| E-mail this to a friend | Printable version |
|
||||||
| Session No | Question Number | To the Ministry of | Sector | Date Asked | ||
|---|---|---|---|---|---|---|
| 9 | 103 | HEALTH AND SOCIAL WELFARE | Health | 8 November 2012 | ||
| Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na pia naomba nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Serikali yetu kwa maboresho ambayo yamefanyika kwa kiwango cha juu na jitihada mbalimbali ambazo bado zinaendelea kutolewa. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza, naomba niulize kama ifuatavyo:- Kwanza, maboresho ya maslahi ya wafanyakazi ni pamoja na vitendea kazi, sasa hivi katika hospitali yetu ya Muhimbili mashine ya CT Scan ni mbovu kwa kipindi kirefu na mtu kabla hajaanza kupata matibabu inabidi apate vipimo vya CT Scan. Kwa sasa hivi wagonjwa wengi wanaambiwa waende Regency au waende Aga Khan ambako pesa zake ni nyingi na wengi wanashindwa. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kununua CT Scan machine nyingine ya pili wakati tunangojea hiyo ya kwanza itengenezwe? Pili, malipo ya kipimo cha CT Scan kwenye hizo hospitali inakuwa ni kama 250,000/= wakati Muhimbili ni 170,000/= au 180,000/= hivi. Kwa hivyo, kuna tofauti ya kama 70,000/=. Kwa sababu hao wagonjwa wengi hawana uwezo na bado wanangojea mashine itengenezwe au hii CT Scan nyingine inunuliwe, kwa hiyo, wanashindwa na wengi wataweza kufa na ugonjwa kabla hawajapata matibabu. Je, Serikali inaweza kuchangia hizo 70,000/= ambazo wale ambao hawajiwezi kabisa waweze kuongezewa ili wakapate vipimo kutoka hizo hospitali za nje? |
||||||
| ANSWERS TO SUPPLEMENTARY QUESTION # 103 SESSION # 9 | ||||||
|
||||||
| WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kipimo cha CT Scan Muhimbili kimeharibika tena, kilitengenezwa, kikafanya kazi kwa muda mfupi, baadaye kimeharibika kwa mara nyingine tena. Lakini Wizara imechukua uamuzi wa makusudi kwamba tulete mashine mpya na utaratibu umeanza, tumeutaka Mfuko wetu wa Bima ya Afya kutoa fedha hizo ili tuweze kupata mashine mpya ya CT Scan pale Muhimbili. Lakini pamoja na kuleta mashine hiyo, tutaangalia upya gharama za kipimo hicho kwa nia ya kufanya wananchi waweze kuzimudu kuliko ilivyo kwa hospitali za binafsi. Kwa hiyo, hilo liko mbioni, tunalipa umuhimu na ustahili ili kipimo hicho kiweze kupatikana haraka iwezekanavyo. Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la kutoa fedha kwa ajili ya kuwasaidia watu kufanya nje ya Muhimbili kwa sasa, utekelezaji wa jambo hilo utakuwa mgumu sana kwa sababu, kwanza hatuna uhakika wa idadi ya watu wanaohitaji hicho kipimo. Lakini pili kutoa fedha hizo kwa kweli kwa sasa ziko nje ya bajeti, kwa hiyo, haitakuwa rahisi. Cha msingi ni jitihada zetu za kufanya haraka ili tuweze kuleta CT Scan ya Serikali itakayotoa huduma kwa gharama nafuu kuliko hospitali za binafsi. |
||||||