taarifa ambazo zina mgongano wa kimaslahi wa kibiashara. Kwa hiyo, tunajua madhara yanayoweza kupatikana kama taarifa zenye mgongano mkubwa wa kibiashara kuruhusiwa kutoka. Kwa hiyo, kifungu hiki pia kimezuia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia kifungu hiki cha muswada utaona orodha ndefu ya taarifa ambazo zimezuiliwa zisitoke. Mwisho kifungu hiki cha 6(6) kimetoa adhabu ya mtoa taarifa kama atabainika ametoa taarifa ambayo imezuiliwa kutoka na nakubaliana na kifungu hiki lakini napendekeza marekebisho kidogo kwa sababu kifungu hiki kimetoa adhabu moja ya jumla kwa makosa yote yaliyoorodheshwa, wakati ukiangalia makosa haya yanapishana uzito. Kwa mfano, makosa ya mtu aliyetoa taarifa inayopelekea kuhatarisha usalama wa Taifa na makosa ambayo yanatoa adhabu kwa mtu ambaye ametoa taarifa inayopelekea kuhujumu uchumi wa nchi, ni tofauti kabisa na makosa ya mtu ambaye ametoa taarifa ambayo pengine imeleta tu mgongano wa kibiashara kwa washindani wawili wa kibiashara. Kwa hiyo, Kifungu cha 6(6) kimetoa adhabu moja tu, kwamba wote hawa wakipatikana wataadhibiwa kwenda jela kipindi kisichopungua miaka 15 na kisichozidi miaka 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naona hapa tufanye marekebisho kwamba yale makosa ya mtoa taarifa ambaye anatoa taarifa zinazohatarisha usalama wa Taifa na yule anayetoa taarifa zinazohujumu uchumi, hao wapewe adhabu hiyo ya miaka 15 mpaka 20; lakini wale wengine wanaotoa taarifa zinazopelekea matatizo madogo tu kama mgongano wa kibiashara, kwamba mtu ametoa taarifa ambayo imefanya mshindani wake ajue labda yeye raw material ananunua wapi au analipaje wafanyakazi, kwa hiyo, ameleta mgongano wa kibiashara, kwa hiyo, watu kama hawa adhabu yao napendekeza angalau iwe kifungo kisichopungua miaka mitatu na kisichozidi miaka mitano. Naona siyo sahihi sana hawa nao kuwafunga miaka 20 sawasawa na mtu ambaye ametoa taarifa za kuhujumu uchumi. Kwa hiyo, pendekezo langu hapa ni kwamba adhabu zitofautiane kutokana na uzito wa kosa na siyo kwamba makosa yote yawe na adhabu moja, jambo ambalo naliona kama haliko sahihi.
Kifungu cha 18 cha muswada kinakataza upotoshaji na kimetoa adhabu kwa mtu yeyote atakayepata taarifa halafu akazitumia taarifa hizo kupotosha, basi akibainika afungwe kifungo kisichopungua miaka mitano. Mimi nakubaliana na pendekezo la Muswada huu kwa sababu tukiacha hivi hivi kuna baadhi ya watu ambao watatumia hii kama loophole, hasa baadhi ya waandishi wa habari ambao wanataka kuuza kwenye vyombo vyao, wanaweza wakaenda mahali fulani kuchukua taarifa ambayo ina mlengo fulani lakini wao wakaipotosha ili tu kuuza gazeti au kufanya biashara yoyote. Kwa hiyo, pendekezo la kifungu hiki la kutoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka mitano kwa mtu anayepotosha taarifa, nakiunga mkono kwamba kiendelee kama hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 19 kinatoa fursa kwa mtu aliyeomba taarifa kama amekataliwa kupewa taarifa na haridhiki na sababu za kukataliwa anaruhusiwa kukata rufaa kwa Mkuu wa ile Taasisi ambayo amekwenda kuomba taarifa na pale ambapo bado haridhiki na sababu za huyo Mkuu wa Taasisi kumkatalia kumpa taarifa, basi kifungu hiki kimesema anaweza akakata rufaa kwa Waziri na uamuzi wa Waziri utakuwa wa mwisho.
Napenda hapa tufanye mabadiliko kwamba baada ya huyu mtu kukataliwa kupewa taarifa na Afisa Habari akakata rufaa kwa Mkuu wa Taasisi bado akakataliwa, basi aruhusiwe kwenda mahakamani kupata haki yake ya kupata taarifa kwa sababu tukisema uamuzi wa Waziri utakuwa wa mwisho, inawezekana pengine Waziri akawa na msimamo mmoja na Mkuu wa Taasisi, kwa hiyo, ukakuta mwomba taarifa akakosa haki ya kupata taarifa ambazo anazihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kifungu hiki kitoe ruhusa, kisiishie kwamba Waziri ndio ana mamlaka ya mwisho kumkatalia mtu kupata taarifa. Kifungu hiki kitoe ruhusa kwa mtu ambaye amekataliwa na watu wote hao watatu aweze kwenda mahakamani ili kupata haki yake ya kupata taarifa ambayo yeye anaona ni muhimu na anastahili kuipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeiti, hayo ndiyo yalikuwa mapendekezo yangu, naunga mkono sana muswada huu, umekuja kwa wakati muafaka na utasaidia sana katika kujenga jamii na nchi ambayo inathamini misingi ya uwazi na uwajibikaji. Ahsante sana.

The Legal Aid Bill, 2016

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Muswada huu muhimu sana ambao ni Muswada wa huduma ya msaada wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme naunga mkono Serikali kuleta Muswada huu kwa asilimia mia moja na kwa mtazamo wangu ni kwamba Muswada huu umechelewa sana kuletwa. Ulipaswa kwamba uwe umeshaletwa siku nyingi sana, kwa sababu ni Muswada muhimu sana sana kwa watu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Muswada huu, kwa sababu ni Muswada unaokwenda kusaidia wananchi wetu ambao kimsingi hawana uwezo wa kulipa gharama za mawakili na wanahitaji kupata huduma za kisheria. Pia wote tunafahamu kwamba matatizo ya kisheria ambayo yanaweza kumfanya mtu ajikute yupo mahakamani kwenye mkondo wa kisheria yanaweza kumkuta mtu yeyote yule, bila kujali hali ya kiuchumi, au hali yoyote ile. Pia kuna ushahidi wa kutosha kwamba kuna wananchi wetu wengi tu ambao wamejikuta wanapata matatizo ikiwemo hata kuhukumiwa kufungwa, lakini kimsingi ni kwa sababu tu hawakupata msaada huu muhimu wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kutoa mchango wangu kwa baadhi ya vifungu vya Muswada huu, ambavyo naona inabidi viboreshwe. Muswada huu unakwenda kuwatambua kisheria taasisi ambazo zitakuwa zinatoa huduma za kisheria na ndani ya taasisi hizi kutakuwa na mawakili kutakuwa na wanasheria na kutakuwa na wasaidizi wa kisheria ambao wanaitwa paralegals.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa paralegals wasaidizi wa kisheria sasa hivi tunao lakini Muswada huu ndio unakwenda sasa kuwatambua kisheria na hawa wako maeneo karibu yote ya vijijini, wilaya zote kwenye kata mpaka vijijini, sasa hivi wapo lakini Muswada huu unakwenda kuwatambua kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo naomba liboreshwe kwenye kifungu cha 19 ni sifa za hawa ma-paralegal (wasaidizi wa kisheria) ambao kimsingi wako maeneo yetu ya kata na vijijini kule. Muswada unasema kwamba hawa wasaidizi wa kisheria watakaokuwa wanakaa na wananchi huko vijijini na kimsingi watakuwa wanatoa usaidizi huu wa kisheria bila kuwatoza gharama wale wateja wao wanaohitaji msaada kisheria, sheria inataka wawe na sifa zifuatazo; wawe na degree ya sheria, wawe na diploma ya sheria, wawe na certificate ya sheria.
Mheshimiwa Spika, sipingi vigezo hivi, sipingi wawe na degree, diploma au certificate lakini nilikuwa naomba tuboreshe, kwamba tusibague wale ambao wana elimu chini ya hapo. Kwa mfano watu ambao wana elimu ya kidato cha nne na darasa la saba; kwa sababu katika Kamati tuliita wadau mbalimbali na baadhi ya wadau hawa zilikuwa ni taasisi ambazo tayari sasa hivi zina ma-paralegal, zina hawa wasaidizi wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipata ushuhuda kwamba sasa hivi nchi yetu tuna wasaidizi wa kisheria, hawa ma-paralegal, waonaweza wakafika takribani 9,000 nchi nzima wamesambaa kwenye kata na vijiji, na walio wengi elimu yao ni kidato cha nne na darasa la saba, na kuna maeneo mengine wengine hawakumaliza hata darasa la saba, ilimradi wanajua kusoma na kuandika, lakini pia wamepata mafunzo ya kisheria ya kuwa paralegal.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliweza kupata mfano wa paralegal mmoja, (msaidizi wa kisheria) ambaye alikuwa maeneo ya watu wa kabila la Wahadzabe ambaye aliweza kuwasaidia Wahadzabe wenzake wasiweze kudhulumiwa ardhi na mwekezaji, wakati huyu ni paralegal ambaye amepewa mafunzo na hajakwenda shule hata darasa la saba na kimsingi anajua tu kusoma na kuandika na amepewa mafunzo ya u-paralegal.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mapendekezo yangu hapa ni kwamba sawa wawe na degree, wawe na diploma, wawe na certificate, lakini tusibague wale wa kidato cha nne, wale wa darasa la saba, hata wale wanaojua tu kusoma na kuandika ilimradi katika maeneo yao wanaweza wakapata mafunzo ya kisheria na wakatoa huduma za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukizingatia hawa ma-paralegal (wasaidizi wa kisheria) ni watu ambao wanaishi vijijini na jamii kule kule. Kwa hiyo, tuki-restrict sana, degree na diploma, tunaweza tukawaengua watu muhimu sana ambao wangeweza kusaidia wananchi wetu katika maeneo ya vijijini na maeneo ya kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine ambacho napendekeza mabadiliko ni kifungu cha 27(b). Kifungu hiki kinawapa mamlaka Majaji na Mahakimu kuamua kesi inapokuja mbele yao kuweza kufanya analysis na kuona kwamba huyu mtu anahitaji msaada wa kisheria na kuagiza Msajili amtafutie usaidizi wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napendekeza haki hii ifikishwe pia kwa Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Kata. Kwa sababu watu wetu wa vijijini kule wana mashauri mengi, mengine yanahusu ardhi, migogoro ya ardhi, ambayo hawaendi mahakamani kwanza, wanaenda kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Kata. Kwa hiyo, wale Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi za Vijiji na Kata hata Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya pia sheria hii iwape uwezo wa kuona kwamba shauri hili linahitaji msaada wa kisheria au shauri hili halihitaji msaada wa kisheria. Kwa hiyo, isiishie kwa Majaji na Mahakimu peke yao, bali uwezo huu upelekwe mpaka kwa Wenyaviti wa Mabaraza ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine ambacho napendekeza maboresho ni kifungu cha 49(2). Kama kilivyo sasa kwenye muswada kinasema kwamba baada ya sheria hii kupitishwa na kuwa sheria, wale wote ambao sasa hivi wanatoa huduma ya msaada wa kisheria baada ya miezi 12 wanatakiwa wasimamishe huduma zao waombe upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ikibaki kama ilivyo kuna hatari ya wananchi ambao sasa hivi wanahudumiwa na ambao baada ya miezi 12 kesi zao zitakuwa hazijaisha kukosa haki ya kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu ni kwamba muswada huu wa sheria utambue kwamba wale wote ambao ni taasisi halali zinazotoa legal aid sasa hivi sheria hii mpya izitambue automatically, kwamba waendelee kutambulika na sheria mpya kuwa ni watoa huduma halali wa msaada wa kisheria badala ya kuwaambia kwamba baada ya miezi 12 wajisajili upya kwa sababu kitendo cha kujisajili upya kinaweza kikafanya shughuli zao zisimame na zile kesi walizokuwa wanaendelea nazo ziishie hapo; italeta usumbufu na kukosesha haki wananchi wetu ambao tayari walikuwa na mashauri ambayo yanaendelea kuhudumiwa.
Kwa hiyo, sheria hii mpya iwatambue automatically na waendelee kutoa hizo huduma muhimu za kisheria ambazo wananchi wetu kwa kweli wanazihitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine ambacho napendekeza kifanyiwe maboresho ni kifungu cha 16(3), ambacho kama kilivyo sasa kwenye muswada kinasema kwamba hii taasisi inayotoa msaada wa kisheria ambayo ndani yake kuna Mawakili, kuna Wanasheria, kuna Paralegal ni kwamba mmojawapo kati ya hawa watu, hawa office bearer, aidha awe wakili au mwanasheria au paralegal akifanya kitendo chochote kinachokiuka maadili ya taaluma basi taasisi nzima inafungiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho yangu hapo ni kwamba tuweze kutenganisha makosa ambayo yamefanywa na individual wakili au mwanasheria au Paralegal yasiiadhibu taasisi nzima ikafungiwa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja. Unaweza kukuta taasisi ina mawakili saba, ina wanasheria kumi, ina paralegal 20, kwa hiyo mwanasheria mmoja akifanya kitendo cha kukiuka maadili basi, eti taasisi nzima ifungiwe. Naona halijakaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maboresho yangu hapa ni kwamba, taasisi isifungiwe kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa sababu tu eti wakili mmoja au mwanasheria mmoja au paralegal wa ndani ya taasisi hiyo amefanya kitendo cha kukiuka. Badala yake huyo mtu mmoja ambaye amefanya kitendo hicho yeye ndiye aadhibiwe, kama ni kufukuzwa kazi na hiyo taasisi yake basi yambo hilo lifanyike, lakini taasisi nzima isiadhibiwe kwa kosa la mtu mmoja na tukiruhusu jambo hili litasababisha watu wetu kukosa haki muhimu ambayo tunaihitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla niseme kwamba, sisi ni wawakilishi wa wananchi wa hali zote na tuna wananchi wengi kimsingi ambao kiukweli kabisa hali zao haziwawezeshi kumudu kulipia mawakili na kumudu huduma za kisheria ambazo zinalipiwa kwa gharama. Kwa hiyo, muswada huu lengo lake kubwa ni ku-enhance access to justice kwa watu wasio na uwezo wa kifedha wa kuwalipia mawakili na gharama nyingine za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa vyovyote vile mwakilishi yeyote yule ambaye anawakilisha watu wa aina hii hawezi kupinga muswada huu, atauunga mkono kwa sababu unakwenda kutoa suluhisho la wananchi wake anaowawakilisha ambao kimsingi hawana uwezo wa kulipia mawakili; na sasa hivi Serikali inakuja na programu ambayo watu hawa sasa wataweza kupata huduma hiyo bila kulipia, bila gharama yoyote. Kwa hiyo ni muswada ambao kimsingi unapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote na wawakilishi wote wa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema naunga mkono kwa asilimia mia moja muswada huu, na ninasema muswada huu umechelewa sana, ulipaswa uje siku nyingi sana. Nashukuru sana kwa nafasi hii.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's