Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Ally Mohamed Keissy

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ila na mimi nichangie hotuba ya Mtukufu Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Hotuba ya Rais kwanza kutoa muda wa kuchangia ni kama vile tunapoteza muda, ile hotuba haina matatizo. Mwelekeo wake ni mia kwa mia hakuna mtu anaweza kuipinga. Ya kukazia ni yale mambo aliyoyaeleza mwenyewe tuyafuate na yatekelezwe haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuunda Mahakama ya Mafisadi ifanywe kwa haraka sana. Pili, wakati wa bajeti hapa Bungeni wanakuja Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa, Ma-RAS
wanakuja kufanya nini? Hilo nalo liondoke. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kufuta Sherehe za Uhuru na ikiwezekana afute na Sherehe za Mwenge iwe hata mara baada ya miaka mitano. Tunabana matumizi, Mwenge kila mwaka unapita na tunapoteza pesa. Nimezungumza mimi Mwenge ukipita Wilayani
kwangu siku tatu kazi hakuna. Siku ya kwanza wanalaki Mwenge, Ofisi za Halmashauri zinafungwa. Siku ya pili wanapokea Mwenge kwa hiyo wanakesha kwenye Mwenge. Siku ya tatu Mwenge ulipopita wanalala wamechoka. Sasa ndugu zangu ni uharibifu, ni lazima twende
kama anavyosema kazi tu, hiyo ndiyo kazi tu. Hatuwezi kufanya sherehe wakati watoto wanalia, hawana madawati, dawa, viatu na chakula, tupunguze sherehe za ajabu ajabu.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilishangaa sherehe za Mapinduzi Zanzibar wanapakia watu elfu moja kutoka Pemba. Sasa kulisha chakula watu elfu moja ni gharama wakati wananchi hawana hela? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tupunguze Majimbo yamekuwa mengi, Wabunge wamekuwa wengi gharama za kuendesha Bunge ni kubwa Rais alizungumza hapa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Bunge linatumia gharama kubwa. Mabunge mengine ni watu ishirini na tano au watu kumi na tano. Ndugu zangu hatuendi namna hiyo. Twende na Bunge la kisasa, tumekalia kusema ma-DC wapungue, Wakuu wa Mikoa wapungue na Wabunge
tupungue kutokana na idadi ya ukubwa wa Majimbo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta Jimbo kama la Kwela kwa Mheshimiwa Malocha ukubwa wake ni sawa na Rwanda, anapewa pesa za kuendesha Jimbo sawa na Mbunge mwenye watu elfu mbili. Hapa uhalali uko wapi? Lazima twende na sera ya „Hapa Kazi Tu‟ na kazi ianzie kwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wanaunda mpaka vikosi vya michezo wanakwenda na ndege ya Rais na kurudi na ndege ya Rais, huu ni ubadhirifu wa hali ya juu.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani wakati wa bajeti wanatoka wataalam wa Nkansi wanakuja Dar es Salaam wanakaa wiki mbili, wao na madereva wao, gari sita, zinakuja Dar es Salaam eti bajeti. Karne ya 21, Namanyere ije ifanyiwe bajeti Dar es Salaam! Mkurugenzi na kundi lake atoke Bukoba aje Dar es Salaam, atoke Tarime aje Dar es Salaam, ndugu zangu hii haiwezekani, kuanzia sasa bajeti zifanyike Wilayani itumike mitandao tu. Haiwezekani Madereva na Wakurugenzi wa kila Wilaya kuja Dar es Salaam
kuchezea hela za Serikali wakati wananchi hawana maji, dawa wala barabara. Tunafanya sherehe kubwa kama nchi za Kiarabu, haiwezekani lazima tubanane, tule kwa jasho letu, hatuwezi kwenda kienyejienyeji. (Makofi/Kicheko)
Kisa kingine kuhusu madereva wa Serikali, madereva hawa wanapunjwa, madereva wa Mashirika ya Umma wanakuwa kama wako peponi madereva wa Serikali hawapati chochote. Hata akistaafu anapewa shilingi milioni mbili, itamtosha nini shilingi milioni mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi wa marine service wa Lake Tanganyika, Lake Victoria, Lake Nyasa, hawaajiriwi, ni vibarua miaka yote. Hawana likizo, hawana insurance yaani wamekaakaa tu, wanaona bora wagongeshe meli watu wafe kwa sababu hawathaminiwi
kabisa. Kwanza hii marine service ni shirika la nani, ni la umma kweli? Lazima anayehusika alichunguze hili shirika la marine service. Nimekutana na wafanyakazi wa Liemba wanasema Mzee hatuna hata likizo, insurance, mishahara duni, wakistaafu hawapewi chochote wakati TRA, Shirika la Nyumba wao ni kama wako peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu NASACO amezungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja, turudishe NASACO i-control mali bandari. Leo kuanzia Bagamoyo mpaka Dar es Salaam bandari bubu nyingi. Wazanzibar ndiyo wamefanya pa kupitishia mali na kufanya huku Bara ndiyo soko. Tunaibiwa mchana mchana! Mali yote inatoka Zanzibar inapitia vichochoroni hawalipi ushuru. Zinaletwa mali za ajabu ajabu, sukari, mafuta na kila kitu. Wanastarehe kuinyonya Bara hawalipi ushuru, hiyo haikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuweke mikakati anayekamatwa mara moja mali yake itaifishwe hamna kwenda Mahakamani. Pia chombo kinachopakia mali ambayo hailipii ushuru kitaifishwe, watashika adabu. Wote ambao wanahisiwa kwamba wanashirikiana na
wafanyabiashara kutuibia, cha kwanza kabisa mali zao zinyang‟anywe kabla ya kupelekwa mahakamani. Apewe form aulizwe hii mali umeipataje, akishindwa kujieleza anyang‟anywe kabla hajaenda Mahakamani. Akienda Mahakamani, Mzee mlango chini anapita anafungwa
miezi sita, anabakia anachezea ile mali. Kwanza mali yake inyanganywe mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mambo ya kuendelea kuleana yaishe sasa.
Nimezungumza sana habari ya Namanyere, miradi ya maji wanahamishwa Wakurugenzi, Maafisa Ugavi na Wahandisi wa Maji, naomba majibu yakatumbuliwe Wilayani Namanyere kuna watu wameiba pesa. Kule kwa vile tuko karibu na DRC-Congo wafanya kama hamna
Serikali, wanafanya mambo wanavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza hapa Bungeni, mtu anaandika gharama ya gari Namanyere Dar es Salaam gari tani kumi shilingi milioni kumi na mbili badala ya shilingi milioni tatu. Anaandika mabomba yameingia ndani gari tisini na nane milioni wakati bomba
hakuna yaani gari hewa, mabomba hakuna, Serikali imelala usingizi. Tunataka tutumbue majipu tupeni idhini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya mbolea haya, mbolea hazifiki kwa wakulima wanaandika hewa tupu mpaka majina ya marehemu wanaandika. Hatuwezi kukubali safari hii, namwambia Waziri wa Kilimo, Kamanda wangu Mwigulu, anipe kibali nitembee kijiji kwa kijiji,
nikague mimi mwenyewe simwamini DC, simwamini OCD, siiamini TAKUKURU maana ndiyo wamefanya njia za miradi yao. Nitatembea mwenyewe, Mheshimiwa Mwigulu nipe kibali nikakague kijiji kwa kijiji, nyumba kwa nyumba kama mbolea au mbegu imefika. Serikali ya CCM inatukanwa ni kwa sababu ya Watendaji hawa, wamefanya miradi yao binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo, kuanzia sasa bajeti ijayo hakuna kuja cha Mkuu wa Mkoa, hakuna kuja cha RAS, hakuna bajeti za Wilaya kupangiwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi jioni ya leo.
Waheshimiwa ndugu zangu Wabunge, ukiona mtu kapigika ujue amekwisha. Ndugu zangu wameshaona, wameshafanya utafiti huko nje, hali zao ni mbaya, speed ya Magufuli inawatisha, walipania mwaka huu ndiyo waingie Ikulu, Ikulu ndiyo hawataiona tena kwa speed ya Magufuli. Sasa hawa jamaa ni wa kuonea huruma tu wameshapigika vibaya, hawajiwezi…
Mheshimiwa Magufuli anasifiwa dunia nzima. Kwa ushahidi Nigeria nimesikia Nigeria wanamsifu, Kenya wanamsifu, Uarabuni wanamsifu, Ulaya wanamsifu, hapa wanakaa wanampiga vijembe!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo Katiba amevunja Katiba gani? Katiba kuwasaidia mafisadi kutuibia pesa? Mimi nilizungumza hapa Bungeni, mafisadi wauwawe mapema na makaburi yao yawekwe minyororo, nilimwambia Mheshimiwa Magufuli…
Kwanza hawa jamaa hakuna haja ya Kuwapeleka Mahakamani. Haiwezekani mtu ana nyumba 70 bado unampeleka mahakamani, alipata wapi? Wewe tuchukue watu wa vijiweni, nenda pale Nyerere Square wako watu wanahangaika pale. Wako tayari kufungwa miaka miwili miwili wapewe milioni 100 wako tayari, itakuwa fisadi unamfunga miezi sita au unampa kifagio anafagia Sinza akitoka anakula mabilioni ya shilingi ya hela? Haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wameshaona wamepigika, speed ya Magafuli inawatisha, hawana chao, iliyobaki jiungeni na CCM mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kugusia habari ya mapato ya Serikali, mapato ya Serikali yanavyopotea katika nchi hii.MHE. ALLY K. Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kugusia habari ya mapato ya Serikali, mapato ya Serikali yanavyopotea katika nchi hii.
Ninyi tulieni mmeshakwisha, speed ya Magufuli inawatisha, hamna leo, hamna lolote, mnajiona mmefanya utafiti huko nje hamuungwi mkono na wananchi wote. Mlituambia hapa hapa Bungeni kwamba tukapimwe akili zetu kama tunamuunga Mheshimiwa Lowassa!
Je, ninyi mlipimwa akili zenu wakati mnamuunga Lowassa? Mlifanya utafiti, mliandika na vitabu, mkapita nchi nzima kumwambia Lowassa ni fisadi, je, mmepokeaje huyo fisadi mwenzenu? Sasa mmegeuka ninyi ndiyo mmekuwa mafisadi, CCM imekuwa safi, tulieni.
Magufuli speed anayokwenda nayo ni hiyo hiyo hamna kupunguza, hamna kupunguza aendelee zaidi ya mara mbili au mara tatu, hamna chenu. Tumepewa wajibu wa kuiongoza Serikali kwa miaka mitano na mmeona speed inavyokwenda mkajua mwaka 2020 hamtapata kura, hamkutegemea speed hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia vinasaba. EWURA waliingia mkataba vinasaba na shirika moja bila kupitia tenda, huyo jamaa anajichukulia kila mwezi shilingi bilioni 9.8, tulieni ninyi vimeshawauma hivi hampati kitu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vinasaba anavyotumia EWURA kuweka kwenye Mafuta. Vinasaba vinagharimu shilingi 12.50. Vinasaba vyenyewe gharama yake ni shilingi 5.25 na mwenye vinasaba huyo mwenye hiyo kampuni anapata shilingi 7. Kwa hiyo anakusanya kila lita kwa mwezi jumla anapata shilingi bilioni 14 amekaa tu bila sababu yoyote!
Ndugu zangu wakati anaingia Mkataba Waziri Mkuu alikwa ni Mheshimiwa Lowassa ambaye mmemnadi nchi nzima, na hii kampuni ya vinasaba ni Lowassa ana ushirika ndani yake, vinasaba vya Lowassa. Ni kampuni ya Lowassa na ndiyo alituingiza mkenge, ni Lowassa alipokuwa Waziri Mkuu.
Hili fisadi, anachukua Lowassa kila mwezi shilingi bilioni 14 hii kampuni yake, sasa ndiyo nawaambia mkakae mkachunguze huko. Mafisadi wakubwa. Mnaniharibia hata kuchangia kwangu. Mmemnadi ninyi nchi nzima, juzi ndugu yangu Mheshimiwa Khatib hapa anasema mwaka 2020 mtamleta yule yule Mheshimiwa Lowassa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Serikali ilipiga marufuku kuagiza sukari nje. Ninachowaomba, wapige marufuku kuagiza mchele kutoka nje. Kuna mchele kutoka India, kutoka Thailand katika nchi yetu hii wakati mchele wetu uko mwingi, tuokoe hela za kigeni kama tunavyofanya mambo ya sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kuagiza mchele nchi za nje wakati tuna mchele umerundikana Kyela, Tunduma, Sumbawanga. Kwa hiyo upigwe marufuku mchele kuingizwa kama ilivyopigwa marufuku sukari ili kuokoa wakulima wetu.
Kuhusu usafiri mwambao wa Ziwa Tanganyika, Serikali ya Awamu ya Nne ilituahidi meli mbili, ninashangaa hata Awamu ya Tano hata meli hakuna ni kukarabati MV Liemba tu! Sasa inakuwa ni matatizo, hakuna cha kutengeneza meli mbili, hata hiyo moja nimeona kuna ukarabati MV Liemba. MV Liemba ina umri wa miaka 112, hatukatai kukarabati MV Liemba, ikarabatiwe, lakini tunahitaji na meli mpya.
Kuhusu suala la uvuvi, wavuvi wetu katika Ziwa Tanganyika wako duni sana. Tunaomba wafikiriwe ili na wao waweze. Zambia ina asilimia sita ya maji ya Ziwa Tanganyika lakini Zambia ndiyo inakuwa muuzaji mkubwa wa samaki na dagaa, ina asilimia sita ya maji lakini ndiyo muuzaji mkubwa wa dagaa na samaki za Ziwa Tanganyika, wakati sisi tuna asilimia 38 ya Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Idara ya maji, nimezungumza sana habari ya idara ya maji ni majipu na Namanyere. Siyo lazima kumngoja Rais au Waziri Mkuu nimezungumza mara kwa mara hapa. Wanaiba, wameandika gari hewa Dar es salaam na Namanyere na mabomba hewa hakuna kilichopelekwa, kila mara nazungumza hapa, ni hewa tupu hakuna kitu kinachofanyika!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Namanyere wananchi wana taabu ya maji miaka na miaka, wananidanganya hapa eti watanipa bilioni tatu, hamna cha bilioni moja, wala 500 milioni. Kwa hiyo, naomba bajeti ya safari hii, mradi wa maji na Namanyere ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mafisadi hukumu yao haitoshi kuwapeleka tu mahakamani. Haiwezekani mtu anakamatwa na nyumba 70 au 40, Serikali inachukua muda kumpeleka mahakamani na anapata dhamana.
Kwanza naiomba Serikali zile nyumba zinyang’anywe, kama alikuwa polisi, nyumba ziende Polisi, kama alikuwa mtu wa TRA (Tanzania Revenue Authority) ili wafanyakazi wa TRA wakodishe zile nyumba. Haiwezekani wewe mtu umefanya kazi yako inajulikana mshahara wako ni mdogo leo unanunua nyumba 40 au 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapato na matumizi ya Bunge, Wabunge wengi nilizungumza hata mara ya kwanza hapa, wanasafiri kama wakimbizi wa Burundi. Wanapishana airport kama Wakimbizi, Magufuli amedhibiti hii wanaanza kumpiga vita, ndugu zangu kwa vipi? Mpaka timu za mpira zinakwenda kwa ndege Rwanda, hamna lolote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba apige marufuku timu zote za Bunge kwenda nje ya nchi. Safari za hovyo hovyo marufuku, Wabunge tuishi hapa tufanye kazi majimboni kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, safari za nini kwenda nje? Hakuna cha kutoa safari kwa Wabunge, Wabunge tukae hapa hapa tufanye kazi kwenye Majimbo kwa wananchi waliotuchagua. Kwenda nje iwe marufuku na mimi ninamuunga mkono Mheshimiwa Magufuli azuie safari zote za Wabunge za michezo hovyo hovyo kwenda nje, Wabunge wakakae majimboni kwao baada ya Bunge kutekeleza majukumu yao Majimboni. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa nichangie Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachangia kuhusu mapato. Naomba Serikali irudishe kodi ya mifugo ili Halmashauri zetu zipate pesa za kujiendesha. Miaka ya nyuma kulikuwa na kodi ya mifugo, nashangaa Serikali ikafuta kodi ya mifugo wakati Serikali yetu ni maskini na Halmashauri zetu zinaharibiwa na mifugo lakini hatuna chochote tunachopata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo mifugo peke yake, hata mashamba ya kuku. Watu wanaofuga ng‟ombe mijini wanauza maziwa lazima walipe kodi. Ulaya wanajiendesha kwa kodi, Uingereza hawana chochote siku hizi ni kodi. Nilizungumza hapa hata tv, watu wana tv mpaka 20, 30, Uingereza wanalipa kodi ya tv lakini hapa hakuna mtu analipa kodi ya tv. Kama Serikali Kuu imeshindwa kulipia kodi ya tv, halmashauri zetu zikusanye kodi za tv maana wanajulikana wenye tv 10, 20, alipe kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi karibu watumishi wote wa Idara ni makaimu muda mrefu. Ujenzi kuna Kaimu, maji kuna Kaimu, utumishi kuna Kaimu, kilimo ni Kaimu karibu idara zote ni makaimu, ndiyo maana utendaji wa kazi unakuwa sio mzuri. Wengine hawana uwezo na kama wana uwezo wapandisheni washike hizo idara tumalizane. Siyo miaka 10, 20 mtu anakaimu, hakuna anayepeleka watumishi kule kwetu. Cha ajabu juzi juzi tu hapa Mkoa wa Rukwa RAS alikuwa amestaafu, wamemfanyia sherehe ya kustaafu, juzi wamesema amerudi tena Rukwa, ndugu zangu si hatari hii? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara. Nimezungumza muda mrefu Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi haina uwezo wa kujenga barabara katika mwambao wa Ziwa Tanganyika inataka nguvu ya Serikali. Akina mama wajawazito wanakufa wakifuata huduma ya afya kwenye vituo vya afya. Kuna kibarabara cha kilometa 35, wananchi wa kule tangu dunia kuumbwa hawajaona hata bajaji, kijiji cha Kazovu, Chongotete, Isaba, Bumanda, hawajaona lolote, wanapata taabu. Ziwa Tanganyika likichafuka hamna msalie Mtume wanazama. Tumekaa hapa viongozi tunajali mikoa mingine, unashangaa mkoa mmoja unapata shilingi bilioni 27, mingine shilingi bilioni sita wakati wana kila kitu. Watu wanaomba lami hata kwenye Wilaya zao sisi hatuna hata barabara za vumbi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni miaka 40 Wilaya Nkasi pale Namanyere lakini hakuna Hospitali ya Wilaya. Wilaya ya Nkasi pale Namanyere leo miaka 40 wanapata maji kwa 16%. Kila siku tunapiga kelele habari ya maji Serikali haisikii. Sasa itakuwa namna gani, tunakuja kutetea wananchi au tunakuja kula posho za wananchi hapa? Kama tumekuja kula posho hakuna haja ya kuwa Mbunge maana hapa tunawakilisha watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijali Mkoa wa Rukwa kwa sababu hii. Kuna mikoa wamegawa majimbo hata hayastahili kuwa majimbo. Tumelalamika kuhusu Jimbo la Kwela hapa, la Mheshimiwa Malocha lina kata 26, watu 400,000, jiografia yake ngumu ukubwa kama Burundi. Cha ajabu mwaka jana wamegawa majimbo hata hayastahili kuwa majimbo lakini Kwela wameiacha vilevile. Mimi nina kata kule kwangu, Kata ya Nkwamba na Kata ya Kolongwe ni kubwa kama majimbo mengine hata kugawa kata mnashindwa, kugawa tarafa mnashindwa? Mnapendeleana tu, kiongozi akitokea sehemu fulani anagawa anavyotaka, haiji. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa TASAF. Wengi wamelalamika kuhusu TASAF, kusema kweli TASAF ni donda, ni jipu. Wamepeleka pesa kuwapa watu ambao hawastahili…
MHE. ALLY K. MOHAMED: Wanagawa kwa kupendelea, akiwa Mwenyekiti mjomba wake anampa hata ana miaka 18 anachukua hela ya TASAF. Kwa macho yangu na kwa ushahidi katika Jimbo langu wapo. Hili jambo mfuatilie hatukubali, hela zinakwenda kwa watu ambao wana uwezo. Watu ambao ni yatima, wasimbe sijui wanaitwa hawapati, wanakwenda kupewa watu wenye uwezo miaka 18, 20, watoto wa viongozi, hii haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha afya cha Kirando nimelalamika miaka yote, kimezidiwa na wagonjwa mpaka wagonjwa wanatoka DRC Congo, kipandishwe hadhi kuwa hospitali lakini wapi masikio yamejaa pamba. Ndugu zangu nataka kituo cha afya cha Kirando kipandishwe hadhi kuwa hospitali. Mpaka wakimbizi kutoka DRC Congo wanakuja kutibiwa pale, vijiji vyote vya mwambao wa Ziwa Tanganyika wanakuja kutibiwa pale, hakitoshi, hali ni mbaya. Kimezidiwa sana kile kituo cha afya Kirando, hakifai. Wagonjwa wamekuwa wengi kuliko uwezo wa kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Jimbo, ndugu zangu naomba majimbo yapitiwe upya kuhusu Mfuko wa Jimbo. Haiwezekani tupewe pesa zile zile. Mimi mfano jimbo langu kata nzima imeongezwa kutoka jimbo lingine naendelea kupata hela ile ile, itawezekana wapi? Majimbo mengine ndugu zangu tukiyapima humu hayana uwezo. Unakuta Mbunge anasema mimi nataka madawati, wewe una jimbo la kuomba madawati hapa, huna uwezo. Lazima hata haya madawati tunayogawiwa twende kwa vigezo. Jimbo gani ambalo watoto wanakaa chini sana na majimbo gani watoto wana madawati. Tusigawe tu madawati kila mtu sawa, haiwezekani, kuna majimbo mengine ndugu zangu yako taabani hayajiwezi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkansi ina eneo kubwa sana la Ziwa Tanganyika na kuna aina nyingi za samaki na hata dagaa, lakini wavuvi wengi karibu wote hali zao ni mbaya sana hawana zana bora za uvuvi kabisa. Wavuvi wengi au karibu wote ni raia kutoka DRC-Congo ndiyo wanaofaidika na maliasili ya Ziwa Tanganyika, maana Vijiji karibu vyote vya mwambao mwa Ziwa Tanganyika upande wa Tanzania ni wavuvi kutoka DRC-Congo.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kuna halali gani Wakongo kuwa upande wa Tanzania bila hata uhalali wa kukata leseni zinazostahili wageni toka DRC-Congo? Naomba Wizara yako ichukue hatua kwa wageni wote wanaokwenda kinyume, pia wale waliopewa majukumu huko. Nadhani wanafanya kutotekeleza sheria kwa ajili ya kupewa chochote na hao wavuvi wageni. Hata uvuvi haramu kwa kutumia nyavu zilizopigwa marufuku mwambao mwa Ziwa Tanganyika wamezagaa Tanganyika karibu kila kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkasi kuna mapori shamba kama vile waliohodhi hawayatumii na walipata kwa kuwarubuni Wenyeviti wa Vijiji, wakati hakuna sheria wao kutoa ardhi zaidi ya hekari 50. Unakuta kuna mashamba pori ya hekari 100 na kuendelea. Mfano; shamba la Kowi, Kalumwalwedo,shamba la Msomali Tatumbila, shamba la Mastar Mashete, mashamba yote hayo yalipatikana kwa vijiji kukiuka sheria ya uwezo wao wa hekari 50 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna baadhi ya wafugaji walipewa block katika shamba, yaani Ranch ya Kalambo lakini hawajapeleka mifugo na wanakodisha hizo block tu, Wizara ikalitazame upya na kuwapatia wafugaji wenye ng‟ombe.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi haipati matangazo toka TBC redio hasa wananchi wanaokaa mwambao wa Ziwa Tanganyika, naomba Wizara yako iweke mnara wa kuongeza nguvu Redio Tanzania, Namanyele - Nkasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matangazo ya Bunge live; mimi nashauri liwe linaoneshwa siku ya Jumamosi saa tatu usiku kwa sababu mchana watu wote wako kazini wanatafuta riziki na sababu ya pili wanafunzi na walimu wao wako kazini na masomoni mchana hawana muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya tatu hata ukichunguza mji kama Dar es Salaam kila mtu yuko na shughuli zake siku nzima hawana muda wa kuangalia tv mchana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya nne ni kwamba madereva wote wa magari ya abiria, malori, daladala na abiria zao wako safarini. Wapi nafasi wanayo? Tuache ushabiki, wanaotaka kuuza sura zao wakaombe kazi kwenye vituo vya tv.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi. Kwanza mimi natoa pongezi sana kwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu wote. Kusema kweli tunachotaka sasa ni Serikali kuipa fedha zote Wizara hii ili ikatekeleze mipango kama ilivyo kwenye bajeti yao. Mimi katika mkoa wangu wa Rukwa hasa Wilaya ya Nkasi nimeshukuru sana, miaka sita barabara yetu toka Sumbawanga - Mpanda ilikuwa haijakamilika kwa bajeti hii naona barabara Disemba itakuwa lami tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nilikuwa napiga kelele sana kuhusu shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kwenda kukamilisha Bandari ya Kipili. Leo naona kwenye bajeti kuna pesa ya kutosha kwa ajili ya kutengeneza barabara mpaka Bandari ya Kipili. Naipongeza sana Serikali na Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitoe masikitiko yangu makubwa, alipokuwa hapa ndani, leo ni Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi, aliniahidi barabara ya kutoka Kirando - Kazovu - Korongwe na shahidi ni Alhaji Iyombe alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na alikubali kunisaidia. Wakati wa kampeni zake tena alipokuwa Namanyere aliniahidi hii barabara atanisaidia. Vilevile aliahidi kwamba Namanyere Mjini atanipa pesa za kilometa tatu za barabara ya lami, lakini sikuona humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusu usafiri Lake Tanganyika. Awamu ya Nne tuliahidiwa meli mbili, Awamu ya Tano hakuna cha meli, ni utengenezaji wa Liemba kwa shilingi bilioni 5.6. Ndugu zangu, tuliahidiwa meli moja leo hamna meli ni matengenezo, tuna meli kule MV Mwongozo haitajwi kabisa, ilikuwa pacha pamoja na ile iliyozama kule Bukoba, zilitengenezwa siku moja…
MBUNGE FULANI: MV Bukoba.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Ndiyo MV Bukoba, lakini sisi ile meli tunayo mpaka sasa, haina matengenezo haina chochote imekaa pale Kigoma kazi yake kukodishwa na wafanyabiashara kidogo kidogo haijulikani inafanya kazi gani. Tunaomba Serikali kama haina pesa za kutosha ya kununua meli mpya iifanyie ukarabati wa hali ya juu MV Mwongozo ili iweze kuwahudumia wananchi wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kibaya zaidi ni kuhusu wafanyakazi wa Liemba, hii Marine Service inatesa watumishi. Mpaka leo mshahara wa mwezi wa nne wafanyakazi wa Liemba hawajapata, hawana bima ya afya, hawana hela ya likizo hata waliostaafu hawajalipwa mafao yao mpaka leo. Hata meli ya mtu binafsi ungesikia kelele, hii siyo meli siyo chochote na wakati wowote inaweza kutokea ajali maana hata engine zake zinazimika mara kwa mara ndani ya Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishukuru sana Serikali, nilipiga kelele tokea bajeti ya kwanza kuhusu Bandari ndogo ya Kabwe lakini kwenye bajeti hii nimeona kwamba itaanza kutengenezwa mwezi Julai. Naomba Mheshimiwa Waziri hicho kipindi cha mwezi Julai itakuwa Bunge hapa hakuna na mimi nitakuwa Kabwe, nataka nihakikishe huo mwezi Julai bandari ya Kabwe imeanza kutengenezwa kama ulivyoahidi kwenye bajeti yako. Maana bajeti ya mwaka 2015/2016 zilitengwa shilingi bilioni moja kwenye bajeti kwa ajili ya Bandari ndogo ya Kabwe lakini sikuona chochote mnasema tu vifaa vimeshawasili Dar es Salaam. Mmesema bandari ya Kabwe na Lagosa zitaanza kujengwa mwezi Julai na kipindi hicho Mheshimiwa Waziri tutakuwa huko, nitakuwa kwenye jimbo langu nihakikishe bandari ya Kabwe imeanza kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Serikali ni yetu wote, kuna mikoa hapa inapendelewa siyo uongo na ni mikoa ambayo iko mbele ukienda utafikiri uko Durban au uko Johannesburg na sisi wengine hata barabara za vumbi hatuna. Kuna watu wanadai viwanja vya ndege, kuna watu wanadai barabara za lami, sisi tunataka barabara za vumbi. Katika hayo maombi 3,000 watu walioomba kuhamisha barabara kutoka halmashauri kwenda TANROADS, lazima tufikirie mikoa mingapi ina lami, mingapi ina barabara za TANROADS ili tuinue mikoa ambayo iko nyuma kabisa. Kuna mikoa mingine iko kama peponi, leo unakuja kusema hapa maneno ya ajabu ajabu sijui kisungura na kadhalika, tuangalie mikoa hii.
Ndugu zangu, nchi hii tumetembea kila kona, labda ninyi hamjakwenda mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma mkaangalia jinsi tulivyokuwa nyuma katika suala la barabara…
MBUNGE FULANI: Na Simiyu.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Nendeni Simiyu, ninyi mnataka mpaka lami ziwafikie kwenye majumba yenu binafsi, hilo Mheshimiwa Waziri hatutalikubali. Ni lazima tuangalie upya mkoa upi una kilometa nyingi za lami, una kilometa nyingi za TANROADS ili na sisi mikoa mingine bajeti iende kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wilaya nyingine zina lami mpaka kwenye mitaa, miji yao ina lami makao makuu ya Wilaya…
MBUNGE FULANI: Sema.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Lakini Wilaya nyingine hazina lami hata kilometa moja. Ni kweli, mwenzangu ametoka kuzungumzia hapa, utashangaa, unabandua lami unabandika lami wakati zina mashimo, sisi wengine za vumbi hatuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hapa, toka Kirando kwenda Kazovu kuna vijiji zaidi ya sita mpaka Korongwe, tangu uhuru hawajaona hata bajaji. Wananchi wanapata taabu, Ziwa Tanganyika likichafuka mitumbwi inazama, akina mama wanakufa hawana njia nyingine ya usafiri ni kwa mguu au kwa mitumbwi, Lake Tanganyika wimbi lake ni la ajabu utashangaa mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Waziri aachane na wanaoomba viwanja vya ndege ndugu zangu hata abiria hakuna, wanapanda Wabunge, nilizungumze hapa, wanapanda Wabunge baada ya Ubunge kuisha hata tiketi hawakati, leo wanaomba viwanja vya ndege kila Wilaya atapanda nani. Akina mama na bibi zetu wanapanda magari, wanapanda treni, leo mnakwenda kuchukua mabilioni ya hela, tuchukue mfano kidogo wa uwanja wa ndege wa Mpanda nani anautumia? Tuseme ukweli nani anautumia uwanja wa ndege ya Mpanda, kuna ndege ya abiria inayokwenda Mpanda? Nimekwenda Tabora na ndege hakuna abiria anayepanda wala anayeshuka, Tabora hapo ndiyo mji mkubwa, leo unaomba kiwanja wakati abiria hakuna. Watu wa Tabora wanataka reli, watu wa Mpanda wanataka reli siyo viwanja vya ndege. Tusiwe tunadanganyana hapa, tugawane sawa hiyo keki. Mnabandua lami, mnabandika lami wengine hawajaona hata lami, ndugu zangu tunakwenda wapi, tuoneane huruma. Wengine nchi hii mpaka leo wanatembea kwa mguu hawana barabara, wewe unaomba kiwanja cha ndege, ndugu zangu, huoni hata aibu! Unakuja kuzungumza uwanja wa ndege mbele ya Bunge, mbele ya nchi hii wakati wenzako hawana barabara!
TAARIFA...
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi ninaosema reli ndiyo itakayotuletea uchumi, siyo ndege. Hayo makontena ya vifaa vya viwanda itapakia ndege? Wewe mwenyewe umelalamika ndege wanatoza shilingi 200,000 sanduku, ndege gani si unadanganya Bunge hapa, hakuna kitu kama hicho. FastJet bei yake ni rahisi kuliko ndege zote hapa leo unataka kuwapakazia FastJet begi shilingi 400,000 begi gani hilo jeneza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bandari, bandari yetu inatuletea msongamano mkubwa Dar es Salaam inatumiwa na nchi nyingi. Tuliomba bandari ya nchi kavu na kuokoa msongamano, reli ichukue mizigo mpaka Kibaha kule mbali au Chalinze ili magari yote ya kutoka nchi jirani yabebe mzigo kwenda nje. (Makofi)
Kwa kufanya hivyo, tutaondoa msongamano katika Jiji letu la Dar es Salaam. Hizi flyovers mnazoweka, sijui mnapanda mabasi yaendayo kasi haitasaidia kama bado mizigo inakwenda kuchukuliwa bandarini na magari makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mafuta lazima kuwe na mpango ili bomba la mafuta liende mbali kidogo na Dar es Salaam ili magari yote yakachukulie huko mafuta kwenda nchi za nje. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Sawa sawa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Bila kufanya hivyo msongamano utaendelea kuwa pale, magari kutoka bandari kupitia Mandela road ni foleni ya ajabu, saa tatu mpaka nne ni foleni, ndugu zangu tunapoteza muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri fanya kazi yako, wewe ni Waziri mzuri unafanya kazi, usitishwe na mtu yeyote, endelea kusaidia sehemu ambazo hazina barabara, hazina mawasiliano, lakini kusema mimi nataka uwanja wa ndege achana na viwanja vya ndege, achana kabisa havina maendeleo kwa nchi yetu bado changa vilivyopo vinatosha. Tuendelee na viwanja vya Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Kigoma pembezoni kule vinatosha lakini vingine vya katikati ndugu zangu ni kupoteza wakati hakuna abiria, nimefanya utafiti hakuna abiria. Sisi wa kule Sumbawanga kiwanja cha Mbeya kinatosha sana, tusidanganye. Tunakwenda na ndege FastJet asubuhi abiria hawajahi, leo unataka kiwanja kijengwe Sumbawanga, Mpanda, Mbozi, Kibaha, ndugu zangu hela zitatoka wapi? Tuendelee kujenga barabara na reli ili nchi yetu itoke katika uchumi huu uende uchumi wa mbele, tusidanganyane! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani unakuwa Mbunge hapa unasema Morogoro wanataka kiwanja cha ndege, Tabora uwanja wa ndege, dai gauge Tabora reli itakusaidia.
Tarime uwanja wa ndege, utapanda wewe peke yako Mbunge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri ahadi ya Rais alipokuwa Waziri aliniahidi hapa akatuma na wataalam kwenda kukagua barabara kilometa 35 tu, aliniahidi atanisaidia alipokuwa Waziri na alipokuwa Rais, nakuomba itekelezwe. Shahidi ni Mheshimiwa Mzee Lukuvi alikuwa anaambatana naye na yuko humu aliahidi kujenga hiyo barabara. Kwa hiyo, naomba hiyo barabara tafuta hela popote ikatengenezwe kusaidia watu wa Kazovu na Korongwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ujumbe wangu umefika.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, kwanza natoa shukrani za dhati kwa kunipa nafasi. Namshukuru sana Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kumteua Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Dkt. Medard Matogolo Kalemani kuwa Naibu Waziri na Makatibu Wakuu wote.
Ndugu zangu, hili Bunge tusifanye vichekesho au viigezo, tukumbuke Bunge la Tisa, sikuwa Mbunge, nilikuwa naangalia kwenye TV. Hapa Bungeni alikuwa rafiki yangu, kipenzi wangu, Waziri Mkuu anaitwa Edward Ngoyai Lowassa. Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa alijiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, hapa Bungeni. Cha ajabu jamaa wa pili hao hao wamemchukua kumpa tiketi agombee Urais awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, wanaona ajabu wakati si kweli kama Mheshimiwa Sospeter Muhongo alihusika na Escrow Account ila alisingiziwa kwa ufisadi wenu ninyi baadhi ya Wabunge, tunalijua hilo, lakini Mheshimiwa Edward Lowassa hapa alitolewa, alijiuzulu, lakini ninyi mkamkumbatia mkatembeza nchi nzima, je angekuwa Rais nchi hii ingekuaje? Ndugu zangu mnasahau matapishi yenu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sipendi kuwakashifu ninyi rafiki zangu, lakini mnashika pabaya lazima tuwaambie ukweli, mnakuwa na akili ya kusahau kama vile kuku wa kizungu au samaki anakwenda kunasa kwenye nyavu. Leo siku hata tano haijapita unasahau unataka ripoti ya kumkashifu Mheshimiwa Sospeter Muhongo na Magufuli kumchagua kuwa Waziri wa Nishati na Madini, akupe wewe kuwa Waziri, wakati ninyi hapa mmemtembeza Lowassa nchi nzima na Bunge hilihili, nchi nzima walifahamu kwamba amejiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, sasa si ajabu hii? Mnasahau…
TAARIFA...
MHE. ALLY K. MOHAMED: Hiyo ya Rais Mwinyi usizungumze, Rais Mwinyi alikuwa amelala nyumbani kwake…
…kule Magereza Shinyanga ni tofauti kabisa, wala hakuwa fisadi kama unavyofikiria wewe. Unamsingizia, Mwinyi hakuwa fisadi, Mwinyi alijiuzulu kutokana na kashfa ya Magereza Shinyanga, tofauti kabisa na rafiki yangu. Achana na ninyi, mlimtembeza mtu mnamjua kabisa mtu kajiuzulu kwa sababu ya rushwa, mkamtembeza nchi nzima, mtacheka wenyewe. Nimeshawapasha! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Wizara ya Nishati na Madini, hasa REA, imesaidia kabisa katika vijiji vyetu kupata umeme. Ninachoiomba Serikali, iwapatie pesa ya miaka mitatu ya nyuma, REA walikuwa hawajapata pesa, wanadai karibu bilioni 272 maana yake Wakandarasi wako vijijini wanadai hizo pesa mpaka sasa. Haiwezekani hizi hela za mwaka huu, bajeti ya mwaka huu, bilioni zaidi ya 500 waanze kuzimegua ili kuwalipa Wakandarasi ambao wapo kazini, lazima tuhakikishe kabisa kwamba wanapewa hela zao za miaka mitatu ya nyuma, bilioni 272 Wakandarasi wakalipwe ili awamu ya pili ikamilike bila matatizo yoyote na hizi Milioni 540 zifanye kazi kwa vijiji vyote katika nchi hii kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nataka kuzungumzia alipoishia jirani yangu Mheshimiwa Silinde, kuhusu vinasaba. Vinasaba vimepitwa na wakati, vinasaba tumezungumza mara nyingi hapa, tuliruhusu vinasaba kwa sababu ya tofauti ya bei ya mafuta. Leo bei ya mafuta inalingana nchi nzima, nani atachakachua? Tuliamua hapa mafuta ya taa yapande bei ili wasiwe wanachakachua na mafuta ya taa kweli yameteremka hayaagizwi tena nchini kutokana na kwamba walikuwa wanachakachua kwa sababu bei ya mafuta ya taa, bei ya diesel vinalinganalingana.
Mheshimiwa Spika, tunaona uchungu, yule wa vinasaba kutokana na mafuta yanayoingia nchini kwa mwaka mzima zaidi ya lita bilioni mbili, anachukua zaidi ya bilioni tisa kwenye gharama ya vinasaba. Huyu wa vinasaba faida yake ni bilioni 14. Usimamizi wa EWURA unachukua zaidi ya bilioni 13.9, wakati ukaguzi wa mafuta TBS yenyewe inachukua bilioni 2.8 kwa ajili ya kudhibiti mafuta kama yana ubora. Sasa vinasaba vina faida gani?
Mheshimiwa Spika, halafu cha ajabu, EWURA hao hao wako chini ya Idara ya Maji wakati vipato vyao vyote vinachukuliwa katika Wizara ya Nishati na Madini. Wenyewe ukiwauliza hawahusiki kabisa moja kwa moja na Wizara ya Nishati na Madini, lakini mapato yao, kila kitu wanachukua kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, nilizungumza Bunge lililopita kabla halijaahirishwa. Mpaka hawa jamaa wakawa wanatumia pesa kwenda gym, wanalipa kila mfanyakazi wa EWURA Dola 400, akienda gym asiende gym. Wanajipangia mishahara wanavyotaka, wananyanyasa watu wanavyotaka. Hivi vinasaba vimepitwa na wakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu TRA kukagua magari ya mafuta, TRA wana vituo njiani (checkpoints) tatu au nne, lazima magari yapite, TRA ikague mafuta kama yameteremshwa njiani au hayajateremshwa njiani. Kama watumishi wa TRA ni wabovu wanagongesha mihuri, je hao EWURA ndiyo watakuwa waaminifu kama malaika? Ni kuongeza mzigo kwa walipakodi kupandisha bei ya mafuta bila sababu. Nashauri hizi pesa za EWURA ziende REA moja kwa moja kutatua matatizo ya umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka mzima pamoja na usimamizi, EWURA wanachukua shilingi 18 na senti 85 kutoka kwenye gharama za vinasaba, halafu wanachukua shilingi sita kwa ajili ya usimamizi, jumla bilioni 42 . Hizi pesa zikienda REA kule zitasaidia kutatua matatizo ya umeme vijijini, kuwalipa Wakandarasi. Kwa hiyo, naomba Serikali irudie upya hivi vinasaba, iangalie kama vina umuhimu ama havina umuhimu. TRA ndio wasimamizi wa mafuta kama yanavuka mipaka au hayavuki mipaka.
Ndugu zangu na uchakachuaji ulipitwa na wakati, tulikuwa tunachakachua kwa sababu mafuta ya taa yalikuwa chini kabisa, mia tano, mia sita, tumeongeza ile bei ili wananchi wapate umeme vijijini, sasa nashangaa bado wanaendelea na vinasaba ili kuumiza wananchi wetu na havina faida wakati huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, hawa jamaa wa REA tuwape pesa kama inavyotakiwa. Hizi pesa ziende moja kwa moja REA zisipitie Hazina. Zikipitia Hazina zinakuwa na vigezo, miaka mitatu mfululizo, REA hawakupata hela kama inavyopangwa, miaka mitatu nimepiga hesabu hapa ni milioni 272, REA hawajapata hela. Wakandarasi wanadai kule vijijini, wanadai tozo kule vijijini, lakini sababu pesa ziko Hazina, hizi pesa zimeshatoka kabisa sasa kwa nini zisiende moja kwa moja REA ili REA wafanye kazi na tuwawajibishe kama hela hawajawapa wakandarasi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile naishauri Serikali, kwanza naishukuru sana kupunguza tozo ya umeme ili wananchi wetu wapate, lakini vilevile ndugu zangu wa mijini wamekaa wanaiba umeme, tatizo kubwa. Ni tatizo kubwa, haiwezekani mtu ana AC tatu, ana kiwanda hawafuatilii, Serikali kama wanashindwa REA peke yake kufuatilia TANESCO watafute JKT wapite nyumba kwa nyumba hasa mijini. Watu wa mijini wamekuwa wezi wakubwa wa umeme, wanaiba umeme mchana kutwa, Manzese wanasaga usiku wanaiba umeme, viwanda vidogovidogo wanaiba umeme, wanaoumia ni watu wa kijijini ambao hawana utaalam wa kuiba umeme.
Mheshimiwa Spika, mpaka baadhi ya watu wakubwa Serikalini wanaiba umeme, mashule makubwa makubwa yanaiba umeme, mahoteli yanaiba umeme. Ndugu zangu hatuwezi kufika, tuibe umeme, tuibe na maji, halafu hapa tunakuja tunalalamika tunataka kila kitu wakati sisi wote tunasaidia wizi.
Mheshimiwa Spika, unakuta Mbunge anamwona mtu anaiba umeme, hatoi ripoti, bado anamsaidia, tuna kazi ya kuilaumu Serikali, hatuipigi vita kwa njia ya namna hiyo, tumsaidie Rais Magufuli kutumbua majipu hata katika wizi wa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mkurugenzi wa TANESCO, Mkurugenzi wa REA, wanafanya kazi, inabidi tuwaunge mkono. Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo usisikie maneno ya majungu, mimi nilikuwa kwenye Kamati ya Public Account Committee, ni uzushi yule James Rugemalila alikuwa anadaiwa kodi, ndipo tuliamua alipe kodi; hana kashfa yoyote, kashfa kama mnayo nyie kwa majungu yenu hatoki na anakaa pale kwa niaba ya Serikali ya CCM. Ataendelea kufanya kazi na katika Mawaziri wachapakazi hakuna kama Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, hana siasa. Mnataka kwenda kwa vigezo vya rushwa, huyu hali rushwa, wala kashfa ya ESCROW Account hamkumwona hata kapewa kiroba cha hela waliopewa hela walitajwa humu yeye hahusiki.
Mnamsakama bure hamfanyi lolote, aliyemchagua Rais Magufuli kwa niaba ya Serikali ya CCM, kwa hiyo hawezi kubanduka atachapa kazi. Ngojeni na ninyi wananchi watawachagua na kutokana na uongo wenu wameshawagundua hamuwezi. Mmeshapigika huko nje mnaleta fitina za uongo hapa, hamkubaliki kwa speed ya Magufuli inayokwenda kama umeme. Kwa hiyo, Rais Magufuli speed yake hamuipati, shemeji zangu nawaambia ukweli, mliboronga kuchagua mtu aliyekataliwa na Bunge, akajiuzulu, mkamtembeza nchi nzima, sasa safari hii ndugu zangu kaeni chonjo mtapungua siku hadi siku. Ahsanteni sana. (Makofi)
SPIKA: Mlichokoza wenyewe jamani, jamani taratibu tufike au siyo. Haya, ahsante sana Mheshimiwa Ally Keissy hayo ndiyo mawazo yake, msimlaumu wala msimshutumu. Mheshimiwa Ahmed Shabiby mchangiaji anayefuata na Mheshimiwa Stephen Masele ajiandae.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi katika kuongelea Wizara hii muhimu sana katika nchi yetu. Bila Wizara hii kuwepo vyanzo vya maji vyote vingekauka, kama Wizara hii haikuwepo hakuna miti katika nchi hii, ingekuwa jangwa. Kusema kweli lazima tufuate sheria. Leo kuna maziwa kwenye bahari, Lake Tanganiyika, Lake Nyasa, Lake Rukwa, Lake Victoria na mwambao wa bahari, lakini nyavu haramu zinakamatwa zinachomwa hatusikii kelele. Kwa sababu wanakwenda kinyume na sheria. Watu wanaojenga kwenye road reserve wanavunjiwa maghorofa yao, hatusikii kelele. Lakini kelele ng‟ombe anapoingia kwenye Game Reserve au National Park tunasikia kelele, kwa nini tusikie kelele? Tufuate sheria, kila kitu kina mpaka wake, haiwezekani mimi leo niingie kwenye nyumba ya mtu bila hodi. Ile ni sheria, ni nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungu na ubaya wao, lakini tangu enzi za zamani walikuwa wanaita mashamba ya bibi, ilikuwa mwiko hata kuchuma jani. Leo tunakwenda kuchoma pori, tunafanya tunavyotaka na kila kitu, lazima tufuate sheria ndugu zangu. Morogoro tulikuwa tunaita Morogoro maji yanatiririka, leo Morogoro maji yako wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri, kabla ya Bunge kuisha nipe magari kwenda kwenye doria kule Lwafi Game Reserve na Rukwa, kupambana na waingiza mifugo mle ndani, wanatuharibia mbuga zetu. Nilizungumza na Mheshimiwa Nyalandu hapa akiwa Waziri, alikuwa tayari kunipa gari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaingiza ng‟ombe kule, tuna mbuga kule, game reseve ya kilometa 6,800 lakini hakuna gari, majangili wanaua tembo hovyo, leo hata mavi ya tembo hatuyaoni. Wanachoma pori hovyo, ng‟ombe wamekuwa ndiyo nyati badala ya nyati mle ndani, hatuwezi kukubali, sheria zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kugeuza jangwa ndugu zangu, nchi itakwenda wapi? Tutapata wapi maji ya kunywa! Bora mimi Lake Tanganyika inaweza ikawa na maji mengi, ninyi mtakwenda wapi, Dodoma itakwenda wapi? Acheni kuwa na jazba, fugeni ng‟ombe kama Denmark, Denmark wana ng‟ombe chache lakini wanauza maziwa nchi nzima. Leo mnafuga ng‟ombe, ng‟ombe moja ana kilo 70 unasema una ng‟ombe! Hatuwezi kukubali kuharibu mazingira kwa ajili ya wafugaji, hatutakubali!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu ni asilimia 75, wewe umezungumza wafugaji milioni mbili na wakulima wako wangapi nchi hii? Leo hawana sehemu ya kulima, watakosa maji wakulima wetu, tutapata wapi chakula tukikosa mvua, hatuna uwezo wa kumwagilia nchi nzima, kwa hiyo, ndugu zangu lazima tufuate sheria. Game reserves zipo kwa sheria national parks zipo kwa sheria na mfugaji yupo kwa sheria na mkulima yupo kwa sheria, hatukubali mkulima kwenda kulima kwenye game reserve wala mfugaji kwenda kwenye reserves.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoma nyavu hapa kila siku mnasikia, wavuvi haramu kule Ziwa Tanganyika. Mimi mwenyewe shahidi, nilishaenda kushuhudia wanachoma nyavu za milioni saba, milioni nane, Mwanza wanachoma nyavu, Bukoba wanachoma nyavu, Pangani wanachoma nyavu, huku kote wanachoma nyavu, hatusikii kelele, kwa sababu wanavunja sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba zote zinavunjwa, juzi wamevunja nyumba Dar es Salaam kwenye njia za maji, nani anapiga kelele hapa, kwa sababu wamejenga kinyume na sheria.
Wewe unaingiza ng‟ombe wako kwa nguvu zako utegemee pesa zako na wakulima wetu wanapata shida, wanakwenda kuhonga Mahakimu, hakuna kesi ya mkulima ilishida, mimi nina ushahidi. Hakuna kesi ya mkulima na mfugaji imekwenda mahakamani mkulima akashinda, hakuna! Hatuwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwangu kule kuna ng‟ombe 200,000 wakati tulikuwa na ng‟ombe labda 200 au 300. Wafipa ng‟ombe wao ni wa kulimia. Mfipa kabisa mfugaji ng‟ombe 50, leo kuna ng‟ombe 200,000. Na mimi nimeshazungumza, walipe kodi. Hatuwezi kuwaachia namna hii walipe kodi, wana uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi inalalamika haina hela MCC imetufinya misaada, wakati kuna mahali wanasema wana ng‟ombe wengi, hawalipi kodi hawa. Vyanzo vingi vya hela hapa mnaviacha, ndiyo maana wanakuja kutambukatambuka hapa. Sisi hatukuona siku ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mkulima hapa nje, Wizara hii tumeona wafugaji wamejazana hapa. Ndugu zangu tukiachia watachunga ng‟ombe mpaka Ikulu. Hatuwezi, twende kwa sheria. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kule kwangu kuna matatizo, mamba ndiyo wametuzidia. Watu wangu waliumwa na mamba, tumepiga kelele walipwe hiyo fidia maana yake huwezi kulipa maiti aliyekufa, thamani yake ni kubwa sana. Lakini sheria inasema mtu akiliwa na mamba, akiliwa na tembo, alipwe. Kwa hiyo nafuata taratibu, nina watu wangu kule wameliwa na mamba Lake Tanganyika, walipwe fedha zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, lazima tuheshimu sheria nchi hii. Ni kama wewe una nyumba yako mimi nikuingilie mle ndani, ninywe chai bila idhini yako, ninywe maji bila idhini yako utanipeleka Polisi. Ni kama Katavi Game Reserve, Luafi Game Reserve, hizi zote zina sheria na sheria zimetungwa hapa Bungeni na nyingine tangu Mkoloni ametunga sheria hizi, tukiachia hivi wenyewe ndugu zangu ni mwaka mmoja hakuna mnyama nchi hii, kuna watu wanachukua national parks ndugu zangu, ajabu kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila national park, bila game reserve ndugu zangu mvua hakuna, vyanzo vya maji vitakwisha. Mnaweza ninyi, mna hela Wabunge mnanunua maji ya chupa, watu wetu hawana hela ya kununua maji. Hatuna hela ya kununua maji, ni haya maji ya mvua ndiyo yanakwenda ardhini tunachimba visima. Leo miaka mitatu ikiwa hakuna maji hapa, mvua hakuna, tutakufa na ng‟ombe wenu watakufa na mbuzi watakufa na kondoo watakufa na nguruwe vilevile, mtabaki na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawaambia ndugu zangu, hakuna kwenda kinyume cha sheria, sheria ni msumeno, mtu yeyote anavamia ni kama vile wavuvi wanavua haramu, lazima wakamatwe wachomewe nyavu zao ili samaki waendelee kuishi. Samaki watakwisha, kwa hiyo tunaomba sheria itekelezwe. Hatuwezi kubembelezana, hatuwezi kutishana humu ndani, hakuna kumtishia mtu humu ndani. Mheshimiwa Maghembe amekuta sheria ipo. Nawapongeza TANAPA kwa kutupa madawati, kafanyeni kazi. Serikali yetu ina meno ya tembo yamejazana, msifanye kama Kenya. Uzeni, tupate pesa tununue magari na silaha kupambana na majangili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tupambane na haya majangili kwa hali yoyote. Vijana wetu hawa ma-game rangers wakienda mule ndani wanapambana kwa bunduki na yale majangali, akimuwahi anamuua. Kwa hiyo na ninyi wafanyakazi wa Serikali ma-game rangers, mtu unamkuta game reserves, national parks, mpige risasi afe! Kwa sababu ukimuachia atakuua wewe. Kaenda kufanya nini mule ndani, kwa idhini ya nani! Kaenda mfano, Katavi National Park, kufanya nini mle ndani kama siyo jangili, nani kampa idhini? Ni kumtandika risasi tu maana yake ukichelewa kumpiga risasi anakupiga wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni watu wabaya, tumewakamata Namanyere na bunduki nakuambia Mheshimiwa Maghembe, lakini wanaachiwa polisi. Nimekuletea ushahidi, wamekamatwa majangili na nyama ya tembo kilo 200 imepakiwa ndani ya gari linaitwa Noah, lakini siku mbili tatu wanaachiwa. Wanakamatwa na bunduki, siku mbili tatu wanaachiwa mpaka vijana wa TANAPA wanachoka! Kesi zao zinaishia hovyo hovyo tu. Nimekuletea sijapata majibu mpaka leo, nina wiki ya tatu, kwa ushahidi kabisa kwamba majangili wamekamatwa kule Nkasi lakini wanaachiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Rais Magufuli anasema, unamkamata mtu red-handed na jino la tembo, unamkamata na bunduki, na nyama ya tembo, unampeleka mahakamani anashinda kesi, red-handed! Hapa kuna nini, rushwa kubwa, siyo ndogo. Hawa dawa yao ni kule wanapokamatwa maana yake ukimpeleka mahakamani anakushinda, ni kumtandika risasi mambo yaishe huko huko mbugani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuchezewa, kuharibu mapori yetu kwa ajili ya faida ya ninyi kizazi cha leo, kumbukeni kizazi kinachokuja. Je, miaka ya nyuma wangekuwa wanaharibu kama mnavyoharibu ninyi mikaa, kuni, ng‟ombe mle ndani, tungeishi hapa? Kumbukeni na ninyi bado mnaendelea kusihi nchi hii. Mwenyezi Mungu kawaambia dunia karibu miaka miwili iiishe? Mna ahadi ya Mwenyezi Mungu dunia karibu iishe? Kwa hiyo, kuna vizazi na vizazi vinavyokuja na hii ni mali yetu wote, lazima tuitunze na tufuate sheria, sheria ni msumeno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Nkasi na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla tuna pori la akiba la ukubwa wa kilometa za mraba za 6,462.26; pori la akiba la Rukwa ukumbwa wake kilometa 4,194 na pori la Rwamfi kilometa 2,228.26 hilo pori linahujumiwa sana na majangili yaani wawindaji haramu ni kwa kuwa hilo pori la akiba limepakana na nchi jirani inakuwa vigumu sana kwa wafanyakazi wa idara kwa sababu hawana magari ya doria. Niliahidiwa kupewa gari jipya na Waziri wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Nyalandu lakini mpaka leo sijapokea hilo gari kwa ajili ya kuokoa mali kwa ajili ya wanyama na miti. Tafadhali hilo gari ni muhimu kwa doria na pia kwa upande wa Ziwa Tanganyika, kwa hiyo, usafiri wa majini ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ahadi ya aliyekuwa Waziri Mheshimiwa Nyalandu itekelezwe maana pori hilo la akiba linashambuliwa sana na wafugaji na majangili na wakata mbao. Naomba jibu kabla ya mwisho wa Bunge la bajeti kuhusu hilo gari maana ahadi ni deni na dawa ya deni ni kulipa, pori linaangamia sana sana.
Mheshimiwa Waziri gari jipya ni muhimu sana kwa ajili ya doria ya hilo pori.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi kwa dakika tano nizungumze kuhusu Wizara muhimu sana, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ambayo inahusiana na ushirikiano wa nchi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyozungumza wenzangu kuhusu Ubalozi wetu mdogo pale Lubumbashi, madereva na wafanyabiashara wetu wanapata tabu sana pale. Ubalozi mdogo Lubumbashi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchumi wa nchi yetu Congo ni muhimu sana kuliko Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuikamata Congo kwa sababu ni nchi kubwa, ina watu wengi na ina kila kitu itasaidia sana uchumi wa nchi yetu na tukiimarisha reli ya kati. Niliomba siku nyingi na nilipokuwa Kamati ya PAC tuliomba Ubalozi mdogo Lubumbashi na kama haiwezekani tumtafute Mtanzania yeyote ambaye yupo pale apewe hadhi ya kibalozi kusaidia wananchi wetu wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Muungano. Yupo Mbunge anazungumzia mambo ya ajabu kabisa kwamba tumewapunja, sheria ya masuala haya ya mambo ya nje lazima Waziri mmoja atoke Zanzibar sijui Waziri wa Mambo ya Ndani atoke Zanzibar. Ndugu zangu tuna Mawaziri watatu muhimu, Waziri wa Ulinzi katoka Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi, tuna Wizara kubwa ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano chini ya Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Naibu Waziri yupo hapa Mheshimiwa Masauni bado mnataka nini zaidi? Ndugu zangu tukitaka hivyo hata sisi tutasema, kwa mujibu wa population ni four percent. Hata mimi Rukwa nitasema tunataka Waziri maana hatuna Waziri na tuna idadi ya watu kama Zanzibar mbona hatuna Waziri hata Naibu Waziri na hatulalamiki hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuja kulalamika hata Rais akitaka kwenda nje awachukue Wazanzibari. Rais Magufuli anasema safari za nje hakuna unakuja Bungeni unataka safari za nje, hakuna tegemea pesa zako uende nje. Tusianze kuleta mambo ambayo hayatakiwi kwenye Muungano, tumeshaungana ndiyo hivyo hivyo, sasa ninyi mnataka nusu kwa nusu ndugu zangu? Itawezekana wapi? Haiwezekani ndugu yangu! Nusu kwa nusu haiwezekani! Ninyi mpo four percent mtapata four percent ya kila kitu.
Mheshimiwa Khatib tulia, usipige kelele hapa kwamba mnataka Mabalozi wengi, hapana! Nchi yote tuna Mabalozi 21 mkipata hata Naibu Mabalozi shukuru Mungu. Mheshimiwa Khatib tukikuambia ulipie Balozi mmoja tu nchi yako italipa gharama ya Balozi kule nje?
Mheshimiwa Khatib tulia, usipige kelele hapa kwamba mnataka Mabalozi wengi, hapana! Nchi yote tuna Mabalozi 21 mkipata hata Naibu Mabalozi shukuru Mungu. Mheshimiwa Khatib tukikuambia ulipie Balozi mmoja tu nchi yako italipa gharama ya Balozi kule nje?
Tulieni! Hatuwezi kwenda hivyo unasimama hapa unasema sisi tumepunjwa, hamkupunjwa kitu bado tumewasaidia. Bungeni hapa mmekuja 54, mngejaa kule Zanzibar mngeenea kwenye Jimbo ninyi Ma-CUF, mngeweza kuenea kule kweli? Tukiwaambia tu sasa hivi nendeni kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine amezungumzia ndugu yangu, mimi nilikuwa kwenye Kamati ya PAC kuhusu mgonjwa kutoka Zanzibar, mgonjwa yule alipelekwa na Serikali ya Zanzibar hakuna kukanusha hapa. Nilikuwa mjumbe wa Public Accounts Committee, mgonjwa yule alipelekwa na Serikali ya Zanzibar na atahudumiwa na Serikali ya Zanzibar, Serikali ya Tanganyika ilisema ahudumiwe kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafahamu kwa sababu nilikuwa mjumbe wa Public Accounts Committee hesabu hizi zilikuja kwetu. Huyu bwana alipelekwa na Serikali ya Zanzibar akatibiwe kule, Wizara ya Afya siyo ya Muungano. Kwa hiyo, hili deni ni la Serikali ya Zanzibar likadaiwe huko huko, hatuwezi kulipa sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndugu zangu tusiende papara kwa habari za kutaka zaidi vyeo au namna gani na sisi tutadai vyeo. Rais anapanga Mawaziri kutokana na jinsi anavyotaka yeye huwezi kumlazimisha awape Zanzibar Mawaziri 10 au 15, ninyi kwanza kule kwenu mna Mawaziri zaidi ya 20, mna Wabunge kule kwenu hawatoshi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine na nimezungumza mara nyingi hapa, Wizara ambazo siyo za Muungano muwe mnatungoja nje tunabaki peke yetu hapa tukimaliza za Muungano ndiyo tunawaita mnaingia ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani uje kuchangia Wizara ya Kilimo inakuhusu? Wizara ya Maji inakuhusu. Kwa hiyo, muwe mnachagua Wizara za kuchangia kuanzia sasa, changia Wizara inayokuhusu basi Wizara nyingine tuachiaeni wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa, naipongeza Wizara ya Nishati na Madini hasa Mkurugenzi Mkuu wa REA na Mkurugenzi wa TANESCO kwa kusaidia mradi wa kupeleka umeme kwenye Bwawa la Mfii, tegemeo kubwa la
maji Namanyere kupunguza kutoka shilingi bilioni 59 mpaka shilingi bilioni 23.

Mheshimiwa Naibu Spika, dawa ya deni ni kulipa. TANESCO inadaiwa shilingi bilioni 820 na TANESCO yenyewe inadai pesa. Kuna Mashirika maalum yanadaiwa pesa. DAWASA, Idara ya Maji, inadaiwa; yenyewe inauza maji, kwa nini isilipe hela za TANESCO? Wakala wa Umeme Zanzibar (ZECO) wanadaiwa pesa shilingi bilioni 123. Wakala tofauti na kitu chochote, ni sawa na mimi na duka langu, wewe unaleta mali yako nakuuzia kwa bei unayonipa mimi nakurudishia zile hela. Cha ajabu ZECO hairudishi hela TANESCO, ni aibu! Serikali nzima ya Bara inadaiwa shilingi bilioni 40, ZECO inadaiwa shilingi bilioni 123, tutafika wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba TANESCO wawe na mtindo wa kukatia umeme popote wanapodai.
Haiwezekani kuleana namna hii! Kuna Wizara zote za Serikali ya Bara zinadaiwa. Hakuna Wizara hata moja isiyodaiwa na TANESCO, ni ajabu. Mtu binafsi, mwanakijiji ambaye hana mbele wala nyuma, ananunua umeme kwa LUKU. Mwisho wa mwezi hana hela, hapati umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Wizara za Serikali hapa pamoja na Mashirika ya Serikali makubwa, hayalipi deni la TANESCO. Haiji kwenye akili ya binadamu kabisa! Dawa ya deni ni kulipa. Mwanakijiji hana mbele, hana nyuma, hana chochote analipa deni la TANESCO, anawekewa LUKU. TANESCO lazima ifanye operation nchi nzima hasa miji mikubwa. Kuna wizi wa ajabu wa umeme katika nchi hii. Kuanzia Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Sumbawanga, popote pale kwenye mji mkubwa, kuna wizi mkubwa wa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya Nishati na Madini, kama haina wafanyakazi wa kutosha wakaazime JKT. Wachukue kwenda nyumba kwa nyumba, kijiji kwa kijiji; haiwezekani Shirika kupata hasara namna hii! Kuna wizi mkubwa wa umeme! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naiomba Serikali, msongo wa umeme kutoka Mbeya kwenda Kigoma kupitia Sumbawanga na Mpanda, hii mikoa mitatu au minne hii, inaleta hasara kubwa sana kwa Shirika hili la Umeme. Tunatumia majenereta, mafuta yanalika kwa kiasi kikubwa, hakuna faida TANESCO inapata kwenye Mikoa hii ya Kigoma, Katavi na Rukwa, Shirika hili linapata hasara, ndiyo maana Shirika hili linaingiza hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haiwezekani tusipate umeme wa gridi ya Taifa kutoka Mbeya kwenda Kigoma mpaka Nyakanazi ili kuondoa mzigo kwa TANESCO. Haiwezekani mchakato kila siku; tupate umeme wa uhakika. Kwingine wanapata umeme wa uhakika, lakini mikoa hii mitatu, ni majenereta tu yananguruma. Kwanza yanaharibu mazingira kwa kusababisha moshi mijini. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu REA. Tatizo la REA ndugu zangu ni kutokupata hela za Serikali. Tuliamua hapa mafuta shilingi 150 iende REA, lakini hela haziendi. Asilimia 40 ndiyo hela zinakwenda, zikiingia Hazina hela zile, hazitoki kwa wakati. Wakandarasi hawafanyi kazi kwa sababu hawapati pesa. Mradi wa shilingi milioni 200 utafika milioni 300 kwa riba kwa sababu pesa hazipelekwi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, hela tunazoamua hapa Bungeni za 150 kila lita ziende moja kwa moja REA. Haiwezekani zikifika Hazina zinakwama zinatoka kwa masharti au zinabadilishwa njiani, haiwezekani. Kwa hiyo, naiomba Hazina ipeleke hela za REA ili wananchi wafaidike na umeme. Hatuwezi kumaliza vijiji hivyo 7,000 kama pesa haziendi, tunadanganyana hapa. REA wanapata kiwango cha chini cha pesa, hawawezi kuendelea kuweka umeme vijijini kama hawapati pesa. Tumeamua hapa na mafuta ni hot cake, mafuta
yanauzika. Tunauza mafuta, hela zinaingia, lakini hazijulikani zinakokwenda. Haiwezekani, lazima
wapewe pesa zinazohitajika ili Wakandarasi waanze kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naishauri TANESCO, sehemu za mapori makubwa, REA wapeleke nguzo za zege kuondoa hujuma ya kuchoma mapori na nguzo kuungua. Kuna mapori mazito na watu wetu hata ukiwapigia mbiu, useme mpaka uchoke, lakini kila msimu
lazima wachome mapori. Hawa watu ni hatari sana! Kwa hiyo, nawaomba, sehemu ambazo ni misitu minene, waangalie kutafuta nguzo za zege ili kuepuka kuitia hasara TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimefurahi na REA III. Waziri ametuhakikishia kwamba transformer zote na waya zote watanunua katika viwanda vyetu. Hiyo itasaidia kabisa kwanza kuharibu hela zetu za Kigeni kwenda kununua transformer mbovu nje au China wakati Arusha
kuna transformer imara na zinatosha miradi yetu kuzalisha umeme. Tuna viwanda vingi pamoja na TANESCO ina-share katika East Africa Cable, wanunue waya pale. Haiwezekani kwenda kununua waya nje wakati tuna waya zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wajiepushe kupitia Wakandarasi ambao ukienda, inapitia kwa watu wanazidisha bei ajabu! Miradi ya ajabu; unakuta mtu unayechukua tenda kuagiza waya nje, haijulikani ananunua bei gani kule anakuja kutubamiza bei wakati tuna viwanda vyetu wenyewe hapa nchini. Huu ni ubadhirifu na ufisadi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bandari. Ndugu zangu hii nchi ina bandari Mungu kaibariki. Nilikwenda Bandari ya Mtwara hata Afrika Kusini hakuna bandari kama ya Mtwara. Bandari ya Tanga ambayo ingesaidia Mkoa wa Kilimanjaro, Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Mara na Tanga yenyewe, ni ajabu watu wa Tanga na Kilimanjaro wanatumia Bandari ya Mombasa. Ni aibu kubwa kwa Serikali, wakati tuna bandari yetu wenyewe. Mungu katupa bandari katika mwambao wa bahari, lakini ni ajabu tunatumia Bandari ya Mombasa kuliko kutumia Bandari ya Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mpaka watu wa Dar es Salaam, wafanyabiashara wa Dar es Salaam wanatumia Bandari ya Mombasa, ni aibu kubwa kwa Serikali. Ni aibu, tumekuwa kama Burundi au Rwanda ambao hatuna bandari! Tujiulize mara mbili mbili, kuna nini hapa?
Kuna mdudu gani? Lazima tuimarishe bandari zetu ili wananchi wafaidike na bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kwenda hovyo hovyo, tunafanya kazi hovyo hovyo. Serikali iwe kali kidogo kwa kiongozi yoyote anayeingia tenda, manunuzi ya ajabu ajabu yanayotuumiza sisi, mdudu wa manunuzi huyu; lazima achukuliwe hatua kali. Haiwezekani wewe kitu unajua, hata mimi ambaye sikusoma na wala sio Mkandarasi, unajua kabisa hiki kitu sh. 10/= unakwenda kuandika sh. 500/= na unatia saini cheque inatoka! Kusema ukweli hao ndio maadui wa nchi. Hawa nilikuwa nazungumza siku zote! Huyu mdudu manunuzi, tungewakamata hawa tukawapiga risasi siku ya Ijumaa au Jumapili watatu au wanne, wangeshika adabu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani hii Serikali ni tajiri kuliko Ubelgiji, kuliko Ureno, leo unashangaa hapa wanasema Ureno inajenga reli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro. Ni aibu, wakati sisi ni matajiri kuliko Ureno. Ureno maskini wa Mungu wale leo hata chakula
hawana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali ifuatilie. Naishukuru sana REA lakini wapewe hela kwa wakati ili wafanye miradi yetu na vilevile wafikirie vijiji ambavyo viko nyuma sana, kuna mikoa iko nyuma sana, ndiyo waelekeze REA III. Kuna mikoa mingine kuna umeme
mpaka chooni. Sasa watufikirie na sisi kule Rukwa ambao tumekuwa nyuma kabisa, tumepata umeme miaka miwili iliyopita. Ni ajabu kabisa katika nchi hii! Ndiyo tufikirie zaidi kutupelekea huu mradi wa tatu na wananchi wetu wapate mwanga. Wananchi wa kule siyo wezi kama hawa
wa Dar es Salaam au Dodoma. Huku kuna wizi; tukipita leo hapa hapa Dodoma, tutakamata wezi siyo chini ya 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani Shirika lipate hasara, ni wizi mkubwa! Pamoja na mashule haya, viwanda hivi, wanasaga usiku, wote ni wezi. Kwa hiyo, nawaomba sana Wizara ya Nishati na Madini wanisikilize. Operation maalum ifanyike, pamoja na Waheshimiwa Wabunge humu tumo, haiwezekani. Ndiyo nimesikia juzi juzi wanalaumu sana Ma-DC. Leo kuna Wabunge walikuwa Ma-DC humu, walikuwa wanakemea mpaka bangi, Mheshimiwa Mwamoto ni shahidi kule Kibondo, lakini leo ni Mbunge, akiona bangi,…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Anaogopa kura zake zitapotea.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Keissy muda wako umekwisha, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ahsante sana kwa kunipa fursa hii nichangie kidogo kuhusu
Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa
Waziri Mkuu, kwa muda mfupi aliokuwa Waziri Mkuu alikuja
Namanyere akafanya ziara katika Jimbo langu la Wilaya ya Nkasi akatembelea mpaka vyanzo vya maji ambavyo
nilikuwa napiga kelele hapa kila mwaka habari ya shida ya
maji Namanyere. Sasa mwaka huu tatizo la maji Namanyere
litakuwa historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile namshukuru Waziri
wa Maji, alifika Namanyere mpaka kwenye vyanzo vya maji
na akaahidi kusaidia mitambo ya kusukumia maji.
Namshukuru vile vile Waziri wa Mambo ya Ndani alifika
Namanyere, pia Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Makamba
alitembelea Namanyere. Mawaziri wote walitembelea
Namanyere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa
namshukuru Mheshimiwa Magufuli. Mimi nilikuwa Bunge la
Nne hapa ndugu zangu, nilikuwa msumari nazungumza ukweli
kuhusu mafisadi, wezi wa mali ya umma, nilizungumza mpaka
makaburi yao yafukuliwe wafungwe minyonyoro kwenye
makaburi. Nilizungumza vile vile safari za Wabunge kwenda
nje hazina manufaa, tunapishana airport kama wakimbizi.
Nilizungumza hapa kabla Mheshimiwa Magufuli hajawa Rais,
nilisema hizi safari hazifai! Hebu niambieni Mbunge hata
mmoja aliyekwenda nje alete tija hapa kama sio ubadhirifu
wa hela humu. Wengine walikuwa wanarudia airport,
nimezungumza hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushahidi wakamate
hata passport zao waangalie, kama walipewa hela
wakaenda, passport zitaonesha. Wengine wanapewa siku
kumi wanakaa siku mbili wanarudi. Ndugu zangu tumsifu
Magufuli amedhibiti nchi! Nilimwambia Rais Magufuli Kinyerezi
kwenye kuzindua mtambo wa umeme nikasema; spidi yako
bado sijaiona, bado spidi ni ndogo. Nchi hii bado mafisadi
wengi, wanatuibia! Juzi juzi tu tender ya EWURA wanataka
kutuingiza kutuibia bilioni sita kwa mwaka, shilingi bilioni kumi
na tatu za Kitanzania kwa miaka mitatu mkataba huo
tutaibiwa bilioni 40 wakati hatuna zahanati, hatuna
madawati, hatuna kila kitu. Ndugu zangu bado watu
hawaogopi Serikali, wapo! Hao wanataka wabanwe
ikiwezekana kunyongwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Jimbo.
Nimezungumza, Mfuko wa Jimbo kwanza usimame. Wapitie
upya majimbo sio sahihi. Uchaguzi uliopita safari hii
tumezidishiwa Kata kutoka Kusini kwenda Kaskazini, majimbo
yameongezeka. Jimbo langu kata nzima imehamia kwangu
lakini Napata mfuko wa jimbo ule ule, nitahudumiaje kata ile
nyingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa
Simbachawene nikampelekea na taarifa kwamba kata
nzima imekuja kwangu. Haiwezekani niendelee kupata mfuko
wa jimbo ule ule. Simamisha kwanza nchi nzima, fanya
mchakato upya. Wabunge wengi wamelalamika hapa.
Halmashauri ya Mji wa Namanyere ina vigezo vyote cha
ajabu wamekwenda kutoa halmashauri zingine hazina
vigezo! Ushahidi tunao, upendeleo wa hali ya juu na ugawaji
wa majimbo vile vile kwa upendeleo. Haiwezekani! Nchi ni
moja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majimbo kama kwa
ndugu yangu huyu hapa, Sikonge square kilometers 27,000,
kwa Malocha, 15,000, kuna majimbo mengine square metre
1,000 humu, kuna mengine 200! Haiwezekani! Hatuwezi
kwenda hivyo. Lazima twende sambamba, haiwezekani
Mbunge yule yule anapata pesa ile ile, gari ile ile, mafuta
yale yale, jimbo lake linakuwa kubwa kama Rwanda, kama
Burundi, haiwezekani! Hii ni kuoneana. Lazima Namanyere
sisi tupate halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mikoa imeanza juzi juzi
halmashauri tano, sita. Cheki Mkoa wa Rukwa, Mkoa mkubwa
kabisa halmashauri zile zile nne, haiwezekani! Ni maonezi
hatuwezi kwenda. Ahadi ya Rais alituahidi alipokuja,
barabara ya lami kilometa tatu tunaitaka Namanyere,
alituahidi kilometa tatu za lami, tunazitaka!
Mheshimwa Mwenyekiti, hospitali Namanyere. Tuna
miaka 40 Wilaya ya Namanyere haina hospitali ya wilaya,
miaka 40! Watu wanasema miaka 20, miaka mitano mpewe hospitali. Kuna wilaya zimeanzishwa juzi zina hospitali ya
wilaya, sisi miaka 40 hamna hospitali ya wilaya. Haiwezekani,
haya maonezi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu DC wetu wa Nkasi.
Tangu ameanza hana gari, hana usafiri. Anahudumia wilaya
square kilometers 13,500 hana gari! Leo kasimamia shule 105
kujenga madarasa matatu shule ya msingi katika kila shule
kuhamasisha wananchi na anajenga, anasimamiaje? Hana
gari DC, anaombaomba magari. Polisi Namanyere hawana
hata matairi. Ndugu zangu tuoneane huruma, kuna wilaya
zingine zinapewa magari matatu, manne hata hadhi ya
wilaya hazina, ziko humu humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge hata
ukubwa wa Kata kama Kata yangu hakuna! Wanapewa kila
kitu. Lazima tufanye mchakato upya. Ikiwezekana Rais
Magufuli aangalie, kama majimbo mengine ayafute!
Ayavunje majimbo na halmashauri zingine. Hatutaki mambo
ya kuoneana. Kupanua halmashauri ambazo hazina hata
uwezo, hazikusanyi chochote! Mzigo kwa Serikali. Tuambizane
ukweli hata kama unauma. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri wa ziwa Tanganyika;
Awamu ya Nne tumeahidiwa meli mbili katika ziwa
Tanganyika lakini nakuja kusoma tena ni utengenezaji wa
Liemba ina miaka 113. Ndugu zangu, tunataka usafiri wa
ziwa Tanganyika, meli mpya! Liemba itengenezwe maana
bado inafaa, bado ni nzuri ikarabatiwe, lakini meli mpya
tunaitaka katika Ziwa Tanganyika, wananchi wanapata
matatizo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu pembejeo. Hao
wanaogawa ruzuku ya pembejeo, ndugu zangu haiwezekani
mtu anasema ana deni milioni 360 wakati tukipiga hesabu ni
mbolea bilioni 1.8 alipeleka katika jimbo langu.
Wanachakachua, lazima wafuatiliwe. Nimemwambia hata
Waziri wa Kilimo, Waziri Mkuu nimemwambia, katika Jimbo
langu la Nkasi kuna kata kadhaa, hakuna kuwapa pesa
wamechakachuka, ni wezi wa hali ya juu. Ndiyo hawa Rais Magufuli anawatafuta awafunge mara moja hao. Hawa
hawafai katika nchi yetu, haiwezekani anakuja mtu na
briefcase anapewa kuleta mbolea, analeta gari moja la
mbolea anataka milioni 360, huu ni wizi wa hali ya juu. Hawa
ni watu wabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ya mbolea
ndugu zangu bora iuzwe bei chini, mambo ya pembejeo
hakuna tena ruzuku waache ruzuku, kila mtu anunue kama
vile ananunua vocha ya simu, mambo yaishe! Wametajirika
watu kwa hela za vocha hizi, nchi hii ni wezi wa hali ya juu.
Waaminifu ni wachache! Kwa hiyo, agenda zangu ni hizi hizi;
nataka Namanyere kuwa Halmashauri ya Mji. Mheshimiwa
Waziri Mkuu uliona Namanyere ilivyokuwa, kuna halmashauri
zingine ukitembelea hakuna lolote, mnawapa halmashauri,
ni uonezi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri Ziwa Tanganyika;
namwomba Rais Mheshimiwa Magufuli aendeleze, azidishe
mara mbili. Asionee huruma mtu yeyote anayeiba hela za
walipa kodi. Wananchi wetu, ndugu zangu majimboni
kwangu kuna matatizo. Nazungumza habari ya usafiri kutoka
Kilado kwenda Kazovu miaka 50, tangu uhuru hatujaona gari!
Nashukuru Ofisi ya Rais imenipatia pesa, mwaka huu
wananchi wa Kazovu wataona gari! Niseme nini sasa? Nikose
kumshukuru? Nilikuwa napiga kelele hapa wananchi
hawajona gari, hawajaona bajaji lakini mwaka huu wananchi
wataona gari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba na Waziri wa
Ujenzi aniongezee tena hela nipasue ile barabara Kazovu
kwenda Korongwe, wananchi wafurahie uhuru katika nchi
yao. Rais asikate tamaa aendelee kupambana na watu
kama hawa. Hakuna kuoneana aibu!
Haiwezekani ndugu zangu katika nchi zingine, mtu
anaimba wimbo wa matusi kumtukana Rais mwanzo mwisho
anaachiwa! Nchi gani hii? Utawala gani huu? Wewe mtu
unamtukana Rais unaachiwa? Aende Rwanda kule
akaangalie au nchi za Kiarabu, watakunyonga! Wewe unamtukana Rais wa nchi, wewe umekuwa nani? Uhuru
gani? Demokrasia gani hii? Unaimba nyimbo, wewe nyimbo
na mtu wa studio anarekodi nyimbo, ama kweli sio utawala
huu! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wangeniachia mimi dakika
mbili niwaoneshe hawa! Haiwezekani! Kiongozi wa nchi
anatukanwa na nyimbo, ukiisikia hiyo nyimbo ya Roma sijui
Mkatoliki, ndugu zangu nyimbo ya aibu. Haiwezekani mtu
unasikiliza nyimbo kama ile. Halafu unamshabikia mtu!
Haiwezekani! Kusema kweli ni makosa, ni kukosa adabu. Rais
wa nchi hatukanwi popote pale. Haiwezekani! Nendeni nchi
zingine, nenda Rwanda hapo, nenda Burundi, nenda DRC
ukaangalie, watakushughulikia! Nyie mnacheka cheka hapa,
haiwezekani kumchezea Rais namna hii. Huu ni utovu wa
nidhamu. Huyu Rais anaheshimika, dunia nzima wanamsifu
Magufuli. Leo nyie wenyewe ndiyo mnamwona hafai kwenu,
kote ukienda wanamsifu, Uarabuni wanamsifu, Ulaya
wanamsifu, sijui ukienda…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante

The Finance Bill, 2016

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Wabunge wote tuliopo hapa tuna matatizo kwenye majimbo yetu, tuna shida ya maji, barabara na mawasiliano, hakuna Mbunge hata mmoja hapa asiye na shida kwenye jimbo lake, hatuna barabara kabisa. Kwa hiyo, Serikali lazima ijipange kukusanya kodi kwa kila mtu bila kuona huruma.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya makampuni ya simu yajiunge na Dar es Salaam Stock Exchange mara moja, tuwadhibiti. Vilevile tulipe kodi kwa wafuga kuku, wafuga ng‟ombe, baiskeli kama zamani Wakoloni walikuwa wanadai kodi kwenye baiskeli mpaka mbwa alikuwa analipiwa kodi, nashangaa siku hizi hakuna cha kodi, kila kitu kodi, bila kodi hatuwezi kwenda. Hizi hela za Wazungu zinazokuja hapa ni kodi yao, hata vyama za siasa vinavyopata ruzuku vikatwe kodi. Haiwezekani vinapata ruzuku ya Serikali vinachukua moja kwa moja, vinanufaika bila kukatwa kodi na vyenyewe vikatwe kodi mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mkoloni tulikuwa na mikoa tisa na barabara zilikuwa mbovu ajabu katika nchi hii. Leo tunaongeza mikoa na watendaji, tunaongeza shida kwa Serikali, imekuwa nakama. Kila mtu anadai mkoa, kila mtu anadai jimbo, kila mtu anataka kila kitu wakati Serikali yenyewe tunataka matumizi yaende kwa wakati, tunataka barabara sisi, hatutaki mikoa kuwa mingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo natoka hapa nakwenda Mbeya kwa saa nane zamani Mbeya huioni labda siku tatu, hapa na hapa mkoa, hapa na hapa jimbo. Serikali ipitie upya majimbo yaliyopo katika nchi hii, vigezo vitumike sio mimi nilikuwa mkubwa, mimi ndiyo Waziri Mkuu au mimi ndiyo Rais nagawa majimbo navyotaka, mkoa wangu unapata majimbo, Kilimanjaro leo majimbo tisa, Tanga majimbo 11, ndugu zangu, hatuendi hivyo, mikoa mingine kama Rukwa majimbo matano, lazima tupitie upya tubane hela za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na utitiri wa majimbo, tugawe majimbo kutokana na vigezo. Mimi nimetoka huko nagawa majimbo navyotaka, nagawa halmashauri navyotaka, tunaongeza gharama ya nini? Twende kwa vigezo tupate haki sawa kwa kila mtu. Haiwezekani mkoa mmoja idadi ya watu walewale majimbo 11, mikoa mingine kama nchi ya Burundi majimbo matano, haiji! Gharama za nini hizi? Lazima twende na wakati. Hatuwezi kudekeshana hapa, hatuwezi kubembelezana, majimbo yaende kwa vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siogopi kugombana na mtu, nasema ukweli, twende kwa vigezo, huwezi kunitisha, twende kwa vigezo. Tanga leo au Kilimajaro inaingia mara mbili kwa Mkoa wa Rukwa, nani atabisha hapa? Twende kwa vigezo, mimi nasema ukweli, hatuna barabara hatuna chochote, tubane hela za Serikali twende kwa vigezo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu alipe kodi, hawa wanaotembeza mali barabarani na wenyewe walipe kodi. Wengine wanatembea na mali kuliko mwenye duka. Leo mama muuza nyanya kila siku analipa sokoni Sh.500 kwa mwezi analipa Sh.15,000 wewe unatembea.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mtu ana ng‟ombe 300,000, ana ng‟ombe 30,000 halipi kodi, nazungumza kila siku hapa, mifugo ilipe kodi, kwa nini hamleti kodi ya mifugo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua property tax ya nyumba, ndugu zangu basi halmashauri wapeni wadai kodi za mifugo, hawana chanzo chochote cha rasilimali. Kwa hiyo, wapeni na wenyewe wadai kodi ya mifugo, wadai kodi ya mbwa na wadai kodi ya baiskeli.
Michango ya harusi, harambee za vyama, harambee za harusi na yenyewe idaiwe kodi.
Michango ya misiba tumeona mikubwa hata humu Bungeni. Waheshimiwa Wabunge wanachanga Sh.100,000 kwa misiba, idaiwe kodi. Hatuwezi kusamehe kodi, VAT ya Sh.18,000 itolewe kwa kila Sh.100,000, wanachanga Wabunge humu.
Sadaka zitolewe kodi. Wazungu wanalipia kodi kila kitu, hatuwezi kuendelea na Serikali yetu hii, Serikali yetu ina watu wengi ndugu zangu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapitwa na Rwanda kwa makusanyo ya simu tu, ni kitu cha ajabu kabisa, wakati watu wana simu nne mpaka tano hapa Tanzania, hatuwezi kwenda namna hii bila kodi. Hatuwezi kumwambia Waziri wa Fedha leo tufute kodi ya pikipik na magari, akatoe wapi hela yeye wakati mnamdai maji, barabara na madawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nasema kila kitu kipangiliwe, ng‟ombe walipiwe kodi, baiskeli zilipiwe kodi, mifugo yote ilipiwe kodi, kuku alipiwe kodi na ruzuku ya vyama ilipiwe kodi na michango ya harambee yote ilipiwe kodi. Tuwe wakali kwa kodi, leo Uingereza hawana chochote lakini ndiyo wanaotusaidia sisi ni kwa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa wanyonyaji kwa Wazungu namna hii kwa sababu gani, haiwezekani! Tujibane tulipe kodi. Ni aibu wewe unazaa watoto wako unakwenda kulisha nyumba ya jirani, haiwezekani! Tubanane sisi wenyewe, hakuna kusema chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii migodi ibanwe, haiwezekani Mheshimiwa Mbunge kuja hapa anatetea migodi, ndiyo tunakuwa na mashaka na Wabunge wetu humu ndani. Unatetea mashirika ya simu wewe, unatetea migodi, tuna wasiwasi na Wabunge. Mbunge unasimama unatetea mgodi, unatetea shirika la simu, tuna wasiwasi na wewe. Ingawa ushahidi wa rushwa kuukamata ni taabu lakini tutakuuliza mara mbili wewe una nini hapa na hili shirika, umepewa nini wewe mwenzetu? Hapa hakuna kuteteana, tunakuja kujenga nchi yetu ili ijitegemee kama Rais wetu alivyosema. Haiwezekani wewe nchi yetu kubwa, ina kila kitu tunakwenda kuombaomba, haiji hiyo! Mbunge atakayesimama hapa kutetea habari ya kutolipa kodi tuna wasiwasi na wewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, yangu ndiyo hayo.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's