Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

All Contributions

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA YA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitambue michango ya Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge lako hili Tukufu waliochangia kuhusu taarifa ya Kamati yetu ya Katiba na Sheria. Waheshimiwa Wabunge 21 walichangia kwa kuzungumza lakini pia Wabunge watatu walichangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitambue michango ya Waheshimiwa Mawaziri waliosimama mbele ya Bunge lako hili hususani Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja. Nami nitajikita kwenye baadhi ya hoja ambazo ziliibuka na kuzitolea maelezo na pia kuliomba Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na maoni na mapendekezo yaliyomo kwenye taarifa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema natoa shukrani za kipekee kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia taarifa yetu hii ya mwaka ambao ni 21. Naanza na hoja ya Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab, Kamati inakubaliana dhahiri kabisa na mapendekezo yake kwamba Bunge liazimie kuitaka Serikali kufanya jitihada za kutosha kupunguza misongamano magerezani, tatizo la ucheleweshwaji wa kesi Mahakamani zinazohusiana na makosa ya mauaji na madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kwamba Kamati ina uwezo wa kulazimisha mahakama na kubadilisha taratibu ili kesi zichukue muda mfupi, sina hakika sana na hoja hii. Niseme tu kwamba kwa kuwa nilipata fursa ya kutumikia mhimili wa Mahakama kwa muda mrefu kidogo nafahamu zipo taratibu za kimahakama ambazo zinafuatwa na Mahakama zetu ikiwa ni pamoja na Katiba na Sheria ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Judicial Administration Act ambayo ilipitishwa na Bunge lako hili Tukufu mwaka 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mchakato wa kunyongwa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa na kama Serikali inashindwa basi kifungu husika kibadilishwe kama ambavyo imezungumzwa na Mheshimiwa Adadi nitalitolea ufafanuzi hapo mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa Mheshimiwa Abdallah Mtolea kuhusu watu wenye ulemavu na kwamba Kamati iliombe Bunge liazimie kwamba bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu iongezwe hasa kwa Fungu la 65 linalohusika na kazi na ajira ili kuwe na mazingira bora ya kutengeneza ajira kwa vijana. Kamati pia inapenda kuikumbusha Serikali kwamba kile kiasi cha asilimia 10 kilichotengwa kwa ajili ya vijana na wanawake basi kiasi hiki kisipunguzwe na ile asilimia 50 iliyotengwa kwa ajili ya maendeleo pamoja na OC asilimia 40. Kwa hiyo, Kamati inaitaka Serikali kwamba kile kiwango cha asilimia 10 kilichotengwa kwa ajili ya akinamama na vijana kiwe ni kiwango asilia isipungue hata shilingi moja ili sasa vijana wetu pamoja na akinamama waweze kufaidika na kiasi hiki cha asilimia 10. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunatambua kwamba, nchi yetu inaongozwa na Chama cha Mapinduzi. Kwa mujibu wa ukurasa wa 110 wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ilitengwa kiasi cha Sh. 50,000,000 kwa ajili ya kila kijiji. Tunaiomba Serikali kuhakikisha kwamba kiasi hiki cha fedha sasa kimetolewa ili kwenda kusaidia vijiji vyetu katika maeneo yetu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia inakubaliana na mawazo ya Mheshimiwa Mtolea kwamba Serikali iweke msisitizo mkubwa katika kusimamia haki na maslahi ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu adhabu ya kifo, katika taarifa yetu ya Kamati kuhusu Muswada Na.4 wa mwaka 2016 iliishauri Serikali kupunguza misongamano magerezani na kufuata sheria ili adhabu ya kifo ambayo inatambulika kwa mujibu wa Kanuni za Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 iweze kutekelezwa. Adhabu hii ya kifo ipo katika kifungu cha 197 na kifungu cha 196 ambacho kina-establish kosa la kuua. Kamati iliishauri Serikali kwa kuwa kuna mrundikano mkubwa wa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa adhabu hii iweze kutekelezwa mara moja kwa sababu jukumu hili ni la kikatiba na la kisheria. Pia kama Serikali inaona adhabu hii haitekelezeki basi ni vyema ikawasilisha maoni ili iweze kuondolewa kwa mujibu wa Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunaendelea kuishauri Serikali utekelezaji wa adhabu hii uendelee kama ambavyo umeainishwa katika kifungu cha 197 cha Kanuni za Adhabu, Sura 16. Tunafahamu ni mateso makubwa sana wanayapata wale waliohukumiwa kunyongwa wakisubiri adhabu ya kifo. Wao wenyewe wako tayari kupatiwa adhabu yao ya kifo iwapo itatekelezwa hata kama ni kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengine ni Mheshimiwa Taska Mbogo ambaye yeye amezungumzia suala la NSSF ambalo sitalizungumzia zaidi hapa kwa sababu tayari Mheshimiwa Waziri ameshalidokezea kuhusiana na mchango mkubwa wa hifadhi za jamii katika Taifa letu. Pia kama ilivyoagizwa katika taarifa za Kamati, Kamati inaendelea kusisitiza kwamba maagizo ya Bunge yatekelezwe na taasisi zote kama yalivyoelekezwa kuhusiana na uwasilishwaji wa mikataba ya uwekezaji unaofanywa na taasisi hii ya NSSF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu taasisi za usimamizi wa haki, katika taarifa yake Kamati imesisitiza Mahakama na Tume ya Haki za Binadamu ziongezewe bajeti katika mwaka wa fedha ujao wa 2017/2018 ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi hizo. Bajeti hiyo itasaidia utolewaji wa semina ili wadau wawe na uelewa wa kutosha wa sheria zinazopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lucia Michael alizungumzia kwamba jukumu la Polisi sasa limebadilika kutoka ulinzi wa amani na kuelekea kwenye ukusanyaji wa kodi. Kamati pia inaendelea kushauri Serikali kwamba siyo jukumu la Polisi kukusanya kodi kama ambavyo inafanyika leo hii Polisi wanakusanya kodi kwa makosa mbalimbali ya barabarani ambapo wanawakamata washtakiwa na wanakusanya kodi kama wao ni TRA. Kamati inaitaka Serikali jukumu la ukusanyaji kodi liendelee kubaki TRA na kulitaka Jeshi la Polisi kuacha mara moja kufanya kazi hizi ambazo hawawajibiki kwa mujibu wa taratibu na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chikota alizungumzia kuhusiana na fedha kutolewa chini ya kiwango kilichopitishwa. Msimamo wa Kamati ni kwamba fedha ziongezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ucheleweshwaji wa kesi mahakamani ombi la Mheshimiwa Adadi, kama nilivyosema hapo awali jibu katika taarifa ya Kamati kuhusu utekelezaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, tarehe 3 Mei, 2016, Kamati iliagiza Wizara na taasisi zake kuhakikisha kwamba Mahakama inapunguza wingi wa kesi yaani backload of cases mahakamani na kwamba haki itolewe kwa haraka na kwa mujibu wa sheria kwani justice delayed is justice denied.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nimpongeze Mheshimiwa Jaji Mkuu Msatafu Mohamed Chande Othman kwa jitihada zake kubwa alizofanya katika kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani ambapo naamini Kaimu Jaji Mkuu wa sasa hivi anaweza kuendeleza ile njia nzuri ambayo alianzisha Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu taarifa ya Kamati kwa ujumla, Mheshimiwa Mtolea alisema kwamba taarifa imebeba maudhui mengi ya kikatiba na kisheria. Labda niseme tu kwamba Kamati ya Katiba na Sheria mpaka sasa imeshawasilisha Bungeni taarifa tisa, tatu za kibajeti na sita za Miswada ya Sheria. Kamati pia ilitoa maoni na mapendekezo ya jumla kuhusu Wizara na taasisi inazozisimamia, masuala ya kazi, ajira na watu wenye ulemavu yapo katika taarifa rasmi ya Kamati yaliyosomwa hapa Bungeni tarehe 19 Aprili, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ngombale alizungumzia kuhusu Mabaraza ya Ardhi pamoja na uboreshwaji wa Kamati. Kamati pia inaishauri Serikali hususani Wizara ya Katiba na Sheria na tutaona uwezekano wa kukaa na Wizara hii ili kuweza kuzungumza na Mheshimiwa Waziri kuona uwezekano wa kesi za ardhi kurudishwa katika Mahakama ya Tanzania; kwa sababu tunafahamu kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107 inaitaja Mahakama kama ndiyo mhimili wa utoaji haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba upo mkinzano unaotokana na Mabaraza kuwa chini ya mihimili tofauti. Mfano, Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji yapo chini ya TAMISEMI, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya yapo chini ya Wizara ya Ardhi lakini pia ipo Mahakama Kuu ambayo inawajibika chini ya Mahakama. Hivyo, Kamati inaona kuna mwingiliano mkubwa wa haki katika Mahakama na Serikali na ipo sababu kubwa hapo baadaye kuwepo na kesi nyingi za kikatiba kupinga hukumu zilizotolewa katika Mabaraza ya Ardhi kwa kuwa jukumu la mwisho la utoaji haki lipo chini ya Mahakama ya Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Omary Mgumba amechangia kuhusiana na mgogoro wa wakulima na wafugaji. Jambo hili sina hakika kabisa kama limeelekezwa kwenye Kamati yangu au ile Kamati ya Utawala lakini nataka niseme tu kwamba ni kweli kabisa mgogoro wa ardhi ni mkubwa sana katika nchi yetu na tunaona kabisa kwamba ile misingi imara aliyotuachia Mwalimu Nyerere ya Watanzania kupendana inakwenda kuvunjika iwapo migogoro hii ya wakulima na wafugaji haitatatuliwa mara moja. Hivyo, tunaona kabisa kwamba Wizara ya Kilimo na Mifugo imeshindwa kutatua mgogoro huu na tunaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu sasa kuingilia kati ili kuweza kuondoa matatizo haya yaliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima itambulike kwamba hakuna mgogoro wa ardhi, mgogoro uliopo ni mwingiliano wa kijinai yaani criminal trespass kati ya wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, hatuna migogoro ya ardhi na naamini kabisa kwamba nchi yetu ina ardhi kubwa, mgogoro huu iwapo utatatuliwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa utaweza kwisha mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Frank Mwakajoka alizungumzia kuhusiana na watu kukata tamaa kupiga kura. Kamati yetu kwa kuwa inasimamia Tume ya Uchaguzi tunaiagiza Serikali kuongeza fungu kwa ajili ya Tume ya Uchaguzi ili kuendelea kutoa elimu ya mpiga kura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wananchi kukamatwa kwa kutoa taarifa za njaa, tunaishauri pia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira kuendelea kutoa taarifa kuhusiana na majanga na maafa ili iweze kuondoa kero kubwa ambayo inajitokeza hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Cecilia Paresso alizungumzia kuhusiana na ucheleweshwaji wa kesi kwamba viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakikamatwa na kesi zao hazichukui muda mrefu. Ni jukumu la utendaji haki kama ilivyo katika Katiba kwamba ni lazima haki iendelee kuonekana imetendeka. Naamini kabisa kwamba siyo jambo la busara kwa kiongozi kuendelea kubaki mahakamani kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tunaishauri Mahakama kuendelea kusikiliza kesi haraka hususani zinazowahusu viongozi wa vyama vya kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia itambulike kwamba zipo taratibu za rufaa ambazo zimeainishwa katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunawaomba wale wote ambao wana malalamiko kuhusiana na kesi basi wafuate taratibu za rufaa ambazo zimeainishwa katika Katiba, lakini pia katika sheria mbalimbali za nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la akinamama magerezani, Mheshimiwa Mbaruk alizungumzia suala hili. Kamati inakubalina na mawazo ya Mheshimiwa Mbunge kwamba maslahi ya watoto yazingatiwe yaani best interest of the child pale ambapo wafungwa wanajifungulia magerezani. Kamati inasisitiza kwamba watoto wanaozaliwa katika mazingira haya watazamwe kwa umakini kwa ajili ya haki zao kama watoto kwa mujibu wa Sheria ya Watoto ya mwaka 2009 lakini pia na Mkataba wa Haki za Watoto wa mwaka 1989. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Paresso pia aliendelea kusisitiza kuhusiana na mrundikano wa wafungwa gerezani na utawala wa sheria. Suala hili Kamati inalitambua na inaungana na maoni ya Mbunge kwamba Serikali na Mahakama zifanye jitihada za kutosha kupunguza mrundikano wa kesi na wafungwa magerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango iliyotolewa kwa ujumla ni kuhusu mrundikano wa wafungwa magerezani, wingi wa kesi mahakamani na kasi ndogo ya kumaliza kesi, haki za watu wenye ulemavu, suala la ajira na vijana, uongezaji wa bajeti katika Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ukaguzi wa miradi ya maendeleo, muda wa kikanuni uongezwe na jengo la Mwanasheria Mkuu wa Serikali lipewe kipaumbele. Kamati inakubalina na mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge na inaomba yawe sehemu ya mapendekezo ya Kamati na Bunge hili iyakubali kama maazimio ya Bunge yalivyotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba Bunge lako sasa lipokee na kuikubali taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na maoni na mapendekezo yaliyomo kwenye taarifa hiyo pamoja na yale mengine ambayo nimeyasoma katika Bunge lako hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia afya njema sote kuwa hapa. Pia, shukrani za kipekee niwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Rufiji kwa namna ambavyo wameniamini na wakanichagua kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa mara ya kwanza Jimbo la Rufiji tumeweza kuandika historia kwa sababu katika nchi hii toka tumepata uhuru na toka mfumo wa vyama vingi ulipoanza haijawahi kutokea Rufiji kwa Mheshimiwa Rais kupitia Chama cha Mapinduzi kupata kura nyingi. Kwa hiyo, nawapongeza sana wananchi wote wa Jimbo la Rufuji. Pongezi pia nikupe wewe Mwenyekiti, naamini kwa uzoefu na uwezo ulionao wa kisheria utatusaidia na utaliongoza Bunge hili vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwa Mpango huu wa Maendeleo kama ulivyowasilishwa, binafsi nina masikitiko makubwa sana kwa sababu sielewi sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji tuna matatizo gani katika nchi hii kwa sababu katika Mipango yote ya Maendeleo Rufiji tumeachwa mbali kabisa. Labda nilikumbushe Bunge lako kwamba Rufiji tumechangia asilimia kubwa ya upatikanaji wa uhuru wa nchi hii, tukizungumzia Pwani lakini na Rufiji kwa ujumla.
Pia Rufiji inabaki kuwa ni miongoni mwa Wilaya pekee ambazo tumeshawahi kuendesha Vikao vya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi lakini sasa ukiangalia Mipango mingi ya Maendeleo imetuweka mbali kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianzia suala zima la kilimo kama lilivyozungumzwa katika ukurasa wa 17, napata tabu kabisa kwa sababu Mpango huu wa Maendeleo hauzungumzii kabisa ni namna gani Rufiji itarudi katika ramani ya kilimo. Sote tunafahamu kwamba Rufiji miaka ya themanini ndiyo Wilaya pekee ambayo ilikuwa na uwezo wa kulisha nchi hii. Tunalo Bonde la Mto Rufiji, bonde hili ni zuri sana na tunaiomba Wizara pamoja na Kamati zinazohusika basi kufikiria ni namna gani wataweza kuliendeleza bonde hili. Pia tunafahamu kuna baadhi ya miradi kwa mfano ule mradi wa RUBADA ambao ulikuja pale Rufiji, naamini kabisa mradi huu ni mradi ambao watu wameutengeneza kwa ajili ya kujipatia pesa na hauna faida yoyote kwa Wanarufiji. Kwa hiyo, naomba kwanza Serikali ikae chini na kufikiria ni namna gani wataweza kupitia kumbukumbu zote walizonazo ili kuangalia ufisadi mkubwa ambao umeshawahi kufanywa katika mradi huu wa RUBADA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Rufiji tunayo ardhi nzuri na ardhi kubwa isiyokuwa na tatizo lolote la migogoro ya ardhi, tunaiomba Serikali sasa kufikiria mpango wa kuanzishwa Chuo cha Kilimo Rufiji ili sasa kiweze kusaidia suala zima la kilimo kwa sababu tunayo ardhi nzuri sana. Pia mchakato wa uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao, naishauri Serikali uanzie Rufiji kwa sababu tunayo ardhi nzuri yenye rutuba na tunalo bonde zuri. Niseme tu katika nchi hii hakuna ardhi iliyo nzuri kama ya Jimbo letu la Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika suala zima la viwanda, kumbukumbu zangu zinanionesha kwamba Mheshimiwa Rais pamoja na Makamu wake tarehe 9 Septemba, Makamu wa Rais alituahidi mchakato wa ujenzi wa viwanda Rufiji. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa hivi viwanda ambavyo vitajengwa kuanzia Rufiji kwa sababu kila aina ya kilimo sisi tunacho na tunaishauri Serikali sasa mchakato huu uanze haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye tatizo la maji. Ukurasa wa 46 wa Mapendekezo ya Mpango huu wa Maendeleo umezungumzia suala la maji. Sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji pamoja na Majimbo ambayo tunakaribiana, nazungumzia Kisarawe, Mkuranga, Kibiti pamoja na Rufiji yenyewe, tuna shida kubwa sana ya maji. Labda niseme katika Jimbo langu ya Rufiji ni 5% au 6% tu ya wananchi ndiyo wanaopata maji safi na salama. Katika eneo dogo la Tarafa ya Ikwiriri ambayo ndiyo walikuwa wakipata maji safi mota imeharibika huu ni mwezi wa tatu. Mchakato wa tathmini ya utengenezwaji wa mota upo katika Wizara hii ya Maji, huu ni mwezi wa tatu hatujui Katibu Mkuu wa Wizara hii anafanya mchakato gani ili kuweza kuharakisha mota hii kuweza kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoweza kuona maeneo mengine, Ziwa Viktoria wana uwezo wa kutoa maji sehemu moja na kupeleka sehemu nyingine katika Mikoa mbalimbali na sisi tunaishauri Serikali sasa Mpango huu wa Maendeleo kufikiria mchakato wa kuboresha huduma ya maji kwa kutoa maji katika Mto wetu wa Rufiji na kusambaza katika Wilaya zetu zote ambazo zinazunguka katika Jimbo la Rufiji, hii itasaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo, kwa mfano kule Ngarambe kuna tatizo kubwa sana la maji. Akinamama pamoja na watoto wanawajibika kuamka alfajiri kwenda kuchota maji na wengine hawarudi majumbani, wanachukuliwa na tembo, wanauwawa na maeneo mengine wanachukuliwa na mamba! Kwa hiyo, shida ya maji katika Jimbo la Rufiji ni kubwa sana. Tunaomba Mpango huu wa Maendeleo kulifikiria suala hili la maji kwa kuliboresha vizuri kwa kutumia Mto wetu wa Rufiji katika kuliweka sawa.
Mhershimiwa Mwenyekiti, nikija katika suala zima la afya, mimi nina masikitiko tena makubwa. Niseme tu kwamba tunayo Hospitali yetu ya Wilaya pale iliyojengwa mwaka 60 lakini toka mwaka 60 hakuna ukarabati wowote ambao umeshawahi kufanywa. Mimi mwenyewe nilishaanza mapambano kuweza kuhakikisha kwamba tunapata wawekezaji kutusaidia. Sasa tunaiomba Serikali kuharakisha huu Mpango wa PPP ili wawekezaji wa kutoka Uturuki waweze kutusaidia kujenga hospitali ya kisasa kabisa ambayo itakuwa na European Standard yenye mashine zote za kisasa. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kuharakisha Mpango huu wa PPP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tukija suala zima la elimu, niharakishe kidogo kwa sababu ya muda, niseme tu kwamba sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji tuko nyuma sana kwenye suala zima la elimu, hata Serikali imetuacha yaani tumekuwa kama watoto wa kambo, hatujui sisi tuna matatizo gani? Suala la elimu ni shida kubwa hasa ukizingatia Rufiji ni kubwa kuliko hata Mkoa wa Kilimanjaro lakini tuna shule moja tu ya sekondari ya kidato cha tano na cha sita kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa. Tunaiomba Serikali kufikiria mchakato wa kuboresha elimu katika Jimbo letu la Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo, kwa mfano kule Mtanange na maeneo mengine watoto hawasomi kabisa kutokana na umbali wa shule za msingi ambapo mtoto inabidi asafiri umbali wa zaidi ya saa tano, saa sita kwenda kufuata shule. Hali hii imewafanya wazazi wengi kushindwa kuwapeleka watoto wao shule. Kwa hiyo, naona kabisa kwamba mchakato huu wa elimu bure sisi wa Rufiji tutaachwa kando kabisa kwa sababu wazazi watashindwa kuwapeleka watoto wao shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija suala zima la mchakato wa benki, mimi niseme Rufiji ni Wilaya ya sita wakati wa mkoloni na ni Wilaya ya 21 wakati tunapata uhuru lakini utashangaa Wilaya hii ya Rufiji kwa namna ambavyo Serikali imeamua kuiacha hatuna hata benki kabisa. Tunawajibika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 120, kwa wale wananchi wanaotoka kule maeneo ya Mwaseni na Mloka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaishauri Serikali huu mchakato wa uanzishwaji wa Benki za Ardhi, kama ulivyoainishwa katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 35, tunaiomba Serikali sasa kufikiria benki hizi waanze kujenga katika Jimbo letu la Rufiji kwa sababu tunayo ardhi ya kutosha, hatuna migogoro ya ardhi, ardhi ni bure kabisa tunawakaribisha lakini tunaiomba Serikali pia kuona namna gani ya kuwekeza kwenye suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika suala zima la miundombinu, nina masikitiko haya mengine kwamba Rufiji japokuwa ni Wilaya ya zamani lakini tunabaki kuwa ni Wilaya pekee ambayo hatuna hata nusu kilometa ya lami. Kama tulivyoona Mapendekezo haya, hakuna hata sehemu moja ambayo inazungumzia Rufiji tutasaidiwa vipi kuboresha miundombinu yetu. Mama yetu Makamu wa Rais pamoja na Rais mwenyewe alituahidi kwamba tutajengewa lami barabara ya kutoka Nyamwage - Utete, ili iweze kusaidia kupunguza vifo vya akina mama ambao inabidi wakimbie Utete kwa ajili ya kwenda kujifungua. Pia barabara ya kutoka Ikwiriri – Mwaseni - Mloka yenye kilometa 90, tunaiomba Serikali kuharakisha mchakato wa ujenzi wa barabara hii na barabara nyingine kutoka Mwaseni - Mloka - Kisaki pamoja na kutoka Mwaseni - Mloka - Kisarawe. Barabara hizi iwapo zitajengwa zitasaidia kufungua biashara na wananchi wa Jimbo langu la Rufiji wataweza kufanikiwa katika mambo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunaishauri Serikali na tunaiomba iharakishe mchakato wa ujenzi wa Chuo cha Utumishi pale Ikwiriri. Tulishatoa ardhi kubwa lakini mpaka leo hii Wizara husika haijachukua hatua zozote za mchakato wa ujenzi wa Chuo hiki cha Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaishauri Serikali kuachana kabisa na mchakato huu wa mambo ya retention. Suala hili litatuletea shida kubwa na tunaiomba Serikali kuepukana nalo, kuacha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuishauri Serikali kuanzisha community centre. Community centre hizi zitaweza kusaidia wananchi wetu kwa maeneo mbalimbali ya vijiji ili waweze kujifunza mambo mbalimbali kwa ajili ya kunyanyua uchumi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naomba maombi yangu haya yote kama nilivyozungumza yaweze kuchukuliwa na kufanyiwa kazi. Vinginevyo kama Serikali haitachukua basi sitaunga mkono kabisa mapendekezo mwezi Machi yatakapoletwa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipewe taarifa kuhusu ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma ambacho kiliidhinishwa na Serikali ya Awamu ya Nne kujengwa katika Wilaya ya Rufiji ambayo tayari ilitenga eneo zaidi ya hekari 200 ambazo hazijatumika mpaka sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufahamu ujenzi wa Chuo hiki utaanza lini?

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapa pole Waheshimiwa Majaji na Mahakimu wote ambao wametajwa ndani ya Bunge hili ambao hawawezi kufika ndani ya Bunge hili kujitetea. Kanuni zetu za kilatini Mheshimiwa Tundu Lissu atakuwa mwenyeji kwenye hili right to be heard, rule of law ambazo zinatuongoza anazifahamu vizuri, lakini nitambue mchango Jaji Mkuu Mheshimiwa Mohamed Othmani Chande, amefanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha kwamba mahakama zetu zinakwenda vizuri kupunguza kesi za mahakama ambazo zilikuwa msongamano kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Rufiji kwa kunielewa, wananifahamu kule Rufiji naitwa jembe, wengine wananiita sururu. Ninashindwa kutambua uwezo wa kisheria au uwezo wa kufahamu wa ndugu yangu Tundu Lissu, kwa muda mrefu sana nimekuwa nikifuatilia mchakato na namna ambavyo akiendesha Bunge kwa muda mrefu sana kwa zaidi ya miaka sita nimekuwa nikimfuatilia. Mheshimiwa Tundu Lissu namfananisha na mwandishi wa vitabu vya movie, aki-act mwaka 1940 ile movie ya Ndugu Charlie Champlin. Kuna movie moja, political satire, hii ukiifuatilia vizuri inaendelea kiundani, Mheshimiwa Tundu Lissu ni mtaalam mzuri wa kuiga kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielezee uteuzi wa Mawaziri. Tunaongozwa hapa na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977, kama ambavyo imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara. Lakini katika Katiba hii, Ibara ya 54 na 55 inazungumzia kwa uwazi uteuzi wa Mawaziri. Ibara ya 56 inazungumzia mchakato mzima wa nani anaweza ku-qualify kuwa Waziri yaani kwamba mchakato huu, mtu atakuwa Waziri baada tu ya kuapishwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaongozwa na Sheria Na. 15 ya mwaka 1984 kama ambavyo Mheshimiwa Tundu Lissu ameizungumzia. Katika instrument of appointment ya Mawaziri ambayo Mheshimiwa Tundu Lissu amekuwa akiikazania kwa muda mrefu, siyo yeye tu hata Mwenyekiti wa Chama chao amekuwa akizungumza sana kuhusiana na sheria hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge hili lipate fursa ya kutufundisha kizungu inaonekana kuna shida ya kufahamu kizungu. Kwa mujibu wa Sura ya 299 ya sheria inayompa mamlaka Mheshimiwa Rais ya kuwaapisha pamoja na kuunda instrument yaani sheria hii inaitwa The Minister‟s (Discharge of Ministerial Functions) Act, Sura ya 299. Ukisoma kifungu cha tano cha sheria hii kinasema hivi ninaomba wataalam wa linguistic watusaidie ili waweze kumuelewesha huyu bwana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha tano cha sheria hii kinasema hivi; “The President may, may na shall ina maana kubwa sana kwa kizungu. Wataalam wa linguistic watusaidie kumfahamisha may ina maana gani na shall ina maana gani. Siyo hivyo tu kifungu hiki kimekwenda moja kwa moja kuzungumzia kwamba from time to time by notice published in the Gazette specify the departments, business and other matters responsibility for which he has retained himself or he has assigned under his direction to any Minister, and may in that notice specify the effective date of the assumption of that responsibility. (Makofi)
Sheria hii inasema wazi ni wakati gani. Mheshimiwa Rais wakati wowote anaweza kutengeneza instrument kwa sababu sheria hii haija-specify ni wakati Mheshimiwa Rais anapaswa kutoa gazette la Rais. Sheria hii haitoi muda. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais hajavunja Katiba yoyote kwa mujibu wa sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende mbele zaidi, amezungumzia suala zima la ESCROW kuna Majaji walishutumiwa not kushtakiwa. Naomba nimkumbushe vifungu vya sharia vinasema allegation however strong it may it cannot convict the accused person, hata kama shutuma zitakuwa na uzito wa kiasi gani haziwezi kumtia hatiani mshitakiwa.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 112 inazungumzia Tume ya Utumishi wa Mahakama. Tume hizi zimepewa uwezo mkubwa wa kujadili nidhamu za Majaji na Mahakimu. Ibara ya 113 inakazania kwenye suala hili zima. Bunge halina mamlaka juu ya Mahakama, hali kadhalika Serikali haina mamlaka dhidi ya Bunge na Mahakama. Kilichofanyika baada ya mapendekezo ya Bunge, Mheshimiwa Rais alikabidhiwa mapendekezo ya Bunge, kwa mujibu wa Ibara hii ya 113 Mheshimiwa Jaji Mkuu aliunda Tume, Tume ya Utumishi wa Mahakama ipo kwa mujibu wa Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Tume Rais hana mamlaka ya kumfukuza Jaji isipokuwa tu Ibara ya 113 inampa mamlaka Mheshimiwa Rais iwapo itaonekana Jaji amefanya utovu wa nidhamu na maadali baada ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kutoa mapendekezo yake. Jambo hili lilifanyika na Waheshimiwa Majaji hawa baada ya kupitia na jambo kubwa ambalo lilifanyika, Mheshimiwa Jaji Mkuu pamoja na Tume hii walitumia the Code of Ethics for Judicial Officers, pia kwa kuzingatia the independence of the judiciary walizingatia haya yote kimsingi na ilionekana kabisa wazi kwamba hakuna jambo lolote lililofanyika na taarifa hii ipo mbele ya Mheshimiwa Rais kwa tafiti zangu binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaenda kwa haraka. Kuhusu Mahakama ya Mafisadi imekuwa ikipigiwa kelele sana, sasa sijui kwa nini ndugu zetu hawa wanakuwa waoga, wanaogopa nini? Kwa mujibu wa taratibu na sheria kinachoweza kufanyika ni kufanya mabadiliko ya Sheria hii ya Uhujumu Uchumi ambayo Mheshimiwa Tundu Lissu ameizungumza hapa, Sura ya 200 imezungumzia kiundani kabisa. Division hizi za Mahakama Kuu zipo nyingi Tundu Lissu anafahamu, tunayo Division ya Ardhi, tunayo Division ya Biashara, tunayo Division ya Kazi, kwa mujibu wa taratibu na sheria hii kwa kufanya mabadiliko Mheshimiwa Jaji Mkuu anaweza akaunda special court kwa kupitia muundo huu ambao nimeuzungumzia hapa ambao inakua division ya Mahakama Kuu hakuna tatizo lolote wala Katiba haijavunjwa kutokana na hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka nizungumzie Muungano. Mheshimiwa Tundu Lissu anasahau kwamba Muungano wetu uliasisiwa na Waasisi hawa wawili, Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao. Kupitia Sheria Na. 4 ya mwaka 1964 iliondoa haya matatizo yote ambayo anazungumzia Mheshimiwa Tundu Lissu. Hata Mwenyekiti wa Marais Afrika anatambua mchango wa Tanzania katika kukomboa Bara la Afrika, siyo kwenda kusababisha Mapinduzi ya Zanzibar, Tanzania ilifanya kazi kubwa Afrika nzima siyo huko. Mimi nilichotegemea ni kwamba kwa Wapinzani wanapaswa kuleta hoja ya kusaidia Wizara hii ya Katiba na Sheria. Siyo kuanza kuzungumza maneno ambayo ni ya uchochezi maneno ambayo hayafai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea Mheshimiwa Tundu Lissu hapa angekuja na akatuambia ni namna gani tutaweza kulizungumzia Fungu Na. 40 ambalo Mheshimiwa Waziri hajalizungumzia, ni namna gani Mahakama itaweza kupatiwa fedha zake kwa mujibu wa taratibu na suala hili halijazungumzwa na Mheshimiwa Waziri. Lakini pia nilitegemea watu wa Upinzani wangezungumzia kuhusu Fungu Na. 55 la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili tume hii iweze kuongezewa fedha.
Ninaishauri Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuweza kuona mchakato wa kuongezea fedha Tume hii ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia niongelee suala la Mahakimu. Mahakimu wetu wanafanya kazi ngumu, nawapongeza sana kwa kuchapa kazi Mahakimu na Majaji wote Tanzania. Ninaomba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kuona uwezekano wa kuwaongezea mishahara Mahakimu wetu, pia kuangalia kuwapatia non- practicing allowance pamoja na rent assistance kwa ajili ya kuwapunguza ukali wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti ya mishahara kati ya Mahakimu na Majaji ni kubwa sana, ninaomba Mheshimiwa Waziri Tume ya Utumishi wa Mahakama kuweza kufikiria uwezekano wa kupunguza ukubwa wa tofauti ya mshahara kati ya Hakimu na Jaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka Tundu Lissu pia amezungumzia kuhusiana na Mkuu wa Wilaya kutoa maelekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na kusimama ndani ya Bunge lako hili Tukufu, lakini nichukue fursa hii kuwaombea Wabunge wote afya njema ndani ya Bunge lako hili, Mwenyezi Mungu awajaliwe afya njema pamoja na akili timamu katika kuisimamia Serikali yetu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu, lakini pia nichukue fursa hii kuwakumbuka wazee wetu waliotangulia, nikianza na Bibi yetu Bibi Titi Mohamed ambaye alikuwa Mbunge wa kwanza katika Jimbo la Rufiji, ambalo leo hii historia yake inapotea, hata pale tunapoona sherehe za kumkumbuka mama Bibi Titi Mohamed amekuwa akisahaulika, nichukue fursa hii kumkumbuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwakumbuke wazee kina mzee Ngauka, mzee Mkali pamoja na Marehemu mzee Mbonde, Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi! (Makofi)
Mheshimiwa Naib Spika, nimkumbuke pia Profesa Idrissa Mtulia ambaye ni Babu yangu huyu, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rufiji na Dkt. Seif Seleiman Rashid ambaye pia alikuwa Mbunge wa Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nizungumze hili kwa kuwa Rufiji imetoa mchango mkubwa sana katika Taifa hili letu. Asilimia zaidi ya 60 ya wapigania uhuru wa nchi hii wote walitoka Rufiji na kama hakutoka Rufiji basi atakuwa na asili ya Rufiji, hata wale Wamakonde watakuwa ni asili tu ya Rufiji. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme hili kwa kuwa Rufiji imekuwa ikisahaulika sana kwa muda mrefu sana! Nimesikiliza kwa umakini sana hotuba za Mawaziri wetu wote hata waliopita. Hotuba hata ya Waziri wetu wa Kilimo ameshindwa kuizungumzia Rufiji. Mimi sielewi unapozungumzia kilimo ukashindwa kuisema Rufiji, Bonde la Mto Rufiji, lakini pia hata Mawaziri wengine hata nikija pale kwa Maliasili na Utalii tunafahamu atasoma hotuba yake siku ya Jumanne, lakini nafahamu matatizo makubwa ya kero za wananchi wa Jimbo la Rufiji na inawezekana siku ya Jumanne nisiwepo, niseme tu, Wizara ya Maliasili na Utalii iliweza ku-introduce kodi ya kitanda ambayo ni gharama kubwa kila mwananchi wa Rufiji analazimika kulipa shilingi 130, 000/= kwa kitanda anachokilalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme hilo japokuwa nitachangia kwa maandishi. Nirudi katika hotuba yetu hii ya siku ya leo ya Wizara hii. Nimesikiliza kwa makini hotuba ya wenzetu Wapinzani baadhi ya waliokuwa wakichangia, lakini pia mchango alioutoa Mheshimiwa Keissy, siku ya jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Mheshimiwa Kessy amezungumza mambo mengi sana ya msingi ambayo, niseme Mheshimiwa Waziri ayachukuwe kwa kina sana, ule mgawanyo wa pato hili la Taifa, mgawanyo huu uende vyema na sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji tuweze kunufaika na pato hili la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wengine katika Bunge lako hili Tukufu wameomba wanunuliwe ndege, wengine wameomba meli, wengine wajengewe reli; tunafahamu siku Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hoja zake hapa atajikita sana kwenye reli na ununuzi wa ndege, lakini atasahau yale maeneo ambayo yanahakikisha Chama cha Mapinduzi kinaingia madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Rufiji limemchagua Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani kubwa sana wakiamini kwamba kero hizi za kwao walizonazo toka Rufiji inazaliwa mwaka 1890, kabla ya 1900 Rufiji ilikuwepo. Pia kwa kutambua kwamba Rufiji ni kubwa kuliko Mkoa wa Kilimanjaro, Rufiji peke yake, Rufiji hii ambayo ina shule moja tu ya Sekondari kidato cha tano na sita, basi Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu atusaidie sisi Rufiji na nazungumza kwa uchungu kabisa, tuweze kupata angalau barabara ambazo zitawasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo huu wa Pato la Taifa nawaomba Waheshimiwa Mawaziri wawe wanazingatia mchango wa Taifa katika Pato la Taifa. Sisi Rufiji tunayo Selous ambayo ni Hifadhi ya Taifa kubwa kabisa Afrika, lakini pia tunayo misitu, katika pato la Taifa Rufiji tunachangia zaidi ya asilimia 19. Mchango huu mkubwa wa Pato la Taifa tunaochangia Rufiji, mchango huu wote unakwenda kujenga barabara na kutengeneza reli maeneo mengine ya nchi na sisi Rufiji ambao tulikuwepo hata kabla ya uhuru, tunapoizungumzia Rufiji tunazungumzia wakati wa mkoloni ambao tulikuwa na wilaya sita nchini, Wilaya ya Rufiji ilikuwepo. Hakuna asiyefahamu boma lile la Utete, hakuna asiyefahamu katika historia ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina imani kubwa sana na Waziri wangu huyu, Profesa, sina ubavu wala uwezo wa kumpinga, kwa sababu kwanza yeye ni Profesa na uwezo wake umejidhihirisha baada ya Mheshimiwa Rais kumteua kwa nafasi aliyopata leo hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, yeye atakuwa shahidi mara ngapi nimemfuata kwa ajili ya kuzungumzia barabara zetu za Rufiji, atakuwa shahidi mkubwa. Nimemfuata mara kadhaa, lakini si kwake tu, nimekwenda mpaka kwa Makamu wa Rais kwa ahadi yake ya tarehe 9 Septemba, 2015 aliyoahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara ya Nyamwage kuelekea Utete. Rufiji ndiyo wilaya pekee ambayo haiunganishwi na lami japokuwa Rufiji ina zaidi ya miaka 55 katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali itufikirie, kipindi hiki kwa kweli tunawaomba sana. Ahadi za Marais, tukianzia ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati anakwenda kule Selous alipita barabara ya Mwaseni- Mloka, Ikwiriri kwenda Mwaseni, Mloka kule, akielea Selous, barabara hii ni mbovu sana. Leo hii kutoka Mwaseni - Mloka kufika Ikwiriri unatumia zaidi ya saa kumi kwa kilometa 90 peke yake, lakini kutoka Nyamwage kuelekea Utete, kilometa 33 tunatumia zaidi ya saa tano. Hii ni aibu, aibu kubwa sana kwa Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana basi Serikali yetu iweze kutufikiria. Ombi maalum kabisa kwake Mheshimiwa Waziri, nina imani na yeye kama nilivyosema, atufikirie barabara zetu hizi ambazo Marais wetu walituahidi. Barabara ya Nyamwage kuelekea Utete kwenye Makao Makuu ya Halmashauri yetu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri akisimama atueleze anafanya nini kuhusiana na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 257 wa kitabu chake umezungumzia barabara hii itakarabatiwa tu ukarabati wa kawaida. Sasa tunashindwa kuelewa, kwa sababu katika kikao chetu cha mkoa cha barabara Mhandisi wa Mkoa alituahidi kwamba barabara hii itarekebishwa kwa kiwango cha lami, lakini nashangaa katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri amezungumzia ukarabati mdogo. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri suala hili atujibu wakati anajibu hoja zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara ya kutoka Ikwiriri kuelekea Mwaseni, Mloka ni kilio kikubwa. Huku ndiko Serikali inakusanya zaidi ya asilimia 19 ya Pato la Taifa, watalii leo hii wanatumia zaidi ya saa kumi, tunawa-discourage. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa barabara hii ni barabara ya TANROADS sasa wafikirie ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda wangu ni mdogo, nikumbushie barabara ya Bungu kuelekea Nyamisati kwa ndugu yangu, Mwenyekiti wa Wandengereko, Mheshimiwa Ally Seif Ungando na barabara ya Kibiti kuelekea Ruaruke pamoja na suala zima la minara ya simu, nimwombe sana…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha!
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukuwe nafasi hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Muhongo kwa weledi wake na uchapa kazi katika Wizara hii ambayo anaimudu sana. Sina shaka na uchapa kazi wa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo machache, naomba uweze kutusaidia sisi Wananchi wa Jimbo la Rufiji wenye wimbi kubwa la umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rufiji ina ardhi yenye rutuba na bonde zuri katika kilimo. Serikali haijawahi kufikiria uwekezaji wa namna yoyote katika bonde hili toka Adam na Hawa mpaka sasa. Hali hii imepelekea uchumi wetu kuwa na hali mbaya. Ukosefu wa maji, hakuna shule za sekondari (Kidato cha Tano) japo kuwa Rufiji ni kubwa kuliko Mkoa mmoja wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wamepata chuki sana dhidi ya Serikali na hili ni dhahiri na matokeo ya uchaguzi uliopita uliokuwa na ushindani

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma alienijalia afya njema kusimama ndani ya hili Bunge lako hili Tukufu. Lakini pia nimtakie pole bibi yangu Nyankulu kutoka kule Mtanange, leo hii anapambana na vita ya kansa, namuombea apone haraka ili aendelee kuniombea.
Tatu niseme tu kwamba niwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Rufiji kwa namna ya kipekee kabisa kuniomba leo hii nibaki ndani ya Bunge kwa sababu siku ya leo ni siku ambayo Mwenge umefika katika Jimbo langu la Rufiji. Kwa kutambua kwamba Jimbo la Rufiji linabeba asilimia 50 ya Hifadhi ya Taifa letu, wakaniambia nibaki kwa ajili ya kuzungumza mambo ya msingi kabisa kwa ajili ya ustawi wa taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba hii ni nchi yetu sote, nianze kwa kusisitiza kwamba nchi hii ni yetu sote. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kumteua Brigedia Jenerali Gaudencia Milanzi. Tunatambua uteuzi wake una changamoto nyingi kwamba anapaswa kufanya kazi, kupambana na majangili ili ni kufuta aibu kubwa iliyotokea mwezi Januari ya kuuwawa kwa rubani wa ndege Bwana Roger Gower. Hakika jina la pilot huyu litakumbukwa katika nchi yetu na litaandikwa katika historia kwani alikuwa ni miongoni mwa wapambanaji wanaosaidia kupambana na ujangili katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia kwa undani sana taarifa za kwenye mitandao lakini pia nimefuatilia kwa umakini uwasilishwaji wa hoja mbalimbali ndani ya Bunge lako hili Tukufu. Pia nina fahamu zipo taarifa za wadau mbalimbali kutumiwa ili kujaribu kukwamisha bajeti ya Wizara hii; wadau mbalimbali wakiwemo na wanasiasa pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango mbalimbali iliyowasilishwa katika Bunge lako hili Tukufu imejikita kwa watu wengi kuzungumzia haki za wafugaji lakini wamesahau kwamba wakulima tunao na wana haki zao za msingi na wanachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa la nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere aliwahi kutukumbusha kuhusiana suala hili la kubagua au kubaguana, kuanza kuwabagua watu fulani kuwaona watu fulani wao ni muhimu kuliko watu wengine. Lakini naomba nisisitize Ibara ya 13(4) ambayo inafafanua kuhusu haki ya kutobagua watu au kundi fulani. Wakulima wamebaguliwa sana ndani ya hili Bunge lako Tukufu. Ninaomba niseme wakati wa uwasilishwaji wa Wizara ya Kilimo tuliona wafugaji wengi walifika hapa Dodoma, lakini pia wakati wa uwasilishwaji wa Wizara hii wafugaji wengi pia wapo ndani ya Dodoma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu Ibara ya 13(5) ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayofafanua mambo kadhaa na emphasis is mine na nisisitize hili:- “Katika kutimiza haja ya haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila, pahali wanapotoka, maono yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsia au hali yao ya maisha kwa namna ambayo watendewe wao ili waweze kupewa fursa au faida katika nchi hii.” Ibara hii inasisitiza haki ya kutobagua watu fulani. Naomba msisitizo huu Waheshimiwa Wabunge wauchukue ili tunapokuwepo hapa tujadili haki za msingi za wananchi wetu wote wa Tanzania bila kubagua huyu ni mfugaji au huyu ni mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vurugu hizi kati ya wakulima na wafugaji nizungumze kidogo, hazikuanza zamani sana sisi kule Rufiji tulizoea kuamka unakutana na mpunga; lakini leo hii mifugo imeingia, lakini silaumu kilichotumika ni Ibara ya 14 ya Katiba yetu ambayo inaruhusu Mtanzania kuishi popote. Ibara hii ya 14 ilitumia baada ya Waziri Mkuu Fredrick Sumaye pamoja Lowassa kuendeleza mchakato huu wa kuhakikisha kwamba mifugo inasambaa ndani ya nchi yetu. Si tatizo baya kwa sababu huu ni utekelezaji wa Ibara hii ya 14. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hapa nikumbushie Ibara hii ya 14 ambayo inakwenda sambamba na ukumbushwaji wa sheria mbalimbali. Ninaamini Wabunge wengi wanasahau kwamba tunazo sheria nyingi ambazo zinatuongoza katika nchi yetu hii, na iwapo tutawashauri wananchi wetu kufuata sheria hizi hakutakuwepo na mgogoro wowote kati ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikumbushie Sheria ya Matumizi ya Ardhi Namba 6 ya mwaka 2007 ambayo inatoa mchakato mzima wa namna gani ardhi itatumika na wapi wakulima waweze kufanya kilimo chao na wafugaji waweze kufuga wapi mifugo yao. Pia tunayo Sheria ya Mpango wa Vijiji sheria ya mwaka 1999 lakini pia tunao Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi. Mpango huu ni wa mwaka 2013 mpaka 2033. Tunayo sheria ya kuhifadhi maliasili pamoja na miongozo mbalimbali ya viongozi isiyokinzana na Katiba. Tunayo Ibara ya 26 ya katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatusisitiza wananchi wetu kufuata sheria. Tatizo hapa ni wananchi kutotaka kufuata sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe tu kwamba sheria hizi zilitungwa na Bunge hili, kama tunaona sheria hizi ni mbovu ni jukumu la Bunge letu hili Tukufu kubadilisha sheria hizi.
Katika kubadilisha sheria hizi Ibara ya 26 inazungumza wazi sina sababu ya kuisistiza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nirudi kwenye hoja zangu za msingi, hoja ambazo wa Rufiji wamenituma nije niwawakilishe hapa. Nianze kuzungumzia kodi ya kitanda. Niende haraka haraka, kodi hii ya kitanda ambayo ilitoka shilingi 8,000 kwenda shilingi 120,000 kodi hii iliundwa ili kuwakandamiza Warufiji. Mimi nikuombe kodi hii ambayo hata kama Mrufiji umelalia kitanda miaka 30 unawajibika kukilipia kodi iwapo unatoka nacho Rufiji unakwenda Wilaya zinazofuata Kibiti na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe kodi hii Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kuiondoa kodi hii ambayo ni kodi kandamizi.
Kwa wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji. Nitaomba taarifa kuhusiana na kuondolewa kwa kodi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 30(3) ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inanipa mamlaka mimi kupitia iwapo sheria au miongozo ya Serikali inakinzana na Katiba, mimi kama Mbunge na mwanasheria nguli nitakuwa na uwezo wa kufungua kesi ya Kikatiba ilikuweza kuomba Mahakama kutoa tafsiri fasaha ya kuondoa kodi hii ya kitanda ambayo ni kandamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa mbele ya Bunge lako hili Tukufu, baada tu ya kumaliza Bunge hili iwapo Waziri hataifuta kodi hii nitafungua kesi ya Kikatiba kwa sababu kodi hii ni kandamizi na ikinzana na Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona hiyo nisiizungumzie kiundani zaidi lakini nirudi kwenye kodi ya mkaa. Kodi hii ya mkaa imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Niliwahi kufanya tafiti kuhusiana na kodi ya excise duty, kodi hizi ambazo zinakuwa zinatolewa na Serikali ili ku-discourage consumption. Kuongezeka kwa kodi ya mkaa kunasababisha ongezeko kubwa la maisha kwa wananchi wetu wa Jimbo la Rufiji ambao wanategemea biashara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende mbele, nikimbie haraka haraka kidogo, naomba nizungumzie kuhusiana na pesa ya upandaji wa miti. Wananchi wangu wamekuwa wakichangia wanapokuwa wanalipa kodi ya mkaa wanachangia kiasi cha shilingi 830 kwa gunia kwa ajili ya kupanda miti. Naomba nipate taarifa kutoka kwa Waziri miti ambayo imeshawahi kupandwa na watu wa TFS ili kuweza kujiridhisha kwamba miti hiikweli inapandwa na pesa hii inatumika inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka kutokana na muda nizungumzie suala la migogoro…
MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitoe shukrani zangu za dhati kwako kwa kuniona. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema kuweza kuzungumza kwa mara nyingine kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze kwa kusema kwamba maji ni miongoni mwa mambo ya msingi kabisa ambayo yameainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020. Ukisoma ukurasa wa 86 wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi unazungumzia mchakato huu wa kusogeza karibu huduma za kijamii, lakini pia tatizo la maji katika Jimbo langu la Rufiji ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda siku zote nimekuwa nikisimama nikizungumza kwa masikitiko, lakini pia hata katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri sijaona sehemu yoyote katika hotuba yake kuzungumzia Rufiji kwa ujumla. Tatizo la maji Jimbo la Rufiji ni kubwa sana. Labda niseme tu kwamba ni asilimia tano tu ya wananchi wa Jimbo la Rufiji ambao wanapata maji safi na salama na hata hii asilimia tano ambayo tunaizungumzia ni katika Kata ya Utete tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata tatizo la maji Tarafa ya Ikwiriri na tumepeleka maombi kwa Katibu Mkuu kuhusiana na ukarabati wa moter ambayo imeharibika kwa muda mrefu toka mwezi wa Kumi na Mbili, lakini mpaka hii leo tunavyozungumza tatizo la maji bado lipo. Shilingi milioni 36 ambayo tuliiomba Wilaya ya Rufiji kwa ajili ya ukarabati wa moter katika Kata hii, Tarafa hii ya Ikwiriri mpaka leo hatujapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia kiundani, Rufiji sisi hatukupaswa kuwa na tatizo la maji kwa sababu kwanza tuna Mto Rufiji ambao una uwezo wa kusogeza maji maeneo yote. Ni masikitiko makubwa, toka Adam na Hawa, mto huu haujawahi kutumika, siyo kwa kilimo wala siyo kwa maji tuweze kutumia wananchi wa Jimbo la Rufiji, lakini pia mto huu kama ungeweza kutumika vizuri, Wilaya ya Kibiti ingeweza kupata maji safi lakini pia Wilaya ya Mkuranga, Wilaya ya Kilwa na Wilaya ya Kisarawe zingeweza kupata maji safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masikitiko makubwa. Niliwahi kuzungumza na Waziri wa Wizara hii akaniambia kwamba kwa sasa hivi Mto Rufiji hautatumika kwa sababu wanategemea visima ambavyo vimechimbwa. Sasa unajiuliza; tunaeleka wapi? Tunategemea maji ya visima ambavyo vinaweza vikakauka wakati wowote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara hii, nina fahamu kwamba Serikali yangu inachapa kazi na siwezi kupingana na ndugu zangu hawa Wahandisi ambao Mheshimiwa Rais amewateua katika Wizara hii. Ninachokiomba kwa mwaka unaofuata, basi Wizara hii iweze kutufikiria sisi wananchi wa Pwani kwa sababu naamini iwapo Serikali itaweka mpango mzuri kwa ajili ya kusaidia wananchi hawa hususan kwenye jambo hili la maji, basi hata Dar es Salaam itapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua matatizo ya maji siyo Rufiji tu, ukienda Temeke leo hii maji hakuna; ukienda Mbagala maji hakuna; ukienda Kigamboni kwenyewe maji hakuna; maji kidogo ambayo yanapatikana yanasaidia maeneo ya Upanga, Oysterbay na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara hii itusaidie. Leo hii tunachukua maji kutoka Kanda ya Ziwa tunaleta mpaka Tabora, zaidi ya kilometa 500, lakini ukisema uchukue maji ya Mto Rufiji uyasambaze maeneo ya Rufiji, Mkuranga, Kisarawe, Kibiti na maeneo mengine ya Dar es Salaam haitagharimu zaidi ya kilometa 200 kwa sababu kutoka Dar es Salaam mpaka Rufiji ni kilomtea 160 tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara hii, ni kwa muda mrefu sasa sisi wananchi wa Jimbo la Rufiji na Pwani tumenyanyasika kwa muda mrefu sana. Naamini ujio wangu Bungeni hapa basi itakuwa ni fursa kwa wananchi wangu waweze kufurahia usururu wangu, kwa sababu mimi najiita sururu kutokana na uchapakazi wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii sasa itusaidie. Matatizo ya maji yako katika kata zangu zote, tukiondoa Kata moja tu ya Utete. Kata ya Ngarambe wananchi wangu wanakanyagwa na tembo kwa sababu tu ya kwenda kutafuta maji; Kata ya Mbwala wananchi wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa tano kufuata maji; lakini pia hata kata nyingine zote hakuna maji safi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kutusaidia, tuingie katika mpango ili mradi mkubwa uweze kutokea pale katika Mto wa Rufiji tuweze kupata maji safi ambayo yataweza kusaidia wananchi wetu wa maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini iwapo tutatekeleza hili, tutakuwa tumetekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi na hii itatusaidia sana kuondoa kero kubwa ya wananchi ambayo imekuwa ni kilio cha muda mrefu. Masikitiko yangu kwa Rufiji nimekuwa nikiyazungumza kwa muda mrefu, inawezekana labda wenzangu walikuwa wakitoa malalamiko haya, hayafanyiwi kazi, lakini namwomba Mheshimiwa Waziri, mimi na Naibu Waziri tumekaa kwa muda mrefu sana tumekuwa tukizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara hii kwa namna ambavyo amekuwa akichapa kazi. Namwomba apate muda ili aweze kufika Rufiji ajionee kero hizi za wananchi. Leo hii watoto wanashindwa kwenda shule ili waweze kufuata maji kwenye maeneo ambapo kuna mito. Katika maeneo hayo ambayo inabidi waende kufuata maji kuna hatari nyingi. Kuna wengine ambao wanaliwa na mamba, lakini pia inasababisha watoto washindwe kwenda shule kwa sababu ya kwenda kutafuta maji. Wanasafiri zaidi ya kilometa tano, kilometa sita kwenda kufuata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kubwa leo hapa ni kumwomba Mheshimwa Waziri; nafahamu katika kitabu hiki, katika hotuba ya leo hajazungumza lolote kuhusiana na Rufiji. Hata kiasi cha fedha ambacho wamekitenga kwa ajili ya Rufiji, shilingi milioni 460 ni kiasi kidogo sana ambacho hakitaweza kutatua kero za maji katika Jimbo la Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikumbushe tu, Jimbo la Rufiji na Wilaya ya Rufiji ni kubwa kuliko Mkoa wa Kilimanjaro. Eneo la Rufiji ni zaidi ya square kilometa 13,600 ambayo ni sawasawa na Mkoa wa Kilimanjaro; lakini utajionea kwamba Rufiji tunapata maji asilimia tano tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Mawaziri, nafahamu wanachapa kazi sana, katika mpango unaokuja waweze kufikiria Rufiji ili kuwasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji kuondoa kero kubwa ya maji ambayo ni kilio na imekuwa ni aibu kwa muda mrefu. Kwa sababu ukianza kuzungumza matatizo ya maji Rufiji wakati tuna Mto Rufiji ambao leo hii wananchi hawawezi kusogea kutokana na hatari ya mamba, kwa kweli ni masikitiko makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yangu ni hayo. Naiomba Wizara ichape kazi kuweza kutusaidia wananchi wa Jimbo la Rufiji, Kibiti, Kilwa ambao tuko karibu; na naamini iwapo mradi huu utatekelezwa na Serikali basi tutaweza kutatua kero ya maji kwa maeneo yote ya Pwani mpaka Dar es Salaam ambako tunaamini kwamba hivi visima ambavyo leo hii Mheshimiwa Waziri anasema kwamba anachimba visima kwa ajili ya Dar es Salaam, ipo siku vitakauka. Sasa sioni sababu ni kwa nini tusichukue maji ya asili ambayo yapo; yalikuwepo toka Adamu na Hawa ambayo hata leo hayajawahi kutumika. Hayajatumika katika irrigation na hayajatumika katika maji safi ya kunywa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba Wizara hii iweze kufikiria. Naamini kabisa hata kama utakuwa na PhD lakini unafikiria visima, ukashindwa kufikiria maji ya asili ya Mto Rufiji, kwa kweli naona kuna matatizo. Labda kama Wizara ituambie kuna mpango mkakati wa kuamua kuitenga Rufiji kwa sababu mambo haya nimekuwa nikiyazungumza kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara hii sasa kukaa na Wataalam kufikiria mradi mkubwa wa maji ambao utaweza kusaidia watu wa Pwani na maeneo mengine ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru na naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia afya njema kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu. Pili, niwaombe Watanzania nchini kuendelea kupuuza kauli za wanasiasa waliochoka (wazee) ambao mimi nawaita wanasiasa wenye vioja wasiokuwa na hoja. Hivi karibuni kwenye Kigoda cha Mwalimu yupo mwanasiasa mmoja amediriki kumtukana Rais wa Awamu ya Nne, tunamshauri afuate Kanuni 21 ya Kanuni za Uongozi zinazowataka viongozi kufanya tafiti kabla ya kutoa kauli zao, nimeona niliseme hilo kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, nikupongeze kwa kuchaguliwa na Bunge hili kuwa Naibu Spika wa Bunge letu hili. Tunaongozwa na Ibara ya 86 ambapo sisi Wabunge ndiyo tumekuchagua. Pia Ibara ya 89 inatoa Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo ni jukumu letu sisi Wabunge kuzifuata ili sasa tunapokuwa na malalamiko tuyaelekeze huko kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama wapongezwa sana humu ndani ya Bunge lako hili Tukufu na mimi niseme tu kwamba, nawapongeza akinamama wote ndani ya Bunge hili na bila kumsahau mke wangu mpenzi Tumaini Mfikwa (Mrs. Mchengerwa na binti yangu Ghalia).
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme hayo nikinukuu yale maneno ya Bibi Titi Mohamed aliyotoa miaka ile ya 55 ambapo bibi huyu kwa mujibu wa wazalendo, wapigania uhuru wa nchi hii wanasema alikuwa ni baada ya Mwalimu Nyerere maana alikuwa tayari kuvunja ndoa yake kwa ajili ya kupigania uhuru wa nchi hii. Nami nawapongeza akinamama wote nchini kwa juhudi kubwa za kupambana na mfumo dume katika nchi yetu hii unaotumiwa na Viongozi wa Chama cha Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona nianze na hilo na nirudi sasa kujikita kwa mujibu wa Kanuni ya 106 ya Kanuni za Kudumu za Bunge hili ambayo inanipasa nizungumze bila kuomba mabadiliko katika bajeti yetu hii iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri. Nami niseme kwamba naunga mkono hotuba hii ya bajeti kwa asilimia mia moja, lakini nitakuwa na reservation zangu ambazo nitaomba Mheshimwa Waziri wa Fedha atakapofika hapa aweze kujibu baadhi ya hoja za msingi ambazo naamini kwamba zitasaidia katika kuinua uchumi wa nchi yetu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianzia kwanza kwa Kanuni za Sera ya Fedha zilizotolewa mwaka 2016 lakini pia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika ukurasa wa 16 unaozungumzia takwimu za umaskini. Nimefanya tafiti sana na kugundua kwamba takwimu zilizotolewa na Mheshimiwa Waziri amezipata kutoka kwa Halmashauri ya kuonesha kwamba Mkoa wa Pwani ni mkoa tajiri kuliko Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Mheshimiwa Waziri amedanganywa kabisa kwani Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa maskini kabisa katika nchi hii pamoja na Mikoa yote ya Kusini. Labda kama kuna ajenda ya siri sisi watu wa Pwani tusiyoijua, basi tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze hizo ajenda ambazo sisi hatuzijui.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitazungumzia takwimu, ukurasa wa tano wa taarifa ya Mkurugenzi iliyokwenda kwa Mheshimiwa Waziri ambayo Mheshimiwa Waziri ameitumia katika Bunge lako hili Tukufu inaonesha kwamba Watanzania wa Rufiji wanaishi kwa kipato cha Sh. 25,000 kwa siku, huu ni udanganyifu wa hali ya juu. Niseme tu kwamba hakuna Mrufiji anayeishi kwa Sh. 25,000 na hii siyo kwa Rufiji tu hata kwa Mkoa mzima wa Pwani hilo suala ni la uongo wa hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu hizi zinaonesha kwamba wananchi wa Mkoa wa Pwani wanapata pato la zaidi ya Sh. 700,000 kwa mwaka, huu ni uongo wa hali ya juu. Mimi kama Mwanasheria niko tayari kula kiapo kuthibitisha kwamba uongo huu haukubaliki ndani ya Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kwamba Rufiji tuna zaidi ya square kilometers 500,000 ambazo hizi zilipaswa zitumike kwa ajili ya kilimo, eneo hili kubwa liko ndani ya bonde la Mto Rufiji. Takwimu pia zinaonesha kwamba ni asilimia 0.6 tu pekee ya wananchi wa Jimbo la Rufiji ambao wanajishughulisha na kilimo katika maeneo haya. Pia ikumbukwe kwamba zaidi ya asilimia 99 ya wananchi wa Jimbo la Rufiji wanategemea kilimo, lakini kilimo hiki hata pale wakati ambapo tuliona matrekta yanakwenda maeneo mbalimbali Rufiji hatujawahi kuona trekta hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu hizi nitaendelea kupingana nazo, kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi iliyokuja kwa Waziri wa Fedha, katika ukurasa wa 23 inaonesha kwamba hata vile Vyama vya Msingi vimeanguka na vinadaiwa na wananchi. Hata ukiangalia wananchi wangu ambao wanategemea korosho, korosho imekwama na imeanguka hata katika soko la dunia. Ukiangalia takwimu wananchi wanadai zaidi ya bilioni moja kwa Vyama hivi vya Msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sielewi Mheshimiwa Waziri wa Fedha ana-rely kwenye information baada ya kutuma watu wake kwenda kutafiti na kupata takwimu za msingi kweli vinginevyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha atuambie agenda iliyopo ili kama wanataka kupeleka maendeleo sehemu fulani ijulikane, lakini siyo kutumia takwimu za uongo, nami niko tayari kula kiapo kutokana na suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia bajeti ya kilimo hakuna sehemu yoyote inayozungumzia Rufiji. Waziri wa Kilimo alikiri hilo na akaahidi kupeleka fedha, tunamshukuru kwamba ameahidi kuwasaidia vijana wa Jimbo langu la Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ukurasa wa 35 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, inazungumzia kwamba zaidi ya 4.9 percent ya bajeti ya Serikali itakwenda kwenye kilimo lakini Rufiji haipo katika maeneo hayo. Kwa hiyo, hii inaonesha wazi kwamba takwimu zilizotolewa ni za uongo na tunamwomba Waziri wa Fedha sasa kujikita katika kusaidia wananchi wanyonge na maskini. Tunategemea sasa asilimia 40 ya pato hili la Taifa ikasaidie wananchi wanyonge.
Mheshimiwa Naibu Spika, turudi katika suala zima la elimu. Tarehe 5 Machi, 1998, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:-
“Nobody is asking us to love others more than we love ourselves; but those of us who have been lucky enough to receive a good education have a duty also to help to improve the well-being of the community to which we belong; is part of loving ourselves!” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu alisisitiza akisema kwamba:-
“Education should be for service and not for selfishness”.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme hili kwa sababu Rufiji tuna shule moja tu ya sekondari kidato cha tano na cha sita japokuwa Rufiji ilianzishwa miaka ile ya 1890. Mgawanyo wa pato la Taifa ni kikwazo kikubwa na tunaona kwamba asilimia 40 iliyotengwa kwa ajili ya maendeleo haitawafikia wananchi wanyonge hususani wa Jimbo langu la Rufiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi majuzi niliuliza swali kuhusu wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji wa Tarafa ya Ikwiriri ambao wanapata maji kwa asilimia ndogo tu. Nilipokea majibu hapa kutoka kwa Waziri akituambia kwamba kiasi cha fedha tulichoomba kwa ajili ya ununuzi wa mota tusubiri bajeti ya 2017/2018, huu ni uonevu wa hali ya juu. Hawa ni wananchi wachache wasiopata maji safi na salama wanaambiwa wasubiri bajeti ya mwaka ujao ili kutoa shilingi milioni 36 tu. Ikumbukwe kwamba katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri kuna maeneo ambapo wametengewa zaidi ya shilingi bilioni 100 ya maji sisi Rufiji hakuna hata senti moja. Huu ni uonevu wa mgawanyo wa pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ninukuu hapa maneno ya Mwandishi Mashuhuri wa mashairi na mwanaharakati, Maya Angelou ambaye aliwahi kusema:-
“People will forget what you did, but people will never forget how you made them feel”.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema kwamba, maneno ya Mheshimiwa Waziri wa Maji yametufanya tusononeke na tuumie sana katika mioyo yetu kwa kuwa eneo hili la Rufiji ndiyo pekee lenye shida ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ninukuu Kanuni 21 za Uongozi, zinazozungumzia The Law of Solid Ground…

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Maxwell aliwahi kusisitiza neno moja la kuwataka...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa, nilifikiri unamalizia kwa kuunga mkono hoja, muda umekwisha.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Hapana siwezi.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa, japokuwa nilidhani kwamba ningeweza kuchangia mchana lakini nakushukuru sana inawezekana mchana kutakuwa na wachangiaji walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia katika Taarifa zote za Kamati kama ambavyo zimewasilishwa na Wenyeviti. Kwa masikitiko makubwa sana, taarifa hii ya Kamati ya Mifugo na Maji iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu, ukurasa wa 12 unazungumzia migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitishwa sana na taarifa hii ya Kamati ambayo kwa namna moja au nyingine wameshindwa kabisa kuona kwamba mgogoro kati ya wakulima na wafugaji ni mgogoro mkubwa ambao unahitaji Serikali kuingilia kati kwa haraka. Nimesikitishwa sana kwa sababu ukisoma taarifa hii, mgogoro kati ya wakulima na wafugaji umeandikwa nusu page, kwa kweli ni masikitiko yangu makubwa na hiki ni kilio cha wakulima wote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maana kwamba hatuwapendi wafugaji, tunawapenda sana wafugaji, lakini kwa namna ambavyo Serikali imeshindwa kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji na ndiyo maana nasimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu na mara zote ambapo nasimama tunaona kabisa hatari kubwa; ile amani tuliyoachiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inakwenda kupotea kwa sababu tu ya mgogoro huu kati ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimelisema hili kwa muda mrefu sana na hata Waheshimiwa Mawaziri wanafahamu hilo. Mgogoro huu kati yetu, sisi Rufiji kule, hatuna mgogoro wa ardhi naomba Bunge lako Tukufu litambue, Rufiji hatuna mgogoro wa ardhi; tulichonacho ni criminal trespass, mwingiliano wa jinai ambao unafanywa na wafugaji katika maeneo ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili ni kubwa na mwezi wa 11 watu wawili wameuawa, mkulima alichinjwa na mfugaji alichomwa moto akiwa hai katika maeneo ya Kilimani. Cha kushangaza sana hakuna kiongozi yeyote wa Serikali au Wizara aliyefika katika maeneo husika ili kuweza kutoa pole na kuweza kuongea ili kuondoa mgogoro huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masikitiko yangu makubwa sana na Wanarufiji wote leo hii wananiangalia kwenye TV, nimesimama mbele hapa; si Tanzania tu, dunia nzima Wandengereko wote dunia nzima na Warufiji wote wanajua; mgogoro kati ya wakulima na wafugaji unapaswa utatuliwe haraka sana vinginevyo unakwenda kuligawa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mambo mazuri ambayo alituachia Rais wetu wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kupendana Watanzania tunaona kabisa kwamba tunaanza kubaguana. Mimi nasema wazi mbele ya Bunge lako Tukufu, mgogoro huu unakuwa mgumu kwa sababu viongozi wa Wizara hii wengi ni wafugaji na wanashindwa kutatua matatizo ya wakulima. Naomba niishie hapo, message sent and delivered kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni tatizo kubwa la RUBADA. Tunayo hii Mamlaka ya RUBADA, Mamlaka ya kuendeleza Bonde la Mto Rufiji. RUBADA ilianzishwa mwaka 1978. Dhamira ya uanzishwaji wa RUBADA ilikuwa ni kuendeleza bonde pamoja na Mto Rufiji, lakini tunasikitika sana Warufiji baada ya Mamlaka hii kukabidhiwa Bonde la Mto Rufiji basi wananchi wa Rufiji wamekuwa maskini wa hali ya juu. RUBADA imeshindwa kuwasaidia Warufiji lakini pia RUBADA imeshindwa kuwasaidia wananchi wote wanaoishi na wanaopitiwa katika Bonde la Mto Rufiji kuanzia Morogoro na maeneo mengine yote ya Tanzania yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge liazimie sasa kuivunja RUBADA mara moja na Mamlaka yote ambayo inamilikiwa na RUBADA ibaki chini ya Halmashauri husika ikiwa ni pamoja na vijiji. Tunaamini kabisa Warufiji tukikabidhiwa bonde letu la Mto Rufiji tutaweza kuwatafuta wawekezaji watakaosaidia kilimo cha umwagiliaji. Naomba katika maazimio liingie azimio la kuifuta RUBADA, haina maslahi yoyote na hawana uwezo wa kuwasaidia Watanzania wanaoishi maeneo ya Rufiji zaidi ya kufanya udalali ambao hata sisi wenyewe tunaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikumbushie jambo lingine la mwisho, ni kuhusu ujenzi wa nyumba zinazojengwa na National housing.Tukiangalia dhamira ya Mwalimu Nyerere, mimi ni mjamaa kweli kweli! Tukiangalia azimio la Mheshimiwa Rais wetu wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, uanzishwaji wa National Housing ulilenga kuwasaidia Watanzania wanyonge, Watanzania wadogo wasio na uwezo, wafanyakazi wa Serikali, lakini leo hii National Housing ipo kwa ajili ya matajiri tu. Hakuna Mtumishi wa Serikali wala Mtanzania mnyonge mwenye uwezo wa kwenda kupanga kwenye nyumba za National Housing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliombe Bunge lako Tukufu, ile dhamira ya uanzishwaji wa National Housing kama ambavyo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza alivyoanzisha, kuchukua nyumba za Mabepari na kumilikiwa na Serikali. Dhamira ile ilikuwa ni kwenda kuwasaidia Watanzania wanyonge pamoja na Watumishi wa Serikali, naomba Bunge lako pia liazimie, National Housing iweze kuchunguzwa na kuangaliwa sasa ni namna gani itaweza kuwasaidia Watanzania walio wanyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe maazimio haya yaingie na niombe Mwenyekiti wa Kamati atakaposimama hapa aweze kujibu hoja hizi kama ambavyo nimeweza kuzieleza. Mgogoro wa wakulima na wafugaji unahitaji kuingiliwa kwa haraka sana na Serikali ili uweze kutatuliwa. Ni jambo la aibu sana kwa Kamati kuandika nusu page mogogoro wa wakulima na wafugaji. Watanzania wanauawa, Watanzania wanauana, wamepoteza dhamira ya kupendana wenyewe kwa wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ile miiko ya Mwalimu Nyerere aliyoianzisha wakati ule wa kupigania uhuru na hata baada ya uhuru. Tunaomba Kamati iweze kujiuliza ni kwa nini wamefikia hatua hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma vizuri ukurasa wa 13 unasema kwamba viongozi wa Serikali ambao wanashiriki katika kutatua migogoro hii hawakuwashirikisha wafugaji. Hili ni jambo la aibu kabisa. Ni wakulima wangapi wameshirikishwa katika mgogoro huu? Hili ni jambo la aibu, lakini tunafahamu kwamba kwa sababu wakulima hawana pa kusemea, lakini sisi kama viongozi wao tunasimama hapa kwa ajili ya kuwatetea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao wapiga kura walio wengi; lakini tunatambua kwamba katika pato la Taifa, kilimo kinachangia asilimia zaidi ya 70. Tuiombe Serikali itambue hilo. Pia hata Wizara ukiiangalia namna ambavyo inatupuuza wakulima. Ukiangalia katika bajeti iliyopita, Wilaya yetu ya Rufiji ambayo tuna ekari zaidi ya 13,000 ambapo kuna bonde zuri kwa ajili ya kilimo tungeweza kuuza Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika ya Kati, lakini Wizara ya Kilimo imetenga sifuri kwenye bajeti yake ya kilimo kusaidia wananchi wa Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusaidia kilimo tunaamini kwamba hata hiyo Tanzania ya viwanda hatutafikia huko. Naomba kuwasilisha lakini naomba; katika maazimio niliyoyaomba ni pamoja na kuifuta RUBADA kwa sababu haina faida yoyote kwa Watanzania. RUBADA wamekuwa madalali na sisi hawatusaidii lolote. Tunaomba bonde libaki chini ya wananchi wanaomiliki bonde hilo na maeneo ya mto ili tuweze kuwatafuta watu watakaoweza kutusaidia katika kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wana Rufiji wote duniani, nasimama hapa nami kuwasilisha ya kwangu lakini kwa kuzingatia maelekezo yaliyowahi kutolewa katika kitabu chake Paul Flynn, mmoja wa Wabunge wazoefu nchini Uingereza kinachozungumzia how to be an MP. Pia Profesa Phillip Collin naye katika kitabu chake aliwahi kuzungumzia mambo ya msingi kabisa ambayo Mbunge anapaswa kuyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumshauri dada yangu Mheshimiwa Sabreena atambue kwamba BAKWATA sasa ina uongozi ulio imara na wachapakazi sana. (Makofi).
Shekhe Mkuu wa sasa, Shekhe Zuberi ni mchapakazi sana na mambo haya ya dini tusiyalete kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu mmoja anaitwa K. Sachiarith mmoja kati ya wa washindi wa Global Award, katika Mkutano wa 136 wa Bunge wa Dunia uliofanyika kule Bangladesh, aliwahi kuzungumza maneno ambayo napenda niyazungumze katika Bunge lako hili Tukufu. Ndugu Sachiarith aliwahi kusema kwamba kama akinamama wangewezeshwa miaka 50 iliyopita basi dunia tungekuwa na Taifa jema sana (if women were empowered in the last fifty years we could have a better world).
Mheshimiwa Mwenyekiti, aliendelea kwa kusisitiza kwamba iwapo vijana wangezaliwa na akinamama waliowezeshwa miaka 50 iliyopita basi tungekuwa na vijana wazalendo wa Taifa, waadilifu na tungekuwa na Taifa lenye nguvu sana, Tanzania ingekuwa ni Taifa lenye nguvu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niseme maneno haya kwa sababu tunaona kabisa kwamba vijana waadilifu utawakuta upande huu tuliokaa wengi. Hapa nataka nimtofautishe ndugu yangu Bwana Tundu Lissu ni miongoni mwa ignorant pan-politician. Nimeona niseme hivi kwa sababu Tundu Lissu hana uzalendo wa Taifa hili, anaendekeza harakati, yeye ni mwanaharakati lakini si mwanasiasa. Kwa hiyo, tunawaomba Watanzania kumuepuka na kuepukana naye kwani dhamira yake ni kuligawa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 na 64 ni kutunga sheria na kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasheria wote duniani wanatambua kwamba nchi hii inaendeshwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa......
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii naikataa kwa sababu Shekhe Zuberi ni Shekhe ambaye anatambua elimu ya dunia pamoja na ya akhera. Ni mtu muadilifu na mchapakazi sana na ameweza kui-transform BAKWATA kuwa ni chombo kizuri sana kwa Waislam. Niwaombe Waislam wote kuendelea kuiamini BAKWATA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasheria wote duniani wanatambua kwamba nchi inaongozwa na katiba, sheria, kanuni na taratibu. Vilevile inaongozwa na taratibu za Chama Tawala ambacho ndicho kimeiweka Serikali madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niseme hili kwa sababu upo upotoshaji mkubwa uliozungumzwa na Tundu Lindu kuhusu Rais kwamba haitaki Katiba Mpya. Naomba nikumbushe Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 ambayo katika ukurasa wake wa nne (4) inazungumzia mambo yatakayotekelezwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Katika Sura ya Saba ya Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi pamoja na maneno mengine ukurasa 163 katika aya ya 144 inazungumzia mambo yafuatayo ambayo naomba niyanukuu hapa.
“Mchakato wa kutunga Katiba Mpya umeendeshwa na umefikia hatua ya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba ambayo itapigiwa kura ya maoni”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo nchi hii inaongozwa kwa mujibu wa taratibu kama ambavyo nimezisema.
T A A R I F A...
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii naikataa kutoka kwa layman huyu na naomba nimsaidie kwamba nchi inaongozwa na katiba, sheria na kanuni na taratibu ambazo Chama Tawala ndicho kilichosimamisha dola madarakani. Chama cha Mapinduzi kilikuwa na Ilani ya Uchaguzi ambayo wananchi walio wengi waliiona na kuisoma wenzetu walikuwa na tovuti ambayo ilikuwa ni vigumu kwa wananchi wa vijijini kuiona na kuisoma na kuikubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 118 ya Katiba ambayo Tundu Lissu amepotosha hapa jamii kwa kusema kwamba Mheshimiwa Rais amevunja Katiba kwa kutomchagua Jaji Mkuu wa Tanzania. Ibara ya 118 haimlazimisha Rais kuchagua Jaji Mkuu wa Tanzania. Ibara ya 118 iko wazi kabisa. Mheshimiwa Tundu Lissu anaifahamu sheria na anaijua Ibara hii imezungumza vizuri lakini anachofanya ni kupotosha Watanzania na kuleta taharuki katika nchi yetu hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa masuala mengi kuhusu demokrasia na utawala bora. Chama cha Mapinduzi kinaongozwa na Ilani na ukurasa wa 146 umezungumzia demokrasia na utawala bora. Nataka niseme hapa kwamba chama hiki kina demokrasia ya kutosha na unapomwona nyani anamtukana mwenzie ni vyema akajiangalia nyumani kwake. Chama hiki kimekuwa na Wenyeviti kadhaa kila baada ya miaka kumi wenzetu wamekuwa na Mwenyekiti amekaa madarakani zaidi ya miaka 20. Hauwezi kuzungumzia demokrasi wakati nyumbani kwako kunaungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii mwaka 1961 ilikuwa na Rais wa kwanza alikuwa Mzanaki, Mheshimiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Baada ya Mwalimu Nyerere wananchi walimchagua Rais wa Awamu ya Pili, Mzee wetu Mheshimiwa Ally Hassan Mwinyi, alikuwa Mzaramo wa kutoka Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1995 baada ya kupitishwa mfumo wa vyama vingi 1992 tulimchagua Mheshimiwa Benjamin Mkapa, huyu alikuwa Mmakonde kutoka kule Kusini. Mwaka 2005 tulimchagua Mheshimiwa Dokta Jakaya Mrisho Kikwete huyu alikuwa Mkwere kutoka pale Pwani. Taifa letu leo hii tunashuhudia kuwa na Rais Msukuma kutoka Kanda ya Ziwa. Hii ni demokrasia ya hali ya juu ambayo wenzetu hawana.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema nyani akawa anaona kundule kuliko kutukana wenzio wakati wewe mwenye una matatizo.Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeze katika kuishauri Serikali yangu njema ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianzie hapo kwenye uzalendo, miaka ya 90 Mwalimu Nyerere aliwahi kumthibitisha Kawawa katika moja ya mikutano yake pale Mnazi mmoja kusema kwamba Kawawa ni muadilifu sana na alikuwa tayari kutoa machozi kuthibitisha kwamba Kawawa alikuwa ni muadilifu. Nami ndani ya Bunge lako Tukufu naomba kuthibitisha kwamba iwapo siku moja Wabunge walio wengi wakasema kwamba mambo mazuri anayofanya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa nchi hii si uzalendo, basi nitaliomba Bunge lako hili Tukufu kufuta hili neno uzalendo katika dictionary ya Kiswahili. Kwa sababu mambo makubwa anayoyafanya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni uzalendo wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwa maneno mawili matatu ambayo nimeyaacha pembeni. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana wakati unahitimisha hoja yako hapa...
Nikukumbushe jambo moja, kwanza, tuiangalie kada ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo ambao wamekuwa wakipata mishahara midogo. Zipo taarifa wako Mahakimu zaidi ya 118 ambao hawajapandishwa vyeo na hao ni Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kwa hali ya uchumi tuliyonayo ni vyema tukawaangalia Mahakimu pamoja na Wanasheria wa Serikali ili kuwawezesha fedha kidogo kwa ajili …
(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa napenda niseme kwamba Taifa hili linategemea Bunge na uzalendo wetu ndio utakaoliweka Bunge hili katika…
(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja na nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kila jambo alilolifanya katika Bunge hili.
MWENYEKITI: Ahsante sana.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nampongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mbunge na Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ya kuwatumikia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache sana. Jambo la kwanza, naipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri ya kuwatumikia wanyonge; pili, nyongeza ya Wizara, hii Bajeti itaweza kuwasaidia Watanzania wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Jimbo langu la Rufiji. Kwa bajeti mbili sasa za Wizara hii, Serikali imesahau Wilaya ya Rufiji. Mwaka 2016 haikutengwa fedha yoyote kwa ajili ya Hospitali yetu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rufiji ni moja ya maeneo ambayo Serikali inapaswa kutoa kipaumbele sana. Hii ni kutokana na kwamba, kwa muda mrefu Jimbo la Rufiji limesahaulika. Kwa sasa tuna changamoto kubwa sana za kiusalama; kumewepo na ujambazi mkubwa na mauaji yanayoendelea; na kunahitajika mahitaji makubwa ya huduma bora za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali yetu ilijengwa mwaka 1960, lakini mpaka sasa haijawahi kukarabatiwa na majengo mengi ni mabovu yanayohitaji kubomolewa. Hakuna hata vitanda vya upasuaji; kilichopo kimoja ni cha miaka ya 1960; hali ya hospitali ni mbaya sana. Wakati wote yanapotokea matatizo makubwa kwa watu kudhuriwa kwa risasi, tunalazimika kusafirisha majeruhi kwenda Wilaya ya jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rufiji ilizaliwa kabla ya uhuru, lakini ndiyo Wilaya yenye matatizo makubwa. Umuhimu wa kuiboresha Hospitali ya Wilaya hauepukiki, kwa kuwa umbali uliopo kutoka Rufiji kwenda Hospitali ya Mkoa wa Pwani ni wa masaa zaidi ya sita kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Utete. Wagonjwa wengi hufia njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naipongeza Serikali kwa kutuletea Mganga Mkuu Mchapakazi. Naomba huruma ya Mheshimiwa Waziri, akisaidie Kituo cha Afya Ikwiriri kuongeza vifaa na ununuzi wa jenereta; Kituo cha Afya Moholo, kutuongezea fedha za ununuzi wa vifaa; na ujenzi katika Kituo cha Afya Mwaseni Mloka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri akifika hapa azungumze kauli ya Wizara yake ili kuweza kusaidia Watanzania wanyonge walioko Rufiji ambao hukosa msaada wa matibabu kutokana na hali ya Hospitali yetu ya Wilaya iliyojengwa mwaka 1960; akinamama wanakufa kutokana na uhaba wa Watumishi, kuwahudumia majeruhi wanaoshambuliwa na majambazi, matatizo yanayoendelea kila wiki sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipa fursa. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema, nawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji kwa kuendelea kuniombea dua hususani katika kipindi hiki ambacho ni kipindi kigumu kabisa kupata kutokea kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani hususani wakazi wa Kibiti, Rufiji na Mkuranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kufanya kazi nzuri kabisa katika Wizara hii ambayo ni moja ya Wizara ngumu kabisa katika nchi yetu hii. Mheshimiwa Waziri yeye pamoja na timu yake wamefanya kazi nzuri na mimi nawapongeza sana, sisi wananchi wa Rufiji wametusaidia kwa mambo kadhaa ambayo nitayazungumza hapo mbele lakini pia nimpongeze Mkurugenzi yule wa Misitu Ndugu Mohamed, nimpongeze Meneje wetu wa TFS kutoka kule Rufiji ambae marazote amekuwa akitatua kero za wananchi wangu na mimi namfananisha Profesa Maghembe na kanuni ya kwanza ya uongozi iliyowahi kutolewa na Dkt. John Maxwell ambae aliwahi kuandika kitabu chake The Laws of the Leadership akisema kwamba; “Personal and organizational effectiveness is proportional to the strength of a leadership” na mimi namuona yeye kama ni kiongozi ambaye ameweza kuimiliki Wizara hii na ninaamini Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati anakuteua aliamini wewe ni muadilifu na umechapa kazi. Wizara hii ina madudu mengi sana na kama ungekuwa umeyumba kidogo basi Wizara hii kwa kweli ingekushinda mapema sana.

Lakini nikupongeze kwa kusimamia Ibara ya 26 ya Katiba na kumtaka kila Mtanzania kusimamia na kufuata sheria za nchi yetu na hii nimeiona kwasababu wakati wa mijadala ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii tumeona hoja nyingi zinazoibuka ni hoja zilizopo kwenye Wizara ya Kilimo na Mifugo na ni wewe sasa umekuwa kama Waziri wa Kilimo na Mifugo lakini pia umekuwa kama Waziri wa Ardhi na umeendelea kuchapa kazi na mimi naomba niwakukmbushe Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakumbuke kwamba Ibara ya 26(2) inatupa mamlaka sisi Wabunge iwapo tunaona sheria yoyote ambayo inasimamiwa na Profesa Maghembe sheria ile inakinzana na matakwa ya nchi yetu tuliyonayo sasa basi ni vyema Wabunge sasa tukaleta sheria ile ndani ya Bunge lako hili tukufu kupitia Ibara ya 64 ya Katiba ili tuweze kubadilidha sheria ile na tusimlaumu Profesa Maghembe kwa kuwa anasimamia Ibara ya 26 ya Katiba ya kusimamia na kufuata sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magazeti mengi ya wiki hii yameandika mambo mengi kuhusu Rufiji, Kibiti na Mkuranga. Gazeti la leo la Citizen limeandika taarifa kwamba; “Why Rufiji residents are reluctant to cooperate over murders” lakini gazeti la jana ninalo hapa limeandika taarifa kwamba; “Rufiji families pain after losing their lovely ones.”

Jana mmoja wa wahanga aliyepigwa risasi siku tatu zilizopita amefariki jana alipigwa yeye na baba yake, yeye lipigwa risasi ya tumbo na jana amefariki na tunamshukuru Mbunge wa Kibiti kwa kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba mwili ule unafika Kibiti na shughuli za maziko zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie katika Bunge lako hili tukufu, unao Wabunge watatu ambao wanaishi katika maisha magumu sana kupata kutokea katika nchi hii; Mbunge wa Mkuranga, Mbunge wa Kibiti pamoja na Mbunge wa Rufiji. Tunaishi katika maisha magumu sana na siyo sisi tu hata katika familia zetu, lakini pia hata wapiga kura wetu wanaishi katika maisha magumu sana. Wananchi wamekonda sana hawawezi hata kushiriki katika shughuli za maendeleo hali ni mbaya sana na tunaiomba Serikali jambo hili kulifanyia kazi haraka kwasababu jambo hili linaendelea kutanuka na jambo hili siyo dogo kama ambavyo Wabunge wengine wanaweza kufikiria hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wamekuwa wakihoji maswali ni kwa nini Wabunge hawazungumzi ndani ya Bunge? Tunafanya hivi kwa makusudi kabisa lakini tunataka wananchi wetu wajue tunafanya kazi kubwa kuhusiana na jambo hili lakini yapo mambo sisi hatuwezi kuyazungumza kwenye Bunge hili.

Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani wananchi wangu wa Ikwiriri wanakushukuru sana kwa kufika, kujionea familia ambazo ziliathirika ambazo waume zao wamepigwa risasi na kufariki, wananchi wangu wanakushukuru sana. Lakini nataka niseme Serikali isikie na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ajue kwamba mambo haya yanayotokea hayatokei kwa bahati mbaya, mambo haya yana root cause, mambo haya yamepangwa, tunataka Serikali ijue hilo. Yapo mambo mengi, zipo chuki nyingi ambazo zimejengwa kwa wananchi, zipo chuki nyingi, yako mambo mengi ambayo yalifanyika yanatoa kero kubwa kwa wananchi ndiyo maana hata gazeti la leo lilipoandika taarifa hizi mimi siashangaa sana kwasababu ninajua kwamba yako mambo ambayo Serikali sasa inapaswa kuyafanya na inatakiwa iyafanye sasa wala isisubiri kwa sababu jambo hili ni kubwa na linaendelea kutanuka kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi naomba katika miongoni mwa mambo ambayo sisi tunaendelea kumpongeza Rais wetu ni terehe 31.03.2017 Rais Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kufanya kikao chake na Waziri Mkuu wa Ethiopia alikubali kuwasaidia Watanzania kwa kuonyesha dhamira ya kujenga Stigler’s gauge iliyopo kule Rufiji ili wananchi wetu waweze kupata umeme wa uhakika kwani tunaamini kabisa miongoni mwa kero kubwa za wananchi wangu ni kutokuwa na umeme kwa takribani miaka miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mwaka wa pili sasa wananchi hawana umeme wa uhakika sasaa hizi ni miongoni mwa kero kubwa ambazo wananchi wangu wanazo na leo nazungumza kwa uchungu kabisa, kero hizi muunganiko wa umeme ni kilometa nane tu lakini Waziri wa Nishati na Madini ameshindwa kutuunganishia umeme kwenye Gridi ya Taifa kwa miaka mwili wananchi wa Kibiti, wananchi wa Rufiji na wananchi wa kutoka kule Kilwa hawapati umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili na tunaamini kabisa kwamba uzalishaji wa umeme upo kwenye Stigler’s gauge utasaidia upatikanaji wa umeme katika maeneo mengine hiyo ni miongoni mwa kero kubwa tulizonazo kwasababu tatizo hili ni kero kama nilivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo tatizo la barabara ambalo Mheshimiwa Rais amekubali kutujengea barabara yetu ya Nyamwage kwenda Utete na mimi naomba nimpongeze na ninaomba wananchi watambue kwamba kero hii ya barabara imepatiwa ufumbuzi nasema haya kwa sababu ya kiini cha tatizo tulilonalo, wananchi wanalalamika sana na hatuna sababu ya kwa kweli kwa nini tuendelee kukaa kimya.

Nikuombe sasa Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii nirejee kwako, zipo kero katika maeneo yetu. Kwa mfano, katika Kata ya Kipugira watu wako wanaweka GPS kwenye nyumba za wananchi wetu, lakini naomba niikumbusghe Wizara yako kwa kusimamia Katiba; Ibara ya 16 ya Katiba inatoa uhuru wa faragha, lakini swali hili nilimuuliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ni kwa nini Wizara yako inaweka GPS kwenye nyumba za wananchi wangu? Wanavunja ibara ya 16 ya Katiba ambayo inatoa haki ya faragha ambayo kila mwananchi anayo haki ya ku- enjoy haki ya faragha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimuombe Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa unipe majibu kuhusiana na jambo hili ni kwa nini Wizara yako sasa inakiuka Ibara ya 16 ya Katiba lakini pia nimuombe Mheshimiwa Waziri akisimama hapa atuelezee tarehe 9 Septemba Waziri Mkuu alifika Rufiji na katika maeneo aliyokwenda ni pale Utete na alijionea wananchi walikuwa na malalamiko mengi sana. Upo msitu wa Kale ambao wananchi wa Utete pamoja na Chemchem wamekuwa wakiutumia kwa kilimo kwa miaka mingi sana.

Mheshimiwa Waziri naomba nikukumbushe nafahamu kuna tamko la Waziri Mkuu la upimaji upya wa maeneo yetu, lakini tukumbuke kwamba michoro ya awali ambayo Wizara yako inatumia ni michoro iliyochorwa na wakoloni mwaka 1936. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utambue dhamira ya wakoloni ya kuchora michoro ile ni kwa sababu population ya Tanzania ilikuwa bado ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ule wa mkoloni tulikuwa tunazungumzia population ya watu milioni nane mpaka milioni 10. Lakini leo hii Mheshimiwa Waziri tuna watu zaidi ya milioni 55 na Rufiji wakati ule tulikuwa kuna watu ambao walikuwa hawazidi hata 20,000; 30,000, lakini leo hii tunapozungumza tuna wananchi zaidi ya 200,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe ulisimamie hili, lakini hii ni pamoja na Kata yangu ya Mbwala katika vijiji vya Nambunju pamoja na Kitapi, maeneo haya yote Wizara yako imeanza kuyapima upya na Wizara sasa inachukua maeneo yote ambayo wananchi walikuwa wakiishi na kutaka kuyafanya maeneo yale ya misitu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri uzingatie hili kwani ukichukua maeneo haya wananchi hawatakuwa na pa kwenda kabisa. Nikuombe ulisimamie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine kuhusiana na hotel levy; kodi hii ya hotel levy ambayo imekuwa ikitolewa kwenye nyumba za kulala wageni, kodi hii ni kero kubwa sana. Tukuombe sasa Wizara yako iweze kulingalia kulipitia kwani wananchi wanaomiliki nyumba hizi za wageni wanalipa shilingi 100,000 ya leseni kwenye Halmashauri, lakini pia wanalipa hii hotel levy. Wakati huo huo wanalipa tena kodi ya mapato TRA shilingi 560,000, wakati huo huo wanalipa hotel levy, wanalipa tena leseni, wanalipa gharama kubwa sana. Wananchi wangu kuanzia Jaribu Mpakani kwenda moja kwa moja Kibiti mpaka kule Mkuranga na Rufiji wanalalamika sana kuhusiana na kodi hii. Na nikuombe Mheshimiwa Waziri basi muweze kuingalia na kuweza kuona namna gani mtaweza kuitatua suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija pia katika suala zima la mahusiano kati ya Wizara yako na wananchi wetu wanaozunguka vijiji, nikuomba Mheshimiwa Waziri sasa ukija kujibu hapa ueleze mkakati wako wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 4, mwezi wa Tano, mwaka huu, 2017, nilisimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu, nikitoa pole kwa familia ya ndugu Chanjale aliyepigwa risasi kule Ikwiriri Kata ya Umwe, na leo nimesimama kwenye Bunge hili Tukufu nikitoa pole kwa familia ya mmoja wa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM aliyepigwa risasi zaidi ya nane jana, Ndugu Alife Mtulia ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kutoka Rufiji pia ni mkazi wa Jimbo la Kibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio haya yanayoendelea katika eneo letu la Pwani yanadhamiria kutukwamisha kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo nami nataka niendelee kuwasihi wananchi wa Rufiji, Mkuranga na wakazi wa Kibiti kuendelea kuchapa kazi na kuendelea kuwa na imani na Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi. Hapa nataka niwakumbushe tu kwamba hakika Mwenyezi Mungu amekadiria maisha ya kila mwanadamu, na tunaamini kabisa kwamba mwanadamu anapozaliwa miezi mitatu tu akiwa tumboni mwa mama yake tayari Mwenyezi Mungu anakuwa ameshamuandikia mambo yake yote katika dunia. Qurani inasema Kulla maagh yuswibana inna maagh katana llaahu lanah ikimaanisha kwamba hakika Mwenyezi Mungu ameshamkadiria mambo yake kila mwanadamu aliyezaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu, kwanza kabisa wananchi wa Rufiji tunatambua sana umuhimu wa elimu na umuhimu wa elimu hii kwa sisi wenye imani ya kiislamu tunatambua kwamba wahyi wa kwanza kabisa Mtume wetu Muhammad kuupokea ilikuwa inahusu elimu. Katika Sura ile ya Iqra ambayo Mtume wetu alikabidhiwa na akiambiwa asome, niseme mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba umuhimu wa elimu umesikilizwa katika kila sehemu na wananchi wa Rufiji wamepata bahati kubwa ya kupata Mbunge ambaye ni msomi na ana uwezo wa kusaidia kuwapambania katika jambo hili la elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza sana Serikali, nimpongeze sana Waziri wa Elimu. Kwanza kabisa Waziri wa Elimu alivunja historia na rekodi kwa kufika Rufiji kwa mwaliko wa Mbunge, alifika Rufiji akajionea hali ya miundombinu ya shule zetu za Rufiji, wananchi wa Rufiji wamenituma nikuambie wanakupongeza sana na uchape kazi sana. Wako nyuma yako, lakini kwa namna ya kipekee kabisa wanakushukuru sana kwa kutoa shilingi milioni 259 kwa ajili ya ukarabati wa shule ya sekondari ya Utete. Wananchi wa Rufiji pia wanakupongeza Mheshimiwa Waziri kwa kukubali ombi la Mbunge la kutoa kibali cha shule ya sekondari Umwe ambacho kilikaa kwa zaidi ya miaka kumi kutosajiliwa. Wananchi wote wa Ikwiriri wanakupongeza sana na wanakukubali kweli, tunakuombea afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wamenituma, wameniambia kwamba walikupa maombi ya kukarabati shule yetu ya sekondari ya Muhoro pamoja na shule ya sekondari ya Ikwiriri. Hali ya miundombinu ya shule zetu umejionea Mheshimiwa Waziri, tunakuomba sasa utusaidie. Kwa sababu katika Mkoa wa Pwani, Rufiji umeweza kutupatia shilingi milioni 259 tu, tunakupongeza. Wananchi wa Kibiti pia kupitia kwa Mbunge wao, Mheshimiwa Ally Seif Ungando, wameniambia pia nikuambie wanakupongeza sana kwa kutoa kiasi cha shilingi 1,700,000,000 kwa kukarabati shule ya sekondari Kibiti, wanaomba pia uwasaidie kukarabati shule ya sekondari Zimbwini, shule ya sekondari Bungu, shule ya sekondari Mlanzi pamoja na shule ya sekondari Nyamisati ambayo umetoa shilingi milioni 260 pamoja na shukrani kwa kutoa shilingi milioni 253 kwa kukarabati shule ya sekondari Mtanga kule Delta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Rufiji umetoa kwa shule moja, nikuombe sasa utusaidie wananchi wa Rufiji, wapo wengi hapa wanaomba wapatiwe viatu kwa kuwa wana miguu, binafsi miguu sina.

Kwa hiyo, nikuombe lile tamko lililowahi kutolewa na Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Kwanza la miaka ya 1970 la kuboresha elimu katika maeneo ya watu ambao walikuwa hawajasoma sana, leo hii tumejionea Maprofesa hapa kama Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, ni miongoni mwa watu waliosoma wakati ule ambapo waliweza kusaidiwa na Mwalimu Nyerere na wakapata elimu kwa kuwa maeneo yao hayakuwa na mwamko wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuomba watu wa Rufiji sasa utusaidie, utuletee mwamko wa elimu kwa kuboresha miundombinu ya shule zetu na wananchi wanaamini kabisa kwamba maombi yao haya utayachukua, utayapokea na kuyafanyia kazi. Pia kwa namna ya kipekee wanaomba utusaidie kwa kupitia Mfuko wa Elimu utuboreshee shule yetu ya msingi Umwe, shule ya msingi Mgomba, shule ya msingi Muhoro, shule ya msingi Ngarambe, na ninamuomba Waziri wa TAMISEMI pia alichukue hilo na aone umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaboresha suala zima la elimu katika maeneo yetu ya Mkoa wa Pwani, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa namna ya kipekee kabisa, tuwaangalie wananchi wa Pwani; kama ambavyo alifanya Mwalimu Nyerere, haitakuwa dhambi kufanya ili kuwapa manufaa wananchi wa Mkoa wa Pwani ambao kwa kweli wameathirika kwa hali na mali kutokana na tatizo la kukosa elimu. Nikuombe wakati Mheshimiwa Waziri unahitimisha hapa utusaidie suala zima la mikopo, Bodi ya Mikopo iweze kuwaangalia wananchi wa Rufiji, watu wa Mkuranga, watu wa Kibiti na watu wa Kisarawe ambao wamekosa elimu, wakati wa mgao huu wa Bodi ya Mikopo basi waweze kufikiriwa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Rufiji wamenituma, wameniambia kwamba wanacho Chuo cha Maendeleo pale Ikwiriri (FDC), ulifika mwenyewe ukajionea, wanaomba chuo kile sasa kiwe ni Chuo cha VETA kwa sababu kutoka Rufiji kwenda Kibaha kufuata elimu hii ya VETA ni mbali sana kwa zaidi ya saa sita. Wanaomba sasa Chuo hiki cha FDC uje utuambie mtakiboresha ili kiwe ni Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mnaboresha elimu kwa watoto wetu, tunaomba muangalie, yapo maeneo Rufiji ambapo hakuna shule, ni umbali mrefu, kwa mfano kule Mtanange kijijini kwangu wapo watoto zaidi ya 500 ambao hawasomi kabisa, lakini yapo maeneo Kata ya Mgomba kule Mupi, wapo watoto wengi ambao hawasomi kabisa. Tukuombe Mheshimiwa Waziri tuletee wataalam wako waweze kuangalia ni namna gani wataboresha elimu. Ninaamini kabisa iwapo tutaboresha elimu tatizo hili ambalo linaendelea leo hii halitakuwepo tena kwa sababu tutakuwa na wasomi wengi eneo letu la Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, zipo shule ambazo tunahitaji kukarabati, tunakuomba kupitia Mfuko wa Elimu utusaidie. Kwa mfano, ipo shule ya msingi Mchengerwa iliyopo kule Miangalaya ambayo nimeanza ujenzi wa darasa moja lakini pia tunayo shule ya msingi Kilindi ambayo imetoa madaktari wengi lakini shule hii ni shule ya miti tu na watoto wetu wanapata taabu sana inaponyesha mvua na wakati mwingine jua linapokuwa kali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wakizungumzia suala zima la kuwaruhusu watoto wetu waliopata ujauzito kuendelea na masomo. Mimi ninaomba niwakumbushe sana Waheshimiwa Wabunge kwamba suala hili iwapo wataendelea kulisogeza mbele sana wakumbuke wanavunja Ibara ya Tano ya Katiba kwa kutaka kuwaruhusu watoto wetu kushiriki kwenye shughuli za ngono.

Mimi ni muislamu, nilisema hapa, nitashangaa sana kuona Wabunge waislamu wakishabikia suala hili na kutaka watoto wetu washiriki kwenye shughuli za ngono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Qurani inatuambia nilisema hapa, nataka nirudie inasema kwamba wallah takrabu zinah inah kanah taishatan wasahalan sabilah. Waislamu tumezuiwa kabisa, na jambo hili iwapo tutaendelea kuwasaidia watoto ambao wamepata ujauzito waendelee na masomo ni sawana kwenda kuongeza mafuta katika moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe, wakati ule ambapo Wazungu wanaondoa biashara ya utumwa, miaka ile ya 1800 ....

TAARIFA...

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa aliyoitoa ni sahihi, suala hili syo la udini lakini nataka niseme tu kwamba suala hili ni muhimu sana kwa Watanzania wakalitambua ni vema Watanzania sasa wakalea watoto wao kwa misingi ya elimu ya dunia na elimu ya ahera, ndiyo maana nikasisitiza hapa kwamba kuliweka jambo hili ni kusisitiza na kuwataka watoto wetu washiriki katika mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 2 Februari, 1835, Lord Maclay, mmoja wa Wabunge mashuhuri kule Uingereza aliwahi kusema kwamba Afrika hatuwezi kuitawala mpaka pale ambapo tutaweza kudhibiti elimu yao na kuhakikisha kwamba wanafanya mambo kutokana na tunayotaka kuyafanya. Ninaamini, nimeona Wazungu wakiwepo katika Bunge lako hili Tukufu na ninaamini… (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: …ninaamini suala hili wapo watu wana-engineer ambao wanalitaka jambo hili. Mheshimiwa Lord Maclay alisema maneno haya, naomba niwanukuu kwa kiingereza:

“I have travelled across the length and breadth of Africa and I have not seen one person who is a beggar, who is a thief such wealth I have seen in this country, such high moral values, people of such caliber, that I do not think we would ever conquer this country, unless we break the very backbone of this nation, which is her spiritual and cultural heritage and therefore, I propose that we replace her old and ancient education system, her culture, for if the Africans think that all that is foreign and English is good and greater than their own, they will lose their self esteem, their native culture and they will become what we want them, a truly dominated nation”

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya siyo ya kwangu ni maneno yaliyowahi kutolewa tarehe 2 Februari,1835. Ninaomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge iwapo wanasisitiza jambo hili wakumbuke Bunge lililopita tulifanya marekebisho ya sheria hapa, Sheria Na. 253. Kwa mujibu wa marekebisho haya ya Sheria Na. 353, kifungu cha 61 ambacho kilitoa mamlaka kwa Serikali kuhakikisha kwamba watoto wote wanaoshiriki katika masuala ya uasherati pamoja na ngono wadhibitiwe. Kuliruhusu jambo hili ina maana kwamba tunakinzana na kifungu hiki cha Sheria Na. 61 ambayo Bunge hili lilitunga kifungu hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa wa Sheria ya Elimu, kifungu cha 60(b) ambacho kimetoa mamlaka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dakika ni chache sana, nami nichukue fursa hii kuwatakia pole Watanzania wote ambao wamekubwa na majanga mbalimbali hususan ya watoto wetu kule Arusha; lakini pia Watanzania wote kule Rufiji ambao wamekumbwa na matatizo mbalimbali ya ujambazi ambayo niseme tu kwa hali ya kawaida, tatizo hilo la ujambazi limeacha wajane wengi na watoto wengi yatima. Naliomba Bunge lako wakati mwingine tunapochangia kwenye mambo ya sherehe, basi mnikumbuke kule Rufiji, mnifikirie kwani nina wajane wengi na watoto yatima wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kutoa pole kwa wale wote waliokumbwa na mafuriko makubwa kule Rufiji hususan Kata yangu hii ya Mohoro, kwa kina Chii kule mpaka kwa mzee Mikindo, Kata ya Mwasemi, Kipugila, Ikwiriri, Umwe, Mgomba, Ngarambe pamoja na Chemchem.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe watu wa Rufiji msemo mmoja katika Quran unaosema kwamba kullama yuswiibana, illamaa qataba Allah lana, ikimaanisha kwamba nothing will happen to us, except what Allah has decreed for us. Hakuna linaloweza kutokea mpaka pale ambapo Mwenyezi Mungu amelipanga litokee baina yetu. Mwenyezi Mungu ametuandikia kila jambo litakalotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kuwatia moyo wananchi wangu wa Rufiji wasibabaike na jambo linaloendelea na hili ni tatizo la amani, waendelee kuijenga nchi yao, kwani Tanzania hii ni ya kwetu sote nasi tutaendelea kuwapigania huku katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini pia wale ambao wamesoma vitabu mbalimbali watakumbuka kitabu cha “Comperative Government and Politics,” watatambua ni namna gani Mheshimiwa Rais ataweza kulisaidia Taifa hili hapo mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nampongeza sana na tuseme tu kwamba nchi hii inamhitaji sana. Mabadiliko makubwa katika nchi kama Bangladesh ambao wameweza kubadilika kwa kipindi cha miaka 10, tunaamini kabisa kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anaweza kuivusha Tanzania kutoka hapa ilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mengi ya kuzungumza, lakini niseme kwa uchache tu kwamba suala hili la maji limezungumzwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi. Ukiangalia Ilani yetu ya Uchaguzi; Serikali imeundwa na Chama cha Mapinduzi na utekelezaji ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Pia tunaongozwa na Kanuni za Uongozi wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mujibu wa Ilani, katika ukurasa wa nne wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, inasisitiza Serikali kufanya yale yote yanayoletwa ndani ya Serikali kwani ni yale ambayo yanaongozwa na Ilani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 66 wa Ilani yetu ya Uchaguzi inasisitiza katika kusogeza huduma za kijamii karibu na kwa wananchi. Suala la maji safi na salama limezungumzwa katika ukurasa wa 83 wa Ilani, nami nataka nijikite katika ukurasa wa 85 wa Ilani yetu ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo imedhamiria kutua ndoo kichwani kwa mwanamke. Niseme tu kwamba kwa mujibu wa ukurasa 85, Ilani imedhamiria kuongeza asilimia 53 ya maji vijijini mpaka kufikia asilimia 70. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme, kule kwangu Rufiji niliwahi kufanya ziara katika kijiji kimoja pale Kikobo. Wananchi wa Kikobo wamehama kijiji kile kwa sababu ya tatizo la maji na walichonieleza ni kwamba kule Dar es Salaam ukiwa na pesa kidogo unaonekana unatoka kipara kichwani, lakini akinamama wa eneo la Kikobo wanatoka vipara kwa sababu ya kubeba ndoo kwa muda mrefu. Wanasafiri na maji kwa zaidi ya kilometa saba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tatizo hili ni kubwa sana kwa nchi yetu, nami niseme tu kwamba sisi tulishaanza utekelezaji wa Ilani. Mimi binafsi nilishaanza uchimbaji wa visima mbalimbali katika eneo langu, yale maeneo korofi kabisa!

Mheshimiwa Naibu Spika, nimechimba visima katika Kata ya Mgomba Kusini, Mgomba Kati, Ikwiriri Kati, Nambanje, Mpalange, Mtanange tunakwenda kuchimba pamoja na Mpima; lakini pia Mpalange kwa Njiwa kote tunakwenda kupeleka visima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo korofi ambayo tunaamini kabisa Serikali ikiweza kutusaidia, tutaweza kutatua kero ya maji. Hapa nazungumzia katika Kata ya Chumbi, hususan katika Kijiji cha Nyakipande, pamoja na Miangalaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati kabisa, napenda niwapongeze watani wangu hawa wawili kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja pamoja na marekebisho yatakayofanywa na Wizara. Ahsante.

The Public Procurement (Amendment) Act, 2016.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mengi ya kuchangia siku ya leo na nilifanya tafiti za kutosha kuhusiana na marekebisho ya muswada huu hususani suala zima la tafsiri ambazo hazipatikani katika marekebisho ya sheria hii hata sheria mama hususani tafsiri kwa mfano local firms ambayo haipo katika sheria hii inayorekebishwa na hivyo wakati mwingine italeta tabu hapo baadae. Lakini pia nimeona Ibara ya 11 inayopendekeza marekebisho katika kifungu cha 31 ili kuondoa sharti la kubainisha katika kanuni la kusimamia ununuzi Halmashauri yaani Madiwani sasa kuondolewa katika usimamizi wa manunuzi yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia kwamba siku ya leo nina majonzi na kwamba kwa kuwa wananchi wangu wamekatizwa haki ya kuishi kwa mujibu wa Ibara ya 14 lakini pia kwa kuwa Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatamka kwamba wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Ibara ya 9 kwamba lengo kuu la Serikali itakuwa ni ustawi kwa wananchi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, majonzi haya yamenifanya nishindwe kuchangia siku ya leo na nitaomba nichangie kwa maandishi ili nishirikiane na ndugu zangu wa Rufiji ambao wameuwawa ikizingatiwa kwamba mmoja wa mtu aliyefariki ni ndugu bwana Ngayonga.
Kwa hiyo, naomba kwamba yale mapendekezo yaliyoletwa na Serikali mimi niaafikiana nayo na kwa siku ya leo kwa kuwa nina majonzi nitashindwa kuchangia, ahsante.

The Access to Information Bill, 2016

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wandengereko wote duniani pamoja na Warufiji wanaoishi kule Rufiji, naomba nichangie mambo machache. Nikiwa kama Mwenyekiti, tayari nilishawasilisha baadhi ya mambo ya msingi, lakini naona nitakuwa siwatendei haki Warufiji iwapo sitazungumza mambo kutokana na muswada huu na ni namna gani Muswada huu utawasaidia Wandengereko wa Rufiji pamoja na makabila mengine wakiwepo Wamakonde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kutoa pole kwa viongozi wa Serikali ambao wamepata ajali siku ya jana katika Jimbo langu la Rufiji akiwemo Mkuu wetu wa Wilaya Mheshimiwa Juma Njwayo pamoja na DAS wetu ambaye leo hii yupo pale Muhimbili anapata matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu wa upatikanaji wa taarifa kama ambavyo umeelezewa na wenzangu, muswada huu ni muhimu sana kwa nchi yetu, ukizingatia kwamba ni muda mrefu sasa Serikali imekuwa ikijaribu kupitia hili na lile ili muswada huu uweze kuwasilishwa kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba muswada huu uliwahi kuwasilishwa katika Bunge lililopita na tatizo kubwa la muswada huu wakati ule ni kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge na watu mbalimbali walidhani kwamba ni Muswada wa Habari badala ya Muswada wa Upatikanaji wa Taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme kwamba muswada huu unaleta sheria hii ya upatikanaji wa taarifa kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa zilizopo chini ya himaya ya Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake. Niseme tu kwamba muswada huu unatambua haki ya Watanzania ya kupata taarifa kutoka katika mamlaka mbalimbali, nikinukuu Ibara ya 8(1)(a) ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua kwamba nchi hii ni ya wananchi na kwamba mamlaka ya nchi yapo chini ya wananchi; na kupitishwa kwa muswada huu kunatoa fursa kubwa kwa wananchi wetu kuweza kupata taarifa kuhusu miradi pamoja na mambo mbalimbali ya msingi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nirejee Ibara ya 18 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ambayo inatoa fursa kwa kila Mtanzania kuwa na haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa. Naomba pia ninukuu maneno ya Mheshimiwa Dkt. Dale McKinley kutoka kule Afrika ya Kusini. Katika chapisho lake aliwahi kusema kwamba; “the state of access to information in South Africa;” katika page ya pili alisisitiza kwamba “if there is one right contained in the constitution that symbolically connects all other rights, it is their right to access to information. The control of information and enforced secretely was at the heart of anti-democratic character of the apartheid system.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ninukuu maneno hayo ili Waheshimiwa Wabunge wafahamu kwamba muswada huu umuhimu wake siyo tu katika Bunge hili, bali kwa wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla. Upatikanaji wa taarifa utatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme kwamba Serikali hii ya kipindi hiki ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imedhamiria kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba wale wasimamizi, viongozi wa taasisi za umma na pamoja na Serikali wanatoa taarifa sahihi kwa wananchi wetu wanapozihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, demokrasia hii ni ya hali ya juu ukizingatia kwamba Tanzania katika Afrika itakuwa ni nchi ya tano kupitisha sheria ya namna hii. Ukiangalia idadi ya nchi tulizonazo Afrika lakini siyo tu Afrika, dunia nzima, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi ya 67 kupitisha sheria ya namna hii. Japokuwa tunasema kwamba katika dunia nchi ya kwanza kupitisha sheria hii ilikuwa New Zealand miaka ile ya 1766 lakini Tanzania tunaingia katika record ya dunia kwamba miongoni mwa nchi ambazo zinaweka uwajibikaji mbele kwa watendaji wetu wa Serikali pamoja na taasisi mbalimbali za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hapa nijikite sana katika Jimbo langu la Rufiji. Upatikanaji wa taarifa utawasaidia Wandengereko wa Rufiji, Kibiti pamoja na wananchi mbalimbali waliopo kule maeneo ya Kilwa, Kibiti pamoja na Rufiji. Nimeona niseme hili kwa sababu kwa mfano, pale kwangu Rufiji kuna tatizo la umeme kwa takribani huu ni mwezi wa 11, lakini wananchi hawana taarifa sahihi ni kwa nini umeme haupatikani kipindi hiki chote? Upitishwaji wa sheria hii utamruhusu Mrufiji popote pale alipo kuweza kuhoji na kupata taarifa kutoka kwa viongozi wetu ambao watakuwa wameidhinishwa yaani information officer wa maeneo husika ili waweze kujua hasa tatizo kubwa la umeme ni nini katika Jimbo letu hili la Rufiji pamoja na Kibiti kwa Mwenyekiti wa Wandengereko pale Bwana Ally Seif Ungando. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kuhoji tu ni kwa nini kuna shida ya umeme, tunafahamu Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda na Rufiji tunategemea kuwa na viwanda kwa mujibu wa Waziri wetu ambaye ametuahidi, tutakuwa na kiwanda cha kwanza pale Chumbi. Kiwanda cha Sukari tutakuwa nacho pale Chumbi, lakini ukiangalia tatizo la umeme linalotukabili ambalo Serikali haijatoa taarifa ni kwa nini tuna tatizo la umeme, sheria hii itawawezesha wananchi kupata taarifa, lakini pia Serikali itaweza kuboresha tatizo tulilonalo pale katika Jimbo letu la Rufiji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri kwamba sheria hii itawasaidia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo langu katika Kata ya Utete pamoja na maeneo mengine kuhoji miradi mbalimbali ambayo imekuwa ni kero kubwa. Upatikanaji wa taarifa kuhoji miradi kwa mfano; Mradi wa Nyamweke, Segeni pamoja na miradi mingine mikuwa ambayo iko ndani ya Jimbo langu la Rufiji, wananchi wangu wapiganaji wa kule maeneo mbalimbali wataweza kupata taarifa kujua miradi hii imeidhinishiwa fedha kiasi gani na ni kwa nini mradi huu haujakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii pia kuzungumzia, yupo mkandarasi mmoja aliwahi kukabidhiwa moja ya barabara pale Rufiji kuikarabati. Mkandarasi huyu wakati wa ukarabati wake alikuja na kitoroli pamoja na chepeo kukarabati barabara ambayo ni ndefu. Sasa wananchi wanahoji lakini hawawezi kupata taarifa ni kiasi gani kiliidhinishwa katika mradi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti sheria hii itawasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji kuweza kuhoji mambo ya msingi ambayo yameidhinishiwa fedha katika vikao vyetu vya Madiwani lakini pia yameidhinishiwa fedha na Serikali yetu hii. Kama nilivyosema hapo awali, demokrasia hii ni kubwa kabisa kutokea katika nchi yetu na ni historia kubwa ambayo tutaifanya katika Bunge lako hili Tukufu. Waheshimiwa Wabunge wetu wataingia katika historia kwa kupitisha sheria hii ambayo itaifanya Serikali kuwajibika na kuwepo kwa uwazi (transparency) ili wananchi waweze kupata taarifa za msingi kuhusiana na jambo lolote lile isipokuwa tu yale ambayo yanagusa usalama wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo, naomba niwasilishe kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji. Ahsante sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's