Parliament of Tanzania

Timu ya Bunge yarejea na medali 16 kutoka katika mashidano ya michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Timu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imerejea na medali kumi na sita (16) kutoka katika mashindano ya michezo ya Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Jijini Bujumbura nchini Burundi.


Akizungumza mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Jijini Dodoma na Bombardier 5H-TCE, Kiongozi wa Msafara wa Timu ya Bunge ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt Tulia Ackson alisema katika medali hizo 16 walizoshinda medali saba ni za Dhahabu, shaba tano na fedha nne.


Akitoa taarifa fupi kuhusiana na mashindano hayo mbele ya Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai ambaye aliwaongoza Viongozi na Watumishi wa Bunge katika kuipokea Timu hiyo ya Bunge, Naibu Spika alisema kuwa maandalizi yaliyofanyika kabla ya kwenda kwenye mashindano hayo yamewafanya wachezaji wacheze kwa hamasa sana na hatimaye kujinyakulia medali hizo.


Mhe. Tulia alifafanua kuwa katika medali saba za adhabu zimeletwa na Mhe. Yosepher Komba ambapo alishinda katika mbio za mita 1,500, 800 na 400.


“Mhe. Spika pia kupitia mbio za kupokezana vijiti tulipata medali ya dhahabu ambapo Mhe. Rose Tweve, Halima Mdee na Zudeda Sakuru walituwakilisha vizuri,” alisema Naibu Spika.


Naibu Spika aliongeza kuwa medali nyingine ya dhahabu alishinda yeye mwenyewe mara baada ya kushinda shindano la kutembea mwendo kasi.

“Medali nyingine ya dhahabu imepatikana kutoka kwa Wabunge Wanaume wavutaji kamba na kusaidia kufikisha idadi ya medali za dhahabu kuwa saba,” alisema Mhe. Tulia.


Medali tano za shaba na nne za fedha zimepatikana kupitia michezo mingine iliyobaki ikiwemo mpira wa miguu wanaume, wavu, mpira wa mikono na riadha kwa Wanawake na Wanaume.


Kwa upande wake Mlezi wa Timu ya Bunge Mhe. Salma Kikwete alisema wanamshukuru Mungu kwamba walipokelewa vizuri walipofika nchini Burundi na wachezaji walicheza vizuri kwenye kila nyanja.


Aidha, Mwenyekiti wa Timu ya Bunge, Mhe. Willian Ngeleja amesema wameshiriki katika kila michezo isipokuwa mchezo wa gofu na wanaamini kwamba mwaka kesho Mhe Spika atasaidia wawe katika mazingira ambayo yatawasaidia kushiriki katika kila mchezo.


“Michezo hii hatushiriki kama burudani tu lakini ni mojawapo ya vigezo vya kuimarisha ushirikiano pamoja na utengamano wa wanajamii katika nchi hizi sita zinazounda jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Mhe. Ngeleja.


Kwa upande wake Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai aliwakaribisha Wanamichezo hao Wabunge na kuahidi kuandaa siku maalum ya kuzungumza nao.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's