Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Jaku Hashim Ayoub

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, unapokuta maji yakoge, mwanzo hujui mbele kama utayakuta tena.
Kwanza nichukue fursa hii kukushukuru wewe kunipa hizi dakika nne au tano hizi zilizobaki kumalizia ngwe hii iliyobaki na nitakuwa si mwingi wa fadhila kama sikumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyeniwezesha kusimama hapa na kuvuta pumzi zake na kurudi tena kwa mara ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo Mheshimiwa Waziri kipindi kilichopita mwaka jana, nilikigusia sana na nikazuia shilingi, na hii leo hii nafikiri Mheshimiwa Waziri kuna vijana 13 kutoka Zanzibar. Nazungumza kuhusu maslahi ya Zanzibar kuhusu Wizara hii, kutokana na mambo yanayohusu masuala ya Muungano.
Kuna vijana 13 mmewasomesha Chuo cha Diplomasia, bahati mbaya mkawachukua saba, lakini kwa masikitiko makubwa na unyonge na huruma kubwa mpaka hii leo vijana hao saba hamjawaajiri. Mwaka jana nilihoji kwenye bajeti na Mwenyezi Mungu si Athumani kanirudisha tena leo hii, nipo hapa, kwa hiyo, nitahitaji maelezo ya vijana saba hawa wa Zanzibar mpaka leo hamjawaajiri na hii ilikuwa si hisani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni makubaliano katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Vijana hawa hamjawaajiri hadi hivi leo, nataka maelezo ya kina kuhusu suala hili na umri wao unakwenda, na mmechukua barua Zanzibar kama kuwaazima, si kitu kizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka hapo kwa haraka haraka nitahitaji maelezo lakini haya vilevile ni ya kusikitisha, Wizara hii huko nyuma au uzoefu unaonesha Waziri anatoka Bara, Naibu Waziri kutoka Visiwani. Lakini kwa masikitiko Wizara hii wote wazee mmekalia kiti chenu, lakini si maamuzi yangu ni maamuzi ya Mheshimiwa Rais. Lakini kama hapatoshi hapo, hata Wizara ya Fedha haya mambo ya Muungano tulikuwa tupokezane, hapatoshi hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwa umakini wake na Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu, alikuwa akijitahidi katika safari za nje, kuwachukua Mawaziri kutoka Zanzibar katika safari zake, je, mpango huu utaendelea tena vilevile au utalala?
Mheshimiwa Mwenyikiti, nitoke hapo nataka kuulizia haya maslahi ya Mabalozi wangapi wa Zanzibar waioajiriwa, huu ni wimbo wa Taifa wa muda mrefu. Wimbo huu umekuwa wa muda mrefu, kuhusu ajira katika Wizara hii nataka kujua Mabalozi kutoka Zanzibar ni wangapi wanaowakilisha hivyo? Vilevile senior officer kutoka Zanzibar, katika Mabalozi wako wangapi, wimbo huu umekuwa ni wa muda mrefu lakini hautoshi...
MWENYEKITI: Ahsante,

The Government Chemist Laboratory Authority Bill, 2016

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kusimama hapa. Huu sio uwezo wangu wala nguvu zangu wala ubabe wangu ni neema yake hii, na pumzi alizonipa hapa za kuniazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipa fursa hii kuchangia muswada ulio mbele yetu, muswada muhimu na sijui niseme niilaumu Serikali kidogo kwa kuchelewa kuleta muswada huu. Muswada muhimu kwa wananchi, umechukua muda mrefu haujafika hapa, wananchi wakaendelea kuumia.
Mheshimiwa Nibu Spika, lakini vilevile nitakuwa sijamtendea haki Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Msaidizi wake Naibu Waziri, Dkt. Hamisi Kigwangalla, team captain wa timu ya Bunge kwa muswada huu.
Mheshimiwa Nibu Spika, lakini mimi ni mdau wa Kamati hii, lazima ni-declare interest. Sifa pekee za aina yake ziende kwa Mkemia Mkuu wa chombo hiki. Mkemia Mkuu amekuwa akifanya kazi katika mazingira magumu bila kujali mvua, jua, usiku mchana. Mkemia Mkuu hongera sana na usitegemee malipo kwa binadamu, tegemea malipo kwa Mwenyezi Mungu. Kazi uliyofanya Mheshimiwa Mkemia Mkuu ni kazi nzito sana katika mazingira mazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape pole sana watendaji wa kitengo hiki, wamekuja Kamati karibu mara nne, kwenda na kurudi hawapungui watu 20. Ndipo pale Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi nilipotaka Mwongozo wako kwa vitengo hivi kwenda na kurudi, gharama ya mafuta, kulala, kula, kunywa, inakuwa ni gharama kuliko Bunge likabaki pale Dar es Salaam, ndicho kilio change hiki nilikiona muda mrefu na nilikuwa na Kamati jirani palepale, Wizara ya Ulinzi walikuwa wanakuja kwa ndege, gharama ni kubwa, tulifikirie hili suala kwa ajili ya kubana matumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa nisichangie, nimekaa sana kwa kipindi kirefu kusikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge, lakini kazi hii yote mwisho wake ingekuwa bure. Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize kwa makini hivi sasa na ukaanza ku-note hizi point ninazozungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, DNA Tanzania nzima ni moja. Tanzania na ukubwa wake tuliokuwa nao ni moja kwa utambuzi wa vipimo vya binadamu. At least Serikali itafute angalao DNA sita kwa Tanzania ili baadhi ya Kanda ziwekwe. Huwezi mtu kumtoa Mtwara kuja kufuata kipimo Dar es Salaam. Huwezi kumtoa mtu Arusha kuja kufuata kipimo Dar es Salaam! Kweli tunaitendea haki? Niliyazungumza haya Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwenye Kamati haya na yote ukayakubali kwa mdomo, si vitendo, sijui vitendo viko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mashine moja inahitaji angalao shilingi milioni 700 kwa utafiti niliofanya, lakini Serikali isiogope hasara kwa ajili ya wananchi wake. Serikali hii isingekuwa madarakani bila kuwa wananchi, wananchi ndio Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili, kwanza Serikali ibanwe itoe fedha haraka, ije sheria maalum ya kuibana Serikali kuhusu vyombo hivi vya DNA. Hatuwezi kuja kuzungumza maneno yote hapa wakati vitendea kazi hatuna, hii ni sawa sawa na kutwanga maji kwenye kinu, kazi yote hii itakuwa bure. Kama hawajawezeshwa hawa tunapitisha muswada huu kwa malengo gani? Ndiyo yale tunayosema tuna huruma kwa mdomo, sio kwa vitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hapatoshi changamoto ya tatu, watumishi ni kidogo. Waliopo hivi sasa kwa mujibu wa taarifa niliyokuwa nayo kwenye Kamati ni 192, at least wapatikane watumishi 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio pale niliposema nilikuwa sitaki kuchangia, lakini kama sikuzigusa changamoto hizi tukiwa tunachangia muswada huu, wale watenda kazi watafanya kazi katika mazingira gani? Watu sita watafanya kazi gani? Watu 12 watafanya kazi gani Tanzania kutokana na ukubwa wake? Hata sisi Zanzibar tunaitegemea DNA hii, ndio ukweli ulivyo; mtu avuke bahari aje apime kipimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mazingira wanayofanya kazi ukiyaona utalia. Hiyo wafanyakazi 208 wapatikane hivi sasa tukijaliwa. Hapa nitahitaji maelezo Mheshimiwa Waziri, watu 400 wanahitajika, wafanyakazi wako 192, hapa nitahitaji maelezo yakutosha, majengo ya Kanda hayapo. Kama mfano Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya, huu mji mpya mnaotaka kuufanya sasa hivi, Dodoma, hatujawa tayari. Changamoto hii Mheshimiwa Waziri nitahitaji maelezo ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa kumalizia, nimuombe Mheshimiwa Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini Waheshimiwa kama nitawakera kidogo niombe radhi hasa akinamama kuhusu nywele zetu hizi kidogo za kubandika, zina mitihani jamani, zina maradhi. Nazungumza kwa nia njema kabisa, haya mambo nimeyapata mimi kwenye Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkemia Mkuu wa Serikali kama itawezekana kabla ya kuondoka kesho ukatupa semina bure siku ya Jumamosi kuhusu namna ya kubandika hizi nywele, zina maradhi Waheshimiwa. Niombe radhi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's