Parliament of Tanzania

Spika apokea ripoti za Kamati ya Almasi na Tanzanite na kuzikabidhi kwa Waziri Mkuu

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tazania Mhe Job Ndugai amepokea taarifa za Kamati maalum mbili alizounda wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge kwa ajili ya kuchunguza juu ya mfumo bora wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya Madini ya Almasi na Tanzanite hapa Nchini.

Aidha mara baada ya kupokea ripoti hizo wakati wa hafla iliyofanyika katika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma, Mhe Ndugai alizikabidhi ripoti hizo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa kwa ajili ya utekelezaji.

Ripoti ya uchunguzi wa Biashara ya Madini ya Alamsi iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Mussa Azzan Zungu wakati ripoti ya Kamati ya pili iliyochunguza uchimbaji wa Madini ya Tanzanite iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Dotto Biteko.

Akizungumza mara baada ya kupokea ripoti hizo Spika Ndugai alisema kuwa mapambano ya kuhakikisha kuwa raslimali za Watanzania zinakuwa mikononi mwao ni jambo la maana sana na hivyo; si vyema kumuachia Rais pekee yake.

Kutokana na hilo Mhe Ndugai alisema kuwa Bunge kama mhimili lazima lijipambanue katika kuhakikisha kuwa raslimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote.

“Hongereni sana kwa kazi nzuri mliyoifanya, wakati mwingine mlikaa mpaka usiku wa manane, mimi sina cha kuwalipa na wala Bunge hatuna cha kuwalipa bali mtalipwa na Mwenyezi Mungu kwa kazi yenu nzuri mlioifanya kwa Taifa letu”alisema.

“Wito wangu Watanzania wote tuwe pamoja katika mapambano haya, lazima tuungane sote dhidi ya hao wanaotuumiza,” alisema Mhe Ndugai.

Mhe Spika aliongeza kuwa baadhi ya matatizo yamekuwa yakijurudia ikiwemo Mikataba mibovu ya uchimbaji madini, utendaji mbovu wa Bodi na mifumo mibuvo ya kitaasisi zinazosimamia uchimbaji wa Madini

“Ni lazima sasa tubadilike kwa kuanza na upitiaji wa mikataba hiyo, upitiaji wa mifumo ya utendaji wa taasisi zinazosimamia uchimbaji madini na kuwa makini katika uundaji wa bodi mbalimbali,” Spika Ndugai alisisitiza.

Pia Mhe Ndugai, ameitaka Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo yote ya Kamati hizo na kusisitiza kuwa maoni yaliyowasilishwa ni maoni ya Bunge zima na kwamba wataendeleza ushirikiano na Serikaliili kuhakikisha wanawasidia Watanzania kufaidika na rasilimali za madini.

“Ni aibu sana kwa madini yanayopatikana nchini mwetu pekee kunufaisha watu wa mataifa mengine na kuwaacha Watanzania katika dimbwi la Umaskini” alisema.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa aliahidi kuikabidhi kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli mapema kesho asubuhi na kwamba Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote ya Kamati hizo haraka.

Awali akizungumza kabla kukabidhi ripoti kwa Mhe Spika Mwenyekiti Mhe Zungu alisema kuwa, katika utendaji wake Kamati imebaini madudu mengi ikiwa ni pamoja na mikataba mibovu wa uchimbaji madini,upotevu wa mapato, usimamizi mbovu wa uchimbaji wa madini hayo, tofauti za kitwakwimu za uuzaji wa madini hayo nje ya nchi na udanganyifu juu ya hali na gharama ya mitambo ya uchimbaji wa Madini ya Almasi.

Mhe Zungu amesema ripoti imependekeza kuwa Serikali iwahoji wajumbe wa bodi na wote wanaohusika na usimamizi wa uchimbaji wa madini ya Almasi na ikibainikina kuwa wamehusika na mapungufu yaliyoanishwa na ripoti basi wachukuliwe hatua.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati iliyoudwa kuchunguza biashara ya Madini ya Tanzanite Mhe Dotto Biteko alisema pia kumekuwa na usimamizi mbovu wa uchimbaji wa Madini hayo ya tanzanite, mikataba mibovu, vitendo vya rushwa na udanganyifu katika biashara hiyo.

Kutokana na hilo Mhe Biteko aliiomba Serikali kufanyia kazi mapendekezo ya Kamati ambayo yatasaidia katika kuboresha uchimbaji wa Tanzanite hapa nchini.

Hafla ya kupokea ripoti hizo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu wakuu wa Wizara, Wakuu wa Taasisi za Serikali, Viongozi wa Dini, Wabunge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Viongozi wastaafu na watumishi wengine wa Umma.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's