Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi, lakini juu ya hayo namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukamilisha uchaguzi. Nawashukuru wapiga kura wa Biharamulo na Watanzania kwa ujumla kwa kukamilisha zoezi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea nina maneno machache ya utangulizi. Siku moja nilikuwa kwenye benki moja ambayo sitaitaja jina, nikakumbana pale kwenye meza ya huduma kwa wateja na mzee mmoja ambaye alikuwa na malalamiko yanayofanana na ya kwangu. Yeye anasema ameweka kadi kwenye ATM, karatasi ikatoka kwamba pesa zimetoka, lakini pesa hazikutoka, nami nilikuwa na tatizo kama hilo. Alipowaeleza wale wahudumu, wakaja kama watano wanaeleza namna ambavyo mfumo wa computer unafanya transaction na maelezo mengi ya kitaalam. Yule mzee akawaambia vijana sikilizeni, mimi kama mteja wa benki yenu nina kazi mbili tu, nina kazi ya kuweka pesa na kutoa pesa. Hiyo habari ya mchakato unakwendaje, transaction system kazungumzeni huko halafu mje na pesa. Kwa nini nasema hivyo? Watanzania hawa ambao wanalitazama Bunge hili nao wana kazi tatu…
MBUNGE FULANI: Hawasikii hao!
MHE. OSCAR R. MUKASA: Vyovyote, watafahamu na watasikia, kuna namna watasikia. Wana kazi ya kufanya kazi, wana kazi ya kulipa kodi na wana kazi ya kudai huduma kwenye sekta mbalimbali basi, hawana kazi nyingine. Kazi hizi za kwamba kanuni iko hivi na nini ni muhimu, lakini mwisho wa siku wao wanataka matokeo.
Leo Mheshimiwa Zitto Kabwe, sijui kama yupo, huwa namheshimu sana, lakini leo amenishangaza. Amefanya…
Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana rafiki yangu Zitto ni Mbunge makini. Nakwambia wewe Mwenyekiti, namheshimu sana Mheshimiwa Zitto, ni Mbunge makini na ninyi mnafahamu; lakini leo na siku chache zilizopita nimeshangaa kidogo na namwomba asiendelee kunishangaza.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Kwamba Ijumaa Bunge lilipoahirishwa nimefanya hesabu ya haraka haraka, nakubaliana kabisa kwamba kazi ya wapinzani ni kuisimamia Serikali na hawakuja hapa kuishangilia, hilo linafahamika kabisa. Hata hivyo, kazi hiyo lazima ifanyike kwa namna ambayo ina maslahi kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ijumaa lilipoahirishwa Bunge, kwa hesabu ya haraka haraka, kwa kutofanya kazi kuanzia saa tano ile mpaka muda uliopaswa kufanywa zimepotea kama milioni thelathini na tatu. Zimepotea kwa sababu mmoja wa Wabunge alitaka kuonesha namna anavyoweza kusoma Kanuni. Ungeweza kuonesha unavyosoma Kanuni, lakini ukawaacha Watanzania salama kwa kutotumia hela yao vibaya. Watanzania wanatarajia matokeo, lakini Wabunge wenzangu wa CCM na mimi nakuja kwenu. Tuna kazi ya kuisimamia Serikali, nje ya Bunge kwenye vikao vyetu na tuna kazi ya kuisimamia Serikali hapa ndani. Kilichotokea Ijumaa na yaliyotaka kutokea leo ni dalili kwamba kazi yetu Wabunge wa CCM hatujaifanya kwa kikamilifu. Huo ndio utangulizi kwa Wabunge wa CCM na Wabunge wa Vyama vya Upinzani. Watanzania wanatarajia matokeo, hawali Kanuni, hawali Sheria. Nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuchangia Mpango wa Maendeleo, napenda kuwa na kipaumbele kimoja ambacho ni mtambuka. Kipengele ambacho ni mtambuka, kwangu ni namna gani jitihada zetu za kukuza uchumi zinaendana na maendeleo ya uchumi. Ni namna gani chochote tulichokiandika kwenye mipango hii kinakwenda kugusa maisha ya mwananchi wa kawaida. Tukijenga reli, tukazungumzia barabara, tukazungumza yote hayo, kama hayagusi maisha ya mwananchi wa kawaida, Watanzania hawatuelewa, tutakuwa tunaimba wimbo wa kila siku ambao hauna tija kwao, wakati wao kazi yao ni kuona maisha yao yanabadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano, ukurasa wa 27 wa hiki kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo unazungumzia namna ya kufunganisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu. Wanaonesha dalili hizo kwamba wanataka kusema hivyo, lakini ukienda kwenye maandishi kwa ndani, kwenye maudhui yenyewe, maeneo mengi huoni namna ambavyo Mpango huu unakwenda kugusa maisha ya mtu wa chini kabisa, nitatoa mifano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, tumezungumza barabara, lakini utaona hapa tunazungumza barabara kubwa tu; za Mikoa, barabara za Wilaya, lakini ndugu zangu nikumbushe kitu kimoja. Barabara kubwa ya lami ina maana, lakini kama kule kijijini anakoishi mwanandhi, ndani Kijiji cha Kalenge, Kijiji cha Kitwazi hakufikiki hata kwa baiskeli, hata kwa pikipiki, maana ya barabara kubwa inapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetarajia tuone namna gani sasa tunaweza kuweka mipango ya kushuka chini. Wakati tunajenga barabara kuu zinazotuunganisha na mikoa umefika wakati sasa hata barabara zile zinazotoka (feeder roads) zinazokuja kukutana na barabara hizo ionekane wazi kabisa kwenye mpango kwamba sasa mwelekeo wetu ni kwenda kugusa mawasiliano ya barabara kwa mwananchi aliye kijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu, ukiangalia kwenye elimu hapa kwenye utekelezaji na kwenye vipaumbele, utaona tunaongelea maabara, madarasa, lakini mwalimu tunasahau kwamba ndiye mfanyakazi wa umma wa nchi hii ambaye anafahamika anapofanya kazi, lakini hafahamiki anaishi wapi. Hatuzungumzii nyumba za walimu, hatuweki mkakati nyumba za walimu miaka nenda rudi, tunazungumza mambo ya maabara. Ni mazuri, lakini ukipita kwa mwalimu utakuwa umegusa mengine yote kwa upana na kwa namna ya kwenda kubadilisha maisha ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara, nimeshangaa sana kwamba pamoja na kwamba nimezungumzia habari ya feeder roads, nashangaa sana kuona kwamba siioni barabara ya kutoka Bwanga kwenda Kalebezo, barabara inayounganisha Mkoa wa Geita na Mkoa wa Kagera na nchi jirani ya Rwanda; barabara ambayo inakwenda kwenye Wilaya mama ya Rais anayeongoza nchi hii. Alikuwa mgombea wa Ubunge mara mbili pale Bihalamuro, lakini Mikoa hii ya Geita na Kagera kama haitaunganishwa na nchi jirani kwa kiwango kinachostahili tunaua biashara pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, unaona pale kwenye utekelezaji wanaongelea tu hospitali za rufaa, ni vizuri kabisa. Hata hivyo, hospitali za rufaa bila kuweka nguvu kwenye zahanati na vituo vya afya hatutagusa maisha ya watu. Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ya Dar es Salaam au ya Bugando ni muhimu iwepo lakini haina maana kama mtu hawezi hata kupata mahali pa kupata huduma ya kwanza ili aambiwe nenda rufaa. Ni lazima mpango huu ujikite kwenye zahanati na vituo vya afya kwamba sasa tunakwenda kuwagusa ili wakishindwa kutibiwa pale ndipo waende kwenye hospitali kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujumbe wangu ni kwamba, mipango yote tunayoiweka tuwe na kipaumbele mtambuka ambacho kinasema chochote tunachokifanya lazima kionekane wazi kwamba kinakwenda kugusa maisha ya mtu wa chini, vinginevyo maana yake inapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nawaombea kila la kheri Waheshimiwa Wabunge wa CCM tuisimamie Serikali, lakini na Wabunge wa Upinzani tuibane Serikali kwa namna ambayo inaleta tija kwa wananchi. Nawashukuru sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia na mimi kwenye Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, nawashukuru Wabunge wenzangu wote kwa kazi tunayoifanya, nakupongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha vizuri, ukisikiliza unaona kabisa matumaini kwamba amejipanga kwa maana ya kufikiria na kuweka mkakati, lakini nina haya ya kusema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu moja ambayo nadhani ni vizuri tuitazame na inaendana kidogo na msemaji aliyetangulia, Mheshimiwa Waziri uangalie pia namna ya kufanya kitu kinaitwa tathmini ya mambo ambayo yanaweza kuwa hatarishi kwenye hii mipango uliyoiweka na mambo ambayo yanawezesha utekelezaji wa mipango uliyoweka, SWOT analysis. Kwa sababu yako mambo ambayo pamoja na mipango mizuri ambayo ukiisikiliza hii hotuba unavutiwa lakini yasipofanyiwa kazi hatufanya lolote kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza wakulima wa Wilaya ya Biharamulo, Ngara na Bukombe na jirani huko kwa sababu wote tunawasiliana wanajiandaa, ni kutengeneza mishale sasa hivi kwa sababu wafugaji tarehe 15/06 wanatoka kwenye hifadhi kurudi huku. Kwa hiyo, haya yote tunayoandaa kama hatukabiliani na mambo haya ambayo ni hatarishi kwa mipango hii ni bora tu tukaongeza bajeti kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo itakwenda kutuliza ghasia kuliko kuweka mbolea na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu limekuwa sasa ni jambo la kawaida, unakumbuka Mheshimiwa Waziri, namuomba anayemsemesha Waziri wa Kilimo atupe nafasi kwa sababu tunaongea mambo makubwa. Mwenyekiti naomba unilinde, naongea na kiti lakini Waziri mhusika asikie.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu imekuwa ni kawaida sasa tarehe 27/28 Disemba, sikumbuki exactly tarehe ila wiki ya mwisho ya mwezi wa Disemba, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo akiambatana na Naibu Waziri wa Maliasili walikuwa Benako pale mpakani mwa Biharamulo na Ngara kwa sababu tulikuwa tumewaita kwenda kutatua mgogoro kama huo ambao ulikuwa unataka kutokea watu walikuwa wameandaa mishale. Leo pia mimi Mbunge wa Biharamulo badala ya kujadili mkakati sasa najadili namna gani tuzuie mapambano ili baadaye tuje kwenye mkakati, kwa hiyo, hili suala limekuwa la kawaida sasa.
Kwa hiyo, tusipoondokana na hili tunapoteza muda na tunapoteza muda kwa mambo ambayo yako ndani ya uwezo wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nateta na mtu mmoja hapa naambiwa Rwanda ndiyo wanapeleka mzigo mkubwa wa nyama ya ng‟ombe Congo lakini ng‟ombe hao wanatoka Tanzania, Ngara, Biharamulo, Bukombe sasa sisi ni waajabu, wanatushangaa. Kwa hiyo, badala ya kugeuza mifugo hii iwe neema tunaigeuza kwamba ni sehemu ya kuanzisha mapambano kati ya wakulima na wafugaji. Tuondoke hapo ndipo tutaweza kuongea mambo haya kwa maana ya kuweka mikakati na kwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza hapa hali huko kwa kweli ni mbaya. Ukizungumza na mfugaji Biharamulo, Ngara, Bukombe sasa hivi hamuwezi hata kuongea lolote ni tarehe 15 imekaribia, tunafanyaje, tuondoke hapo Mheshimiwa Waziri na tunataka tuweke nguvu kubwa kwenye kutatua jambo hili, tumalize tufanye mambo mengine. Wakulima wamechoka, wafugaji wamechoka, Wabunge hatufikirii jambo lingine, unafikiria tu wafugaji na wakulima kila asubuhi, kila jioni. Tunaharibu rasilimali na akili tulizozileta humu Bungeni, tumalize jambo hilo twende kwenye jambo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo za kilimo. Mwezi Disemba nilikwenda kijiji kimoja kinaitwa Ntumagu kiko Kata ya Nyanza - Biharamulo. Nimefika pale kabla sijaongea ajabu wananchi mara nyingi wanapenda tunazungumza halafu nao wanapata nafasi ya kuzungumza, wakasema leo tunaanza sisi. Wakaniambia wewe bwana tunajua umekwenda shuleni, unasema sijui una digrii ya ngapi, Mkuu wa Wilaya tumesikia ana digrii moja, mbili, Mkurugenzi ana digrii mbili, Bwana Shamba alikuja hapa juzi ametuletea mbegu za kupanda wakati sisi mahindi yameshafika kiunoni naye tunaambiwa ana digrii moja, sasa mna digrii zote hizo lakini hamjui mahindi yanapandwa lini ni nini? Wananchi wanashangaa. Nalo tumelisikia kwenye hotuba lakini limekuwa linasemwa tena na tena hata tukiwa na mipango mikubwa sana huku juu kama yale ambayo ndiyo yanawagusa wananchi hayafanyiki yote haya mengine yanapoteza maana yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa yale mambo yanayogusa wananchi tumetaja la kwanza, vurugu za wakulima na wafugaji zishughulikiwe. Mheshimiwa Maghembe anasema ni tarehe 15 anakwenda kuwatoa wafugaji wote kwenye hifadhi, ni jambo zuri kwa sababu hawapaswi kuwa kwenye hifadhi, lakini si tupange? Mkulima anatekeleza wajibu wake, analima mpunga, mahindi, tunanunua tunakula, mfugaji naye anatekeleza wajibu wake, tukienda butchery pale hatuulizi kwamba naomba kilo tano; mbili za ng‟ombe aliyekula hifadhi halafu tatu za ng‟ombe wa maeneo mengine, hatusemi hivyo. Tunaomba kilo tano tunapewa ametimiza wajibu wake. Serikali yenye wajibu wa kuwapanga ili haya yote yafanyike haitekelezi wajibu wake. Kwa hiyo, tunapoteza muda kufikiria migogoro badala ya kwenda kwenye mambo ya mkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni hilo tumesema linagusa wananchi, habari ya pembejeo ambalo tunaomba pamoja na michakato yote zifike kwa wakati. Baada ya kuongea na wale wananchi walioniambia mbolea ya kupandia imefika wakati mahindi yamefika kiunoni nilikwenda kuongea na watu wa Halmashauri, nikakutana na Bwana Kilimo pale. Nilivyomuelezea akanipa story nzuri ambavyo mchakato wa kufikisha hiyo mbolea kwa mwananchi ulivyo, ikitoka hapa inafika pale lakini haya ni maelezo tu, mwananchi hayamsaidii. Kinachomsaidia ni pembejeo kufika kwa wakati ili apande kwa wakati tupate tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukanda wa wafugaji ambao unajumuisha Biharamulo, Ngara na Bukombe na kwingine wana umoja wao. Wakikupa takwimu utashangaa, wanasema kwa wastani kwa mwezi kuna kodi wanailipa kwa njia ya rushwa kwa hao watu wanaowafukuza kwenye hifadhi ya karibu milioni 30 mpaka 50. Kwa hiyo, kodi hiyo hiyo tukitafuta namna ya kuigeuza iwe halali itatusaidia hata kuwapanga hawa, lakini inatoka kwa mwezi na wenyewe wametunza takwimu vizuri kabisa lakini ni kodi ambayo inakwenda kwa njia ya rushwa kwa sababu watu wanatengeneza tu mazingira kwamba leo tukafanye doria, tutaondoka na milioni 30, kesho tukafanye hivi. Kwa hiyo, tutumie rasilimali tuliyonayo kwa njia ambayo inaleta tija ili kodi hiyo hiyo ilipwe kihalali badala ya kulipwa kwa namna ambayo haifaidishi Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya 30% ya mifugo ya ukanda ule inapata chanjo na hao wafugaji wanasema wao wako tayari hizo huduma zikipatikana wanazilipia tu. Ukiweka mfumo sahihi wa kulipia huduma hizo ina maana una mfumo sahihi wa kuweka takwimu, una mfumo sahihi wa kufuatilia kodi na wao wako tayari kulipa kodi. Hivi tunavyozungumza wafugaji wa ukanda ule wanalipa tu ushuru wa Halmashauri lakini hakuna namna wanalipa kodi ya Serikali Kuu na ukizungumza nao wanasema wako tayari, sasa hiyo potential tunayo mbona hatuitumii? Ukishatatua suala la wafugaji umetatua la wakulima kwa sababu sasa hivi mkulima ambaye angekuwa anafikiria afanyeje kwenye msimu unaokuja anafikiria namna gani atapambana na hawa jamaa watakavyotoka msituni huko kwenye hifadhi tarehe 15/06.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limekuwa tatizo sugu na sisi wananchi wa ukanda ule tunadhani sasa inatosha. Kwa hiyo, tunamuomba Mheshimiwa Waziri afanye uratibu na Wizara nyingine zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuambiwa siku moja kwamba tunawafukuza hawa wafugaji kwenye hifadhi kwa sababu wako wengine wanatoka Rwanda, sasa hiyo siyo kazi ya mfugaji wa Tanzania kujua kwamba huyu ni wa Rwanda asiwe hapa ni kazi ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwa hiyo, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Mambo ya Ndani na wa Maliasili wakae waseme huyu ni mfugaji wa Tanzania afuge, alipe kodi, awekewe miundombinu lakini unakuta kiongozi anasema kabisa tunawafukuza kwa sababu wako wafugaji wa Rwanda, sasa hii siyo kazi ya mfugaji wa Tanzania.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kuzungumza leo kwa niaba ya wananchi wa Biharamulo, lakini nawashukuru Wabunge wote waliotangulia kuzungumza kwa michango yao mizuri sana ya kuisimamia Serikali yetu, Wizara hii ya Elimu, Teknolojia na Ufundi. Kwa namna ya pekee pia nakupongeza Waziri na timu yako kwa kazi nzuri, lakini nina haya ya kukuambia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako makubwa, watu tuna matumaini na wewe Mheshimiwa Waziri, lakini unaingia kwenye Wizara ambayo yako hata madogo ambayo umekuta haiwezi kuyafanya. Sasa una kazi kubwa mbele hapo! Naanza na mfano mdogo tu halafu nitakuja kwenye hotuba yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 kijana aitwae Kuzima Suedi wa Biharamulo, Shule ya Sekondari Kagango, alikuwa miongoni mwa vijana kumi bora wa masomo ya sayansi Kitaifa. Akafurahi sana na sisi tukafurahi sana! Wizara ikamwalika kwenye Wiki ya Elimu mwaka 2015 hapa Dodoma, akaja mzazi, Afisa Elimu, chereko chereko nyingi! Mgeni Rasmi akatoa zawadi kwa watu wachache, akasema waliosalia akiwemo wa Biharamulo, zawadi yao ya laptop na cheque itawafuata. Mpaka leo ni kuzungushana! Afisa Elimu wa Mkoa, wa Wilaya! Hayo ni madogo tu, nakuja lingine la utangulizi kabla sijaja kwenye hotuba. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii habari ya watoto wetu wa kike wanapopata ujauzito kuondolewa shuleni, nafikiri tusilitazame kwa namna tu ya haki yao ya kusoma, nadhani tulipe picha ya ziada. Hii ni habari ya mfumo dume ambao tunauendeleza kwa kiwango kikubwa sana. Mimi najiuliza jambo moja, linapofanyika lile tendo, ni mmoja tu ambaye masikini matokeo yake yanaonekana hadharani, tumbo linakuwa kubwa. Kungekuwa na utaratibu kila mwanaume anayempa mtu ujauzito naye anavimba nundu tunaona, tungejua na mtu mwingine wa kufukuza; kwamba wa kike anafukuzwa shule, wa kiume kama ni mwanafunzi mwenzake naye anafukuzwa; kama mwanaume ni Mwalimu, ama Mbunge, ama Polisi naye anakamatwa siku hiyo kwa sababu ana nundu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunawaonea hawa kwa sababu sisi ushahidi wa kwamba tumeshiriki kwenye hilo, hauonekani mara moja, mpaka tutafute tafute, tunakaa kubishana jambo ambalo liko wazi. Hebu tuwape haki wanawake! Tutafute namna ya kuwezesha watoto wetu wa kike wasipate ujauzito; hiyo ndiyo kazi ya kwanza, lakini inapotokea bahati mbaya limetokea hilo, tusiwahukumu peke yao. Huo ndiyo ujumbe wangu wa kwanza. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja sasa kwenye mchango. Ukiangalia kitabu cha hotuba pale sura ya kwanza, picha ya kwanza kabisa, umeweka picha ya Mheshimiwa Rais na kuna nukuu ya maneno anayoyasema kuhusu elimu; anamalizia, “Serikali ya Awamu ya Tano, itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa, ni pamoja na kuongeza mkazo katika masomo ya Sayansi. Hiyo ni nukuu. Tunapozungumza hivi, Biharamulo Wilaya nzima, tuna Walimu 560; Walimu wa Sayansi 30; lakini ukiangalia ukurasa wa 19 wa hotuba hii, umeeleza, “katika udhibiti wa ubora wa elimu kwa mwaka wa fedha huu unaokuja, Wizara imepanga kufanya yafuatayo.” Yametajwa mengi pale, lakini sioni mkakati wa kushughulika na suala la Walimu wa Sayansi. Hakuna hata pale! Sasa tunaongea tu nadharia lakini hatuweki mikakati; hatuwezi kutoka hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dunia ya sasa kama tutaendelea na Walimu 30 wafundishe shule 18 zenye wanafunzi 8,900, Walimu 30 wa Sayansi, hatuwezi kutoka tulipo. Inabaki ni jitihada za Afisa Elimu tu kule Biharamulo masikini anahangaika, hivi tunavyoongea ana Walimu wanane wanaojitolea. Amenituma nikuombe uhakikishe kwenye mgao unaokuja kwa sababu ni walimu na wana degree na walishajitolea pale, usiwatoe pale. Usije na ubabe baadaye kwamba sisi tunakupangia uende tunakotaka sisi, wakati wamejitolea mwaka mzima pale kabla wewe hujaweza kulipa. Nitakupa majina uwaweke pale, kwa sababu wameshajitolea na wanaipenda Biharamulo na wana sababu kwa nini walijitolea bila kulipwa wakiwa Biharamulo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije habari ya mitaala. Mwaka 2014 kama siyo mwaka 2015 mlibadilisha mitaala kwa Darasa la Kwanza na la Pili, mkaondoa masomo sita, mkaleta kusoma kuandika; KKK tatu zile. Hivi tunavyozungumza, watoto walio Darasa la Tatu, Walimu wa Kiingereza hawajui wawafundishe kuanzia wapi, kwa sababu walisoma Kiingereza mpaka mwezi wa Tano mwaka 2015, wakiwa la Pili. Mtaala mpya wa Darasa la Tatu unaochukua hali ya sasa, kwamba Kiingereza kianze Darasa la Kwanza haupo. Kwa hiyo, Walimu wanabahatisha tu; na watakaoingia Darasa la Tatu mwaka 2017 wana habari hiyo hiyo. Hatuwezi kufika kwa mtindo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza, nina vitabu vitatu; viwili vya sayansi Darasa la Saba; kimoja cha sayansi Darasa la Sita. Nchi hii ukiwa Darasa la Sita ubongo wako una sehemu tatu, ukiwa Darasa la Saba ubongo una sehemu nne. Tutakwenda kweli? Hebu imarisha hivyo vitengo vya ukaguzi, tujue tunawafundisha nini wanafunzi kwa standard na consistence. Tutapanga mipango mikubwa kabisa, ambayo ukisoma kwenye makaratasi inaingia akilini, lakini uhalisia kule chini ni shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu Wizara, hebu tusikie, Waheshimiwa Wabunge wamesema sana kuhusu Walimu, ni Sekta ya Elimu tu ambayo ukitaka kujenga darasa ni lazima Mtendaji wa Kata amkimbize mwananchi kuchanga, lakini sijawahi kusikia Mtendaji wa Kijji anamfuata mwananchi kumkamata achange pesa ya umeme wa REA. Tumeweka kwenye mfumo. Sijawahi kusikia Mtendaji wa Kijiji anamfuata mwananchi kumkamata achange mfuko wa barabara ili tujenga lami; hakuna! Hata hivyo anachanga na tumeweka kwenye mfumo. Ni darasa tu na nyumba ya Mwalimu ndiyo lazima wakimbizwe na Mtendaji wa Kata, hebu tuondoke kwenye ujima, tutafute tozo kwenye kodi ambazo tutakamata Sekta ya Elimu na mundombinu yake, tushughulike nayo kama Taifa, ndiyo tutaondoka kwenye hali hiyo.
Napenda pia kuongelea kidogo COSTECH, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia. Hebu tuiwezeshe! Tunataka huo ubunifu waanze kuufanya kuanzia kwenye Shule za Sekondari, wawezeshwe waende kule; wawezeshe Walimu kutambua vipaji mapema, namna gani tutashughulika navyo, kikiwa kipaji bado kiko Biharamulo, kiko kidato cha pili, kipaji kiko kidato cha tatu, tunakijua kipo na tunapanga mpango wa kukiendeleza na kukikamata kitakapofika Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi tena kwenye hoja ambayo nilitaka kuisahau kuhusiana na vitabu vyetu mashuleni. Kuna kitabu kimoja nimekutana nacho kwenye shule moja huko, kimoja kinasema tuna sayari tisa, kingine tuna sayari kumi. Sasa mimi nikachanganyikiwa, hawa watoto wakitoka hapo unataka huyu huyu ndiye aje kushiriki kwenye dunia ya sayansi na teknalojia? Haiwezekani na hatutafika kwa mwendo huo, nashukuru. (Makofi)
MHE. OSCAR R. MUKASA: Ni kengele ya kwanza?
MWENYEKITI: Ya pili Mheshimiwa

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya hatukuweza kuona performance report ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha tulionao. Endapo ningepata fursa ya kuona ripoti hiyo, kungekuwa na fursa ya kusema yafuatayo kwa takwimu zaidi. Kuna dalili nzuri kwenye viashiria vya uchumi mkubwa (macro economic indicators), lakini kuna kila dalili kuwa tunaporomoka kwenye micro economic indicators.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu ni kwamba mpango wa 2017/2018 pia hauonekani kuzingatia upungufu huu. Mfano, tungeweka nguvu kubwa kwenye viwanda vya kiwango (size) ya kati badala ya vikubwa ingekuwa rahisi kuweka kichocheo kwa sekta ya kilimo kwenye mikoa tofauti tofauti kwa kuzingatia zao la kilimo linalopatikana eneo husika. Tuwe na mtiririko (sequence) sahihi wa nini cha kufanya. Kilimo kifunganishwe na upatikanaji wa umeme na maji, soko la ndani ya Tanzania na soko la Afrika Mashariki litatosha kwa awamu hiyo ya kwanza. Hii pia itaongeza wigo wa walipa kodi, miundombinu (ndege, meli, reli) ili kutanua soko nje ya Tanzania na Afrika Mashariki.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's