Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Albert Ntabaliba Obama

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa asilimia mia moja. Naomba kutoa mchango wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Waziri unatambua kwamba Wizara yako iliahidi kushughulikia wizi uliofanywa na Karinzi Coffee Organic kwa kununua kahawa kwa wakulima 435 wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Manyovu 2014/2015 ambapo Serikali iliwaahidi kulipa malipo hayo ya dola za Kimarekani 75,000. Karinzi Coffee Organic inasema Kiwanda cha Kubangua Kahawa hawajawalipa. Tunakuomba kufuatilia suala hili kwani ni kero inayokatisha tamaa wakulima wa kahawa, tunakualika ufike Manyovu ukutane na wakulima wa kahawa kwani wewe utakuwa mkombozi wao.
Naomba ufuatilie juu ya kero ya pembejeo, muda wa pembejeo hizo kulingana na maeneo. Mkoa wa Kigoma unapokea mbolea nje ya muda ambapo tija yake haipatikani. Pili, wajibisha na tumbua majipu ya wezi wa pembejeo, Mawakala na Wakuu wa Wilaya.
Mwisho, nawatakia mafanikio mema.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze hotuba nzuri ya Waziri wa Elimu. Kwa ufupi naomba nichangie yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uandaaji wa Walimu. Tunaomba Wizara isimamie vyuo vya Walimu kwa karibu kwani vyuo vingi ubora umepungua sana:-
(i) Maabara za sayansi hakuna katika baadhi ya vyuo, kufanya Walimu kukosa umahiri wa ufundishaji; na
(ii) Walimu wa Hesabu. Ubora wa Walimu wa hesabu umepungua na kufanya output kuwa hafifu. Nashauri programu maalum ya hamasa kwa Walimu wa hesabu Kitaifa na kutoa zawadi maalum kwa wakufunzi wa hesabu. Hesabu ni tatizo kubwa kwa watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa VETA. Tunaomba kuleta maombi ya kujengewa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Buhigwe kwani ni Sera ya Wizara yako ya kujenga Chuo cha VETA kila Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa Nyumba za Walimu/Madarasa. Kwa kuwa, bajeti ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI ni ndogo, kwa nini Wizara ya Elimu isishirikiane na Social Security Fund (Mifuko) ili iwasaidie kujenga na Serikali kuwalipa yearly?
Mheshimiwa Mwenyekiti, TCU na Bodi ya Mikopo. Nashauri Wizara isiishie tu kufukuza, naomba uchunguzi uende mbele zaidi kwani inaonekana rushwa ipo kubwa kwenye sekta hizi mbili; maamuzi ya kubadili Secretaries ni muhimu sana, nao wanaweza kuwa ni chanzo cha rushwa. Bodi ya Mikopo wapewe malengo makubwa ya kukusanya mapato kuliko kuachwa kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri zaidi:-
(1) Fanya ziara za kushtukiza katika taasisi zako.
(2) Komesha siasa mashuleni.
(3) Toa zawadi kwa vyuo bora kwa vigezo vya Wizara.
(4) Toa zawadi kwa wanaofaulu hesabu.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza Mawaziri wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Napenda kusisitiza kwamba kwa kazi nzuri mnayoifanya ingawa bajeti yako ni ndogo sana kulingana na mahitaji ya nchi hii, ninayo machache ya kuchangia:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya kati ni ukombozi wa wananchi wengi ndani ya nchi hii. Tunaomba Serikali ilifanyie kazi kwani sasa ni hitaji kwa wananchi na kusafirisha mizigo mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mnamila – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, tunaomba ipewe umuhimu wa kipekee kwani ni kero kubwa sana. Kigoma nayo ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais aliahidi kutupatia fedha za kupasua barabara mpya za Nyakimue hadi Muhinda, Rusaba hadi Nyamboze, Kibande hadi Nyamugali, Kilelema hadi Mugera, Munzeze hadi Kwitanga, Kajana hadi Kasumo, Mwayaya hadi Buhigwe. Tunaomba fedha za kupunguza urefu kwenda makao makuu ya Wilaya, kwani ni kero kubwa sana, bajeti ya Wilaya hairuhusu kupasua barabara mpya. Tunaomba mtusaidie na ahadi ya Rais iweze kutekelezwa. Tunaomba special fund na wataalam waje wapitie barabara hizi na cost analysis iweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho tunawatakia mafanikio mema.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mawaziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wa Wizara hii. Napenda kuchangia yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Buhigwe Makao Makuu tunashukuru umeme umefika na baadhi ya vijiji umeme umefika. Tatizo ni kwamba kati ya vijiji 48 tumefikisha umeme vijiji tisa tu. Tunaomba kipaumbele kwani Mkoa wa Kigoma tumeachwa sana na mikoa na wilaya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, REA III, tunaomba vijiji vyangu vya Wilaya ya Buhigwe vipate kuwekewa umeme kwani imeanza kuwa kero na siasa kupamba moto kwamba CCM hawawapendi. Kata ambazo hazijapata umeme Buhigwe ni Muhinda, Janda, Munzeze, Mkatanga, Kibwigwa, Kibande, Munyegera, Kilelema, Kajana, Mugera, Bukuba, Kinazi na Rusaba
Mheshimiwa Naibu Spika, jamani tuoneeni huruma.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawakumbusha kuwa vijiji vyetu ni vikubwa sana na wananchi ni wengi, tunaomba transformer za kutosha kwani vijiji vilivyopata vitongoji, wengine wanalalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Wizara kwa uamuzi wa kuzalisha umeme pale Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nawatakia ufanisi bora wa kazi zenu.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Waziri na Naibu Waziri na timu yake kwa kuandaa hotuba nzuri ya bajeti yetu ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeisoma bajeti hii, naiona katika mambo yafuatayo:-
Kwanza, bajeti hii inajaribu kutuambia kwamba lazima watu wawajibike. Watu walioomba fedha kwenye Taasisi, Wizara, lazima wawajibike! Hata hivyo, nikiiangalia inajaribu kutuonesha kwamba nidhamu ya matumizi kwa walichopangiwa ni kitu muhimu sana. Pia inanionesha kwamba fedha zilizopangwa zinabadili mwelekeo kwa yale tuliyoyazoea na hatimaye kuwaza mambo mapya. Jambo la mwisho naiona kama inaenda kulenga maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nimesoma kitabu chake cha Hali ya Uchumi ukurasa wa 10 pale, kuna kitu amekisema kizuri sana pale. Hali ya umaskini; ametaja mikoa yeye mwenyewe kwamba kuna mikoa ambayo kipato chake ni kidogo. Mikoa mitano yenye umaskini mkubwa wa kipato ni Kigoma, asilimia 48.9, Geita asilimia 43.7, Kagera asilimia 39.3, Singida asilimia 38.2, Mwanza asilimia 35.3. Sasa nataka nimuulize; je, anafurahia kuitaja tu humu au ana mikakati gani aliyoipangia mikoa hii? Hii Mikoa ambayo anafurahia kuiandika kwenye vitabu vyake, kwenye bajeti ili aweze kuikomboa amepanga kitu gani? Hiyo ndiyo, ningependa atuambie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu naangalia Mkoa wangu wa Kigoma, Mheshimiwa Waziri ameutaja kwamba ni maskini. Jimbo langu lina mgogoro na Serikali yake, vibanda 120 katika Kijiji cha Mnanila walijenga kwa kupewa ramani na Halmashauri yao, lakini TANROADS wakaja wakavunja na mpaka sasa wanawadai, kila kibanda milioni nane, jumla yake ni shilingi milioni 960, wamewafanya maskini, hawataki kuwalipa, lakini kuwaandika kwenye vitabu kwamba ni maskini wanapenda! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wakulima 435, Waziri wa Kilimo yupo hapa Mwigulu Nchemba nimemwona, wamelima kahawa yao wameuza, wamepeleka kwenye vyama vyao vya ushirika ambavyo wamewapa leseni mpaka sasa wakulima hao tangu msimu uliopita fedha zao hawajalipwa. Bado anapenda awaandike kwamba hao watu wa Obama au watu wa Kigoma ni maskini na watu wanalima hawawapi hela zao! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kigoma katika mipango ya REA, Kigoma ni kati ya mikoa ambayo mpaka sasa hivi performance yake ni ndogo sana, ni Serikali yake hiyo anayoandika kitabu kwamba Kigoma wako nyuma na huku hawataki kuwapelekea fedha. Hivyo hivyo ukienda kwenye data za maji, ukienda kwenye pembejeo, Mkoa wa Kigoma tunapata pembejeo kidogo na zinakuja zimepitwa na wakati, lakini wanapenda watuandike kwamba sisi ni maskini! Kwa hiyo, hayo mambo mengine tunaomba mikakati ya kuokoa mikoa hii sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo hizi fedha milioni 50 ambazo mmesema, najua na nina uhakika, Mkoa wa Kigoma haujapangiwa kuanza na hizi fedha. Mnapeleka kule ambapo ni matajiri. Je, kama mnaionea hii mikoa kwa nini tusianze na hizi fedha zikaenda kwenye mikoa hiyo waliyoitaja? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili sikupendezwa nalo ni kuhusu madhehebu ya dini kwamba wanapoagiza vitu vyao walipie kodi kwanza halafu ndiyo waje wa claim! Tujue kwamba nature ya madhehebu yetu mengine yana shule, mengine yana hospitali na hawana fedha, kwa hiyo, ningeomba hilo mliangalie ili tusije kuwa na matatizo na madhehebu yetu ya dini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye pay as you earn, katika kitabu page 60, Rais alikubali kwamba pay as you earn itakuwa digit kutoka 11 kwenda tisa lakini ukiangalia ile schedule watumishi wa Serikali wanaonufaika na hiyo asilimia tisa ni wachache sana kwa sababu inatakiwa uwe chini ya 170,000. Kwa hiyo, watumishi kule wanafurahia kwamba Serikali imepunguza lakini digit za pale juu ni kuanzia asilimia 20, asilimia 25 mpaka asilimia 30, kwa hiyo kile kilio cha watumishi wengi hata Walimu wanaokuwa wanafurahia hakitaweza kuwafaidisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine tumeandika kwenye hotuba yetu ya Kamati ya Bajeti, nami nilikuwa sehemu ya Kamati, sina mengi ya kusema nilitaka nimkumbushe Waziri kuhusu hiyo mikoa maskini anayoisema ana mikakati nayo ipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

The Public Procurement (Amendment) Act, 2016.

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niwezeze kuchangia muswada ulioko mbele yetu wa kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016.
Kwanza kabisa naomba nipongeze Serikali, nimpongeze Waziri na Naibu wake, kwa kutuletea sheria nzuri kabisa ambayo itaweza kutuokolea fedha nyingi. Kwenye bajeti ya mwaka huu tumepitisha asilimia 40 ya fedha zote kwenye shughuli za maendeleo; sasa kama tumepitisha asilimia 40 maana yake ni fedha nyingi. Fedha nyingi hizi, bila kuwa na sheria ya kuzilinda hazitafikia wananchi. Kwa hiyo naomba niipongeze Wizara kwa kweli, na Mheshimiwa Waziri Mpango, kwa kuleta mpango mzuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya muswada huu wa kupunguza gharama na kuleta ufanisi ni jambo jema ambalo wote Wabunge lazima tuliunge mkono ili sheria hii iweze kufanya kazi. Lakini nipongeze kipekee kwa sheria hii kuja kuangalia wazawa, kwamba wale wenye makampuni ya wazawa, local waweze kupewa kipaumbele, nalipongeza sana na naipongeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kujali makundi mbalimbali, kina mama, walemavu, wazee ni jambo jema na Serikali makini lazima iangalie watu wake na makundi yake waweze kushiriki kwenye uchumi huu, kwa hiyo nalo nisuala ambalo nimesimama kuipongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ku-promote local production ya bidhaa zetu ni jambo zuri ambalo kwa kweli nahamasisha kwamba Wabunge wengine tuweze kuiunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria imekwenda mbele zaidi kwa kurekebisha ushiriki wa Madiwani kwenye manunuzi. Mimi naishurukuru Serikali kwamba kazi ya Madiwani iwe ni kuisimamia Serikali kwa maamuzi iliyoyafanya, siyo na Madiwani kuwa wanashiriki kwenye tender ambacho kinakosesha ile roho yenyewe ya usimamizi wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu uko kwenye bei ya soko. Hatuna tafsiri ya bei ya soko na sioni kama kuna mtu yeyote anajua bei ya soko. Bei ya soko inategemeana na bidhaa yenyewe, lakini kwa kuwa ni manunuzi ya Serikali, mimi nilikuwa napenda kwamba Serikali iwapongeze wazabuni na wakandarasi wote, kwa sababu wakandarasi hawa wanaikopesha Serikali, kabla hawajawalipa. Kwa hiyo wana umuhimu mkubwa sana katika Serikali hii, kwamba wanafanya vitu in advance kwa kutumia fedha zao, Serikali inakuja kuwalipa baadaye. Kwa hiyo hawa ni wabia muhimu sana; na hasa kwenye PPP tunayoisema kila siku, kwa hiyo mimi naona kwamba bei ya soko ili tuweze kuipata Waziri inabidi sasa ujipange, je, unazo fedha za kuwalipa wakandarasi kwa muda ili waweze kukupa bei ya soko?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama unawalipa baada ya mwaka, miezi sita hakuna mfanya biashara yeyote mwenye kampuni ambaye anaweza ku-predict bei ya vifaa baada ya mwaka mmoja, kwa hiyo lazima aweke bei ambayo itakuja ku-compensate loss yoyote ile atakayo ipata. Lakini ni vizuri ujipange sasa kwa fedha hizi uweze kuwalipa wazabuni, na wenyewe watakupa bei ya soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipo kipengele cha kujadiliana ni kipengele kizuri, lakini wasiwasi wangu itakuja kuleta migongano ya makampuni kulingana na ulivyofanya majadiliano, kama ulijadili na kampuni moja ambayo unaitaka ipate na ikashusha bei na ukaiacha nyingine, hapa ndio utakuwa ni kwenye mgogoro. Kwa hiyo hiki kipengele ni vizuri tukiangalie kwa makini, tuweze kujua namna ya kuja kutatua migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali kwenye ujenzi kwa nini isiboreshe vituo vyake vya ujenzi, kwa kununua mitambo, ma-grader ili gharama ya kutengeneza barabara iweze kupungua. Kama mnataka gharama zipungue basi ningeshauri kwamba mboreshe kila Wilaya ipelekewe mitambo ya ukandarasi, iwepo kitengo cha ujenzi, na iwe inatengeneza barabara wawe weka mafuta na madereva wanaajiriwa. Hiyo inawezekana, kama mmeamua kwamba tuweze kupunguza gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko emergency procurement ambayo kwa kweli naona kwenye muswada huu haijasema vizuri, labda kwenye kanuni za Waziri, Hospitali huwa zinaishiwa gloves, zinashindwa kununua kwa sababu mlolongo wa manunuzi umekuwa mrefu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ninakuomba kwenye ununuzi wa ghafla hasa kwenye dawa hospitali, MSD ni vitu muhimu lazima uziweke kwenye kanuni, kama hujaweka kwenye kanuni mtu anaweza akafa nashindwa mtu kuchukua hela ofisini au ndani ya kituo kwa sababu milolongo ya manunuzi iko mbali; kwa hiyo kanuni tunaomba uweze kuiweka vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sina mengi, ninashukuru na sheria ni nzuri tuipe nguvu tuipe support, nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye kwa kutuandalia sheria nzuri, na mara nyingi amekuwa akifanya hivyo, naye tunampongeza sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Aida Joseph Khenani

Special Seats (CHADEMA)

Questions (3)

Supplementary Questions (3)

Contributions (5)

Profile

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Lupa (CCM)

Questions (7)

Supplementary Questions (10)

Contributions (4)

Profile

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Songwe (CCM)

Questions (2)

Supplementary Questions (6)

Contributions (4)

Profile

Hon. Mbaraka Salim Bawazir

Kilosa (CCM)

Questions (0)

Supplementary Questions (1)

Contributions (3)

Profile

Hon. Sabreena Hamza Sungura

Special Seats (CHADEMA)

Questions (2)

Supplementary Questions (3)

Contributions (2)

Profile

View All MP's