Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Bhagwanji Maganlal Meisuria

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MAGANLAL M. BHAGWANJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii kuchangia leo. Kwanza, naomba kuipongeza Serikali kwa kupitia kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Baraza la Mawaziri, kwa kufanya kazi nzuri na kurudisha imani kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali iangalie zaidi kuboresha Utawala Bora, pamoja na jitihada hizo zilizofanywa ni vizuri kuwe na suala la huduma kwa mteja. Itolewe elimu katika ngazi zote, Tume au Sekretarieti ya Utumishi wa Umma iboreshwe ili waweze kufanya kazi ngazi zote Taifa, Mkoa na Wilaya ila zile kazi za kada ya chini zipewe Halmashauri jukumu la kuajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu pia tuwe na Maafisa Mipango zaidi katika ngazi zote, Halmashauri, Kata na Vijiji ili miradi iweze kuibuliwa, pia wakiwemo, katika miradi ya TASAF wananchi wapate fursa ya kuibua miradi yenye manufaa kwao. Pia TAKUKURU isaidie kuondoa kabisa rushwa, kero ndogondogo mfano wa traffic barabarani, vibali vya dhamana, kupata leseni, ni mifano michache. Vile vile kwenye elimu, Serikali iangalie namna ya kuboresha na kukomesha shule na vyuo feki ambavyo havitoi elimu kwa viwango na zisizofuata Kanuni na Utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. BHAGWANJI M. MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushukuru Kiti chako kwa nafasi hii ya kuchangia kwa maandishi katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kujenga Taifa hili kwa falsafa ya “Hapa Kazi Tu” na kwa kweli tunaona kazi inafanyika kweli kweli na wananchi walio wengi wana imani na Serikali ya CCM.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa kumsaidia Rais wa Tanzania kutekeleza majukumu ya Serikali na sasa tunaanza kuona matunda yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa ushindi mkubwa alioupata hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hotuba ya Wizara hii ya Kilimo kwa kuzungumzia mambo machache. Napenda kuishauri Serikali kuweza kuwakusanya vijana wasio na ajira na kuwatengea maeneo maalum ya mashamba na kupewa taaluma ya mifugo, uvuvi na Kilimo na baadaye wapewe mikopo kutoka Benki ili waweze kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naiomba Serikali kujipanga vizuri katika kukabiliana na changamoto zifuatazo:-
(a) Uharibifu mkubwa wa mazingira ya Bahari, Mito na Maziwa; na
(b) Kukabiliana na migogoro mikubwa ya wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Rais na Makamu wake kwa kuchaguliwa kwao na kazi nzuri wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Naibu Spika, kwa ujasiri wake wa kuongoza vikao vyetu ndani ya Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa hotuba yake nzuri yenye mipango yake ya utekelezaji kwa kipindi hiki cha mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee chombo chetu cha habari TBC. Hatuna namna yoyote ya kutosaidia kukihudumia chombo hiki kama Serikali, ni chombo cha Serikali kinachotoa habari za ukweli na uhakika. Isingekuwa vizuri kuona chombo hiki kinashindwa kufanya kazi zake kama ilivyokusudia kwa kukosa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo hiki kinasaidia sana kuitangaza nchi yetu kisiasa, kiutamaduni, kimichezo na mambo mbalimbali ya nchi yetu. Ninaomba Serikali kukisaidia kwa kukipa fedha tena kwa wakati ili katika mambo yanayoendelea katika nchi yetu wananchi wetu wapate kujua taarifa za ukweli na uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ubadhirifu na uvunjwaji wa amani unatokea kwa sababu wananchi wamepata taarifa zisizo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutumbua majipu, kwa hilo hongera sana. Pia naomba kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Spika kwa kazi nzuri anayoifanya na kuliongoza Bunge vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishauri Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwamba zile za nyumba za National Housing Corporation zilizopo Dar es Salaam ambazo zinakodishwa kwa shilingi 370,000 kwa mwezi kwa kweli bei hiyo ni kubwa mno ukilinganisha na kipato cha wananchi kilivyo. Walio wengi hawamiliki fedha hizo na wakati mwingine nyumba hiyo ikiharibika unaambiwa fedha hakuna, inakubidi utekeleze mwenyewe kazi ya matengenezo au upakaji wa rangi. Kwa hiyo, naiomba Wizara hii ipunguze kiwango hicho ili wananchi walio wengi wafaidike asimilia mia.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru nimepata nafasi hii mara ya kwanza. Namshukuru Mwenyezi Mungu, tumejaliwa sote tuko pamoja na Insha Allah Mungu ataleta neema yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Spika wa Bunge pamoja nawe Naibu Spika kwa kazi yako nzuri. Katika Bunge hili mimi ni Baniani peke yangu. Kama nimekosea, mtanisamehe, lakini nitajitahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napongeza Kamati yangu ya Miundombinu, imefanya kazi nzuri kabisa, pamoja nami, nimetembelea bandari, uwanja wa ndege, reli na barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Rais wangu wa Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, yeye amefanya kazi nzuri kabisa katika Tanzania yetu na nchi yetu.
Ameboresha miundombinu, barabara na mambo mengine ya reli na bandari. Nasi Wabunge tunamsaidia kufanya kazi apate sifa, kazi tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nampongeza Mheshimiwa Rais wangu wa Zanzibar, amefanya kazi nzuri na kuiboresha Zanzibar kwa miundombinu ya barabara, taa za solar Michenzani, Amani na sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza vile vile Waziri Mkuu. Waziri Mkuu anafanya kazi nzuri pamoja nasi na anakwenda kila mahali anafanya kazi yake nzuri, nasi tuko pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja katika mada yetu ya Kamati yetu ya Miundombinu.
Kamati yetu tumetembelea barabara zote na hivi juzi tumekwenda kuanzia Dar es Salaam, tumetoka Dodoma kwenda Arusha, tumeona barabara inajengwa na madaraja. Naipongeza Tanzania yetu na Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri na kuweka uchumi bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nataka kuzungumza kuhusu Uwanja wa Ndege.
Nimetembea viwanja vya ndege mbalimbali. Tumetoka kwenda Arusha, tumeona mambo mazuri, lakini yanatakiwa kuboreshwa. Mnara wa uwanja wa ndege ni mdogo sana, unatakiwa ufanywe mkubwa upate kuonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati yetu na mimi nimefaidika kumsaidia Mheshimiwa Rais, uwanja wa ndege wa Kilimanjaro wa International ni mzuri kabisa; lakini uwanja wa ndege wa Moshi, tunatakiwa tutie mkazo katika Serikali. Yaani uwanja wa ndege wa Moshi ile ndege inatua katika barabara mbovu kabisa. Tokea enzi ya British ipo pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali pamoja na Mheshimiwa Waziri, tuboreshe uwanja wetu ule, kwa sababu katika uwanja wa ndege wanakuja watalii. Watu wanakuja kwa utalii wanashuka Arusha wanateremka Kilimanjaro, lakini pale uwanja wa ndege wa Moshi upo
karibu na mlima wetu wa Kilimanjaro na Mount Meru. Uwanja wa ndege wa Arusha ndege nyingi zinatua pamoja na ATC, kwa hiyo, kwa nini usiboreshwe pale Moshi? Kwa sababu pale Moshi ni centre, wanakuja watalii wapate kwenda moja kwa moja katika mambo ya kutazama
wanyama pamoja na Mlima wetu wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetembelea bandari nyingi sana. Bandari hii inahitaji kuboreshwa hasa. Tumekwenda Tanga, Mwanza, tumeona Bandari ya Mwanza ni nzuri, lakini inatakiwa kutiwa nguvu kabisa kuboreshwa ili kukuza uchumi, kusafirisha mizigo nchi za jirani.
Bandari ya Tanga ipo jirani na Zanzibar na Mombasa. Tumeona kuna uzito na ipo haja kubwa sana ya kuboresha, kupanua na kuleta meli kubwa za makontena makubwa kuliko Dar es Salaam ambapo tunateremsha kontena zetu. Ni bora kufika Tanga kwenda kwa nchi za jirani.
Vilevile tuboreshe bandari yetu ya Bagamoyo. Tumetembezwa, tumeridhika na tumesema Tanzania yetu naomba Mheshimiwa Rais aboreshe ile Bandari ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye sekta ya reli. Standard gauge ya reli sisi Kamati tulikwenda kutembea, nampongeza Mwenyekiti na Kamati yangu. Mara ya kwanza nimekwenda Tanzania nimeona reli. Standard gauge imekwama sehemu fulani, haikuweza kuboreshwa, lakini nashukuru Mheshimiwa Rais wetu amepata ufadhili mpya, tutaboresha tufanye kazi; reli yetu kwa upande wa Congo tupate kupeleka mali yetu Burundi na Rwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutakuwa tunaongeza uchumi wa nchi na hiyo ndiyo sekta muhimu. Wenzetu wa Kenya kutoka Mombasa wamefika Nairobi, wataunganisha na jirani pale Congo na wapi, sisi tutakosa soko. Naiomba Serikali tufanye kazi na namshukuru Mwenyezi
Mungu na naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, Mungu ampe uzima na afya Mheshimiwa Rais wetu afanye kazi ya ziada…
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda
wangu umekwisha, naunga mkono Kamati hii na Bunge letu. Ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme jambo moja, kama nimekosea, ulimi hauna mfupa. Ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's