Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Richard Phillip Mbogo

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu kwa namna ya pekee ambavyo ametujalia mpaka tupo hapa na uhai tulionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naomba niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Nsimbo kutoka Mkoa wa Katavi, kwa jinsi walivyoniamini. Nilivyowaeleza kwamba nitawatumikia, kazi tumekwishaianza, naomba waendelee kuniamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, imesheheni mambo mazuri sana. Kwanza tukiangalia huduma za jamii na matatizo na kero ambazo zinazunguka jamii zote za Watanzania. Mimi namuunga mkono kwa hatua ambazo amechukua kuanza kushughulikia kero zetu, naamini Serikali anayoiongoza itafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba Mheshimiwa Rais atafanikiwa kwa sababu amelenga pia kuongeza mapato na kupunguza matumizi. Mtanzania yeyote mfanyabiashara huwa haitaji kupata hasara katika biashara anayoifanya. Siku zote ataangalia mauzo yaongezeke na apunguze gharama. Mheshimiwa Rais wetu ameliangalia hilo ili aweze kuboresha na kupeleka fedha nyingi kwenye miradi. Mimi namuunga mkono mapato yaongezeke na matumizi yapungue na sisi Wabunge tutaendelea kumshauri maeneo mengi ambayo yatakuwa na upotevu wa fedha ili ziweze kuongezeka na wananchi wetu waweze kufaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Nsimbo limezungukwa na kero nyingi sana. Kwanza, wananchi wangu zaidi ya 80% au 90% ni wakulima wa mazao ya biashara na mazao ya chakula. Ndiyo maana mkoa wetu ni moja ya mikoa inayotoa chakula kingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna matatizo ya ardhi kuchoka sana, maeneo mengi tumekuwa hatupati mazao ipasavyo. Pia kuna tatizo la pembejeo na tunamwomba Waziri wa Kilimo katika ile ziara yake ya Tabora afike mpaka Mkoa wa Katavi ili aweze kuliangalia suala hili. Tunajua Naibu Waziri alipita lakini ratiba yake ikuruhusu pia kukanyaga na Jimbo la Nsimbo. Wakulima wa tumbaku wanapata taabu sana, kodi ziko nyingi, makato mengi, mikopo unamlipia hata yule ambaye hakuhusu. Kwa hiyo, tunaomba awaangalie sana wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Nsimbo ni jipya, kuna kata zimeongezeka na mojawapo ni kata ambazo zilikuwa ni makazi ya wakimbizi lakini Serikali ya Awamu ya Nne ilitoa uraia na mwaka jana wamepiga kura, tumepata Madiwani. Hata hivyo, zile kata zina mahitaji mengi sana. Kwanza, bado ziko kwenye hadhi ya Mkuu wa Makazi, kwa hiyo sheria iliyopo pale ni ya Mkuu wa Makazi, utendaji wa Halmashauri pale ndani umekuwa hauendi ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri wa TAMISEMI kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, awasiliane na Waziri wa Mambo ya Ndani, kata au maeneo yaliyokuwa makazi ya wakimbizi ya Katumba, Mishamo na Bulyanhulu tuangalie jinsi gani hadhi za makazi ya wakimbizi zinafutwa yabakie kuwa maeneo huru ya raia. Wale raia ambao hawajapata uraia, nimkumbushe Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kwamba suala hili litashughulikiwa haraka ili waweze kupewa uraia.
Kwa hiyo, tunaomba sana ahadi ya Mheshimiwa Rais itekelezwe wale ambao bado wapate uraia na makazi hayo ya wakimbizi hadhi yake ya ukimbizi iondoke ibakie eneo huru.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu lina kata 12 tuna vituo vya afya viwili tu na zahanati ni chache mno, vijiji vingi havina zahanati. Kwa hiyo, taabu ya huduma kwa mama zangu ambao ndio mara nyingi wanahitaji huduma za afya, imekuwa ni shida. Vilevile Jimbo langu la Nsimbo, sekondari ya juu hakuna na sekondari za kawaida ziko chache mno na tuna kata mpya. Kwa hiyo, tunaomba Serikali katika bajeti hii iliangalie kwa jicho zuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakumbwa na shida ya miundombinu na Jimbo la pili baada ya Mheshimiwa Rais kufungua kampeni mwaka jana lilikuwa ni la Nsimbo baada ya Jimbo la Mpanda Vijijini. Nilimwomba barabara kutokea Kanoge – Mnyake - Msaginya na aliahidi itatengenezwa kwa fedha za ndani. Nami nitamwomba Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa anisaidie liingie kwenye bajeti ya mwaka huu 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi, tunashukuru Serikali ya Awamu ya Nne, alhamdulillah imetupa majimbo, Halmashauri na pia umeme. Nimshukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo kwa umeme wa vijijini, kata nne zimepata umeme lakini pia tupate umeme kwenye kata zilizobakia. Vilevile Halmashauri yangu inahitaji Wakuu wa Idara, kati ya Wakuu wa Idara 19 waliopo ni nane tu wengine wanakaimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, naomba tuangalie suala la viwanda ambalo lipo hata kwenye Mpango wa Miaka Mitano, tumesahau pia kuangalia viwanda vidogo vidogo. Kuna maeneo mengi ambayo tunahitaji viwanda vidogo vidogo, kama dada yangu Mheshimiwa Hasna alivyochangia jana kuhusu Kigoma kwa lile zao ambalo linatengeneza sabuni, basi tuangalie viwanda vidogo vidogo kulingana na maeneo yetu tulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichangie suala la bandari, kuna mpango wa Serikali wa kujenga bandari ya Bagamoyo lakini tujue faida na hasara zitakuwaje katika uchumi wa nchi yetu. Tukiweka mwekezaji maana yake mpaka arudishe gharama yake, tuangalie na bandari tuliyonayo tutakosa mapato kiasi gani? Tunaiomba Serikali iangalie suala hili kwa jicho la karibu zaidi.
Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais alizungumzia Air Tanzania. Air Tanzania kwa muda mrefu imekuwa inaenda kwa ufadhili wa Serikali, ndege moja gharama kubwa za uendeshaji. Serikali imepanga kununua ndege nyingine mbili kwa katika Mpango wake wa Miaka Mitano. Tusiende kihasara, ni bora watumishi waliopo walipwe, waende wakaanze maisha mapya tubakize wafanyakazi wachache ili Air Tanzania ifanye kazi kibiashara na kwa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kodi kwa wastaafu, mtu amefanya kazi miaka 30, miaka 20 analipia kodi, lakini anakuja kwenye mafao ya kustaafu pia napo anakatwa kodi na hata TRA ukiuliza formula sahihi hakuna mahali ambapo pamenyooka kuhusiana na kodi hii. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iwasamehe wastaafu kodi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Serikali, miundombinu kwenye jimbo langu ni shida na sasa hivi Mto Koga umejaa na kuna watu wamepoteza maisha. Kwa hiyo, tunaomba reli yetu kama ilivyoahidiwa treni ipite wakati wote, fedha za dharura zije, barabara ziweze kupitika, Mkoa wa Katavi tumekuwa kama tuko kisiwani. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali kwa kupitia Wizara mtuangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia ni kuwa ajira ni kitu muhimu kwa watu wote. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliahidi kwamba Serikali italeta mikopo (revolving fund) ya jumla ya shilingi milioni 50. Kwa hiyo, tunaomba utaratibu uandaliwe haraka, mfuko huo uanzishwe tuupitishe ili watu wetu waweze kupata mikopo na kufanya kazi ambazo zitawasaidia katika kunyanyua uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ajira jimbo langu lina wachimbaji wadogo wa dhahabu lakini Serikali imewapeleka Kaparamsenga kwenye copper. Hiyo haina msaada na sasa hivi kuna mwombaji mpya Kijani Investment kwa eneo lililokuwa linamilikiwa na GBA.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iachie wachimbaji wadogo wadogo eneo hilo, ni kilometa kumi tu kutoka Mpanda Mjini. Bahati nzuri ndugu yangu, kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Muhongo barua imekuja ofisini kwako ya Chama cha Wachimbaji wadogo wadogo, wakiliomba hilo eneo wapewe wao badala ya kampuni mpya ya Kijani Investment. Maana wao hawana uwezo wa kwenda kuchimba copper, mashapo hayo ya copper hawawezi, inahitaji uwekezaji mkubwa sana. Kwa hiyo, tunaomba waachiwe sehemu ambayo wataweza kupata fedha kidogo kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao, dhahabu ni rahisi kuliko copper.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niiombe Serikali, Halmashauri zetu zinapewa ceilling ya bajeti lakini Serikali huwa haiangalii mahitaji husika ya kila halmashari. Kwa hiyo, Serikali ifanye upembuzi mzuri ili hizi ceilling za bajeti inazotoa iangalie na uhalisia wa mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuleta haya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2016/2017. Wamejitahidi sana kuweza kuoanisha na nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango na timu yake kwa kiujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huu Mpango naomba nichangie maeneo machache kwa sababu ya muda. Jambo la kwanza ambalo ningependa nishauri, ili tuweze kuwa na maendeleo katika huu mwaka mmoja, tuendelee kupunguza urasimu uliopo katika maeneo mbalimbali, ambayo ndiyo yanaongeza kipato cha Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ambayo imeshaanza kufanyika bandarini, TRA na kwenye border zetu kama Tunduma, Kyela, Namanga kote huko tuendelee kufanyia kazi. Pia Mamlaka husika kama ya mazingira na yenyewe pia iendelee kuangalia muda ambao wana-process vibali mpaka mtu anapata kuweza kufanya shughuli ambayo ameiomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie eneo lingine ambalo ni suala zima la uchumi. Ili uchumi uweze kukua kuna vigezo mbalimbali, lakini kuna michango ambayo inachangia kukua kwa uchumi na vipato vyetu. Tumeangalia kipato kimekuwa mpaka kimefikia shilingi 1,700,000/=, ni hatua nzuri ya kuonesha kwamba uchumi umekuwa, lakini kuna sekta hambazo hazikufanya vizuri katika kipindi kilichopita na hasa upande wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kufikia 3.4%, na lengo lilikuwa ni 6% na upande wa kilimo ndio eneo ambalo limeajiri zaidi ya watu 70%. Sasa tunaomba kwenye huu Mpango wa mwaka mmoja 2016/2017 na katika bajeti, Serikali iangalie matatizo yaliyojiri, tukafikia 3.4%, badala ya 6% na iweze kurekebisha na hasa ni katika fursa mbalimbali na pembejeo ambazo wakulima hawapati ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika Mpango huu tumezungumzia kuboresha fursa upande wa viwanda, lakini hatujagusa upande wa viwanda vidogo vidogo. Sehemu kubwa ambayo naiona bado elimu ya ujasiriamali kwa watu wetu haijafika ipasavyo na wafanyakazi wa Halmashauri hasa Maafisa Biashara, wanatakiwa waifanye kazi hiyo ili watu wetu wajue na wapate hizo fursa za kufungua biashara ndogo ndogo na hizi ziendane kutokana na maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, katika kuongeza mapato, ni Taasisi za Serikali, zamani tuliona Jeshi la Magereza likiwa ni mojawapo likijishughulisha na uzalishaji, mazao ya biashara na mazao ya chakula. Hata hivyo, sehemu nyingi sana sasa hivi za Magereza hayazalishi, sasa tatizo liko wapi? Liangaliwe na wenyewe waingie katika kuchangia kwenye pato, tunawagharamia sana Magereza lakini uingizaji ni mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mapato na kukuza uchumi na swali leo limeulizwa na Mheshimiwa Risala ni utalii, mbuga ya Katavi, Ruaha, Udzungwa, Mikumi ni sehemu ambazo haziangaliwi na kupewa kipaumbele. Matatizo ambayo yameoneshwa tunaomba Serikali kupitia Wizara zake, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa pamoja ziangalie kwenye bajeti hii ya mwaka 2016/2017, kuboresha miundombinu ambayo inakwenda kwenye hizi mbuga ili tuweze kuongeza kipato, pamoja na kuzitangaza. Kwa hiyo, tunaingia gharama lakini Serikali itaingiza fedha kwa kupitia watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine napenda niizungumzie tena, ni kuhusu mashirika ya umma. Tumekuwa na mashirika ya umma ambayo yanaendelea kuitia hasara Serikali, hayajiendeshi kibiashara. Namuunga mkono Mbunge wa Kigoma Mjini, Mheshimiwa Zitto, suala la Air Tanzania liangaliwe, retrenchment ifanyike, watu waingie kwenye mikataba ya ajira mipya, wapunguzwe wafanyakazi na tuweze kwenda kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na yote tunayozungumza hapa, lazima turejee kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, tuone kitu gani ambacho kimeandikwa na tuangalie utekelezaji. Katika ilani ya Chama cha Mapinduzi tumeahidi kutengeneza reli katika kiwango cha Kimataifa, standard gauge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, katika haya mapendekezo gharama za upembuzi yakinifu, reli mpya kuanzia Mpanda kwenda Kalema na kukarabati kuanzia Kaliua mpaka Mpanda, iingie na iwemo na reli ya kuanzia Uvinza kwenda Burundi na yenyewe iingie iwemo katika upembuzi yakinifu kwa mwaka huu 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini iwe hivyo? Kwa sababu tayari nchi ya Burundi ina uhitaji wa haraka na wenzetu wa Kongo na wenyewe kwa habari ambazo sina hakika wameshaanza kutengeneza reli ya kuja Ziwa Tanganyika ili mizigo ipitie Kalema. Sasa sisi kwa upande watu tuanze kazi haraka iwezekanavyo na tunamwomba Mheshimiwa Waziri iingie katika bajeti hii, huu upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika ripoti ya miaka mitano iliyopita ya maendeleo, tulisema tutajenga reli kilometa 2,707. Mwaka huu wa mwisho tulisema tutajenga kilometa 197, lakini tumeweza kujenga kilometa 150. Tuangalie ni wapi tulikwama, tatizo ni fedha au tatizo ni utawala? Tunaomba reli yetu ya kati iwekewe kipaumbele, iweze kutengenezwa katika kiwango cha Kimataifa na ili tuweze kuingiza mapato kutokana na mizigo ya ndani pamoja na mizigo ya nchi jirani. Hilo nalo liingie katika huu mwaka 2016/2017 na lionyeshwe kwa kutajwa kilometa zitakazotengenezwa na maeneo wapi mpaka wapi na isiwe tu nadharia inayotaja idadi bila kujua na maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie kwenye suala zima la elimu. Tumeelezwa kwamba kutokana na mafunzo ya kiujumla kusomesha watu, lakini kuna Kanda nyingine hakuna Vyuo Vikuu. Tanzania ukanda wa Mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa ukanda ule pia hakuna Vyuo Vikuu. Sasa katika kugawa rasilimali kijografia na yenyewe tuangalie tuweze kupata Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niongezee katika suala zima la miundombinu. Tumeeleza fursa Tanzania ni nyingi na lazima kuwe na viwezeshi, kiwezeshi kimojawapo pia ni kuboresha miundombinu ili wawekezaji waweze kufika. Hata hivyo, katika sehemu nyingi barabara hatuna na hasa Mkoa wa Katavi. Tuna fursa nyingi, tuna madini, gesi, mafuta, lakini barabara hakuna. Barabara ya kuunganisha kutoka Uvinza kuja Mpanda tunaomba ianze na iingie kwenye bajeti hii na pia tuweze kupewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii na naunga mkono na naomba yote niliyopendekeza yafanyiwe kazi. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napongeza Mawaziri na Watendaji wote katika Wizara kwa kuwasilisha hotuba ya makisio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa elimu na ualimu. Tumeshuhudia zaidi ya miaka kumi mitaala mingi ikifanyiwa mabadiliko ambayo yameleta shida kwa wananchi kwani ubora wake umeshuka ukilinganisha na miaka ya nyuma. Vilevile kozi ya ualimu imekuwa haizingatii viwango hasa vyuo vya watu binafsi. Walimu katika shule za Serikali na binafsi hawazingatii taratibu na kanuni katika utendaji hivyo Wizara iangalie namna ya kuboresha kanuni ziendane na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Katika hotuba ya Waziri hakutaja Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Msaginya kilichopo Halmashauri ya Wilaya Nsimbo, Mkoa wa Katavi. Taarifa za hivi karibuni ni kuwa kimehamishwa toka Wizara ya Afya. Chuo hiki kina matatizo mengi kuanzia rasilimali watu, miundombinu na madeni ya wakandarasi ambao wamesimama kazi kwa sababu hawajalipwa. Hivyo tunaomba Wizara ifanye malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo kwa vitendo. Katika kuongeza ujuzi wa wanafunzi, tunashauri Wizara iboreshe mwongozo wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa kuanzia mwaka wa kwanza kushiriki mafunzo haya ili kuwajengea uwezo mzuri wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo. Wizara inahitaji kuboresha utendaji wa Bodi ya Mikopo na hasa kuwawekea malengo kwa kukusanya madeni toka kwa wanafunzi ambao wanadaiwa. Pia muda wa kulipa upunguzwe tena kwa kuwa fedha inahitajika kusaidia wengine na kuondoa mzigo kwa Serikali kutoa fedha kila mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mitihara elimu ya juu. Ili kuboresha elimu ya vyuo vikuu nchini tunashauri Wizara itoe mwongozo juu ya mitahara (course outline) zenye kuendana na hali ya sasa na pia ziwe zenye ubora na kufanana ili shahada, stashahada zipate ubora duniani.
kusahihisha uwe unashirikisha mtu zaidi ya mmoja (panel) kuondoa rushwa za aina mbalimbali kwa wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ruzuku vyuo binafsi vya ufundi. Tunashauri Serikali iangalie namna ya kutoa ruzuku kwa vyuo binafsi vya ufundi ili kuviwezesha kutoa elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia, lakini pia niipongeze Serikali kiujumla kwa kazi ambayo wamefanya tangu walipoingia madarakani mpaka leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia upande wa TAMISEMI tunaelewa kabisa bajeti ya TAMISEMI ni trilioni sita ambayo ni wastani wa asilimia 20.4 ya bajeti nzima ya Serikali. Kwa hiyo, inaonesha ni jinsi gani TAMISEMI imebeba mambo mengi ambayo yanafanya huduma za jamii na mambo yote kwa karibu sana na wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna mambo ambayo ningependa kuchangia katika kuishauri TAMISEMI. Jambo la kwanza upande wa kilimo; mwaka jana wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais aliahidi kushughulikia masuala ya wakulima kulipwa fedha zao taslimu badala ya kuendelea kukopwa na Vyama vya Misingi na hawa mawakala wa mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuiombe sasa, kwa kupitia Wizara yetu hii wamkumbushe au Wizara yenyewe ichukue wajibu wa kuliona suala hili kwa kushirikiana kiujumla katika Serikali waone wanalichukulia vipi. Tumekuwa na matatizo ya ruzuku, Serikali imejitoa, kwa namna nyingine tunaweza kusema maana bei za pembejeo zilipanda karibu mara mbili, sasa watu wetu wanakwenda kufanikiwa vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika masuala ya wakulima ni bajeti ambayo tunaomba iongezwe na mpango bora wa matumizi ya ardhi ili wakulima wetu waweze kupata maeneno mazuri yenye rutuba na kuweza kufanikisha masuala yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la elimu. Binafsi Jimbo langu la Nsimbo hatuna A-level, kwa hiyo, katika maombi yetu kwenye hii Bajeti tunahitaji tuwe na A-level maana shule za sekondari tunazo takribani tano. Kwa hiyo, tunaomba tupate hiyo sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba aliyotoa Mheshimiwa Waziri ameonyesha tuna vijiji vingi na vingi havina zahanati; mojawapo ni vijiji vilivyopo katika Jimbo la Nsimbo na tukizingatia kwamba Jimbo langu ni moja ya Jimbo ambalo lilikuwa lina makazi ya wakimbizi wanaotoka nchi jirani ya Burundi, kwa hiyo, huduma za kijamii zinahitaji kuboreshwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yote hayo kuna jambo ambalo ni zuri sana na ni la muhimu katika maisha ya wananchi, ni kuhusu maji. Halmashauri yangu ilikuwa na bajeti mara ya kwanza shilingi bilioni 1.6 ya miradi ya maji. Serikali ilivyoshusha ceiling ikaenda shilingi milioni 703. Takribani wiki moja iliyopita ceiling imetoka shilingi bilioni 16 imeenda shilingi bilioni 14. Tumepewa ceiling mpya na ceiling hii inalingana na bajeti ya mwaka huu wa fedha 2015/2016. Maana yake hatuwezi kuajiri, hatuna miradi ya maendeleo ambayo mwaka huu haijatimizwa, imeingia kwenye bajeti mpya ya mwaka 2016/2017. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali bora tupunguze fedha za maendeleo katika maeneo kidogo kama ya barabara na sehemu nyingine, lakini sehemu muhimu ya maji tuweze kuongeza fedha ili wananchi wetu wapate maji kwa sababu maji ni muhimu sana na ukikosa maji hayana mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie suala zima ambalo lipo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu mawakala kuondolewa asilimia 100 muda siyo mrefu ujao. Naomba ni-declare interest kwamba nina uzoefu kidogo katika eneo hilo, mimi mwenyewe ni wakala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la dhana ya kuweka mawakala ilikuwa ni kudhibiti mapato ambapo watumishi wa Halmashauri zetu walikuwa wanayapoteza kwa njia mbalimbali; aidha, kwa kuwa na vitabu hewa au kubadilisha zile nakala kutoweka copy, ndiyo maana Serikali iliamua kuweka mawakala. Pia tumeona kwamba kuna tatizo katika kuweka mawakala hawa na kutumia hizi electronic machine, tumeona Mtwara na Arusha kulingana na kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeonesha improvement kubwa kwamba mapato yameweza kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo kuna baadhi ya aina ya ushuru zitaleta shida sana. Kwa mfano, ule ushuru mdogo mdogo kwenye masoko, utatuletea taabu sana, maana yake itabidi tuongeze rasilimali watu kwa ajili ya kukusanya. Tuna ushuru mwingine wa mazao ya asili ya misitu, mazao ya biashara, mazao ya chakula na movement ya yale mazao, ndiyo maana katika hizi Halmashauri kuna mageti yanayofanya kazi saa 24, siku saba kwa wiki, mwezi mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maana yake, Halmashauri itabidi iajiri na tukiajiri zaidi watu tunaongeza gharama za staff, ndiyo hiyo mishahara na gharama nyingine ambazo zinahusiana na watumishi. Kwa hiyo, tuishauri Serikali, tunaunga mkono wazo hili, lakini tunaomba maeneo mengine ambayo kuna changamoto ya ukusanyaji, basi tuendelee kutumia mawakala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna mfano dhahiri; kuna baadhi ya maeneo tumepeleka watumishi wetu wamekwenda kukusanya, unakuta makusanyo yanakuja tofauti na wakala alivyokuwepo. Kwa hiyo, japokuwa tutatumia hizi electronic machine, lakini tuangalie namna ya kuimarisha udhibiti wetu wa ndani yaani internal control, lazima tuimarishe. Yawezekana ushuru wa shilingi 5,000 mtu akamkatia shilingi 2,000; lakini kwa sababu ni ya kielektroniki na imejisajili kule TRA, sasa sisi tutaona tumedhibiti lakini kumbe kuna njia nyingine ambayo tutaendelea kuporwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kiutendaji katika Halmashauri. Mfumo wa kuandaa hizi bajeti kwenye Halmashauri yetu unatuongezea gharama na tunashindwa kuboresha huduma za jamii. Mfano mzuri, Halmashauri yangu mwezi Februari posho za kulala nje na movement zote katika kuandaa hii bajeti wametumia shilingi milioni 29. Sasa Serikali imewekeza katika Mkongo wa Taifa, tuangalie katika kutumia teknolojia na katika movement za Halmashauri zote 181 ambapo wote wanakuja Dar es Salaam ndiyo wapewe zile ceiling, wanaingia gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama uongozi wa Mkoa ndiyo huo wenyewe ulete zile Bajeti na Serikali itoe zile ceiling ambazo ndiyo zenye ukomo. Maana leo inatoa ceiling ya kwanza, siku nyingine tena ceiling ya pili, kwa hiyo, tunakuwa na movement nyingi za watumishi wetu kuja Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ikitoa ceiling iwe imetoa ili watu wasiwe wanakuja Dar es Salaam mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kanuni za kudumu za Halmashauri, kwani zimekuwa zinakingana na miongozo inayotolewa na TAMISEMI. Kwa mfano, kuna mwongozo ulitoka takribani mwaka uliopita au mwaka juzi, unaelekeza Kamati za kudumu katika Halmashauri kama tatu, lakini kanuni inataja Kamati zote tano ni za kudumu. Sasa kipi kinafuatwa; kanuni za kudumu zilizopo au ni miongozo? Kwa hiyo, tuone ni jinsi gani iweze kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu fedha za majimbo zinagawanywa kwa kufuata masuala ya umaskini, idadi ya watu na ukubwa wa eneo. Kuna majimbo mengine ni makubwa lakini yana idadi ndogo ya watu, kwa hiyo, uwiano hapa hauendani kabisa. Bora tuondoe suala la ukubwa wa jimbo, tutumie idadi ya watu, hali ya umaskini ili kuwe na uwiano mzuri kwa kugawana hii rasilimali. Njia nzuri, tutumie hata ile weighted average ili Majimbo yetu yapate fedha kulingana na hali halisi iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na tunaomba sana bajeti yetu na kikubwa zaidi Halmashauri yangu ipandishwe bajeti yake kutoka shilingi bilioni 14 mpaka shilingi bilioni 18 ili tuweze kukidhi mahitaji katika Jimbo. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kuweza kuandaa bajeti na kusimamia Wizara kiujumla. Kwa sababu dakika ni tano, naomba kwa ufupi tu nisemee kwanza suala la wachimbaji wadogo wa madini ambao wapo katika Jimbo langu la Nsimbo, Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya kuna watu wanaopewa leseni ambazo ni ndogo (Primary Mining License), wamekuwa wakishirikiana vizuri na wananchi katika uchimbaji wa madini, lakini pale inapotokea mtu anapopanda daraja anaenda leseni kubwa, (Mining License - ML) anakuwa sasa na masharti magumu ya kushirikiana na wananchi katika uchimbaji wa madini. Hii imepelekea kuwa na mgogoro mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mfano mzuri, mwaka huu imetokea Kampuni ya Sambaru, imeweza kuingia kwenye mgogoro na wananchi wa Kijiji cha Ibindi mpaka ikahatarisha amani. Sasa ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri; tuna takriban vijiji 10 ambavyo wananchi hawa ndipo wanapata kipato. Tunaomba maeneo haya yawe ni kwa ajili ya wachimbaji wadogo tu na tusiweke uchimbaji mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunasema hivi? Maeneo haya yapo kilometa 15 mpaka 20 kutokea mjini na ndiko ambako inapatikana dhahabu.
Watu wanachimba na uchimbaji wao mdogo mdogo na wanaweza kukidhi maisha yao ya kila siku; kulipa ada na vitu mbalimbali katika maisha. Sasa tukiwekea namna hii, itakuwa inapelekea mgogoro na kuhatarisha amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile katika mlolongo mzima wa kazi za Wizara, tumewahi kupata taarifa, kuna ule ufadhili wa World Bank kwenye kusaidia wachimbaji wadogo wadogo tu, ufadhili takriban Dola milioni nne. Sasa katika vile vituo saba vya mfano, namwomba Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo, maeneo ya Jimbo la Nsimbo yawe ni moja ya Kituo cha mfano katika hivyo vituo saba ambavyo vitapata msaada wa Benki ya Dunia katika huo ufadhili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wachimbaji wadogo wana malalamiko kuhusiana na gharama za upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Gharama kwa hekta moja ni takriban sh. 1,500,000/= kwa mtu ambaye ameingia kufanya machimbo maeneo ya hifadhi ya misitu. Wakati huo huo, kwa hekta moja kwa upande wa madini, analipia sh. 80,000/=. Sasa imekuwa inawawia ngumu kuweza kukidhi hizi gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Wizara hizi mbili zikae kwa pamoja ziweze kuona namna gani hizi gharama zinapunguzwa ziendane na uhalisia wa uharibifu unaotokana na uchimbaji. Ni mara kumi zaidi watu wachajiwe kulingana na miti ambayo imeharibika kuliko kuchukua tu eneo wakati watu wengine wanachimba hata miti mingi anakuwa hajaikata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vile vile nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa awamu ya II ya REA. Nashukuru Jimbo langu Kata nne zimeweza kupata umeme, lakini bado Kata nane. Kwa hiyo, naomba katika hii Awamu ya Tatu, ule upembuzi yakinifu ambao tayari umeshafanyika, wasiruke vijiji. Maana kuna vijiji vingine wamepitisha umeme lakini hawakuweka zile transformer na wenyewe waweze kufaidika na umeme huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze viongozi wote wa Wizara ya Nishati na Madini katika kufanikisha uandaaji mzuri wa hotuba ya bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Nishati na Madini ni muhimu katika mpango wa Serikali wa maendeleo na kufanikisha nchi yetu kuwa ya viwanda, kwa kuwa nishati ni kiungo muhimu katika viwanda vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, REA; kwanza naomba Waziri aendelee kuwa imara katika Wizara hii na kuwezesha umeme vijijini kufikia malengo. Katika Jimbo la Nsimbo Mkoani Katavi, jimbo lina kata 12, lakini kata nne tu ndiyo zilizopata umeme wa REA. Sambamba na hilo, umeme umepita Kijiji cha Kapalala bila kuwekewa transformer. Tunashauri Wizara ikamilishe umeme katika kijiji hicho tukizingatia kuna wananchi wahitaji. Vile vile, tunahitaji, majibu ya Waziri ni lini kata zilizobaki nane zitakamilika kupata umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, gridi ya Taifa; Mkoa wa Katavi ni moja ya mikoa hapa Tanzania, ambayo haina umeme wa uhakika, yaani wa gridi ya Taifa. Hivyo, tunatumia umeme wa jenereta ambazo zilitolewa Shinyanga na tayari ni chakavu hazifanyi kazi kulingana na uwezo. Hivyo basi, tunahitaji Serikali ikague umeme uliopo Wilaya jirani ya Kaliua kwa kuwa ni jirani sana na Jimbo la Nsimbo. Hivyo, tunahitaji kauli ya Serikali ni lini itafanya upembuzi yakinifu wa kuleta umeme Jimbo la Nsimbo kupitia Kata ya Ugala?
Mheshimiwa Naibu Spika, madini; mradi wa wachimbaji wadogo wa Benki ya Dunia, Jimbo la Nsimbo ni mojawapo lina vijiji 11 ndani ya kata sita zina wachimbaji wadogo. Hivyo, tunaomba Serikali kuchagua maeneo ya mfano kati ya hayo saba. Naomba na Jimbo la Nsimbo tuna sehemu mbalimbali. Kwa mantiki hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atoe tamko la Nsimbo kuwa kati ya vituo saba vya mfano.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la wachimbaji wadogo; wachimbaji wadogo, ambao wana uwezo wa kuwa na leseni, waweze kupata leseni kwa mujibu wa Sheria (Primary Licence) na waweze kurahisisha wananchi wasio na leseni kuchimba katika maeneo yao na kuweza kuuza dhahabu na kupata mapato kuwasaidia kujikimu wao na familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Wizara ikitoa leseni kubwa mining licence (ML) wenye uhalali huo wanakataza wananchi kuchimba. Mfano mzuri ni kampuni ya SAMBARU, Kata ya Ibindi iliingia katika mgogoro na wananchi na hali siyo shwari. Pia, eneo la Dirifu, Kata ya Magamba nako kulitokea vurugu Januari, 2016. Kwa mantiki hiyo, tunahitaji Serikali kutoa tamko vijiji vifuatavyo viwe kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Jimbo la Nsimbo, Kata ya Machimbi, Kijiji cha Katisunga na Kapanda; Kata ya Ibindi, Kijiji cha Ibindi, Kapandamu na Kasherami; Kata ya Sitalike, Kijiji cha Mtisi; Kata ya Urwira, Kijiji cha Urwira, Usense; na Kata ya Itenka, Kijiji cha Msangama. Jimbo la Mpanda Mjini, Kata ya Magamba, Kijiji cha Dirifu Society.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu sana maeneo ya vijiji hivyo kuwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa kuwa eneo la awali ni Wilaya ya Tanganyika, eneo la Kipalamsenga, ambako kuna madini zaidi ya aina ya shaba. (Copper)
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za maliasili kwa wachimbaji madini utafutaji wa madini kuna wakati wananchi au kampuni huingia katika hifadhi za misitu. Wananchi hutozwa gharama za uharibifu wa misitu. Tatizo lililopo ni tozo zipo kwa ukubwa wa eneo badala ya kuangalia idadi ya miti na kupelekea watu wengi kushindwa kumudu gharama hizo. Hivyo, tunaomba, Wizara hizi mbili zikae pamoja na kuangalia gharama hizo, zipitiwe upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti wa mafuta Lake Tanganyika kwa kuzingatia maendeleo ya nchi tunahitaji Serikali kupitia Wizara isaidie utafiti wa mafuta katika eneo la Ziwa Tanganyika. Hivyo, taarifa ni muhimu nasi wananchi kujua maendeleo ya utafiti huo na vyema kuwasilisha Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo hayo juu, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutengeneza hotuba nzuri na pia na taasisi yake kiujumla, wameweza kutupatia makabrasha ambayo yatakuwa ni msaada kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa kulichangia ni masuala mazima ya kuhusu vijiji. Vijiji vyetu ambavyo vilitangazwa mwaka 1974 tuna matatizo ya mipaka; tunaomba Mheshimiwa Waziri kwa kupitia Halmashauri zetu na taasisi zilizopo mipaka mingi kwa sasa hivi haijulikani, kwa hiyo, kumekuwa na uingiliano na matumizi ya kilimo. Hii inasababisha mpaka wananchi wetu wanapata matatizo. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Jimbo la Nsimbo, Mkoa wa Katavi, eneo la kwenda Kata ya Ugala limekuwa na matatizo sana ya kujua mipaka ya kijiji iliishia wapi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika upande wa ardhi tunajua wamefanya kazi yao na wanafanya vizuri, lakini kuna mamlaka ambazo wanaingiliana! Tutahitaji waweze kukaa kwa pamoja ili tu wapate ufafanuzi na wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuishi. Mamlaka ya Hifadhi ya Misitu; tunahitaji wawe na mawasiliano ya karibu ili mipaka ambayo Mamlaka hii ya Hifadhi ya Misitu ambayo inaitoa na wakihusisha pia na Wizara ya Ardhi kwa kupitia hizi Halmashauri zetu waweze kuwa pamoja kwa sababu, sehemu nyingi kumetokea mkanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa jinsi anavyoshughulikia migogoro. Halmashauri yangu na mimi binafsi nitaleta maombi, tumekuwa na migogoro kutokana na idadi ya watu kuongezeka. Maeneo mengi ya nchi ya Tanzania yamekuwa sasa hivi yanavamiwa kwa sababu ya ongezeko la watu. Watu wameongezeka na hasa wanaofanya shughuli za kilimo na ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Halmashauri ya Jimbo la Nsimbo maeneo mengi yameingiliwa na hasa ya hifadhi za misitu, ardhi imekuwa ni haba. Sasa kuna mpango ambao Mheshimiwa Waziri ameuzungumza wa matumizi bora ya ardhi, lakini tuna tatizo la bajeti katika hizi Halmashauri zetu. Sasa tungeomba kwa upande wa Wizara waweze kusaidia, kwa kuwa wanaweza kupata mafungu aidha, kupitia taasisi nyinginezo. Tunajua kwenye bajeti itakuwa haitoshi, lakini kama Waziri anavyotumia jitihada kuwapata wafadhili mbalimbali, ili fedha ipatikane kwa ajili ya huu mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa sababu, kuna maelekezo mengi ametoa kwamba Halmashauri zetu ziweze kupima maeneo, lakini shida ni bajeti iko finyu kwelikweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, bajeti ya mwaka 2016/2017 ni shilingi bilioni 14 na bajeti inayoishia 2015/2016 ni shilingi bilioni 14, kwa hiyo, hatujapiga hatua! Matokeo yake ni kwamba, miradi mingi haiwezi kuja kufanyika. Sasa kama Wizara itaweza kusaidia Halmashauri zetu kwa kupata fedha sehemu nyingine, litakuwa ni jambo bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni masuala ya utapeli kuhusu viwanja vyetu. Tunaomba Wizara iangalie mpango ambao utakuwa ni mzuri kwa watu wanaohitaji kununua au kuuza viwanja. Ni kweli, Wizara inatoa huduma mtu akitaka kufanya searching anafanya na anaona jina kabisa pale, Mheshimiwa Richard Philipo Mbogo, lakini kuna tatizo Hati hizi zinavyotoka hazina picha moja kwa moja, sasa zingeweza kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kesi nyingi sana za watu wametapeliwa kuhusu uuzaji wa nyumba au viwanja katika maeneo mengi sana ya nchi yetu. Sasa tuombe Wizara itengeneze mpango mzuri ambao utasaidia kupunguza watu kutapeliwa na ndio maana ukipita sehemu nyingi mijini unakuta imeandikwa “Nyumba Haiuzwi” kwa sababu, watu wengi tayari wameshaingia katika hali ya utapeli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Wizara imeweka suala la TEHAMA, maana yake hutumia teknolojia katika kupata taarifa zake na kufanya kazi sehemu mbalimbali. Kwa sababu, sehemu nyingi Mkongo wa Taifa bado haujaanza kufanya kazi, basi tunaomba Serikali iweze kuhakikisha kwamba, Mkongo huu unafanya kazi ili tuweze kuhakikisha kwamba, Halmashauri zetu zinakidhi mahitaji ambayo Wizara inaweza kuagiza katika Hotuba ya Waziri ambayo ameitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia naomba sasa kwa upande wa Wizara tuongezewe huduma mikoani, watu waweze kupata Hati. Tuna makazi mengi ya vijiji, watu wengi hawana Hati, kwa hiyo, ikitokea pale mtu anahitaji dhamana Mahakamani, anahitaji apate mkopo, watu wengi hawana Hati. Kwa hiyo, tutaomba zile gharama kwa upande wa vijijini zishushwe ili watu waweze kupata Hati na hata hizo za category karibu tatu ambazo ameweza kuzieleza Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naunga mkono hoja na naomba Wizara iendelee kutimiza wajibu wa Serikali. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri na watendaji wa Wizara kwa maandalizi na kuwasilisha bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Katavi katika Mkoa wa Katavi upande wa Kaskazini inapakana na Kijiji cha Sitalike lakini kwa mujibu wa mipaka sehemu ya kijiji ipo eneo la hifadhi. Hivyo, tunaomba mpaka urudishwe nyuma mpaka ng‟ambo ya Mto Katuma kwa kuwa wananchi hapo wanaishi tangu miaka ya 1990.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA inahitaji kuwa na ujirani mwema yaani tunaomba sehemu ya Mto Katuma iruhusiwe wananchi kuvuna samaki angalau eneo lenye urefu wa kilometa tano ili kuwezesha wananchi kupata vitoweo na pia kuondoa ugomvi. Hivi karibuni vijana watatu walikamatwa eneo la mto na walipigwa sana na kuumizwa ambapo hali zao siyo nzuri. Jambo hili lilipelekea wananchi kutaka kuchukua hatua zinazopelekea kuvunja amani kati ya watumishi na wafugaji. Kwa mantiki hiyo, tunaitaka Serikali itoe tamko la watumishi wa TANAPA kufuata taratibu, kanuni na sheria katika utendaji wao ili kuondoa hali ya kuvunja amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu promosheni ya hifadhi, kwa muda mrefu sana Serikali imekuwa ikitangaza sana baadhi ya hifadhi maarufu na kubwa hapa nchini bila kuhusisha pia hifadhi ambazo zinahitaji kutangazwa sana. Mfano mzuri ndege zetu zinabeba majina ya hifadhi kubwa. Tunahitaji Mbuga ya Katavi kuboreshwa na kutangazwa ili kupata watalii kwa kuwa uwanja wa ndege upo. Vilevile miundombinu na huduma nyingine ziboreshewe zaidi kama zilivyo sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujangili, Serikali imekuwa na juhudi kubwa zaidi kupambana na ujangili lakini uhalifu huo bado unaendelea. Tunahitaji Serikali iboreshe mbinu za kukabiliana na wahalifu. Watumishi wa TANAPA wameonekana kuhusika, hivyo utaratibu wa kuwahamisha utumike na kuwafuatilia mienendo yao. Pia Serikali lazima ifuatilie taarifa zinazotolewa na vyombo vingine vya usalama. Vilevile maeneo yanayozunguka Hifadhi za Taifa yawe yanachunguzwa mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya misitu na pori la akiba. Nchi yetu imekuwa na ongezeko la watu kila mwaka, vilevile nchi yetu ilipokea wakimbizi kutoka jirani za Burundi, Rwanda na Congo DRC hivyo kuhitaji maeneo. Vilevile baadhi ya maeneo ya nchi yamekuwa na ufinyu wa maeneo yenye rutuba na nyasi za kulisha mifugo na wafugaji na wakulima kuhamia maeneo mengine. Athari zilizotokea ni uvamizi wa maeneo ya hifadhi za misitu na mapori ya akiba. Vilevile migogoro imekuwa mingi. Pia tatizo la zana za kilimo imepelekea watu kutafuta maeneo mapya ya kulima. Athari imekuwa wananchi kuchomeana nyumba na kufyeka mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na athari hizo tunaishauri Serikali iongeze kusimamia sheria husika kuanzia ngazi ya kijiji mpaka Taifa kwa kuwa rushwa imekuwa tatizo. Pili, ufugaji bora kwa kulima nyasi zinazokaa muda mrefu. Serikali ipange matumizi bora ya ardhi kwa kutoa fedha za kupima maeneo. Serikali ipunguze maeneo ya hifadhi ambayo tayari yamevamiwa muda mrefu, zaidi ya miaka 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vitalu vya uwindaji, kwa kupitia utaratibu wa sheria, wahitaji au kampuni zinaomba na kupata leseni za uwindaji kwa mfumo wa vitalu lakini tatizo lililopo ni taarifa kamili za mapato na uvunaji unaofanywa na kampuni zenye leseni. Hivyo, kuna umuhimu wa Serikali kuangalia upya mfumo wa vitalu kwa takwimu za kifedha na idadi ya wanyama. Vilevile vitalu vifanyiwe uchunguzi katika kudhibiti ujangili wa nyara za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo za misitu; Wizara imekuwa na tozo mbalimbali za mazao ya misitu lakini tozo kwenye mbao ni kubwa. Vilevile wachimbaji wadogo wa madini wanatozwa ada kubwa kwa hekta moja shilingi 1,400,000 ambayo haiendani na ukubwa na uharibifu. Hivyo tunaomba Serikali tozo ziendane na miti inayokatwa katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Memorandum of Understanding, Serikali ya Tanzania mwaka 2015 ilisaini mkataba kudhibiti biashara ya magendo kati ya Tanzania na Kenya na kuokoa fedha nyingi. Hivyo tunaomba Serikali iangalie upya MoU na nchi nyingine pia hata za mbali ili kuokoa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwanza nimshukuru Mungu kwa kupata hii nafasi, lakini pia naomba kuchukua nafasi hii nikupongeze Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uimara na tunaomba Mungu aendelee kukujalia kwa afya njema ili uendelee kukalia hicho kiti na kusimamia kanuni na sheria mbalimbali na Chama cha Mapinduzi hakikufanya kosa kukupendekeza kwa kuwa hiyo ni fani yako na unaitendea haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze bajeti, ni bajeti nzuri ina muelekeo mzuri kwa kuongeza pande wa Maendeleo na tumefikia asilimia 40 na vilevile imezidi kwa trilioni saba bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016; kwa hiyo tunategemea kupata mambo mazuri.
Pamoja na kuiunga mkono bajeti kuna mambo machache ambayo ningependa kuchangia na zaidi nianze na suala la kodi kwenye masuala ya Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi siungi mkono hii hoja ya kuondoa msamaha kwa Wabunge kwa sababu Serikali iliangalia kwa mantiki kabisa mwaka ambao iliweza kuwapa Wabunge na viongozi wengine msamaha wa kodi waliona kuna maana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia kwa mujibu wa Katiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Wabunge ndio chombo kikubwa katika Jamhuri ambacho kina wajibu wa kusimamia na kuishauri Serikali. Kwa hiyo, na tuko hapa kwa niaba ya wananchi, kwa hiyo unapomuongezea gharama Mbunge ni sawa na unamuongezea gharama mwananchi. Kwa hiyo, tunaomba sana sasa Serikali tuko kwenye hiki chombo, tunaisimamia Serikali; kwa hiyo, tunaomba hili kusudio liweze kuondolewa maana kupitisha haya marekebisho ya hii sheria ni sawa na mtu umepanda kwenye mti unakata tawi ambalo umekalia mwenyewe, sasa sidhani kama Wabunge tutaweza kuiunga mkono hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwenye kodi (Capital Gain Tax) kwenye mambo ya hisa, Serikali tuna soko la hisa na moja ya faida kubwa ya kuwa na soko la hisa ni kuweka uwazi katika makampuni ambayo yameingia pale, na makampuni ambayo yako pale kwenye soko la hisa yanatoa mahesabu yao kwa uwazi, utendaji wao wa kazi. Kwa hiyo, wananchama ambao ndiyo wale wenye hisa wakati wa kuuza zile share zao kuna faida wanayoipata kwa utofauti wa bei ya kununua na kuuza. Sasa kwa kusudio la Serikali kutoza kodi liangalie suala zima la kwamba tuhamasishe uwekezaji.
Kwa hiyo, niishauri Serikali tuangalie namna ambayo ya kutoza kodi kwenye hii faida mtu anapouza zile hisa zake ambayo itakuwa inaudhibiti mzuri. Ukichukua mtu amenunua share mwaka mmoja uliopita amekuja ameuza leo sasa ile bei aliyonunulia kumbukumbu nani anakuwa ameitunza?
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeshauri kwamba kwa sasa hivi share zikiuzwa inachukuliwa asilimia mbili ambapo broker anapata asilimia yake, soko la hisa linapata na capital market wanapata mgao wao. Sasa Serikali iangalie namna kwenye hii asilimia mbili tuongeze labda tupeleke asilimia tatu, asilimia moja ndiyo iwe kipato ambacho kinaenda kuingia upande wa Serikali badala ya kuweka kodi ambayo kui-manage kwake itakuwa inasumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri mkubwa katika watu ambao wapo kwenye masoko ya hisa wanatuwezesha kuongeza ufanisi, natoa makampuni zaidi ya 20 hatujafikia wenzetu kama Wakenya wana makampuni 62. Kwa hiyo, tuhamasishe makampuni mengi zaidi yaweze kuingia kwenye Soko la Hisa ili kuwe na utandawazi na Serikali iweze kukusanya kodi zake zote ipasavyo. Kwa hiyo, tutaomba sana Serikali namna ya kutoza hapa tuongeze asilimia hii mbili inayotozwa sasa hivi badala ya kuangalia kodi ambayo itakuwa kui-manage kwake pale itakuwa ni kazi ngumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia kuondoa au kufuta baadhi ya tozo kwenye mazao ya kilimo. Tunaomba Serikali iangalie kwa umakini kwa sababu kuna maeneo ambayo Halmashauri zetu ndipo wanapopatia kodi. Lakini vilevile kuna kodi na tozo ambazo haziingii kwenye Serikali au kwenye hizi Halmashauri zinaenda kwenye Vyama vya Msingi na wakulima wamekuwa wakilalamikia sana. Kwa hiyo, ninaunga mkono kuondoa zile kodi ambazo hazina tija zinaongeza gharama kwa wakulima na hasa zinakuwa zinafaidisha tu vyama vya msingi na makampuni mengine ambayo yananunua hayo mazao ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi ya hapo tungependa kwamba katika hotuba ya Waziri hatukuona upande wa tumbaku kwamba ameweka ni tozo zipi ambazo zinapendekezwa kuondolewa. Wakati Wabunge tumeshazungumzia sana kwenye upande wa tumbaku kuna gharama nyingi, wakulima wanapata taabu kwenye bei na hizo tozo mbalimbali, kwa hiyo tunaomba ziweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la maji, sera ya maji ilianza mwaka 1991 ikafeli, 2002 ikaboreshwa lakini ukiangalia mtiririko wa bajeti upande wa maji ndiyo una asilimia ndogo sana.
Kwa hiyo, nashauri angalau tuweke kati ya shilingi 20 kwa lita mpaka 50 ili tuweze kupata nakuunda mfuko wa maji tuweze kuboresha maji zaidi kwa wananchi ambao wengi wanakuwa na tabu kwenye kupata huduma ya maji na sera ya maji vijijini bado haijafikiwa ukamilifu wa zile mita 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la VAT kwenye upande wa Bima, Serikali inakusudia kuondoa VAT kwenye Bima upande wa ndege, lakini tujaribu kuangalia ni soko ambalo halina ushindani na je, kuondoka kwake kuondoa huu msamaha kuondoa VAT kwenye hizi bima upande wa ndege tunaathiri vipi mapato yetu na ni soko ambalo halina ushindani kwa hiyo, tutakuwa hatuna kwamba tunavutia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitoa fedha na cealing kwa Halmashauri zetu, lakini tuombe mwaka ujao wa fedha Halmashauri ziangalie bajeti zao tukiangalia kiutawala Halmashauri ndizo zenye wajibu mkubwa wa kusimamia huko chini kwa sekta zote, lakini wanapangiwa kiasi kidogo kwa hiyo upande wa maendeleo kwa Halmashauri ambao ndiyo tunaangalia wapi tuna mapendekezo zaidi tunakuwa tunazuiwa na ukomo wa bajeti. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri Halmashauri zetu kwa mwaka ujao wa fedha ziweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naunga mkono hoja.

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nimshukuru Mungu kwa namna pekee ametujalia mpaka muda huu tuna afya njema. Naomba tu niseme mimi ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na naanza kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza naomba Serikali iiangalie Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwanza kwa masuala ya bajeti. Tulisema na wenzangu wamesema basi ni wakati muafaka sasa kushughulikia suala hili. Waziri wa Fedha aliahidi mwezi Disemba ataangalia utekelezaji na ataongeza fedha kulingana na kazi zinavyoenda. Tunaomba ahadi hiyo ikifika Disemba wakati wa kupitia bajeti aliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanya, tumeona matunda yake kwani wameibua hoja nyingi, kwa hiyo tunawapongeza sana. Pamoja na pongezi hizi tunahitaji Ofisi ya CAG iboreshwe zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa vikao vya briefing vya kupitia hoja zao ambazo wamezikagua na wamezileta kwenye Kamati tuliweza kugundua upungufu mdogo mdogo aidha ni wa wafanyakazi au mfumo, hili tutaomba aliangalie. Kwa mfano, kuna wakati tuliwahi kuwauliza maofisa wanaotoka CAG, kwenye auditing kuna kitu kinaitwa analytical review, una-check movement, una-analyze kati ya mwaka wa fedha huu na mwaka wa fedha hata miwili, mitatu iliyopita. Hiyo ndiyo auditing ambayo inafanyika tukaona kwamba hii Ofisi ya CAG ni kama vile inafanya kazi kama internal auditor badala ya external auditor. Kwa sababu uki-check movement ya accounts mbalimbali hiyo ndiyo audit japokuwa utaenda kwenye item na ukapata zile schedule na utaangalia utajiridhisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunahitaji wa-improve maeneo mbalimbali kwenye audit procedures, audit technique na audit plan ili waweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika utendaji wa Ofisi ya CAG tunajua wanaangalia muhtasari wa vikao vya Kamati za Fedha za Halmashauri zetu, lakini inabidi waongeze juhudi kwa sababu kwenye Kamati hizi za Fedha na Mipango ndipo mahali ambapo maoni mengi yanatolewa kuhusiana na matumizi mbalimbali ya fedha za Halmashauri. Kwa hiyo, tunaomba waongeze sana juhudi kwenye kuangalia muhtasari wa vikao vya Kamati vya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukizihoji Halmashauri mbalimbali tuligundua kuna upungufu kwenye mfumo wa kihasibu kwa kutumia computer (EPICOR). Maoni yangu ni kwamba Serikali iangalie mfumo huu wa EPICOR tangu tumekuwa nao kwa miaka yote hii umetusaidia nini? Kama hauna msaada wowote ambao umeutoa kwa nini tusipate mfumo mwingine wa kihasibu kwa kutumia computer? Kwa sababu kumekuwa na upungufu mbalimbali, modules nyingi zimekuwa hazifanyi kazi na maeneo mengine kweli Halmashauri wanakuwa hawajawekewa mfumo huu, lakini ile link pamoja na platform zingine za kiuhasibu na za report zimekuwa hazifanyi kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ifanye upembuzi yakinifu kuangalia upungufu ulioko kwenye EPICOR. Dunia ya sasa hivi ina mifumo mingi ya accounting package ambayo inakuwa ni strong hata internal control yake inakuwa ni strong, huwezi uka-temper data. Kwa hiyo, tuhame kutoka kwenye EPICOR twende kwenye software zingine ambazo zitakuwa na msaada kwenye Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona maeneo mengi pia kama TAMISEMI haijaweza kukamilisha ufungaji wa EPICOR na wakati huo huo kwenye Halmashauri zetu kumekuwa na tatizo la mtu mmoja ndiyo anakuwa mtu wa EPICOR tu watu wengine wanakuwa hawajifunzi pale pale ndani. Kwa hiyo, hilo nalo Waziri wa TAMISEMI aangalie, kwenye Halmashauri isiwe anategemewa mtu mmoja kama atahama au atakufa au atakuwa anaumwa mambo mengine yatakuwa yamelala.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni upande wa Hazina, miradi mingi haijatekelezwa kwa sababu fedha zimekuwa hazipelekwi kwa wakati au zimepelekwa kiasi. Kwa hiyo, tumuombe Waziri wa Fedha akaangalie commitment ambazo zimefanywa na Halmashauri zetu, wengi walishatoa GPN wapelekewe fedha ili miradi ya maendeleo iweze kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni upande wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa. Wakati wa vikao vyetu Katibu Tawala wa Mkoa wameji-commit kwenda kuhakikisha kwamba Halmashauri zinafanya kazi ipasavyo.
Kwa hiyo, tumuombe Waziri wa TAMISEMI akahakikishe kwamba anawakumbusha, maana Wakurugenzi wengi wameahidi kushughulikia ule upungufu ulioonekana na wengi wameahidi kwa maandishi. Tuombe Ofisi ya Katibu Tawala ya Mkoa kuhakikisha kwamba anazisimamia hizi Halmashauri ipasavyo ili hata masuala mengine CAG anakuwa anapunguziwa kazi kwa sababu wao wapo kila siku na wana watumishi katika ngazi ya Mkoa wenye fani mbalimbali na wanaweza kusimamia hizi Halmashauri ndani ya Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni deni la 10% ambapo Halmashauri zinatakiwa zitenge fedha kwa ajili ya kukopesha vijana na akina mama ili waweze kupata mikopo ambayo riba yake ni nafuu sana. Tatizo ambalo tumeligundua fedha hizi hazina akaunti maalum benki, kwa hiyo, zinakuwa kwenye pool moja na Halmashauri zetu pale OC zinapochelewa wanatumia fedha hizi. Kwa hiyo, niombe Waziri wa TAMISEMI alichukue hili, apeleke mwongozo waidhinishe Halmashauri ili ziweze kufungua account bank ziwe maalum kwa ajili ya kuweka hizi fedha za 10% baada ya kuwa wamezikusanya ili kuongeza udhibiti wa kutokutumia kwenye matumizi mengine. (Makofi)
Jambo lingine ni suala zima la Kamati za Bunge kuwa na ufinyu wa bajeti. Tunaelewa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 63, wajibu wa Bunge ni kutunga sheria na kuisimamia Serikali na kupitia hizi Kamati tunakuwa tunaisimamia Serikali lakini fedha zimetengwa kwa kiasi kidogo na hatukamilishi kazi. Kwa hiyo, tutakuwa tuna-save kumi lakini kwa usimamizi ambao hatuufanyi tunapoteza mia. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwenye mapendekezo ya mpango tulichangia hivyo na Waziri wa Fedha ahakikishe kwamba bajeti ya Bunge isiwe chini ya 20% ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/2016. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu operesheni za Halmashauri zetu. Makusanyo ya ndani yana mgawanyo kwa mujibu wa kanuni na sheria, kuna 60% iende kwenye miradi ya maendeleo, 20% maeneo mengine na 10% kwa vijana na akina mama. Niombe Ofisi ya CAG ikasimamie sana mgawanyo wa hizi fedha wanazokusanya wenyewe (own source) kulingana na sheria ili tuhakikishe kwamba miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu na kwa wananchi wetu hasa maeneo ya afya, elimu na maji inafanyika kwa fedha za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwa kuunga mkono ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na niombe Serikali ikatekeleze mapendekezo yote ambayo yameonyeshwa mule ndani na sisi kama Kamati ihakikishe kwamba tunapata mrejesho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, mapato, kutokana na ongezeko la mapato shilingi trilioni tatu nukta nne kuna haja ya Serikali kuangalia maeneo mengi zaidi ili kuongeza mapato kama ifuatavyo:-
(i) Kupitia upya tozo mbalimbali zisizo za kodi katika Serikali na Taasisi zake ambazo hazijapandishwa kwa muda mrefu.
(ii) Kushawisha Kampuni nyingi kuandaa mahesabu badala ya kuwa katika mlipa kodi asiyeandaa hesabu.
(iii) Kufuatilia aina zote za kodi kuwa zinatumika ipasavyo. Mfano stamp duty on contracts. Kodi hii kampuni nyingi hazilipi.
(iv) Ripoti ya kuboresha mapato “CHENGE ONE AND TWO” itumike ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; Serikali itoe kipaumbele zaidi katika kilimo kwani mchango wake ni mdogo wa asilimia 2.9 wakati lengo ni asilimia sita hivyo suala la pembejeo lipewe kipaumbele hususani ruzuku ili kilimo cha jembe la mkono kiondoke kama ilivyoahidi Serikali. Tumbaku bado tuna tozo nyingi na mkulima ananyonywa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tozo katika mafuta sh. 50, tunaomba Serikali iweke sh. 50 kwa lita ili kukidhi mahitaji ya wananchi juu ya maji vijijini na zahanati kwa kuwa uwezo wa halmashauri nyingi ni mdogo hivyo bajeti ya 2017/2018 Serikali ikubali ombi hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Bunge, kutokana na changamoto za utendaji 2016/2017 tunahitaji Waziri ahakikishe kuwa bajeti ya shughuli za Bunge iongezwe kwa kiasi kikubwa kukidhi shughuli za Bunge kwa mujibu wa katiba angalau 130 bilioni.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi inayoendelea, Serikali ihakikishe miradi hii inakamilika ili kupunguza gharama. Tunaomba barabara ya Sumbawanga-Mpanda, Manyoni-Itigi-Tabora na Sitalime-Mpanda zikamilike 2017/2018. Pia Shirika la Reli lipewe pesa kuboresha mabehewa na ofisi ili usafiri utumike mwaka mzima hata masika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba ya msamaha; tunaunga mkono hoja ya kupitia upya mikataba hii ya msamaha wa kodi na kuwezesha Serikali kuongeza mapato pia kusaidia zaidi wakulima kufanya kilimo cha kisasa.
Mheshimiwa Mweyekiti, ubia katika uwekezaji; zoezi la uwekezaji katika ubia lipewe muda maalum ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi hususani wawekezaji wa ndani wenye uwezo wapewe kipaumbele.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa hii nafasi. Nami kwanza nianze kuunga mkono hoja ya Kamati hii ambayo report yake ni nzuri kweli kweli na imesheheni mambo mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nianze kwa kuchangia upande wa Mfuko wa kusaidia Kaya masikini (TASAF). Mfuko huu tunamaoni kwamba uendelee kuwepo. Uendelee kuwepo kwa misingi kwamba sisi ni Wabunge, tumezunguka, tumefanya ziara maeneo mbalimbali, wazee bado wanalilia uwepo wa pension. Sasa kama wazee tu wanalilia walipwe pension kwa ajili ya kuwasidia sasa je, hizi kaya masikini kwanini tuziondoe? Kwa hiyo tunaomba sana Serikali huu mfuko uendelee kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi ni kuboresha, katika kupitia majina kila baada ya miaka mitatu ikibidi iwe miaka miwili, kwa sababu kumekuwa na changamoto za maeneo mbalimbali, Watendaji wetu kule chini wanakuwa wanachakachua majina wanaweka watu ambao hawana sifa za kufaidika na huu mfuko. Katika kuboresha, badala tu ya kuangalia kutoa fedha, tuone jinsi gani tutoe fedha kiasi na tutoe hata shughuli ndogondogo kama za ufugaji wa aina mbalimbali wa ndege au wanyama ili ziweze kuwaongezea kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili lililozungumzwa kwenye ripoti ya Kamati ni kuhusu fomu za maadili, Watumishi wengi wa Serikali kwa mujibu wa sheria tunatakiwa tujaze fomu za maadili, lakini kwenye ripoti ya Kamati humu wamehimiza kuhusu TEHAMA. Serikali iangalie jinsi gani TEHAMA iweze kutumika ili tuweze kupunguza gharama na kuwa na ufanisi pia kwenda na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, uwasilishaji wa fomu za maadili Wabunge wengi waliweza kusafiri tena kurudi kuzileta fomu kwenye Kanda, Watumishi wa Serikali wamesafiri kwenda kwenye Kanda kuwasilisha fomu, ilikuwa ni gharama magari ya Serikali yametumika na fedha za Serikali. Kwa hiyo, tuombe sasa tupate mfumo wa kuwasilisha hizi ripoti kimtandao – web based reporting. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nichangie kuhusu utawala bora. Kweli Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wameteuliwa na Mheshimiwa Rais katika kutekeleza na kumsaidia, lakini tuombe wajaribu kuangalia ile sheria inayowaruhusu kutoa amri mbalimbali kama vile amri za kukamata. Ni makosa gani ambayo yanapaswa kuingia kwenye hiyo amri ya masaa 48 ya kuweza kukamatwa. Kwa hiyo, yaangaliwe ni makosa ya aina gani, kwa sababu sheria ilitungwa na wana mamlaka hiyo ya kuitumia basi waende kwenye Kanuni na kuangalia ni makosa ya aina gani, hatubezi utendaji wao bali tunaunga mkono wanavyofanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litakuwa sambamba pia na masuala ya kiutawala kwa upande wa utumishi. Tumesikia kauli mbalimbali, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa anamshusha mtu cheo au anamfukuza kazi badala ya kufuata taratibu za kiutumishi katika kuchukua hatua hizo. Kwa hiyo, tuombe sana Serikali wayaangalie makosa ambayo yamekwishafanyika kwa kipindi hiki na Waziri husika afanye utaratibu wa kutoa barua au mwongozo ambao utaweza kusaidia utendaji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tunapenda sana katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni mfuko ule wa kuwakopesha vijana na akinamama kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri zetu. Ufuatiliaji umekuwa ni hafifu sana, OC ziende kwa wakati ili mapato yetu ya ndani yaweze kutengwa. Inatakiwa asilimia 60 iende kwenye miradi ya mendeleo. Ndani ya asilimia 60, asilimia 10 ni kwa ajili ya vijana na akinamama. Sasa Halmashauri nyingi mpaka sasa hivi ukiwauliza miezi hii sita wametenga kiasi gani utakuta hakuna Halmashauri ambayo imeshatenga zaidi ya hata asilimia 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba OC ziende ili mapato ya ndani yote yasitumike kwenye shughuli za kila siku na vijana wetu na akinamama waweze kukopeshwa fedha na ndiyo utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Tume ya Utumishi ya Walimu. Tume hii imeanzishwa na kwa mujibu wa Kamati kuna changamoto sana kwenye upande wa bajeti na baadhi ya sheria na kanuni zinazoongoza. Tujaribu kuangalia kwanza mfumo. Tume hii sasa hivi inavyofanya kazi kwenye Wilaya kuna zile Kamati za kinidhamu, kwa hiyo kama Wilaya ina Halmashauri mbili au tatu sasa ushughulikiaji wa ile Kamati unakuwa ni mgumu kidogo kwa sababu ya composition ya Wajumbe wa ile Kamati wanatoka sehemu mbalimbali na ruzuku fedha zinakuwa hazipatikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri mfumo huu uende kihalmashauri na Mkurugenzi azifadhili hizi Kamati za nidhamu za Walimu kwa ajili ya ufanyaji kazi. Kama zitakutana mara tatu kwa mwaka au mara mbili ili kuwa na mapitio kabla ya bajeti na baada ya bajeti na Walimu wanapata promotion mbalimbali. Pia coordination ndiyo itaenda vizuri kati ya TAMISEMI na Utumishi kuhusu upandaji wa madaraja ya Walimu, mambo ya kinidhamu ndiyo yataenda vizuri. Kwa hiyo, tunaomba Tume hii Sheria ibadilishwe ambayo itakuwa inaweza kuongoza katika kuhakikisha kwamba Walimu wetu, maslahi yao na kesi zao ambazo zimekuwa ni nyingi na ndiyo ajira kubwa ya Halmashauri au upande wa TAMISEMI idadi kubwa ni Walimu. Kwa hiyo, ni muhimu sana tuweze kubadilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho tungeomba sasa upande wa Serikali kuhakikisha kwamba Halmashauri zetu zinalenga kwenye kufuatilia promotion au madaraja ya Walimu na mishahara yao ibadilishwe na iendane na bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Kamati hii. Ahsante sana.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kumshukuru Mungu wote tupo salama mpaka siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa namna ya pekee ambavyo wameweza kunyanyua kiwango cha ukusanyaji wa mapato yanayotokana na kodi na yale ambayo hayatokani na kodi, tunapongeza sana. Tukiangalia miezi hii sita ya mwanzo TRA wameweza kukusanya 7.2 trillion ukilinganisha na miezi sita kama mwaka wa fedha uliopita 6.4. Kwa hiyo, ni hatua nzuri na Mheshimiwa Rais aendelee na juhudi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini upande wa Halmashauri zetu zimefanya vibaya kidogo. Wamekusanya shilingi bilioni 117 ambayo ni sawa na asilimia kama 70, sababu ni zipi? Bado tuna vyanzo vichache vya mapato au kuondolewa kwa property tax na kukusanywa kwa upande wa TRA? Kwa hiyo, tungeomba Serikali waweze kuangalia suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo lililopo pia ni haya mapato ya Halmashauri jinsi gani yanapelekwa kwenye miradi ya maendeleo. Halmashauri nyingi kutokana na uhaba wa OC wanatumia fedha zote na kwenye miradi ya maendeleo haziendi. Kwa hiyo, Serikali ifanye tathmini ya hii miezi sita, mapato ya ndani kila Halmashauri ilikuwa ni ngapi na kulingana na sheria ya asilimia 60 kwenda kwenye miradi ya maendeleo wamepeleka asilimia ngapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Kamati kwa kazi nzuri sana ambayo wameifanya. Wametoa maoni na tunaomba Serikali iyachukue. Kwanza tukianza na pendekezo la kujenga zahanati kwa Serikali kutoa shilingi bilioni 30, ni muhimu sana. Tuna vijiji karibu 12,800 sina takwimu za haraka sidhani kama vijiji zaidi ya asilimia 60 vina zahanati. Halmashauri yangu nina vijiji 59 lakini zahanati zipo kwenye vijiji 17 tu na ukiangalia uwezo wa Halmashauri nyingi kuweza kukamilisha masuala haya ni ngumu. Kwa hiyo, tuombe Serikali hiyo shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati kwenye bajeti ya 2017/2018 waiweke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Kamati imeiomba Serikali kuongeza tozo kwenye mafuta kwa ajili ya Mfuko wa Maji. Sera ya Maji ya mwaka 2012 inasema kwamba wananchi watapata maji ndani ya mita 400 lakini mfano kwenye Jimbo langu mtu anakwenda kufuata maji mpaka kilometa tatu, ni tofauti na sera. Sasa tukishaitunga sera ni lazima tuweke mipango ya kuweza kuitekeleza. Mipango yenyewe ndiyo hayo maoni ya Kamati tuongeze kwenye mafuta kutoka sh. 50 mpaka sh. 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge la bajeti ya 2016/2017 tulihimiza sana hapa ndani, lakini Serikali haikuchukua ikasema tutaangalia bajeti hii, sasa bajeti hii tunaomba msiangalie basi mkubaliane na maoni ya sisi Wabunge ili tukatatue matatizo ya maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu asilimia 34 ya wananchi ndiyo wanaopata maji safi na salama. Kwa hiyo, ni jinsi gani tutaweza kutatua hili tatizo la maji, tuongeze hii shilingi 50 na tunaomba sana hiki kilio mkisikie. Kwa kufanya hivyo ndiyo utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwani wananchi wana kilio sana na maji na sisi Wabunge tunasema tukitatua tatizo la maji hata 2020 mtatuona tena humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumeahidi kutoa shilingi milioni 50 na Serikali imekubaliana, wametenga kwenye bajeti shilingi bilioni 59. Hata hivyo mpaka sasa hivi ule mpango mzima wa jinsi gani huu mfuko utaendeshwa ili tuondokane na yale matatizo ya awali yaliyotukumba kwa zile fedha maarufu zikiitwa za JK ambazo watu waliona ni za bure na hata hizi shilingi milioni 50 wananchi kule wanafikiria ni za bure, hapana! Tunaomba tuwaambie wananchi hii itakuwa ni revolving fund, mnakopa kwa riba iliyo ndogo ili na wengine waweze kukopa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie uwezekano wa kwenda angalau kata chache kwa kila Jimbo. Kupeleka shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji itahitaji fedha nyingi sana. Sasa hivi tukiangalia makusanyo ya ndani ya Halmashauri, zile asilimia 10 kwa ajili ya vijana na akinamama wanaojitokeza kukopa hawakopi kwa kiasi kingi. Kwa hiyo, hata hii shilingi milioni 50 kwa kuwa itahitajika hela nyingi na makusanyo yetu hayatoshelezi kama bajeti ilivyo, basi tuangalie kata chache ziwe kama za mfano tuguse kila Jimbo angalau hata kata mbili shilingi milioni hamsini hamsini ndiyo tuanze kama mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamezungumzia kuhusu mapato. Naomba nichangie, zile ripoti, Chenge I na II bado Serikali irudi mle ikapekue. Suala la deep sea fishing hatujalisikia na masuala mengine. Kwa hiyo, tunaomba sana kwenye hii bajeti, Waziri wa Fedha na Kamati ya Bajeti mrudi kwenye ile ripoti ya Chenge I na II muangalie maeneo yote ya mapato ambayo yalielezwa ambayo yatasaidia katika bajeti yetu. Mwelekeo wa bajeti ni shilingi trilioni 32, tunatoka kwenye shilingi trilioni 29. Sawa, mmeweka vyanzo vingine pale lakini muangalie jinsi gani tunaweza tukafika hata shilingi trilioni 34 kutokana na vyanzo vingine vipya vya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamelalamika kuhusu Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye utalii, basi Serikali ifanye utafiti, je, kweli hii kodi ambayo imewekwa kwenye auxiliary services za watalii imepunguzwa kwa kiasi gani ili watu wapate uelewa? Nafikiri wakati Waziri Mkuu anafunga Bunge, naomba Waziri wa Maliasili na Utalii ampe hiyo taarifa aweze kuisoma hapa tupate uelewa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara imeshazungumzwa upande wa transit goods, tumeweka VAT ambayo imeleta mgogoro sana na mizigo yetu mpaka kupungua. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais jinsi alivyoweza kujenga mahusiano na viongozi wa nchi jirani na sasa biashara imeanza kurudi na tumeona kwenye vyombo vya habari hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya kilimo kama ndiyo Uti wa Mgongo na asilimia 70 ya ajira. Tunaomba ruzuku iongezwe na pembejeo zije kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo ambalo bado hatujaona ni jinsi gani tunaweza kupata fedha ni upande wa mifugo. Tuweke blocks za ulishaji na watozwe. Kwa hiyo, Serikali iangalie suala hili na tupunguze migogoro hii ya wakulima na wafugaji na tuone ni kwa jinsi gani tunaweza kupata mapato kutoka kwenye mifugo, hili ni eneo ambalo bado hatujaliweka sawa. Tunatoza mifugo tu inapouzwa mnadani lakini kwa kila siku inavyokuwepo na uharibifu wa mazingira kama tunavyoelewa, tuangalie tunawekaje tozo katika mifugo ili tuweze kuongeza mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati wameeleza suala la utawala wa Kibunge kwamba Bunge sasa litakuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wabunge na Kamati nyingi hazikuweza kwenda kukagua miradi ikiwa ni sehemu ya kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 63 kwamba Bunge tuna wajibu wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali. Sasa tunavyoenda kama Kamati kukagua miradi ya Serikali ndipo tunapoisimamia. Kamati nyingi hazijafanya safari na maslahi ya kiujumla kwa mfano, je, Mbunge anatakiwa akakae hoteli ya nyota ngapi? Kwa hiyo, tuangalie maslahi ya Wabunge na gharama kiujumla katika kufanya kazi zao za kuweza kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyokagua miradi ndiyo tunatia chachu kwa watumishi wetu kule, wakisikia Kamati inakuja ndipo utaona mambo mengi yanakwenda mbiombio wanakimbizana. Tunapotoa maagizo inasaidia sana katika kutekeleza miradi na ndipo tunaleta tija kwa wananchi ili waweze kujua kwamba Serikali yao sasa imewaletea miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho naomba niseme kwamba, tunaenda nchi ya viwanda lakini tunaomba Serikali iangalie uwiano. Siku za nyuma Hayati Mwalimu Nyerere alijaribu kuangalia uwiano wa Kikanda kuweka viwanda ili kuweka usawa katika ajira. Kwa mfano, Mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora, Chunya wanalima tumbaku. Je, hatuna haja Serikali ikashawishi NSSF au PPF, hii Mifuko ya Jamii wakaingia ubia na Vyama vyetu vya Msingi kutoa mchango wao kwa kujenga kiwanda Tabora ili …
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Kwanza
nianze kwa kuunga mkono hoja za Kamati zote mbili, Kamati ya Mindombinu na Kamati ya
Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwa haraka, hoja yangu ya kwanza ni kutoa
msisitizo kwa Serikali juhudi ambazo wameonyesha katika vipande vingine upande wa reli
kwenda kwenye standard gauge basi wasisahau na reli yetu ya Mpanda ambapo inaanza
kuchepuka kutokea Kaliua kwenda mpaka Mpanda na vilevile reli kufanyiwa usanifu kutokea
Mpanda mpaka Karema, upande wa Karema tunatarajia kuwa na bandari ambapo pana
upana mdogo katika Ziwa Tanganyika na upande wa pili wa nchi yetu ya jirani ya DRC.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa hizi reli pamoja na bandari kule Karema ni
kupitisha mizigo, sasa na tunaona nchi nyingi ambazo hazina bandari (landlocked conutries),
tutumie hiyo fursa ili tuweze kuongeza mapato katika bandari yetu. Taarifa ya Kamati
imeonyesha jinsi gani mizigo kwenye bandari imeweza kushuka kwa asilimia 0.1 na sehemu
nyingine asilimia 5.2, kwa hiyo tuombe sana Serikali iangalie reli upande wa Wilaya ya Mpanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwanja wetu wa ndege wa Mpanda, uwanja wa
ndege wa Mpanda hauna gari la zimamoto, hamna mkandarasi wa mafuta, kwa hiyo tunahitaji
Serikali iweze kushawishi hivyo vitu. Tuna Mbuga ya Katavi ambapo ni moja ya maeneo ya
mbuga ambayo wanasema ni very virgin, wanyama wana asili sana, ukienda Mbuga ya Katavi
utaona asili yao ukishuka kwenye gari samba anakimbia, tofauti na maeneo mengine kama
Serengeti. Kwa hiyo, uwanja wa ndege huu ni muhimu sana kwa ajili ya utalii kwenye Mbuga
yetu ya Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la mawasiliano tunahitaji kampuni za simu
ziendelee kuimarisha mawasiliano, na hasa Kampuni ya Halotel ambayo ilianzia vijijini, maeneo
yetu mengi tuna matatizo ya mawasiliano. Ukiwa unasafiri kutoka Mpanda kuja Tabora kuna
maeneo ya katikati unatembea kilometa karibu 90 hakuna mawasiliano, sasa inapotokea
dharura yoyote na dunia sasa hivi iko kwenye kiganja, kwa hiyo, tunaomba Serikali iendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la SUMATRA, mamlaka hii ipo lakini usimamizi wa bei
bado ni hafifu sana. Tumepata kero nyingi kwenye ziara tulizozifanya, kwa mfano watu wetu
wanaotoka Mpanda kwenda Ugala wote wanachajiwa shilingi 5,000 lakini katikati hapa kuna
sehemu wanatakiwa walipe shilingi 2,000, shilingi 3,000 na shilingi 4,000 lakini wote wanalipa bei
moja. Kwa hiyo, SUMATRA wasiwe wanasubiri malalamiko ya wananchi, wawe wanafanya
testing ya hizi control zao zinafanyaje kazi na wachukulie hatua watu wenye vyombo hivi vya
usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapohapo kwenye mawasiliano, TCRA watusaidie
Halmashauri zetu, na ningeomba mwongozo wa Serikali, hii minara inakuwa na rekodi ya
mawasiliano yamefanyika katika lile eneo na yale mapato ambayo yametokana na kampuni
za simu kwenye mnara husika.
Sasa ile service levy haya makampuni wanalipa wapi? Kwa hiyo, unakuta Halmashauri
zetu hazipati mapato toka kwenye makampuni ya mawasiliano kwa sababu ya mawasiliano au
muunganiko katika ya TCRA na Halmashauri kidogo uko tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye madini, tumekuwa na changamoto kwa
wachimbaji, wamekuwa na migogoro na watu ambao wamepewa leseni. Kwa mfano kwenye
Jimbo langu la Nsimbo, eneo la Kijani Investment imekuwa ni mgogoro, Kampuni ya Sambaru
imekuwa ni mgogoro wanasema hakuna muhtasari, sasa shida iliyopo ni nini, tungeomba
Serikali itenge maeneo kwa ajili ya watu ambao hawana leseni, watu leo anaamua akachimbe
anunue unga au alipe ada na yawe chini ya uongozi wa kijiji ndiyo uweze kusimamia. Tukifanya
hivyo tutaondoa migogoro kwenye haya maeneo ya watu ambao wanakuwa na leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile upatikanaji wa service levy toka kwenye makampuni
haya yanayochimba yenye leseni ndogo (PML) na leseni kubwa, rekodi zao haziko sahihi kwa
hiyo, Halmashauri zetu hazipati service levy. Kwa hiyo, nashauri Serikali iangalie fixed amount
kulingana na aina ya leseni na sehemu nyingine iwe ya kiasilimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe upande wa nishati, REA III, kwa Mkoa wetu wa Katavi
vijiji 74 haviko kwenye huu mpango wa sasa hivi, kati ya vijiji 191 tumepewa vijiji 117 na ni mkoa
wa pembezoni ambao ulisahaulika sana kimaendeleo. Kwa hiyo, tunaomba vijiji 74 viongezwe
na wakandarasi waongezewe mikataba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, tunaomba Serikali iendelee kutoa ushirikiano kwa
kampuni inayofanya utafiti wa mafuta Ziwa Tanganyika na pia gesi na maeneo mengine ya
madini katika Mkoa wa Katavi na mikoa jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja za Kamati
hizi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika,
nakushukuru kwa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu kwa
kuweza kutufikisha siku hii ya leo. Binafsi naomba nimpongeze
Waziri Mkuu na timu yake na Mawaziri wote kwa jinsi
ambavyo wameshirikiana naye katika kuandaa bajeti hii.
Naomba nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama na
Naibu Waziri, Mheshimiwa Mavunde kwa kushiriki vyema
kwenye bajeti hii pamoja na uwashaji wa mwenge Kitaifa kwenye Mkoa wetu wa Katavi. Wametupa ushirikiano wa
hali ya juu, tumekwenda nao na wamefanya kazi kubwa
kwa kweli tunawapa pongezi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo,
naomba kidogo nigusie kwenye hotuba ya Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Mbowe. Kuna mahali
alizungumzia kwamba bajeti ya Serikali ni ya kisiasa, kwamba
ina vyanzo hewa vya mapato. Naomba alichukue hili, yeye
hotuba yake ndiyo ya kisiasa kwa sababu kwenye hotuba
yake ile amesema kwamba Serikali kwenye bajeti ya mwaka
2016/2017 iliweka chanzo cha kodi kwenye kiinua mgongo
cha Wabunge wakati kodi hiyo itakwenda kutozwa mwaka
2020. Naomba nimwambie kwamba yeye ndiyo amefanya
kisiasa, sio sahihi. Nakumbuka mwaka jana nilileta schedule
of amendment kwenye eneo hili na Kanuni ilifuatwa, kulikuwa
hakuna financial implication kwenye masuala ya kodi kwenye
kiinua mgongo cha Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kwenye bajeti
hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu ameweza kuzungumzia kwa kina
kuhusu uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Naunga mkono,
wameweza kutoa shilingi bilioni 1.5 kwa vijana kutoka kwenye
ofisi yake na takribani shilingi bilioni 4.6 kwa upande wa
mapato ya ndani kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tatizo ninaloliona ni
Halmashauri nyingi kutotimiza ile kanuni inayoelekeza kutoa
asilimia tano kwa vijana na asilimia tano kwa akina mama.
Kwa hiyo, niombe sasa ili tuweze kufikia kuwawezesha
wananchi wetu kufanya shughuli za kiuchumi, Serikali iweke
msisitizo kwenye kuhimiza Wakurugenzi na kuwasimamia ili
waweze kuhakikisha kwamba fedha hizi zinakwenda, maana
Halmashauri nyingi maombi yapo lakini watu hawajapewa
hizo fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia yale mafunzo ambayo
yaliweza kutolewa chini ya Ofisi hii ya Waziri Mkuu kupitia
VETA, Don Bosco, tunaomba yawe endelevu na hapa ndipo itakapokwenda kutusaidia katika kujenga ajira maana kuna
watu wameweza kupata mafunzo haya na cheti. Naomba
Serikali, Halmashauri zetu tuna mwongozo tunapeleka
magari yetu kwa mfano TEMESA, lakini utaangalia gharama
ile ambayo Halmashauri zinalipa kule TEMESA kwa baadhi
ya huduma ni ghali sana.
Kwa hiyo, tuombe sasa Serikali kwa mafunzo haya
ambayo yanaendeshwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tuweke
ajira za mikataba kwa watu ambao wamepata mafunzo
ya ufundi ili tuwe na mafundi wetu katika Halmashauri
tupunguze gharama ambazo zinakuwa hazina tija kwa
upande wetu, tukiwezesha vijana tayari tumejenga suala la
ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni migogoro.
Ofisi ya Waziri Mkuu hili liko chini yenu kuna CMA na Mabaraza
ya Wafanyakazi lakini kuna matatizo ya watumishi
wanakuwa wanahamishwa bila tija tu kwa malalamiko ya
baadhi ya viongozi. Utakuta kiongozi eneo moja tu
analalamika kwa makosa ambayo mtu anaweza
akasahihishwa basi anahamishwa, kwa hiyo, tunaongeza
gharama kwa Halmashauri na ndiyo tunazidi kuweka madeni
upande wetu wa Serikali kwa uhamisho ambao hauna tija.
Tunakumbuka wakati Mheshimiwa Rais alivyoapishwa
alisema kwamba hatamhamisha mtu, mtu atakuwa
anachukuliwa hatua za kinidhamu kwenye eneo ambalo
yuko. Sasa tunaomba Ofisi ya Waziri Mkuu itoe mwongozo
kwa Wakurugenzi wasifanye uhamisho ambao hauna maslahi
ya kihalmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la Bunge letu
hili. Wabunge wamechangia, tumeona kwamba kuna
ongezeko la bajeti karibu shilingi bilioni 21. Napenda kujua,
kwa mwelekeo mpaka mwisho kuna upungufu wa shilingi
bilioni 21 na gharama nyingine za msingi ambazo Serikali
iliweza kuziomba na kuziahirisha, je, hii bajeti ya sasa hivi ya
shilingi bilioni 121 kweli inakidhi? Kwa hiyo, tuangalie zile
gharama nyingine, kwa mfano, ile wiki ya kwanza kutokana
na Kanuni tarehe 11 Machi hatukuweza kufika, je, ile gharama imekuwa-incorporated kwenye hiyo shilingi bilioni 21? Kwa
hiyo, tunaomba kwa misingi ya Katiba kama Bunge
tunaofanya hiyo kazi bajeti hii iweze kuangaliwa kwa undani
zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea kuhusu
walemavu. Ofisi ya Waziri Mkuu ina wajibu huo na sheria ipo
ya mwaka 2010, Sheria Na. 9 na kuna Mabaraza ya
Walemavu katika ngazi ya Kitaifa, Mkoa mpaka kwenye Kata.
Je, nani mwenye wajibu wa kuhakikisha kwamba Mabaraza
ya Walemavu kwenye Kata na Wilaya yanafanya kazi na
kanuni zake zipo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofanya kazi
TASAF basi na walemavu wawe na mfuko wao tuweze
kuwawezesha iwe ni sehemu ya ruzuku na isiwe mkopo
ambao una riba na wapewe mafunzo kulingana na ulemavu
mtu alionao ili aweze kufanya kazi yoyote ile. Siku moja redioni
nilisikia mtu mwenye ulemavu wa macho anampima mtu na
anashona nguo. Kwa hiyo, tunahitaji sana tuwaendeleze ili
waweze kuondoka kutoka kwenye utegemezi. Kwa hiyo,
tuombe sasa Ofisi ya Waziri Mkuu huu mfuko kama haupo
basi muuanzishe na angalau hata kabla Bunge hili
halijamalizika tuweze kuupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Mifuko ya
Jamii. Mwaka 2012 tuliweka sheria ya kuzuia lile fao la kujitoa
lakini sina uhakika, ila ni kwamba NSSF japokuwa hii sheria
ilikuwa inazuia waliweza kuendelea kutoa fao la kujitoa. Nchi
yetu tunahitaji hii mifuko ya hifadhi ya jamii iweze kusaidia
katika kuleta viwanda na tumeona maelekezo kwenye
randama humu kuna karibu mikoa 14 ambayo mifuko ya jamii
inaelekezwa kwenye kuwekeza. Maoni yangu kwa sababu
kuna mwingine anakuwa ameachishwa kazi na hana uhakika
wa kupata kazi basi Serikali iangalie angalau katika lile fao
la kujitoa ama akate asilimia 25 ya akiba mtu aliyonayo au
theluthi moja yule mtu aweze kupewa ili katika kipindi cha
mpito wakati anatafuta kazi ziweze kumsaidia katika
kuendeleza maisha aliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa kisekta
tunajua tuna Wizara zinahusika na haya mambo ya kisekta,
upande wa viwanda, lakini nizungumzie kuhusu barabara
ambayo kwenye bajeti hii ipo, ya Mpanda - Tabora kwa
kiwango cha lami. Tender zilitangazwa lakini mpaka sasa
hatujafahamu ni watu gani wamekwishapewa hizo tender
kutokana na marekebisho ya mkandarasi mshauri. Kwa hiyo,
tuombe watu wa TANROADS watuharakishie. Sisi tukifanya
ziara kule wananchi wanatuuliza ujenzi wa barabara kwa
kiwango cha lami Mpanda mpaka Tabora lini unaanza? Sasa
kama fedha ipo tulishapata toka ADB kwa nini watendaji
wetu wa TANROADS Makao Makuu wanachelewesha
kurekebisha hiyo BOQ ili kazi ziweze kuwa awarded?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa kilimo
tumeona taarifa kwenye mpango, kilimo kimekuwa kimekua
kwa asilimia 2.9 tofauti na malengo ya asilimia sita. Sasa tatizo
ni nini na hapa ndiyo ajira kubwa ya wananchi wetu ilipo.
Kwa mfano, Jimbo langu la Nsimbo asilimia 90 ya wananchi
wangu ni wakulima wanalenga zaidi kwenye shughuli hii ya
upande wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa maliasili, tuna
Mbuga yetu ya Katavi, tunahitaji miundombinu iboreshwe
na huduma ya Bombardier ya ATCL ianze ili watalii waje. Tuna
viboko, Ziwa la Katavi, twiga mweupe ambaye atakuwa
ndiyo kivutio zaidi kwa watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo,
naunga mkono bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ahsante.

The Valuation and Valuers Registration Bill, 2016

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza namshukuru Mungu kwa siku ya leo, lakini pia naipongeza Serikali kwa ujumla na hasa Wizara husika kwa kuweza kuwasilisha muswada huu. Mazuri mengi ambayo tutafaidika kwenye muswada huu yameelezwa ikiwa ni mambo ya fidia, watu kufanya kiutaalam, mambo ya mikopo, wawekezaji na kupunguza utapeli kwa ujumla. Naipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Waziri Mkuu alifanya ziara Mkoa wa Katavi na Rukwa, aliweza kutatua kero ya ardhi kuhusu utapeli wa wanakijiji waliokuwa wanatapeliwa. Pamoja na hayo kuna masuala madogo ambayo naomba Mheshimiwa Waziri akija aweze kutupa ufafanuzi au kuelewa kwa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni ukataji wa rufaa kama ambavyo ameeleza kwenye hotuba yake, lakini kwa haraka haraka sijaona kifungu cha kisheria ambacho kinamwezesha mtu aliyefanyiwa thamani au kuthaminiwa kwamba atakitumia kwa ajili ya kukata rufaa na endapo hajaridhika na Mthamini Mkuu hiyo rufaa yake anaweza kuipeleka wapi? Tutaomba Mheshimiwa Waziri aweze kutufafanulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile endepo Mthaminiwa atakuwa haridhiki na uthamini uliofanywa na Serikali, je, kuna uwezekano wa kumweka Mthamini wa binafsi (independentvaluer) halafu iingie kwenye Bodi? Hilo nalo Mheshimiwa Waziri tutaomba utusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika muswada huu Kifungua cha 25 kinazungumzia adhabu kwa lugha nyepesi tuiite vishoka, lakini pia ukienda Kifungu cha 62 kwenye masharti ya jumla kinazungumzia adhabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kifungu cha 25 kwamba mtu atapewa adhabu kati ya shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 20 ikiwa ni mtu, lakini kama ni kampuni ni shilingi milioni 20. Ukienda kwenye masharti ya jumla Kifungu cha 62 kinazungumzia adhabu itakuwa kima cha juu ni Shilingi milioni tano au kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naona hivi vifungu viwili kama vinaoana kutokana na makosa; kwa sababu kifungu cha 25 ni mtu ambaye hana cheti; lakini ukienda kifungu cha 62 ni mtu ambaye anafanya kazi, mtu ambaye hajasajiliwa, kwa hiyo, wanafanana na wanaoana kwamba mtu ambaye hajasajiliwa ni sawa sawa na mtu ambaye hana cheti. Kwa hiyo, hizi hesabu tusiwe na double standard na kuondoa katika maamuzi ya mahakama kutokuweka mazingira ya rushwa, basi adhabu iwe ya aina moja kati ya kifungu cha 25 na 62.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu taarifa ya utekelezaji, kwamba Bodi ikishafanya kazi yake baada ya mwaka, itatakiwa ndani ya miezi mitatu itengeneze taarifa ya utekelezaji. Sasa katika kifungu cha 61 inaelekeza Bodindani ya miezi minne wapeleke taarifa kwa Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri copy ataipeleka katika Bunge, ikiwa Bunge maana yake ni Kamati husika. Sasa wasiwasi wangu ni kwamba taarifa hii itakuwa ni taarifa ambayo haijakaguliwa na Mkaguzi wetu, CAG.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwenye kifungu hiki, taarifa iende kwa Mheshimiwa Waziri wakati imekwishakaguliwa ili anavyoileta katika Bunge iwe ni taarifa ambayo imeshapita kwa Mkaguzi Mkuu. Ukiangalia zile timing ni mwezi Septemba na mpaka mwezi wa tatu ambapo Mkaguzi Mkuu anatoa taarifa zake. Kwa hiyo, hilo nalo tutaomba Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia, ikiwezekana basi alete schedule of amendments nyingine baada ya mapendekezo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu cha 57, inazungumzia masuala ya adhabu. Sasa kuna lugha pale imenitatiza kidogo, inasema Bodi itakavyoona. Kwa hiyo, tumeacha uhuru,Bodi iangalie ni adhabu kiasi gani. Sasa ni bora kwamba Waziri atakapotengeneza kanuni kwa kurejea kifungu hiki cha 57, aangalie ni adhabu gani ambazo Bodi itaweza kuzitoa kuliko kuacha mazingira yaBodi kufanya uamuzi wakati kosa limetokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu kingine ambacho ningependa kuchangia ni kifungu cha 49 kwamba Mthamini anavyoandika report anatakiwa aandike sababu za kufanya huo uthamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni bora Waziri katika upande wa zile kanuni aoanishe hizo sababu, tuwe na sababu ambazo ni standard ili watu wetu wanavyoandika hizi report za huu uthamini ambao wameufanya, mtu asitoe sababu zake na lugha zake ambazo zinakuwa hazieleweki; tuwe tayari na sababu zionyeshwe kwenye kanuni ambazo zitakuwa ni standard.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wengi tunahitaji kuchangia, nishukuru kwa leo, ni hayo tu. Ahsante sana.

The Chemist Professionals Bill, 2016

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza, nimpongeze Waziri na Naibu wake na kwa msaada wa Mwanasheria Mkuu kuweza kuuleta muswada huu tuweze kuujadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo lingekuwa ni maoni katika hii miswada ambayo tunapatiwa ni suala zima la tafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili, wakati mwingine kunatufanya Wabunge kidogo tuweze kuelewa tofauti. Kwa mfano, unakuta Kiingereza kinasema kwamba Mkemia Mkuu anateuliwa na Rais lakini ukienda kwenye Kiswahili imetafsiriwa kwamba Mkemia Mkuu atateuliwa na Waziri. Sasa inakuwa inatupotosha kwenye upande wa Kiswahili na sisi wengine siyo wengi tunaojua lugha hii ya Kiingereza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala zima la huu muswada, muswada uko vizuri, nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kuweza kupokea maoni ya Kamati lakini na sisi Wabunge tuna maoni kidogo ambayo tungeomba yaingie na tutaweza kuleta Jedwali la Mabadiliko.
Sehemu ya kwanza ni kifungu cha 5(2)(a) katika dawa zilizotajwa pale upande wa kemikali zimetajwa tu za viwandani lakini kiujumla kwenye huu muswada tuna kemikali za viwandani na za majumbani. Sasa labda Waziri atatuambia ilikuwa ni kosa la kusahaulika au kiutaalamu kwenye kifungu hiki cha 5(2)(a) kwamba kemikali za majumbani hazitakiwi kutajwa. Hiyo tutaileta kwenye schedule of amendment.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine ni kwenye sifa za Mkemia Mkuu. Kifungu 10(1) kinasema kwamba Mkemia Mkuu atateuliwa na Mheshimiwa Rais. Sasa kwenye sifa pale kuna uzoefu na masuala ya elimu, lakini kuna kitu kimoja ambacho kimesahaulika. Leo hapa tuna miswada miwili, wa Maabara na Wataalam (Chemist Professional Act). Sifa mojawapo ya Mkemia Mkuu ambaye atateuliwa na Rais awe ni yule ambaye amesajiliwa katika Baraza letu la Wataalam wa Mambo ya Kemia, hilo nalo ni muhimu sana. Kuna watu ndiyo wamesoma, wana elimu nzuri lakini unakuta kwamba hayuko professional, mtu ana miaka 20 na elimu yake. Hata wenye fani zingine za uhasibu kama sisi kama hujasajiliwa na Bodi ya Uhasibu wewe siyo mhasibu, ni karani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi kimesema sifa awe ni mtu ambaye amefanya kazi kwenye taasisi za Serikali. Kwa mujibu wa michango ambayo imetolewa na Wabunge hapa tunahitaji tupate Mwenyekiti wa Bodi ambaye hatakuwa tu na uzoefu wa mambo ya utumishi lakini pia awe na utaalam wa mambo ya kemia ili awe ni mtu ambaye anasimamia vizuri hiki chombo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 7(2) katika ile Bodi nzima kuna mwakilishi anayetoka Wizara ya Afya. Ukiangalia katika ile Bodi nzima ina wataalam wa fani mbalimbali, kuna mtu anayetoa Hazina, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kwenye vyuo lakini tungeomba kwa sababu hii taasisi ni nyeti na ni mambo ya kitaalam sana hayahitaji ubabaishaji basi mwakilishi anayetoka Wizara ya Afya awe angalau na uzoefu hata wa miaka mitatu na elimu yake iwe ya mambo ya kemia ili aungane na yule mwingne ambaye anatoka kwenye upande wa vyuo ambaye amesomea mambo ya kemia, pathology na baiolojia na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye huu muswada, kifungu cha 13(1) tumeona kwamba katika teuzi za watu wa maabara Waziri anashauriwa na Mkemia Mkuu lakini ukienda kifungu cha 14 kwenye uteuzi wa wakaguzi Waziri anashauriwa na Bodi. Sasa ukienda kwenye hierarchy maana yake kifungu cha 13 pale Bodi inakuwa imerukwa, Waziri anashauriana moja kwa moja na Mkemia Mkuu kwa hiyo Bodi itakuwa haijui Mkemia Mkuu na Waziri wameshauriana nini. Kwa hiyo, tunahitaji kifungu cha 13(1) Waziri ashauriwe na Bodi. Kwa hiyo, hii nayo tutaileta kwenye schedule of amendment. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 15 cha wajibu wa hawa wakaguzi kwenye kuteketeza zile sampuli, pale inaonesha kwamba huyu mkaguzi aidha yeye au kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinaweza kuteketeza hizi sampuli ambazo zimetumika kwa mujibu wa hii sheria, lakini sasa ukiangalia hapa tunakuwa hatuna ule udhibiti (internal control). Kwa hiyo, tungeomba kwamba ashirikiane na isiwe ni mbadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine ni cha 39 cha mambo ya mahesabu. Tunahitaji tuangalie kwamba baada ya mwaka wa fedha kuwe na miezi mitatu ya kuandaa ripoti halafu tena miezi mitatu inaongezeka kwa ajili ya ukaguzi, halafu ndiyo inaenda kwa Waziri na kwenye Bunge. Hapa kwenye hii Bill yetu tumeweka miezi mitatu ambapo mahesabu yanakuwa hayajafungwa. Kwa hiyo, lazima iwe miezi sita kwa Waziri kupewa na miezi mitatu wawe wamekamilisha kufunga mahesabu kama ilivyo kwenye Sheria ya Fedha. Pia director‟s report ni muhimu sana iwepo kwenye hii taarifa ili sasa aoneshe mwenendo mzima wa hii taasisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa professionals na yenyewe inaendana na hii kwenye mahesabu hapa vipindi viko tofauti. Tutavileta kwenye schedule of amendment ili Bunge liweze kutuunga mkono ili tuendane na sheria zingine za mambo ya fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa yoye hayo, naomba kushukuru na naunga mkono hoja.

The Tanzania Agricultural Research Institute Bill, 2016

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi, nitaenda haraka kidogo kwa sababu muda siyo rafiki sana. Kwanza niipongeze Serikali na Wizara husika kwa kuweza kuwasilisha huu Muswada, kwa sababu sasa hivi Serikali yetu mwelekeo ni kwenye nchi ya viwanda na tukiangalia nchi ya Tanzania imebarikiwa sana. Tuna Bahari, tuna Maziwa katika hii dunia tumebarikiwa mno. Kwa hiyo, hizi sheria kuja kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali inabidi tuziboreshe na ziweze kutumika ipasavyo kwa ajili ya kunyanyua uchumi na kutengeneza ajira katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Muswada huu kuna maoni maeneo mbalimbali ambayo nimeweza kuyaona, nikianzia na Muswada huu wa agriculture, kuna comment ilitoka kuhusiana na mambo ya mifugo. Ingekuwa ni bora iunganishwe iwe ni kilimo na mifugo ili na wenyewe tuweze kutengeneza ajira na kunyanyua uchumi, mifugo iweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kifungu cha Nane uteuzi wa Mkurugenzi kinaeleza kwamba Rais atamteua baada ya kushauriwa na Waziri. Tumepitisha Miswada takribani minne, lakini ushauri kama huu nakumbuka hapa haukuungwa mkono suala la kushauriwa Rais kupitia Mawaziri wetu katika uteuzi. Kwa hiyo, itabidi tuwe na consistency tuweke kama katika Miswada mingine ambayo tumepitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Baraza la Taifa la Ushauri. Naona tuone jinsi gani ya kuhusisha pia na Bodi mbalimbali za Mazao wawe ni moja ya Wajumbe kwenye hili Baraza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 14 ni maeneo ya tafiti, lakini nilivyoangalia humu ndani kuna baadhi ya Mikoa ambayo imesahaulika kuwekewa kuwa ni sehemu pia ya Vituo vya Tafiti. Kwa mfano; mapendekezo ambayo nitayaleta Mkoa wa Njombe tuwe na Kituo cha Utafiti ili kiweze kukidhi Mkoa wa Iringa na Ruvuma; na pia Mkoa wa Katavi tuwe na Kituo cha Utafiti ili tuweze kukidhi Mikoa ya Katavi, Kigoma na Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu cha 16 kwamba tutakuwa tuna-commission baadhi ya kazi, sasa ni wakati gani ambapo tutaweza kuwajengea uwezo vijana ambao wamemaliza kwenye vyuo vyetu, kwa nini tusiwajiri na wafanye hizi kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tukienda Kifungu cha 18(2) kwamba Taasisi inaweza ikafanya biashara kwa kuuza, kununua hizi tafiti. Ningeshauri kwamba Waziri ajaribu kuangalia tusije tukauza utafiti ambao ukatoka na Tanzania isiweze kufaidika. Tukienda Kifungu cha 19, kuhusu utangazaji wa matokeo ya utafiti, tumeonesha tu kwamba tuna-review na kupitia kwa mtu ambaye ametutumia mali za Taasisi na kufanya utafiti, ili tuweze kuwa na tafiti zilizo bora, nitashauri Waziri aangalie hata wale ambao wanafanya tafiti kwa gharama zao wenyewe wawe wanakuwa reviewed na hii Taasisi ili tuwe na matokeo mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 20 kimenifurahisha kuhusu kufanya utafiti mpaka nje ya mipaka. Tunakumbuka Vietnam miaka ya 1970 walichukua zao la korosho lakini walichukua kwetu wamepeleka nchini kwao na ni moja ya nchi duniani ambazo zinatoa sana zao la korosho. Kifungu cha 20(3) kuna masuala ya watu ambao wameathirika kutokana na huu utafiti, tutaomba Waziri aziweke athari kwenye Kanuni ili ziweze kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 23, mtu anayeomba kusajiliwa kama Mtafiti au Taasisi yake anaweza akakataliwa, lakini hapa hakuna nafasi ya jinsi gani mtu anaweza akakata rufaa au akarekebisha makosa aliyoyafanya na kuweza kuomba tena, hilo nalo tutaomba Waziri aliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya utafiti kufanywa na mtu wa nje lazima ashirikiane na wa ndani yaani Mtanzania kifungu cha 24, basi kwenye Kanuni ielezwe faida itakayopatikana, Mtanzania atakuwa na asilimia kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la adhabu, masuala ya adhabu kwa makosa mbalimbali hayana consistency, adhabu zake kidogo zimekuwa ni ndogo na suala ambalo limepigiwa kelele sana mtu anapofanya kwa nia njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa research, upande wa Wavuvi, Kifungu cha 6(1)(c) kwamba utafiti na uchunguzi magonjwa ya samaki lakini kwenye maji hatuna samaki tu, tuna viumbe wengine pia wanaishi ndani ya maji sasa wenyewe kuhusu magonjwa yao utafiti hautafanyika? Kuna hadithi zile za nguva, tuna mamba, tuna viboko, tuna vyura na tuna nyoka wengine ambao wanaishi ndani ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wavuvi kuna Kifungu cha 8(4) kidogo kinanitatiza hapa, Waziri anapewa Mamlaka ya kubadilisha kwa namna yoyote ile atakavyoona suala la Jedwali baada ya kuwa ametangaza. Sasa majedwali tunapitisha humu ndani Bungeni na hayo marekebisho Waziri akifanya atarudisha tena Bungeni? Kwa hiyo sioni haja ya kumpa Mamlaka haya Waziri kufanya mabadiliko kwenye majedwali wakati majedwali haya tumepitisha hapa ndani Bungeni maana yake akifanya marekebisho lazima alete tena huku. Kwa hiyo, ni bora tumwachie huru kwenye upande wa Kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine upande wa Wavuvi ni uteuzi wa Naibu Mkurugenzi. Ametajwa lakini kazi zake hazijatajwa. Kwa hiyo, tutakuwa na mtu ambaye functionally atakuwa yupo kusubiri Mkurugenzi hayupo yeye ndiyo akaimu, hivyo sioni haja ya kuwa na Naibu Mkurugenzi katika hii sheria na nitaleta mapendekezo kwamba aondolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mtu ambaye hajakamilisha utafiti arudishe gharama, sasa je, akishindwa na hizo adhabu zimetajwa? Kwa hiyo basi, tuweke mazingira ya kwamba mtu awe na dhamana kwa pesa tunayompa ili akishindwa utafiti basi iwe ni moja ya kinga ya kumwezesha kurudisha pesa ambayo tuliweza kumpatia kufanya hiyo kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la kuomba vibali katika kifungu cha 20, napendekeza taasisi yenyewe ndiyo itoe kibali na siyo mtu aende kwenye Tume ya Sayansi na Teknolojia, tutaweka ukiritimba kwenye utoaji wa vibali kwa watu wanaotaka kufanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni dhana nzima ya watu ambao wamefanya vizuri, kuna suala la intellectual property inabidi tuliangalie kwa umakini zaidi ili watu wetu ambao Mungu amejaalia na wameweza kufanya utafiti waweze kufaidika na kile ambacho wamejaaliwa. Kifungu cha 31, masuala ya report, kinasema siyo chini ya miezi miwili, hii inatakiwa iwe miezi mitatu na kifungu cha 33 imeandikwa miezi mitatu kwenye report ambayo imekaguliwa iwe angalau miezi sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala mengine ni jedwali; tumetaja bahari, tumetaja vituo lakini tumesahau Ziwa la Rukwa ni moja ya Ziwa kubwa nalo liingie kwenye jedwali la kwanza kama moja ya vituo vya utafiti kwa sababu hata hivyo hivi karibuni tu Serikali ilisema kuna madini yamepatikana kule ambayo ni adimu. Mapendekezo mengine nitayaleta kwenye jedwali la marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's