Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Livingstone Joseph Lusinde

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mungu kwa kupata muda, lakini mimi siyo wa kuzungumza dakika chache ila nitajitahidi maana mara nyingi huwa napiga hapa nusu saa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Dkt. Mpango kwa kuleta taarifa nzuri. Nianze na suala la viwanda mimi nizungumzie kilimo cha biashara. Ni vema Serikali ikajikita kwenye kuanzisha viwanda vidogo ili wakulima hasa wa matunda, badala ya makampuni yanayotuuzia juice kununua juice nje ya nchi, yanunue matunda yetu ya ndani. Tukifanya hivyo tutakuza na tutakuwa na kilimo cha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme watu wamekuwa wakizungumza sana humu ndani ya Bunge, wanazungumza kuhusu Polisi kuingia humu ndani. Nataka leo nisimame kuwatetea Polisi kwa sababu wao hawawezi kuja humu. Polisi ukimwona mahali popote kaenda kama Field Force, ujue ameitwa na watu wa eneo hilo. Wabunge, tuache tabia ya kuwaita Polisi, ukifanya fujo unawaita Polisi, na Polisi wameshaingia Kanisani wakati wa mgogoro ule wa Dayosisi ya Pare, Polisi wameshaingia Msikitini wakati wa fujo, Polisi wameshaingia Bungeni baada ya Wabunge wa Upinzani kuanzisha fujo. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukimwona Polisi kaingia mahali ujue kaitwa, na kama ninyi ni wageni hamuelewi utaratibu wa humu ukianzisha fujo umeita Polisi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna watu wamekuja hapa bado hawajapigwa semina, kwa hiyo ngoja leo niwaelimishe. Mmesema vizuri na mfano uliotolewa na Mheshimiwa Heche hapa mdogo wangu ambaye mimi nimemfundisha siasa, kwamba eti anataka kulinganisha Chama hiki na kina Hitler, lakini leo nawaambia Chama chochote cha Upinzani duniani kikishindwa kushinda uchaguzi katika vipindi vitatu, kinageuka kuwa chama cha kigaidi, ndiko wanakoelekea hawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ndipo wanapoekelea, maana kinakuwa chama sugu, kinakuwa Chama cha Upinzani sugu, tulikubaliana wakati ule, kwamba ili kuthamini haki za binadamu walau kila chama kitakachoshinda basi kilete mtu mmoja walau mwenye ulemavu wa ngozi. Yupo wapi albino wao hawa? Wabaguzi hawa na inawezekana hata wakati ule wa mauaji wako inawezekana walikuwa wanahusika hawa, yuko wapi? CUF waliwahi kuleta hapa alikuwepo Mheshimiwa Barwany, CCM yule pale wa kwao yupo wapi hawa? (Makofi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze hapa, kwamba usiwaone wanazungumza hivi na nataka nichukue fursa hii kumpongeza sana, nimpongeze sana Mzee Lowassa, Lowassa aligundua hawa wamemchafua sana akaamua kwenda kwao wamsafishe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee Lowasa aligundua walimwita fisadi, walimwita fisadi papa, Edward Lowasa ana akili sana. Mchawi mpe mtoto amlee, akajua nakwenda kwao wanisafishe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Mtanzania mwenye akili atakayewasikiliza tena hawa, hivi wewe unakaa na jirani yako mwanaume anakuja anakwambia mke wako malaya, mke wako mhuni unamuacha, asubuhi anamuoa utamwamini tena? Hawa hawaaminiki, hakuna kitu watakachokieleza wakaaminiwa duniani. Kwa sababu wana ndimi mbili kama za nyoka hawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachokisema leo kesho watakibadilisha hawa, ndimi mbili za nyoka…
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mnawaona leo wanasema hiki, leo wanageuka hivi, nataka nichukue fursa hii kumpongeza Jecha, kwa utaratibu huu wa kila Mzanzibar kuwa Tume ya uchaguzi, Jecha alikuwa sahihi kufuta yale matokeo. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mtu anajifanya Tume, wenyewe unaowaona hapa wameletwa baada ya Tume ya Uchaguzi kuwatangaza ila Mheshimiwa Seif wanamtangaza wao, hawa ni wanafiki wakubwa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde, nakushukuru. Muda wako umekwisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kawaida yangu, nataka nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia zawadi ya uhai, kunipa afya bora ili niweze tena kusimama kwenye Bunge lako na niweze kutoa mchango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niweke sawa kumbukumbu, katika Bunge hili kuna Wizara tatu zinachangiwa kwa mfumo wa aina yoyote mchangiaji anayotaka. Wizara ya kwanza ni Ofisi ya Waziri Mkuu, unachangia kwa hoja zozote unazojisikia Mbunge. Wizara ya pili ni TAMISEMI, unapiga kokote Mbunge unakotaka kupiga; na ya tatu ni Finance Bill, kwa hiyo, kama mtu huelewi, Mbunge ukisimama Wizara hizo, usiache kitu! Kula moto, tema madini, watu watakusikiliza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, amefanya kazi kubwa tangu ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Tuna uhakika kwamba Rais hajakosea kukupa kiti hicho Mheshimiwa Majaliwa na wala sisi Wabunge hatujakosea kukuidhinisha. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika Majimbo ya Waheshimiwa Wabunge wengi hapa Tanzania likiwepo la Mtera, kuna baadhi ya miradi imekuwa ya muda mrefu, imekuwa miradi sugu. Tufanye utaratibu wa kila Mbunge akuandikie ni mradi gani umechukua muda mrefu haujatekelezwa, tukuletee ili kuwe na bajeti maalum ya kuondoa viporo vya miradi iliyopita. Tukifanya hivyo, tutakufanya uanze sasa kutekeleza miradi mipya wakati umekamilisha ile miradi ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilisema kwenye Bunge hili kwamba, ndugu zangu hawa wamechanganya mayai yote kwenye kapu moja, tupige. Nilizungumza nikiwa mahali hapa! Leo tumepiga, si mnaona biashara imekwisha?
Kwa hiyo, niwaambie tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, kuna wengine wanasema anatafuta umaarufu; hivi ukimshinda mtu anayesema mafuriko hayazuiwi kwa mikono, wewe ukayazuia, unataka umaarufu gani tena? Mheshimiwa Dkt. Magufuli anatafuta umaarufu upi kama amekuwa binadamu wa kwanza duniani kuzuia mafuriko kwa mikono? Anatafuta umaarufu upi? Tuliwaeleza hawa na leo nataka niwathibitishie, nataka niseme na nchi, nataka niwaambie Watanzania kwamba hawa jamaa mliowapigia kelele, leo hii wameonesha wamefeli, hawana uwezo wowote hata ndani ya Bunge hawa! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Rais. Leo wanasimama hapa, watu wa Dar es Salaam mnisikilize. Anasimama hapa Kiongozi wa Upinzani anasema, Rais anafanya makosa kuamrisha pesa zilizokuwa ziende kwenye sherehe zijenge barabara ya Morocco. Wapinzani wanasema ni makosa. Hivi watu wa Dar es Salaam mnawapendea nini hawa? Hawa watu hawataki maendeleo! Wanataka domo! Mnawaona, wanataka waonekane kwenye TV wanasema bajeti ile na hela za kutengenezea barabara ya Mwanza, wanataka tukupe Mheshimiwa Nape halafu urushe live TBC ili waonekane hawa. Kutengeneza barabara na kuonekana kwenye TV lipi bora jamani?
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hapa na nazungumzia hapa kwenye ukurasa wa 11, 17 kipengele kinachohusu demokrasia. Someni hapo! Mheshimiwa Waziri Mkuu huwezi kukuza demokrasia kama una Wapinzani wa jinsi hii. Haiwezekani! Utakuzaje demokrasia katika nchi kama Wapinzani ulionao ni wa aina hii?
TAARIFA
MBUNGE FULANI: Taarifa Mwenyekiti! Mwenyekiti taarifa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde kaa!..
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kumwonya mzungumzaji anayezungumza. Mimi ni Mbunge senior na mwenye jina kubwa kuliko wewe. Unaposema kwenye Bunge hili, unamtolea mtu taarifa; wewe kama unaweza kusema umeambiwa, sema; kama hujafukuzwa Chama! Simama useme humu! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kukua kwa demokrasia. Mimi hapa nataka leo nitoboe ndiyo maana nimesema leo najitoa muhanga. Katika maisha yangu nimewahi kuwa Kiongozi; Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CHADEMA. Kule ndani kulikuwa na siri kubwa! Tulikuwa tumepanga siri wakati huo, niliyoikataa mimi, mpaka nikahama Chama hiki ya kuua Vyama vingine. CHADEMA wamefanikiwa kuua Vyama vyote hapa Tanzania.
Kwa hiyo, tunapozungumzia kukuza demokrasia tujue kwamba NCCR-Mageuzi ilikuwa na Wabunge watano na sasa ina Mbunge mmoja tu. Sijui ni maendeleo gani hayo? Wanaviua Vyama! Hawa wako kwa ajili ya kuua Vyama vingine! CUF walikuwa na Wabunge chungu nzima, sasa hivi Zanzibar sifuri. Hawa! Hawa wanaua Vyama vingine. Wanataka kubaki peke yao.
Kwa hiyo, nakuomba Msajili wa Vyama vya Siasa, endelea kusajili Vyama, ukifanya mchezo nchi hii demokrasia itakufa kwasababu kuna Chama kinataka kuhodhi Vyama vingine vyote viwe ndani yake. Hawa wanataka kufanya hivyo! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM huko nyuma tulikuwa na zidumu fikra za Mwenyekiti. Tumetoka, hawa wameingia huko. Hawa sasa hivi zidumu fikra za Mwenyekiti, ndiyo maana unaona kila wakiambiwa kitu, wanafanya. Jambo la aibu sana! Unasimama kwenye Bunge hili, unasema Serikali imevunja Katiba, haiko Kikatiba, Serikali hii imekosea, kwa hiyo, hatutasema, lakini posho wanachukua, hawa! Yaani kama ni Waislamu; kama una Muislamu anasema hali nguruwe, anakula maini tu, ndiyo hawa! Wanasema Serikali hii imekosea, haiko Kikatiba, lakini mishahara na posho wanachukua hawa. Hawako tayari kusema! (Kicheko/Makofi)
Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa nimegundua siyo tu tuna wafanyakazi hewa, tuna Wabunge hewa; hawa! Bunge hili lina Wabunge hewa! Nataka nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Nape. Wizara yako Mheshimiwa Nape ilikuwa haijawahi kuchangia maendeleo yoyote vijijini zaidi ya habari, tunasikia michezo lakini kwa mara ya kwanza, pesa ulizozizuia ambazo mmeshauri, sasa zinaelekea kuchimba visima vya maji. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka maji, hawataki kumwona Mbunge kwenye TV. Tunafahamu wamepata political mileage sana kwa sababu ya kusema mambo ya hovyo, watu wanayasikia, lakini kwa sasa watatakiwa kwenda kufanya kazi na kutoka jasho ili wananchi wawakubali. Ofisi ya Waziri Mkuu inashughulika na TASAF. Kwenye TASAF kuna malipo hewa. Wako watu wamekufa, lakini wanaendelea kupokea zile hela kama ambavyo tuna Wabunge wamekufa, hawazungumzi Bungeni, lakini wanapokea hela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi hewa wako wengi sana kwenye nchi hii, tuwashughulikie. Kuna watu hapo wanazungumza habari ya kumponda Rais kwamba anakurupuka kuchukua maamuzi. Rais, watu wote anaowafukuza na wanaosimamishwa ni kweli majipu. Kwa mfano, mchukulie ndugu yangu Kabwe. Mbunge wa Upinzani alisimama hapa, Mheshimiwa Wenje akasema Kabwe ni jipu hafai atolewe na hawa wakampigia makofi. Leo kasimamishwa, hawa wanasema anaonewa. Huwezi kuwaelewa hawa! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu wana-CCM pamoja na Waheshimiwa Mawaziri, kwa Baraza hili aliloliunda Mheshimiwa Rais, kule Mheshimiwa Majaliwa, pembeni Mheshimiwa Nape, kule kuna Mzee Handsome boy, hapa Mheshimiwa Mavunde, Mheshimiwa Jenista Mhagama; hawa hawachomoki, ndiyo maana mnaona wanapiga kelele! Mnawaona wanapiga kelele hawa, anazungumza habari ya shule wakati CHADEMA ilimsimamisha Rajabu Jumbe kugombea Umakamu wa Rais akiwa darasa la saba, wewe umesahau? Sasa kama ninyi mlitaka kuleta Makamu wa Rais darasa la saba, itakuwa Mbunge! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali. Nataka niwaambieni, katika siasa duniani, mimi ni Mwanafalsafa, nikija kufa ndiyo mtaelewa kwamba yule mtu alikuwa wa namna gani. Katika watu ambao wanajua siasa na wamefanya, nawaambieni Tanzania hatuwezi kusonga mbele. Wana-CCM tujigawe; wawepo Wabunge wa Upinzani kutoka CCM, tuisaidie Serikali. Hawa tuachane nao! Hakuna kitu wanachokifanya hawa! Tukiendelea kuwaamini hawa, tutapoteza point nyingi sana. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote, Chama cha Upinzani kinakuwa na hoja moja tu. ANC wameshinda uchaguzi pale, hoja yao ilikuwa Ubaguzi; lakini hawa umeme, barabara, maji nini, hawa Wapinzani wa wapi? Hakuna Wapinzani wa namna hiyo! Mpinzani anakuwa na hoja moja tu. Anaijenga na anaaminika kwa watu. Hawa hawaaminiki, wanazungumza kila kitu! (Kicheko/Makofi)
Nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, maendeleo katika nchi yetu kuna mikoa imechelewa kupata maendeleo kwa sababu resources zetu kuwa ndogo, igeukieni hiyo, acheni mikoa ambayo wananchi wameshiba, wanachagua Mbunge kuja kunyamaza tu Bungeni, achaneni nayo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakati wa kutekeleza hoja hii, fanyeni kazi kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia shida zao; hawa walionyamaza achaneni nao, hawana shida hawa. Mbunge anatoka nyumbani anakuja kukaa hivi, hasemi shida yoyote halafu baadaye wanakuja kwenye viti vya Mawaziri kunong’ona; Waziri mtu mzuri. Unafiki wa namna hiyo haukubaliki! Tunataka waseme wazi. Wakisimama hapa, wanakashifu Mawaziri, wanawatukaneni, halafu wanakuja kwenye kiti, naomba umeme. Tunataka maombi wanayoyaleta mezani kwenu, wayaseme wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunakufahamu, wewe ni mtaalam; umekuwa Bwana Mpango, umeongoza maeneo mengi. Tunataka safari hii, Serikali ya Awamu ya Tano, mipango yenu yote mliyoipanga na mkatupa asilimia 41 ya pesa, zishuke kwa wananchi ili maendeleo yapatikane, tuwakate mdomo hawa. Sasa hivi tutafanya!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, tutatengeneza umoja wa kutembea Jimbo kwa Jimbo kuwaambia hawa wasichaguliwe tena 2020. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumzie barabara. Ukitoka hapa kwenda Iringa, kuna kipande cha barabara ambacho Mheshimiwa Rais ameshakiahidi kutoka barabara ya lami inayokwenda Iringa ipite barabara ya lami mpaka Hospitlai Teule ya Mvumi. Naomba kipande hicho mkikamilishe ili mimi niwe Mbunge wa maisha wa Jimbo lile. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, katika wanasiasa wanaoniuma; nazungumzia demokrasia, lazima niwe mkweli; ananiuma sana kaka yangu Mheshimiwa James Mbatia. Mheshimiwa Mbatia ni mwanasiasa wa siku nyingi kuliko Mheshimiwa Mbowe. Sijui kalishwa nini, siku hizi anaambiwa na Mheshimiwa Mbowe, nyamaza! Naye ananyamaza kweli! Ananyamaza! Yaani sielewi kilichotokea!
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mbatia ni Mwanasiasa wa siku nyingi, Chama chake kilikuwa na Wabunge watano. Akanambia yeye amesoma, mimi sijasoma, sasa anakwenda mbele. Kutoka watano kuja mmoja! (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde inatosha kwa leo, muda wako umemalizika!
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Kweli hata mimi ambaye sijasoma siwezi kufanya ujinga kama huo! Hata mimi ambaye sijaenda shule, siwezi kufanya kitu cha namna hiyo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Hawa tunawamudu, hamna kitu na tutahakikisha tunawafagia. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo na mimi niweze kusema mambo machache ya muhimu kuhusu hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kaka yangu Mheshimiwa George Boniface Simbachawene. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ameonesha namna gani anataka kuirudisha Tanzania kwenye msimamo hasa wa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu. Kwa sisi Wagogo tuna usemi unasema; mdabula nhili mwana na kalanga ganyina mmeso. Ukitaka kuonja uji wa mtoto, mtazame kwanza mama yake usoni. Ukimwona namna alivyokaa, unaweza ukaamua aidha, uonje au usionje. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Magufuli ameonesha yuko makini na mkali sana kwenye matumizi ya hovyo hovyo. Nataka niseme haya mnayoyaona wengine kushindwa kumwelewa ni kwa sababu Rais Magufuli amewashangaza wengi katika utendaji wake wa kazi. Ndiyo maana mtasikia mengi! Mtasikia Katiba imevunjwa, mtasikia nini! Kwa sababu wengine hawana namna ya kusema, inabidi waseme hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri, tunakufahamu kwa msimamo wako Mheshimiwa Simbachawene. Tuna hakika utaitendea haki kama ambavyo umeonesha tangu mwanzo Wizara hiyo, ni Wizara kubwa, tuna hakika mkijipanga vizuri na Jafo kama mlivyokaa, mna uwezo wa kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele. Tunawapa big up, tunawaomba mwendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme maneno machache hapa. Tunapozungumzia pengine kuna mtu hapa ameshindwa kuelewa anasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali anatafsiri mambo ki-CCM. Ndugu zangu, nchi hii Ilani inayotekelezwa ni ya CCM. Nchi hii hakuna Sera ya Serikali peke yake tu inayojiendesha! Mlikataa wakati wa Bunge la Katiba. Tulipowaambia tuwe na Sera ya Serikali tuachane na Sera za Vyama, mkakataa! Leo tumeenda kuuza sera kwa wananchi; CHADEMA walikwenda nayo, CUF walikwenda nayo na CCM walikwenda nayo. Wananchi wamechagua ya CCM. Sasa mtu anaposema unaongea ki-CCM hata wewe Mbunge unatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Tuelewane hapo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wala tusitake kuzungumza hapa vitu kama vile tunaimbiana mapambio. Upinzani watakuwa wanafanya kazi kama vile ambavyo tunaweza tukasema, wanafanya kazi waki-support kazi ya shetani, kwamba unapinga lakini wenzako wanaotawala wanafanya kazi ya Mungu. Wakati unaeleza upungufu, kwanza unashukuru kwa vichache vilivyotolewa. Hawa kazi yao ni kuponda, halafu baadaye wanaomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kazi yetu ni kusifu baadaye tunaomba. Wote kazi yetu ni moja, lakini utajiuliza mwenyewe, je, wa kuponda anafurahisha? Maana kwanza anaponda, halafu baadaye anapiga mzinga. Sisi tunasifu baadaye tunapiga mzinga. Kwa hiyo, tunafanya kazi ya Kimungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namwomba Mungu sana, anipe uwezo watu wanielewe. Sitaki kuingia kule kwenye siasa ambazo watu wamepanga; anasema tu kwa sababu Lusinde tumemwona, yeye anataka kuhamisha vita kutoka kwa Mawaziri kuja kwake; tutampakazia! Wewe useme kwamba Lusinde amepigiwa simu ya Mheshimiwa Rais, kaambiwa asiwatetee. Mimi Wakili? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Wakili, sifanyi kazi ya Mahakama na wala simtetei mtu yeyote katika Mahakama yoyote ya nchi hii. Kwa hiyo, unaweza ukaona; na mimi nataka niwaambieni mkitaka kuleta siasa za uzushi mimi ndiyo natisha kwenye upande huo. (Makofi)
Nirudie tena kuwaonya, mimi mtu kunitaja namruhusu kwasababu hili jina kubwa na nimelitengeneza kwa gharama kubwa. Kwa hiyo, kuna watu watajitahidi kutaka kulifikia jina hili, lakini ni kazi ngumu sana. Waitara nimemfundisha siasa akiwa CCM, leo tena yuko CHADEMA nitaendelea kumsaidia taratibu lakini asifikie huko; Rais ni matawi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, humu ndani tunafanya kazi mbili tofauti. Wako Wabunge ambao kazi yao tangu anasimama mwanzo, ataponda halafu mwishoni anakuja kwenye kiti, nisaidie maji. Yupo Mbunge atasimama, atasifu halafu baadaye atatoa shida zake. Ndiyo tofauti! Ninyi Mawaziri mtapima, yupi anayezungumza vitu vya msingi? Mtapima maana mimi siamini, hata kutafuta mchumba umkute msichana wa watu, umwambie dada una sura mbaya, lakini naomba nikuoe. Akikubali, ujue huyo hana akili. Hana akili huyo! Lazima umsifu kwanza! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewaeleza juzi kwa uchungu sana, nikasema nchi yetu tunajenga demokrasia, tuangalie kwa umakini sana. Hii nchi inapita kwenye mawimbi makubwa ya kujengwa demokrasia. Tunapojenga demokrasia, ni lazima hivi vyama tuvipe uhuru mkubwa wa kufanya mambo yao kama ambavyo tunafanya. Ndiyo maana nikawashtua wenzangu, Chama cha CUF, nikawashtua NCCR Mageuzi; siamini kwamba katika ndoa waliyonayo wanajenga demokrasia. Naamini wanakwenda kuuawa! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaweza kumwona Mheshimiwa Zitto hana akili, yuko peke yake, lakini nawaambia katika miaka ijayo, pengine chama chake ndiyo kitakuwa maarufu kuliko vyama vingine hivyo. Maana kinapata muda wa kufanya siasa. Leo kuna watu wanazuiwa na Mwenyekiti, usiseme; wanakaa kimya. Sema, wanasema! Watu wa namna hii ni watu wanaoendeshwa kwa remote, hawawezi kuwa wanasiasa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia Tanzania ina Chama cha Upinzani pengine kimoja tu, ACT, vingine vyote ni vyama shindikizo. Ni Vyama vinavyokwenda na hoja. Meli ikizama, wanahamia kwenye meli; ikitokea kashfa, wanahamia kwenye kashfa. Serikali hii inaziba kila kitu. Wamehamia kwenye tv live. Hebu ngoja nizungumze kidogo hapa! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wasomi mnasema nchi ina Executive, Parliament na Judiciary, hebu tujiulize; mbona Executive mambo yao hayaoneshwi live kila siku? Nayo ndiyo Executive inayoongoza nchi! Mbona hatuoni live kila siku mambo ya Ikulu? Mbona hatuoni Mahakimu wakiendesha kesi live kila siku na wao ni mhimili? Mbona hatuoni Majaji Mahakamani wakiamua mashauri wakiwa live na wao ni mhimili? Iweje watu wang’ang’anie mhimili mmoja? Huku ni kufilisika! Watu wamefilisika, hawana nafasi, wanataka kwenda kujitangaza kwa njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema leo nitoe somo. Katika nchi yenye mfumo wa vyama vingi tuangalie hivi vyama, tuangalie hata aina ya Wabunge. Mimi nawaambia tutakwenda mahali tutajikuta tunatumia resource kubwa, kupoteza muda hapa, hatuisaidii Serikali. Kwa hiyo, naomba niwaambie Waheshimiwa Mawaziri, tunapokuja kuwaambia shida zetu na juzi nilisema, hapa mnatukanwa, mnadharauliwa, halafu wakija wanasema naomba maji. Leo nchi ielewe hakuna Jimbo lolote la mpinzani linalopelekwa maendeleo. Maendeleo katika Majimbo yao tunapeleka sisi CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ndio tunakubali bajeti itekelezwe. Leo tunamwomba Waziri wa maji apeleke maji Moshi, Arusha; Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa huo wanakataa. Mwisho wa siku wanasema tumeleta maendeleo. Unaleta maendeleo kwa kusema hapana? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ifahamu maendeleo yanaletwa na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Aah, niendelee! Niliona Mheshimiwa Mch. Msigwa amesimama nami namheshimu kwa sababu nimeoa kwao. Unajua mimi nimeoa Iringa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu waelewe hata barabara zilizojengwa Iringa Mjini aliposimama Mheshimiwa Msigwa, mimi nilitetea humu ndani ya Bunge. Maana mke wangu anatoka pale.
KUHUSU UTARATIBU.......
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru na nimshukuru hata Mheshimiwa Mch. Msigwa. Mheshimiwa Msigwa na mimi hatujawahi kupingana, sijui leo kimemkuta nini? Mimi juzi nimemwacha ameongea propaganda zake hapa, lakini leo yeye kashindwa kuvumilia. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa George Simbachawene, Mheshimiwa Waziri kupitia Bunge hili, aitazame Halmashauri mpya. Tumezungumza kuhusu mgawanyo wa nchi yetu. Tumeomba Halmashauri mpya ya Mtera, lakini atazame hata jina la Jimbo la Mtera. Kata ya Mtera iko kwako, Kijiji cha Mtera kiko kwako, mimi naitwaje Jimbo la Mtera? Haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikasema Mheshimiwa George hakuna sababu ya Jimbo langu kuitwa Jimbo la Mtera. Unanipa jina la utumwani. Mimi ningependa Jimbo langu liitwe Jimbo la Mvumi ambako anatoka Chifu Mazengo. Kwa hiyo, naomba Halmashauri yetu uitazame, Jimbo letu libadilishwe jina, lisiitwe jina la kijiji kilichoko kwako, kwa sababu sisi hatuwezi kuitika kwako. Watu wengi wanafikiri sisi tuko Mtera; Mtera ni ya George Simbachawene. Sielewi mzee alipoiita, aliita kwa sababu gani.
Mheshimiwa Mweyekiti, naomba kwenye Bunge hili uturudishie majina ya kwetu ya asili. Sisi pale tuna Mvumi karibu ziko 20. Kwa hiyo, ungetuita Jimbo la Mvumi ungekuwa umetutendea haki zaidi kuliko kutuita Jimbo la Mtera ambalo liko kwako wewe Mheshimiwa Simbachawene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunaloliomba, kuna barabara za TANROADS na kuna barabara za Halmashauri. Halmashauri nyingi hazina uwezo wa kujenga barabara ndefu.
Kwa hiyo, naomba kwa niaba ya Wabunge wenzangu, angalia kila Jimbo lenye barabara ndefu, badala ya kuiachia Halmashauri ambayo haina uwezo, zipandishwe hadhi ziende TANROADS ili ziweze kutengenezwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza hivi kwasababu tuna uzoefu; kuna barabara nyingine Halmashauri hazina mapato ya kuweza kutengeneza urefu wa hizo barabara, lakini mkiwapa TANROADS wana uwezo. Kwa mfano, chukulia barabara inayotoka Dodoma Mjini. Kuna barabara inatoka Dodoma Mjini, inapita moja kwa moja kwenye Jimbo la Bahi kwa Mheshimiwa Badwel, inaenda moja kwa moja tena kwenye Jimbo langu la Mtera, halafu ndiyo inaenda kupakana ng’ambo kule kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ile barabara tuipandishe hadhi iwe barabara ya Mkoa kwasababu inapita kwenye Manispaa na kwenye Halmashauri mbili. Ukipata hela Chamwino ukitengeneza kipande, wenzako Bahi wanakosa, panabaki mashimo; kunakuwa hakuna mtengenezaji. Kwa hiyo, naomba kupitia Wizara yako, barabara tulizoziombea zipandishwe hadhi, mzipandishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie, kuna Halmashauri nyingine, kata nne Halmashauri; kata tatu Halmashauri; hebu tuangalie, sisi tuna Jimbo lina kata 22. Tumeomba tugawanywe Wilaya, mkasema hapana tutawapa Halmashauri. Tupeni Halmashauri ili tuweze kusukuma maendeleo mbele. Tunataka kuendelea kufanya kazi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tulisema…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Aaah, naendelea, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. Naona jamaa wanasema umemaliza. Ahsanteni, nimemaliza.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kubwa, kunipa zawadi ya uhai ili nami nisimame leo kuchangia katika Bajeti ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamekupongeza kwa umahiri wako wa ufanyaji kazi, lakini nataka nifafanue kidogo. Kuna kipindi watu wanachanganya sana hizi mada. Wapinzani walipotaka kuelezea kutoridhishwa kwao na Naibu Spika, kwanza walianza kuzungumzia habari ya uteuzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo Mbunge wa kwanza kuteuliwa na Rais wa nchi yetu. Katika Bunge lililopita Mheshimiwa James Mbatia alikuwa Mbunge wa kuteuliwa na Rais na hapo ndipo alipopatia na mtaji wa kugombea Ubunge; lakini siku zote tulikuwa tunamwita Mheshimiwa Mbunge na Wapinzani walikuwa wanamwita Mheshimiwa Mbunge Mbatia. Hakuna mtu aliyemwita ndugu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo wamekuja na hoja nyingine tena; imekuwaje umetoka kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ghafla, umeingia na kuchaguliwa kuwa Naibu Spika? Nikawaambia tu, ndugu zangu, mbona Mheshimiwa Tulia alishaoneshwa njia na Mzee Lowassa? Mheshimiwa Lowassa Jumatano katoka CCM, kahama; Alhamisi ni Mgombea Urais CHADEMA. Mheshimiwa Tulia naye alitumia ile ile! Amechomoka kwenye Unaibu Mwanasheria Mkuu, amezama Bungeni – Naibu Spika wa Bunge.
Tena kwa kupigiwa kura, wala siyo kwa kuteuliwa. Wewe tumekuchagua sisi. Mheshimiwa Rais alikuteua kuwa Mbunge, lakini nafasi hiyo tumekupa sisi Wabunge. Siyo kwamba Rais amesema Mheshimiwa Dkt. Tulia awe Naibu Spika, aah, tumesema sisi kwa kukuamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo lingine ambalo watu wengi wamelisahau. Tanzania imezalisha viongozi wanawake wengi mahiri. Akina mama Mongella tunakumbuka, walikuwepo akina Bibi Titi Mohamed, wapo sasa hivi akina Samia Suluhu Hassan, akina mama Magreth Sitta; wamefanya kazi kubwa kwenye nchi hii. Leo nataka niwaambie msifikiri Wapinzani wanakimbia tu, kushindana na kiongozi shupavu mwanamke siyo kazi rahisi. Ni kazi ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaambia wakajifanya mahiri wa kujenga hoja za kisheria, sijui wana uwezo mkubwa; huyu ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaani amebobea kwenye nafasi hiyo. Kwa hiyo, walipoona yameshindikana, ndiyo unaona wanachomoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, duniani wanaume ndio tumeshika nafasi kubwa ya kuwa viongozi mahali pengi, lakini ikitokea mwanamke akapata nafasi, ogopa! Angalia akina Magraret Thatcher, amekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza pale. Mwangalie Indira Gandhi, amekuwa Waziri Mkuu wa India pale; mwangalie Golda Meir, amekuwa Waziri Mkuu wa Israel. Hawa ni akinamama wachache waliofanya mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nikuhakikishie kwamba unakoelekea ni kuzuri. Komaa, endelea kufanya kazi nasi tunakuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Bajeti ya Serikali. Waheshimiwa Wabunge wamesema kwa uchungu sana, tunakuomba Mheshimiwa Waziri; tumefikia kipindi ambacho makusanyo sasa ni makubwa. Impact ya makusanyo yenu yatakuwa na maana sana kama yatashuka kwa wananchi wa chini maskini. Vinginevyo, hata mkijisifu kukusanya itakuwa haina maana. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais anabana matumizi, Serikali nzima inabana matumizi, lakini mategemeo yetu ni kuona bajeti hiyo ni kwa namna gani itashuka kumaliza matatizo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamesema habari ya kujichanganya kwenu hapa. Amesimama Mheshimiwa Waziri hapa anasema amefuta ushuru. Hao vijana mnaotaka tuwainue kiuchumi, mwaka huu ndio wamelima ufuta na alizeti. Leo bado kuna mageti ya vijana kuchangishwa kutoka kwenye kilimo chao duni walicholima, siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufuta umeshuka bei, alizeti haina bei, halafu mageti ya kuwachangisha ushuru mkubwa. Hili mlitazame, linatupaka madoa Waheshimiwa Wabunge tuliotoka kwenye Majimbo ya vijana wakulima. Watu wanataka kuinuka kiuchumi. Kwa hiyo, naomba Serikali wakati wa kutoa majibu ilisemee hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia habari za Zahanati hasa za Vijijini, zinahitaji pesa. Akinamama wengi wanaojifungua wanapoteza maisha yao kwa kukosa vyumba vya kufanyia upasuaji kwenye hospitali zetu za Kata. Tumesema tuwe na Vituo vya Afya kwenye kila Kata. Vituo vile havina theatre maalum ya kuwafanyia upasuaji akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Soika, kwa hiyo, inatupa shida na Kata nyingine zina kilometa ndefu sana kutoka Kata moja kwenda Kata nyingine. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, asukume fedha kwenye Wizara muhimu; Wizara ya Afya na Wizara ya Maji ili kuweza kuwapunguzia usumbufu wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchezo wa kuigiza unaofanyika kwenye nchi yetu ni wa ajabu sana. Mwaka 2015 tulikuwa na mashindano ya kisiasa ya nchi nzima. Kila mwanasiasa maneno aliyokuwa nayo aliyasema. Wananchi wamepiga kura, siasa zimehamia Bungeni. Haiwezekani tena ukakimbia Bungeni ukaenda kuwaambia wananchi yanayoendelea Bungeni, wamekutuma kazi hiyo? Hili lazima niweke sawa! Serikali haiwezi kuleta maendeleo kama nchi haina utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nchi lazima iwe na utulivu, iwe na amani yake ili hayo makusanyo ya Serikali yanayotafutwa yaweze kuwafikia wananchi. Kwa hiyo, hiki kiini macho kinachotumiwa na Wapinzani kwamba tunaenda kuwaambia wananchi yanayotokea Bungeni, tuko Wabunge wa Majimbo, hiyo tutaenda kuwaambia wananchi wetu waliotutuma! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kila Mbunge akafanye kazi kwenye Jimbo lake. Hivi, Mbowe anavyosema anaenda Kahama, Kahama kuna Mbunge wa CHADEMA? Kwa nini asiende kuwaambia wananchi wa Hai? Aende akawaambie wananchi wa Jimbo lake; lakini kwenda Kahama ambako hakuna Mbunge wa CHADEMA, ni uchokozi na ni kuwapotezea muda wananchi wa Kahama wasifanye kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kuhusu udikteta. Hili sitaki kuficha, moja ya viongozi madikteta kwenye nchi hii ni pamoja na Mheshimiwa Mbowe. Anawatoa Wabunge kwa nguvu. Waheshimiwa Wabunge wako hapo kwenye chai, wamenituma nije niwasemee humu ndani. Wameniomba, wamesema, Lusinde, kuna mambo sisi hatuwezi kumwambia Mbowe, nenda kamwambie.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kumwambia Mheshimiwa Mbowe warudishe Wabunge ndani ya Bunge! Usiwanyanyase! Anawapigia simu wakae kwenye chai badala ya kuingia Bungeni. Tabia gani hiyo? Hiyo ni kutumia Uenyekiti vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya siyo maamuzi ya Chama ndugu zangu, tusiwalaumu. Hawa wamepigiwa simu, wamekatazwa; atakayeingia atapewa adhabu. Kwa hiyo, wako kwenye chai, wameniomba; nenda katusemee Bungeni, sisi hatuwezi kusema. Najua huko waliko wananipigia makofi kwa sababu natekeleza agizo walilonituma. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendeleza siasa uchwara za kufanya fujo wakati Serikali imeshapatikana, tutamnyima fursa Mheshimiwa Dkt. Magufuli ya kuwahudumia Watanzania. Tumpe nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, wengi hapa mnajua mpira; mpira una sheria zake. Hivi mchezaji wa Simba au wa Yanga anapewa kadi nyekundu kwenye mchezo wa mpira, Wanayanga wanaweza kuandamana nchi nzima kupinga? Haiwezekani! Mbunge akipewa kadi nyekundu ndani ya Bunge, ni kwa kufuata kanuni za ndani ya Bunge, siyo nje ya Bunge. Haiwahusu wananchi hiyo. Hiyo inatuhusu wenyewe; tumewekeana sheria, tumewekeana kanuni; Mbunge akifanya kosa hili, red card, anatoka nje. Hiyo huwezi ukaandamana nchi nzima kwenda kuwaambia ooh, demokrasia inaminywa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna demokrasia isiyo na mipaka. Demokrasia isiyo na mipaka ni fujo. Tunaitaka Serikali isimamie amani, Serikali idumishe utulivu ili pesa zinazokusanywa ziende ziwahudumie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya usambazaji wa umeme. Mkisambaza umeme kwenye vijiji, mnainua uchumi na mnapunguza msongamano mijini. Leo kama kila kijiji kitakuwa na umeme; kila kijiji wananchi watakuwa wamejiwekea pale miundombinu ya kujiletea maendeleo, wana sababu gani ya kwenda Dar es Salaam? Hawana sababu. Kwa hiyo, hata ile foleni ya Dar es Salaam itapungua na hayo yote yatafanyika kama nchi ina utulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mjumbe wa Kamati ya PAC, hapa nataka ku-declare interest. Naiomba Serikali badala ya kupeleka bajeti ya shilingi bilioni 72 kwa TAKUKURU, waitazame Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Leo unawapa shilingi bilioni 34 na point ngapi sijui, siyo sawa. Huyu ndio Mkaguzi. Huyu ndiye anayekwenda kuwaonesha TAKUKURU hapa kuna wezi. Huyu ndiye anayekwenda kuonesha ubadhirifu, ndio jicho la Bunge. Kwa hiyo, naomba, sisi Wabunge kwa kulithamini jicho letu, tunaomba jicho lisafishwe, liwekewe dawa, liwekewe miwani ili likawaone wabadhirifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali iwe makini kwenye ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge tunapoomba, Serikali itusikilize; Ofisi ya CAG ni Ofisi kubwa. Ndiyo Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali; akikosa pesa hawezi kufanya kazi hiyo.
Kwa hiyo, tunawaomba waongezewe pesa ili wakafanye ukaguzi ili hata hiyo Mahakama ya Mafisadi iende na ushahidi. Hawa wasipofanya kazi yao vizuri, wote mtakaowashtaki watashinda kesi kwa sababu kutakuwa hakuna ushahidi wa kuaminika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme, kwenye Bunge, tunapokutana Waheshimiwa Wabunge, yanakutana Majimbo yote kuzungumzia maendeleo ya nchi nzima. Wabunge wa CCM tunao wajibu; sisi ndio tumepewa dhamana na wananchi wa Tanzania kuongoza nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Wabunge wao wanapokosa hoja za msingi, tusimame kutetea Majimbo yale kwa sababu yana wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutakapofika, wananchi watagundua, wananchi sio wajinga, watagundua kwamba amekuja Mheshimiwa Rais, anafanya mabadiliko ya vitendo; Mheshimiwa Rais anapozungumza, unamwona mpaka macho yanalenga lenga machozi kwa uchungu alionao. Watu wanamwona, wamemwamini, leo hawa wamekosa hoja wanapokimbia nje kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Mbowe, inawauma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi Waheshimiwa Wabunge wa CCM tuzibe lile pengo kuhakikisha kwamba tunayasemea Majimbo yao, wananchi watusikilize kwamba Iringa ipelekewe maji, kwamba Kigoma ipelekewe maji na miundombinu ijengwe na Moshi Mjini pale patekelezewe miradi yao. Hiyo ndiyo kazi tuliyonyo Wabunge wa CCM maana sisi ndio mama, sisi ndio baba, sisi ndiyo tumeaminiwa na wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kweye miradi ya maendeleo. Kwa mara ya kwanza, Serikali imetenga asilimia 40 kwenye bajeti ya maendeleo. Miaka yote Wapinzani wamekuwa wakilalamika, bajeti ya maendeleo ndogo, hakuna pesa zilizotengwa; lakini mwaka huu Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Serikali yake amekuja na asilimia 40 ya maendeleo…
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na namshukuru sana Mheshimiwa Kanyasu kwa kuniongezea dakika zake tano kwa niaba ya nchi hii, nami naendelea sasa kupiga dawa taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tujifunze. Kama nchi inataka kufanya siasa za ustaarabu, tufanye siasa za ustaarabu. Tusiige kila kinachofanywa na watu wengine na sisi tukakileta hapa Tanzania, haiwezekani. Hata mashindano ya ma-miss tu, yakiisha, hakuna ugomvi tena. Hakuna mtu anapita kujitangaza kwamba yeye mzuri kuliko aliyechaguliwa, hakuna! Wanakuwa wamemaliza. Siasa za Tanzania ni siasa gani ambazo hazina muda? Lazima tuwe na muda wa kampeni, ukiisha tumwachie Rais atekeleze kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa sababu tukiendeleza tabia hii, nataka niwaambie, itakuwa ndiyo Taifa peke yake ambalo watu hawafanyi kazi, wanafanya siasa muda wote. Haiwezekani! Lazima tuwe tunajitenga. Tukimaliza kampeni, viongozi wamechaguliwa, tunawapa fursa ya kutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais aliyeko wa Awamu ya Tano, slogan yake na msimamo wake ni Hapa Kazi Tu! Anachotaka ni watu wafanye kazi. Watu tufanye kazi, siyo turudi kwenye majukwaa tena sijui ooh, Dkt. Tulia kafanyaje! Haiwezekani. Mheshimiwa Dkt. Tulia hawezi kuwa msingi wa Wapinzani kutoka; wamekimbia kwa sababu hoja haipo. Mheshimiwa Mbowe ametumia nafasi hiyo vibaya kuwaambia sasa tokeni, kaeni kwenye chai mpaka mtakaponisikiliza. Huo ndiyo uongozi bora? Siyo uongozi bora! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia uongozi bora, tunazungumza kwa wote sisi, ndiyo kodi yetu inatumika kulipa Upinzani, kulipa Chama kinachotawala na kuleta maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, mchango unapokosekana, lazima CCM tuzibe lile pengo, kama ambavyo imetokea Kambi Mbadala. Huo ndiyo wajibu wetu na tuwaambie wananchi kwamba kinachofanywa na Wapinzani siyo kweli, siyo sahihi. Hata viongozi wa dini wanajua, akishachaguliwa Mufti, hakuna uchaguzi mwingine tena. Anaachiwa Mufti aongoze. Akichaguliwa Askofu, hakuna uchaguzi mwingine wa Askofu. Anaachiwa aliyechaguliwa afanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachotaka kufanyika kupitia upinzani, ile ni fujo; kuiweka nchi katika fujo za maandamano yasiyo na msingi. Haiwezekani! Serikali isimamie amani, isimamie haki, isimamie maendeleo kwa nchi nzima. Mbunge anayejisikia kwenda kuwaambia wananchi wake kaonewa Bungeni, akafanye kwenye Jimbo lake, siyo kwenye Jimbo la Mbunge mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge yeyote akitoka hapa Bungeni naye ataenda kueleza nini tumepata, nini Serikali itafanya katika miaka mitano. Hatuhitaji msaada toka kwa Mheshimiwa Mbowe wala kwa mtu mwingine yeyote. Pale Kahama yuko Kishimba wamemchagua, atakwenda kuwaeleza yanayotokea hapa. Hatuhitaji msaada wa mtu mwingine. Hatuwezi kufanya siasa muda wote, haiwezekani. Tunafanya siasa, tukishamaliza, siasa zinahamia Bungeni, wananchi wanachapa kazi kuleta maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumza kidogo kuhusu kiinua mgongo. Waheshimiwa Wabunge, naomba mnisikilize. Naamua nijitoe muhanga kwenye jambo hili. Kujitoa kwangu muhanga ni hivi, hili jambo Serikali imesema kama yatakuwepo hayo makato, yatakatwa 2020. Sisi tunahoji kwamba kwa nini hoja hiyo muilete saa hizi? Sisi hatuitaki saa hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, jambo hili tukae wote. Serikali hii ni ya kwetu na sisi ni Wabunge tunaoongoza nchi hii. Wananchi wasije wakatuelewa vibaya wakafikiri sisi hatutaki kuchangia maendeleo, hapana. Moyo wa kuchangia maendeleo na sisi tunao. Tunachosema, jambo hili linahitaji mazungumzo, twende tukae, tukubaliane, utaratibu gani utumike ili kuweza kusonga mbele, wala siyo la kubishania hapa. Wala hatuwezi kusema hatutaki, haiwezekani. Huu ni ushauri wa Serikali na sisi hatuwezi tukailazaimisha Serikali kwa nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashaurini kwamba jambo hili linahitaji mjadala wa pande zote mbili. Waheshimiwa Wabunge, tunalipa kodi, tunakatwa kwenye mishahara yetu. Kama mnataka kuendelea mbele kukata tena gratuity, tuzungumze, tuone impact yake, maendeleo yatakavyosukumwa, wala siyo jambo la kubishania hapa. Jambo hili ni zuri. Isije ikachukuliwa kwamba Waheshimiwa Wabunge wote wanapinga kukatwa hela zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie, kuna waandishi wanasema, Waheshimiwa Wabunge wa CCM, imewauma kusikia wanakatwa hela. Mimi haijaniuma, niko tayari hela yangu ikatwe, lakini kwa mazungumzo. Tuone hiyo hela inakatwa kuelekea wapi na utaratibu gani utatumika ku-balance jambo hili ili liweze kuleta afya badala ya malumbano hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ni yetu wote. Siyo kazi yetu kuwashtaki wengine kwamba viongozi wote wa kisiasa lazima wakatwe. Hiyo siyo kazi yetu. Kazi yetu sisi ni kuangalia kitakachopatikana. Kama hakitoshi, ndiyo tutashauri Serikali sasa iangalie na viongozi wengine ili kuongeza mfuko, maendeleo yaweze kupatikana. Tusikae tunabishania hapa, tunabishania kitu gani? Kwa sababu juzi hapa tumeondoa matangazo live ili pesa itakayopatikana iende kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na hoja za msingi hapa, tukasema anayetaka kurusha live, hata harusi siku hizi watu wanarusha live; kalipie mwenyewe. Nenda lipia pale TBC, mtakapopewa dakika 15, rusheni live wananchi wako wakuone. Mbona tulipitisha na tukakubaliana? Hili lisilete ugomvi. Hili ni jambo dogo sana. Tunahitaji muda wa kuzungumza na Serikali kukubaliana juu ya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Mbunge anayepinga Bungeni, sijui kumekucha, sijui Waheshimiwa Wabunge wameamua kumkatalia Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Mheshimiwa Dkt. Magufuli tumemchagua sisi, ni Rais wetu, tutamuunga mkono kwa hoja yoyote atakayoileta humu ndani, tukiwa na imani kwamba Rais hakosei. Rais hawezi kukosea. Nia yake ni njema katika kuitumikia nchi hii. Anataka Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote turudi katika mstari sawa. Kama Mheshimiwa Mbunge ulikuwa unakunywa bia kumi, kunywa moja ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna mwezi Mtukufu huu, Waislamu wamefunga, wanaweza kuombea nchi hii watu wakaachana kabisa na ulevi. Nawahakikishieni kabisa, tutapata maendeleo makubwa ya kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kuwatia moyo sana Waheshimiwa Mawaziri, Dkt. Mpango na dada yangu pale, fanyeni kazi. Tuna imani na nyie. Mheshimiwa Rais anawaamini na sisi Waheshimiwa Wabunge tunawaamini. Tutafanya kazi kwa mshikamano kuhakikisha nchi hii inasonga mbele bila mikwaruzano, bila nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa nimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi na kunijalia zawadi ya uhai ili niweze kusimama kwenye Bunge lako Tukufu niweze kutoa mchango wangu kwa Wizara hii ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza hii ni kwa ajili kuweka rekodi vizuri tu, nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wananchi wa Iringa na hasa makanda wa Chama cha Mapinduzi wa pale Iringa Mjini. Kumbe walifanya kazi nzuri sana ya kumkaba mpinzani wao mpaka leo anaonesha kwenye Bunge hili kwamba ushindi wake ni ajabu sana hakuutegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa hii ya Kambi Rasmi ya Upindani, unaona kuna vitu vimeandikwa kijinga kabisa. Moja ya kitu kulichoandikwa kijinga neno Mungu anaandikwa kwa herufi ndogo mimi sijawahi kuona mahali popote pale, ukitaka kutaja Mungu lazima uandike kwa herufi kubwa. Kwa hiyo, uchungaji wa Msigwa unanitia mashaka makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia Chuo cha Diplomasia. Chuo cha Diplomasia ni chuo kinachofanya kazi kubwa sana ya kuwaelimisha, kuwafundisha, watu, wananchi wanaoteuliwa kuwa mabalozi, wake wa viongozi, Wakuu wa Nchi, ili kuweza kujua diplomasia inafanyaje kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali itenge fedha ya kutosha kwa chuo hiki ili kiweze kufanyakazi yake kwa ufanisi na nimuombe Waziri atakaposimama hapa kutoa majibu atueleze ni fedha kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya chuo hiki ili kiweze kufanya kazi yake kwa ufanisi.
Tunasemwa maneno mabaya lakini tunavumilia mpaka wasemaji wamalize, lakini sisi tukitaka kujibu kidogo unasikia kelele za kuwashwa washwa upande wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme moja ya diplomasia kubwa iliyojengwa katika nchi yetu ni kuwa na upinzani japo kwamba upinzani wenyewe ni dhaifu. Tunao upinzani lakini ni dhaifu hata kwenye kujenga hoja. Mtu anasimama hapa kuzungumzia habari ya Mabalozi hawafanyi kazi, anasimama hapa kuzungumzia habari ya Rais haendi nje. Tulikuwa na Rais Kikwete, anasafiri kila siku. Hawa walisimama Bungeni hapa kusema kwamba Rais anasafiri sana, Rais anatumia fedha nyingi, leo tumempata Dkt. Magufuli, Rais anabana matumizi, fedha zinaelekezwa kwenye maendeleo, hawa wanasimama kupinga, watu gani hawa. (Makofi/Vigelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanataka tufanye nini, leo nataka niwaambie ndugu zangu kweli kazi kubwa ya upinzani ni kupinga lakini sio huu, huu ni upinzani hewa kwa sababu hakuna wanachopinga, wao wenyewe wanaingia wanasaini wanaondoka bila kufanya kazi, leo hii wanataka kusema kwamba nchi hii haina demokrasia wangekuwepo hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo upinzani wa Tanzania naufananisha kama mtoto mchanga tumboni. Mtoto mchanga tumboni haelewi ukubwa wa dunia. Kwa hiyo, anafikiria eneo la tumbo la mama yake ni eneo kubwa linalostahili hata kucheza. Hajui kwamba akitoka duniani kuna eneo kubwa mno, kuna eneo la kukimbia atachoka, kuna eneo la kucheza atachoka, kuna eneo la kulima atachoka, kuna eneo la kutembea atachoka. Hawa wanafikiria kama mtoto mchanga tumboni anayefikiria eneo la tumbo ni eneo kubwa sana. Leo unamkosoa Balozi eti kwamba tunao Mabalozi wenye hadhi ya nyumba kumi, haya ni matusi wa Mabalozi wetu. Mabalozi wetu ni Mabalozi waliochunjwa, wameiva, ukiwepo Balozi Mahiga, nani asiyejua kwamba Mahiga ni moja ya watu waliobobea katika masuala ya kidiplomasia ya kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanasimama hapa kutuambia as if kwamba sisi ni watoto wadogo. Hivi ingekuwa Watanzania wote au viongozi wote wa nchi hii wanatakiwa kusafiri nje ya nchi kwenda kuwasilisha masuala ya nchi hii wao wangekuwa Wabunge hapa. Si kila mwananchi wa Jimbo lao angekuja hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wananchi wote kuja kwenye jengo hili ndio maana tumekuchagua Msigwa, ndio maana tumekuchagua Januari, ndio maana umechaguliwa Lusinde, kwa sababu wana nchi wa Jimbo zima hawawezi kuhudhuria katika kikao hiki. Sasa leo wanataka nchi nzima kila mtu akajiwakilishe kule, katika kimataifa aende akazungumzie matatizo ya nchi, haiwezekani ndio maana kuna Mabalozi wameteuliwa. Jifunzeni ninyi! Kwa hiyo, nataka niwaambie, anazungumza pale mwisho, anasema nchi ya kifisadi kama hii wakati fisadi mkuu mnaye nyie. (Makofi/Vigelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao upinzani ambao unachosema haukielewi, wanachopinga hawakielewi, walichosema mwaka jana mwaka huu wanakuja wanajijibu. Walichokataa mwaka juzi, mwaka huu wanakuja wanakikubali. Nataka nimpongeze Rais Magufuli, amewafanya wapinzani wa nchi hii hawana hoja, ndio maana mnawaona wakisimama humu hakuna lolote la msingi wanalolisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, amewafanya wapinzani wa nchi hii hawana hoja ya msingi, sasa imekuwa moto ukiwaka wanatoka nje ya Bunge, daladala ikiungua wanatoka nje ya Bunge kwa sababu hoja ya msingi hawana maana Rais anafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishe Rais akienda kwa speed hii kufika mwaka 2020 hawa watakuwa hawapo ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaitumia diplomasia ya nje kuhakikisha kwamba nchi hiii inapata uchumi mkubwa utakaowafanya wananchi wanufaike, na utakaowafanya wapinzani wa nchi hii waondolewe na wananchi kwenye Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie, nina uzoefu wa kuongeza na hawa, nina uzoefu nao, unapowaona wanapiga kelele jua sindano zinaingia ndio maana unaona wanapiga kelele. Huwezi ukasimama kwenye Bunge hili ukiita Tanzania ni nchi ya kifisadi wakati fisadi mkuu mmemchukua, na itafika mahali nataka nikuambie, hata Mheshimiwa Mahiga hawa wakubeze vipi, siku ukijiunga kwao utakuwa mgombea Urais wa chama hicho, za kwao hawa ni kuokoteza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namtia moyo Mheshimiwa Waziri na Naibu wako, Katibu Mkuu na Mabalozi wote wakilisheni nchi kama Rais alivyowaamini, watanzania tunawaamini, na ndio maana tuko nyuma yenu tunawaunga mkono.Chapeni kazi na hiyo kazi italeta manufaa hata kwenye Majimbo ya hawa wanaopiga kelele leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie, nina uzoefu wa kuongeza na hawa, nina uzoefu nao, unapowaona wanapiga kelele jua sindano zinaingia ndio maana unaona wanapiga kelele. Huwezi ukasimama kwenye Bunge hili ukiita Tanzania ni nchi ya kifisadi wakati fisadi mkuu mmemchukua, na itafika mahali nataka nikuambie, hata Mheshimiwa Mahiga hawa wakubeze vipi, siku ukijiunga kwao utakuwa mgombea Urais wa chama hicho, za kwao hawa ni kuokoteza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namtia moyo Mheshimiwa Waziri na Naibu wako, Katibu Mkuu na Mabalozi wote wakilisheni nchi kama Rais alivyowaamini, watanzania tunawaamini, na ndio maana tuko nyuma yenu tunawaunga mkono.Chapeni kazi na hiyo kazi italeta manufaa hata kwenye Majimbo ya hawa wanaopiga kelele leo.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutuzawadia uhai na kwa huruma yake tuko salama na tuko ndani ya Bunge hili kwa sababu ya kujadili Mpango wa Maendeleo wa Serikali 2016/2017 na 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nataka nichukue fursa hii ndugu zangu kwa unyenyekevu mkubwa sana kutoa pole kwa wananchi wenzangu watatu watafiti kutoka Chuo cha Seliani waliouawa katika Kijiji cha Iringa-Mvumi, katika Wilaya ya Chamwino, nawapa pole sana familia. Vilevile nitoe pole sana kwa wananchi kadhaa wa Kijiji cha Mvumi Mission pamoja na Kata ya Manda na Kijiji chenyewe cha Iringa-Mvumi kwa familia ya Tatu ambaye naye pia aliuawa wiki moja kabla ya wale watafiti kukumbwa na kadhia hiyo. Naomba Mungu azipumzishe roho za marehemu wote mahali pema peponi, lakini niitake Serikali kuchukua hatua madhubuti kuwatafuta watu waliokimbia ambao kwa kweli kwa kiasi kikubwa wanatajwa kuhusika na mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, nina mambo machache ya kuzungumza. Jambo la kwanza, naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri. Ndugu zangu nataka nirudie tena maneno ambayo nimekuwa nikiyasema mara nyingi kwamba katika kazi rahisi duniani, hakuna kazi rahisi kuliko kupinga, kupinga jambo lolote ni kufanya kazi rahisi sana. Maana mtu anajenga nyumba kwa gharama kubwa wewe unatumia dakika mbili tu kumwambia nyumba yako mbovu. Kwa hiyo, unaweza kuona namna ambavyo kupinga ni kazi rahisi sana na inayoweza kufanywa na mtu yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango, maneno mengi mazuri ameyaandika katika kitabu chake, mojawapo ni kukua kwa uchumi ambapo sasa hivi umekua kwa 5.7% na unategemewa kukua kwa 5.9%. Tatizo tulilo nalo Dkt. Mpango ni namna gani tunahusianisha kati ya ukuaji wa uchumi kwenye vitabu na hali halisi kwa wananchi wenyewe. Hapa ndiyo inatakiwa sasa mtusaidie ku-link kwa sababu tunavyoelewa ni kwamba uchumi unapokua ni lazima uguse baadhi ya wananchi au pengine wananchi wengi zaidi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini. Huko bado tuna matatizo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda vidogo vidogo, nashauri Serikali tujikite zaidi kwenye viwanda ambavyo vitainua kilimo. Tujikite kwenye viwanda vya mazao yanayolimwa na wananchi. Kwa mfano, kwa Mkoa wa Dodoma ukianzisha kiwanda kwa ajili ya kuinua zao la zabibu utakuwa umetusaidia zaidi kuliko tukiwa tunazungumza ukuaji wa uchumi wa point za kwenye karatasi ambao hauakisi wananchi wenyewe wanainukaje kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niyaseme haya maana imeonekana kwamba Wabunge wa CCM tuna uoga wa kumshauri Rais, lakini leo nataka nitamke kwenye Bunge hili, Rais anafanya kazi nzuri sana na aendelee kuifanya. Bahati nzuri tumekuwa na Rais kama Mbunge mwenzetu kwa miaka 20, anatujua Wabunge, anaijua nchi, anajua namna ambavyo tuna tabia za kuzusha, hawezi kubabaishwa na maneno yanayotoka humu. Katika nchi yetu kwa miaka mingi sana tumekuwa na malalamiko kwamba Serikali yetu inalindana, mtu anaharibu hapa anahamishiwa hapa, mtu anaharibu hapa anapelekwa hapa, tunataka mabadiliko, amekuja Rais wa mabadiliko, ukiharibu unakwenda kupumzika nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu nataka niwaambie wala hakuna mtu anayetisha wala hakuna mtu anayeshindwa kumshauri. Ila nataka niwapongeze sana, mimi mara chache sana huwa nawapongeza Wabunge wa Upinzani lakini safari hii nataka niwapongeze, nawapongeza kwa sababu wamejitoa mhanga. Wanaposimama kusema Serikali imefilisika msifikiri wanaisema Serikali, hapana, wana sehemu wanayolenga kwa sababu ili ujue kwamba huyu mtu amefilisika kuna vielelezo. Cha kwanza, lazima ashindwe kulipa madeni, mtu akishindwa kulipa madeni ujue amefilisika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wabunge wa Upinzani acheni uoga, badala ya kusema Serikali imefilisika, Serikali inayolipa mishahara, Serikali inayowalipa nyie, Serikali inayosomesha watoto bure, tamkeni wazi kwamba Mbowe umefilisika maana umeshindwa kulipa madeni. Tamkeni wazi, hakuna sababu ya kuzungukazunguka unapiga kona ooh mimi nitakamatwa, sasa unatuambia sisi tuje tukuwekee dhamana, ukikamatwa ni kwa makosa yako. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ameteua Wakuu wa Mikoa wengi wazuri, lakini wachache nitawataja hapa, wa kwanza Mrisho Gambo, nampongeza sana. Wa pili Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rugimbana Jordan nampongeza sana. Wa tatu, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, nampongeza sana Mongella anafanya kazi nzuri. Rais anawajua watu wake, anapowapanga anajua kabisa nani anaweza kufanya kazi wapi. Big up sana Dkt. Magufuli, endelea kufanya kazi ukiamini kwamba nyuma yako wako watu wanaokuombea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie msamiati mgumu sana. Ni bora mtu ufe mawazo yako yabaki hai kuliko mtu uwe hai halafu mawazo yako yawe yamekufa, ujue wewe umepotea kabisa. Hatuwezi kuogopa kuchukua hatua. Leo hii tunasimama ndani ya Bunge hili tunasema utumishi ni uti wa mgongo, kwenye utumishi haitakiwi kuingiza siasa inakuwaje mtu aliyefikia level ya kuwa mtu mkubwa mpaka Katibu Mkuu leo Mbunge wa CHADEMA, alianza lini? Lazima alianza akiwa huko huko katika Utumishi, ndiyo maana lazima tufukue kila sehemu kuangalia tunao watumishi au tunao watu wanaopiga porojo za siasa badala ya kufanya kazi, lazima tusimamie nidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mtu anafikiria kwamba eti tutakuwa na Taifa ambalo halina mabadiliko, haiwezekani! Tumeyaomba sana mabadiliko, tumelala tunasisitiza kwamba tunataka mtu atakayekuja kubadilisha. Kama kuna mfanyakazi anaenda kazini akiwa hana hakika kwamba ajira yake ipo, sawasawa, yeye akachape kazi. Kazi peke yake ndiyo itasababisha ajira yako iendelee kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusidanganyane hapa. Tunasimama hapa na kuanza kusema ooh kwenye kikao cha chama cha Wabunge wa CCM wamepewa hela, aaah, wamepewa hela na nani? Mbona ninyi mnachangishwa kila siku hapa? Wabunge wanachangishwa kila siku milioni moja moja, wengine wanakuja wanalia wanasema Lusinde angalia meseji hii tunatakiwa tutoe milioni moja moja kwa ajili ya kesi, mbona sisi hatuyasemi yenu? Sisi tupewe pesa na nani? Wabunge wote tulipewa fursa ya kwenda kukopa, kila Mbunge kakopa, wengine wamekopa 200, wengine 300, leo hii uje upewe milioni 10 ili iweje, ni kutudhalilisha tu.
Msichukue fursa hiyo kutudhalilisha, Wabunge wa nchi hii wote wa Upinzani, wa CCM tulipewa fursa, tumekopa hela nyingi, hakuna Mbunge wa kuhongwa milioni 10 wala wa kupewa milioni moja. Ndiyo maana nyie mnachukua hela zenu kukichangia chama chenu, hakuna mtu anayewazungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana wakati huu ambapo tunazungumzia mpango, baada ya kuwa nimeshawapa dawa kidogo, ni vyema tukajikita kwenye sekta binafsi. Serikali imeambiwa uti wa mgongo ni sekta binafsi. Rais amekwenda kufungua kiwanda kuna watu wanapiga kelele tena, mnaenda kwa Bakhresa, katika sekta binafsi kuna mtu mjasiriamali jamani katika nchi hii anayemfikia Bakhresa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bakhresa akimuita au akimuomba Rais kwenda kufungua kiwanda chake, uharamu wake uko wapi? Au Bakhresa kuacha kuwachangia wapinzani ndiyo imekuwa nongwa? Maana nashangaa unaanza kumlaumu eti kwa nini Rais kaenda kufungua kiwanda cha Bakhresa kampa na ardhi, kuna vivutio vya kuwafanya wawekezaji wa ndani nao waweze kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mpango kelele anazozisikia uchumi wa ndani una booster yake. Booster yake ni kuwalipa wadeni wa ndani, ukiweza kuwalipa wadeni wa ndani hela itaonekana mtaani na hizo kelele zitapungua. Mnapokumbuka madeni ya nje ni sawa, lakini kumbukeni na madeni ya ndani. Kuna wazabuni mbalimbali waliofanya kazi kwenye Serikali, hawa wakipata pesa mzunguko wa pesa ndani ya nchi nao utaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawashauri Serikali muangalie pande zote. Mnaposomesha bure tunaona, mnaponunua ndege tunaona, tunajua yatasemwa mengi lakini endeleeni kufanya kazi kwa sababu hata Mungu angeleta majadiliano na wananchi hicho kikao kisingekwisha. Ndiyo maana ukaona akakaa mbali akaamrisha kama ni mvua, mvua, kama jua, jua. Mwambie Rais tunamuunga mkono, kazi anayofanya ni njema, tumepata Rais wa kunyooka, akinyooka na jambo linaenda kama alivyopanga na ndicho tunachokitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanalalamika hapa ooh Rais anafanya kazi yeye mwenyewe. Halafu mimi nashangaa hawa jamaa wanasema halafu wanajijibu wenyewe. Wananikumbusha Sauli kwenye Biblia alipokutana na kibano cha Mungu Sauli alisema, ni nani wewe Bwana? Yaani aliuliza swali halafu akajibu kwamba huyu ni Bwana, ndiyo hawa! Huku unasema Rais anafanya kazi zote, huku tena unabadilika unasema Rais anawatisha watumishi. Mtu anayewafanyia kazi zote atawatishaje sasa wakati kazi zote anafanya yeye mwenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Rais ananyooshe hii nchi na tuna uhakika Magufuli nchi hii atainyoosha kutoka pale ilipokuwa imeishia kwenda mbele zaidi. Nawaambia moja ya vitu ambavyo nataka Watanzania watusaidie 2020 nchi zetu za ulimwengu wa tatu hizi kuwahi kila kitu nalo ni tatizo, hata kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi tuliwahi ndiyo maana mnaona hoja zenyewe…..
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Nimalize? Sasa unaingiaje Bungeni kujadili kaptura ya Mfalme wa Morocco hiyo ina uhusiano gani na matatizo ya wananchi? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana Mungu kwa kutupa nafasi nzuri kabisa ya kujadili juu ya huu Mkataba wa EPA. Vilevile sina budi nichukue fursa hii katika Bunge hili kumpongeza sana Profesa Kabudi kwa namna alivyotufumbua macho. Profesa Kabudi ni moja ya Watanzania wenye uwezo wa walichonacho kuwasaidia na wengine waweze kuelewa. Hilo ni jambo zuri sana na kwa kweli tunajivunia sana kwamba elimu yako inawafaa wengi na inaifaa nchi. Hongera sana Profesa Kabudi.
Mheshimiwa Spika, ni ngumu sana kusimama hapa kuutetea huu mkataba na ndiyo maana unaweza kuona kuna baadhi wanaojaribu wanapata shida sana. Hauna namna yoyote ya kuuzungumzia uzuri wa Mkataba huu, hata kama umeandaliwa au umejiandaa; ni jambo gumu sana. Ndiyo maana umeona hata waliojaribu kufanya hivyo, wamejikuta wao wenyewe wakipata shida sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Khatib, ameonyesha kwamba isiyo kongwe haivushi, kwamba ukongwe wa CCM ni jambo zuri na inaendelea kuvusha nchi hii. Amesema chama hiki ni kikongwe. Ukishasema kikongwe, maana yake hicho ndicho chenye uwezo wa kuvusha baadhi ya mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama umewasikiliza wazungumzaji wachache waliotangulia, nataka niungane nao kwamba hata kuchukua muda mwingi kuujadili mkataba huu ni kutumia tu fedha za Watanzania vibaya, huu mkataba haukustahili hata kufika huku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huu ni moja ya mikataba mibovu kabisa ambao pengine nimsaidie hata mzungumzaji aliyepita, kwa nini Kenya wamesaini? Wamesaini bila kuutafakari kwa makini. Wangetafakari kwa makini; na nikubaliane na Mhesimiwa Zitto kwamba wamesaini kwa ajili ya kufanya biashara ya maua, siyo kwa ajili ya usalama wa mkataba wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 140, hakiruhusu nchi moja kujitoa baada ya kuingia. Mimi nataka niseme, Jumuiya yetu ya East Africa, kama kuna jambo mmetuangusha ni katika jambo hili. Kwa nini msingekaa wenyewe kwanza mkaupitia huu mkataba? Secretariat ya Jumuiya ya East Africa mkakaa mkausoma kwa pamoja kabla ya kuruhusu nchi moja moja kwenda kujisainia yenyewe? Kwa hiyo, hapa tunaanza kona kuna problem kwenye Jumuiya yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki iwe inakaa pamoja kwenye mambo ya muhimu na mazito kama haya, leo tusingeona aibu ya Kenya kutangulia kusaini kama mngekaa pamoja mkashauriana, kwamba jamani hivi unaingiaje kwenye mkataba ambao unakuchagulia rafiki? Unaingiaje kwenye mkataba ambao unakulazimisha kushirikiana na adui? Huu mkataba kadri unavyousoma, kuna sehemu unakuchagulia rafiki wa kufanya naye biashara na kuna sehemu unakulazimisha kukaribiana na mtu ambaye wakati huo humhitaji.
Mheshimiwa Spika, ukitazama kwa makini mkataba huu wa EPA, ni sawa sawa na mzee wangu pale kijijini kwenda kupelekewa zawadi ya kuku halafu akachukuliwa ng‟ombe wake kumi; kitu ambacho hakiwezi kukubalika!
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni moja ya mikataba mibovu kabisa. Nasi tunapoukataa mkataba huu na kuitaka Serikali, isiusaini, tunaukataa ili kuwaonesha Jumuiya ya Ulaya kwamba Afrika sasa inao wataalam, wanajitambua na wanaweza kufanya biashara huria na mtu yeyote. Sisi sio watu wa kupangiwa na kuletewa mikataba ya namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niishauri Serikali; kwa mkutadha huu, huu mkataba haufai kusainiwa hata kidogo kwa sababu una vipengele vingi vinavyodhalilisha Afrika.
TAARIFA...
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, namshukuru na namheshimu sana Mheshimiwa Millya, lakini ni mmoja wa watu wachache ambao wamerubuniwa na wazungu. Hawa wazungu waliokuja wamemwona Millya. Maana hapa hatutakiwi kutafuna maneno; kuna baadhi ya Wabunge wamewaona, inawezekana na Mheshimiwa Millya akawa ni mmojawapo kati ya waliowaona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hukatazwi, unawezaje kutoa notice halafu mwaka mzima ukaendelea kubaki mle? Unabaki humo kwa sababu zipi? Khah, maana wewe mwenyewe unasoma, halafu unajijibu. Bahati nzuri wewe mwanasheria na pengine unaelewa zaidi, lakini umepata majibu kwamba ukishatoa notice, mwaka mzima unaendelea kubaki mle. Ukifanya nini kama unao uhuru wa kutoka moja kwa moja? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nirudie, hili ni jambo letu wote kama Bunge, tusianze kushindana humu. Tukubaliane kwamba mkataba huu haufai, maana ndani una vi-package vya ushoga, una vitu vya ovyo ovyo vimefichwa humo, Watanzania watatushangaa sana.
Mheshimiwa Spika, sisi hatuwezi kuburuzwa na nchi yoyote, sisi ni Taifa huru! Iwe wamasaini nchi nyingine ambazo pengine wao wanavutiwa na ushoga, sisi hatuvutiwi nao. Kwa hiyo, hatuko tayari kukubaliana na jambo hili.
TAARIFA...
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, hiyo itakuwa imetusaidia wote, lakini zaidi sana, Mheshimiwa Millya ameelewa kwamba ni ile block ndiyo inatakiwa kuomba kutoka lakini siyo nchi moja ambayo imezuiwa na mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, tuseme tu kwa kifupi, mkataba huu haufai. East Africa wawe makini na mikataba ya namna hii, waipitie wao wenyewe kama Sekretatieti na wao na uchungu na nchi zao kabla ya kuangalia manufaa watakayopata. Kwa sababu wakati mwingine kuna hadithi moja; watu waliwahi kushangilia kwenda kufanya kazi kwa Mfalme, wakati huo huo kulikuwa kuna agizo kwamba ili ukafanye kazi kwa Mfalme, ni lazima uhasiwe kwanza ndiyo uruhusiwe kufanya kazi kwa Mfalme. Kuna watu wakashangilia, walipofika pale kukuta masharti, yakawa magumu kwao. Kwa hiyo, kila mikataba ya kimataifa inapokuja, tuwe na Sekretarieti zinazotazama kwa makini, siyo kukurupuka! Tutakuja tuingie kwenye matatizo makubwa na tuziingize kwenye shida kubwa. Tutakuja kupata adhabu ambazo hazina msingi. Maana kadri unavyousoma unakutana na sehemu inasema EU inaweza kuchukulia hatua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza kuona ambayo tunaweza tukaingia kwenye matatizo makubwa ya kuchukuliwa hatua na uhuru wa nchi zetu ukawa unatekwa bila sisi wenyewe kuelewa.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono mkataba usisainiwe.

The Access to Information Bill, 2016

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru Mungu kwa kunijalia zawadi ya uhai na afya njema ili na mimi niweze kusema machache juu ya mchango wangu kuhusu Muswada wa Upatikanaji wa Taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa kuuleta Muswada huu. Kabla ya Muswada huu, suala la kutoa taarifa halikuwa la lazima. Mtu angetaka kutoa anatoa; hataki, anakaa hivyo hivyo; lakini leo kwenye Muswada huu Afisa analazimishwa kutoa taarifa kama sheria tutakavyoipitisha. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake wa kuleta Muswada huu Bungeni ili watu wasitafute habari kwa kuomba, wasitafute habari kwa hisani, bali wazitafute habari kisheria. Hili ni jambo zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yanazungumzwa humu ndani kwamba Katiba inatoa haki, ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge, Katiba haifanyi kazi ya utendaji wanaotenda ni watu sio Katiba yenyewe ndiyo inayotekeleza. Leo Katiba inasema kila Mtanzania ana haki ya kuishi popote, lakini Rais au Waziri mwenye dhamana ya makazi ana uwezo wa kusema watu watoke hapa kuna mafuriko wakati Katiba haisemi hivyo. Kwa hiyo, tusiishi kama tumejifungia; maana yake kila mtu hapa anasema Katiba, Katiba. Katiba haitekelezi, Katiba ni sheria mama ya nchi. Zinatungwa sheria kutafsiri Katiba na ndiyo kazi ambayo tunataka kufanya hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasikitika sana ninapoona watu wanakimbilia kujificha kwenye Katiba. Katiba haitekelezi, wanatekeleza watu na hao watu wanaweza kutekeleza kitu ambacho kiko kwenye Katiba. Leo hii hapa tuna jengo la Bunge, lakini pakipita mafuriko litahama, hata kama imeandikwa hivyo kwenye sheria kwamba jengo la Bunge liwe hapa. Kwa hiyo, watu waelewe tu kwamba hapa tunatunga Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa na hakuna sehemu tunapokwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakuna sehemu tunapokwenda kinyume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Waheshimiwa Wabunge wanajaribu kuwatisha baadhi ya Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivi kumbe ninyi mngeshinda nchi mngetunga sheria ambazo zingewa-favour akina Lowassa? Sheria ni msumeno, inatakiwa ikate kote kote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kama kuna mtu alikuwa Waziri akaivunja sheria amefungwa ni sawasawa. Hatutungi sheria kwa ajili ya wananchi tu; tunatunga sheria kwa ajili ya Watanzania wote na sisi wenyewe. Sasa naona kuna mtu anasimama anasema, shauri yenu, akina Mramba walikuwa hapo, leo wamefungwa. Hata ninyi mtafungwa, hata sisi Wabunge tutafungwa, hata mimi nitafungwa. Sheria inataka kila mtu aitekeleze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe wenzetu wangepata Serikali hawa, wangetunga sheria za kukandamiza wananchi, wao zisingewahusu. Ndiyo maana mnaona kila wakisimama hapa, wanajaribu kukutisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanajaribu kukwambia eti leo hii Lowassa anapigwa mabomu, angepigwa mabomu angekuepo? Amepigwa gesi za kutolea machozi, siyo bomu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusidanganyane hapa! Watu wanaowazungumza, hata kukimbia hatua tano hawawezi, apigwe bomu ataweza kuvumilia yule? Acheni mambo ya kudanganya kwenye Bunge hapa. Tusidanganyane! Watanzania lazima tuelewe, tunapotunga sheria na Wabunge tuelewe, hatuwatungii watu, tunajitungia na sisi wenyewe, hili ndiyo nataka lieleweke.
Kwa hiyo, isije ikafikiriwa kwamba kuna kundi tu tunalolilenga, hapana. Kumbe wenzetu wametupongeza kwamba Serikali ya CCM inatenda haki, inatunga sheria zinazowalamba mpaka Mawaziri, wametupongeza. Hizi tuzichukulie kama pongezi kabisa, kwa sababu leo hii kila kitu wanataka kiandikwe kwenye Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna Chama kimoja, Mwenyekiti wao anadaiwa, walikutana kikao kujadili deni, kwenye Katiba yao imeandiwa wapi? Imeandikwa wapi? Wapi kwenye Katiba yao imeandikwa Mwenyekiti akidaiwa mtaacha shughuli zote mkutane kwenye kikao kujadili deni? Kwa hiyo, kuna mambo mengine ya utekelezaji yanafanyika nje ya hizo Katiba kwa sababu ya hali halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa namna unavyoliendesha Bunge kisayansi na linavyokwenda. Nataka niseme leo, tajiri hanuniwi! Ukimnunia tajiri, inakula kwako. Kwa hiyo, hizi siku mbili mnazowaona watu wana uhuru fulani wanazungumza humu ndani, ndiyo uhuru umepatikana hivyo. Kwa hiyo, tuendelee kuwavumilia, tutakwenda nao vizuri tu hawa wa kwetu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya adhabu; hakuna sheria inayoweza kutekelezwa kama haitoi adhabu. Haiwezekani. Sheria yoyote ili itekelezwe, ni lazima iwe na adhabu. Kwa hiyo, kama kwenye sheria hii kuna mtu ataikosea sheria, atakwenda jela miaka mitano, iko sawa. Kumbe tutatungaje sheria bila kuweka adhabu? Hiyo sheria itatekelezwaje sasa? Sheria ili itekelezwe ni lazima iwe na upande wa kuadhibu ili watu tuogope; ili watu waogope. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusimama hapa na kusema upatikanaji wa habari ni haki ya Kikatiba. Kweli ni haki ya Kikatiba, lakini kwa mfano, kama mtu nyumbani kwake hajanunua redio, hana betri, anapataje habari? Hawa watu wa ajabu sana! Ni haki kweli, lakini kuna haki ambazo ni lazima uzigharamie. Leo upatikanaji wa habari, huna TV, huna umeme unapataje hiyo habari? Wenzetu wanalazimisha, ooh, ni haki ya Kikatiba, haki ya Kikatiba, sasa Serikali igawe TV nchi nzima, Serikali igawe redio nchi nzima, igawe betri nchi nzima? Kwa hiyo, kuna vipande kwa vipande. Kuna haki na kuna wajibu. Uko wajibu! Ukitaka habari, ni lazima uwe na wajibu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusitake kutumia fursa hii kudanganya. Zipo haki zimetajwa kwenye Katiba, lakini uko wajibu. Kila Mtanzania ana haki ya kuishi, lakini ana wajibu wa kulima ili apate chakula kitakachomfanya aishi. Sasa kama hafanyi kazi, hapiki chakula, anaishije? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusidanganye watu kwa kutumia kisingizio cha Katiba, inatoa haki, Katiba inaminywa. Katiba inatoa haki na Katiba hiyo hiyo inatoa fursa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, watu wakikusonga sana, jua uko sahihi. Kwa hiyo, wewe endelea kufanya kazi zako, ndiyo maana unaona wanasimama wanakushutumu. Mawaziri endeleeni kupiga kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kila mtu akisimama hapa, mnataka kupotosha watu kwamba Mheshimiwa Rais amekataza kufanya mikutano!
Hakuna mahali Mheshimiwa Rais amekataza kufanya mikutano. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mbunge anatakwa kufanya Mkutano kwenye Jimbo lake. Kilichokatazwa ni kuendelea na kampeni kwa tabia ambayo tulikuwa tumezoea. Uchaguzi unaisha, watu wanaendelea na kampeni miaka mitano, hiyo ndiyo haikubaliki. Mbunge gani, wa Jimbo gani, kaenda kufanya mkutano kwenye Jimbo lake akakatazwa? Nani? Hakuna mahali. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa walikuwa wameshazoea. Watanzania kwa sasa hivi hawana nafasi ya kupokea tena maneno, wanataka kupokea maendeleo, siyo maneno. Maneno mengi yameshazungumzwa, maneno mengi yameshasemwa, nyimbo nyingi zimeimbwa mpaka nyingine zimezuiwa kuimbwa, sasa hivi ni wakati wa kufanya kazi, siyo wakati wa maneno kama walivyokuwa wamezoea hawa.
Kwa hiyo, mkisikia wanalaumu, ooh, Mheshimiwa Rais ametukataza kufanya mkutano; wewe Jimbo lako la Tarime, nani kakukataza kufanya mkutano? Nenda kahutubie wananchi wako waliokuchagua, isipokuwa kutoka Tarime unafunga safari kwenda Mpwapwa; Mpwapwa wana kiongozi wao waliomchagua, acheni afanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho leo nataka nikiseme, kauli ya Mheshimiwa Rais imewaumiza baadhi ya watu. Walikuwa wanatumia ruzuku vibaya, wakati huo wanajifanya kuna operesheni sijui nini; sijui operesheni ndorobo; sijui operesheni nini, kumbe wanakula hela za wananchi kwa kutumia mgongo wa operesheni. Sasa hiyo hakuna. Hakuna nafasi hiyo, kila Mbunge afanye mikutano kwenye Jimbo lake, ahamasishe maendeleo, shughuli za maendeleo zifanikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuja kumsingizia Mheshimiwa Rais kwamba kazuia mikutano, siyo sahihi, lazima tuliweke vizuri jambo hili. Ulaji wa ruzuku kupitia vyama vya siasa umezuiwa, ndiyo maana mnaona kelele. Maana ilikuwa saa hizi unaona maspika yamefungwa, bendera zimefungwa; wapi? Mtera, kufanya nini? Mtera kuna Mbunge wake, mnakwenda kufanya nini? Miezi mitatu imepita tumefanya uchaguzi, leo hii tuendelee tena kuwajaza watu maneno? (Makofi)
Ukisikia kelele, ujue tayari!
MWENYEKITI: Ahsante. Ahsante sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's