Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Deogratias Francis Ngalawa

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukupongeza kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Naitwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kukishukuru Chama cha Mapinduzi kwa namna kilivyoiandaa Ilani yake. Ilani yake ni Ilani nzuri ambayo imetengeneza mpango mzuri wa mwelekeo wa Taifa ambako linatakiwa kwenda. Katika chaguzi zetu tuliinadi Ilani na wananchi wakatuchagua. Kwa hiyo, napenda kukipongeza chama. Hawa wanaotoka sasa ni kwa sababu hoja zao nyingi zinapwaya, hawana kitu cha kukizungumzia zaidi ya kutengeneza vijembe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda kujikita katika hotuba ya Mheshimiwa Rais moja kwa moja. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake katika ukurasa wa 12 ameizungumzia reli toka Mtwara – Songea – Mbamba Bay mpaka Liganga. Mimi napenda kumshukuru kwa hilo na tulipokuwa tunaizungumzia hiyo reli ya kutoka Mtwara mpaka Liganga ni kwa maana tunazungumzia suala la makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma – Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma – Liganga limekuwa ni suala la muda mrefu. Nadhani sasa ni kipindi cha miaka 50 limekuwa likizungumziwa na halina utekelezaji wowote. Nimshukuru Waziri Profesa Muhongo, tarehe 4 na 5 alifika kwenye makaa ya mawe Mchuchuma na vilevile alifika pale chuma – Liganga; alijionea type ya wawekezaji ambao tunao na namna gani wanaweza wakaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisikitike, wana wa Ludewa wana masikitiko makubwa. Wameachia ardhi yao miaka ipatayo 10, ardhi ile haitumiki, hawaitumii kwa maana yao na hakuna utaratibu wowote wa matumaini wa kulipwa fidia katika maeneo ambayo wao wameyaachia.
Sasa nipende kuliambia Bunge lako, wananchi wanataka fidia ya maeneo waliyoyaacha na kibaya zaidi hata ule mpango wa kimkakati wa huyu mwekezaji bado hauonekani!
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Waziri Muhongo tarehe 5 Mchuchuma, pale Nkoma Ng‟ombe na vilevile tulikuwa Liganga pale Mndindi; Serikali imekuwa ikiwakilishwa na NDC na wawekezaji ni Wachina, lakini katika majadiliano na maongezi yao wana contradiction kubwa. Ile miradi ni mikubwa, kuna mamilioni ya tani za makaa ya mawe, leo nchi inazungumza kwamba haina umeme! Lakini tunaamini mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma ukianza umeme katika Taifa hili inaweza ikawa ni historia.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme utakaozalishwa Liganga una uwezo wa ku-supply ndani ya nchi hii katika miaka isiyopungua 150, lakini leo Taifa bado halijachukua hatua madhubuti. Ni miaka mingi, sisi wengine toka tunasoma, kabla hatujazaliwa tunaambiwa kuna makaa ya mawe – Mchuchuma, tunaambiwa kuna chuma – Liganga! Mwekezaji aliyepo ameonesha incompetence kubwa mbele ya Waziri Profesa Muhongo! Hakuna maandalizi ya kutosha ya hiyo miradi kuanza!
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nipende tu kushukuru na kumshukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini, aliwaeleza wananchi wetu ukweli kwamba Taifa tunapoamua kuingia mikataba hii iwe ni ya wazi na kusiwepo na uficho wowote.
Mimi ninaamini Waziri usingekuja Ludewa, usingekuja pale Nkoma Ng‟ombe – Mchuchuma, usingekuja Liganga bado wananchi wetu wangekuwa wanaendelea tu kudanganywa danganywa na tusingejua fate yoyote ambayo inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nipende kuchukua fursa hii kwamba, tupate wawekezaji ambao ni serious. Tupate wawekezaji ambao wana uhakika, ili mwisho wa siku watu wetu tuwajengee matumaini, ili nchi iweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukizungumza sana Bungeni kwa nini nchi haiendi, wakati tuna madini ya kutosha, tuna mazao ya kutosha, lakini hatuchukui hatua. Huyu mwekezaji amekuwa akikumbatiwa! Haoneshi dalili yoyote ya namna gani tunaweza kwenda! Fidia hataki kulipa, anaulizwa kama hizo hela anazo anasema hela hana anasubiri kukopa nje ya nchi! What type of mwekezaji is? Sasa investor wa namna hii kweli tunakaa na kumkumbatia namna hii? Mimi nadhani siyo sawa! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Ludewa wanaisubiria Liganga ianze mara moja kwa sababu, imeshakuwa ni hadithi za muda mrefu. Liganga aanze, Mchuchuma aanze, tuachane na hii biashara kwamba hatuna umeme, hatuna umeme, hatuna umeme! Hii inatakiwa kubaki kuwa ni historia. Lakini mimi ninamuamini Waziri Muhongo atalishughulikia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna barabara ya Itoni – Njombe kuelekea Manda; barabara hii Mheshimiwa Rais ameahidi kwamba iwekwe lami, lakini nashukuru TANROADS juzi imetangaza kipande cha kilometa 50 kutoka Lusitu kuelekea Mawengi kwamba kitawekwa lami. Kwa hiyo, tunaomba hili lizingatiwe na lifanyiwe kazi haraka vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna barabara kutoka Mkiu kwenda Madaba na yenyewe Mheshimiwa Rais ameizungumzia kwa kiwango cha lami. Tunaomba lami hiyo iwekwe na wananchi wana matumaini, wana mazao yao mashambani, ila usafiri umekuwa ni shida, pindi hizi lami zikiwa tayari naamini kabisa mazao yatafika kwenye maeneo ya masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna suala la miundombinu ya mawasiliano ya simu. Leo hii Tarafa nzima ya Mwambao, Ukisi kule Ziwa Nyasa tunapakana na Malawi, vijiji 15 havina mawasiliano ya simu kabisa! Sasa sijajua Serikali inajipangaje na inawaonaje hawa watu? Hawa watu wako mpakani! Huku tunapakana na Kyela na Dkt. Mwakyembe! Huku tunapakana na Nyasa na Engineer Manyanya! Hapa katikati pamekuwa hamna mawasiliano ya aina yoyote! Wananchi wale wameniambia wataanza wao kutafuta hayo mawasiliano. Hatuna mawasiliano ya barabara, hatuna mawasiliano ya simu! Kwenye upande wa barabara wanasema wao wataanza na jembe la mkono. Na ninaiomba Serikali sasa ituunge mkono, ili tuweze kuviunganisha hivi vijiji na waonekane na wao wapo ni sehemu ya nchi hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiahidiwa muda mrefu juu ya daraja la Mto Ruhuhu unaounganisha Wilaya ya Ludewa na Wilaya ya Nyasa. Wananchi wanapata shida na kivuko kile na kivuko kimekuwa hakifanyi kazi. Dada yangu Injinia Manyanya unalifahamu hilo. Tunaomba Serikali ilichukue hilo na ilifanyie kazi, ili mwisho wa siku tuweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mambo mengi sisi wana wa Ludewa. Mheshimiwa Rais alipokuja Ludewa alitoa ahadi ya kipande kidogo cha lami cha kilometa 25 kutoka Ludewa mpaka Lupingu. Kwa hiyo, tungeomba ahadi hizo zitekelezwe.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda wako umeisha!
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabla ya yote nipende tu kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nipende kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, pia na watendaji wote na viongozi wakuu wa taasisi ambazo zipo chini ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha kwanza ambacho pengine ningependa kuchangia leo ni juu ya mtandao wa mawasiliano ya simu. Ikumbukwe kando kando ya Ziwa Nyasa yaani Ziwa Nyasa lilivyo eneo kubwa ni eneo la Ludewa. Upande wa Nyasa kama Wilaya lina urefu wa kilometa 112 na upande wa Kyela lina urefu kama kilometa 10; lakini sisi Wana-Ludewa tuna kilometa zipatazo kama 220, cha kushangaza na cha kusikitisha, mpaka hivi ninavyoongea kando kando mwa Ziwa Nyasa tuna tarafa moja na tuna kata sita, hakuna kijiji wala Kata ambako kuna mawasiliano ya simu. Ikumbukwe kwamba eneo lile la ziwa lipo mpakani mwa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, enzi zile sisi tukiwa watoto, yule bwana mkubwa akija unakuta kuna Sub Marine imesimama juu, wazee wetu walikuwa wanakimbia wanajifungia kwenye mahandaki, lakini mahandaki hayo sasa hivi hayapo. Kwa hiyo, eneo hili hata kama ni kutoa taarifa za kiulinzi na kiusalama tunashindwa. Kwa hiyo, nipende tu kumuomba Mheshimiwa Waziri alipe kipaumbele cha juu lile eneo kwa sababu ni eneo kubwa, kwa sababu ukiangalia ni kama vile tumetengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nyasa yenye kilometa 112 vijiji vyake vyote vinamtandao wa mawasiliano, Kyela yenye kilometa kama 10 vijiji vyake vyote vina mtandao wa mawasiliano. Lakini unapoanza mipaka, beacons za Ludewa hakuna kijiji hata kimoja; vijiji 15, tukiweka kata sita vinakuwa vijiji 18 kata sita hakuna kijiji wala kata ambayo ina mawasiliano ya simu. Kwenye hili tunajiona kama ni wakiwa na kama vile tumetengwa. Ukija pia kwenye eneo hilo hilo la barabara yaani barabara zimeishia Nyasa na Kyela. Eneo la Ludewa halina kabisa. Tuna vijiji 15 ambavyo havijawahi kufika hata baiskeli, wananchi wameamua kuchimba wenyewe kwa mkono. Kwa hiyo, tunaiomba sasa Serikali ije iwaunge mkono wananchi wale ili waweze kupata barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii hata nikizungumzia suala la road upgrading Ludewa imeachwa kabisa. Kuna upgrading Makete kama mkoa, kuna upgrading Makambako, Wanging’ombe na Njombe lakini Ludewa imeachwa. Sasa huwa tunashindwa kujua Ludewa ina matatizo gani mpaka tusi-upgrade barabara hata moja? Mimi nipende kutoa masikitiko ya Wana-Ludewa kwa sababu inakuwa sio jambo jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ndani ya mkoa yanafanyia road opening, paving way, lakini eneo la Ziwa Nyasa ambalo lipo mpakani mwa nchi; hata kipindi kile wakati wale jamaa wanakuja kuja na ule mtafaruku tukawa tunashindwa wapi pa kwenda, barabara sehemu ya kukimbilia hatuna, mawasiliano kusema kwamba tutatoa taarifa kwenye vyombo vya usalama hakuna. Sasa nipende tu kujua labla pengine Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha utatuambia inawezekana Ludewa ina makosa ambayo imeifanya ndani ya Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja upande wa bandari. Tunaishukuru Serikali kwa zile meli tatu, meli mbili za mizigo na meli moja ya abiria. Vilevile kuna ujenzi wa gati ndani ya Ziwa Nyasa bado tunakuja kuona hapo hapo, upande wa Wilaya ya Nyasa kuna gati zinajengwa na kwenye bajeti mmeweka, upande wa Kyela kuna gati zinajengwa lakini ni upande wa Ludewa tu pekee yake ndiko hakuna gati.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunakuja tunajiuliza maswali mengi sana, Ludewa ina tatizo gani na nchi hii? Kyela wanawekewa gati, Nyasa inawekewa gati. Halafu mahali huku ndiko ambako tunasema leo tuna uchumi wa viwanda. Tunapozungumzia uchumi wa viwanda huwezi ukaisahau Liganga na Mchuchuma. Liganga na Mchuchuma inakuja lakini miundombinu hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu angalia upande wa barabara; tunashukuru barabara ya Itoni - Njombe - Manda - Ludewa, mkandarasi yupo, ipo kwenye mobilization finalization, lakini kuna zile barabara ambazo ndio zinakwenda kwenye ile miradi, kuna barabara ya Mkiu kuelekea Madaba.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunaambiwa inafanyia rehabilitation, lakini mimi nilikuwa najua tungeiweka sasa kwenye upembuzi yakinifu baadae iende kwenye usanifu wa kina ili twende kwenye lami, kwa sababu barabara hii ndiyo inayoelekea kwenye mradi mkubwa wa Liganga. Kwa sababu utakuta sasa miundombinu Ludewa ni miundombinu ya kizamani na hakuna consideration ambayo inafanyika kwa ujio wa miradi mikubwa kama ya Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unaponiambia kwamba kuna flagship project za Liganga na Mchuchuma; na ndiyo maana huwa tunauliza, hii Liganga na Mchuchuma itaanza lini? Maana tungeweza kupewa schedule kwamba mwaka huu mpaka mwaka huu kuna hiki kuna fidia inafanyika, mwaka huu mpaka mwaka huu kuna hiki kinafanyika then baada ya hapo tunajua sasa mradi una- takeoff. Kwa inawezekana tunaona kwamba hata hii miundombinu inakuwa haiwekwi kwa sababu hata huo mradi wenyewe haufahamiki utaanza lini? Kama ungekuwa unafahamika utaanza lini mimi ni naamini kwamba hizi barabara zingeanzwa kutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababau Nchi inavyoelekea kwenye viwanda mnakitegema chuma cha Liganga, Nchi inavyoelekea kwenye viwanda mnakitegemea umeme utakaozalishwa Mchuchuma, megawati 600; lakini kwa nini leo hatuweki hiyo miundombinu?. Wenzetu wote ambao wako ndani ya Mkoa kuna activities zinafanyika lakini ni Ludewa tu. Ukija gati inafanyika Nyasa na Kyela; Ludewa inaacha, ukija mawasiliano ya simu kuna Nyasa na Kyela; Ludewa inaachwa. Ukija barabara zinaishia kwenye beacon ya Kyela na huku inaishia kwenye beacon ya Nyasa lakini Ludewa inaachwa. Sasa lazima tujiulize panashida gani na Ludewa?

T A A R I F A...

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Hiyo taarifa siipokei, kwa sababu haiwezekani watu wengine wanapewa fursa wengine hawapewi halafu uniambie kwamba… tena unanifundisha hata namna ya kusema, haiwezekani, tunazungumza vitu vilivyo-live. Mimi bajeti ninayo kila kitu kipo humu wakati mwingine mnaaweza mkaenda mbali labda kwingine labda pengine huku kwa sababu kuna Mawaziri na Ludewa hayupo Waziri, ndiyo mnataka kuniambia hicho, kwa nini Ludewa isipewe? Hiyo ndio hoja yangu mimi ya msingi

T A A R I F A...

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo taarifa siipokei. Mimi naongea kwa niaba ya wananchi wa Ludewa na wananchi wa hii. (Makofi)

Kwa hiyo, kama sehemu kipo na wakati huo mahitaji yetu yanalingana naona ni kama tunabaguliwa. Kwa sababu katika eneo la Ziwa Nyasa sisi ndio wenye eneo kubwa kuliko Nyasa, kuliko Kyela, sasa kule kuna kitu gani kikubwa ambacho hiyo miundombinu inapewa kipaumbele kuliko huku kwingine, kwa nini? Maana ukiniambia unajenga chuo lakini barabara hamna chuo hicho kitakuwa hakina maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lazima ifike mahali kwamba hizi fursa lazima tupewe wote sawa. Kama ni chuo hata Nyasa kinajengwa, kipo kwenye programu, kwa hiyo, maana yake utakuwa una barabara, una gati na hicho chuo kitakuja. Ndiyo maana tunazungumza hapa Ludewa ina tatizo gani? Kama ni uvuvi, uvuvi mkubwa unafanyika Ludewa kuliko Nyasa na Kyela, wao wanajua, sisi ndio mabingwa wa kuvua, mabingwa wakuvua ni Wakisi kuliko Wamatengo, kuliko Wanyakuysa, sisi ndio tunaowafundisha, tumeenea kwenye mabwawa yote ya Tanzania. Ndiyo maana tunazungumza, kwa nini hatupewi kipaumbele? (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Marehemu Deo Filikunjombe, Mungu amuweke mahali pema, amekuja hapa, amezungumza sana juu ya haya mambo; kapita kaenda. Ndiyo kwa maana sisi tunasema kwamba tunakosa gani? Licha ya kwamba tumekuwa tukiwasiliana na Waheshimiwa Mawaziri juu ya masuala haya. Si kwamba ni mara yangu ya kwanza mimi kuzungumza hapa Bungeni, nimezungumza sana na Mheshimiwa Mbarawa, ni mezungumza sana tu na Mheshimiwa Ngonyani, na inafikia kipindi hata Katibu Mkuu nimejaribu kuwa nampigia simu amekuwa hapokei, na mpaka nikajitambulisha naitwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa still yet hapokei! Inawezekana Ludewa kuna matatizo. Ndiyo maana tunazungumza hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama ni suala la fursa basi tupewe fursa sawa. Leo hii Ludewa barabara hazipitiki, hii barabara tunayozungumza ya Mkiu – Madaba imekata, watu wanakaa siku mbili njiani why, wakati wenzetu wanapeta? Vijiji havijawahi kufika baiskeli hata siku moja, pikipiki haijawahi kufika vijiji 15. Wananchi wameamua wenyewe kuchimba, kwa nini Serikali isije? (Makofi)

Tumeamua wenyewe clips za wananchi kuchimba Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri niliwaonesha kwamba tumeamua kuchimba wenyewe kwa majembe kwa nyundo kwa mitalimbo. Leo hii tunapokuja kuzungumza unasema tusilinganishe, tusilinganishe kwa base ipi? Ifike mahali fursa lazima tupewe sawa, mimi langu ilikuwa ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

HE. DEOGRATIAS F. NGALAWA …kufikisha ujumbe huo na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwanza kwa kupata nafasi ya kuweza angalau kujadili hotuba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Kwanza kabisa napenda kutoa kilio changu cha wana wa Ludewa, kwa sababu Ludewa sasa inaonekana ni eneo ambalo limesahaulika kwenye mambo mengi. Hivi ninavyoongea sasa, Jimbo la Ludewa lina uhaba wa Walimu 496, tuna shule 108; katika shule hizo 108 ni shule saba tu ndizo ambazo zina Walimu wanaoweza kukidhi. Shule nyingine zote 101 zina Walimu wanne kushuka chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule ambayo ina Walimu wawili na shule zilizo nyingi zina Walimu watatu. Kwa hiyo, cha kwanza napenda tu kutoa masikito yangu kwamba tuna uhaba wa Walimu 496 na bahati mbaya kabisa katika kipindi hiki mmetupatia Walimu 30. Hata hivyo kuna Walimu 25 ambao wanastaafu Septemba na kupelekea uhaba wa Walimu 521.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuwasiliana na TAMISEMI, sasa napenda kutoa kilio hiki kwako Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe ndiye msimamizi wa elimu Tanzania. Kwa hiyo, naomba tu mwisho wa siku nikuletee majina kwa watu ambao wanataka kwenda kufundisha Ludewa na ikiwezekana basi mfanye utaratibu mtuletee Walimu. Kwa kweli hali ni ngumu na ndiyo maana nimeamua nije nizungumze katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hata vyuo vyetu vikuu havipeleki wanafunzi kwenda kufanya field kule, kwa sababu ya miundombinu mibovu ya barabara na miundombini mibovu ya mashule yetu, kiasi ambacho kimepelekea hata wanafunzi wenyewe wanaotoka kule kuomba msaada huo. Kwa hiyo, naomba nikuwasilishie hilo na hasa Chuo Kikuu cha Dodoma, kwamba hawawezi kupeleka Ludewa, lakini maeneo mengine yote ya Tanzania wanafunzi wanaweza kwenda kufanya field. Hii inapelekea shule zetu za Ludewa kuwa na pass ya chini kabisa na vijana wetu wengi kufeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda ku-declare interest, mimi ni mmiliki wa shule. Nianze na ada elekezi. Nadhani shule hizi za binafsi ndiyo zinazoleta fundisho kwa Serikali yetu kwamba ni namna gani shule zinapaswa ziwe na ninadhani zimeshaweka standard ya kuweza ku-move. Kwa hiyo, sababu ya kuweka ada elekezi, siyo za msingi na wala hazifai. Ninajiuliza swali, tusingekuwa na shule za private, watoto tulikuwa tunapeleka Kenya na Uganda. Je, kule Uganda tungeweza kupeleka hizo ada elekezi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suppose huku tungekuwa hatuna na kipindi kile kabla ya St. Marys kuanza, watoto tulikuwa tunapeleka Kenya. Kwa hiyo, kosa letu ni kuboresha elimu, kutengeza miundombinu mizuri, mpaka inapelekea kuwa tunaongoza kwa hamsini bora. Hilo ndiyo kosa ambalo Serikali imeliona. Nadhani Serikali ingeshukuru, kwa sababu ninaamini kabisa wanafunzi wengi ambao wanang‟ara ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, ni wale ambao wanatoka private school, wanatuwakilisha. Kwa hiyo, tungewatengenezea miundombinu mizuri, ikiwezekana hata kuchukua mishahara mlipe nyie Serikali, kwa sababu watoto wanaofundishwa ni watoto wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sababu zile za msingi kupelekea kuweka hizo ada elekezi hamna. Kwa sababu usi-justify makosa unayoyafanya, usi-justify kutokuweka jitihada zozote ili uweze ku-capitalize kwenye shule za binafsi. Play your part, fanya shughuli zako, ninaamini ukitengeneza miundombinu mizuri, ukiwa na Walimu wa kutosha, hakuna mtu atakayeenda kwenye shule zenye gharama kubwa. Kwa hiyo, isifike kipindi Serikali inashindwa kufanya wajibu wake, kwa madai tu iende ika-suppress kwenye hizi shule za binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi ziachwe ziendelee, kwa sababu yale mazingira yaliyowekwa vizuri, wamiliki wa shule wengi wamekopa mikopo, wana madeni yenye riba kubwa. Kwa hiyo, maana yake utakaposema unatoa ada elekezi, tutashindwa kulipa yale madeni na mwisho wa siku sasa wakati huku tayari shule za private zimeshakaa vizuri, tunabomoa wakati huku kwetu kwenye government schools hatujaparekebisha bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya ujenzi wa Shule ya VETA Shaurimoyo, katika Jimbo la Ludewa. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hajaiweka kabisa. Shule hii ya VETA kimsingi ilikuwa inaanzishwa pale kwa ajili ya kupokea miradi mikubwa miwili ya makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga, kuwaandaa vijana kwenye shughuli za kiufundi ili kuweza kushiriki katika hiyo miradi inayokuja. Nakumbuka mwaka 2012; kama siyo 2012, ni mwaka 2013, Serikali iliji-commit kwamba itajenga chuo hiki. Naamini sababu zile zile za kukitaka kukijenga hazijatoweka, sababu hizo zipo. Mlipeleka wataalam, ardhi imepimwa, hati mmepata, michoro mnayo, BOQs zote mnazo na mlisema mlishatenga hela kwa ajili ya kujenga hicho Chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza tena swali hili, Chuo hicho kwanini kimeachwa? Matokeo yake, vile ambavyo wala havikuwepo katika kipindi hicho cha miaka miwili, mitatu iliyopita, leo ndiyo vimewekwa. Sasa watu wa Ludewa wanajiuliza maswali ya msingi, pana tatizo gani? Kwanini kisijengwe na kwanini hakuweka kwenye program yake? Kwenye hili Mheshimiwa Waziri hatutakubali kwa sababu kinachoonekana ni kuibagua Ludewa na Ludewa haitaweza kubaguliwa kwa sababu na yenyewe ipo katika nchi ya Tanzania.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja lakini tunaomba Chuo Ludewa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuzungumza na kuchangia hoja ya Wizara ya Viwanda. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwa kishindo na Mawaziri wote kwa namna nzuri wanavyofanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu inajikita zaidi kwenye maeneo ya biashara. Hoja ya nchi kutaka kwenda kwenye viwanda ni nzuri, lakini kitu ambacho nakuwa na wasiwasi nacho ni namna ya utekelezaji wa hoja zetu. Ninavyojua, suala la viwanda ni mtambuka, sasa sijajua kwamba Serikali imejiandaaje katika kuhakikisha kwamba inawaandaa Watanzania katika mapokeo hayo. Ki-mind set Watanzania bado hawajawa tayari kwenye hilo, hivyo wanahitaji training ya namna gani ya kuweza kuipokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunapozungumza, tuna wafanyabiashara wengi sana ambao wako informal na kundi hili la wafanyabiashara ni kubwa. Asilimia 70 ya wafanyabiashara wote wa Tanzania wako kwenye kundi ambalo ni la informal. Kwa hiyo, bado Serikali haijafanya mchakato mzuri wa kuhakikisha kwamba tunawaandaa wafanyabiashara wetu ili mwisho wa siku waweze ku-formalise biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini hizi biashara ziko informal? Ziko informal kwa sababu sheria haziko friendly. Tuna kundi kubwa la wafanyabiashara ambao wanashindwa ku-formalize biashara zao kwa sababu ya usajili; namna ya kuzisajili zile biashara inakuwa ni ngumu; na namna ya kupata leseni inakuwa ni ngumu. Leo hii tunaambiwa TIN number ni bure lakini ukijaribu kuangalia na kwenda, kupata hizo TIN number kwa ajili ya kufanyia hizo biashara, zile TIN number zina usumbufu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unaambiwa, unapotaka kuanza kufanya biashara zako ni lazima kwanza utoe kiwango fulani cha hela hata kabla hiyo biashara hujaifanya. Sasa lile linawasumbua sana wafanyabiashara wetu mpaka inafikia kipindi kwamba anaamua acha afanye biashara kiholela, Serikali inakosa kodi na watu wanaweza wakafanya biashara nje ya mfumo sahihi. Nadhani umefika wakati sasa tuendeshe training na ikiwezekana hawa watu wetu tuwatengenezee namna ya kujua fursa za biashara zilizopo na ikiwezekana tupate elimu nzuri ya namna hawa watu wetu watafanya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la elimu ya ujasiriamali na fursa za biashara bado tuko nyuma. Kuna fursa nyingi ambazo vijana wetu na watu wetu wanazo na wanatakiwa kuzifanya, lakini hawajawa exposed. Nadhani ifike wakati sasa Serikali ifanye hatua za makusudi kuendesha training kwenye vijiji, kwenye mitaa, ili mwisho wa siku watu wajue ni vitu gani wanaweza kufanya. Kwa sababu fursa zipo zinawazunguka, lakini watu hawajui wafanye nini na mbinu gani watumie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna Maafisa Biashara kwenye Manispaa zetu, kuna Maafisa Biashara kwenye Halmashauri zetu, lakini tukijaribu kuwauliza Mpango Kazi wao ni upi? Walio wengi wala hawajui. Waulize Maafisa Biashara kwenye Halmashauri zetu, kuna wafanyabiashara wangapi ndani ya Halmashauri? Hawezi kukupa takwimu. Kwa hiyo, hili nalo ni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ifike mahali Serikali lazima itambue ina wafanyabiashara wangapi? Hata tunapozungumza kwamba kuna mfumo ule PPP maana yake nini? Kwa sababu kuna watu wengine hawajui. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo, maana yake kwanza tutawatambua wafanyabiashara na mwisho wa siku ni kwamba hata unapoamua kupanga kodi, unapanga kodi kwa watu ambao unawafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la viwanda. Kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 52, umezungumzia mradi wa kasi mpya wa kuzalisha chuma ghafi. Mara nyingi huwa napata shida, pale unapozunguza kwamba utatekelezwa halafu usiseme utatekelezwa lini.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ndiyo tupo kwenye bajeti ya kwanza ya utekelezaji wa miaka mitano kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Naamini unapozungumza mradi, lazima uwe na mahali pa kuanzia na mahali ambapo panatakiwa kuishia. Kwa sababu ukiileta statement too general unakuwa hujatupa tool ya sisi kuku-assess wewe, kwa sababu hata mwakani tukija, utasema hivi hivi, kwamba mradi huu utatekelezwa na Kampuni ya Maganga Matitu Resources Development. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ifike mahali sasa unapozungumza mradi, hata kama utataka kuutekeleza mwaka 2018, mentioned, kwamba mradi huu utatekelezwa muda fulani na unatarajia labda kwisha muda fulani, hivyo tutakwenda vizuri. Kitu chochote unachokiita ni project lazima kiwe na mwanzo na lazima kiwe na mwisho. That is a project. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini statement zisiwe too general. Leo hii unasema unatekeleza mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma kuendeleza utekelezaji wa mradi unganishi wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga, kwenye ukurasa wako wa 161. Chuma cha Liganga tumeshaanza kukisikia toka 1906, kwa hiyo, ni kabla hatujazaliwa na inawezekana hata kabla babu zetu wengine hawajazaliwa. Kwa hiyo, ifike kipindi sasa Serikali iseme, wakati tunauliza swali hili kwenye Wizara ya Madini walituambia kwamba fidia itaanza kulipwa mwezi Juni, mwaka 2016 na mradi utaanza mwezi Machi, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa natarajia kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ange-mention hii kitu, kwamba mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga utaanza Machi, 2017 kama swali lilivyokuwa limejibiwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini ili tuwe tunakwenda kwa takwimu. Kwa sababu usipotoa takwimu na muda (time frame) maana yake hatutaweza kuku-assess na kuku- pin.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii Serikali tumeshazungumza kwamba ni Serikali ya viwanda na tunatarajia kwamba tutaenda kwa kasi kubwa. Natamani kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, aseme kinaga ubaga, kwamba tutaanza muda fulani ili tutakapokuja hapa mwakani tuwe na maswali ya kumuuliza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, hivi viwanda vya kimkakati kwa sababu ameshasema ni National Flagship Project, haitakiwi kuwa na majibu general. Leo hii watu hawajaandaliwa kwa maana hii miradi itahitaji support. Licha ya ukubwa wa hivi viwanda vinavyokuja kule, nilikuwa natarajia kwamba Mheshimiwa Waziri angesema, kwa sababu makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga inaanza, kutakuwa na vitu vya ku-support patakuwa na SIDO; hawa watu tuwaandalie uwezo wa kiufundi ili mwisho wa siku waweze kuji-engage kwenye zile bidhaa au kazi zitakazofanyika na hiyo miradi mikubwa inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunavyozungumza hakuna barabara ya lami inayoelekea huko. Wimbo huu umekuwa ukiimbwa muda mrefu na hata marehemu Mheshimiwa Deo Filikunjombe alikuwa akiizungumzia kwa kasi sana hii kitu. Mungu amlaze mahali pema peponi. Haijafanyiwa kitu chochote! Kwa hiyo, tuombe kwamba hivi vitu vingine lazima viwe na support ya sekta nyingine ili kuhakikisha kwamba hili gurudumu linakwenda. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuongea tena katika Bunge lako la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja zangu zinajikita katika maeneo machache sana kama mawili hivi au matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza kabisa ni juu ya flagship project, makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma Liganga. Kwa hiyo, tunapozungumza ni flagship project maana yake ni project ambazo zinatiliwa mkazo kwa kiasi kikubwa ili kuweza kuifanya nchi isonge mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, najikita kwanza kwenye fidia. Mradi hauwezi ukaanza kabla fidia haijalipwa na katika valuation ya ulipaji wa fidia, tunaona ripoti inasema wananchi wale wa Ludewa kwa maana ya Chuma na Liganga wanatakiwa walipwe shilingi bilioni 14. Hapo hapo nikijaribu kuangalia bajeti iliyokuwa imepangwa na Wizara hasa Wizara ya Viwanda inaonyesha ni shilingi bilioni 10.
Sasa nakuja kujiuliza swali la msingi, hii shilingi bilioni nne iko wapi? Kwa sababu katika majibu ya awali ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, pindi nilipokuwa nimeuliza swali tarehe 19 Aprili, tuliambiwa kwamba fidia inalipwa mwezi Juni, mwaka 2016. Kwa sasa tumebakiwa na muda mchache sana kuifikia Juni. Tumebakiwa na kama siku kumi au kumi na moja Juni hiyo ifike.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu tulishawaaminisha Wanaludewa kwamba tunalipa hiyo fidia na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri akasema miradi hiyo itaanza mwezi Machi, 2017, nikiwa namaanisha kwamba fidia hizo zitakuwa tayari zimeshalipwa, lakini bado napata utata mmoja, kwenye strategic plan. Kwa sababu naamini nilivyokuwa nimejibiwa kwamba hizi fidia zitalipwa mwezi Juni na mradi ule unaanza 2017 mwezi Machi, naamini kwamba ningeona kwenye ripoti. Ripoti ingesema kwamba mradi huu unaanza Machi, 2017 ili kutengeneza assurance. Tusipozungumza hivyo, bado mwakani tutakuja na hadithi hizi. Hatutaweza kum-pin Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu ni moja tu, tunapozungumzia project, project ina time frame. Kwa hiyo, mwisho wa siku ni lazima utueleze mkakati wako na namna utakavyoanza na maadam umeshatu-assure kwamba mwezi Juni, 2016 unalipa fidia, watu wa Liganga na Mchuchuma na Mradi unaanza mwezi Machi, 2017, kwa hiyo, ipo kwenye plan yako. Hiyo plan inapaswa na sisi tuifahamu. Bila hivyo, nasi inatupa matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Mchuchuma, kwa mujibu wa wataalam na Wizara unatarajia kutupa umeme wa megawatt 600, kwa maana ya hii Mchuchuma coal. Kwa hiyo, naamini kuna haja sasa ya kutengeneza nguvu ya kutosha, huu umeme tuufanyie kazi ili uweze kuongeza kwenye pato la nchi, ili twende kwenye uchumi wa viwanda ambao tunautaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachojua, kwenye flagship project kama hii, kuna maeneo mtambuka; kuna suala la VETA. Suala hili la VETA lilizungumzwa sana na hata kipindi hicho Hayati mtangulizi wangu, Marehemu Mheshimiwa Deo Filikunjombe, Mungu amweke mahali pema peponi, alilizungumza kwa kasi, aliliuliza ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano na majibu nakumbuka yalitolewa na Mheshimiwa Mhagama kwamba feasibility study ilishafanyika, michoro ilishakuwa tayari, hati ipo na inatakiwa kuanza kujengwa. Kwa maana ya kuwaandaa vijana kushiriki kwenye mazoezi maalum kwa maana ya kazi na mambo mengineyo ambayo yatakuwepo katika hiyo miradi ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijaribu kuangalia documents zetu ambazo sisi Wabunge tumepewa, hiki Chuo sasa hakipo kabisa. Kwa hiyo, inamaanisha kwamba hatuna maandalizi ya kutosha kwa sababu ile VETA ilivyokuwa imewekwa pale, ilikuwa ni kuwaandaa watu katika kazi za ufundi ili ku-support operations ambazo zinakwenda kufanyika ndani ya miradi hii mikubwa inayokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii shughuli ni mtambuka na inashirikisha vitu vingi, naiomba Wizara ya Madini, Viwanda na hata na Wizara ya Elimu ambayo inashughulika na mambo ya ufundi, tukae pamoja kuhakikisha kwamba miradi hii wakati inaanza, basi tuanze vile vile maandalizi ya ujenzi wa VETA. Kwa sababu ni kitu cha muhimu na bahati nzuri Bunge lako Tukufu lilishaelezwa kwamba kile chuo kitajengwa. Kama hakitajengwa, lazima tupewe sababu za msingi, zimeyeyukia wapi? Kwa nini hakijengwi? Kwa sababu tulishawaaminisha watu VETA ilishaenda mpaka Shaurimoyo kwa ajili ya kutayarisha eneo; eneo walipata limepimwa hati ipo, michoro ipo na BOQ zote zipo, kwa nini hiki chuo kisijengwe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo, kwa kweli tunapaswa tulifuatilie na madamu kwa sababu Serikali ilishasema na sababu za kujengwa zilikuwepo, naamini zile sababu hazijakwisha, bado zipo, kwa hiyo, kijengwe ili tuweze kutoa mafunzo kwa wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala la Maganga Matitu Resources. Suala hili la Maganga Matitu Resources, hawa wako kwenye partnership na NCD.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa katika mipango ya uanzaji wa miradi ya Mchuchuma wa makaa ya mawe na Liganga chuma. Wizara ya Nishati na Madini tarehe 19/4/2016 ilijibu kuwa fidia ya kulipa wananchi itafanywa mwezi Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe fidia hii ilipaswa kulipwa mwezi Februari 2016. Wizara ya Viwanda na Biashara imetenga sh. 5,000,000,000 Liganga na kwa Mchuchuma sh. 5,000,000,000 kiasi kilichopangwa ni sh. 10,000,000,000 ambacho ni kidogo ukilinganisha na fidia ya sh. 14,000,000,000. Naomba maelezo pesa nyingine ambazo ni pungufu zitapatikanaje ili ziweze kulipwa katika kipindi kifupi kilichobaki cha Juni, 2016.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mimi naomba moja
kwa moja nijikite kwenye Wizara ya Miundombinu. Ikumbukwe kuwa Wilaya yetu ya Ludewa,
eneo kubwa liko mpakani mwa Malawi. Tanzania imepakana na Malawi, lakini eneo kubwa la
mpaka ni eneo la Wilaya ya Ludewa, ukilinganisha na Wilaya za Kyela na Nyasa. Lakini mpaka
sasa ninavyozungumza, eneo lile halina mawasiliano ya barabara, katika eneo la tarafa ile ya
mwambao ambayo ina kata tano na vijiji 15 vilivyoongozana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuna kipindi palitokea mgogoro, sasa mimi nikawa
najiuliza maswali, hivi mgogoro ule ungeendelea wakati hatuna barabara ya uhakika hali
ingekuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kukwambia na niiambie na Wizara wananchi wale
kwa sababu ya kuchoshwa kwa kutokuwa na barabara wameamua kuanza kulima wenyewe
kwa kutumia jembe la mkono. Wanalima kwa sururu, wanalima kwa jembe, wanalima kwa
chepe na mitarimbo. Ile ni dhamira ya dhati kabisa kuionesha Serikali kwamba wale watu wana
uhitaji wa hicho kitu. Vile vijiji vyote tumepangana, tunalima kwa jembe la mkono. Sasa niiombe
Serikali iwa-support wale watu na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri niliwaonesha
hata clips za watu wakiwa wanalima kwa jembe la mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, usafiri mkubwa tunaoutegemea ni usafiri wa maboti, kwa
sababu meli inaweza ikapita mara moja kwa mwezi na isitoshe lile Ziwa huwa linachafuka sana,
kwa hiyo, inafikia kipindi usafiri unakosekana kabisa. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwamba sasa
ichukue hatua kwa sababu wenzetu wa Nyasa wanayo barabara inayopita kando kando ya
Ziwa; wenzetu wa Kyela, wanayo barabara inayopita kando kando ya Ziwa. Kwa hiyo,
tuwaombe sasa na sisi upande wa Ludewa tuwe na barabara ambayo inaunganisha, kwanza
itakuza utalii, halafu pili italeta maendeleo kwa sababu kuna mazao kule ya uvuvi ambayo
yanapatikana kwa wingi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia eneo lile halina mawasiliano ya simu kabisa. Mimi
ninaamini katika nchi nane tulizopakana nazo, eneo ambalo halina mtandao wa mawasiliano
ya simu inawezekana ikawa ni mwambao wa Ziwa Nyasa. Tuna kata tano, tuna vijiji 15 halafu
viko mpakani. Sasa cha kushangaza tumekuwa tukifatilia hii kitu sijajua tatizo liko wapi lakini
ningependa tu niseme watu wa Ludewa nao wangependa kuwa na maendeleo, wangependa
kuwa na mawasiliano ya simu maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu bandari. Pamoja na kuwa wakati mwingine
meli ile inatembea mara moja kwa mwezi, lakini bado bandari zake ziko kwenye umbali mrefu
sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nijaribu kujadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Moja kwa moja nijikite juu ya suala la Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Liganga na Mchuchuma ni suala ambalo hata tafiti zake zimefanyika toka mwaka 1929. Serikali imekuwa ikilizungumzia suala hili kwa miaka chungu nzima, lakini tulijaribu kupata faraja hasa sisi watu wa Ludewa pale tulipoambiwa kwamba miradi hii inaanza. Ikumbukwe katika Bunge lako Tukufu niliuliza swali tarehe 19/4 juu ya fidia kwa wale ambao wamepisha hii miradi kufanyika. Tulijibiwa kwamba Juni ndugu zetu wale wa Ludewa wangeweza kulipwa fidia yao na vilevile Bunge liliambiwa mradi ule ungeweza kuanza Machi, 2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ludewa waliaminishwa na sasa wanapiga kelele sana juu ya hili. Nipende tu kutoa taarifa katika Bunge lako kwamba hawa watu wanajiandaa kuja Dodoma kujua hatma yao. Vinginevyo waruhusiwe yale maeneo waliyopisha kwa sababu ni maeneo ya kilimo na ndiyo wanayoyategemea waendelee na kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango Mheshimiwa Waziri anazungumzia sana hili suala la Liganga na Mchuchuma, lakini jinsi ninavyoiona ni kwamba, hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa. Mpango unazungumza hapa kwamba mradi wa umeme wa megawatt 600 unaendelea, sasa najiuliza unaendelea wapi? Mimi sijaona kitu chochote kinachoendelea pale Mchuchuma. Hakuna kitu kama hicho! Labda Mheshimiwa Waziri aje atueleze na alithibitishie Taifa kwamba nini kinachoendelea kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa juu ya Power Purchase Agreement ndiyo inayosumbua, lakini mpaka sasa hatujui fate yake na mradi utaanza lini? Je, coordination ipoje kati ya Wizara na Wizara na kati ya Waziri na Waziri? Huyu anasema fidia italipwa Juni, sasa hivi tokea Juni ni miezi minne imeshapita hakuna fidia na wala hakuna tamko la Serikali linalosema kitu chochote juu ya fidia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapotuaminisha kwenye Bunge sisi tunaenda kuwaambia wananchi Serikali imesema moja, mbili, tatu, nne; sasa leo hii nikienda kule mimi ndiyo ninayeonekana mwongo! Sasa suala la mimi kuonekana mwongo haiwezekani, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje na tamko ili tulichukue na kulipeleka kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nijikite kwenye miundombinu. Leo hii tunasubiri suala la standard gauge kwa reli ya kati, tunaowategemea kuja kufanya hii kazi ni Wachina. Leo hii kitu kidogo kabisa cha Liganga na Mchuchuma tunakaa tukiyumbishana kwa suala la Power Purchase Agreement. Ninachofahamu mkataba huu siyo wa jana wala sio wa juzi, lazima kuwepo na continuity, walipoishia wenzetu sisi tuendelee. Kama pana tatizo basi tujue kwamba hili ni tatizo la msingi na tupeane maelekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tukiwafuatilia Mawaziri wetu hawana majibu na tunarushiana mpira. Ukienda kwa Waziri wa Madini anazungumza hivi, ukienda kwa Waziri wa Viwanda anazungumza hivi, ukienda kwa Waziri wa Fedha anazungumza hivi, inafika wakati tunakata tamaa juu ya suala hili. Waziri alikuja Mchuchuma Januari na alikuwa anazungumzia hili, sasa haya mazungumzo yanachukua muda gani, lazima tuwe na time frame! Ifike mahali tuseme itakapofika tarehe hii basi hii kazi iwe imekwisha, hapo tutakuwa tunaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya miundombinu. Kule kwetu Ludewa tumepakana na nchi ya Malawi, kuna eneo la kilometa zinazokadiriwa kuwa 200, eneo hilo halina miundombinu ya barabara hata moja na hilo ni eneo la mpakani. Nakumbuka juzi juzi hapa wenzetu walikuwa wana-demand lile ziwa na pakawa na kitu kama mgogoro. Sasa najiuliza, eneo la mpakani lenye urefu wa kilometa 200 halina miundombinu ya barabara, halina mawasiliano ya simu, hakuna umeme, je, likitokea la kutokea defense yetu ipoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kulieleza Bunge lako, wananchi kule wameamua kuchukua hatua kulima barabara kwa mikono. Tumeshalima kilometa 40 kwa jembe la mikono na sururu. Sasa kutokana na umuhimu wa eneo hilo kiulinzi na kiusalama na kiutalii Mheshimiwa Waziri aliweke kwenye mpango. Ziwa letu lina matatizo makubwa. Hivi ninavyozungumza wiki iliyopita watu watatu wamefariki kwa sababu ya usafiri na huwa linachafuka halitoi taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuchukua fursa hii kuomba Serikali iwasaidie wale watu ambao wameamua bila kulipwa kulima barabara kwa kutumia mikono yao. Eneo la Ziwa Nyasa, eneo kubwa ni eneo la Ludewa kuliko Kyela, Mbinga na Nyasa. Kwa hiyo ni lazima hawa watu tuwape kipaumbele. Tuna vijiji vinavyokadiriwa 20 hakuna mawasiliano ya simu kabisa yaani ukishazama huko umeshazama, taarifa zako huwezi kuzipata. Kwa hiyo, ifike kipindi watu hawa tuwaonee huruma na Serikali itu-support kwenye hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu, mpaka sasa Ludewa ina deficit ya Walimu 521 lakini tunapangiwa Walimu 40. Tumejaribu kulipeleka kwenye Idara na Wizara husika watusaidie. Sasa Mheshimiwa Mpango aliweke kwenye mpango wake kwamba Ludewa tuna uhaba wa Walimu na hata ukiangalia performance imeshuka sana kwa sababu hiyo. Kuna shule kama nane (8) hivi zina Walimu wawili au watatu, maximum ni Walimu wanne na tuna shule za misingi 108. Kwa hiyo, hivi vitu ni lazima tuviweke kwenye mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la afya, kweli Ilani ya Chama cha Mapinduzi inazungumzia vituo vya afya kila kata na pia inazungumzia zahanati kila kijiji. Labda tuzungumze sasa hapa wajibu wetu sisi kama Wabunge ni nini? Wabunge ni wahamasishaji wa maendeleo na vilevile tuna wajibu wa kukusanya nguvu na ku-mobilize watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, najikita moja kwa moja kwenye Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Ikumbukwe katika Bunge lako tarehe 19 mwezi wa Nne niliuliza swali Liganga na Mchuchuma, fidia kwa waliopisha maeneo itakuwa ni lini? Nikajibiwa kwamba italipwa mwezi Juni, 2016. Pia Bunge lako lilitaarifiwa kwamba Mradi wa Liganga na Mchuchuma ungeweza kuanza mwezi Machi, 2017. Sasa kitu ambacho nakiona ni kwamba, Serikali haina dhamira ya dhati juu ya Mradi wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kufuatilia maelezo ya Mheshimiwa Waziri, naomba ninukuu kwa kusoma, Mheshimiwa Waziri anasema:-

“Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2016/ 2017 Wizara kupitia NDC iliendelea na majadiliano juu ya mauziano ya umeme kati ya Shirika la Umeme TANESCO na kampuni ubia. Mfumo uliokubalika na pande zote mbili ni mwekezaji kujenga mtambo wa kufua umeme, kumiliki na kuendesha, (build, own and operate). Mauzo ya umeme kwa TANESCO hayajumuishi gharama za uwekezaji kuhusu ujenzi wa mradi. Kamati ya Taifa ya uwekezaji imepitia kwa mara nyingine vivutio vilivyoombwa na mwekezaji kwa lengo la kutafuta manufaa zaidi kwa Taifa katika mradi huo”.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Mradi wa Liganga na Mchuchuma umewekwa kama ni mradi kielelezo (flagship project). Hata hivyo, kitu ambacho nakuja kukiona hapa inaonekana kwamba hakuna master plan ya mradi huu kuanza. Leo hii tunauzungumzia hata fidia haijalipwa, wakati mwekezaji anasema tayari ana hela za kulipa, lakini sisi kama Serikali yenyewe inazungumza kwamba bado wanaendelea na mazungumzo juu ya power purchase agreement kati ya mbia na TANESCO. Sasa najiuliza pana tatizo gani? Kwa sababu tungepewa schedule of activities mpaka mradi ku- take over, lakini leo hii bado tunazungumzia kwamba tunaendelea na majadiliano sasa tujiulize haya majadiliano yataendelea mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nachangia Wizara hii mwaka wa jana tulizungumza kwamba tungepewa road map. Ifike mahali kwamba tujue kwamba mwezi huu mpaka mwezi huu, mwaka huu mpaka mwaka huu activity fulani inafanyika ili tuweze kujua kwamba itakapofika muda fulani mradi huu uwe ume-take over. Hiyo tulikuwa tunaizungumza hivyo kwa maana ya tuweze kum-pin mtu ambaye anatuletea shida hapa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kama tunaamua kuzungumzia tu kwamba tutaendelea tu na majadiliano itafika 2020 huu mradi haujaanza, fidia haijalipwa, hayo makubaliano ya TANESCO hayapo, hizo incentives ili Serikali ije itoe GN haziatakuwepo. Kwa hiyo, napenda kusikitika kwamba huu mradi hatujauwekea kipaumbele. Inawezekana zipo incentives ambazo zinatakiwa na mwekezaji lakini vile vile lazima tuangalie multiplier effect ya mradi wenyewe upoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unaleta ajira 33,000, hiyo hatujaiangalia, lakini tunaangalia zile taxation tu za mwanzo. Ifike mahali; kwa sababu Baraza la Uwekezaji Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu, kwa hiyo, maana yake huu mradi unafahamika vizuri. Kama kuna shida basi tujue kwamba huu mradi haufanyiki ili watu waendelee na mambo mengine. Leo hii ndugu zetu wa Ludewa kule wamepisha mradi lakini fidia hawana, maeneo yale yanashindwa kuendelezwa, yanashindwa kulimwa, lakini hakuna tamko lolote la Serikali ambalo linawapelekea sasa wananchi wale wafanye nini. Mwekezaji anasema hela anayo, kama hela ya mwekezaji inaleta shida, basi Serikali ingebeba jukumu la kulipa fidia huku ikiendelea na hayo mazungumzo ili iwafanye wale watu waendelee na shughuli nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kuangalia licha ya ajira 33, 000 zitakazokuwa zimeletwa na mradi huu, tunatarajia kwamba huu mradi ungeweza kuleta population ya watu wasiopungua laki tatu ndani ya eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuja kwa mradi huu maana yake ungeweza kuanzisha viwanda vingine kwa ajili ya kuweka value addition ya mazao yanayolimwa na mikoa na wilaya jirani. Hata hivyo, inaonesha ni kwamba Serikali yenyewe ime-base tu kwenye maeneo machache, kitu ambacho na chenyewe si sawa kiuchumi. Ifike mahali kwamba hiyo tax kwa mfano tukii-wave, kuna impact nyingine kwa jamii kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza kwamba huu mradi haupewi kipaumbele kwa sababu pia unakuta hata ile miundombinu yenyewe haijawekwa. Leo hii tuna barabara inayoenda kwenye chuma cha Liganga, barabara ya kutoka Mkiu kuelekea Madaba, mpaka leo hii tunaambiwa tunafanya rehabilitation hakuna utaratibu wowote kusema inaingia kwenye upembuzi yakinifu, iende kwenye usanifu wa kina, barabara zijengwe ili kwenda kwenye huo mradi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nchi inazungumza haina chuma, lakini chuma kimelala pale Liganga, leo chuma tunaagiza. Kwa hiyo ikifika mahali unakuta sasa hivi vitu vinasuasua. Tumezungumzia juu ya Reli ya Mtwara kuja Mbamba Bay kutoka Mbamba Bay inakuja Mchuchuma inakwenda Liganga; sijajua utaratibu ukoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unaweza kuona kwamba Serikali na yenyewe inakwepa. Kama tatizo ni mwekezaji, basi ifute huo utaratibu ili tujue kwamba huu mradi haupo tunatafuta mwekezaji mwingine ili tuweze ku- move, kwa sababu haiwezekani miaka mitano, sita tunazungumzia Liganga tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Liganga kwa mara ya kwanza imezungumziwa mwaka 1929. Sasa mwaka1929 mpaka leo tunazungumza tu Liganga, wazee wetu wanakufa, watoto wetu wanakufa sisi wote tutaenda tutakufa Liganga itaendelea kubaki palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapozunguzia uchumi wa viwanda Tanzania huwezi ukaiondoa chuma cha Liganga na huwezi kuondoa makaa ya mawe Mchuchuma. Makaa ya mawe Mchuchuma yanatoa megawati 600, leo nchi inatumia megawati 1050... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kusimama kwenye Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuchangia mjadala wa Wizara ya Ulinzi na Usalama. Kwanza nilipongeze Jeshi letu kwa kazi ambazo linazifanya, kwa kweli ni kazi zilizotukuka na zinastahili kupewa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nijikite moja kwa moja katika suala la ulinzi na usalama. Mimi natoka Ludewa ambako Ziwa Nyasa lipo na kama kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani kwenye ukurasa wao wa 14 na 15 walizungumzia juu ya mgogoro wa Ziwa Nyasa. Labda tu nipende kuweka vizuri taarifa yao kwamba Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu; limezungukwa na Tanzania, Malawi na Msumbiji. Kwa hiyo, katika hali ya kawaida Malawi hawezi ku-demand eneo la Msumbiji, analo-demand ni eneo la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulinzi na usalama eneo lile ni pana hasa eneo la upande wa Ludewa. Eneo la upande wa Ludewa bado ninaendelea kusisitiza kwamba lina urefu wa kilometa zisizopungua 250 around the shore of the lake, lakini kiusalama na kiulinzi bado limewekwa nyuma. (Makofi) (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukijaribu kuangalia eneo lote hilo lenye urefu huo mkubwa bado hakuna vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo vipo huko. Napenda kuchukua tu fursa hii kuliomba jeshi, kuiomba wizara na kumuomba Mheshimiwa Waziri kwamba kuna haja ya kuweka mkakati wa makusudi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazungumza hivyo? Nazungumza hivyo kwa sababu eneo lile halina mawasiliano ya simu; eneo hilo halina miundombinu ya barabara kwa urefu wote huo niliokua nimeuzungumza. Kwa hiyo basi, ifike mahali sasa kwa sababu ya haya mambo yanayoendelea hapa sasa hivi inakuwa ni ngumu sana incase ikitokea kitu chochote wananchi kuripoti, incase kuchukua kitu chochote, wananchi hata kukimbia basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ikizungumzwa kwamba hapa pana mgogoro na ilifika mahali kipindi kile yanachimbwa mafuta, unakuta ndege ya Malawi inakuja Tanzania na wananchi hawana facilitation yoyote ya kusema kwamba wanaweza wakaripoti. Kwa hiyo, ina maana kuwa kama litatokea janga lolote uwezekano ni mkubwa sana kwenda hayo maeneo na ukakuta kwamba mambo yameshaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napende tu kuisihi Wizara ikiwezekana sasa na kama itakuwa imeruhusu basi kuwepo na vyombo vya kiulinzi ambavyo vina-patrol, angalau kuwepo hata na marine boats ambazo zitakuwa zinazungukia kule kwa ajili ya kuimarisha usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naweza kulizungumzia ni juu ya Uwanja wa Ndege Sagalu, uwanja ule ni wa Jeshi lakini kwa mara ya mwisho inaweza kuwa ni miaka 30 iliyopita, ule uwanja umeshakuwa ni pori. Sasa kwa sababu kuna ujio wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga naamini kabisa facility ya uwanja ni muhimu. Labda twende kuliuliza Jeshi kwamba incase kama utakuwa hauna matumizi kwa sasa, turudishieni Halmashauri ili tuweze kuandaa mazingira ya kufanya kazi nyingine yoyote ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kusema hivyo basi naamini; tuna kambi moja ya Jeshi pale Manda ambayo ipo mpakani kabisa mwa Mto Ruhuhu. Sasa ukiangalia lile eneo lote mpaka unakuja unaigusa Kyela hakuna chombo chochote cha ulinzi, hakuna mawasiliano ya simu na hakuna mawasiliano ya miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, nichukue tu nafasi hii kuishauri Serikali kwamba ipeleke vyombo vya usalama kule angalau basi hata wananchi wafarijike incase kama kitatokea kitu chochote waweze ku- accommodate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ningependa kukizungumzia hapa ni juu ya dhana ya viwanda kwa Jeshi. Ifike mahali sasa Jeshi letu lijiendeshe kisayansi, kwa sababu ninaamini kwamba Jeshi letu lina multi professionals, lina madaktari na ma-engineer. Kwa hiyo nalo lipange mpango mkakati na ifike mahali jeshi lenyewe kama Jeshi lijitegemee na lisiwe inategemea ruzuku tu peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ninaamini kabisa jeshi lina uwezo wa kujiendesha kisasa kama ilivyoanza ule Mradi wa Nyumbu bado unaweza likaanzisha miradi mingine yoyote ambayo inaweza ikaliingizia kipato japo kwamba litaendelea kupata ruzuku kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache mimi niishie hapo, ila napenda tu kwa dhati ya moyo wangu, eneo lile la Ziwa Nyasa sasa hivi lipewe kipaumbele kwani wananchi wameamua kulima barabara wenyewe. Kwa hiyo, tunaiomba Wizara ya Ulinzi maeneo ambayo ni magumu basi tutakapoomba baruti watuletee, na maeneo ambayo yana madaraja ikiwezekana basi tupate hayo madaraja. Kuna baadhi ya maeneo Jeshi huko nyuma lilishaweka madaraja; sasa bahati nzuri maeneo yale imeshapita barabara yale madaraja yanakuwa sasa hivi ni kama hayana kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tungeomba sisi tutakapokuwa tunaomba yale madaraja basi tuletewe kwa ajili ya kufanya facilitation ya wananachi wetu kule ili paweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia huu mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kutoa shukrani zangu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kwa mambo yafuatayo ambayo yanafanyika sasa hivi kule Ludewa. Kuna barabara ya lami kutoka Njombe kwenda Ludewa - Manda, umeme wa Gridi ya Taifa ambao unatoka Makambako kwenda Songea unakatisha pale Madaba unakuja Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna miundombinu wezeshi ambayo inaweza ikaifanya chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma kuanza kwa maana ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara za Madaba kwenda Mkiu na barabara kutoka Nkomang’ombe kuelekea Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo kuna baadhi ya mambo ambayo napenda kuyaelezea kidogo hasa kuhusu makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga. Chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma ni miradi kielelezo katika Serikali hii ya Awamu ya Tano lakini bado hatujaona mpango ambao unaweza ukaonesha kwamba chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma yanaanza lini. Kwa sababu hii project, project inatakiwa iwe na mwanzo pia iwe na mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado haijaweka ule utaratibu mzuri wa kusema kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano, mwaka huu tunafanya kitu hiki, mwaka wa pili hiki, mwaka wa tatu mpaka ule wa tano. Kwa hiyo, statement ambayo inakuja ni statement ya jumla sana kiasi ambacho sasa hata ku-access huu mpango ambao ni mradi kielelezo cha Taifa inakuwa ni mgumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa Serikali sasa ianishe kwamba kwamba kwa sababu huu leo ni mwaka wa pili unakwisha tunaelekea kwenye mwaka wa tatu, bado hatujaona zile activities ambazo zinatakiwa zifanyike katika huu mradi husika. Tukiweka na kuainisha maana yake tutakuwa tumeweka vizuri kiasi ambacho unaweza sasa kufanya tathmini kwamba mwaka huu tunafanya hiki, mwaka wa pili tunafanya hiki na hata kama tunakwama sehemu tunakuwa tunajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye hilo ningependa tu Serikali ije na ile mipango kwa sababu kuna eneo pale ambalo wananchi wetu wamepisha mpaka leo bado hawajalipwa fidia na wala hatujui fidia ile italipwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu mpango ambao tumesema kuna Power Purchase Agreement, ni kweli tunapata maelezo lakini hatujui kwamba sasa hiyo Power Purchase Agreement itakamilika lini kiasi ambacho sasa itapelekea ile Government Notice kutoka. Naamini kwamba hii yote ipo ndani ya uwezo wa Serikali, Serikali ikijipanga haya mambo yanaweza yakaisha na mwisho wa siku hata hawa watu ambao wamepisha ile miradi kwa sababu yale maeneo waliyoyapisha ni makubwa kiasi ambacho sasa wanashindwa kufanya kitu chochote na hawajui kwamba fidia yao watalipwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulichangia ni juu ya suala la zao la mahindi. Nyanda za Juu Kusini ambako Ludewa ipo, zao la mahindi ni zao la biashara. Kwa wengine wanaweza wakasema kwamba ni zao la chakula, lakini hakuna zao kubwa na muhimu ambalo linatiliwa nguvu kubwa na wananchi wetu kama zao la mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba tunapolima mahindi yanapotosheleza kwa chakula, mengine yanayosalia ndiyo ambayo yanaenda kwenye biashara ambazo zinawafanya watu wetu walipe ada, wajenge nyumba na wafanye maendeleo yao mengine. Kipindi cha sasa wananchi wetu wame-stuck na walikuwa wanaitegemea Serikali kwa kiasi kikubwa kununua yale mahindi, sasa hivi mahindi hayanunuliwi na mwisho wa siku sasa inabaki kwamba uchumi wa wananchi mmoja mmoja na uchumi wa maeneo husika unabaki ku-stuck.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kwamba mahindi yale ambayo wakulima tuliwahamasisha walime kwa kiasi kikubwa basi yanunuliwe sasa. Hali ni ngumu kwa wananchi wetu kule na tunaulizwa maswali mengi sana na bahati mbaya zaidi sasa hivi Serikali imezuia kuuza haya mahindi kwenye maeneo mengine. Tunaweza tukasema hivyo kwa sababu kuzuia kwake hatujapewa sasa altelnative kama lipo soko la ndani basi soko hilo lipo wapi ili mwisho wa siku hawa watu wetu waweze kuuza mahindi yao ili tupate faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya suala la maji. Maeneo ya kusini kuna ufadhili mkubwa sana ambao wananchi au Serikali inapata kutoka kwa donor funded. Kwa hiyo, katika ufadhili huo kuna sehemu ambayo Serikali inatakiwa ichangie, tunajikuta sasa kuna miradi mingi, kuna proposal nyingi tunaziandika lakini inapofika sasa kuchangia Serikali tunakwama sana na wale wafadhili wanatupa support ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sasa Serikali pindi tunapokuwa tunaleta kwenye meza zenu kwa wataalam na kwenye mamlaka husika, basi tupewe ushirikiano wa kutosha ili tuweze kutatua hili tatizo la maji kwa sababu hawa wadau wana-support kwa kiasi kikubwa ili mwisho wa siku matatizo na kero za maji ziweze kwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia uchumi wa viwanda maana yake ni lazima twende kwenye mapinduzi makubwa ya kilimo. Sasa kitendo cha kutokununua mazao ya wakulima au kutokutafuta masoko, uwezekano ni mkubwa sana wa kuona kwamba hatutaweza kufanikiwa kwa kiasi kile ambacho tumekilenga. Hii ni kwa sababu wananchi wanakosa matumaini, wanakata tamaa na mwisho wa siku sasa drop inakuwa kubwa katika kuhakikisha kwamba hawa watu wanaendelea ku-concentrate na ile motivation inakuwa hamna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sasa Serikali ije na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunatengeneza utaratibu mzuri (platform) ya kuhakikisha kila ambacho kinazalishwa kinakuwa kipo motivated ili mwisho wa siku tuweze kuendelea na kuhamasisha hawa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara kandokando ya Ziwa Nyasa; kule wananchi wamejitolea kwa kiasi kikubwa kulima kwa majembe ya mkono. Kwa hiyo, pindi mara nyingi tunapoomba msaada kwamba hawa watu wasaidiwe kutokana na kero ambayo inawakuta mpaka imefikia kipindi wao wenyewe wanaamua kuchukua uamuzi tuwasaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru TASAF; tumelima barabara ya kilometa 28 lakini tunashukuru TASAF kwa kuweza kutu-support na matokeo yake sasa tunatumia zana ambazo ni mashine kwa maana ya grader na excavators ili kuhakikisha kwamba tunazipanua hizi. Vilevile katika maeneo mengine ambako wananchi wanajitolea zaidi, tunaomba mkono wa Serikali ufike kwa sababu kero hiyo ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ludewa kuna Vijiji 15 ambavyo havijawahi kuona gari toka kuumbwa kwa ulimwengu. Sasa imefikia wananchi wameamua sasa kushika majembe na sululu ili waweze kupata hizo barabara. Kwa hiyo, naiomba Serikali kwenye maeneo kama hayo tunapokuja kuomba msaada kwa sababu ile ni kazi ya Serikali na wananchi basi tushirikiane na wananchi hawa kuwatia moyo kuhakikisha kwamba haya malengo yanakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo nalizungumza ni lile eneo ambalo ni kando kando ya Ziwa Nyasa ambalo ni mpakani mwa Malawi na Tanzania, ni eneo muhimu kiulinzi na kiusalama. Kwa hiyo, wananchi wanapochukua hatua hizo tunaamini kwamba Serikali ije nayo ituunge mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuishukuru Serikali lile eneo la mwambao wa Ziwa Nyasa ambalo ni eneo kubwa kuliko eneo lingine lolote, tulikuwa hatuna mtandao wa mawasiliano ya simu; tunaishukuru Serikali sasa hivi angalau asilimia 75 ya eneo hilo sasa kuna mtandao wa simu. Nipongeze na niweze kuishukuru kwa hayo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono mapendekezo. Ahsante.

The Tanzania Telecommnications Corporation Bill, 2017

MHE. DEOGRATIUS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia Muswada huu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania. Kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na timu zao kwa namna nzuri ambavyo wameuwasilisha Muswada huu. Muswada huu ni muhimu sana kwa namna ambavyo umeelezwa, kwanza kwa ajili ya usalama na ulinzi, pili kukuza uchumi na tatu kwa ajili ya masuala ya kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TTCL ilikuwa tayari imeshazama, kwa hiyo mpango ambao Serikali imeuleta ni mzuri. Pamoja na Waheshimiwa wenzangu wote kuchangia lakini mimi kubwa najikita katika masuala matatu. Suala la kwanza liwe ni suala la mtaji, la pili miundombinu na pia wakati mwingine lazima tuziangalie hizi sheria zetu hasa tunapoyapeleka mashirika ya umma kwenda ku-compete na mashirika mengine. TTCL inatakiwa kupewa mtaji, ikishapewa mtaji naamini kabisa ni shirika ambalo linaweza likafanya kazi yake vizuri na likapeleka gawio Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mtaji siyo lazima utoke direct kwenye Serikali lakini bado Serikali ina uwezo wa kutoa guarantees na kulifanya hili shirika liweze kusimama na kujiendesha kibiashara. Kipindi kile TTCL ilikuwa haiwezi sana ku-move, inawezekana ni kwa sababu tu ya mwingiliano wa maslahi ya kibiashara, kwa sababu kuna component ambapo Airtel naye alikuwa tayari ni shareholder pale wakati wanafanya the same business.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali kama hiyo shirika lisingeweza kwenda kwa sababu kuna mdau mwingine
ambaye alikuwa ndani ya TTCL yenyewe na yeye anafanya biashara ambazo zinafanana lakini sasa hivi huyo mdau hayupo. Kwa hiyo naamini kwa sababu ya shirika kuwa ni asilimia 100% government ownership lina uwezo wa kwenda na ku-compete kama ambavyo yanafanya mashirika mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumziwa suala la Mkongo wa Taifa. Mkongo wa Taifa ni mali ya Serikali kwa hiyo katika hali ya kawaida huu Mkongo wa Taifa kwa sasa kwa namna tunavyokwenda apewe TTCL moja kwa moja ili aweze kuimarisha hiyo miundombinu na aingie kwenye soko akiwa tayari ana nguvu za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo ilo eneo la Data Center kwa sababu ni mali ya Serikali hatuna sababu TTCL isipewe umiliki wa moja kwa moja Data Center hizo. Vilevile tuangalie hizi Data Center ambazo zinaanzishwa nje ya ule mfumo wa Data Center ya Kitaifa, naamini kwamba Serikali ina nguvu na uwezo wa kutosha kuhakikisha ina-control hiyo na wote ambao wanatumia data wakatumia data hizi za TTCL ili mwisho wa siku ziweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hii Sheria ya Procurement, TTCL sasa hivi anaenda kwenye ushindani, hawa wenzake hawana vizuizi katika kufanya business na katika kuagiza baadhi vifaa ambavyo vinaweza vikafanya waweze ku-dominate soko la biashara. Kwa hiyo, kuna haja ya kuangalia kwa maana ya kutoa exemption fulani fulani katika hii Sheria ya Procurement ili kuifanya hii TTCL iweze kufanya biashara yake smoothly.

Mheshimiwa Naibu Spika, la sivyo wakati wengine wana uwezo wa kuagiza vifaa na components zozote bila kizuizi chochote sisi wakati tunaiwekea kizuizi kampuni yetu ya TTCL, naamini kabisa uwezekano wa kuingia kwenye competition na kudumu kwenye soko utakuwa ni mdogo. Hatukatai kwamba hii sheria ipo, ni kweli ipo lakini kwenye baadhi ya maeneo ambayo tunaona kwamba inaweza ikawa ni kipingamizi au kizuizi cha kufanya biashara yake vizuri basi TTCL apewe hizo exemptions ili aweze kufanya hiyo biashara ili mwisho wa siku ijiendeshe kwa faida na Serikali ipate gawio lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo upungufu ambao TTCL ya sasa inayo na naamini upungufu huo ndiyo uliopelekea kubadilishwa kwa sheria. Upungufu wa kwanza ni kwamba mdau aliyekuwepo ndani alikuwa na yeye ni mshindani kwenye biashara. Kwa hiyo, kutoweka kwake ndiyo maana sasa tunaileta ile sheria ya kwamba kwa nini tunatoka sasa kwenye kampuni kuja kwenye shirika? Tunatoka kwenye kampuni kuja kwenye shirika kwa sababu ni 100% government ownership, ni jibu rahisi tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunapokuwa tunazungumzia biashara, biashara inafika kipindi inakuwa na kikomo, biashara inategemea mazingira, jibu linakuja kwamba mazingira ya sasa hairuhusu TTCL kujiendesha kama inavyojiendesha na ndiyo maana Serikali inaleta Muswada huo. Kwenye business life cycle, business inapitia challenges nyingi, sasa hatuwezi kubaki stagnant eti kwa sababu tu kwa nini ulianzisha vile, kwa nini ulianzisha vile, teknolojia imebadilika, mazingira ya ufanyaji biashara yamebadilika na ndiyo maana na sisi sasa tunapaswa kubadilika ili tuweze ku-move. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikuwa haiwezi kutoa mchango wake kwa sababu kulikuwa na percentage kwenye share, hilo nalo limepelekea Serikali kuleta Muswada huu kwa sababu huwezi kupeleka tu kama unavyotaka wakati huo kuna mwingine mnaye pale mnapaswa mjadiliane. Kwa hiyo, inategemea wakati mwingine mnaweza mkawa na convincement power ya namna gani ili kuweza kumshawishi mbia muweze kwenda sawa. Sasa hivi ni 100% government ownership, kwa hiyo inaweza ikatengeneza bila kuhujumiwa na mtu mwingine yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mamlaka au madaraka au uhuru usiokuwa mipaka. Nakubali CEO na Bodi yake ifanye kazi kwa uhuru, lakini lazima kuwepo na scenario ambayo Serikali kama mwenye kampuni aweze kuona nini kinachoendelea. Mimi siamini kwamba Waziri atakuwa kazi yake kuleta directions tu kwa Bodi au CEO na atakuwa anafanya hivyo kwa sababu ya kupewa ushauri fulani fulani. Kwa hiyo, naamini ile component pale ya Waziri iendelee kuwepo kwa maana Waziri ndiyo aliyepewa mamlaka na Serikali katika kuhakikisha kwamba anahakikisha ile taasisi inakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna uhuru usiokuwa na mipaka ila ijaribu tu kuangaliwa kwamba ule uhuru au ile dhamana ambayo Waziri anayo ifanyiwe marekebisho kiasi ambacho haitaifanya kampuni iweze kutetereka au kurudi nyuma katika kufanya biashara zake za kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niishie hapo, lakini niendelee kusisitiza tu taasisi hii inayokuja ni lazima ipewe mtaji, taasisi inayokuja ule Mkongo wa Taifa uumiliki kwa 100%, Data Center imilikiwe na TTCL na taasisi zote za kiserikali zitumie data za TTCL kwa sababu TTCL ni baba na mama wa hivyo vitu. Kwa hiyo, inapokuwa kwamba wewe mwenyewe unayo taasisi ambayo inafanya kazi hiyohiyo halafu wewe ni mmoja unatoka unaenda kufanya kazi kwenye taasisi nyingine nadhani haiwi nzuri sana. Nipende kushauri kwamba taasisi zote za kiserikali, taasisi za umma zitumie TTCL katika matumizi yake ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Special Seats (CCM)

Supplementary Questions / Answers (4 / 0)

Contributions (5)

Profile

Hon. Vicky Paschal Kamata

Special Seats (CCM)

Supplementary Questions / Answers (1 / 0)

Contributions (2)

Profile

Hon. Wanu Hafidh Ameir

House of Representatives (CCM)

Contributions (1)

Profile

Hon. Rehema Juma Migilla

Special Seats (CUF)

Profile

Hon. Justin Joseph Monko

Singida Kaskazini (CCM)

Profile

View All MP's