Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naitwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi niungane na wengine waliotangulia kusema kukupa pole na mtihani mzito uliokukuta tangu tukupitishe huna hata siku tatu humu Bungeni. Lakini mimi nishauri vyombo vya ulinzi na usalama hali hii ilionekana kwa muda mrefu tumeiachia kwa muda mrefu, na kilichonisikitisha kwa sababu nimekuwa Mkuu wa Wilaya karibuni miaka kumi, ni pale ambapo na vyombo vyetu vya dola vilipoingia humu ndani vikaanza ku-negotiate muda wote waliosimama tunajiuliza hivi wanafanya nini pale wakati kitu umeshatoa amri. Mimi niombe sana tukiendelea kufanya hivi wenzetu hawa watadharau na vyombo vya dola, yaani imeniumiza sana nimeona hili niliseme kabla sijachangia kitu chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nizungumzie sekta ya viwanda, kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini tunalima michikichi, michikichi ndiyo inaleta mafuta ya mawese, lakini kinachosikitisha kwenye hii hotuba ya Mheshimiwa Rais anazungumzia dhamira yake ya kuanzisha viwanda kwenye ukurasa wa 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wamalaysia walikuja Kigoma kwa ajili ya kuchukua mbegu, leo Wamalaysia ndiyo wanaoongoza kuzalisha mafuta ya mawese lakini Kigoma kama Kigoma mpaka leo tumebaki kwamba tumetoa mbegu na mbegu zimekwenda Malaysia hata kama na wao walikuwa na michikichi yao walitambua fika kwamba mbegu ya Kigoma ndiyo mbegu bora, wakaipeleka Malaysia na kwenye takwimu zao wanakuambia mwaka 2011 Pato la Taifa Malaysia zao la mchikichi lilikuwa ni kama zao la nne kuwaingizia mapato, income ile ya Taifa, na wanakwambia walipata kwenye ile ringgit pesa yao ile wanaita ringgit, ringgit bilioni 53 sawa na dola bilioni 16,000.8.
Lakini sisi Kigoma mpaka sasa hivi mawese yanatengenezwa na wanawake wale wa kijijini na tunatengeneza kwa ile teknolojia ya kizamani ya asili, tunachukua masufuria makubwa tunachukua katika ule mti wa mchikichi ukishatoa ngazi kuna yale yanayobaki yale ndiyo tunakoka moto, tunaweka masufuria makubwa au mapipa tunachemsha ngazi, tukimaliza tukamua, ndiyo haya mawese mnayoyaona kwenye soko la Kariakoo pale Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana mimi inaniuma sana nilikuwa nimeingia kwenye website inayozungumza masuala ya palm oil, nikaona kwamba Tanzania yaani sisi tumejiweka kabisa kwamba Tanzania siyo nchi ambayo iko tayari ku-produce mafuta ya mawese. Inasikitisha kwa sababu moja, sisi pale tuna Lake Tanganyika, Congo DRC, lakini hata Congo Brazzaville, Burundi, Rwanda, Zambia tuna uwezo pia wa kuwapelekea mawese, kwa sasa tu kwa teknolojia yetu hiyo ya kizamani lakini bado tunayatoa mawese Kigoma, tunayapeleka Burundi, tunayapeleka Rwanda, tunayapeleka Congo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe sana hii dhamira ya Mheshimiwa Rais wetu, hebu tuombe Wizara husika ione namna ya kutuletea wawekezaji kwenye Mkoa wa Kigoma watuanzishie basi kiwanda cha mawese. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mchikichi hili ni zao la mchikichi tunatoa pia sabuni, wengi mnazifahamu zile sabuni za rangi mbili ambayo ina rangi nyeupe na blue, zile sabuni zinatengenezwa kwa mise. Mise ni ile mbegu ya mchikichi tukishatoa mawese tunabaki na ile mbegu ya ndani ndiyo inayotengeneza sabuni. Sasa mimi niombe viwanda vya sabuni inawezekana kabisa tukavitumia pale Kigoma na angalau uchumi wa wanawake, hasa wanawake wa Kigoma ukaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile huwezi kuzungumzia viwanda bila kilimo, hapa wajumbe wengi wamezungumzia kilimo cha tumbaku. Kilichonisikitisha ni kama vile tumbaku inalimwa tu Tabora, jamani tunalima tumbaku Wilaya ya Uvinza na ndiyo maana Tarafa ya Nguruka pale taasisi ya kifedha hii ya CRDB imeona umuhimu kuja kufungua benki pale hawafungui hivi hivi. Kama wangekuwa hawapati faida wasingekuja kufungua branch ya CRDB pale Nguruka, wamefungua kwa sababu wanajua zao la tumbaku ndiyo zao ambalo pia linatuingizia sisi Halmashauri ya Uvinza kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka Disemba Halmashauri ya Uvinza, tumepata shilingi milioni 800 kwenye zao la tumbaku, ndiyo Halmashauri inayoongoza kupata ile own source kupitia zao la tumbaku. Kwa hiyo, mimi niombe Mheshimiwa Waziri Mwigulu anapokuja asisahau kulifuatilia na hili zao la tumbaku hata kama hatuna Chama Kikuu ndani ya Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie reli. Kwenye ukurasa wa 12 Mheshimiwa Rais amezungumzia umuhimu wa kujenga reli kwa maana ya kuboresha inayotoka Dar es Salaam, Tabora, Mwanza na Kigoma. Lakini vilevile amegusa reli ya Uvinza, kwa maana ya kutoka Uvinza, Msongati, Burundi, Isaka, Kigali, Rwanda.
Mimi niombe sana Wizara husika tusiwe tunazungumza tu maneno ambayo hayatekelezeki, niombe kweli kweli Uvinza siyo ile mnayoifahamu, maana tatizo ukisema wewe Mbunge wa Kigoma Kusini, watu wakikumbuka Mbunge aliyepita alikuwa maneno mengi humu Bungeni wanadhani tuna hali nzuri, tuna hali mbaya sana Jimbo la Kigoma Kusini. Hatuna maji, barabara hatuna, umeme wenyewe umewashwa wiki tatu zilizopita tangu uhuru, umeme kwenye Jimbo la Kigoma Kusini tulikuwa hatuna umeme. Tumewashiwa umeme kwenye Kata tatu, Kata ya Kandaga, Kata ya Kazuramimba, Kata ya Uvinza na kwa kupambana mimi kuongea na Mkurugenzi wa TANESCO Ndugu Mramba na namshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno mengi hatuna maendeleo yoyote katika Jimbo la Kigoma Kusini, niombe sana Serikali iliangalie Jimbo la Kigoma Kusini kwa jicho la huruma, safari hii wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini wamepata Mbunge, wamempata Mbunge wa vijijini, hawajapata Mbunge wa Mataifa. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini na niwaambie ule upotevu na maneno mengi ya propaganda yanayoenezwa kule Jimboni, mimi ndiyo Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini. (Makofi)
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana nitawatumikia na tumeshaanza kazi nzuri, sasa hivi tunajenga zahanati karibu vijijini 20; tunaongeza madarasa kwenye shule ambazo miaka kumi shule ina darasa moja hapa mtu alikuwepo anajiita eti Mbunge wa Mataifa, Mbunge wa Dunia, Mbunge wa Dunia kwa wananchi waliokupa kura. Mimi niwaombe sana wananchi wa Jimbo langu la Kigoma Kusini kwamba niko imara nachapa kazi propaganda zinazoendelea Jimboni msizisikilize Mbunge wenu niko hapa, nitawafanyia kazi na Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itaniunga mkono kuhakikisha tunatekeleza ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala moja lililozungumzwa hapa nadhani alikuwa Msigwa maana wote tumemsikia, tusiwa-criticize ma-RC na ma-DC. Bila ma-RC na ma-DC amani na utulivu kwenye maeneo yetu…
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono hoja hotuba ya Rais. (Makofi/Vigelegele)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nichangie kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu Kigoma Kusini lina jumla ya shule za msingi 119; lakini kati ya hizo tuna shule nne zina darasa moja na zingine zina madarasa mawili. Kwa kweli hali ya shule hizi inatisha; nyumba za walimu hakuna, nimwombe Mheshimiwa Waziri, aliangalie Jimbo la Kigoma Kusini kwa jicho la huruma ukizingatia miundombinu ya barabara kuwafikisha walimu kutoka wanakopanga nyumba hadi kwenye shule ni mibovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri ahakikishe bajeti ya Halmashauri ya Uvinza inakuja bila kukosa kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017. Wilaya ya Uvinza tuna shule mbili za A-level na O-level za Lugufu Boys na Lugufu Girls; nimuombe Mheshimiwa atusaidie kuzisajili kuwa ya bweni ili ziweze kupata mgao wa chakula kwani tangu zianze zimekuwa ni za bweni ilhali zilisajiliwa kama za kutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe pia Mheshimiwa Waziri, atusaidie kusajili shule mbili mpya za sekondari za kata za Mloakiziga na Basanza. Kwani wanafunzi wa kata hizi mbili wanatembea zaidi ya kilometa 15 kufuata sekondari za kata za jirani. Kwa kuwa hizi ni nguvu za wananchi tuiombe Wizara ijitahidi kuzisajili japo kuwa hazijakuwa na miundombinu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie pia uhaba wa vyoo. Kwenye shule zangu za Jimbo la Kigoma Kusini niombe pesa za ujenzi na ukarabati zielekezwe kama tulivyoomba kwenye bajeti ya Halmashauri ya Wilaya kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uhaba wa nyumba za walimu ni tatizo kubwa ndani ya Jimbo langu. Sambamba na haya niombe Wizara ituletee walimu kwani Halmashauri ya Wilaya, bado ina uhaba wa walimu hususani walimu wa sayansi na walimu wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nitoe pongezi kwa dada yangu Mheshimiwa Waziri Profesa Joyce Ndalichako, kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, kuteuliwa kuwa Mbunge na kupewa dhamana ya kuiendesha Wizara hii nyeti ya kufuta ujinga kwa watoto wetu. Nizidi kukuombea afya na achape kazi kwani wanawake tukipewa nafasi tunaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi kwa namna unavyoliongoza Bunge. Naomba kuchangia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa maandishi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kigoma Kusini liko Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma na ni Jimbo ambalo wananchi wake wanajishughulisha na kilimo cha michikichi pia ni wavuvi. Naomba Waziri aone namna ya kuwapatia wananchi wa uvinza miche ya michikichi ya kisasa inayozaa kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema wawekezaji wako tayari kuja kuanzisha viwanda vya mawese Uvinza. Namwahidi Mheshimiwa Waziri kama Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, niko tayari kuhamasisha wakulima wa zao la michikichi, kulima zao hili kwa nguvu zote na mimi pia nitakuwa mfano wa kulima zao hili la michikichi. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atupe kipaumbele kutuletea mbegu ya michikichi ya muda mfupi ili na sisi wananchi wa Uvinza tuweze kupata wawekezaji wa kuja kuanzisha viwanda. Pia nampongeza sana Waziri kwa mipango yake mizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie viwanda vya uvuvi. Wananchi wa Uvinza pia ni wavuvi wa samaki na dagaa, hivyo, kwa kuwaanzishia viwanda itawasaidia wavuvi kupandisha thamani mazao haya ya uvuvi. Hivyo naomba Mheshimiwa Waziri, mipango yako hii mizuri izingatie kuwaletea wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini viwanda vya Mawese na Viwanda vya Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichangie Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu, niwashukuru pia na wapiga kura wangu wa Jimbo la Kigoma Kusini kwa dua na maombi yao yaliyowezesha kesi iliyokuwa na mvuto mkubwa zaidi ya miezi sita hatimaye tarehe 17 Mahakama imeweza kutupilia mbali shauri la Ndugu David Kafulila. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nijikite kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Kwenye Wilaya yangu ya Uvinza tuna matatizo katika baadhi ya maeneo kwa mfano kwenye Kata ya Uvinza kuna Kitongoji cha Tandala. Kile kitongoji kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na wananchi wanaishi pale, lakini tatizo kubwa ambalo liko pale wananchi hawawezi kufanya shughuli yoyote ya maendeleo kwa sababu wanaambiwa pale ni eneo la hifadhi. Sasa unajiuliza inakuwaje eneo la hifadhi ambalo wananchi wanaishi zaidi ya miaka 35.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye hotuba yake ameonesha kwamba kwenye Halmashauri za Wilaya ana hekta karibu milioni 3.1, lakini kuna maeneo mengine yapo tayari yanakaliwa na wakaazi, tungeomba maeneo kama hayo yaweze kuachiwa na hatimaye yatumiwe na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hicho Kitongoji cha Tandala hawana shule, wanasoma kwenye kibanda. Nimeweza kuwasaidia vitabu, nimewasaidia vifaa mbalimbali vya kujifundishia, kuna mzee mmoja amejitolea pale kufundisha watoto, watoto hawawezi kutembea kutoka pale mpaka kwenye Kijiji cha Chakuru kwenda kutafuta elimu. Kwa hiyo, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hapa hoja yake, basi aweze kuangalia maeneo kama hayo, Wizara iweze kuachia tuendelee na masuala ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo vilevile tatizo kama hilo kwenye Kata ya Nguruka, Kitongoji cha Nyangabo. Tunalo eneo la hifadhi linaitwa Rukunda Kachambi, nimeenda kutembelea pale, unakuta nyumba ya mkaazi hii hapa na GN iko nyuma ya choo. Wananchi wamebanwa kabisa, hawawezi kulima na hawawezi kufanya shughuli zozote za maendeleo. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri washirikiane na Wizara ya TAMISEMI kama ikiwezekana zile GN zisogezwe ili wananchi wapate maeneo ya kulima na kufanya shughuli zao za kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye Kata ya Itebula tuna eneo linaitwa Ipuguru. Eneo la Ipuguru ni hifadhi lakini kwa bahati nzuri hakuna wanyama wowote mle kwa zaidi ya miaka 20. Sasa kwenye maeneo kama hayo tungeomba basi hata wakulima waruhusiwe, lakini hata wafugaji pia waruhusiwe kutumia maeneo hayo. Wafugaji wamekuwa wanahangaika, wanaingiza mifugo yao kwenye mashamba, wanaingiza mifugo yao kwenye maeneo mbalimbali kwa sababu hakuna maeneo halisi ya kuchungia mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuna eneo la Kurora, nadhani Mheshimiwa Waziri analifahamu. Hili eneo lilitengwa kwa ajili ya matumizi bora ya ufugaji, lakini kwa bahati mbaya wakulima wamevamia na kusababisha wafugaji watoe mifugo yao na ianze kuhangaika kwenye mashamba. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha ajaribu kuangalia kwenye Wizara yake kuna maeneo mengi yanaitwa kama hifadhi lakini kwa bahati mbaya wananchi wameshavamia na vijiji vimeshasajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namsikia Mheshimiwa Magdalena Sakaya hapa anazungumza kwamba Tabora wana zaidi ya vijiji 50 vimesajiliwa kisheria ndani ya hifadhi. Tatizo hilo Mheshimiwa Waziri na sisi pia tunalo. Kwa mfano, sisi tuna ile Hifadhi ya Mahale ambayo ipo kwenye Kijiji cha Kalilani lakini Waziri anafahamu kuna mgogoro wa zaidi ya miaka 20 baina ya wananchi wa Kalilani na watu wa hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu mgogoro unapelekea mpaka watu wa hifadhi hata zile shughuli za kijamii za kuwachangia wananchi wa Kijiji cha Kalilani wanakuwa hawatekelezi na badala yake wanakwenda kusaidia vijiji vingine ambavyo havipakani na ile Hifadhi ya Mahale. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili, ni mgogoro ambao uko ofisini kwa Mheshimiwa Waziri akiuliza ataambiwa. Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Kinana alipokuja tulimwambia na tulimkabidhi documents zote kwamba mgogoro baina ya wananchi wa Kijiji cha Kalilani na watu wa Hifadhi ya Mahale, tunaomba Mheshimiwa Waziri auangalie ili utatuliwe waweze kukaa kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba pia nitoe shukrani kwa watu wa TANAPA kwa sababu sisi kwenye ile Hifadhi ya Mahale watalii wanapokuja wanatumia usafiri wa boti kwa sababu barabara hakuna. Tunazo kilometa kama 30 ambazo mtu hawezi kupita kwa gari na tuna mito kama mitatu ambayo inahitajika ijengewe madaraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru watu wa TANAPA kwenye bajeti hii ya 2016/20167, wameweza kututengea shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kutengeneza barabara ile na tulipitisha kwenye kikao chetu cha barabara cha Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, nimeona pia nitoe shukrani zangu za dhati maana wangeweza kupeleka sehemu nyingine, lakini wameona waje kusaidia ili watalii nao waweze kupita bila tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia Mheshimiwa Waziri aangalie sana kama inawezekana kuboresha zile speed boat za Mahale kwa sababu kwenye Ziwa Tanganyika tuna kitu kinaitwa Rukuga, ni upepo mkali sana, unapokuwa mkali hata meli ya Liemba haiwezi kupita. Hata kama sikuangalia kwenye bajeti kama wametenga namna yoyote ya kuboresha usafiri maeneo yale, naomba waone umuhimu wa kuwaongezea watu wa Mahale speed boat nyingine kwa ajili ya kubeba watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 32. Asubuhi mdogo wangu Mheshimiwa Doto alichangia kuhusiana na masuala ya unyanyasaji wa wafugaji kwenye hifadhi. Mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Mbogwe ilizaliwa kutoka Bukombe, Mkoa mpya wa Geita. Matatizo hayo kwenye Hifadhi ya Kigosi wakati yametokea kwenye ile Operesheni Tokomeza, nilikuwa Mkuu wa Wilaya pale. Kwa kweli kabisa alichosema mdogo wangu ni kweli, unyanyasaji ni mkubwa sana. Wanapowakamata, hawawakamati tu kwamba wafuate sheria, sheria imewekwa kwamba watu wanapokamatwa wameingiza mifugo kwenye hifadhi wachukuliwe hatua gani. Wale maaskari badala ya kufanya hivyo wanawa-harass wale wananchi na wanawapiga risasi ng‟ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge kwamba tuko hapa leo kuipitisha bajeti ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii, tunatambua fika kwamba Mheshimiwa Waziri ndiyo kwanza amepewa dhamana kwenye hii Wizara na hii ndiyo bajeti yake ya kwanza. Kwa hiyo, badala ya kumshambulia au kum-attack moja kwa moja tumpe ushauri ili aweze kupokea, aangalie upungufu uliojitokeza kwenye Wizara yake siku za nyuma na aweze kuyafanyia kazi. Huu ndiyo ushauri ambao napenda kuutoa. Namfahamu Mheshimiwa Maghembe, najua ni mchapakazi na msikivu, yote haya tunayoyasema hapa atayasikia, atayapokea na atayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee tu kumtakia kila la kheri Mheshimiwa Waziri na nimwambie kwamba aangalie sana sekta ya wanyama pori. Wale maaskari wanaolinda hifadhi hizi wamekuwa ni shida kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niombe Mheshimiwa Waziri wa Maliasili kuna mambo mengine wawasiliane pia na Waziri wa Kilimo. Kwa mfano, haya matatizo ya mifugo kuvamia hifadhi na wakati Uvinza tunazo ranch za Serikali kama tatu lakini zile ranch inaonekana siku za nyuma walipewa watu ambao hawako tayari kuzitumia na badala yake wanazikodisha kwa pesa nyingi. Kwa hiyo, kwenye matatizo kama haya wakae chini Wizara na Wizara, kwa mfano Wizara ya TAMISEMI na Wizara hii waone matatizo hayo ya GN ambazo zimeingia mpaka kwa wananchi walikojenga waweze kusogeza ili kutatua migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.

The Tanzania Fisheries Research Institute Bill, 2016

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nishukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hii Miswada miwili kwa maana ya Muswada wa mambo ya uvuvi lakini pia na Muswada wa masuala ya kilimo. Naomba nijikite kwenye huu Muswada wa Uvuvi kwa sababu kwenye Jimbo langu tunalo Ziwa Tanganyika na limekuwa maarufu sana kwa kutoa samaki anayeitwa mgebuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye hii taarifa yake aliyotoa, kwenye mambo muhimu ya Muswada huu kuna kipengele hapa kinasema kuweka utaratibu na kumbana mtafiti anaposhindwa kuwasilisha taarifa ya mwisho ya utafiti. Siku za nyuma tulikuwa na Kampuni ya Wagiriki iitwayo YOROGWE ilifanya kazi ya utafiti na ilikuwa inavua samaki kwa kutumia meli zile kubwa. Ziwa Tanganyika lina kina kirefu sana duniani lakini ninachojaribu kusema…
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kigoma wale ambao wamezungukwa na ziwa hili kwa maana ya Jimbo la Kigoma Kaskazini, Jimbo la Kigoma Kusini na Jimbo la Kigoma Mjini wanashindwa kuvua samaki walio wengi kwa sababu zana zao za uvuvi haziwafai kwenda chini zaidi. Hii Kampuni ya Wagiriki ambayo ilikuwa inatwa YOROGWE wakati inavua Kigoma wale samaki walikuwa hawaishi kwa sababu walikuwa wanatumia zana zenye hadhi ya kuvua samaki kwenye Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba tunaweka sheria hii na na-support kwamba utafiti wa kina uweze kufanywa, lakini Wizara iwe inahakikisha hawa watu wanapofanya utafiti wawe wanatoa taarifa pia kwenye Halmashauri husika zinazozunguka hilo Ziwa Tanganyika. Kwa mfano, kwenye miaka ya 2000 tumekuwa na wenzetu hawa wa FAO ambao waliwahi kufanya utafiti na wakatoa taarifa kwamba Ziwa Tanganyika lina aina ya samaki zaidi ya 250.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuulizane ukizungumzia Ziwa Victoria unazungumzia sato na sangara lakini sangara ametolewa Ziwa Tanganyika. Walifanya utafiti, wakamchukua sangara kutoka Ziwa Tanganyika wakampeleka Ziwa Victoria na hatimaye ndiyo wakampa jina la sangara. Sangara ni jamii ya singa na nonzi kutoka Ziwa Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali ikilitumia vizuri Ziwa Tanganyika kupitia Wizara ya Kilimo na Mifugo tunaweza kuingiza kipato cha Taifa kwa kuvua samaki wengi walioko kwenye ziwa hili. Hata hivyo, kinachoonekana bado Wizara haijajipanga vizuri kutumia mazao haya ya uvuvi kwenye Ziwa Tanganyika ili kuiingizia kipato Serikali yetu. Kwa hiyo, tunapitisha Muswada huu mzuri lakini pia tuweke taratibu za kuwabana watafiti watakaofanya utafiti kwenye maziwa yetu haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo maana nikitaja tu samaki tunaowavua kwenye Ziwa Tanganyika kwa kutumia zana zetu hizo hizo ambazo siyo bora, tuna samaki ambaye anaitwa babukubwa, kuhe, nonzi, sangara, singa, kibonde, kavugwe, kuku maji, mibanga, jamani tuna zaidi ya samaki 30 wanavuliwa na wavuvi wa Kigoma kwa kutumia zana ambazo hazina tija. Je, Serikali ikiweka nguvu, ikawapa wavuvi zana ambazo zina tija tutavua samaki wangapi kwenye Ziwa Tanganyika? Tutaingiza shilingi ngapi katika Taifa letu? Sisi tumepakana na Zambia, Burundi na Kongo na mazao haya ya samaki na dagaa tunakwenda kuuza Kongo, Burundi, Rwanda na Zambia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilimsikia mchangiaji mmoja kama sikosei Mheshimiwa Haonga alikuwa anazungumzia namna ambavyo dagaa wa Ziwa Viktoria wanavyopelekwa Kongo. Sasa fikiria mpaka dagaa wa Ziwa Viktoria wanaenda Kongo. Kwa hiyo, ninachojaribu kuomba hapa ndugu zangu ni kwamba tuweke akili yetu yote kwenye mazao ya uvuvi. Nimepitia taarifa ya Kamati nimeona imejikita kwenye Muswada wa Kilimo tu haijajikita kwenye Muswada wa Uvuvi. Sasa nikapata shida, hivi kilimo ndiyo kinaingiza zaidi mapato kushinda zao la uvuvi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba katika utafiti huu tusijikite tu kwenye utafiti wa kilimo tujikite pia na kwenye utafiti wa zao la uvuvi. Kwa mfano, sisi watu wa Kigoma tunao mwalo pale Mwakizega. Tumejenga mwalo mzuri na Halmashauri sasa hivi inaendelea kuumalizia japo wavuvi wameshaanza kuutumia ili angalau kupandisha hadhi mazao yao ya dagaa na samaki waweze kupata kipato zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachoomba Serikali itupie jicho la huruma kwenye majimbo haya matatu, Jimbo la Kigoma Kusini, Kaskazini na Mjini ili kuwawezesha wavuvi wetu kwa zana zenye ubora zaidi ili waweze kuzitumia kuvua samaki wengi na kuongeza kipato cha Halmashauri zetu lakini pia kipato cha nchi maana tunawatoza ushuru. Kwa mfano, gunia moja la dagaa, wavuvi wanalipa Sh.3,000 mara wavuvi waliopo ni shilingi ngapi, ni pesa nyingi. Hizi ni own source zinazoingia kwenye Halmashauri zetu na sisi tunazielekeza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya majimbo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili nichangie pia kwenye upande wa Muswada wa Kilimo. Niunge mkono taarifa ya Kamati ya kutoa pendekezo lao la uanzishwaji wa Mfuko Maalum wa Utafiti wa Kilimo. Nimekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Newala na Mtwara, Naliendele hawana tu uwezo wa kutafiti zao la korosho bali wanafanya utafiti wa mazao yote, lakini tatizo kubwa hapatengwi pesa za kutosheleza ili hizi tafiti ziweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aweze kutuambia pendekezo hili la Kamati la kuanzishwa Mfuko Maalum wa Utafiti wa Kilimo amelichukuliaje ili kuwezesha upatikanaji wa fedha zaidi za utafiti. Kwa sababu Naliendele na taasisi zote za utafiti Tanzania zikiweza kutengewa pesa zitafanya kazi kubwa na nzuri ya kufanya utafiti wa mazao mbalimbali nchini ili wakulima wetu waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia pale Kilimanjaro Hai, tunayo TACRI ambao ni watafiti la zao la kahawa. Nikiwa pale kama Mkuu wa Wilaya nilichojifunza Serikali haitengi pesa ya kutosha kuipa taasisi hii ya utafiti ya TACRI. TACRI inategemea ufadhili wa European Union, ukiwa pale unakuta unapokea Mabalozi wa European Union wanakuja kuangalia uendelezaji wa TACRI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, hivi hawa European Union wakitoa mkono wakasema kwamba hawasaidii tena ile TACRI itaendelea? Kwa hiyo, ninachojaribu kuomba taasisi hizi za utafiti zitengewe pesa zisiwe zinatupwa au zinawekwa pembeni. Wizara inapokuja hapa kwenye bajeti ijayo iweze kuona namna ya kuwezesha taasisi zetu hizi za utafiti ili ziweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pale Kigoma tunao hawa TAFIRI na wanaendelea na utafiti wao wa kuonesha tuna idadi ngapi ya samaki kati ya wale 250. Hata hivyo, TAFIRI hawa wamekuwa wanafanya kazi Kigoma Mjini, tuombe basi Wizara ione namna ya kujenga hata chuo kimoja cha utafiti ndani ya Mkoa wa Kigoma hata kama ni branch ya utafiti kwenye zao la uvuvi ili vijana wetu waweze kujifunza zaidi masuala ya uvuvi, waachane na uvuvi haramu na wafanye uvuvi halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, niseme Miswada hii miwili wa Uvuvi na wa Kilimo ni mizuri na naunga mkono hoja. Ahsante sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Special Seats (CCM)

Questions (3)

Supplementary Questions (5)

Contributions (9)

Profile

Hon. Zainabu Nuhu Mwamwindi

Special Seats (CCM)

Questions (1)

Supplementary Questions (1)

Contributions (5)

Profile

Hon. Prosper Joseph Mbena

Morogoro Kusini (CCM)

Questions (3)

Supplementary Questions (3)

Contributions (8)

Profile

Hon. Omary Tebweta Mgumba

Morogoro Kusini Mashariki (CCM)

Questions (4)

Supplementary Questions (9)

Contributions (16)

Profile

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Mkuranga (CCM)

Questions (2)

Supplementary Questions (11)

Contributions (8)

Profile

View All MP's