Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Muhammed Amour Muhammed

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema mwenye kurehemu. Pia nampongeza Mheshimiwa Spika, yeye binafsi kwa kuwa makini sana kusimamia Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika meneo yafuatayo: maslahi duni ya Walimu, kubadilisha syllabus pasi kushauriana na Wizara ya Elimu Zanzibar; NECTA; kutolipatia stahiki somo la dini ya Kiislam mashuleni kuhusiana na ufaulu wa wanafunzi; shule za binafsi; mikopo ya elimu ya juu; kufuta mfumo wa GPA na kurejesha divisions; na elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na maslahi duni ya Walimu. Hapa ndipo hasa penye matatizo makubwa sana katika kada ya elimu. Walimu wanalipwa mishahara duni. Hii inapelekea sana Walimu kufanya kazi bila ya utulivu kwa sababu umasikini ni mwingi, wanashindwa hata kujikimu. Ingekuwa vyema maslahi ya Walimu yakaangaliwa upya. Mwalimu wa Tanzania amekuwa kama mshumaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubadilisha syllabus bila kushauriana na kupeana taarifa kwa wakati stahiki inasumbua sana. Wizara ya Elimu Zanzibar haishirikishwi wakati wa kubadilisha syllabus hasa kwa madarasa ya Kidato cha Kwanza hadi cha Nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie chombo cha NECTA. Naomba nipatiwe majibu, Zanzibar inashiriki vipi katika chombo hiki? Ni vyema pangejengwa Ofisi ndogo basi ya NECTA kule Zanzibar ili kuzuia kwenda Dar es Salaam kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu ambao wanachaguliwa kusimamia mitihani ya CSEE wengi wao hawana sifa na kwamba masharti yanayotakiwa hayazingatiwi. Hii hupelekea kuwepo na matatizo mengi sana wakati wa kufanya mitihani hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubadilishaji wa mitihani (matokeo) kutoka GPA kwenda Division ni vyema ukaangaliwa tena kwa utafiti wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye shule binafsi. Shule ni nzuri na mimi binafsi ninakubaliana nazo sana. Ila ni vyema Serikali nayo ikazifanye shule zake ziwe na uwezo angalau kama hizi. Maabara za shule za Serikali ni vituko! Walimu wazuri wote wamepotelea katika shule za binafsi, matokeo mazuri yako ndani ya shule binafsi. Kuna nini hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasadikika kwamba somo la dini halipatiwi stahiki zake katika ufaulu wa kuendelea Kidato cha Tano. Naomba hapa nipatiwe jibu, ni kweli au la? Kama ni kweli, ni kwanini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu ni vipi Zanzibar inapatiwa gawio lake na kwa wakati upi? Pia dhana ya elimu bure haijaeleweka ipasavyo? Ni vyema ikaelezwa vizuri sana na ikaonekana kiutendaji, naomba kuwasilisha

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ni vema nikamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye rehemu. Ninakupongeza pia Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kulisimamia Bunge hili Tukufu kwa umakini mkubwa. Pia nitoe shukrani zangu za dhati kwako kwa kunipatia fursa na mimi kuchangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie hapa “kufufua viwanda” na kufanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Ingekuwa busara kama kwanza tungefanya utafiti wa kina hadi tukaelewa chanzo cha kufa viwanda vyetu hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema kwanza tukaandaa miundombinu itakayowezesha Tanzania kuwa ni nchi ya viwanda kweli. Umeme bado ni tatizo, umekuwa siyo wa uhakika unakatika hovyo hovyo, maji pia ni tatizo ni vema tungeboresha miundombinu hii kwanza.
Mheshimwia Spika, ni vyema viwanda vyetu vikaanza na sekta hii ya kilimo kwani ni rahisi kupata malighafi. Tungetumia zana za kisasa sana pamoja na mbolea hata mbegu za kisasa ili kupata tija baadaye tukipeleka kwenye viwanda vyetu. Nyanya zipo kwa wingi, miwa ya kutosha na matunda mengine. Hata mpunga kama tutalima kisasa tutavuna vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenda kwenye viwanda vya general tyre. Mimi hapa napata mashaka kidogo, sidhani kama tutaweza kumudu soko vizuri.
Bahari yetu pia ina samaki wengi wa aina tofauti, samaki hawa wanavuliwa na wageni, ni vyema viwanda pia vikaangaliwa kushindika samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema Tanzania ya viwanda tunayotaka ikaangalia mapema kuimarisha bandari zetu zote ambazo zitaweza kutuunganisha vizuri, tuweze kuuza vizuri mali zetu zitokanazo viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema kabla ya kuanzisha viwanda tukaandaa mpango mkakati wa kuvilinda viwanda hivyo. Lakini pia ni vema kukawa na maelewano ya karibu sana baina ya Wizara ya Kilimo, Miundombinu, Biashara, Viwanda na Uwekazaji wakatengeneza “unit” ili wakafanyakazi kwa pamoja, kwa baadhi ya wakati ikawa ni rahisi sana njia za mawasiliano na kukamilisha kwa wepesi lile lililopangwa mashirikiano baina ya Wizara hizi yanahitajika ili tupate Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwa hai, mzima na kunipatia nguvu ya kuweza kuchangia mada ambayo ipo hewani sasa. Pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Spika kwa namna ambavyo analiongoza Bunge hili kwa upendo na umahiri pia na uvumilivu mkubwa anaouonyesha ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia mambo sita yafuatayo:-

Moja, UKIMWI; Taifa letu sasa linahujumika kwa maradhi haya na wengi wao ni vijana ambao ndio manpowers ya Taifa. Naomba hapa Wizara husika iendelee kutoa elimu ndani ya nchi yetu namna unavyoambukizwa bila ya kuona haya, hali inatisha. Kwa upande mwingine ni vyema hizo dawa za ARV zikawekwa maeneo mengi zaidi tena kwa waziwazi pasi na kuficha.

Pili, malaria; nikienda kwenye malaria, haya ni maradhi bado yapo ijapokuwa yamepunguka. Jitihada za makusudi za kuyamaliza maradhi haya zinahitajika. Malaria ni maradhi ambayo huenezwa zaidi na mbu, mbu hawa kama tukiweka mikakati ya kusafisha maeneo, kupiga dawa za kuulia wadudu (insecticides) nchi nzima hasa kwenye mitaro ya maji machafu utapungua ama kwisha kabisa. Pia malaria ina kina, ni vyema tukaangalia zaidi kuwapatia watu wetu chanjo ya malaria.

Tatu, Madaktari na Wahudumu wengine wa Afya; ni vyema wakaongezewa mishahara kwani kazi ambazo wanafanya ni kubwa sana na maslahi bado ni duni kwa watumishi hawa. Nikiendelea kuchangia mada hii ni kwamba kwenye hospitali zetu na vituo vya afya bado watumishi ni haba, hawatoshi. Niombe Serikali kwa heshima zote iongeze watumishi katika sekta hii.

Nne, vituo vya afya; naomba Serikali iangalie tena upya namna ya kuboresha vituo vya afya hasa vilivyoko vijijini kwani havitoshi kulingana na mahitaji.

Tano, vifaa vya kisasa; hapa ndipo penye matatizo makubwa. Hospitali zetu hasa za Serikali hazina vifaa vya kisasa vya kutosha. Niiombe Serikali kwa heshima zote iliangalie suala hili kwa huruma sana, tunahitaji X-ray, Ultra- sound, CT Scan na vifaa vingine maana ni vichache sana.

Sita, maradhi yasiyo ya kuambukiza. Maradhi haya kama pressure, sukari yanazidi kuendelea kuwaumiza watu wetu. Kwa heshima zote niiombe Serikali/Wizara husika itoe elimu ya kutosha juu ya kujilinda na maradhi haya nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's