United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wakulima wa Tanzania wanaelekea sasa kwenye msimu mwingine wa kilimo ikiwa mazao yao bado wanayo manyumbani hawajauza. Tuliona wakulima wa nyanya, mbaazi, mahindi na mazao mengine, na Serikali ilitoa kauli katika Bunge hili kwamba wanatafuta masoko nje ya nchi nilijibiwa na Naibu Waziri wa Kilimo. Naomba nifahamu mchakato huo umefikia hatua gani maana wakulima mpaka sasa wana mazao yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, majibu ya Waziri ni kwamba, wanaanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao ili mazao haya yapate soko na mtawezesha sekta binafsi na Serikali haitoi moja kwa moja fedha kwa ajili ya viwanda hivyo watu binafsi waanzishe. Wakulima wa Tanzania wasubiri kwa muda gani mpaka hivyo viwanda vianzishwe ili mazao yao yapate soko?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nianze na hili ambalo ni rahisi. Wananchi wasubiri kwa muda gani kuanzisha hivyo viwanda?
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunajenga viwanda. Lengo la kujenga viwanda ni kuongeza thamani na kupunguza uharibifu wa mazao (post-harvest loss). Jambo la kufanya Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote na Watanzania nendeni SIDO, na nimekuwa nikilisema, kusudi waweze kutambua na Naibu Waziri wa Ajira alizungumza hapa, kuna kitu kinaitwa ODOP (One District One Product) inalenga kuangalia katika eneo lenu tatizo ni nini, fursa ni ipi.
Mheshimiwa Spika, sasa watakuongoza wale na watakuvuta mpaka uje ufikie kwangu tuweze kupatia suluhisho lakini mimi nina imani na Watanzania wakielekezwa, wakiongozwa wanauwezo wa kuwekeza. Kwa hiyo suluhisho ni tutaanza lini, tumeshaanza sasa hivi tunajenga viwanda. (Makofi)
Tatizo lake Mheshimiwa Mbunge nenda kamuone Meneja wa SIDO kama ukiwa na wepesi njoo unione mimi nitaweza kukupatia suluhisho.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; tatizo la nyanya na tatizo la mbaazi. Tanzania kama Taifa tumepata tatizo kubwa la bei ya mbaazi na ndiyo maana wananchi unao wazungumzia wameweka mbaazi zao. Mwaka jana kilo ya mbaazi ilikwenda mpaka shilingi 2,000 lakini bei ya soko la mbaazi imeshuka mpaka shilingi 500 tatizo tunalijua.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, tunawasiliana na Serikali ya India ili tuwe na makubaliano ya moja kwa moja kuuza mazao hayo ya mbaazi kwa kushirikiana na Serikali ya India. Tanzania tulikuwa tunauza tani laki moja ya mbaazi, Mheshimiwa Mo ametupa order ya tani milioni mbili nina uhakika tutafanikiwa kuwapa majibu Watanzania.