Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Supplementary Questions
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyama vya Upinzani vimekuwa vikileta vurugu, kutotii amri ya halali za Serikali na Jeshi la Polisi na wakati mwingine kuleta vurugu, kwa mfano, katika Jimbo langu la Ulanga kwenye kijiji cha Iputi - Nambuga walichoma nyumba sita za wananchi. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na suala hili, ili kutokomeza kabisa tabia hii.
Pili, kumekuwa na Wabunge, wakileta uchochezi wa kisiasa katika maeneo yetu ya makazi. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na Wabunge kama hawa?(
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kutuangalia sisi kambi mbadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha afya cha Lupilo ndiyo kama Hospitali ya rufaa katika kata tano za Ilagua, Lupilo, Kichangani na Milola. Je, ni lini serikali itaifanyia ukarabati kituo hiki cha afya maana kina hali mbaya ya majengo?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Japokuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema majibu yatakuwa ni yaleyale na mimi naomba nikumbushie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Maswa linafafana na tatizo lililoko Ulanga katika Kata ya Ilagua, Lupilo, Minepa na Milola ambapo Mheshimiwa Rais aliahidi kuhalalisha hili eneo la buffer zone ili wananchi hawa wafaidi tunu ya pekee ya ardhi tuliopewa. Je, ni lini Serikali itahalalisha na itatekeleza ahadi hii ili wananchi hawa wafaidi?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kutupa kipaumbele sisi Kambi mbadala.
Kwa kuwa matatizo ya mawasiliano yaliyoko katika Jimbo la Nanyamba yanafanana na Jimbo la Ulanga, Kati ya Kata ya Ruaha, Chilombola, Ilagula, Ketaketa na Ilonga; je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu za mkononi katika Kata hizi ili na wananchi hawa wafaidi mawasiliano ya simu za mkononi?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba nitoe pole kwa wananchi wangu wa Lupilo wanaopata misukosuko ya kubambikiziwa kesi na Jeshi la Polisi, nalaani vikali matumizi mabaya ya nguvu za Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, mradi huu tangu uanze una miaka mitatu sasa hivi; upembuzi yakinifu sijui nini vinafanyika. Sasa Mheshimiwa Waziri anawaambia nini wananchi wa Lupilo wanaotarajia mradi huu uwe mkombozi wa maisha yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu wa kuiunganisha ofisi yake ya kanda na Mkurugenzi wangu wa Ulanga ili iwe rahisi kwa ajili ya ufuatiliaji na utekelezaji wa mradi huu?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; kwanza naomba nioneshe masikitiko yangu kwa kiwango cha juu kwa Waziri kijana kujibu majibu ambayo hayaendani na kasi ya Serikali kwa sasa hivi. Haya
mashirika ambayo ameyataja TRA, BOT, ANESCO, NHC na TPA mimi mwenyewe binafsi nilitembelea wakati nipo NHIF lakini ni tofauti ya anavyosema Waziri sasa hivi. Je, katika michakato ambayo imeshawahi kutokea nchini kwetu
mchakato mgumu ulikuwa wa kuhamia Dodoma, Rais alisema mwaka jana mwezi wa Saba lakini sasa hivi Mawaziri wote wamehamia Dodoma.
Swali la kwanza; je, ni nini kinashindikana mashirika haya ya umma kuhamia NHIF wakati ni kitendo cha muda mfupi tu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ofisi yako ni
shahidi Wabunge tulipotoka mashirika ya private insurance kwenda NHIF tuliweza ku-save kiwango kikubwa cha pesa mpaka tukanunua madawati nchi nzima. Kumekuwepo na ubadhirifu mkubwa wa pesa za Serikali kwa haya mashirika ya umma through private health insurance. Je, Serikali
itakubaliana na mimi sasa hivi kufanya mchakato wa kuangalia kiwango gani cha pesa kinachopotea iwapo mashirika ya umma yataendelea kutumia private health insurance badala ya NHIF?
MHE.GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Sasa hivi ninavyoongea barabara ya Ifakara - Mahenge haipitiki kabisa, wananchi wanakosa huduma za muhimu kama petroli, dizeli na dawa kwa ujumla. Je, wananchi wa Ulanga wanataka kusikia kauli ya Serikali nini kitafanyika sasa hivi ili watu hawa wa waweze kusafiri kwenda Mahenge? (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wapogoro tunajulikana dunia nzima kuwa chakula chetu kikubwa ni wali na kambale, kwa kuwa Ulanga tunalima sana mpunga.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga kiwanda ili sasa wakulima wasiuze mpunga wauze mchele ili kuwaongezea kipato? (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, katika ngo’mbe milioni 28 ni ng’ombe 700,000 tu wanaozalisha maziwa, hii inatokana na wafugaji kutokuwa na watetezi katika nchi wakiwemo wafugaji wa Iragua. Je, Wizara sasa iko tayari kuhakikisha wafugaji hawanyanyaswi na watu wa maliasili? (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jimbo langu la Ulanga tumebahatika kuwa na mto mkubwa sana, Mto wa Kilombero lakini wananchi wanaoisha maeneo yale hawajawahi kunufaika na chochote kile kuhusu uvuvi.
Je, sasa Wizara iko tayari kutoa ushauri wa kitaalam na vifaa ili wananchi wanaoishi karibu na mto ule wanufaike na shughuli za uvuvi na Serikali ipate mapato? (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa nafasi ya pekee napenda nikipongeze Chama changu cha Mapinduzi kwa kutimiza miaka 41 ya utawala bila kung’oka, na kwa utendaji huu tuna miaka 41 mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri atakuwa shahidi tangu hili pori lianzishwe ni miaka mingi sasa na watu wameongezeka kwa kiasi kikubwa, sheria hizi zilizoanzisha mapori ndiyo sheria hizi hizi zilizoanzisha vijiji, inapotokea maeneo wanayoishi wananchi yakagundulika madini wananchi wanatolewa, lakini wananchi wanapohitaji kulima maeneo ya mapori wanaambiwa sheria zizingatiwe. Kwa nini sheria ziko bias upande mmoja kwa kuwaonea wananchi ambao ni wanyonge?
(b) Mheshimiwa Waziri tulikuwepo nae Ulanga wiki mbili zilizopita ameona jiografia ya Ulanga ilivyo ngumu maeno yote ya matambalale ambayo wananchi wanaweza wakalima ni Mapori Tengefu, ni Hifadhi na Bonde la mto Kilombero, naomba busara zitumike ili wananchi wapate maeneo ya kilimo kwa sababu wameongezeka kwa kiasi kikubwa.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Katika Jimbo langu la Ulanga kuna mradi mkubwa wa maji wa Mahenge Mjini ambao tayari umeshakamilika. Tatizo la huo mradi umeshindwa kuanza kwa kuwa tu, Idara ya Maji haina mita za kuwafungia wateja, kwa kisingizio cha fedha zikipatikana, fedha zikipatikana. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa ili Idara ya Maji iwafungie mita wananchi wa Mahenge Mjini ili waanze kufaidi matunda ya Mbunge wao kijana machachari?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba nitoe pole kwa wananchi wangu wa Ipanko, usiku wa leo kuvamiwa na Polisi na kupigwa sana na kuumizwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sasa hivi taasisi za kifedha zimeleta ugumu kukopesha taasisi za Serikali kwa sababu ya ugumu wao wa kulipa haya madeni. Je, sasa Serikali haioni kuwa inahitajika ifanye mpango wa dharura kwa ajili ya kutengeneza barabara za vijijini?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba ni-declare interest, na mimi ni mchimbaji mdogo japokuwa sijawahi kunufaika kutokana na mfumo mbovu wa Serikali. (Kicheko)
Tatizo lililoko Mpanda Mjini linafanana na lililoko katika Jimbo langu la Ulanga. Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kuwaelimisha na kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo wa Jimbo la Ulanga ili waweze kuyathaminisha madini haya wanayoyapata ili waweze kuyauza katika thamani halisi inayoendana na soko?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Swali langu ni hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ajali zinaendelea kutokea kwa wingi, hata hivi sasa hivi ninavyoongea ukipita barabara ya Morogoro – Dodoma kuna ajali nyingi sana, lakini traffic wamegeuka agent wa TRA kazi yao ni kusimamisha magari na kutoza faini. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba atoe tamko kuanzia leo hii matrafiki waache kutoza faini wakazane na kutoa elimu kwa kutoa elimu kwa watumia vyombo vya moto na wasafiri ili wajue ni haki gani watapata pindi ajali zinapotokea. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, asante sana, Wilaya ya Ulanga pamoja na kuwa na Mbunge kijana machachari lakini haina Mahakama ya Wilaya. Je, wananchi wa Ulanga wanaisikiliza Serikali yao ya hapa kazi tu inawaambia nini kuhusiana na jengo la Mahakama ya Wilaya? (Kicheko/Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Wanaulanga kwanza naomba niishukuru Serikali kwa ukamilishaji wa Daraja la Mto Kilombero, haya ndiyo matunda ya Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo yanazunguka Mto Kilombero yana shida kubwa sana ya maji…
Mheshimiwa Spika, Daraja la Mto Kilombero la kwenda Ulanga, limelamilika.
Mheshimiwa Spika, lile limekamilika, lile kubwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, kabisa na tunapita pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu ni hili, maeneo ambayo yanazunguka huu Mto Kilombero yana shida kubwa sana ya maji kwa upande Wilaya ya Kilombero, kwa maana ya Ifakara Mjini, pamoja na Tarafa ya Lupilo. Je, sasa Wizara ina mpango gani wa kubadilisha matumizi ya Mto Kilombero ili uwe unatumika kwa matumizi ya binadamu, kwa maana ya maji ya kunywa na kupikia?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naomba niishukuru Serikali kwa kuitupia sekta ya afya jicho la pekee katika Jimbo langu la Ulanga. Kituo cha Afya cha Lupilo karibu kinakwisha, sasa wananchi wa Ulanga wategemee nini katika huo mgawo? Siyo kwamba Madaktari ni wachache tu lakini ni pamoja na kuwa na watumishi wa afya wasio na sifa. Ulanga inakusikiliza sasa hivi Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ulanga limepewa kipaumbele sana kwenye sekta ya afya, hilo naishukuru Serikali, hicho ndiyo kipaumbele cha Mbunge wao, kipaumbele cha kwanza afya, cha pili afya, cha tatu afya. Shida kubwa iliyopo ni watumishi wachache, Mheshimiwa Waziri katika majibu yake haya ya kugawa watumishi wa afya wananchi wa Ulanga wanamsikiliza sasa hivi anawaambia nini?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ushoga usagaji na kutukuna matusi mithili ya bomu la nyuklia siyo maadili yetu na desturi ya Mtanzania, lakini vitendo hivyo vimekithiri kartika mitandao yetu ya kijamii. Kwa mfano, wapo mashoga maarufu wanajitangaza katika mitandao yetu ya kijamii na siyo utamaduni wa Kitanzania; kwa mfano kuna mtu mmoja maarufu anaitwa James Delicious.
Mheshimiwa Spika, kuna vikundi vya matusi kabisa katika mitandao ya kijamii. Mfano kuna team Wema, team Zari, team Diamond, team Shilole, hawa wamekuwa wakitukana matusi katika mitandao ya kijamii.
Je, nini kauli ya Serikali kutokana na hili kwa sababu linachangia kwa kiwango kikubwa sana kuharibu maadili na utamaduni wa Kitanzania? (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri machachari na kijana, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo kuongezeka kwa wingi Ulanga limeanza tangu miaka ya 90 na tumepiga kelele lakini Serikali kwenye ujenzi wa majosho wako nyuma lakini kwenye kupiga chapa kwa sababu inawaingizia mapato wamekuwa wako mbele. Naomba commitment ya Serikali iseme kuwa mwaka huu 2018/2019 tutajenga majosho. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwa kuwa kumekuwa na tatizo la masoko ya mifugo, masoko yaliyoko ni minada ya kienyeji ambapo wafugaji wanauza mifugo kwa bei nafuu. Je, lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa masoko ili wafugaji wauze mifugo yao kwa bei ya faida? (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri wakati akijibu hoja zangu za kuhusu fine kwa madereva wa bodaboda alikiri kweli haiwezekani bodaboda anabeba abiria mmoja, anatozwa fine Sh.30,000 wakati basi linalobeba abiria 60 fine ni ile ile Sh.30,000. Tunaomba atuhakikishie katika hayo mabadiliko ya sheria, je, hii sheria ya fine kwa ajili ya madereva bodaboda itakuwepo? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, Shule ya Msingi Iputi iliyoko Kijiji cha Mbunga katika Jimbo langu la Ulanga ina msongamano mkubwa sana wa wanafunzi. Sisi tumejenga wenyewe shule nyingine, tumejenga ofisi ya mwalimu kwa kushirikiana na Mbunge wao, tunachoomba usajili na kutuletea walimu. Je, Serikali ipo tayari? (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Ulanga ya sasa hivi tumeanza uchimbaji wa graphite ambayo tutakuwa tunasafirisha tani 350,000 hadi 500,000 kwa mwaka wastani wa malori 150 hadi 170 kwa siku kwa barabara ya vumbi hatuwezi Serikali peke yake itapata kodi ya mrahaba bilioni 61 hadi 100 kwa mwaka lakini bila barabara ya lami biashara hii hatuwezi kuifanya.
Sasa basi maswali yangu je, Serikali haioni umuhimu wa kukamilisha barabara hii haraka kabla ya mwaka 2020 ili tusizikose hela hizi ambazo tunazihitaji sana kwa sasa hivi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili Serikali ipo tayari kushirikiana na Mbunge kutafuta wafadhili mbalimbali kwa ajili ya kuangalia ni namba gani wataharakisha ujenzi wa barabara hii unafanyika? (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika Jimbo langu la Ulanga Kijiji cha Gombe kuna mradi mmoja mradi wa kiinimacho. Mawaziri wote anapokuja Waziri maji yanajazwa kwenye tanki usiku kucha, akija Waziri asubuhi anakuta yanatoka. Kaja Waziri kafanyiwa hivyo hivyo, kaja Naibu Waziri kafanyiwa hivyo hivyo. Sasa Mheshimiwa Waziri anatoa kauli gani kuhusiana na mradi huu kiini macho ambao unafanya wananchi wanashindwa kupata maji?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika mkakati wa Serikali kuhakikisha mikoa yote inaungana inakuwa na mtandao wa barabara; kuna barabara inayoanzia Mahenge – Mbuga kupitia Mbuga ya Selous mpaka Liwale. Rais aliahidi wakati wa kipindi cha kampeni, lakini sijaona mahali popote katika Wizara kama kuna mchakato wa kutoboa barabara hii kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Lindi. Je, Serikali inatoa kauli gani kutokana na hili?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, mgogoro uliopo Manyara unafanana na mgogoro uliopo Ulanga kati ya Selous Game Reserve na wananchi wa Kata za Ketaketa, Ilonga na Mbuga, Mheshimiwa Waziri analifahamu vizuri. Sasa wananchi wameendelea kukamatwa na kupigwa, huku siyo tu kuwachokoza wananchi, ni kunichokoza hata na mimi mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba majibu ya Mheshimiwa Waziri, lini yuko tayari kwenda kwa ajili ya kumaliza huu mgogoro kati ya Selous Game Reserve na wananchi wa hizi kata?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, mimi nakubaliana na wewe kuwa bila viboko wanafunzi hawawezi wakaenda. Lakini kwa nini Serikali isitoe aina ya mfano wa kiboko ambacho kinatakiwa kitumike kuchapia wanafunzi? Tumeshuhudia walimu wakikata kuni kwa ajili ya kwenda kuwachapia wanafunzi; kwa hiyo watoe kiboko cha mfano.l
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wananchi wengi hasa wa Ulanga wamekuwa na muamko mkubwa wa kujiunga na CHF liyoboreshwa, lakini wamekuwa wakilipa hela wanapoenda hospitali huduma zimekuwa haziridhishi, na hii inatokana na usimamizi mbovu wa CHF iliyoboreshwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali mwezi Aprili, 2018 imetoa mwongozo kuwa mtumishi atakayepangiwa kuwa CHF Manager asiwe na majukumu mengine yoyote, lakini huu mwongozo umekuwa haifuatwi. Je, kauli ya Serikali ni ipi kwa watumishi hawa wanaopangiwa kuwa Mameneja wa CHF, lakini wanapangiwa na majukumu mengine?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu linahusu barabara ya Kidatu – Ifakara; barabara yenye urefu wa kilometa 69.9. Mradi wake wenye thamani ya shilingi bilioni 109 ambao unafadhiliwa na DFID na European Union.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ilifunguliwa tarehe 5 Mei, 2018. Wakati inafunguliwa vifaa viliwekwa vingi na Mheshimiwa Rais lakini Mheshimiwa Rais alipoondoka na Mkandarasi akaondoa vifaa vyake. (Kicheko)

Je, Serikali inatuambia nini kuhusu barabara hii? Ina maana ndiyo tumepigwa changa la macho sisi pamoja na Mheshimiwa Rais?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ukiacha Wakuu wa Wilaya ambao wanafanya vibaya wako Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanaofanya vizuri. Kwa mfano, kwa Wakuu wa Mikoa yupo Salum Hapi wa Iringa amekuwa mbunifu kupita kiasi, Ndugu Alexander Mnyeti, Ndugu Mrisho Gambo na Ndugu Paul Makonda... (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, uliza swali Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali langu ni hili, je, Wizara ina mkakati gani wa kuwaandalia motisha ama tuzo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawa ambao wanafanya kazi vizuri?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kata yangu ya Mahenge Mjini ambapo ndiyo Mji wenyewe ulipo, kuna shida kubwa ya soko. Wananchi walijitolea wakajenga soko, Serikali ikatia hela zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018 Mwenge ulikuja ukafungua hilo soko, lakini mpaka leo hii soko hilo halijaanza kutumika. Kwa hiyo, Mwenge umedanganywa, Mbunge kadangaywa, wananchi wamedanganywa. Je, lini Serikali itasimamia ufunguaji wa soko hilo ili wananchi wapate kulitumia?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ugonjwa wa kifafa una mahusiano makubwa sana na ugonjwa wa akili, kwa sababu mgonjwa wa kifafa akikosa zile dawa zake anakuwa amechanganyikiwa na anakuwa mkorofi na kibaya zaidi mgonjwa wa kifafa huwa anaanguka, kwa hiyo, anaweza kuangukia kwenye moto ama kwenye maji.

Mheshimiwa Spika, Ulanga ni miongoni mwa maeneo kinara duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kifafa na Serikali kwa uzito huo ikaamua kutoa dawa hizo bure kwa nchi nzima, lakini mgao tunaoupata Ulanga haukidhi mahitaji na Serikali inalitambua hilo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuipa Ulanga kipaumbele kwa upatikanaji wa dawa hizi za kifafa?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimpongeze Mkuu wangu wa Wilaya kwa jitihada zote za kunyanyua elimu ya Ulanga Bi. Ngoro Malenya.

Mheshimiwa Spika, chuo anachoongelea Mheshimiwa Waziri ni cha mission na kinachukua wanafunzi wachache sana na fani chache ambazo haziendani na rasilimali zinazopatikana Ulanga kama madini, misitu na uvuvi. Wanafunzi wanaomaliza Ulanga kidato cha nne kwa mwaka ni 1000 hadi 1200 na hiki chuo kinachukua wanafunzi chini ya 150.

Mheshimiwa Spika, kwa nini sasa Serikali isishirikiane na misheni ili kuongeza kukipanua chuo hiki ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna eneo ambalo tulilitoa kwa ajili ya VETA wajenge Chuo cha Ufundi eneo la Mwaya. Je, Serikali inasemaje ipo tayari kutoa hela kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo hiki?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na wimbi kubwa la ongezeko la matumizi ya dawa za nguvu za kiume, enzi zenu nakumbuka kulikuwa na mkuyati, lakini sasa hivi, kuna super moringe, mundende, super gafina, gasosi mix, super shafti, sado power, amsha mzuka, Kongo dust na hii Kongo dust imeonesha kuwa mafanikio makubwa. Je, Serikali imeshafanya utafiti nini kinasababisha tatizo hili la watu kutokuwa na nguvu za kiume kupelekea kutumia sana hizi dawa?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa vinara wa kuwa na viwanda vingi na imekuwa ikitoa ajira nyingi sana kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro enzi hizo za ujana wetu.

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vilikuwepo viwanda vya maturubai, magunia, ngozi, mafuta ya kupikia, vipuli vya mashine, mazulia hata Ulanga tulikuwa na kiwanda cha pamba lakini baada ya ubinafsishaji viwanda vyote vikawa kushne, vikawa magofu ya kufugia mbuzi na Serikali imekuwa ikipiga mikwara mara kwa mara…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je, Serikali inatoa kauli gani sasa kwa magofu hayo ambayo yamegeuzwa na wawekezaji badala ya kufanywa kuwa viwanda?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ukiacha Taasisi nyingi kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake lakini Benki ya Kilimo ndiyo yenye dhamana ya kutoa mikopo. Benki ya Kilimo imekuwa na tabia ya ubaguzi, inatoa mikopo kwa wale wanawake ambao wana uwezo au wake za vigogo, lakini wale wanawake ambao wana uwezo mdogo na wamejiunga kwenye vikundi wamekuwa wakipewa masharti magumu.

Je, Serikali inatoa kauli gani hususan kwa wanawake wa Ulanga, Kilimanjaro na juzi nilikuwa Mbeya kule, hamna hata mmoja aliyepata mkopo?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ugonjwa wa dengue ni ugonjwa hatari sana na umekuwa ukiwa kwa kasi sana katika nchi yetu, lakini ugonjwa huu ni mgonjwa wa mlipuko kama magonjwa ya kipindupindu na magonjwa mengine, na Serikali imekuwa na utamaduni wa aidha wa kutibu bure au kwa gharama ya chini za matibabu.

Je, sasa Serikali ina mpango gani wa kutibu ugonjwa huu bure kwa wananchi ili waweze kupambana nao na usisambae katika nchi yetu?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe kuwa tarehe 24 Januari, 2020 Serikali imesaini makubaliano ya kuchukua asilimia 16 kutoka Barrick Gold Tanzania, kwa hiyo sasa hivi Serikali ina 16%, maana yake watu wengi hawajaisikia hiyo, kwa hiyo inabidi tuongeze sauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Gereza la Ulanga mwaka wa tano sasa hivi mahabusu wanapelekwa mahakamani kwa kutumia bodaboda. Hii ni hatari sana kwa mahabusu kutoroka. Naomba kuuliza swali la nyongeza, je, ni lini Serikali itapeleka gari la mahabusu Gereza la Ulanga? (Makofi/ Kicheko)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vitendo hivi vinasikitisha sana. Huwezi ukakuta ng’ombe dume anapanda ndama, huwezi ukakuta jogoo anapanda kifaranga lakini binadamu aliyepewa utashi anafanya vitu hivyo. Ukiangalia trend ya matukio yanaongezeka kwa kiasi kikubwa. Matukio 13,457 mwaka 2018 yameongezeka kwa 1,000 lakini ukienda Mahakamani hukuti hizi kesi. Je, Wizara ina mkakati gani kuhakikisha haya matukio yote inasimamia upatikanaji wa ushahidi na kuhakikisha yanakwenda Mahakamani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sehemu kubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinasababishwa na mila na desturi potofu. Kwa mfano, katika mila za Kihehe kuna utamaduni unaitwa Nyangusage, katika tamaduni za Kisukuma kuna mila inaitwa Chagulaga na Kigoma kuna Teleza. Wizara ina mkakati gani wa kutoa elimu kuhakikisha mila na tamaduni potofu zinatokomezwa?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niipongeze Serikali kwa dhati kabisa kwa juhudi zake za dhati za kuboresha utalii katika nchi yetu. Kama Mbunge, nimesikitishwa na kauli za baadhi ya Wabunge wa Upinzani kubeza juhudi za Serikali za kuboresha utalii na kuchochea kwa kutumia wasanii wa ndani. Niwaambie tu wasanii, Serikali ya Awamu ya Tano inatambua mchango wao mkubwa katika kuijenga nchi yetu. Kwa hiyo iwapuuze hao, hii ni tabia yao na ndivyo walivyo.

Mheshimiwa Spika, swali langu namba moja, maeneo au halmashauri nyingi ambazo zimezungukwa na National Park hawanufaiki na shughuli za utalii kwa kuwa hoteli zile zimejengwa ndani ya zile mbuga. Sasa je, Seriakli haioni sasa umefika wakati wa kuweka utaratibu wa kujenga hoteli zile za kitalii nje ya zile hifadhi ili wananchi wa maeneo yale waweze kunufaika kama kodi na vitu vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, swali namba mbili, tunafahamu nyamapori ni tamu sana. Mtalii anapoona akatamani na akala, itavutia watalii wengi sana kuja hasa wa ndani. Je, Serikali haioni sasa umefika wakati iweke utaratibu wa kuweka vigenge vya nyama choma ndani ya mbuga zile ili mtalii anapoona nyama ile anaitamani halafu anaila sio aone, atamani, aondoke. Ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kumekuwa na matumizi ya hovyo kabisa katika halmashauri zetu na kupelekea halmashauri hizo kupata hati chafu. Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga imepata hati chafu kwa mwaka mmoja, mimi najiona kama natembea bila nguo, lakini halmashauri kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, Halmashauri ya Ujiji ambayo inaongozwa na ACT anapotoka Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe, miaka minne mfululizo imepata hati chafu wakati yeye akishinda twitter na instagram. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifuta halmashauri hizi? (Kicheko)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ukatili mkubwa wa Wanyama unafanywa pindi Wanyama wanaposafirishwa, tumeshuhudia malori yakipita matani na matani yanatoa ng’ombe Karagwe Kanda ya Ziwa yanapeleka Dar es Salaama.

Mheshimiwa Spika, Sasa kwa nini Serikali isitoe agizo ijengwe Kiwanda huko, ng’ombe zichinjwe ndiyo wasafirishwe wapelekwe Dar es Salaam? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Swali la pili, ukatili mbaya kuliko wote ni upigaji chapa wa ng’ombe, tumeshuhudia ng’ombe wakiteswa kwa kupigwa chapa, Serikali imeshindwa kubuni mbinu nyingine tofauti na hiyo, Je, Serikali inatoa kauli gani na upigaji chapa wa hovyo kabisa na utesaji wa mifugo yetu. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante wananchi wangu wa Epanko tangu wafanyiwe tathimini ni miaka miwili mpaka sasa hivi hawajalipwa, na Mheshimiwa Waziri alishafika huko na anajua shida, sasa sheria inasema mtu akifanyiwa uthamini baada ya miezi sita anatakiwa alipwe na ikizidi hapo analipwa fidia na uthamini ukizidi miaka miwili unakuwa cancelled unafanywa upya, nataka kusikia kauli Serikali. Je, hawa wananchi waliofanyiwa uthamini wao lini watalipwa ni miaka miwili imeshapita?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kwa niaba ya wananchi wa Ulanga, naomba niishukuru Serikali ya CCM kwa kutupa kipaumbele kwenye Sekta ya Afya. Maana yake tumepata shilingi milioni 400, Kituo cha Afya cha Lupilo kimeisha na shilingi milioni 400 imeingia juzi.

(a) Hospitali hii ya Wilaya wakati inajengwa, mwaka 1905 wilaya ilikuwa na watu 23,000, leo hii wilaya ina watu zaidi ya 200,000: Serikali haioni kiasi hiki cha fedha, shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa hospitali hii ni kidogo sana?

(b) Hospitali yetu ya Wilaya ya Ulanga imekuwa na changamoto kubwa sana ya watumishi wachache na wasio na sifa: Je, lini Serikali italeta watumishi wa kutosha na wenye sifa?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ujenzi wa reli uendane sambamba na ujenzi wa barabara hasa kwa maeneo yenye misongamano mkubwa wa abiria na mizigo. Kwa mfano barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro, ile barabara ina hali mbaya sana, ina msongamano mkubwa wa magari na inatumia masaa matano hadi sita kwa basi la abiria. Serikali ilikuwa na mpango wa kujenga barabara (highway) barabara sita, kutoka Dar es Salaam mpaka Chalinze – Morogoro na sasa hivi imesitisha.

Sasa nataka kusikia kauli ya Serikali, je, lini itafufua tena mpango huu wa ujenzi wa hii barabara ili kuondoa kadhia hii?
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Uwepo wa kundi kubwa la watoto wazururaji kunasababishwa na wazazi kutofuata njia bora ya uzazi wa mpango. Njia bora kabisa ya uzazi wa mpango isiyo na madhara yoyote ni matumizi ya mipira ya kike na ya kiume.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa katika jamii yetu kumekuwa na tatizo kubwa la watu kutotumia mipira ya kike na ya kiume licha ya watengenezaji kuweka vionjo mbalimbali katika dhana hii kwa mfano strawberry, ndizi, chocolate na hivyo kusababisha siyo tu kuwa na watoto wa mitaani bali ongezeko kubwa la magonjwa ya zinaa na HIV. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu inayoendana na wakati ya watu kutumia mipira hii ya kiume ili kuondokana na changamoto hii ya watoto wa mitaani?

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Special Seats (CHADEMA)

Questions / Answers(35 / 0)

Supplementary Questions / Answers (46 / 0)

Contributions (42)

Profile

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Ruangwa (CCM)

Questions / Answers(0 / 1)

Contributions (11)

Profile

Hon. Seif Salim Seif

Mtambile (CUF)

Profile

View All MP's