You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Supplementary Question

mp Kitandula, Dunstan Luka[CCM]

Mkinga Constituency
Session No Question Number To the Ministry of Sector Date Asked
8 13 WATER Water 13 June 2012
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Kutokana na tatizo kubwa la maji katika Wilaya ya Muheza, Serikali ilipeleka fedha ili tuweze kuchimbiwa visima, lakini kwa bahati mbaya sana wataalam wetu waliruhusu kisima kichimbwe katika eneo lililokuwa halikufanyiwa utafiti na matokeo yake Taifa likaingia hasara kubwa.

(i) Je, Serikali inatoa kauli gani kwa Wananchi wa Muheza juu ya wataalam
waliosababisha Taifa kuingia hasara?

(ii) Katika utaratibu wa vijiji kumi kupatiwa maji kwa Mradi wa World Bank, Wilaya ya
Mkinga imekidhi vigezo vyote lakini mpaka leo tunapozungumza ni kijiji kimoja tu kimefanikiwa kupatiwa fedha pamoja na kwamba tuna tatizo kubwa sana la maji. Serikali inawaambia nini
wananchi wa Wilaya ya Mkinga?
ANSWERS TO SUPPLEMENTARY QUESTION #  13  SESSION #  8
mp Answer From Hon.Mahenge, Dr. Binilith Satano
WATER
NAIBU WAZIRI WA MAJI:

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Kuhusu tatizo la Wataalam wa Halmashauri ya Muheza kuchimba visima ambavyo havikuwa kwenye utafiti, tumefuatilia tukagundua kwamba ni kweli katika vijiji tisa vilivyokuwa earmarked kuchimbiwa visima, viliweza kupatikana visima katika vijiji vitano. Moja ya vijiji hivyo ni Kijiji kinachoitwa Kilongo, ambacho mkandarasi aliyekwenda kuchimba kile kisima aliacha sehemu tatu ambazo zilioneshwa na wataalam kwa ajili ya uchimbaji akaenda kuchimba eneo lingine. Tumeongea na Mkurugenzi wamemwita mkandarasi na kukaa naye ili aoneshe michoro inayomthibitishia kuchimba eneo lile.

Ninachoweza kuagiza hapa ni kwamba, hii inaonesha dhahiri jinsi wataalam wetu, ukichukua mkandarasi halafu na yule mtaalam anayesimamia Halmashauri, kwanza kwa mkandarasi kuonesha kutofahamu umuhimu wa tafiti zinazofanywa kwa sababu siyo kila mahali panapochimbwa panaweza kuwa na maji kwa sababu ya kihaidrolojia. Kwa hiyo, alitakiwa
kufuata zile sehemu ambazo yule mkandarasi aliyefanya utafiti naye afanye kwenye sehemu tatu
mpaka nne.

La pili, inaonesha utovu wa nidhamu wa Msimamizi wa Halmashauri ambaye aliacha kisima kikachimbwa mpaka dakika za mwisho sehemu ambayo haipo kwenye mchoro. Nninachoagiza Halmashauri ya Muheza iweze kukaa na mkandarasi huyo na kama itathibitika kwamba ni kweli hakutumia michoro inayohusika kwenye sehemu husika, basi anawajibika kuchimba kisima kwenye Kijiji cha Kilongo kwenye maeneo yaliyokuwa yameainishwa na mtaalam.

Kuhusu Msimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Halmashauri inatakiwa imwajibishe kwa kufuata taratibu za kinidhamu kwa sababu alitakiwa asimamie na amwoneshe lile eneo kabla fedha za umma hazijatumika kiwango cha kumaliza halafu baadaye akalipwa wakati anafahamu kuwa hakufanya sehemu hiyo.

Mwisho, niwaombe Wataalam wote wa Halmashauri kusimamia kwa ukaribu Miradi hii ya uchimbaji wa visima vya maji na Miradi mingine kwa sababu tatizo kubwa la Miradi hii imeonekana ni usimamizi ambao ni mbovu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sehemu ya pili ya swali, Vijiji Kumi vya Wilaya ya Mkinga kwa Mheshimiwa Kitandula, tunayo orodha ambayo inaonesha kwamba, kufikia tarehe 30 Mei, Halmashauri 60 ambazo zimeshakidhi vigezo vya Benki Kuu ya Dunia vimeshaidhinishwa kuanza ujenzi wa miundombinu ya maji. Kwa hiyo, ninachomwomba Mheshimiwa Kitandula, tuangalie kwenye orodha kama Mkinga ipo basi ni suala la kufuatilia, Mkurugenzi asaini mikataba na Wahandisi ili utaratibu wa ujenzi uweze kuanza. Ahsante.