Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Edwin Mgante Sannda

Supplementary Questions
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa matatizo yanayoikumba Mafinga yanafanana kabisa na yale yanayoikumba Hospitali ya Mji wa Kondoa kwa maana ya kwamba Kondoa inahudumia Halmashauri tatu za Kondoa Mjini, Kondoa Vijijini pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chemba. Je, Serikali ina mpango gani na inafikiria nini katika kuongeza rasilimali fedha na rasilimali watu ili kukidhi mahitaji?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Kwa kuwa dhamira inaonekana ni dhahiri ni mchakato tu unaendelea, je, ni lini Serikali itatoa maagizo kamili kwa Wizara zake zote ili pale panapotakiwa ujenzi wowote mpya au uendelezaji wa majengo au miundombinu ya Ofisi zake ifanyike Dodoma badala ya kuendelea kufanyika Dar es Salaam?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mazingira ya baadhi ya Halmashauri kuwa upya na changa kama ilivyo Halmashauri ya Mji wa Kondoa, vyanzo vya mapato ya ndani, huwa ni vidogo sana na hafifu; je, Serikali haioni umuhimu kupitia Wizara zake husika zenye dhamana kwa vijana na akina mama kuweka walau ruzuku fulani kufikia ukomo ili iweze kukidhi mahitaji ya vijana na akina mama?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa fursa. Wilaya ya Kondoa hususan pale Kata ya Kolo na nyinginezo, ipo michoro ya mapangoni ambayo ni vivutio vikubwa sana vya kihistoria kwa ajili ya utalii, lakini vimekuwa havitangazwi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvitangaza ili kizazi cha sasa na cha baadaye kitambue hii fursa na kuweza kuitumia ili hatimaye pia kipato kiongezeke?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tunashukuru sana kwa kazi ya barabara inayoendelea kutoka Dodoma - Kondoa - Babati ingawa inakwenda kwa kasi ya kusuasua. Tatizo moja kubwa wakati wa ujenzi kuna alama na maelekezo mbalimbali yanayotakiwa yawepo wakati wa ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara hii hizi alama zinapungua maeneo mengine hakuna kabisa, kwa hiyo, unakuta watu wanapotea kilomita kadhaa halafu ndiyo urudi tena. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi hawa waweke hizi alama ili kuondoa ajali na upotevu wa muda wa namna hii? Ahsante.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa fursa. Wilaya ya Kondoa hususan pale Kata ya Kolo na nyinginezo, ipo michoro ya mapangoni ambayo ni vivutio vikubwa sana vya kihistoria kwa ajili ya utalii, lakini vimekuwa havitangazwi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvitangaza ili kizazi cha sasa na cha baadaye kitambue hii fursa na kuweza kuitumia ili hatimaye pia kipato kiongezeke?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza; kama alivyoeleza Naibu Waziri mpaka sekondari elimu bure, lakini pia ukienda Chuo Kikuu kwa elimu ya juu tunayo mikopo ya wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kundi lililobaki ni kidato cha tano na cha sita. Kwa kuwa changamoto ya uwezo wa kugharamia elimu iko pia kwa wananchi hasa ambao nao wanakwenda kidato cha tano na cha sita ambapo imepelekea baadhi yetu nikiwemo mimi kuweka mpango mahsusi kwenye Majimbo yetu ya kuwalipia wanafunzi wanaofaulu kwenda kidato cha tano na cha sita; pamoja na changamoto ya uwezo wa Serikali; je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kulijumuisha kundi hili la kidato cha tano na cha sita kwenye Mpango wa Elimu Bure? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Swali la pili. Ili mpango wowote ufanikiwe, ni lazima kuwe na lengo na dhamira ya dhati ya kuhakikisha jambo hili linafanikiwa na kuwekewa mikakati. Kama tunavyozungumzia kwenye upande wa maji, tunasema mpaka 2020/2021 tuwe tumefikia asilimia 85 ya Watanzania wawe wanapata maji safi na salama; je, Serikali haioni umuhimu sasa kuweka muda mahususi kwa maana ya time frame na malengo lini tutaanza kutoa elimu bure kwa kidato cha tano na cha sita kama ilivyo kwenye maeneo mengine? (Makofi)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika kuipunguzia mzigo Hospitali ya Halmashauri ya Mji, Kondoa ambayo inahudumia zaidi ya halmashauri tatu, zahanati za Kata mbili za Kolo pamoja na Kingale zimewekwa katika mpango wa kupandishwa hadhi na kuwa vituo vya afya. Je, ni lini sasa Serikali italeta hizo fedha kwa ajili ya kutekeleza hiyo awamu ya kuweka vituo vya afya?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika jitihada za kuendelea kuinua ubora wa elimu suala la kuimarisha kitengo hiki cha udhibiti ubora ni suala ambalo kwa kweli halina mjadala. Hali ilivyo sasa hivi wale wenzetu pale ni kama wamevunjika moyo na wamekata tamaa kwa kukosa motisha.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa Serikali itawaweka hawa watumishi wa kitengo hiki kwenye viwango kama ilivyo maafisa elimu au walau waweze kupewa posho za madaraka kama zilivyo za Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Wataribu wa Elimu Kata? (Makofi)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kondoa Mjini tulichimba visima kumi, tumepata usambazaji wa visima vitano, lakini bila ya ukarabati wa miundombinu ya maji pale mjini, hizi gharama zilizotumika kusambaza visima vitano ni sawa na bure.
Je, ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji mjini ambayo pia ni ahadi ya Waziri Mkuu? Ahsante.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu ni Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, ni sera, sheria na kule kwenye halmashauri zetu lisipotekelezwa ni hoja ya ukaguzi lakini bado kuna changamoto za utekelezaji. Je, ni lini sasa Serikali itatoa waraka mkali kabisa ambao utaelekeza halmashauri zote zitekeleze na zisipotekeleza ziweze kuwajibishwa?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi wa Kondoa Mjini walikusanya nguvu sana wakajenga Kituo cha Polisi kidogo pale Mjini Stand. Kituo hiki sasa kina zaidi ya mwaka kimefungwa kutokana na upungufu na ukosefu wa askari. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea askari kituo kile kifunguliwe na kifanye kazi iliyokusudiwa? (Makofi)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi mvua za mwaka 2017 mwishoni na mwaka huu 2018 zimevuruga sana miundombinu katika Jimbo la Kondoa Mjini. Moja ya barabara iliyoharibika sana ni barabara ya Kingale ambapo mpaka daraja lenye mawasiliano makubwa sana kati ya Kingale na maeneo ya jirani lilivunjika. Daraja hilo limekuja kuangaliwa na watu wa TARURA Mkoa na watu wote wamelichunguza, mpaka sasa hivi bado halijafanyiwa kazi.
Je, ni lini sasa Serikali italeta mpango wa dharura wa kurudisha mawasiliano pale Kingale?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Hapa naweza nikasema ni pale ambapo Golikipa wa Simba anapigiwa shuti la penati na mshambuliaji wa Yanga halafu yeye anaenda kushoto goli linaingia kulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, majibu yaliyotolewa na Serikali pamoja na shukrani zote, lakini kidogo yamekwenda tofauti na malengo ya swali lenyewe. Huu utaratibu wa Hospitali Tembezi tumekuwa tukiufanya hasa sisi wenyewe Wabunge tukishirikiana na Ofisi ya Mkoa. Tumefanya mara kadhaa, kama mara tatu na tunatarajia tena mwezi wa Septemba, 2018 tutapata nyingine kutoka Marekani.
Mheshimiwa Spika, nilichokuwa nikitarajia hapa ni ubunifu huu tulioanza nao kutokana na uchache wa huduma za kibingwa lakini pia na huduma nyingine za afya, kwenye ngazi ya Halmashauri na kwenye ngazi ya Wilaya tuupeleke kwenye vijiji, ndiyo maana niliainisha vijiji vingi ambavyo tunavizungumzia hapa.
Mheshimiwa Spika, kwa kawaida tumekuwa tunachukua gari la chanjo na mengineyo ya miradi kufikisha huduma za kliniki za watoto, chanjo, huduma za akinamama wale, lakini sasa zinafanyika nje kwenye uwazi, jambo ambalo halina staha sana, ndiyo maana tukawa tunahitaji Kliniki Tembezi. Huu ni ubunifu tuliofanya kwenye ngazi ya Wilaya, sasa tuufanye kwenye ngazi ya Vijiji. Je Serikali haioni umuhimu wa kuenzi na kuiga ubunifu huu kwenye ngazi ya vijiji? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuweza kujenga Zahanati kwenye kila Kijiji kama ilivyo sera yetu, gharama yake ni kubwa sana na haya maeneo yote niliyoainishwa unaweza ukazungumzia maeneo matano mpaka sita ambapo ukipata gari moja la namna hiyo la Kliniki Tembezi, linaweza likakusaidia kuweza kumaliza huduma ya kujenga Zahanati nne. Je, ni lini basi, na kwa kuwa tunafahamu uwezo wetu ni mdogo bora tufanye...
Eeh! Mheshimiwa Spika, ni lini basi, Serikali itaiga ubunifu huu na kutuletea Mobile Clinic Van kwa ajili ya maeneo yetu ya Kondoa? (Makofi
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu. Labda niseme tu kweli tunaishukuru Serikali kupata, nitumie lugha ya haka kagari, tumepata gari aina ya Suzuki Maruti ndogo sana ambayo kwa mazingira ya Jimbo la Kondoa lina uwezo wa kufanya shunting katika kata tatu za mjini tu, huku pembezoni litakuwa haliwezi kwenda kabisa kwa sababu njia haziruhusu. Je, ule umuhimu wa uhitaji wa huduma hii, Serikali haioni?.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; barabara kubwa imekamilika ya kutoka Dodoma kwenda Babati. Ongezeko la uhitaji wa huduma za dharura umekuwa mkubwa kweli, ajali ni nyingi kila uchao tunapata taarifa hizi, gari hili haliwezi kumudu. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea gari la wagonjwa lenye kukidhi mahitaji ya hospitali ya Mji Kondoa?(Makofi)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nachukua fursa hii kushukuru na kupongeza majibu mazuri ya Serikali. Pia niseme tu kwamba ushauri wa kuendelea kutumia Chuo cha Munguri kilichopo sasa tumeupokea na tunaendelea kuutumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, uwepo wa VETA utaongeza sana na kupanua wigo wa fursa za elimu ya ufundi ili kuendeleza azma yetu ya viwanda. Siyo hivyo tu, lakini pia kuongeza ajira kwa vijana. Swali; je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba maboresho haya mliyoyasema yanaingizwa kwenye Mpango na Bajeti ya VETA ili azma hii itekelezwe kwa haraka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naelekea huko mzee, swali la pili, azma ya kuwa na VETA ina maslahi mapana sana kwa wanachi, siyo tu kwa wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini, lakini kwa Kondoa nzima kama Wilaya. Pia uwepo wa Taasisi ya kitaifa kama hii yenye hadhi ya VETA na sasa Kondoa ni Halmashauri ya Mji, itaongeza tija kubwa sana kwenye kuchangamsha uchumi wa Kondoa. Swali je, Serikali inatupa commitment gani ya kuhakikisha inaharakisha mchakato huu mara tu baada ya kupokea hiyo barua kutoka Kondoa?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwenye Kata ya Kolo, Jimbo la Kondoa Mjini tulipata ufadhili mkubwa sana wa wenzetu wa MKAJI kwa ajili ya kukarabati Zahanati kwa lengo la afya ya mama na mtoto, na waliweka lengo kubwa sana mkazo mkubwa kwenye huduma ya maji, kimekarabatiwa kisima kirefu, kimemalizika sasa hivi takriban miezi mitatu. Kinachokwamisha ni supply ya umeme pale ili huduma hiyo iweze kuanza kutumika. Tumewaomba TANESCO Wilaya, TANESCO Mkoa mpaka sasa hivi bado tunasubiria. Je, ni lini sasa wenzetu wa TANESCO watatuletea ule umeme ili zoezi zima la wenzetu wa MKAJI lianze kuleta tija?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nipongeze majibu mazuri ya Serikali kutoka kwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu mazuri hayo, basi nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, ripoti hii ya utafiti wa awali sisi kama watu wa Ausia na kule Kondoa hatuna, kwa hiyo hata kuweza kujua kuna kiwango cha chokaa kiasi gani imekuwa ni mtihani na ukizingatia kwamba madini haya ni muhimu sana katika kazi za ujenzi, sasa tunataka kujua, ni hatua gani na wao kama Serikali watatusaidia ili twende kwenye utafiti wa kina tuweze kujua madini kiasi gani yapo kule tuendelee na hatua ya pili ya kupata mwekezaji na hatimaye kuanza kunufaika na uwepo wa madini hayo? Hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ili Mheshimiwa Naibu Waziri akajiridhishe na hali halisi iliyoko pale akifika site, je, anaonaje sasa mimi na yeye pamoja na wataalam wake wa Wizara tukaongozana tukaenda site tuweze kuharakisha mchakato huu wa wananchi wa Kondoa Mjini waweze kunufaika na madini haya ambayo yanaonekana yako kwa wingi.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza, kwanza fursa za vyanzo vya mapato na uwezekano wa kuongeza mapato inatofautiana baina ya halmashauri na halmashauri. Hili suala la malalamiko lina kosa msingi linabaki kuwa dhana.

Sasa je, Serikali huwezi kulinganisha kati ya Kondoa au Geita au hata Dar es Salaam fursa za mapato zilizopo, na Madiwani ni sehemu ya wanaoweka nguvu ya kukusanya mapato na kuongeza mapato. Serikali haioni umuhimu wa kuwaruhusu walipe kadiri ya uwezo wa halmashauri zao ili pia iwe sehemu ya motisha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, lini sasa maana tulipata Waraka wa kutuambia tulipe 40,000 na hapa tunazungumzia posho za vikao peke yake, lini sasa maslahi mengine tunaendelea kuruhusu kadiri ambavyo inafanya kazi. Lini sasa tutapata Waraka wa kufafanua ili ule Waraka uliotolewa mwezi Januari uweze kupitwa maana Serikali inafanya kazi kwa maandishi?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitumie fursa hii kushukuru majibu ya Serikali sambamba na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, namba moja, ni miaka tisa sasa toka tumeingiza zaidi ya milioni 143 kwenye mradi huu na hakuna ambacho kimeweza kuwa realized mpaka leo. Ukichukua faida ambazo tungezipata kwa mradi ule watu 12,000 kunufaika tungekuwa tu kwa mwaka tunapata zaidi ya bilioni 50; mpaka leo tunazungumzia miaka tisa tungekuwa tumetengeneza zaidi ya bilioni 500, ukiangalia hii opportunity cost peke yake acha multiplier effect kipindi cha uchumi wa viwanda na mazao ambayo yangetokana na matokeo yale ya pale kwenye mradi ule tungekuwa tumepiga hatua kubwa sana kwa wananchi wa Kondoa.

Je, ni lini sasa Serikali itafikia hatua ya kuweza kufanya hii tathmini ya kina na hatimaye kufanya hii tathmini ya kina na hatimaye kukamilisha mchakato mradi huu utekelezwe? la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ili Mheshimiwa Naibu Waziri uweze kujiridhisha na fursa iliyoko kule fursa kubwa sana.

Ni lini sasa mimi na wewe na pamoja na wataalam wako tutaongozana tuende pale Mongoroma tukaone nini kinaweza kikafanyika kwa haraka zaidi? Ahsante sana.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimwa Spika, nakushukuru. Labda tu kabla ya kuuliza maswali yangu ya nyongeza, nikuombe tu univumilie kidogo kwa sababu haya majibu ya Serikali sioni matumaini kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwanza tunazungumzia uchumi wa viwanda na tegemeo kubwa lazima tuweze kuzalisha wanasayansi wa kutosha kabisa. Sasa mimi natoa mfano tu wa Mkoa wetu wa Dodoma tulikuwa kwenye vikao vya ALAT hata kwako Mheshimiwa Spika tuko chini ya 20% ya ukamilishaji wa maboma ya maabara. Sasa huu uchumi wa viwanda unakwenda kulishwa na watu kutoka wapi kama tunawapeleka watu wa masomo mengine na siyo wanasayansi?

Mheshimiwa Spika, unapozungumzia shilingi milioni 8 ambazo Halmashauri ya Mji Kondoa tumeidhinisha hizi ni zile fedha ambazo nimezitoa mimi kupitia Mfuko wa Jimbo mwaka jana na tulikwishazitoa. Boma moja la darasa linajengwa kwa shilingi 25 sisi tunazungumzia shilingi milioni nane. Hebu Serikali ione ni namna gani tunakuja na mkakati wa dharura sasa kama ambavyo tumefanya kwenye maboma ya madarasa na kwenye nyumba za walimu ili tuweze kukamilisha hizi maabara nchi nzima. Swali la kwanza hilo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, walau mimi nina maabara moja tu kati ya sekondari nane (8) ambayo imekamilika na yenyewe haina vifaa. Ni lini tutapata angalau hivyo vifaa vya maabara kwenye hata hiyo moja ambayo mpaka sasa imeshakamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba majibu ya Serikali tafadhali.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hospitali ya Mji wa Kondoa inahudumia takriban Halmashauri sita. Tunazungumzia Kondoa Vijijini, Chemba, Kiteto, wakati mwingine mpaka Hanang’ na Babati. Bajeti tunayopata ni shilingi milioni 45 kati ya milioni 160 ambayo tunahitaji kutoka Basket Fund. Nimelizungumzia sana suala hili Bungeni hapa.

Je, ni lini sasa Serikali itakubaliana na uhalisia wa mahitaji hayo na kutuongezea bajeti yetu kukidhi mahitaji ya wananchi wa maeneo hayo?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pale jimboni Kondoa tunazo shule mbili, Shule ya Iboni na Shule ya Ubembeni ambazo zinavitengo vya watoto wenye mahitaji maalum zote ziko kata moja ya Chemchem ambayo ni kata ya katikati kabisa katika jimbo zima. Hali ya mapato yetu ya ndani ya Halmashauri ni ndogo sana ambayo imetupelekea mpaka mimi mfuko wa jimbo kuweza kusaidia miundombinu stahiki kwa ajili ya wale watoto pamoja na choo, walimu pia hatuna.

Je, Waziri ni lini unaweza ukafanya utaratibu wa kutuupa uzito na kuja kufanya tathimini ya kina ili tuweze kuweka miundombinu stahiki na walimu wa kututosheleza ukizingatia watoto hao wenye mahitaji maalum wanaendelea kuongezeka siku hadi siku?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wananchi wa vijiji vya Chemchemi, Tampori, Iyoli kule Kata ya Kingale pamoja na Muluwa Kata ya Serya wamekuwa wakipata athari kubwa sana kutokana na wanyama waharibifu hawa tembo, almaarufu kule Zanzibar, Unguja ya Kusini kama ndovu.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali, wameanza kufanya malipo ya vifuta jasho na vifuta machozi kuanzia mwaka 2016 kwa baadhi ya vijiji, lakini athari hizi zimeanza 2012, taratibu zote zilifuatwa na pia madai yakawasilishwa Wizarani.

Sasa Je, kuna mpango gani wa kufanya malipo ya maeneo yaliyoachwa tangu mwaka 2012 kwa watu wote na kwa maeneo yote ambayo yalipata athari?
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Sisi kwetu pale Kondoa hospitali tunayo lakini hospitali ile inahudumia zaidi ya Halmashauri tatu za Chemba, Kondoa Vijijini, Babati na wakati mwingine mpaka Hanang. Kwa hiyo, mahitaji ya huduma yamekuwa ni makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tunaipongeza Serikali kwa kukamilisha ile barabara ya kutoka Dodoma - Babati. Kunapokuwa na maendeleo na changamoto zinaongezeka sana. Kukamilika kwa barabara ile kumeongeza sana mahitaji ya huduma ya hospitali ikiwemo huduma za dharura. Nimelia sana kuhusiana na suala la ambulance, tuna tatizo kubwa sana la ambulance. Ni lini sasa Serikali itaipatia Hospitali ya Mji wa Kondoa ambulance mpya?

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's