United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe.Atashasta Nditiye amewataka Askari wa wanyamapori kuwa na mahusiano mazuri na raia ili kuthibiti ujangili.
Mhe. Nditiye alitoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati Kamati yake ilipofanya ziara ya kikazi wizarani hapo.
Alisema raia lazima wawe na urafiki na askari badala ya kuwepo kwa uhasama baina yao kiasi cha baadhi ya askari wasio waaminifu kuwabambikizia kesi raia.
"Wizara hii inabidi iongeze nguvu kwa askari ambao siyo waaminifu,askari akiwa na uhusiano mzuri na raia itasaida kupunguza ujangili,raia wawe rafiki na askari,"alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema wizara imekuwa ikichukua hatua za kinidhamu kwa askari wanyamapori wasio na maadili.
Aidha, alisema kumekuwapo na taarifa za upotoshwaji kuhusiana na askari hao na kutaka zipuuzwe.
Katika ziara hiyo Kamati pia ilipata fursa ya kupokea na kuijadili taarifa ya utunzaji wa pembe za ndovu pamoja na kutembelea ghala la kuhifadhi pembe za Ndovu.
Wajumbe hao wanaendelea na Ziara yao ya siku moja Jijini Dar es Salaam.
Aidha kwa upande mwigine, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA) imesema kwa sasa matukio ya ujangili yamepungua ukilinganiisha na miaka iliyopita.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Faustine Masalu alisema kwa sasa kupigwa kwa tembo na wanyama wengine katika maeneo yanayohifadhiwa kumepungua.
Hata hivyo alisema hali hiyo haina maana kwamba ujangili umeisha na kwamba kwa sasa tatizo kubwa ni ng’ombe kuchungwa ndani ya maeneo ya hifadhi.
Akizungumzia aina za ujangili alisema upo ujangili wa kujikimu kwa ajili ya kitoweo na ujangiliwa biashara kwa ajili ya kipato na mali.
Aliwataja baadhi ya wanyama wanaofanyiwa ujangili kwamba ni tembo, simba na kakakuona na kwamba hatua mbalimbali zimekuwa zikichukiliwaza kuwakamata majangili na kuwachukulia hatua za kisheria.
Alisema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2016 Meno mazima 38 ya tembo na vipande 71 vyenye jumla ya kilo 434.33 yalikamatwa na watuhumiwa 40 walifunguliwa kesi.
“Watuhumiwa 1,563 walikamatwa kwa kujihusisha na ujangili wa nyara mbalimbali za Serikali ikiwemo ngozi 41 na mikia 56 ya wanyamapori aina mbalimbali,” alisema.
Akizungumzia changamoto ambazo TAWA inakabilana nazo alisema ni pamoja na uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi kuongezeka hususan katika Mapori ya Akiba.
“Matumizi ya silaha za kivita kufanyia ujangili,silaha nyingi na risasi zinakamatwa maeneo ya magharibi mikoa ya Rukwa, Katavi, Kagera na Kigoma, kupatikana kirahisi kwa bunduki za kivita kunatokana na hali ya usalama kudorora katika nchi jirani,” alisema.
Aidha, alisema kumekuwepo na vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili ambapo baadhi ya watumishi wa Sekta ya Wanyamapori wamekuwa wakitajwa kuhusika na vitendo vya rushwa na kushirikiana na majangili.
‘Sekta ya wanyamapori imedhamiria kuanzisha mfumo wa Jeshi Usu ili kudhibiti nidhamu ya watumishi na kuboresha ufanisi,”alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashista Nditiye aliushukuru uongozi wa TAWA na Mamlaka ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) kwa kuwasilisha mada nzuri iliyowajengea wajmumbe wa Kamati yake uelewa mpana.
“Kamati ipo pamoja na nyie hasa katika suala la migogoro mifugo kuingia eneo la hifadhi, ni vizuri na nyie mjue mipaka yenu inaishia wapi ili na sisi tujue jinsi ya kuwasaidia,” alisema.
Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo
Musoma Vijijini (CCM)