Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Omar Abdallah Kigoda

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. OMAR A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji wake, pia kulitakia kila la kheri Baraza la Mawaziri katika kutekeleza Ilani ya Chama Tawala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, napenda kujikita kwenye ushauri. Kwanza; Serikali ijitahidi kufuatilia kwa karibu fedha ambazo zinakwenda kwenye Halmashauri, bajeti nyingi sana zinapangwa vizuri, lakini inapokuja suala la matumizi huwa zinapotelea Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; kuwe na uwazi wa mapato ya ndani yanayokusanywa na Halmashauri. Hii itasaidia hata kwa Wabunge kujua ni kiasi gani kinapatikana na kiasi gani kinatumika kurudi kwenye huduma za jamii. Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya huduma mbovu kwa jamii kama barabara za mitaa, vyoo na mahitaji mengine madogo madogo ambayo Halmashauri ina uwezo wa kuhudumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu; suala la uajiri wa wafanyakazi ningeshauri pia kuwe na upendeleo wa baadhi ya wafanyakazi wawe wazawa ili kuwe na uchungu wa utendaji. Inaonekana watumishi wengi wa Halmashauri ni watu wanaokuja na kuondoka. Hili pia linasababisha kuzorota kwa maendeleo kutokana na ugeni wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne; napenda pia kumshauri Waziri mara kwa mara wawe wanapeleka wataalam kwenye Halmashauri zetu ili kufanya auditing kuangalia matumizi ya hela ambazo ni hela ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuwapongeza Serikali na mpango wa Tanzania wa Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa unapoongelea viwanda unahitaji infrastructure iliyokamilika ambazo ni umeme wa kutosha na barabara ya kupitika kwa urahisi ambazo tunaipongeza Serikali kwa kuliona hilo na mnalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ya sasa hivi ni dunia ya processing, ni vizuri Serikali iweke utaratibu mzuri kwa wawekezaji wa ndani na wa nje, wakubwa na wadogo wa kuweza kuanzisha viwanda kwa urahisi ikiwezekana kuwe na one stop centre ya kumaliza taratibu zote za leseni na vibali mbalimbali. Vilevile Mheshimiwa Waziri lazima akae na taasisi zake na wawe na speed ya kuweka Mazingira mazuri kwa yeyote anayetaka kuweka kiwanda especially vya processing (processing Industry), napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri akija kwenye majumuisho ni vizuri awaeleze na kuwaelimisha Wabunge kwamba viwanda vya zamani huwezi kuvifungua, Hata mashine zilizopo sidhani kama zina vipuri vyake maana yake ni teknolojia ya zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha viwanda vya zamani vinapatiwa Wawekezaji ambao wataleta mitambo ya kisasa na kuanza upya. Hatuwezi kujadili yote haya kuhusu Viwanda bila umeme wa uhakika. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri awe na angalau taarifa za juu ni lini gesi yetu itakuwa tayari kuanza kutumika na kutoa umeme mwingi ambao utavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba pia Waziri aje atoe ufafanuzi kwa Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali haifanyi Biashara na Serikali haijengi Viwanda, kinachofanywa na Serikali ni kuweka mazingira mazuri kwa Wawekezaji wa aina yote kuweza kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa kuwa wabunge wengi wanasimama na kuomba Serikali iwajengee Viwanda nadhani wakieleweshwa nia ya Serikali wataweza kuwa katika mstari mmoja wa kauli yetu ya Tanzania ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. OMAR A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mungu kutuamsha salama. Na mimi naomba nitoe ushauri wangu kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Lukuvi kwa maamuzi yake mazito ya kubomoa lile ghorofa kubwa pale mjini, ila napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri asiishie hapo, azidi kupambana kwa kuwa majengo ambayo hayana ubora yatakuwa mengi sana, hivyo katika kuokoa maisha ya watu, napenda kuhimiza wataalam wetu wasikae ofisini, waende site na kukagua kila hatua ya ujenzi inayojengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri kuangalia watumishi wake kwa karibu zaidi ili kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua kwa kiwango kikubwa. Malalamiko ya ardhi yanasababishwa na watumishi wa Wizara ya Ardhi kwa uuzaji holela maeneo ya wazi, utoaji wa hati mara mbili mbili ambayo siyo ya kujengea. Tukirekebisha hili, hali hii ya migogoro mijini na vijijini itakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, nadhani wengi hawana elimu ya sheria especially wafugaji. Utakuta mfugaji mmoja ana ng‟ombe 5,000. Kwa idadi hii lazima atagombana na wakulima kwa kuwa eneo lake haliwezi kumtosha. Elimu ya sheria ya kuwa na idadi ya mifugo inatakiwa itolewe sana na isimamiwe kwa makini na kwa ukaribu. Pia wafugaji wapewe elimu ya kupanda nyasi, ikiwezekana Serikali ianze kwa mashamba ya mfano. Hii itapunguza kasi ya wafugaji kuhamahama kwa kutafuta malisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri na watumishi wake, nyumba nyingi zinazojengwa mijini hazifuati sheria ya parking, ni vizuri sheria kali ikatipitishwa kwa yeyote asiyefuata kanuni ya ujenzi mijini. Pia napenda kuishauri NHC kuangalia upya mpango wa kodi zao na hili linaweza kurekebishika kwa kupunguza kodi na linawezakana kama watasimamia vizuri ukusanyaji wa kodi za sasa hasa katika taasisi kubwa ambazo zinaongoza kwa kutolipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jedwali Na. 2 page ya 83, marejesho ya asilimia 30 ya makusanyo ya Halmashauri kwenye mkoa wa Tanga kuna Handeni tu; na sasa kuna majimbo mawili; Handeni Mjini na Handeni Vijijini. Naomba unisaidie ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutufikisha
salama katika Bunge hili. Pia niwape pole wafiwa na majeruhi
wa ajali, pia naipongeza Serikali kwa maamuzi yake ya
kuhamia Dodoma. Pamoja na juhudi zake za Kasi katika
kuinua uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumedhamiria
kuwa na Tanzania ya viwanda, ni vyema sasa Serikali ikajikita
kwa kina katika kuhakikisha kuwa umeme wa kutosha
unapatikana ili tuweze kuendesha viwanda vyetu especially
kwenye umeme wa gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali
kujitahidi kutatua changamoto ambazo zinagusa kwa kiasi
kikubwa wananchi, mfano maji, afya na elimu, hii itasaidia
kwa kiasi kikubwa kunyanyua jamii yetu na kuifanya jamii
yetu ishiriki vyema kwenye maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la maji pamoja
na jitihada kubwa za Serikali kuhakikisha tunapata maji safi
na salama, bado kuna changamoto kwa upande wa
watendaji hususan katika maeneo ya vijijini. Hii inatokana
na utendaji wa mazoea kwa wataalam wa Idara husika.
Mfano unakuta Mhandisi wa Maji amekaa eneo moja kwa
zaidi ya miaka kumi na pamoja na kukaa miaka yote hiyo
tatizo la maji bado lipo palepale pamoja na kulipwa
mshahara na mahitaji mengine.
Nashauri kuwe na uhamisho kwa watendaji ambao
wamekaa sehemu moja kwa muda mrefu na pia ni vizuri
wakaangaliwa performance yao kila mara ili kuona ni jinsi
gani wanafanya kazi ya kutatua kero hii ambayo inagusa
kila jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Elimu; ni vizuri
Serikali ikatoa mwelekeo mzuri kwa Halmashauri ni jinsi gani
wanasaidiwa na wananchi katika ujenzi wa madarasa
mfano kuna mkanganyiko kati ya Halmashauri na wananchi.
Tunaambiwa kama wananchi tujenge boma na Halmashauri
itaezeka juu. kuna maboma mengi yameshajengwa na
wananchi lakini bado Halmashauri zinasuasua katika
mpango wao wa kumalizia juu na ukizingatia idadi ya
wanafunzi inaongezeka kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya,
pamoja na jitihada, kubwa kuhakikisha huduma ya afya
inaimarika, bado kuna changamoto kwenye ununuaji wa
dawa na upungufu wa Madaktari. Nashauri Serikali ihakikishe
MSD wanapata dawa ya kutosha ili kuepuka kuonekana
kulemewa na order kwenye hospitali zetu au kuweka
utaratibu wa kuziwezesha hospitali kununua dawa maeneo
mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa
Madaktari na Wauguzi ni kubwa sana na lipo nchi mzima.
Ningependa kuiomba Serikali ifanye haraka kulishughulikia
suala hili, mfano katika jimbo langu, kuna upungufu wa karibia asilimia ishirini ya Madaktari na Wauguzi na ukizingatia hospitali yetu inahudumia majimbo manne. Upungufu huu, unasababisha vifo vya mara kwa mara kutokana na kuchelewa kuhudumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kuipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuyaondoa maduka yote ya watu binafsi (ya dawa) ila iharakishe kuhakikisha maduka ya Serikali yanaanzishwa haraka.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's