Parliament of Tanzania

Bunge laahirishwa hadi Aprili 3, 2018

Mkutano wa Kumi wa Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeahirishwa hadi tarehe 3 Aprili, 2018.

Mkutano huu wa Kumi ulianza kwa kushuhudia Wabunge wapya watatu waliochaguliwa hivi karibuni wakila Kiapo cha Uaminifu. Wabunge hao ni;

· Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro – Songea Mjini.

· Mhe. Monko Justine Joseph – Singida Kaskazini.

· Mhe. Dkt. Stephano Lemomo Kiruswa – Longido.


Katika mkutano huu pia, Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson alimwapisha Mwanasheria Mkuu mpya wa Serikali (AG) Dkt. Adelardus Kilangi aliyechukua nafasi ya Mhe George Masaju ambaye aliteuliwa na Mhe. Rais kuwa Jaji Mahakama Kuu.


Aidha, katika Mkutano huu wa Kumi, wastani wa maswali 125 ya Kawaida na maswali 346 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali.


Kwa upande wa Miswada ya Serikali, Bunge pia lilipitisha kwa hatua zake zote Miswada Miwili ya Sheria ambayo ilisomwa Mara ya Kwanza katika Mkutano wa Tisa wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 91. Miswada hiyo ni :-

· Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 5) Bill, 2017].

· Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017 [The Public Service Social Security Fund Bill, 2017].


Mbali na hayo, wakati wa Mkutano huu, Kamati 16 za Kudumu za Bunge ziliwasilisha taarifa zake Bungeni, ambapo taarifa hizo zililenga kutoa ushauri, maoni na mapendekezo kwa serikali juu ya masuala mbalimbali.


Akitoa hotuba ya kuahirisha Bunge, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alisema Serikali imepokea hoja nyingi zilizoibuliwa na kamati na kwamba inaahidi kuzifanyia kazi hasa wakati huu wa maandalizi wa mpango wa bajeti wa mwaka 2018/19.

Katika mkutano huu, pia hoja binafsi kuhusu uzalishaji na ununuzi wa zao la Pamba iliwasiliswa na Mhe. Suleiman Masoud Nchambi, Mbunge wa Kishapu.

Akizungumzia hoja hiyo, Waziri Mkuu alimshukuru sana Mbunge huyo kwa hoja yake ambayo imeleta maboresho katika mtiririko mzima wa uboreshaji wa zao la Pamba.

Kwa upande wa mapitio ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha nusu mwaka 2017/18, Serikali iliwasilisha Bungeni taarifa kuhusu tathimini ya hali ya uchumi na utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia mwezi Julai hadi Disemba, 2017.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's