Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Venance Methusalah Mwamoto

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kweli kwa kunifanya niwe mzima mpaka leo lakini niwashukuru sana Wananchi wa Kilolo ambao wamenirudisha baada ya miaka kumi kutoka hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais iko vizuri na jana wenzetu walipotoka nje, bahati nzuri mimi nilipata bahati ya kuwa wa kwanza kutoka lakini kikubwa kilichofanya watoke ni kwamba hawana sehemu ya kuchangia. Sasa kwenye ile hotuba kama hauna sehemu ya kuchangia itakuwa siyo rahisi ubaki humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili wenzetu wanataka kuonekana Live. Mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, kuna watu walikuwa wanajua kuzungumza humu ndani mnawajua sitaki kuwataja na ilikuwa wakati anachanga unakuta vikundi vimeshajikusanya ukiuliza kuna nini wanakwambia leo jamaa anaongea na anataka kumchana live Waziri Mkuu, sasa nafasi hiyo haipo tena.
Kwa hiyo, wenyewe wanataka kuendelea kucheza live humu ndani lakini ukiangalia maendeleo kwenye maeneo yao hakuna, na walio wengi ninyi wenyewe mnahakika kabisa hawakurudi waliokuwa wanazungumza sana humu ndani. Wananchi wanataka maendeleo. Wanataka live kwenye maendeleo siyo live kwenye TV.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi kwa kweli kwa muda ule ambao umependekezwa ni muda ambao wananchi wengi kweli watakuwa wanaweza kuona kinachofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la maji. Wilaya ya Kilolo, Tarafa ya Mazombe - Ilula kuna tatizo kubwa sana. Mimi nina hakika mwaka 2000/2005 nilipokuwa Mbunge, tulipewa ahadi na Mheshimiwa wakati huo Rais Mkapa suala la maji, bahati nzuri haikuwezekana, wananchi walinihukumu wakanipa likizo, na mwenzangu aliyechukua nafasi yangu aliingia akapewa ahadi nzuri na Rais aliyekuwepo, naye inawezekana ni sababu hiyo hiyo amepewa likizo, sasa juzi alipifika Mheshimiwa Rais kuja kuomba kura tukamwambia sehemu moja nzuri anayotakiwa kwenda ni sehemu ya Ilula ambayo ina tatizo la maji. Aliahidi kwamba suala hilo analichukua, na ana hakika kabisa asilimia 100, akawaambia wananchi kwamba nirudishieni Mwamoto na nipeni kura, suala la maji limekwisha. Nitawaletea Waziri ambaye anajua matatizo ya maji.
Mheshimiwa Lwenge naomba uandike vizuri hiyo, kwa sababu ili uende kwenu kwenye Jimbo lako ni lazima upite Ilula. Huwezi kunywa maji, huwezi kupita Ilula. Uhakikishe maji yanapatikana na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Sasa hivi ukienda pale ukimsalimia mtu wa Ilula, maana yake sisi huwa tunasalimiana kule kilugha kamwene, anakwambia maji, ukimwambia kamwene anakwambia maji, ukimwambia kitu chochote anakwambia maji, hapa kazi tu, maji. Sasa dawa yake ni kutoa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ukikaa Ilula ukitaka kupanga chumba unapanga vyumba viwili kama unaanza maisha, unapanga chumba kimoja kwa ajili ya madumu ya maji na chumba kimoja kwa ajili ya kulala wewe. Sasa mimi nawaomba, kwa sababu ni ahadi ya Rais na Mheshimia Lukuvi naomba unisaidie, mimi mdogo wako nipo nisiondoke tena unisaidie maji na maji mengine kwako kule tutakuletea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilula hakuna tatizo la maji, tatizo lake ni mgawanyo wa maji, maji yapo mengi, kuna mito mingi pale lakini unaifikishaje kwa wananchi ndiyo tatizo. Kwa hiyo, mimi naomba, Mheshimiwa Lwenge tuende pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la barabara. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, iko wazi kabisa kwamba kila Wilaya barabara itaunganishwa kwa lami mpaka Makao Makuu ya Mkoa, lakini pia na kufanya uwezekano mkubwa na kuunganishwa na Wilaya nyingine.
Wilaya ya Kilolo toka mwaka 2002 mpaka sasa katika kilomita 35, kilomita zilizojengwa kwa lami ni kilomita saba, sasa sielewi ni kwa nini. Kwa hiyo kwa kuwa Profesa Mbarawa nilishazungumza naye, tutaona jinsi ya kutusaidia, lakini ni pamoja na kutuunganisha ile barabara ya TANROAD inaishia Idete, tulishaipitisha kwenye mpango wa barabara ya TANROAD kwamba iishie sasa Muhanga ili tuunganike na watu wa Morogoro, kwamba itoke Kilolo - Dabaga - Idete - Itonya ifike mpaka Muhanga ili tuende mpaka Mbingu kule Kilombero, Morogoro tuweze kuunganisha nao ili tuweze kufungua uchumi wetu kwa sababu uchumi wa Kilolo unategemea sana Kilimo na ili wananchi wale wapate fedha inabidi wauze mazao yao yale lakini kama barabara zitakuwa ni shida watanyanyaswa, watauza mazao yao kwa bei ambayo haifai.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la pembejeo za kilimo. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alifika Iringa na tukamwambia matatizo ya pembejeo. Lakini tatizo la Pembejeo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo naona unanisikia, naomba hebu washikirishe Wakuu wa Wilaya kwenye suala hili la usambazaji wa pembejeo na ikiwezekana Wakuu wa Wilaya wasiwe Wenyeviti wa pembejeo kwa sababu wao ndiyo wanatakiwa wasimamie, kwa hiyo linapotokea tatizo hakuna wa kumuuliza! Mkurugenzi yupo mle, Mkuu wa Wilaya yupo mle, wao wasimamie tu mwenendo mzima wa pembejeo kwa sababu kuna ujanja mwingi sana kwenye pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ndiyo wanapeleka mbegu Kilolo wakati sasa hivi ni wakati wa kupalilia, wanatakiwa wapeleke mbolea ya kukuzia, kwa hiyo kuna matatizo pale, tunaomba utusaide. Lakini pia na bei ya mbolea iko juu sana, tuangalie uwezekano wa kupunguza kama ni kodi, kama mambo mengine basi yapungue.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala la Mabaraza ya Kata. Mheshimiwa Waziri wa Sheria yupo, TAMISEMI yupo, Utawala Bora yupo, Wizara ya Mambo ya Ndani yupo. Mabaraza ya Kata kuna tatizo, tatizo ambalo lipo wanaoendesha hayo Mabaraza uwezo wao ni mdogo, hawapati mafunzo, lakini kazi ile ni kubwa sana na wamesaidia sana kutatua migogoro.
Kwa hiyo mimi nikuombeni tusaidiane kwenye hilo sambamba na madawati ya jinsia. Mheshimiwa Kitwanga, madawati ya jinsia yamesaidia sana kupunguza kero nyingi sana lakini matatizo ambalo lipo, yale Mabaraza ni vema ofisi zikawa kwa Mkuu wa Wilaya, kwa sababu watu walio wengi Mheshimiwa ukipigwa kibao na mke wako unaona aibu kwenda Polisi lakini ikiwa kwenye Baraza anahisi ni sehemu ya usuluhisho kwa hiyo inakuwa rahisi kwenda na kutoa elimu. Maana yake madawati ya jinsia siyo wanawake peke yake, hata wanaume. (Makofi)
Mimi naomba ikiwezekana tuma watu wako waende pale Kibondo wakaone lile Dawati linavyoendeshwa na kesi nyingi pale ni za wanaume kushtaki kwa kupigwa tena. Kwa hiyo unaona jinsi ambavyo elimu imefika kule. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni suala la ujenzi wa ofisi, Wilaya ya Kilolo toka mwaka 2002 tumekuwa Wilaya lakini Mheshimiwa Kitwanga huna hata jengo moja ambalo limejengwa. Huna Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya, huna nyumba ya Polisi Wilaya ya Kilolo. Kwa hiyo mimi naomba, baada ya Bunge hili mimi tutakwenda pamoja na nitachangia na mafuta maana haukuwa mpango wako ili tuende ukaone hali jinsi ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia na suala la hospitali hamna hospitali Wilaya ya Kilolo. Majengo yapo pale lakini mpaka leo hakuna hospitali ya Wilaya na kuna majengo ambayo wananchi wamejitolea wamejenga zahanati lakini hazijaisha, wamejenga vituo vya afya havijaisha, ukiwauliza wanakuambia bajeti tuliomba lakini tumeletewa bajeti finyu. Kwa hiyo nafikiri Mheshimiwa Kigwangalla tusimsumbue Mheshimiwa Waziri, tuende ukaone hali jinsi ilivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda bado ninao, kuna hili sula la uchangiaji wa elimu ambapo Mheshimiwa Rais amefuta...
Mheshimiwa Naibu Spika, basi naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Waziri na Naibu Waziri wake. Ningependa kuchangia kuhusu suala la mbegu za mahindi zinazotumika kwa sasa, ningependekeza utafiti ufanyike ili tuweze kupata mbegu mpya. Kwani ni mbegu ambazo zinatumika sasa ni za muda mrefu zimechoka sana. Ukilima ekari moja unategemea kupata gunia siyo chini ya gunia 35, lakini mbegu hii iliyopo ukipata gunia nne ni bahati. Hivyo ni vema Serikali ikafanya utafiti kutumia vyuo vyetu ili tupate mbegu bora. „Kama ukitaka mali utaipata shambani’.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri suala la umwagiliaji litiliwe kipaumbele kwani tumeshuhudia mwaka huu mvua nyingi zimenyesha lakini sikuona jitihada za Serikali na hasa Wizara yako na Wizara ya Maji kuweza kuvuna maji ambayo tumeshuhudia maji mengi yakipotea bure.
Mheshimiwa Waziri hata suala la migogoro ya wakulima na wafugaji, tatizo siyo ardhi tatizo ni utengaji wa maeneo ya mifugo kupata sehemu ya kwenda kunywa maji. Hivyo endapo itatenga na kujenga mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji na sehemu ya kunyweshea mifugo suala hili la migogoro ya wafugaji na wakulima litapungua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ningeomba sana Wizara ya Kilimo, iweze kumsaidia mkulima itabidi Wizara yake kushirikiana na wadau kuona jinsi ya kumaliza suala la Lumbesa, wakulima wanapata tabu sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kwa kupongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Ningependa kujua sababu ambazo zimefanya kiwanda cha Chai-DABAGA kutofanya kazi sasa ni miaka zaidi ya 15 wakati wananchi wanalazimishwa kulima chai, nitaomba ufafanuzi.
Ningependa nijue hadi sasa Serikali imejipanga vipi kuwawezesha wazawa zaidi kupunguza ukiritimba ili waweze kujenga viwanda vya matunda na nyanya katika sehemu za Ilula ambako nyanya nyingi zinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Iringa kiwanda cha usagishaji cha N.M.C kilichopo Iringa Mjini kimekuwa kikifanya kazi kwa kusuasua. Ninaomba Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe ufike Iringa na utembelee Kiwanda cha Chai-DABAGA-Kilolo na Kiwanda cha usagishaji ili uone hali iliyopo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Waziri na Wizara yake wawasaidie wananchi, wakulima kuona uwezekano wa kuleta sheria ambayo itamsaidia mkulima kuweza kuuza mazao yao sokoni na kwa kutumia mizani na siyo lumbesa. Tumeshuhudia hata viwanda vimekuwa vikinunua mazao ya wakulima kwa bei ndogo tena bila kutumia mizani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri amtembelee Mtanzania Mzee Sallawa George aliyegundua jinsi ya kutengeneza Ulanzi na kuweka kwenye chupa bila kuharibika. Ninaomba Wizara yako imsaidie ili utaalamu wake usipotee. Wenzetu wa Kenya wanatengeneza juice ya Ulanzi, Bamboo Juice na mimi nitakuwa tayari kumuwezesha Mtanzania huyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Nianze kwanza kwa kuwapongeza Wabunge wanne ambao wameingia safari hii baadaye, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Mheshimiwa Lucy Owenya na Mheshimiwa Ritta Kabati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Serikali. Hakuna kitu ambacho kinanikera kama kuendelea kufanya vibaya kwa timu zetu za Taifa, juzi niliuliza swali Mheshimiwa alijibu, lakini nataka kumshauri leo. Bahati nzuri nimekuwa mchezaji kwa ngazi ya juu kabisa, nimekuwa kwenye Baraza la Michezo, Mjumbe kwenye TFF, nimekuwa Kapteni wa timu wa Bunge lililopita, na sasa hivi ndiye kocha wa timu ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nashauri, kwa kuwa nilipokuwa kwenye Baraza na nina hakika kuwa Baraza letu linajiendesha katika mazingira magumu sana. Hakuna fedha ya kutosha ambayo inapelekwa pale, lipo pale kwa sababu lipo kisheria na sidhani kama linafanya kazi yake kama inavyotakikana. Nimekuwa TFF mzigo ni mzito nitatoa ushauri baadaye kwamba iweje kwa timu ya Taifa. Kwa kuwa Baraza la Michezo lina vitu vingi, michezo yote iko mle pamoja na wasanii wapo mle ndani. Ninapendekeza tuunde Shirika la Michezo. Ukienda Uingereza baada ya kugundua kwamba baadhi ya michezo haifanyi vizuri walianzisha Shirika la Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa kuanzisha shirika la michezo badala ya baraza ni kwamba itakuwa rahisi kujitengemea, litakuwa linakaguliwa kama kawaida na Serikali/CAG, lakini litafanya kazi vizuri kuliko sasa kwa sababu sasa hivi halina fedha lakini tutakapounda shirika itakuwa rahisi wao kufanya mambo mengi. Kwa mfano, wanaweza wakatafuta kwenye harambee, wanaweza kuwa na vyanzo vingine vya mapato na hivyo itakuwa ni rahisi sana kuzihudumia hizi timu za Taifa. Leo kuna kuna mashindano ya olympiki, wakimbiaji wako Arusha, sijui wako camp, hawana fedha wanapata shida. Timu ya Taifa inaachiwa na TFF, TFF wanapata wapi pesa? Kwa sababu kiingilio kile nilitegemea makato ya ile kodi ingerudi baadaye ikasaidia kwenye timu ya Taifa. Lakini tunataka tu tuone timu ya Taifa inafanya vizuri bila kuipa support, hii ni pamoja na michezo mingine. Mheshimiwa Waziri ninashauri tuanzishe Shirika la Michezo, hapa ndipo utakapoona tofauti. Leo ni miaka mingapi hatujafanya vizuri?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri pia kuhusu timu ya Taifa. Ili timu ya Taifa ifanye vizuri ninashauri TFF najua wapo, idadi ya wachezaji ambao wanatoka nje, wanaoruhusiwa kuchezea vilabu vyetu vya ndani ni wengi mno kiasi kwamba leo ukienda timu ya Yanga wanaoongoza kufunga magoli ni wachezaji wa kutoka nje, ukienda timu ya Simba wanaoongoza kufunga magoli ni wachezaji wa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lake ni nini, ukiangalia ligi ya Uingereza ndiyo ligi bora ninaamini kuliko ligi nyingine na ndiyo ligi yenye wachezaji wengi wa nje. Lakini timu ya Taifa ni mbovu sana kwa sababu wanaocheza ligi ile ni wageni, kwa hiyo na sisi tunanufaisha tu timu za Simba na Yanga lakini uwezo wa kunufaisha Taifa kwa kutumia wachezaji wengi wa nje itakuwa ni kizungumkuti, hatutafanya vizuri hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waziri wa Kazi Mheshimiwa Mavunde yupo, hebu kapitie mikataba ya wachezaji wetu kwenye vilabu vyao, kwa sababu tofauti ya mshahara ya wachezaji wa nje na wachezaji wetu inakatisha tamaa. Ukienda pale wale watu unaweza ukafikiri labda wanafanya mgomo lakini wameshakata tamaa kiasi kwamba wanaona afadhali basi hawa wanaolipwa fedha nyingi ndiyo wacheze wenyewe. Sasa nafikiri Mheshimiwa Waziri pita pale kagua ile mikataba yao utaona kinachoendelea pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nigependa nishauri ni kwamba vilabu vyetu vinachukua muda mrefu sana kufanya uchaguzi na hii ni pamoja na mikoa. Mimi natoka mkoa wa Iringa, tunapokea malalamiko mengi sana kutoka kwenye klabu za Lipuli na klabu ya mkoa wa Iringa kwamba chaguzi hazijafanyika. Kwa hiyo, ningeomba taratibu zifuatwe kama ni Baraza la Michezo la Taifa au ni Mabaraza ya Mikoa yasimamiwe yahakikishe chaguzi zinafanyika kwa sababu hapo ndipo ambapo vurugu inaanzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kushauri ni jinsi ya kutenga siku maalum. Mheshimiwa Rais ametenga siku maalum ya usafi, sasa Mheshimiwa Waziri wa Michezo, kuna haja kabisa ya kuangalia kama nchi zingine, mfano ukienda Burundi, Congo na sehemu zingine wana siku maalum ya michezo na hii tungeanza Wabunge kwa sababu michezo ni afya, michezo ni dawa na michezo ni tiba. Tukifanya hivyo tutawafanya na watu wengine wakaona umuhimu wa michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni academy, lazima tuwe na academy. Sisi wakati tunacheza wakati huo tulikuwa tunatumia zaidi michezo ya shule za sekondari, vyuo na mashirika. Lakini ukiangalia hii michezo sasa hivi imekufa kabisa, zile ndizo zilikuwa academy. Leo ukianzisha academy unapata wapi vifaa, uwanja ule wa bandia ambao kodi yake na ununuzi huwezi ku-afford, vifaa vya michezo bei ziko juu, sasa bila kufanya hivyo matatizo yake yatakuwa ni makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wasanii ni vema kama nilivyosema tukiwa na shirika la michezo na wasanii waatakuwa ndani, itakuwa rahisi kuwasimamia haki zao. Wanadhulimika sana, wanafanya kazi kubwa lakini haki zao hazitambuliwi. Tumeshuhudia wacheza filamu, filamu zao zipo mitaani, wanachopata wao hakuna, ni shida tupu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba kabisa hebu kaa na watu wako muweze kuona mnawasaidiaje wasanii na wanamichezo wa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kwa sababu muda bado ninao mimi nilikuwa Rais wa wacheza mpira Tanzania, chama kinaitwa Spurtanza (Chama cha Wachezaji Mpira). Mimi nigekushauri jaribu kuwatumia wale wachezaji tungeweza kuwatawanya kwenye shule za msingi hata kwa posho kidogo wangeweza kusaidia kufundisha michezo na ingekuwa ni academy tayari. Wapo wengi, anapomaliza kucheza mpira mchezaji wa Tanzania wengi maisha yao ni shida, lakini tayari wanakuwa wameshafikia level ya Taifa, kwa hiyo automatically wanakuwa kwenye level ya coaching ya mwanzo, ni kiasi cha kuwaendeleza tu. Kwa hiyo wangetumika kwenye shule zetu za misingi wangesaidia kubadili michezo kwenye nchi yetu kwa baadhi ya michezo kama mpira wa miguu, riadha,ngumi na kadhalika, badala ya kusubiri academy ambayo kwa kweli ni gharama kuziendesha na Serikali bado haijatia nguvu labda wakiamua kuweka ruzuku kwenye michezo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba Mheshimiwa Waziri, pesa hizi ulizoomba ni ndogo hazitasaidia kitu chochote. Hizi ni za semina na mambo mengine, lakini kwenye mambo ya michezo sahau kama kutakuwana mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia asubuhi ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru wananchi wa Jimbo la Kilolo ambao kwa kweli wamenirudisha baada ya miaka 10 kukaa bench, nawashukuru sana. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Mawaziri, kwa mwanzo mzuri wa kazi nzuri ambazo tumeshuhudia Mawaziri wetu wakifanya na kufuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia kuhusu TASAF, kwanza naishukuru Serikali kwa mradi mzima huu wa TASAF, tulianza na TASAF I na II ambazo zenyewe zilijikita kwenye ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na kadhalika. Kazi ilifanyika vizuri na ilikuwa inafanyika kwa ushirikishi kati ya wananchi wa maeneo pamoja na mchango wa TASAF.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosikitisha ni kwamba. baadhi ya maeneo na baadhi ya miradi ambayo ya awamu ya kwanza na ya pili mpaka leo haijamalizwa. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI naomba nikushauri, jaribu kufuatilia ile miradi ya TASAF ambayo haikumalizwa kwenye awamu ya kwanza na ya pili ili iweze kumaliziwa, kwa sababu inavunja moyo sana kuona miradi ile bado ipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, TASAF III, napongeza uongozi mzima wa TASAF kutoka Makao Makuu mpaka Waziri husika. TASAF III ni TASAF ambayo imelenga kuondoa au kupunguza umaskini kwa wananchi, wamefanya kazi kubwa sana. Tumetembea baadhi ya maeneo tumeona jinsi ambavyo wananchi wameanza kubadilika. Kuna matatizo madogo madogo ambayo kama Serikali inabidi iangalie.
Moja ni kwamba wale wanaosimamia TASAF wakiwemo Wenyeviti wa Vijiji, wao wanasimamia kuwapa fedha wale watu maskini lakini wao hawalipwi, hawana posho Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji anasimamiaje mtu kugawa nyama, wakati yeye mwenyewe hali, haiwezekani! Matokeo yake watu ambao wanaingizwa kwenye TASAF III wengine siyo wahusika, wanaingia baadhi ya ndugu wa viongozi, baadhi ya watu ambao wana nguvu zao, baadhi ya watoto wadogo, maana ya TASAF inaharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa Mheshimiwa umesikia, muangalie na mfikirie jinsi gani ambavyo Wenyeviti wa Vijiji, iwepo sheria kabisa ya kutamka kwamba walipwe shilingi fulani, badala ya kusema Halmashauri zichangie asilimia hii itakuwa haiwezekani, kwa sababu kama Serikali wenyewe tumeshindwa kupeleka fedha kwa wakati, Halmashauri ambazo nazo zinategemea mapato ya ndani zitumie katika zile fedha ambazo Serikali ilikuwa ilete, kweli Mwenyekiti atapata hiyo fedha? Kwa hiyo tuiangalie, tuitungie sheria ili Wenyeviti walipwe, inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna jambo lingine naomba Waziri wa TAMISEMI uje utoe ufafanuzi, kwa sababu TASAF wanapeleka fedha kwa watu maskini ili kupunguza umaskini na yule mtu maskini ile fedha anaitumia kwa ajili ya kupika vitumbua, maandazi, anauza nyanya au mama lishe ili apunguze umaskini, lakini cha ajabu Halmashauri zetu zinakwenda kuwalazimisha kulipa ushuru wale watu maskini. Zinamwaga bidhaa zao, wanawekwa ndani kitu ambacho sasa hatujui tunawafanya nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, TASAF inapeleka fedha kupunguza umaskini, Halmashauri inaongeza umaskini kwa kuwatoza kodi na kuwanyanyasa. Naomba Mheshimiwa Waziri utoe tamko kwamba hizi kodi ndogondogo za hawa watu, ambao ni watu wa chini, maskini, ambao kwa kweli anatafuta fedha kwa ajili ya kununua unga ili aweze kupika ugali ale na familia yake, siyo biashara. Halmashauri zijikite kutafuta biashara zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha nyingi za Mfuko wa TASAF tunategemea kutoka nje, Serikali nafikiri imekuwa ikipanga fedha mara nyingi, lakini zile fedha hazijaenda kule. Nafikiri safari hii kwa kuwa tumeamua sasa kubadilika, kufanya kazi na kudhibiti mapato, basi Serikali ihakikishe inatenga fedha za kutosha na kuunga mkono kwenye Mfuko wa TASAF.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kuhusu ukubwa wa Wilaya ya Kilolo. Wilaya ya Kilolo lilishaletwa ombi awamu iliyopita, ikakubalika kwamba igawanywe, eneo ni kubwa lina takribani ukubwa ambao ni sawa na Mkoa wa Kilimanjaro , lakini mpaka sasa hivi siyo rahisi kwa mwananchi wa Kilolo kuona ile impact ya fedha ambayo inapelekwa kwenye ile Wilaya na kugawanya kwenye Kata zote. Kwa kuwa tayari mmegawa Halmashauri, tumepata Halmashauri ndogo ya Ilula, Serikali iamue ile iwe Halmashauri ndogo, hii iwe Halmashauri kamili ili baadaye muangalie uwezekano wa kugawa Jimbo hilo na kupata Jimbo lingine kwenye Wilaya zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika sehemu ya miundombinu. Wilaya ya Kilolo ni Wilaya ambayo ndiyo inayotegemewa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali, tatizo lake kubwa ni miundombinu. Miundombinu ambayo ipo ni ile ile ya miaka 10 iliyopita. Hivyo, nafikiri kwamba, barabara zetu ambazo tumeziomba zipandishwe hadhi, ikiwepo barabara ya kutoka Idete kwenda Itonya, Muhanga kwenda kutokea Morogoro, ipandishwe hadhi iwe barabara ya mkoa, ili iwe rahisi zaidi kufungua maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Kilolo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni suala la Wazee. Wazee pamoja na kuwa tumetamka kwamba wanatakiwa wapewe huduma bure pamoja na matibabu, lakini bado hatujawawekea utaratibu mzuri. Nashauri kwamba katika zahanati, dispensary na hospitali zetu litengwe eneo maalum kwa ajili ya huduma za Wazee, ili Mzee akifika pale hana sababu ya kukaa foleni kwa sababu sisi sote ni wazee watarajiwa, yale ambayo tunayafanya leo yatakuja kuturudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nina muda bado kidogo, zingumzie habari ya Wakuu wa Wilaya. Na-declare interest nilikuwa Mkuu wa Wilaya. Kazi ya Mkuu wa Wilaya ni kubwa, kwa sababu kinapotokea kipindupindu anayeulizwa ni Mkuu wa Wilaya, wanapotokea wafanyakazi hewa anayebanwa ni Mkuu wa Wilaya, unapotokea ujenzi wa maabara anayebanwa ni Mkuu wa Wilaya, yanapotakiwa madawati anayeulizwa ni Mkuu wa Wilaya, zinapoongezeka mimba mashuleni anayeulizwa ni Mkuu wa Wilaya, lakini uwezeshwaji wa Mkuu wa Wilaya bado haujakaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, OC ambazo wanapelekewa Wakuu wa Wilaya zinapita mikono mingi, nashauri kwamba isipunguzwe ile hela ya maendeleo ambayo imepangwa kwa ajili ya Mkuu wa Wilaya zipelekwe moja kwa moja kwake, kwa sababu haifurahishi kuona kwamba, Wakuu wa Wilaya wanakuwa ombaomba. Mtu ambaye anasimamia maendeleo na haki anatakiwa aombe hata mafuta, haipendezi!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, kama kifungu kipo kiende moja kwa moja bila kuguswa na RAS (Regional Administrative Secretary) au Mkuu wa Mkoa, kiende kwa Wakuu wa Wilaya moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amefanya leo nikapata nafasi hii. Lakini moja kwa moja niende kwenye mada. Kwanza nimpongeze sana Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Engineer Patrick Mfugale, lakini pia nimpongeze sana na Meneja wetu wa TANROADS wa Mkoa kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya barabara zetu za Kilolo. Wilaya ya Kilolo iko katika Mkoa wa Iringa, ukienda kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi inasema kwamba kila barabara inayounganishwa na Wilaya itawekwa lami. Barabara zote ambazo zinakwenda Wilaya za Mufindi na Iringa zina lami. Juzi kwenye swali langu niliuliza miaka saba imeanza kushughulikiwa, kati ya kilometa 35 ni kilometa saba tu ndizo ambazo zimewekwa lami, kwa miaka saba kilometa saba ndizo zimewekwa lami. Nilikuwa nauliza tu swali na hata juzi niliuliza kwamba kwa kilometa hizi zilizobaki ambazo ni karibu 28, je, ni kwa miaka 28 ndipo tutapata lami? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba Mheshimiwa Profesa wewe ni mtu makini na kilolo unaijua, umeshafika, hebu angalia uwezekano wa kuhakikisha kwamba, barabara ya kutoka Ipogolo kwenda Ndiwili - Ihimbo - Luganga - Kilolo inawekwa lami; walau tupate kilometa saba tu kwa mwaka huu wa fedha na mwakani ukitupa saba basi tutakuwa tumesogea, ili watu wawe na imani. Kwa sababu ukiangalia katika Mkoa wa Iringa maeneo ambayo yanategemewa kwa kilimo ni pamoja na Wilaya ya Kilolo. Sasa tusiposafirisha yale mazao yakafika kwenye Wilaya nyingine na baadhi ya Mikoa ambayo ina matatizo itakuwa ni tatizo. Kwa hiyo, nakuomba kabisa uhakikishe kwamba angalau mwaka huu tunapata lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nikushukuru kwa kuwa barabara hii ya Mkoa ilikuwa inashia Idete na juzi nilipokuwa nauliza swali langu na tulishaomba kwamba barabara hii kwa kuwa inakwenda kutokea Mkoa wa Morogoro kupitia Idete - Itonya - Muhanga mpaka Mngeta kwa Mheshimiwa Susan Kiwanga, ningeomba hizo kilometa 26 ambazo zimebaki pale, wala pale hatuhitaji lami tunahitaji tu pesa kidogo tuweze kuunganisha ili iwe rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nilisema kwamba leo hii ikitokea barabara ile pale Kitonga, aidha, pakaziba au pakabomoka uwezekano wa kwenda Morogoro unapotoka Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Mbeya na Iringa yenyewe inabidi uje Dodoma, karibu zaidi ya kilometa 400 za ziada. Kwa hiyo, ningeomba Mheshimiwa kwa kuwa ulituahidi juzi hebu angalia uwezekano wa kutusaidia hizo kilometa 26 za kwenda kutokea Mngeta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ningependa kuzungumzia barabara nyingine ambayo inaanzia Ilula - Mlafu - Wotalisoli - Mkalanga - Kising‟a mpaka Kilolo, barabara hiyo ni ya Mkoa na ninashukuru Mungu kwamba imeanza kufanyiwa kazi. Ningeomba tu kwa kuwa barabara ile ni ya mkoa ina vipimo maalum ambavyo inabidi vizingatiwe. Na sisi Kilolo tumeweka msimamo kwamba tusingependa kwa wafanyakazi ambao hawatumii utaalam wakatoka nje ya mikoa yetu. Kama barabara ya Kilolo inatengenezwa basi vibarua watoke Kilolo badala ya kutoka maeneo mengine ili iwe rahisi wao kulinda zile barabara zao, kuona kama kuna udanganyifu kutoa taarifa kwa viongozi kwamba hapa tunaingizwa mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pi kuna madaraja pale. Nashukuru mmetaja habari ya madaraja kwamba mtatusaidia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa kutenga bajeti kubwa ambayo haijawahi kutokea, asilimia alizotenga tuna uhakika kwamba umeme sasa utakuwa umefika sehemu zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba leo mnachozungumzia hapa ni suala la umeme. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda yuko pale bila ya umeme hatofanya chochote, lakini hamuelewi huo umeme mnaozungumza ni umeme gani. Umeme tunaozungumza sasa hivi ni ule ambao unatokana na nguvu za kule Kidatu, Kihansi na ule mwingine unaotoka kwenye bwawa la Mtera, yale maji yanatoka katika Wilaya ya Kilolo. Vyanzo vitano vya maji ambavyo vinajaza Kihansi vinaanza kwenye vyanzo ambavyo vinatoka kwenye Wilaya ya Kilolo, sehemu ya Muhu na Mkasi. Maji yanayojaza bwawa la Mtera yanatoka kwenye vyanzo vikuu ambavyo ni Mto wa Lukosi na Mto Mtitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishaongea na Mheshimiwa Waziri nikamwomba kwamba ni vema sasa tukaenda kule akatembea aone uhalisia. Kwamba wale wanaopika chakula kizuri wenyewe hawali. Mpaka hivi ninavyomwambia kuna Kata ya Kimala, Idete, Ukwega, Udekwa, Kising‟a, Nyanzwa na Mahenge wanausikia tu umeme kwenye bomba, wakati wakijua kabisa kwamba chanzo kikuu ni Wilaya ya Kilolo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa alishaniahidi kufika kule, naomba afike ili aangalie ni jinsi gani atanifikiria tuweze kupata umeme vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishauri tu, kwamba kwa kuwa mwaka wa juzi, mwaka wa jana tulikuwa kwenye kujenga maabara, maabara zile hazitakuwa maabara kama hakutakuwa na umeme, kwa kuwa sasa wananchi wenyewe hali zao si nzuri sana niiombe Serikali, Wizara ya Elimu ikishirikiana na Wizara hii tuweze kuhakikisha kwamba kwenye shule zote za sekondari ambako tumejenga maabara waweze kuingiziwa umeme, hilo atakuwa ametatua na ametusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine na-declare interest, nilikuwa Mkuu wa Wilaya, nikiwa Mkuu wa Wilaya nililetewa kesi hizi zinazohusiana na vinasaba, bahati nzuri nitazungumza yale ambayo ni ya ukweli na Mungu ananiona. Mfanyabiashara yule baada ya kukamatwa alikuja ofisini kwangu, baada ya kuja ofisini kwangu nikaomba watu wa EWURA waje, walipokuja walituelimisha jinsi gani watu wanavyotorosha mafuta. Baadaye alikubali kweli mafuta yale yalikuwa ni ya transit na alikuwa anakwepa kodi.
Baada ya kufanya utafiti ikaonekana kwamba zaidi ya wafanyabiashara 316,000 walikuwa wanakwepa kodi. Wafanyabiashara wa mafuta siyo mchezo ni ma-giant. Kwa hiyo, unaweza ukakuta kelele yote hii ambayo inapigwa hapa ni kwa sababu wale nao wana uwezo wao. Hivi jiulize, kama EWURA wasingeweza kudhibiti mafuta bei hii ambayo ipo sasa hivi ingekuwepo? Tulishafikia mpaka shilingi 3,000 kwa lita, leo tunanunua mpaka Shilingi 1,200 yanashuka, ni kwa sababu ya udhibiti mzuri wa EWURA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi EWURA wasikatishwe tamaa. Kwa sababu juzi nilisikia hapa kwamba hata tenda za kupata mtu wa kutoa vinasaba hazikutangazwa, kitu ambacho siyo kweli, zilitangazwa kwenye magazeti na kwenye tovuti na ushahidi upo, kwa nini tuseme uwongo? Naomba, badala ya kuwakatisha tamaa tuwape nguvu kitu gani tufanye ili mafuta yadhibitiwe, wananchi wetu bei zikipungua waweze kusafirisha mazao yao, waweze kusafiri, kwa sababu bila kudhibiti hiyo nawahakikishieni mifumuko ya bei haitapungua, itaongezeka. Nawaomba wasikate tamaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana watu wa EWURA, endeleeni na kazi hiyo, ongezeeni nguvu. Hawa ambao wanapambana nao wapo wengi wameshawakamata. Mtu anayekamatwa siku zote anakuwa na ugomvi na Polisi, akishaona Polisi anaona huyu mtu hafai. Tumuongezee. Mimi najua watu wameshaambiwa maneno hapa kama alivyosema yule bwana mdogo, siwezi kuwavunja, wana interest zao. Kama mtu ana interest a-declare interest hapa. Mheshimiwa Waziri asikate tamaa, moto ni ule ule, hapa kazi tu, kanyaga twende. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kuhusu viwanda. Kama tunakwenda kwenye viwanda, tumeamua Serikali yetu kuwekeza kwenye viwanda, umeme lazima uwe wa uhakika. Kuna sehemu ambazo tumeweka maeneo kwa ajili ya EPZA, ziangaliwe zile ili Processing Zone zile tuweze ku-process mazao na kuyapa thamani ili kuweza kuuza na kupata bei zinazofaa. Mheshimiwa Waziri wa viwanda apige kelele atakavyoweza, kama umeme hautafika itakuwa haina maana yoyote. Washirikiane vizuri na Waziri wa Kilimo kwa sababu viwanda vyake pia kama hakutakuwa na mageuzi ya kilimo hatafanya chochote! Kama wasambazaji wa pembejeo wataendelea kuwa wababaishaji hatafanya chochote, ubora wake utabakia kwenye vitabu na maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ulanzi unatengenezwa pale Iringa, tunashindwa kwa sababu ya umeme, hebu Mheshimiwa Waziri aje atembelee, wenzetu Kenya wanasema ni bamboo juicy, lakini ndiyo ulanzi huo huo. Ulanzi siku ya kwanza unakuwa ni togwa, togwa ni juicy, siku ya pili unakuwa mkangafu, mkangafu ndiyo unaanza kuwa pombe, siku ya tatu unakuwa mdindifu, mdindifu ndiyo unalewa, yeye alisoma Tosamaganga najua alikuwa anapiga ule! (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Mambo ya Ndani alisoma shule ya Tosamaganga na Naibu Waziri wa Maliasili alisoma Tosamaganga na wenyewe wanatoka Tosamaganga, kwa hiyo asiposaidia wakajenga viwanda atakuwa hajafanya kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nafikiri ni kengele yangu ya mwisho au bado?
NAIBU SPIKA: Bado Mheshimiwa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba kwa kweli tufanye hivyo na kuna mambo mengi, kuna sehemu nyingi, kuna viwanda kwa mfano hata kule Busega hawana umeme, wangepata umeme wangeweza pia angalau wakachinja hata wale ng‟ombe badala ya kuleta ng‟ombe Dar es Salaam kwenye malori wangeleta nyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hawawezi kuleta nyama kama hamna umeme, Eeh! hakuna mabarafu yale zitaoza zile. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie ili tupate umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja!

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie hoja hii. Mimi ninatoka Wilaya ya Kilolo ambayo iko Mkoa wa Iringa, Hifadhi ya Udzungwa asilimia kubwa ipo katika Wilaya ya Kilolo japo Makao Makuu yapo Morogoro. Kuna vijiji ambavyo vinapakana na Udzungwa National Park. Vijiji vya Msosa, Ikula, Udekwa, Mahenge, Wotalisoli na kadhalika kuna tatizo kubwa la mamba, tembo hasa katika kijiji cha Msosa. Kwa sababu maji ya Mto Lukosi ndiyo yanayosababisha wananchi wengi kuliwa na mamba na pia kuuliwa na tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi:-
(1) Tunaomba Wizara iangalie utaratibu wa kujenga post (Kituo cha ulinzi wa vijiji vile pale Msosa), kujenga miundombinu ya maji yaani tanki la maji na kusambaza kijiji kile ili kupunguza ajali za mamba.
(2) Ujenzi wa barabara ya kutoka kijiji cha Mahenge kwenda Udekwa, kilometa 25 tu.
(3) Kuna mapango makubwa katika kijiji cha Udekwa ambayo ni kivutio kwa watalii wa ndani na nje, ningeomba wataalam wafike waone.
(4) Kutelekezwa kwa kivutio cha Kalenga, sehemu ambayo kichwa cha Mkwawa kimehifadhiwa, familia ya Mkwawa wanalalamika na kuna uwezekano mkubwa wa kuomba kukizika kichwa kile.

Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi hii niweze kukushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuleta Azimio hili ili tuweze kulipitisha. Umechelewa kwa sababu mimi ni mmojawapo wa wachezaji ambao wamecheza miaka ya nyuma, baadhi ya kizazi kimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi mabaya ya madawa haya. Kwenye timu zetu ni kitu cha kawaida, wachezaji walio wengi wamekuwa wakitumia bangi, lakini kabla ya kuendelea kuchangia tupeane pole kwa timu yetu ya Taifa kwa jinsi ambavyo tumefanya vibaya juzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili tumechelewa, niungane na wenzangu na wewe jinsi ambavyo umewasilisha hapa, kwamba sasa twende mbele, lakini kazi kubwa ambayo ipo ni kwamba tunafanyaje? Ni nani watahusika katika kulisimamia jambo hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyojua ni kwamba vikundi vingi vya michezo nchini kwetu vimesajiliwa. Ningependekeza kwamba, ukienda nchi nyingine zilizoendelea hamuwezi kuanza ligi mpaka wachezaji wamepimwa afya zao. Kwa hiyo aina ya Madaktari ambao wanakuwa kwenye vile vilabu wanakuwa waliosajiliwa, ni Madaktari wa kweli, ili pale linapotokea tatizo kwenye timu yake, amegundulika mtu ambaye anatumia zile dawa basi wa kwanza kuadhibiwa ni yule Daktari ambaye alimpima afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nachangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri nilipendekeza kwamba sasa hivi umefikia wakati ikiwezekana lile Baraza la Michezo tulivunje, tuanzishe Shirika la Michezo. Kwenye Shirika la Michezo itakuwa rahisi zaidi lenyewe kutafuta fedha au kupata kwa wahisani au kuchangia au hata katika harambee ili liweze kuendesha, kusimamia timu za Taifa kwa udhibiti na kudhibiti dawa za kulevya, ni kazi yao. Leo inawezekana tunapitisha hapa sina hakika kama tulikumbuka kuweka bajeti hii ambayo inakwenda kutusaidia kufanya kazi hii ya udhibiti huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nilizungumza pia, hatuwezi kuendelea kufanya vibaya kwenye timu yetu ya Taifa. Ukiangalia, kama tungewapima wale wachezaji baadhi ungewakuta wanatumia, aidha kwa kujua au kwa kutojua. Kwa sababu dawa hizi zinaweza kutumika hata kwa kula vyakula tu. Kuna baadhi ya vyakula ambavyo vinaweza vikawa vinasababisha mtu kupata nguvu, yaani vikasababisha kupatikana na viashiria vya dawa za kulevya, vyakula ambavyo tunatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilipendekeza kwamba ili sasa timu zetu zifanye vizuri ni pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya madawa ya kulevya, sambamba na kuhakikisha kwamba wachezaji wanaotoka nje wanapunguzwa kwenye timu zetu. Kwa sababu wao wanakuwa bora tu pale vilabu vya Simba, Yanga, Azam vinapofanya vizuri na ukiangalia ndiyo wanaoongoza katika kufunga mabao, lakini unapokuja kutaka kuwatumia haiwezekani kwa sababu wao ni wa nje. Wachezaji wetu wa ndani tayari wanakuwa wamekata tamaa. Badala ya sasa kuitunza miili yao wanakwenda kwenye kuanza kutumia madawa ya kulevya ili wapate nguvu wafanane na wale wa nje, ambapo wenzetu lishe ndiyo bora kuliko kitu kingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Hafidh Ali amekuwa ni referee wa Kimataifa, amechezesha African Cup of Nations, amechezesha World Cup ya Vijana. Mchezaji kama Filbert Bayo mwanariadha, amekimbia Gidamis Shahanga na wengine wengi tu wamefanya vizuri kwa sababu walikuwa wanafuata zile ethics za michezo yenyewe. Leo hii itakuwa ni kazi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kiundwe chombo kizuri cha jopo la Madaktari kuweza kutusaidia kutupa ushauri na kuweza kuangalia jinsi gani tunaweza tukawa tunawapima wachezaji wetu wote kabla ya kushiriki kwenye michezo. Kabla ya kuanza ligi daraja la kwanza, la pili wanakuwa wamepimwa aki-qualify ndipo anaingia, asipo-qualify basi tunam-disqualify, anakuwa hayupo tena kwenye mashindano.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nakutakia kila la kheri katika utekelezaji.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kukushukuru wewe na kukupongeza kwa kufika huu mwaka salama kwa sababu kuna wakati kidogo afya iliyumba, Mungu akubariki kwa sababu tunakuhitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kuwapongeza Mawaziri wote, Mheshimiwa dada yangu Kairuki pamoja na Mheshimiwa George Simbachawene na Mheshimiwa Waziri wa Sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia katika Utawala Bora. Kabla sijaanza kuchangia nitoe pole sana kwa wananchi wa Jimbo la Kilolo kwa accident ya bus ya Vitu Laini ambayo ilitokea hivi karibuni na kuua watu wengi na jana pia ndege moja ndogo ilianguka katika Jimbo la Kilolo, nawapa pole sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia; jana Mheshimiwa Rais alipokuwa kwenye shughuli ile ya haki kuna kitendo ambacho kilitokea pale, kitendo cha yule mama ambaye alipiga kelele alihakikisha kwamba anapata nafasi ya kuongea na Mheshimiwa Rais, lakini ukifuatilia malalamiko ambayo yule mama alikuwa anayalalamikia ni utawala bora. Kwamba ameingia kila mlango lakini alikosa kusikilizwa na kupewa haki zake. Ameingia Mahakama zote yule mama ameshindwa kusikilizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa najiuliza hivi ni akinamama wangapi hasa wajane ambao wanakosa haki zao? Je, watakuwa na ujasiri kama ule? Hii ni changamoto kwetu viongozi kwamba kama hatuwasikilizi watasubiri mpaka Mheshimiwa Rais atakapokuja kwenye mikoa yetu na wilaya zetu ndipo wasimame haki zao zipatikane. Naomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia tunafanyaje jambo hili. Kuna watu wale wa Haki za Binadamu nafikiri wapo, kile kitengo nafikiri kikiimarishwa kikapewa nguvu kingeweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukienda Mahakamani kesi zinachukua muda mrefu, ukienda mahabusu na magereza zetu zimejaa, lakini ukienda pale kesi ambazo mimi nikiri nilishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya, nilikuwa naingia mara kwa mara kwenye magereza, unaweza ukashangaa kesi nyingine siyo za mtu kukaa mahabusu, ukikaa pale utashangaa. Nafikiria sasa ni wakati muafaka Jeshi la Polisi na Mahakama wakashirikiana, sio lazima mtuhumiwa akituhumiwa leo lazima akamatwe leo, upelelezi unaweza ukafanyika akiwa hata bado hajakamatwa, wakati anakamatwa basi moja kwa moja upelelezi unakuwa umekamilika na haki inatendeka, aidha, kuachiwa au kufungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamelalamika kuhusu utendaji wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Kwanza nianze kwa kuwapongeza kwa sababu wenyewe wamekiri kwamba hawajapata semina. Mimi niwape tu semina kidogo ndugu zangu hasa Wakuu wa Wilaya kwa sababu na mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya, kwamba maamuzi yao yazingatie taratibu na haswa washirikishe Kamati zao za ulinzi na usalama, siyo kuanza tu kutoa maamuzi bila kushirikisha ile Kamati ya ulinzi na usalama. Naamini wakishirikisha Kamati ile basi busara zitatendeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia washirikishe vyombo na taasisi za dini, kuna wazee maarufu, linapotokea jambo haina haja ya kukurupuka, lazima usikilize pande zote mbili ndipo utoe maamuzi. Kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao ni watendaji wazuri tunaweza tukawapoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia awamu hii imesaidia sana kutia nidhamu kwenye kazi. Leo hii ukienda Ofisi yoyote ukikaa pale kwenye benchi huwezi kukosa mtu wa kuja kukuuliza kwamba bwana una shida gani, umesikilizwa? Kwa hiyo, nikupongeze Mheshimiwa Kairuki kwamba sasa watumishi wanaanza kurudi kwenye line isipokuwa tu Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na Watendaji wengine wapunguze, wawasiliane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linasikika sana kwa sababu nao kwa kiherehere wanataka kila jambo litoke kwenye vyombo vya habari, mambo mengine yanakuwa kimya kimya, ukitaka kila kitu kitoke madhara yake ndiyo hayo. Hiyo nidhamu ni nidhamu ya uwoga, waache uwoga wafanye kazi wataonekana tu. Mheshimiwa ameshajua nani atabaki na nani ataondoka, wasiwe na wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la TASAF. Niseme wazi kwamba suala la TASAF ni kitu kizuri, niwapongeze sana TASAF kwa kazi nzuri ambayo wanafanya. Mimi ni Mjumbe wa TAMISEMI tumezunguka mikoa mingi, tumeangalia kazi ambazo zinafanyika na nyingine ukienda kama Pemba kule unaweza kushangaa mambo ambayo wanayafanya, wameenda mbali zaidi na sasa hivi wanafanya na mambo ya uchumi kwa kutumia fedha zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwa kuwa baadhi ya sehemu kumeonekana kuna matatizo turekebishe yale matatizo, tatizo kubwa lipo kwa Watendaji wa Halmashauri zetu, kwa sababu hawa Watendaji ndiyo wanapelekewa pesa, kwa hiyo, wao kwa sababu ya mazoea ya miaka ya nyuma walishindwa kubadilika. Sasa hivi nafikiri tukae tuone tunafanyaje ili TASAF iweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiri wazi hata Waheshimiwa Wabunge mmeona msongamano wa wale watu ambao walikuwa wanahitaji msaada kwetu umepungua, umepungua kwa sababu ya TASAF; wengi wanakuwa wamemaliziwa matatizo yao huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kabisa ni ajira. Tunashukuru sana kwa kazi ambayo mmeifanya, mmefanya uhakiki vizuri sana tena tunakuombea na Mungu akubariki. Sasa kazi iliyobaki ni ajira maana vijana ambao tumewasomesha sasa wasije wakaingia kwenye mambo mengine mabaya, juzi Dangote alitangaza kazi za udereva walioomba wengi ni kutoka Vyuo Vikuu kwa sababu hakuna kazi. Kwa hiyo, nafikiri wewe tangaza ajira na hivi umeshaanza basi wengi watapata na mimi niombe kwa kupitia nafasi hii vijana watulize munkari kwamba ajira sasa zitamwagwa na Serikali yetu hii itatujali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kwa sababu muda ninao nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu. Kwa kweli kazi aliyoifanya ni kubwa, mabadiliko tunayaona na mwenye macho haambiwi tazama anaona mwenyewe, kazi iliyobakia ni sisi kuwasaidia. Tuwasaidie tufanye kazi tuwe kitu kimoja ili tusonge mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kanyaga twende, ahsante kwa kunisikiliza.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's