Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Frank George Mwakajoka

Supplementary Questions
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua barabara ya Tunduma - Mpemba yenye kilometa 12 itajengwa lini na Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu barabara ile inasababisha msongamano mkubwa sana wa magari kwenye Mji wa Tunduma na wananchi kushindwa kutimiza majukumu yao. Kwa hiyo, nataka Waziri atueleze ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwenye Mji wetu wa Tunduma haraka iwezekanavyo? Ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa sababu matatizo ya maji katika jimbo langu yanafanana sana na Jimbo la Kigoma Kaskazini, ninapenda nimuulize Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali hii itakamilisha Mradi wa maji katika Mji wa Tunduma kwa sababu imekuwa inaahidi mara nyingi kwamba itatengeneza maji na hata wakati Mheshimiwa Rais anaomba kura kwa wananchi pia alisema kwamba ataweza kuwaletea maji haraka iwezekanavyo ndani ya mwaka mmoja mradi utaanza kutekelezwa. Leo hii kuna kampuni ambayo tayari imekubali kujenga…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, swali si umeshauliza? Nadhani swali umeshauliza, kwamba huo mradi utakamilika lini?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nikumbushe kidogo kwa sababu kuna kampuni leo imekuja hapa na mradi ule umeshapitishwa na Wizara lakini tunashangaa Wizara ya Fedha hawataki kukubali mradi ule uanze kujengwa haraka. Kwa sababu mradi ule ulitakiwa uanze kujengwa mwanzoni mwa mwaka huu lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea. Tunataka kupata majibu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Barabara hii ahadi yake ilikuwa ni kujengwa kwenye bajeti ya mwaka 2009/2010 na daraja lile ilikuwa ni 2009/2010, lakini mpaka leo daraja lile halijajengwa. Je, majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri yataleta matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Momba hasa eneo la bondeni kwamba itaanza kujengwa mapema mwaka 2016/2017?
Swali la pili, Momba ni Wilaya mpya ambayo inaunganisha Mji wa Tunduma na kutoka Tunduma kuelekea Makao Makuu ya Momba, eneo la Chitete ni Kilometa 120. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na kutujengea daraja katika Mto Ikana katika Kijiji cha Chitete, Kata ya Msangano ili wananchi wa Tunduma waweze kufika kule wakiwa wanatumia barabara ile ambayo itakuwa na kilomita 68?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduma ni lango kuu la nchi za Kusini na Kati mwa Afrika na kwa sababu Mheshimiwa Waziri amenihakikishia kwamba mradi mkubwa wa maji utajengwa kwenye Mji wa Tunduma lakini kuna mradi ambao ulijengwa mwaka 1973, mradi wa maji wa kutega kwenye Kijiji cha Ukwire ambapo ulikuwa unahudumia Kata za Mpemba, Katete na Chapwa na sasa hivi mradi ule hautoi maji ya kutosha. Ni lini Serikali itakwenda kukamilisha mradi ule wa Mpemba ambao unalisha kata tatu katika Mji wa Tunduma?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanavyokwenda katika nchi ya Zambia hasa katika Jimbo la Copperbelt wamekuwa wanakamatwa wakiwa stand na wanapelekwa gerezani bila kupelekwa Mahakamani. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na jambo hili kwa sababu kuna vijana wengi sana ambao wako magereza na hawajapelekwa Mahakamani mpaka sasa hivi? Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wangu wa Mji wa Tunduma. Swali la kwanza; Mji wa Tunduma ni mji uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia na ni lango kuu la nchi za Kusini na Kati mwa Afrika. Kwa tafsiri hiyo ni kwamba wageni wote kabla hawajingia katika nchi ya Tanzania ni lazima wapitie Tunduma kutoka katika nchi hizo.
Je, Serikali ina mpango gani wa makusudi na wa haraka wa kupima ardhi katika Mji wa Tunduma ili kuondoa ujenzi holela unaoendelea kwa hivi sasa? (Makofi)
Swali la pili; nini mwongozo wa Wizara ya Ardhi ikishirikiana na TAMISEMI kupitia Halmashauri zetu kwenye Idara ya Ardhi ili kutoa fursa kwa Halmashauri kukopa fedha katika taasisi za fedha, lakini pia kukubali makampuni binafsi ambayo yanaweza yakapima ardhi mfano UTT katika maeneo yetu ili kuhakikisha kwamba tunapunguza ujenzi holela katika maeneo yetu ya Mji wa Tunduma na maeneo yote nchini? (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Tatizo la ardhi kwenye Wilaya ya Mbozi linafanana sana na tatizo lililopo kwenye Mji wetu wa Tunduma. Katika Mji wa Tunduma katika Kata ya Mpemba kuna ardhi karibu ekari 500 ambazo zinamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa na mpaka sasa hivi eneo lile halijaendelezwa zaidi ya miaka minane. Je, Serikali inasema nini ili kuikabidhi halmashauri, ambayo haina hata eneo la kujenga makao makuu ili iweze kutumia ardhi ile?
MHE. FRANK MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio mimi, naitwa Frank George Mwakajoka. Nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa kipindi hiki cha miaka miwili kumekuwa na tatizo kubwa sana la malalamiko ya wafanyabiashara katika nchi hii na wafanyabiashara wengi sana wamekuwa wakifunga biashara zao, wafanyabiashara wa maduka pamoja wafanyabiashara wa hoteli, lakini pia wawekezaji wa kutoka nje, wamekuwa wakifunga shughuli zao na kuondoka. Je, Serikali ina mpango gani wa kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanaendelea kuwekeza katika nchi yetu?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya wananchi wa Mji wa Tunduma, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi wa Mji wa Tunduma wamekubali ushauri wa viongozi wao na kuondoa nyumba katika maeneo mbalimbali na kuhakisha kwamba barabara 42 zimepatikana kwenye Mji wa Tunduma, Serikali ina mpango gani wa kuwaunga mkono ili kuhakikisha kwamba barabara zile zinakuwa kwa kiwango cha lami kwenye Mji wa Tunduma, ukizingatia mji unaendelea kukua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa sana katika Halmashauri mbalimbali nchini baada ya kauli ya Mheshimiwa Rais katika sherehe za Mei Mosi juzi kule Kilimanjaro alivyosema kwamba Halmashauri yoyote au Baraza lolote la Madiwani litakalojitokeza na kutaka kumuondoa Mkurugenzi kazini au kumfukuza, Baraza hilo litavunjwa mara moja na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kumteua Mkurugenzi kwa hiyo atahakikisha anaifuta Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa mujibu wa Sheria
za Serikali za Mitaa, Waheshimiwa Madiwani ndiyo wasimamizi wa shughuli na miradi ya maendeleo na mapato na matumizi ya fedha za Halmashauri.
Je, Mkurugenzi akiwa ametumia fedha vibaya na akatumia madaraka yake vibaya, ni utaratibu gani ambao Waheshimiwa Madiwani watautumia kama siyo kumuondoa Mkurugenzi wakati Rais tayari ameshawaonya na amewaambia kwamba ataivunja Halmashauri hiyo? Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Sera ya nchi na ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kila kijiji na kila kitongoji kuna kuwa na zahanati, na katika mji wa Tunduma katika mtaa wa Makambini eneo la Sogea wananchi wameamua kujenga zahanati katika eneo ambalo lilikuwa limetengwa na Serikali, lakini kutokana na mgogoro uliokuwepo na ambao alikuja kuumaliza Naibu Waziri wa Ardhi, alitoa maelezo kwamba eneo hilo lisianze kujengwa mpaka atakavyotoa ruhusa ya wananchi kuendelea kujenga Zahanati pale. Je, ni lini atatoa ruhusa ili wananchi wa mji wa Tunduma eneo la Makambini waweze kuendelea na ujenzi wa zahanati kama ambavyo sera za nchi zinasema?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Serikali imekuwa ikidaiwa fedha nyingi sana na mifuko ya hifadhi, mfano, PSPF ilikuwa inaidai Serikali zaidi ya shilingi 2,671,000,000,000 pia LAPF ilikuwa inaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 47 kwa ajili ya asilimia 15 ya makato kwa ajili ya wafanyakazi. Je, Serikali imelipa kiasi gani na hali ikoje kwa wastaafu hawa mpaka sasa?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini zipo taarifa ambazo si rasmi sana kwamba zabuni ile ya kumpata mkandarasi wa kujenga daraja la Mto Momba zilisitishwa hivi karibuni na kuleta wasiwasi mkubwa sana kwa wananchi wa mikoa ya Songwe, Katavi na Rukwa kwamba daraja lao inawezekana lisijengwe. Leo Waziri anawathibitishia nini wananchi wa mikoa hiyo kwamba daraja hilo litaanza kujengwa lini?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Momba ina kanda mbili, kuna ukanda wa juu na kuna ukanda wa chini na katika Ukanda wa Chini kuna Kata za Msangano, Chitete, Chilulumo, Mkulwe, Kamsamba pamoja na Ivuna. Ukanda wa Juu kuna Kata za Kapele, Miunga Nzoka, Ikana pamoja na Ndalambo na Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Barabara za kuingia katika Makao Makuu ya Wilaya mpya hazipitiki kabisa. Ni lini Serikali itahakikisha kwamba inatenga fedha za kujenga barabara ya kutoka Ikana mpaka Chitete na Tunduma kuelekea Chitete?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kumekuwa na tafsiri ambayo siyo sahihi sana kwa vijana ambao wananunua Kwacha kwenye mpaka wa Tunduma na Zambia ambapo fedha hizo, Wazambia wanapokuwa wamekuja kununua bidhaa kwenye Mji wa Tunduma wanakuja na Kwacha na baadaye vijana wananunua zile Kwacha na Serikali imekuwa ikisema kwamba vijana wale hawalipi kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kununua zile Kwacha, wanakwenda Lusaka kununua dola na baada ya kununua zile dola wanakuja ku-change kwenye benki zetu za Tanzania. Hawa wafanyabiashara wa Kwacha wanakuwa tayari wamelipa kodi.
Je, Serikali haioni kwamba nao pia ni walipa kodi katika Taifa hili na badala yake wanaendelea kuwasumbua? Wataacha lini? Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali. Dhamira ya Serikali ya kuanzisha Benki ya Kilimo ilikuwa ni kuwainua wakulima nchini. Wakati Serikali inafikiria kuanzisha Benki ya Kilimo ilikubali kutoa mtaji wa shilingi bilioni 800, lakini fedha iliyotolewa ni shilingi bilioni 60 tu na benki hii imeshindwa kabisa kuwahudumia wakulima wa nchi hii.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mikopo na wanalima kilimo chenye tija? (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Tunduma ni mji unaokuwa sana na una msongamano mkubwa sana wa watoto; na mwaka wa jana Waheshimiwa Madiwani kwa kushirikiana na wananchi waliweza kuanzisha shule mpya nane ambazo zingine zina madarasa matatu, zingine zina madarasa nane lakini shule hizi mpaka sasa hivi hazijaanza kutumika kwa sababu DC amewasimamisha Madiwani. Kwa, hiyo kuna baadhi ya shughuli ambazo zilitakiwa zifanyike kama vioo na mambo mengine hayajafanyika kwa sababu wananchi pia walikuwa wanategemea Madiwani. Je, ni lini Serikali itatia mkazo kuhakikisha kwamba Madiwani wanarudi kazini ili shule hizi zianze kutumika haraka iwezekanavyo? Ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka tumeanzisha Wakala wa Barabara (TARURA) katika Mkoa wa Songwe na Wilaya ya Momba hakuna barabara yoyote ambayo inajengwa sasa hivi kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018, je, kazi hii ya TARURA itaanza kutekelezwa lini na hasa barabara ya kutoka Kakozi - Ndalambo kuelekea Kapele? Barabara ni mbaya sana na sasa haipitiki. Ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo ya usalama katika eneo la Bunda yanafanana sana na Jimbo langu la Mji wa Tunduma.
Mwaka 2016 katika swali langu la msingi, niliuliza kuhusiana na ujenzi wa kituo chenye hadhi ya Wilaya, lakini pia niliuliza kuhusiana na nyumba zenye gharama nafuu kwa ajili ya polisi wetu kwenye Mji wa Tunduma. Majibu yake ni kwamba walisema katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 nyumba hizi zingeweza kujengwa pamoja na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na changamoto hizi katika mji wetu wa Tunduma? (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli mbiu ya Serikali sasa ni viwanda, lakini viwanda havitakuwepo katika nchi hii kama hatutoweza kuzalisha mafundi mchundo wengi ili waweze kutekeleza majukumu mbalimbali ndani ya viwanda hivyo. Je, Serikali haioni kwamba inapoteza muda wa kutamka kwamba itakuwa ni Serikali ya viwanda wakati haitaki kuzalisha mafundi mchundo wengi ili waweze kutekeleza wajibu wao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika hali halisi
ya majibu ya Mheshimiwa Waziri jana wakati anajibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge alisema kwamba Serikali imejipanga kujenga Vyuo vya VETA nchi nzima na maeneo mbalimbali katika Taifa hili. Leo katika majibu yake anatuambia kwamba Serikali haina mpango wa kujenga Chuo cha VETA katika Mji wa Tunduma. Je, jana alikuwa akiwadanganya Wabunge katika majibu yake ya msingi aliyokuwa akiyatoa ndani ya Bunge hili? (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Mji wa Tunduma uko mpakani mwa Zambia na Tanzania na ni Mji ambao unahudumia Mataifa zaidi ya Nane yanaotumia Mpaka wa Tunduma, lakini kumekuwa na tatizo kubwa sana la umeme kukatika mara kwa mara na kusababisha usalama wa wageni pamoja na Wakazi wa Mji wa Tunduma kuwa hatarini. Je, ni lini Serikali itaweka umeme wa uhakika, kama ambavyo wenzetu wa Zambia pale ng’ambo walivyoweka umeme wa uhakika? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Tunduma na Wilaya yetu ya Momba kulikuwa na majengo ambayo yalikuwa yanatumika na Kampuni ya CC iliyokuwa inajenga barabara ya kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga. Majengo hayo yaliteuliwa kwamba yangeweza kutumika kama Hospitali ya Wilaya, lakini sasa hivi inaonesha kuna mabadiliko. Waziri anawaambia nini wananchi wa Mji wa Tunduma kuhusiana na majengo yale kwa sababu aliwahakikishia kwamba itakuwa Hospitali ya Wilaya?
MHE. FRANK. G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mji wa Tunduma una shida kubwa sana ya maji na mwaka jana katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ilikuwa imetengwa fedha Euro milioni 100 ambayo ilitaka kutekelezwa na Kampuni ya Aspac International kutoka Ubelgiji, lakini katika bajeti hii fedha hiyo haijatengwa na mradi huo hauonekani kabisa. Nataka nijue mradi wa kupunguza tatizo la maji katika Mji wa Tunduma utatekelezwa siku gani na kwa nini umeondolewa hauonekani katika bajeti ya mwaka 2017/2018?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kabla sijauliza swali la nyongeza ningependa nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali ya Zambia kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya ya kuhakikisha kwamba wanatuazima gari yao ya Zimamoto kwa ajili ya kuzima moto kwenye mji wa Tunduma, ninasema mwasalifya sana mwe wantu wa Kuzambia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; najua kabisa kwamba Tunduma iko mpakani mwa Zambia na Tanzania na shehena kubwa sana ya mizigo inayoshuka kwenye bandari ya Dar es Salaam inapita Tunduma na Tunduma hatuna gari ya Zimamoto. Je, Serikali haioni kwamba inahatarisha maisha ya wana Tunduma lakini pia na mizigo inayopita kwenye mpaka wa Tunduma?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa Tunduma wanaendelea kutoa ada za zimamoto wakati huduma ya zimamoto kwenye Mji wa Tunduma haipo, hatuoni kama huu ni uzulumaji wa wazi kabisa wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa wananchi wa Tunduma kuendelea kutozwa fedha hizi bila kupata huduma ambayo ni muhimu katika maisha yao? (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Bunge lililopita niliuliza swali kuhusiana na hospitali ya wilaya ambayo tulikuwa tumeambiwa kwamba itajengwa katika Kata ya Chipaka kwenye Kijiji cha Chipaka. Sasa hivi inaonesha kwamba kuna mabadiliko ambayo yanataka kufanyika hospitali ile ikajengwe maeneo mengine ambayo hayana majengo kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo tulilokuwa tumeliteua ni eneo ambalo lilikuwa na majengo ambayo yalikuwa yanatumika kwa ajili ya mradi wa kujenga barabara kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga, kuna majengo zaidi ya 20, leo hii wanataka kupeleka maeneo ambayo hayana majengo kabisa. Mheshimiwa Waziri aliniambia hapa atahakikisha kwamba analifuatilia jambo hili na hospitali inajengwa eneo ambalo walikuwa wametuambia kwamba ni lazima itajengwa pale. Je, amefuatilia na anatoa majibu gani kwa wananchi wa Tunduma ili wawe na uhakika wa hospitali katika eneo la Chipaka na Kata ya Chipaka? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa kigezo cha kutoa asilimia 0.3 kwenye Halmashauri ambazo kuna kazi za uchimbaji unaofanywa na migodi inatokana na athari ambazo wananchi wa maeneo hayo wanapata. Katika Mji wa Tunduma kuna forodha ambayo inahudumia nchi karibu nane Kusini na Kati mwa Afrika na kumekuwa na madhara mengi sana kwenye mpaka wa Tunduma ambayo yanafanana kabisa na maeneo wanayochimba migodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kuna magonjwa ya UKIMWI lakini kuna miongamano mkubwa sana wa magari na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wangu ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo vizuri.
Je, Serikali haioni kwamba sasa ni muda muafaka kuona na sisi kama Halmashauri ya Tunduma tunaweza kupata asilimia 0.3 ya ruzuku kama ambavyo wanapata katika maeneo ambayo wanachimba migodi? Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya TAZARA ni reli ambayo ingeweza kusaidia sana kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam na kupeleka nchi za Congo, Zambia na Zimbabwe na kuepusha uharibufu mkubwa wa barabara ambao umekuwa ukitokea kutoka Dar es Salaam kwenda Tunduma. Tumeshangaa kwamba mizigo mingi wanatumia malori kusafirisha badala ya reli ya TAZARA. Je, kuna changamoto gani ambazo Serikali imezigundua kutokana na wafanyabiashara wengi kutokutumia reli hiyo?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko mradi ambao unataka kutekelezwa kwenye Mji wa Tunduma na SADC na Mheshimiwa Waziri katika Bunge lililopita alisema kwamba ameshampeleka consultant pale. Wananchi wa Tunduma wanataka kujua mpaka sasa mradi umefikia kiwango gani katika maandalizi ya utekelezaji?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kuna mpango wa kujenga mradi mkubwa wa maji ambao unatakiwa kutekelezwa na SADC katika Mji wa Tunduma pamoja na Mji wa Nakonde upande wa Zambia. Ni nini mkakati na Serikali imefikia wapi katika kujenga mradi huu mpaka sasa?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa sana katika Deni hili la Taifa, Wabunge wamekuwa wakihoji sana kwamba deni limekuwa kubwa na wanahoji pia kwamba Serikali imekuwa ikikopa fedha na kulipia kwenye madeni ambayo tumekopa katika maeneo mengine. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuleta sheria ndani ya Bunge ili fedha yoyote inayokopwa na Serikali itakiwe kuidhinishwa ndani ya Bunge kwamba sasa Serikali ikope? Siyo Serikali inakopa tu halafu baadaye kunakuwa na hoja ambazo zinaleta mkanganyiko ndani Bunge hili na kwa Watanzania pia wanashindwa kujua fedha hizi zimefanya kazi gani. Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yanayotoa faraja kwa wananchi wa Tunduma pamoja na Ileje, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wananchi wa Kata ya Bupigu, Kata ya Malangali, Kata ya Isoko na Kata ya Ikinga katika Wilaya ya Ileje wamekuwa na adha kubwa sana ya kuamka Saa nane ya usiku na kusubiri usafiri kuja makao makuu ya Mkoa wa Songwe. Ni lini Serikali itajenga barabara hii ya kutoka Isongole mpaka Ikinga, ili kuondoa adha hii ya Wananchi wa Ileje?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna kipande cha barabara kilometa 1.6 kimejengwa katika Mji wa Tunduma na kimejengwa kwa sababu, wananchi wa Mji wa Tunduma wakati Mheshimiwa Rais akiwa Waziri wa Ujenzi, wakati anapita anakwenda Rukwa, walimsimamisha pale na wakamwomba barabara ile ijengwe haraka iwezekanavyo na sasa Serikali imejenga kipande kile cha kilometa 1.6, lakini kipande kile kimejengwa chini ya kiwango. Je, ni lini Serikali itakuja kuhakiki kipande kile cha barabara ili wananchi wa Tunduma waweze kufurahia mpango wa ujenzi wa barabara kwenye Mji wa Tunduma?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijana wengi sana pale Tunduma wamejiajiri kwa ajili ya kufanya escort ya magari yaliyobeba copper kutoka Congo na wamefanya kazi kwa muda mrefu lakini mpaka sasa hivi hawajapata mikataba kutoka kwenye kampuni hizo. Serikali inasema nini kuhusiana na vijana hao kwa sababu imeonesha kwamba kampuni hizo zinavunja sheria; kwa sababu wamefanya miaka mitatu wengine mpaka miaka nne lakini mpaka leo hawana mikataba kabisa? Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mji wa Tunduma ni wa kibiashara na kuna mpaka ambao unatumiwa na nchi karibu nane za Kusini na Kati mwa Afrika. Kumekuwa na msongamano mkubwa sana wa malori yanayovuka mpaka ule na kusababisha wananchi wa Tunduma kuchelewa kufanya shughuli zao kwa sababu ya msongamano ule. Kuna barabara ya kilometa 12 kutoka eneo la Mpemba kuja Tunduma Transfoma ambapo viongozi wengi wameahidi kuijenga kwa kiwango cha lami ili kupunguza msongamano kwa magari yanayotoka Sumbawanga kwenda Mbeya na yanayotoka Mbeya kwenda Sumbawanga lakini pia kuwarahisishia usafiri wananchi wa Mji wa Tunduma. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kama ahadi za viongozi zilivyotolewa? (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Tunduma uko mpakani mwa Zambia na Tanzania na ni mji ambao unapokea wageni wengi wanaotoka nchi za Kusini mwa Afrika lakini huduma ya umeme kwenye Mji wa Tunduma ni haba sana na umeme unakatikakatika mara kwa mara na kusababisha usalama wa wageni na wananchi wa Tunduma kuwa hatarini. Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba inaweka umeme wa uhakika katika Mji wa Tunduma?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa nataka nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Wanatumia kigezo gani katika kupanga ushuru wa dagaa hasa dagaa zinazotokea bahari ya Hindi? Wafanyabiashara walikuwa wanalipwa kwa gunia la kilo 100 shilingi 10,000/=, lakini sasa hivi kilo moja wanalipisha dola moja. Kwa hiyo, gunia hilo sasa hivi limefika mpaka shilingi 250,000/=. Wafanyabiashara wameshindwa kufanya biashara hiyo. Serikali inasema nini kuhusiana na jambo hilo kwa sababu linaathiri biashara katika mpaka wa Tunduma? Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la MKUKUTA na Ilani ya Chama cha Mapinduzi sekta ya kilimo ilikuwa ikue kwa asilimia 8 ndani ya miaka 10 lakini uhalisia kuanzia mwaka 2011 na 2015 sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 3.4. Ndani ya miaka ya Awamu ya Tano katika miaka yake mitatu ya bajeti sekta ya kilimo imekua kwa wastani wa asilimia 1.9. Uhalisia unajionesha kwenye bajeti zake, bajeti ya mwaka 2016/ 2017…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 tulitenga shilingi bilioni 101 katika sekta ya kilimo lakini fedha iliyotoka ilikuwa ni shilingi bilioni 3 peke yake. Pia mwaka 2017/2018 tulitenga shilingi bilioni 150 ikatoka shilingi bilioni 24. Swali, hii ndiyo tafsiri ya Kilimo ni Uti wa Mgongo katika Taifa letu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wote tunajua kwamba Watanzania wengi wanaohitimu vyuo vikuu katika Taifa hili ni 800,000 lakini watu ambao wanaajiriwa kwenye sekta rasmi karibu watu 20,000 tu ambapo 780,000 wanakwenda kuajiriwa kwenye sekta ya kilimo. Hata hivyo, sekta ya kilimo kumekuwa na tatizo la uwekezaji, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wahitimu hawa wanapewa mikopo ili wajiajiri na wainue maisha yao pamoja na kuchangia pato la Taifa?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Migogoro ya ardhi katika nchi hii ipo katika kila wilaya na kila mkoa, lakini katika Mkoa wetu wa Songwe mpaka sasa hivi hatujapata Baraza la Ardhi la Wilaya na Wilaya zetu za Ileje Momba na maeneo mengine zinakwenda Mbeya Mjini. Je,ni lini Serikali sasa itaanzisha Baraza la Ardhi la Wilaya katika Mkoa wetu wa Songwe?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kila mwananchi wa Tanzania ana haki ya kulindwa na Serikali yake na sasa hivi kumetokea wimbi kubwa sana kwenye Nchi ya Afrika Kusini, wageni wanauawa, wanatekwa, wanachomwa moto na wanateswa sana. Je, Serikali ya Tanzania imechukua hatua gani kuwalinda Watanzania wote ambao wako Nchini Afrika Kusini kwa kipindi hiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Mji wa Tunduma ni mji unaokua kwa kasi na kuna miradi karibuni miwili au mitatu inatekelezwa kwenye Mji wa Tunduma, lakini tangu imeanza kutekelezwa mpaka sasa hivi wananchi hawajaanza kupata maji ya uhakika na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja wamekuwa wakiwapa tarehe kila wakati za kumaliza miradi hiyo.

Je, ni lini miradi hiyo itakamilika ili wananchi wangu wa Mji wa Tunduma waanze kupata maji safi na salama kwa wakati?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Mji wa Tunduma ni sawa na Mji wa Mafinga na mji huu uko mpakani mwa Tanzania na Zambia na ni sura ya nchi ya Tanzania ambayo inapitiwa na Mataifa zaidi ya nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa uboreshaji wa miji hasa kwenye miundombinu ya barabara, unatakiwa ufanyike pia katika Mji wa Tunduma: Je, Serikali imejipanga namna gani kuhakikisha kwamba Mji wa Tunduma unapata barabara bora katika mpango huu ambao utaanza mwaka 2020.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na swali la msingi linalohusu Baraza la Kata, pia Mkoa wetu wa Songwe hauna Baraza la Ardhi la Wilaya. Nimekuwa nalalamika sana kwenye Bunge hili na Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu kwamba jambo hili watalishughulikia haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wananchi wangu wa Songwe wanakwenda Mbeya kusikiliza kesi zao na inasababisha gharama kubwa sana za kwenda kufika kule kusikiliza kesi na kurudi.

Je, ni lini Baraza la Kata litaanzishwa katika Mkoa wetu wa Songwe?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini Serikali itajenga barabara ya baypass ya kutoka Mpemba kwenda Tunduma kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati anafanya kampeni zake kipindi cha mwaka 2015?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kumekuwa na msongamano mkubwa sana kwenye magereza mbalimbali hapa nchini na hasa ukiangalia kwa mfano kama Gereza letu la Ilembo pale Vwawa wafungwa wanaotakiwa kukaa pale pamoja na mahabusu ni 120; lakini mpaka sasa hivi kuna mahabusu pamoja na wafungwa zaidi ya 400 na hili limekuwa ni tatizo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua haya magereza kutokana na mrundikano huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kumekuwa na matatizo makubwa sana katika magereza haya, hakuna zahanati katika magereza yetu na kumekuw ana tatizo kubwa sana la wafungwa kutolewa kwenye haya magereza na kupelekwa kwenda kutibiwa katika hospitali mbalimbali hapa nchini wakati huo magereza hawana magari.

Serikali ina mpango gani wa kujenga zahanti katika magereza yetu yote hapa nchini ili wafungwa na mahabusu katika maeneo haya wawe wanatibiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nakumbuka mwaka 2017/2018 Serikali ilitenga karibuni bilioni 900 kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwenye Wizara ya fedha, na fedha hizi, zilikuwa zinakwenda kutoa elimu kwa walipa kodi watanzania, na sasa hivi kumekuwa na kero kubwa sana ya kodi kwenye nchi hii, na biashara nyingi zinafungwa katika Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, Je, Serikali imejipanga namna gani, namna ya kutoa elimu kwa walipa kodi ili Watanzania hawa waweze kujua wanalipa kodi kutoka kwenye faida, au wanalipa kodi kutoka kwenye mtaji? Kwa sababu elimu hiyo hawana mpaka sasa hivi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika Tunduma ni mpakani na kuna msongamano mkubwa sana wa malori yanayovuka mpaka wa Tunduma kuelekea Zambia, lakini pia wananchi wamekuwa wakipata shida sana ya kuweza kutumia barabara moja ambayo iko kwenye mji wetu wa Tunduma, lakini kuna bypass ya barabara inayotokea Mpemba kuelekea Tunduma Mjini kilometa 12 na Mheshimiwa Naibu Waziri alipita kuja kuingalia barabara ile na akatuahidi kwamba barabara ile ingeweza kujengwa katika mwaka huu wa fedha.

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ile ili kupunguza msongamano na kuwapa unafuu Wananchi wa kuendelea kutumia barabara yetu ya Mji wa Tunduma? Ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA:Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Pamoja na majibu ya Serikali ya kuonesha masoko mbalimbali nje ya nchi, lakini ukweli tu ni kwamba Serikali hii imekuwa ikizuia sana wafanyabiashara wanaopata masoko nje kwa kisingizio kwamba kuna njaa na haijawahi hata siku moja kuweka mpango wa kufidia hasara ambazo zinatokana na zuio hilo la Serikali.

Sasa Je, Serikali imejiandaa namna gani kuhakikisha kwamba inawapa taarifa wakulima hawa na wafanyabiashara kwamba haya masoko yapo kwasbaabu Bunge sasa hivi haliko live?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili; Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kuna mpango wa stakabadhi ghalani lakini katika mazao haya ambayo ni ya mpunga pamoja na mahindi hasa katika Nyanda za Juu Kusini mpango huu haujaanza kufanyakazi. Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu huu wa stakabadhi ghalani katika mazoa ya mahindi na mpunga kwenye Nyanda za Juu Kusini?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba vijiji vitano mpaka sasa hivi vimeshakamilika kupata maji katika Jimbo la Momba ambapo jumla ya vijiji vilivyopata maji sasa hivi vitakuwa ni saba (7) lakini jimbo hili lina vijiji 82 ina maana kati ya vijiji 82 ni vijiji saba (7) tu ndiyo vyenye maji ya bomba. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba katika bajeti hii ambayo imetengwa ya shilingi bilioni 1.7 inapelekwa kama ambavyo imetengwa ili kwenda kupunguza tatizo la maji kwenye Jimbo la Momba?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 1973 katika Mji wa Tunduma uliazishwa mradi wa maji wa mserereko katika Kata za Mpemba na Katete. Mradi ule sasa hivi umekuwa ukitoa maji kidogo sana kutokana na kutokukarabatiwa kwa muda mrefu. Serikali ina mpango gani kukarabati mradi ule ili uwahudumie wananchi wa kata hizo mbili?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado kuna malalamiko makubwa sana kwa Madereva wa malori na mabasi na karibu asilimia 90 ya Madereva hao hawana mikataba ya kazi na kwa sababu Serikali inasema kwamba Mikataba yao ilitakiwa iboreshwe toka mwaka 2015 na mpaka sasa mikataba yao bado haijaboreshwa na bado hawajapewa mikataba.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha jambo hili ili wafanyakazi hao waweze kufanya kazi yao vizuri kwa sababu wakiwa na mawazo sana wanaweza wakasababisha ajali na Watanzania wengi wakapoteza maisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na tatizo kubwa sana kwa sisi ambao tunaishi mipakani na mmeona kuna migomo mingi sana inatokea pale Tunduma watu Madereva wanapaki malori kwa sababu tu ya migongano kati ya wamiliki wa mabasi na malori kwa ajili ya mikataba hiyo? Sasa Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba jambo hili linakwisha haraka kwa sababu ni muda mrefu sasa na Serikali ipo, inatoa majibu humu Bungeni lakini utekelezaji unakuwa hakuna? Ahsante. (Makofi)

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's