Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Yussuf Salim Hussein

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata nafasi kwa siku ya leo kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kuweza kusimama kwa mara ya kwanza leo kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Mimi sitaki nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri nataka nikupe pole, mzigo huu ni mkubwa na nadhani Serikali ya Chama cha Mapinduzi hamjajipanga katika kutekeleza na kuwatumikia Watanzania ipasavyo katika suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo, mifugo na uvuvi imebeba sehemu kubwa kama siyo yote ya maisha ya Watanzania. Watanzania wote utawakuta asilimia kubwa wanaogelea katika taasisi hizi tatu. Kwa hiyo, sidhani kama mmejipanga vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali nzima kutokuwa na vision tunakwenda wapi ndiyo tatizo ambalo linapelekea kilimo chetu na masuala yetu yote ndani ya nchi hii hatufikii pale ambapo tunakusudia na inakuwa ni ubabaishaji tu. Hatuna vision tunataka kulima nini, tulime wapi, tupeleke wapi na kwa namna ipi, hakuna!
Kwa hiyo, unakuta Rais anayekuja ana mipango yake katika kichwa, Waziri anayemweka ana mipango yake katika kichwa, hatuna vision ambayo kama nchi tumepanga kwamba tunataka kulima kitu hiki ili tukipeleke kwenye kiwanda hiki au tusafirishe, hakuna hiyo vision. Ni kila anayekuja, anakuja na mawazo yake na fikra yake ndio maana ndugu ni kawapa pole.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hatuna vision, tunataka kulima nini, tulime wapi, tuelekee wapi, hatuwezi kupata maendeleo ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mipango ya Serikali si mipango ya kifamilia, si mipango ya mtu binafsi, lazima tuwe na vision, tuwe na mpango ambao tumejipanga. Hatuwezi kupata mafanikio ya Kitaifa kwa miaka miwili au mitatu yakaweza kuonekana, hii siyo sunsumia bwana. Kuendesha Serikali ni lazima watu wajipange, wawe na vision ili mafanikio yale yataonekana baada ya miaka 10, 15 lakini kwa mfumo huu hatuwezi kwenda na itakuwa kila siku tunacheza chakacha tu hapa. Ni lazima tuwe na vision ambayo itakuwa inatuonesha tunataka kwenda wapi, kila Rais na Waziri ajaye awe anaelekeza nguvu zetu hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013/2014 nchi hii imevuna mahindi mengi sana. Natoa mfano wa kuthibitisha kwamba Serikali haina vision. Kila ukipita humo mikoani unakuta rumbesa za mahidi yamefunikwa maturubai kwa sababu Serikali haikuwa na mpango, haikujipanga mvua ikanyesha mahindi yale yakaharibika yote. Mwaka jana tayari nchi hii unasikia baadhi ya mikoa ina njaa, kwa nini ni kwa sababu hatukujipanga. Hebu kama Serikali kaeni mjipange tunataka kulima nini, kwa wakati gani, tupeleke wapi, tuuze wapi? Tukifanya hivyo tutakuwa tumefanikiwa na haya maendeleo tunayoyazungumza leo kutoka hapa kwenda kwenye uchumi wa kati yataonekana vinginevyo itakuwa tunakata viuno tu hapa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee suala la pili la mifugo. Nchi ya Tanzania imebahatika kuwa na mifugo mingi zaidi ya wananchi wake, lakini tukijiuliza hii mifugo imetusaidia nini, imetupeleka wapi, imesaidia nini katika Pato la Taifa? Matokeo yake badala ya kutupa mafaniko chanya inatupa mafanikio hasi. Leo wananchi kwa wananchi wenyewe kwa wenyewe Watanzania wanapigana kwa sababu ya mifugo yao, kwa sababu ya kilimo chao. Leo wafugaji wanaonekana kama ni maadui ndani ya nchi hii, leo wafugaji mifugo yao haijawasaidia chochote, haijawanufaisha chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Serikali basi ituambie ni mkakati gani wa muda mrefu ambao imepanga ili kuweza kuona kwamba mifugo hii, tena hapa ametaja vizuri tu katika ukurasa wa kumi idadi ya mifugo ile ambayo inamilikiwa na watu tu inazidi idadi ya Watanzania mbali ya hiyo ambayo ipo katika mapori. Sasa itatusaidiaje au sisi tunalewa sifa tu kwamba Tanzania ni nchi ya tatu katika Bara la Afrika kuwa na mifugo mingi lakini inatusaidia nini, tumejipanga vipi? Kwa hiyo, sisi ni sifa tu Watanzania tupo hivi na hivi. Akili za kupanga mapinduzi ya kupindua Serikali ya Zanzibar ya wananchi mnayo lakini akili ya kukaa mkapanga sasa namna gani tutumie rasilimali hii Mwenyezi Mungu aliyotupa ili tuwaletee wananchi wetu maendeleo hiyo hakuna, ni ubabaishaji tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii ambayo unatupa mwaka huu na mwakani kipindi kijacho cha bajeti utakuja kutupa taarifa hii. Hata hivyo, tuseme ukweli kama bajeti iliyotengwa kwa Wizara ya Kilimo wanapewa asilimia 38 tunategemea nini? Tusitegemee kitu chochote kwa sababu asilimia 38 hawawezi hawa kutekeleza majukumu yao, kwa hiyo, atakuja hapa iwe sababu yake sikuwa na bajeti na kweli tutamlaumu nini? Hebu tuacheni kuongeza kimo kwa kinu tupange bajeti kulingana na ule uwezo ambao tunao halafu tumkamate Waziri tumekupa kiasi hiki na hukuweza kufikia yale malengo. Leo unampa asilimia 38, kwa hiyo, badala ya kufanya kazi unampa mzigo sasa wa kufikiri atumie vipi kiwango kile kidogo cha pesa uliyompa kwa ajili ya kufanikisha majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa sekta ya uvuvi, hapa ndipo kwenye mtihani mkubwa. Waziri hapa katika hotuba yake amesema nchi ambayo inatarajiwa angalau tuwe na wavuvi milioni mbili tuna wavuvi laki moja, hatujaitumia hata kidogo sekta ya uvuvi, bahari kuu hatujaitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya 2013/2014, Waziri alisema kwamba wamezalisha vifaranga vya samaki milioni 20 na hivyo ndivyo vitagawanywa kwa wakulima ili iwe ni kichocheo cha kuongeza samaki. Vifaranga milioni 20 Tanzania, haitoshi hata mboga ya siku moja, kweli Serikali mpo serious kwamba mnataka kuongeza samaki? Mwaka uliofuata mwaka jana hajatuambia hivyo vifaranga milioni ishirini vingapi vimepona, vingapi vimekufa na imepatikana faida gani. Kwa hiyo, hakuna kitu chochote ni usanii tu ambao unapita hapa tunapigana usanii, tunakuja hapa tunajidanganya, tunawadanganya na Watanzania kuona kwamba tuna bajeti ya trillions of money lakini mwisho wa mwaka faida hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia kwamba kuna uvuvi haramu, tumefanya nini sasa kukomesha uvuvi haramu, unapiga nyavu moto. Hawa wavuvi umewasaidiaje, umewapa elimu gani na umewapa mbadala gani? Je, ni nani kaingiza hizo bidhaa, zimepita wapi, zimelipiwa kodi au hazikulipiwa? Tumlaumu nani, are you serious Serikali ya CCM? Hamjawa serious jamani, hebu kuweni serious halafu tuone baada ya miaka mitano, kumi tutayazungumza haya? Sasa wapinzani tunaposema tunasema kwa sababu tuna uchungu, tunaumia na ndiyo maana tunasema hebu kaeni pembeni tuwaonyeshe namna gani Serikali inaendeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa vifaa, huwezi kwenda kuvua katika bahari kuu na kidau, lazima…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mchana huu. Aidha, ninakushukuru na wewe kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, wachangiaji wa leo ni wakali sana, kule kwetu tunasema moto umepata magogo sijui kwenye chanja utawaka! Wapemba wana methali inasema; “ukilima patosha utavuna pashakwisha” na ukilima usipo palilia ukivuna utalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru mchangiaji aliyemaliza amemuonyesha chanzo kimoja cha mapato ambacho Mheshimiwa Waziri akikitumia anaweza kuongeza pato katika Wizara yake. Sasa na mimi nataka nimuonyeshe chanzo ambacho kama atakitumia basi Jeshi letu litakuwa ni chanzo kikubwa cha mapato hata pengine kuliko utalii au vyanzo vingine vya mapato katika nchi yetu kwenye Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Jeshi letu limesifiwa sana na linasifiwa sana na ndiyo ukweli kwa utendaji kazi na weledi na nidhamu ya hali ya juu ndani ya nchi yetu na nje ya nchi yetu, ni ukweli kwamba Jeshi letu linashiriki katika UN - Mission nyingi. Tunaomba leo, Mheshimiwa Waziri utakapo kuja hapa utuambie Jeshi letu linashiriki katika mission nyingi za UN; je, ni kiasi gani cha fedha tunazopata kutoka katika mission hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mission hizo kuna dry lease ambazo tunapeleka wanajeshi na logistic nyingine zinafanywa na UN, lakini wet lease ambazo tunapeleka wanajeshi na vifaa, kila kifaa kinalipiwa kwa dola. Kwa mfano gari moja tu linalipiwa kati ya dola 500 hadi dola 800, na inalipwa katika vipindi vya miezi mitatu, mitatu. Tumeshiriki katika UN Mission nyingi, utuambie Mheshimiwa Waziri ni kiasi gani cha fedha za kigeni ambazo Jeshi letu linapata katika mission hizo au pato letu sisi ni yale majeneza tu yanayokuja na maiti hapa tunazika? (Makofo)
Mheshimiwa Spika, hapa lazima tujipange, dunia ya leo, missions hizi za UN ni mtaji. Nchi kama Bagladesh, India, South Africa, Ukraine, wamewekeza sana katika UN Missions majeshi yao na silaha, kwa sababu zinaingiza pato kubwa katika Jeshi la Wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaiomba Serikali sasa, nilisema wakati nachangia Wizara ya Kilimo hapa kwamba Serikali haina vision, tunaiomba Serikali sasa ikae, ipange hapa ili Jeshi letu lisiwe linaenda kule kupigana vita tu, lakini liwe linaenda kule linapigana vita kwa faida ya wao wenyewe, lakini na kwa faida ya nchi yetu na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali lazima ipange tujuwe ni vifaa gani vinatakiwa vinunuliwe viwepo pale na katika ubora wake ili lile pato katika nchi yetu liwe ni pato kubwa na tusiwe tunapeleka askari wetu na kupoteza maisha tu kule! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli inasikitisha, Serikali hii ya CCM kwamba hata jeshi mnalipatia asilimia ndogo ya bajeti ambayo inapitishwa. Jeshi ambalo linalinda mipaka ya nchi yetu, Jeshi ambalo limekomboa nchi zote hizi za Kusini, Jeshi ambalo ni waaminifu, ni waadilifu, ni wasikivu.
Mheshimiwa Spika, Jeshi ambalo linafanya kazi katika mazingira magumu, yakitokea maafa sasa hivi hapa daraja limekatika ni wao huko, mvua, jua huko, leo katika bajeti yao wanaambiwa kwamba wanapata asilimia 18 katika bajeti ya maendeleo, hivi jamani kweli!
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika naendelea, kama kuna Mbunge hajaridhika anione kwa wakati wake nimsomeshe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapopeleka Wanajeshi wetu katika mission hizi kuna Chapter Seven kuna Chapter Six, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie namna gani askari wetu wanalipwa wanapoenda katika Chapter Seven na wanapoenda katika Chapter Six. Atuambie ni namna gani wanalipwa. Kwa sababu Chapter Seven ni ulinzi wa amani, lakini Chapter Six ni vita kamili. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri utupe ufafanuzi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia utuambie Mheshimiwa Waziri kwa mfano, kama hawa waliokwenda DRC hivi karibuni tu, tumepoteza askari wawili muhumu sana! Luteni Rajabu na Meja Mshindo ni askari ambao ni muhimu sana katika jeshi letu, wamepotea katika kuisambaratisha M23 wamefanikiwa; je, waliporudi askari wale ambao walirudi na roho zao, Serikali imewathamini vipi? Wale ambao wamepoteza maisha katika vita ile ya kuisambaratisha M23 hadi leo ni vita ya kawaida tu pale na wao familia zao zitaenziwa vipi?
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iwaangalie askari wetu hawa angalau wawe na bima ya afya, wawe na bima ya ajali, wawe wana bima ya kazi hatarishi zile wanazo zifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni aibu leo kusikia askari mstaafu tena pengine alikuwa na cheo kikubwa anamaliza jeshi anakuwa fundi baiskeli au mziba pancha mtaani au mlinzi, ni vitu vya kusikitisha kwa kweli! Kwa hiyo, angalau basi wapatiwe hizi bima za afya askari wote wawe na bima za afya, wawe na uhakika angalau na maisha yao.
Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, katika ukurasa wa 24 wa hotuba yake amesema miongoni mwa kazi walizozifanya ni kutoa mafunzo katika jeshi, lakini pia na Jeshi la Akiba. Kwa hiyo atuambie hilo Jeshi la Akiba ambao wamepata mafunzo ni askari wangapi na mafunzo ya aina gani ili tuweze kujua hawa askari wetu wa akiba wamepata mafunzo ya aina gani.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kama hatutowathamini wanajeshi wetu na kama tutaendelea na usanii huu wa kwamba tunapitisha bajeti hapa katika Bunge, halafu bajeti zile haziendi hata kwa Jeshi, tunajipalia makaa wenyewe! Tunajipalia makaa sisi wenyewe pamoja na uaminifu na uadilifu waliyonao, lakini hawa ni wanadamu kama wanadamu wengine. Kwa nini bajeti ya Bunge ikamilike, kwa nini bajeti ya Serikali, Mawaziri na Maafisa wengine wapewe kwa ukamilifu, lakini bajeti ya Jeshi iende robo, kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata hawa wanaofanya kazi hizi tunashindwa kuwakamilishia bajeti! Ninaiomba Serikali sasa, tumepita katika Awamu Nne tumebabaisha sana, hii Awamu ya Tano ya hapa kazi tu na mmesema kwamba Awamu ya Tano hii ni nzuri sana, sisi tuna imani hiyo kwamba inaweza ikawa nzuri, basi mkae kama Serikali, mpange ili tuone Serikali inaendeshwaje.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya leo. Mwenyezi Mungu amesema katika Quran, Sura ya 41, aya ya tisa mpaka ya 11 katika juzuu ya 24 kwamba ameitandika ardhi na akaipa neema mbalimbali za ndani ya ardhi na juu ya ardhi, akaipa milima na mabonde, akaipa mito na maziwa, akaipa misitu, akaipa na viumbe hai na madini ili kwayo ituneemeshe na itufaidishe wanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha katika ardhi hii ya Tanzania imekuwa kama ni laana sasa kwetu, badala ya heri inakuwa shari. Mwenyezi Mungu ametuambia hayo na turudi katika vitabu vyake ili tujifunze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi katika uchangiaji wake, Mwenyekiti wangu Mchakachuliwa, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, alikariri falsafa ya Baba wa Taifa, kwamba ili tuendelee tunahitaji mambo manne; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Watanzania tuna ardhi kubwa, tunamshukuru Mungu. Tupo wengi, tunakaribia milioni 50 sasa Alhamdulillah, lakini kwa nini tunagombana, tunahasimiana, tunapigana mpaka tunauwana? Ni kwa sababu ya ardhi. Ni kwa sababu ya ama ya siasa safi, uongozi bora ama yote mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa muda wa miaka 54, bado inawaomba tena mkae chini mtafakari, tatizo letu ni nini mpaka iwe ardhi hii haijatuletea tija? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitu ambacho kinaleta matatizo katika ardhi na kusababisha maafa makubwa ni kukosekana kwa kile kinachoitwa Integrated Land Information Management System. Pamoja na mipango mizuri iliyopangwa na Mheshimiwa Waziri na timu yake, pamoja na World Bank kutoa pesa zaidi ya Dola milioni 20 kwa ajili ya kazi hii, pesa hizi kwa zaidi ya miaka miwili zimezuiliwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, hili halijatendeka. Watanzania wanauana, wanaumizana, wanahasimiana, kwa nini? Siasa safi, au uongozi bora? Tatizo ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikasema kwa miaka 54 hebu wenzetu kaeni chini kuwe na vision, leo kila mchangiaji anasimama anakwambia tunamshukuru Mheshimiwa Lukuvi tokea awe Waziri, amejaribu kutatua migogoro. Mheshimiwa Lukuvi ni mwanadamu, ni kiumbe. Hivi akiondoka Mheshimiwa Lukuvi, tunarudi kule kule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kaeni chini Serikali ya CCM tuwe na vision, yeyote atakayekuja katika Wizara hizi, awe anaanza pale anakwenda mbele. Leo akiondoka Mheshimiwa Lukuvi iwe Wizara hii haipo; akiondoka Mheshimiwa Mwigulu, Wizara ya Kilimo, kwisha! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Namshukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo. Ukienda katika ile Wizara, unajua hasa kwamba anatoka wapi anakwenda wapi, step by step. Amejipanga! Kwa hiyo, pale unajua namna gani mtu amejipanga, anatoka wapi, anakwenda wapi. Jamani ukweli lazima usemwe! Kwa hiyo, tunaomba Serikali ya CCM katika Wizara zote tujipange, tuwe na vision tujue tunakwenda wapi, siyo kusema kwamba aah, Lukuvi! Lukuvi kiumbe! Lukuvi ni binadamu huyu! Akiondoka huyu jamani, tuwe tunarudi kule? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba Bunge hili, leo hii, wakati bwana mkubwa anawasilisha huyo, tujue fedha hii iliyotolewa na World Bank itatoka lini, wapewe wafanye kazi ili Watanzania wasiuwane na wasihasimiane kwa neema waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije la pili. Namwomba Mheshimiwa Waziri Lukuvi, pamoja na kutushawishi sana Wajumbe wa Kamati yake, pamoja na maelezo mazuri sana aliyotutolea, lakini bado tuna wasiwasi na bado mimi binafsi sijakubaliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha miaka nane wananchi wa Kigamboni wamekuwa mayatima, wamekuwa na hofu juu ya hatima ya ardhi yao, Mji wa Kigamboni utakavyokuwa. Pamoja na kupunguza eneo likarejeshwa kwa wananchi, hilo lililobakia la hekta 6000, hadi leo Serikali hii haikupi fedha ya kwenda kufanya hizi shughuli ambazo zinatakiwa kufanywa. Hii miundombinu. Sasa kama hupewi fedha na ardhi ile tayari imezuiwa na wananchi wale wamepewa tu maelezo kwamba mwingie kwenye uwekezaji, mwingie hivi, mwingie hivi, lakini kwa muda wa miaka nane sasa hakuna fedha inayotoka, pale tunategemea nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunasema jamani, Serikali ya CCM tunapanga; lakini tunajitekenya wenyewe, mkicheka wenyewe, kama hamjampa fedha huyo Lukuvi, atafanya nini? Kwa hiyo, kama fedha haijatengwa, wale wafanyakazi na ile Ofisi; wafanyakazi warudi Wizarani na Ofisi ifungwe, mpaka atakapopewa fedha ile itarudi ikae kwa miundombinu, ili ule Mji wa Kigamboni uje katika hilo linalotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika nyumba za gharama nafuu. Kuna wazo zuri, mipango mizuri na kwa kweli namshukuru sana. Kama analipwa hiyo shilingi milioni 40, basi ni haki yake, alipwe Mkurugenzi wa Nyumba na Makazi, kutokana na kazi anayoifanya. Kwa sababu mtu kama anafanya kazi, basi mwache apewe kwa namna anavyofanya kazi. Anafanya kazi na anastahiki. Tunaiomba Serikali waondoe suala VAT katika nyumba za gharama nafuu ili wananchi wanyonge waweze kununua hizi nyumba ziwafaidishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi jamani mtu anayelipwa mshahara wa sh. 150,000/=, ataweza kweli kununua nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 45 kwenda juu? Kama hakuna wizi huko nyuma, ataweza? Sasa tunaiomba kodi hii VAT iondolewe katika hizi nyumba ili nyumba hizi, lile lengo lililokusudiwa la wale wanyonge kuweza kununua na kuishi katika nyumba hizi ziwafikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Waziri, Tanzania imekua, Watanzania wanaongezeka, mahitaji ya ardhi yanaongezeka, lakini na teknolojia ya kutumia ardhi inaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kasi ya upimaji wa ardhi ni ndogo sana. Pamoja na kuruhusu taasisi binafsi, wakawapa vibali wapime ardhi, lakini bado kasi ni ndogo sana hususan huko vijijini. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hii kasi iongezeke ili upimaji uendelee kwa kasi na wananchi wa vijijini wamiliki ardhi ziwasaidie waweze kukopesheka kwa faida yao na kwa faida ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha jioni ya leo kusimama hapa. Jioni ya leo nataka kumshauri tu Mheshimiwa Waziri na kuishauri Serikali. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri awe makini, atulie bardan wasalaman, laa takhaf wa laa tahzan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hadithi ndogo wakati nasoma miaka ya 70, darasa la tatu kulikuwa na kitabu kidogo cha Kiswahili maarufu tukikiita Haji na Selele, kilikuwa na hadithi nyingi ndogondogo. Sasa tukisoma tukimaliza mwisho wake tunaulizwa hiyo hadithi imekufunza nini? Moja kati ya hadithi iliyokuwemo ni ile ya mtu aliyekuwa na kuku wake kila siku akitaga yai moja la dhahabu. Siku hiyo akaamua kumchinja ili apate mayai mengi ya dhahabu matokeo yake akakosa yote. Hadithi hii inatufunza nini? Tamaa nyingi mbaya. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na-declare interest kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Wizara hii, lakini pia nimeshawahi kutumikia Idara ya Misitu na Utalii, kwa hiyo nazungumza kitu ambacho kinaelea katika kichwa changu, nakifahamu. Binafsi wakati nilipoteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati hii na nikakutana na viongozi wa Wizara nilieleza waziwazi baada ya taarifa kwamba sifurahishwi na TFS na nikawa na mashaka nayo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefarijika zaidi baada ya kupata semina na ile hofu yangu ikathibitishwa na mtaalam aliyebobea katika masuala ya misitu kwa utafiti wake alioufanya kwa muda wa miaka mitatu juu ya TFS. Nakushauri nini Mheshimiwa Waziri? Kwa sababu ameyakuta haya lakini kwa sasa yeye ndiye mwenye dhamana na Wizara hii, kwa hiyo, mwaka huu namshauri tu ila mwakani nitambadilikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TFS ni nzuri katika ukusanyaji wa kodi lakini namwomba Mheshimiwa Waziri alinganishe sasa tunachokipata na athari tunayoipata, vinalingana? Misitu ya asili inapotea na itazidi kupotea na kwa mujibu wa mtaalam baada ya miaka 10 Tanzania hii itakuwa jangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwakumbushe wale wanaokumbuka mwishoni mwa miaka ya 80, kazi kubwa tuliyoipata Watanzania na dunia kwa suala la HASHI na HADO kwa Mikoa ya Dodoma na Shinyanga ilivyokumbwa na janga la ukame, kazi iliyofanyika ndani na nje ya nchi. Binafsi nilifika Dodoma hapa kwa ajili ya kupanda miti kutokana na hali iliyokuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri aichambue TFS, aone udhaifu wake. Udhaifu wa TFS ni menejimenti, ni lazima ahakikishe kwamba anabadilisha, wanakusanya vizuri, wanapanda vizuri, lakini katika misitu ya asili suala la kuelekeza nguvu tu kwamba wakusanye kodi wanatumalizia misitu kitu ambacho kitakuja kuwa ni hatari kubwa kwa Taifa hili. Badala ya rehema hii misitu itakuja kuwa nakama kwetu, Mheshimiwa Waziri namshauri hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo hatuwezi kuwa na misitu endelevu, hatuwezi kuwa na misitu yenye tija, hatuwezi kuwa na misitu ambayo itatuletea faida sisi na kizazi chetu kama hatuna wataalam katika fani hiyo ya misitu. Leo nchi hii ina Chuo kimoja tu cha Misitu Olmotonyi, lakini Serikali imekitelekeza. Chuo kile kimekuwa kama yatima, hakina ruzuku yoyote kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kile chuo kiangaliwe, kipewe ruzuku, kisimamiwe, kisomeshe wataalam wengi zaidi ili warudi katika misitu yetu ambayo iko chini ya Wizara, Halmashauri na Vijiji ili iwe ni misitu endelevu kwa faida yetu na faida ya kizazi kijacho. Huo ndiyo ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri kwa siku ya leo katika upande wa misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye utalii. Amezungumza na kutoa ufafanuzi mkubwa juu ya nia yake ya kutoka kwenye watalii milioni moja na zaidi kwenda milioni tatu. Ni wazo zuri, tunaliunga mkono kwa sababu tunafahamu ongezeko la watalii litaleta faida gani kwenye nchi yetu, lakini lazima tujue tunataka aina gani ya watalii katika nchi yetu? Kwanza iwe ni kwa ajili ya kukuza mila na desturi zetu lakini wawe ni watalii wenye faida siyo watalii vishuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, ili kupata watalii wazuri lakini kuwa na wawekezaji wazuri katika sekta ya utalii na kuondoa tofauti baina ya watalii, wawekezaji na jamii inayozunguka hivi vituo vya kitalii lazima kuwa na triangle ambayo itahusisha investors, Serikali na community.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutakapokuwa na triangle hiyo na wakawa pamoja na kujua mwekezaji anahitaji nini, Serikali inahitaji nini na jamii inahitaji nini, mkawa mnasimama katika kitu kimoja, mwekezaji akija hapa katika muda mfupi atakuwa amepata idhini ya kuwekeza lakini pia itakuwa uwekezaji huo una faida kwa sababu kila mmoja atakuwa anajua majukumu yake na yamepangwa yapo. Kwa hiyo, hilo namshauri Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi mtalii anachohitaji ni huduma. Inasikitisha unapokwenda katika hoteli zetu au katika vivutio vyetu vya kitalii kwa zile huduma zinazopatikana pale. Mtalii hahitaji jengo zuri ambalo labda lina ma-AC na kadhalika, anachohitaji hata kama ni kibanda cha nyasi lakini kiko katika kiwango gani? Je, tumeviweka katika viwango vile ambavyo wao wanavifurahia?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli watalii wanafurahia sana tradition yetu lakini je, watendaji wetu ambao wanafanya kazi hiyo, wanafanya kazi wakiwa na uweledi huo? Ndiyo maana katika Kamati nikakikamata sana Chuo kile cha Utalii, je, mnafundisha kulingana na mahitaji tunayoyahitaji ndani ya nchi yetu? Kwa hiyo, chuo kile kitoe wataalam ambao watakuwa ni wale wanaohitajika kulingana na mazingira yetu na matakwa yetu na lengo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana mwaka mmoja wa kuondoa yale yote mabaya ambayo leo tunamwambia ambayo ameyakuta na mwakani hapa atakapokuja katika bajeti tuje tuone improvement. Kama ipo mimi tutakuwa pamoja, kama haipo Mheshimiwa Waziri kwa kweli mimi nitakuwa adui namba moja katika hili. Kwa sababu ninayoyazungumza nayazungumza nikiwa nayajua na najua kuna nini. Leo nazungumza tu hapa vizuri lakini siku nyingine nikiamua kuzungumza vibaya atakuja kuelewa kwamba kweli hiki kitu ninachokizungumza nakifahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunataka kile chuo kinachotoa vijana…
MWENYEKITI: Ahsante.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN:Bismillah Rahman Rahim.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na kwa sababu ya dakika kumi ulizonipa basi niende haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya kwanza ni kuhusiana na ufinyu wa bajeti. Kamati yetu sisi imeshindwa kutembelea maeneo ambayo hasa yana migogoro na kuweza kuishauri vizuri Serikali. Mgogoro wa Ngorongoro kila Mtanzania anaufahamu, Loliondo, lakini uvamizi katika mapori ya akiba ya Kigosi, Moyowosi, Burigi, Kimisi na kadhalika, kote huko tumeshindwa kufanya kazi kwa sababu ya ufinyu wa bajeti, Wizara yenyewe hadi hapa tunazungumza bado robo moja kumalizia ina chini ya asilimia 30 ya bajeti ambayo imetengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliombe Bunge hili, mtu anaonyeshwa njia wakati wa kwenda siyo wakati wa kurudi, bajeti ijayo tuhakikishe tunaweka fedha ya kutosha katika Kamati zetu na katika Wizara zetu ili tuweze kufanya kazi vizuri na kuishauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, suala la pili, tuna tatizo kubwa sana katika nchi yetu lakini tunalidharau na tukiendelea kulidharau kwa mujibu wa tafiti zinazofanywa na wataalam baada ya miaka 20 nchi hii tutalia kilio cha kusaga meno. Waheshimiwa misitu yetu inapotea kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana ndugu yangu Mheshimiwa Kiwanga alilia machozi kama mtoto mdogo alivyokuwa anatembea katika Kamati akaona misitu inavyoathirika. Labda nitoe mfano, uchomaji wa mkaa ni chanzo kikubwa sana cha nishati na asilimia 90 ya Watanzania wanategemea nishati ya mkaa na kuni kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani, lakini vitu hivyo havina sheria, kanuni na hakuna sera ya uchomaji wa mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, kuna vijiji kumi Kilosa vimefanyiwa utafiti, wamepanga matumizi ya ardhi pamoja na matumizi ya misitu, wamegawa vile vijiji katika block 24 na kila mwaka wanatumia block moja kwa kuni, mkaa na matumizi yao. Kwa hiyo, miaka 23 wanaacha zile block zina-regenerate zenyewe. Kwa hiyo, pale tatizo lile limeondoka, faida yake nini? Hakuna uvamizi katika yale maeneo mengine, kijiji kinapata faida zaidi kutokana na mapato yanayopatikana, lakini pia kuna na ile teknolojia iliyowekwa pale ya uchomaji mkaa ile miti inatumiwa vizuri pamoja na majiko yale bunifu waliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusijidanganye, tujiulize, hivi ni miti mingapi inayokatwa kwa mwaka mmoja ndani ya nchi yetu na ni miti mingapi inayopandwa kwa mwaka ndani ya nchi yetu, inawiana? Huo mti utakaopandwa utakaa miaka mingapi ili tuje tukate tena? Kwa hiyo, tusijidanganye mtu anaweza akasema yeye hatumii mbao kwa sababu sasa hivi kuna teknolojia atatumia vioo kutengeneza milango, meza na kadhalika lakini akifa, nani ambaye haendi na ubao?
Kwa hiyo, tusijidanganye hii ni kwa wote Mkristo utaenda na sanduku, Muislam utawekewa ubao, kila mtu siku ya mwisho utaondoka na ubao. Kwa hiyo, miti ina faida kubwa ukiondoa zile tangible na intangible benefit kutoka kwenye miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, hili ni janga, ni kubwa lakini bado Watanzania tunalifumbia macho. Hivi hatuumii kila siku kusikia ndugu zetu wanauana kwa sababu ya tatizo la wafugaji na wakulima?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bismillah Rahman Rahim.Nakushukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwanzo katika siku ya leo katika hotuba iliyo mbele yetu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama walivyotangulia wenzangu na mimi napenda nikukumbushe kwamba kama ambavyo tuliagizwa kwamba tukumbushe hakika ya ukumbusho unawafaa wanaoamini.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ulipoapa kuwa Mbunge ulishika Msahafu na kauli yako ya mwisho ukamwomba Mwenyezi Mungu akusaidie na ulipoapishwa kuwa Waziri Mkuu ulishika tena Msahafu na kauli yako ya mwisho ikawa unamwomba Mwenyezi Mungu akusaidie. Na sisi
tunamwomba Mwenyezi Mungu akusaidie inshaallah. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yako ukurasa wa 52 na 53 umezungumzia suala la amani, lakini amani haiwezi kuwa amani ya kweli kama haijasimama kwenye nguzo zake na nguzo kubwa ya amani ni haki, Katiba na kufuata sheria. Ni dhahiri Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali ambayo sasa wewe ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali hiyo kwa maana ya Mtendaji Mkuu wa Serikali, Serikali
yako au nchi yako unayoisimamia sasa hivi, siyo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya mipaka yetu hatuna vita, lakini ndani ya nchi yetu wananchi hawaishi kwa amani kabisa. Kila mmoja wetu ana hofu ya nini kitatokea baadaye? Kuanzia Mawaziri na watendaji wote wa Serikali hakuna mmoja anayefanya kazi yake akiwa na amani ndani ya nafsi yake akiamini kwamba jua litatua hajatumbuliwa. Wafanyabiashara kuanzia wakubwa na wadogo, hawana amani na biashara zao wakiona kwamba wakati wowote biashara zao zitapotea. Wafanyabiashara wakubwa, wamachinga wenye vibanda vidogo vidogo, anaweza
akaamka asubuhi, biashara yake haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bomoa bomoa za nyumba, mtu ana nyumba yake amejenga kwa miaka 20, 30 anaishi inakuja kubomolewa ndani ya dakika tano. Watanzania hawaishi kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vifo vinavyotokana na
watu wenyewe kupigana, wakulima na wafugaji, wanyama kufa kwa kukatwa mapanga ama sumu, vimezidi kuendelea katika nchi yetu, lakini njaa inayoendelea kwa sababu mbalimbali za ukame, mafuriko ama wanyama waharibifu na ndege, inazidi kuendelea katika nchi yetu na wananchi wakisema wana njaa majibu ya Serikali yanakuwa hayaeleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi sana, nchi hii siyo salama. Baya zaidi hivi sasa kinachotia hofu ni hii kamata kamata, utekaji na uuaji unaoendelea katika nchi yetu. Wilaya za Mkuranga na Rufiji sasa hivi watu wanapigwa risasi, viongozi wa Chama cha Mapinduzi ambao ni Wenyeviti wa Vijiji wanapigwa risasi, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inanishangaza sana kuona polisi wanatumia nguvu kubwa kuondoa mashamba ya bangi huko, lakini watu wanakufa kwa risasi ndani ya nchi hii. Kwa umri wangu wa miaka 54 sasa sishangai suala la utekaji, wala uwekwaji ndani wa watu, wala kupotea watu
wasionekane kama Ben Sanane, sishangai na sitashangaa. Waheshimiwa Wabunge, haya yalianza Zanzibar. Miaka ya 1964 mwanzoni, akina Abdallah Kassim Hanga, Mlungi Ussi, Abdulaziz Twala, Othman Sharrif na Twaha Ubwa walipotea katika mazingira ya kutatanisha na hadi leo
hawajaonekana. Mwaka 1972 mwasisi wa Jamhuri ya Muungano Abeid Aman Karume amepigwa risasi, akauawa. Kesi ikawa inaoneshwa live katika televisheni ya Zanzibar wakati huo ndiyo televisheni ya mwanzo kwa Afrika, ikionesha kesi ile. Mshtakiwa Mr. ‘X’ hajulikani ni nani, kesi ile ikaishia. Wanaotuhumiwa kuwa wauaji wakahifadhiwa na Jamhuri ya Muungano hadi kufa kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeshuhudia kifo cha Edward Sokoine kimeacha maswali mengi sana. Kifo cha Imran Kombe aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa, kapigwa risasi kama ngedere katika shamba lake, lakini pia Horace Kolimba alipotea katika mazingira ambayo yameacha maswali mengi; Balali aliyekuwa Gavana Mkuu wa Serikali kapotea, lakini Wazanzibari hadi leo tunajiuliza kifo cha Dkt. Omar Ali Juma kupotea kule na familia yake imetelekezwa hadi leo. Kwa hiyo, sishangai Ben Sanane, sishangai kukamatwa kwa Wabunge na watu wengine kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haya ni mazoea! Naona ni utamaduni, kwa hiyo, hili silishangai. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninayasema haya kukwambia kwamba Serikali yako pamoja na kwamba unazungumzishwa hapo hunisikilizi, lakini sishangai na napenda tu nikwambie kwamba Serikali yako unayoisimamia ndani ya mwaka mmoja na nusu, haina amani ndani ya nchi
yako na ujue kama wewe ukiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali iko siku utaulizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mtihani, uongozi ulionao ni mtihani; uzima ni mtihani; watoto ni mtihani; madaraka ni mtihani; na iko siko utaulizwa juu ya neema hii aliyokupa Mwenyezi Mungu umeitumia vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadithi fupi tu; Nabii Nuhu aliishi katika dunia kwa miaka 950. Siku anakufa, Mwenyezi Mungu anampelekea malaika wawili kuzungumza naye, anaulizwa, Yaa Nuhu, hebu tupe habari za duniani? Nuhu akasema yeye asiulizwe mambo ya duniani, kwa sababu
hakika ya dunia ni kama nyumba, ameingia kwa mlango wa mbele akatoka kwa mlango wa nyuma. Hajui kilichomo ndani. Miaka 950, seuze sisi wenye miaka 60 na 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nizungumzie suala hili linaloitwa mgogoro wa Chama cha Wananchi CUF. Chama cha Wananchi CUF hakina mgogoro. Mimi ni kiongozi ndani ya Chama cha Wananchi CUF, naingia katika vikao vyote vya Chama cha Wananchi CUF, Chama cha Wananchi CUF kinaendesha vikao na shughuli zake kama kawaida. Unaoitwa mgogoro ambao umepandikizwa na system kwa kutumiwa Msajili wa Vyama vya Siasa na Profesa Ibrahim Lipumba, huu sisi hatuuiti mgogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo lake kubwa huu unaoitwa mgogoro kwa kutumia watu hao ni kuzuia haki ya Wazanzibari ya tarehe 25/10/2015. Hawawezi kuzuia haki hii Profesa Ibrahim Lipumba na Msajili wa Vyama na mwingine yeyote kwa sababu ni haki na maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar na haki ya WazanzibarI itapatikana muda mfupi unaokuja. Msijidanganye wala wasijidanganye katika hili, hamuwezi kuzuia haki ya Wanzibari ya tarehe 25. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie kwa kumwambia bosi wangu, keshakimbia eeh, Mheshimiwa Magdalena Sakaya juzi wakati anachangia hapa alisema anawashangaa Wabunge kwamba ni wanafiki. Nataka nimuulize na kwa sababu kakimbia lakini yupo kibaraka
mwenzie atamfikishia huu ujumbe, ni nani mnafiki? Yeye akikaa na Profesa Ibrahim Lipumba anasema kwamba…
KUHUSU UTARATIBU....
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mwongozo wako. Ninachotaka kusema, hii pilipili usiyoila sijui yakuwashia nini Mheshimiwa Jenista. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema, anapokaa na Profesa Ibrahim Lipumba anasema kwamba Profesa Ibrahimu Lipumba anamuunga mkono na wako pamoja. Akiondoka Profesa Ibrahim Lipumba anawaita Wachungaji anawaambia nimechoka kutumia pesa yangu, Mwenyekiti
akija hapa akiondoka analeta masuala mengine. Nawaomba Wachungaji mwende mkaongee na Seif Sharif suala hili limalizike ili mimi nisitumie pesa zangu, mnafiki ni nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nawaambia tena Msajili wa Vyama vya Siasa, mpango wake alioupanga taarifa tunazo asitegemee kwamba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Bismillah Rahman Rahim. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie jioni ya leo, Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize vizuri, nataka kuendelea kukushauri kwa mwaka wa pili mfululizo.

Mheshimiwa Waziri, Wizara yako ni ngumu sana na unapaswa kuwa mvumilivu sana, tenda wema uende zako usingoje shukrani.

Naanza na utalii, Waheshimiwa Wabunge wengi humu walikuwa wanachangia kila mmoja katika Jimbo lake, katika Wilaya yake anataja vivutio vya utalii ambavyo vipo katika eneo lake, lakini bado havijaanza kufanya kazi. Wengine wamesifia kwamba Rais ameleta ndege na idadi ya watalii wameongezeka, lakini hatuwezi kuvaa koti bila kuvaa shati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushauri kwamba ili kupata watalii wengi ni lazima tuwe na hoteli za kutosha, tuwe na facilities za kutosha kwa hiyo tuongeze number of rooms katika nchi yetu ili idadi ya watalii iongezeke na hilo litafikiwa baada ya kuwa na mahoteli mengi lakini pia baada ya kuweka miundombinu ya kutosha ambayo itawafanya wawekezaji wavutike kuja kuwekeza katika sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu kwa nchi yetu ya Tanzania ukiangalia vivutio vya utalii tulivyonavyo ni natural siyo artificial, lakini unaambiwa nchi yetu inaingiza watalii milioni 1,200,000 ni aibu kubwa sana. Ukiwagawa hawa kwa vivutio tulivyonavyo labda kila mtalii anaweza kwenda katika kivutio kimoja tu. Kwa hiyo, nakushauri tuwe na lengo katika kipindi cha miaka kumi ya Serikali ya hapa kazi tu, basi angalau tuwe tunaongeza milioni moja baada ya miaka 10 tuwe na watalii milioni kumi na hili linawezekana kama tutakuwa na mipango madhubuti ya kuongeza mahoteli na kuboresha miundombinu katika sekta ya utalii kule chini, hizi ndege zitakuwa hazina maana yoyote kama mgeni akifika hapa hapati huduma za kutosha kule chini, hilo la kwanza. (Makofi)

Pili, Mheshimiwa umezungumzia tu suala la utalii wa fukwe, lakini limezungumzwa sana hapa utalii wa baharini, sijaona hasa mkakati madhubuti ambao unatupeleka kwamba katika kipindi kijacho tutakuwa na hoteli ngapi za kitalii au tutakuwa na utalii wa fukwe wa aina gani. Naomba tuweke mikakati, tuweke mpango hasa madhubuti, haya maneno yasikutishe tuweke mpango madhubuti ili ukiondoka tuseme Mheshimiwa Maghembe na Naibu wake mlifanya nini, kwa hiyo maneno yasikutishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toba sikio, narudia toba sikio, nasikia kuna fees zinataka kuongezwa baada ya Bunge hili, hizo fees kama mtakubali na wataalam wako sijui kama mmeshauriana ziingie zitaua sekta ya utalii. Sidhani kama TRA ni wataalam wa sekta ya utalii, siwakatazi kupandisha kodi lakini wakae na wataalam wa sekta ya utalii waone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikia kuna fees za hunting block fees, wanataka kuweka fees asilimia 18. Kuna hunting block application fees, kuna application for hunting block transfer fees, kuna hunting permit fees, kuna conservation fees for hunters, kuna conservation for hunting observer’s fees, kuna intercompany permit fees, kuna travel handling fees, kuna professional hunting licence fees, kuna examination fees, game fees, fees for non consumptive wildlife utilization photographic tourism.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utakubali asilimia 18 katika haya unaenda kuua utalii. Naomba watalaam wa utalii wakae pamoja na watu wa TRA mkubaliane kwenye fee hizi, zikiingia zitaenda kuua utalii. Nakushauri hilo kama mtaalam ambaye nimefanya kazi katika sekta hii. Nafahamu kama mwekezaji, nafahamu kama mzalendo, nakushauri kitaalam kabisa. Serikali mkae mliangalie upya, fees hizi zikiingia zitaua sekta ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwenye hoja ya utalii, suala la makumbusho, suala la Makumbusho ya Taifa limetajwa sana hapa, watu wamezungumza sana, bado halijafanyiwa kazi. Nakuomba uwaangalie wafanyakazi, stahiki zao, mazingira wanayofanyia kazi, tumetembelea makumbusho, tumezungumza na wafanyakazi, mfanyakazi anafanya kazi pale miaka mitano hajapanda cheo, hajaongezwa mshahara, hajaenda kusoma. Wakati mwingine anafanya kazi, masaa ya kazi yanamalizika bado kuna wageni hawezi kuondoka, hana hata malipo ya over time, hili nalo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu suala la misitu na nyuki. Watu wengi hapa wameshauri kwamba tuangalie suala la mkaa, wametoa mfano wa Kilosa. Kilosa imefanikiwa lile kwa sababu wana wataalam. Ule mradi kuna wataalam wa misitu pale ndani, kwenye Halmashauri wana wataalam wa misitu pale ndani, kwa hiyo, ule mradi wa kuchoma ule mkaa endelevu ni kwa sababu wana wataalam wa misitu. Nakushauri Mheshimiwa Waziri ufanye linalowezekana Chuo cha Misitu Olmotonyi kifufuliwe ili kuweza kuzalisha wanamisitu ambao wataweza kuendeleza misitu yetu. Bila kuwa na wataalam wa misitu ambao watakuonyesha hasa mti huu unakua mahali gani, una faida gani na kwa maslahi gani? Hatuwezi kufikia hayo malengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko Kilosa mlikofanikiwa, mlifanikiwa kwa sababu wale Maafisa Misitu wanawaeleza wale wanakijiji kwamba mti huu ukiukata unatoa coppice, mti huu usiukate kwa sababu ndege ni mazalia yake. Mti huu ni mti wa asili ubakie, lakini mtu ambaye hajui yeye
atakata tu kila akiuona mti mnene ndiyo anauona huu nitapata mkaa zadi. Kwa hiyo, Chuo cha Olmotonyi kifufuliwe kitoe wataalam zaidi na siyo wanafunzi wajisomeshe wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wanyamapori. Mgogoro huu wa Loliondo, Ngorongoro naiomba Serikali kwa dhati kabisa ikae chini iamue inataka nini. Kama Serikali wanataka uhifadhi na maliasili zetu za Taifa zibaki kwa ajili yetu na kizazi kijacho basi iamue kutaka hivyo, kama Serikali inataka siasa iendelee na mchezo huu wanaoendelea nao. Suala la Ngorongoro, Loliondo linasababishwa na wanasiasa, tuwe wazi tuseme pale watu wana interest zao binafsi na hawaangalii, wakati hiyo mifugo ipo pale ilikuwa ni mifugo mingapi? Walikuwa ni watu wangapi wanaishi pale na leo ni wangapi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bismillah Rahman Raheem, nakushukuru kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa mwanzo kwa siku hii ya leo kwenye hotuba iliyo mbele yetu. Nisiwe mwizi wa fadhila nami niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Ardhi. Pongezi hizi zinatolewa kwa usimamizi mkuu wa wawili hawa au watatu hawa lakini wameshirikiana vizuri na watendaji wao ndiyo maana wakaweza kupongezwa na kila Mbunge anayesimama leo hii. Ni ombi langu kwao isije ikawa sifa ya mgema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la migogoro ya ardhi, kuna migogoro mingi sana ya ardhi hapa nchini, sina haja ya kuitaja lakini nataka nimshauri tu Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake sasa hizi sifa zao basi ziende katika kutatua haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama eneo la ardhi ndani ya nchi hii liliopimwa ni asilimia 15 ndiyo eneo ambalo limepimwa na kupangiwa matumizi ni dhahiri kwamba mna kazi kubwa ya kufanya ili kuweza kupima eneo kubwa zaidi na kupangiwa matumizi ili kupunguza hii migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa faida za kupima ardhi na kupanga matumizi zimeonekana wazi, mimi kama Mjumbe wa Kamati nilipoenda Kilombero pale imeonekana tumejifunza, tumeona na wananchi wanafaidika sana, kwa sababu ile faida ya kupata Hati Miliki ya yale maeneo yao inawafanya wao sasa kuenda mbele kiuchumi na kufaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili sasa tatizo liko wapi, sasa hapa Mheshimiwa Waziri nadhani utanielewa wewe unaelewa vizuri zaidi lakini kwa mtazamo wangu mimi ninawaomba katika Serikali ni vizuri Waziri Mkuu leo yupo mkae katika Serikali, huu mkanganyiko wa kwamba watumishi wengi wa ardhi wako kwenye Halmashauri au wako chini ya Halmashauri ama TAMISEMI wako kule, na wewe sasa unataka kuipima ardhi ili wananchi wapate hati miliki pamoja na kupanga mipango ya ardhi na hawa watu sasa hawawajibiki moja kwa moja kwako, nani atawapatia vifaa vya kufanya hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri bajeti hii iko kwako, bajeti hii iko TAMISEMI, bajeti hii iko wapi? Sasa hili kama Serikali mkae ili kusiwe na conflict of interest hapa kwenye hii Wizara ama katika eneo hili ili vifaa vya kupimia ardhi vipatikane, wataalam wapatikane, ardhi ipimwe ili kuondoa matatizo. Serikali mpo Waziri Mkuu yupo mkae kama Serikali muondoe haya mambo ya kupeleka hawa TAMISEMI, hawa wapi, hawa wapi, mimi kwa mtazamo wangu ni mipango ya kiujanja ujanja iliyokuweko hapo, wekeni wazi hii Serikali ya Hapa Kazi Tu mfanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili niendelee kukupongeza kwa namna ambavyo umeweza kutumia busara na hekima kubwa kuwahamasisha wamiliki wa ardhi wakaweza kulipa kodi ya pango, ni kitu kimoja kizuri sana kimeleta tija na kila mmoja ameona faida yake. Tunakuomba uendelee kutumia approach hii ya kuwaelimisha na siyo nguvu, wanaomiliki ardhi kama ambavyo unatumia waendelee kulipa kwa faida ya nchi hii na pato la Taifa liongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa utakapokuja kujumuisha utuambie wale ambao wanamiliki mashamba makubwa, wanamiliki ranchi lakini hawajaziendeleza, hawazifanyii kazi ni wangapi na je Serikali ina mpango gani? Pamoja na hayo nipendekeze kabisa kwamba mashamba yale makubwa ambayo hayajaendelezwa pamoja na ranchi yatumike sasa kuwagawia au kuwaazima kwa muda hawa wafugaji wakati mkiendelea kufikiria ili kupunguza migogoro na vita vya wakulima na wafugaji wakati kuna maeneo kama haya ambayo hayajaendelezwa na watu wanayamiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuongelea suala la Kigamboni, ni takribani miaka tisa sasa wananchi wa Kigamboni kwenye ule mradi wa Kigamboni nyumba zao hawawezi kuziuza, hawawezi kutengeneza, hawawezi kufanya kitu chochote wanasubiri mradi, lakini ni miaka tisa mradi haujaanza, Mheshimiwa Waziri hatujui kwamba huu mradi utaendelea kuwepo au hautakuwepo. Kama hautakuwepo wananchi wale kwa muda wa miaka tisa mmewazuia kufanya chochote mtawafidiaje na kama utakuwepo katika kipindi chote hiki mtawafidiaje. Naomba Serikali ijipange hapa ili wananchi wale muwaondoe katika ugumu ule ambao mmewapa hivi sasa, wanakaa wanasubiri mradi, miaka tisa ni mingi sana kwa maendeleo ya mtu binafsi, kwa Serikali ni kidogo, lakini kwa maendeleo ya mtu binafsi ni miaka mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la National Housing, ninaomba Serikali pia ipo, National Housing inafanya kazi moja kubwa sana na kila Mtanzania leo hii anaona kazi inayofanywa na National Housing, wanastahili sifa kweli, wanajitahidi sana. Kuna nyumba za gharama nafuu ambazo wananchi maskini wanatakiwa wanunue zile nyumba lakini ukiziangalia siyo za gharama nafuu kulingana na patol mwananchi wa Tanzania uwezo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba hizi siyo za gharama nafuu kwa sababu ya mambo mengi, moja kama kodi ya VAT kwa vifaa vya ujenzi itaondolewa kwa watu hawa wa National Housing wataweza kujenga nyumba hizo na Mtanzania yeyote ataweza kununua, lakini kama kodi ya VAT haitaondolewa basi suala hili litaendelea kuwa gumu kwao. Vilevile gharama nyingine zinaongezeka wao wanapojenga zile nyumba wanaweka gharama za kuweka maji, umeme, barabara ambazo wao wanapaswa kuweka wenyewe. Sasa Serikali ipo, kama mmeamua kujenga nyumba hizo sehemu fulani, kwa nini Serikali haipeleki maji, ikapeleka umeme, ikapeleka barabara kwenye eneo lile kabla ya watu wa National Housing hawajaanza kujenga? Serikali ni moja lakini kwa nini kunakuwa na conflict of interest?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nchi za wenzetu wanafanya hivyo, ukienda nchi zote za Arabuni na Ulaya kabla ya lile eneo kuendelezwa huduma muhimu za barabara maji na umeme zinapelekwa kwanza, barabara, maji, umeme, shule, masoko yanapelekwa kwanza halafu ndiyo nyumba zinajengwa wananchi wanaenda kuhamia pale ikiwa huduma zote muhimu zipo. Kwa nini kwenye nchi yetu inashindikana?

Kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa Waziri kwamba hili nalo mliangalie katika Serikali ili watu hawa wafanye hiyo kazi kwanza kabla ya kupeleka ujenzi katika eneo basi huduma hizi muhimu ziende ili kupunguza gharama. Mkiendelea kwamba watu wa National Housing walipe gharama za kuvuta maji, walipe gharama za kuvuta umeme, walipe gharama za kutengeneza barabara, wananchi wa Tanzania kwa kipato chao wataendelea kushindwa kuzinunua nyumba hizi na mtazijenga mtaziweka zitakuwa hazileti ile faida iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani, lakini niendelee kukupongeza Mheshimiwa Waziri nikuambie kaza kamba, narudia isije kuwa sifa ya mgema, tunategemea kipindi kijacho tuendelee kukusifu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Edwin Mgante Sannda

Kondoa Mjini (CCM)

Supplementary Questions / Answers (5 / 0)

Contributions (10)

Profile

Hon. Nimrod Elirehemah Mkono

Butiama (CCM)

Supplementary Questions / Answers (1 / 0)

Profile

Hon. Jaffar Sanya Jussa

Paje (CCM)

Profile

Hon. George Mcheche Masaju

None (Ex-Officio)

Supplementary Questions / Answers (0 / 6)

Contributions (32)

Profile

View All MP's