Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Supplementary Questions
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la maji ni tatizo kubwa tuseme nchi nzima, lakini hata Karagwe tuna shida sana ya maji. Wakati wana-Karagwe wanasubiri mradi wa Rwakajunju, Serikali ina miradi ya Benki ya Dunia, lakini kote Jimboni hii miradi haijakamilika. Napenda kuiomba Serikali ieleze wananchi wa Karagwe hii miradi itakamilika lini?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, lakini kwa upande wa kahawa, Jimbo la Karagwe tunalima kahawa sana na zao la kahawa bado lina fursa kubwa sana kuwainua kiuchumi wakulima wa kahawa na uchumi wa nchi kwa ujumla lakini mikopo ya TIB imekuwa ni kidogo mno kwenda kwenye kukopesha walimaji wa kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yangu ni kama ifuatavyo: Kwa vile miche ya kahawa ni ya zamani sana, imepandwa toka enzi za wakoloni na mababu zetu, je, Benki ya Kilimo ina mpango gani wa kuwakopesha wakulima wa kahawa pesa ile waweze kununua miche wakiwemo vijana ambao wana tatizo la ajira na kama miche ikipatikana wanaweza wakajikita kwenye kilimo cha kahawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile kabla ya kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo, TIB ilikuwa ikitoa mikopo kwenye sekta ya kilimo kupitia Dirisha la Kilimo, kwa nini hii portfolio isitoke TIB ikaenda Benki ya Kilimo ili hii fedha shilingi bilioni 58.8 itumiwe na Benki ya Kilimo kukopesha wakulima wa Tanzania?
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Wananchi wa Karagwe tunamkumbuka Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa push-up za kihistoria alizozipiga pale Kayanga. Je, Serikali mnaonaje kama mkitusaidia kujenga uwanja wa Wilaya pale Kayanga ili tuweze kumuenzi Rais wetu kwa ule ukakamavu alioonyesha kwa vijana wa Karagwe? Nashukuru sana
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za Jimbo la Mkuranga zinafanana na changamoto za Jimbo la Karagwe. Naishukuru Serikali kwa kutuunganisha Jimbo la Karagwe na Jimbo la Kyerwa kwa kuweka mpango wa kujenga kwa lami barabara ya Mugakolongo kwenda Mulongo. Nipende kumuomba Mheshimiwa Waziri akisaidie Kijiji cha Rwambaizi, barabara imekwepa kijiji na kama mnavyojua barabara huchochea maendeleo. Nipende kumuomba Mheshimiwa Waziri, atusaidie barabara ya Mgakolongo kwenda Mulongo, ipite kwenye kijiji cha Rwambaizi, ili wananchi wangu wa hicho kijiji waweze kupata maendeleo yatakayokuja na ujenzi wa barabara hiyo la lami, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo. Kata za Igulwa, Kanoni, Kituntu, Ihanda na Chonyonyo, zina shida kubwa sana ya maji. Kutokana na shida hii, Serikali iliahidi kuchimba mabwawa katika hizi Kata ili kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya maji. Je, Serikali itachimba lini haya mabwawa?
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto za Morogoro Kusini zinafanana na Changamoto za Jimbo la Karagwe. Katika Hospitali ya DDH Nyakahanga tuna tatizo kubwa la upungufu wa madawa, vifaa tiba na Wauguzi.
Mheshimiwa Naibu Spka, swali langu ni je, Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo kaka yangu, anaweza kuambatana nami baada ya Bunge hili kwenda kusaidiana nami kutatua changamoto za Hospitali ya DDH ya Nyakahanga
pamoja na kuanza mchakato wa kujenga Hospitali ya Wilaya ukizingatia DDH ya Nyakahanga inahudumia Wilaya mbili; Karagwe na Kyerwa?
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa Serikali wa kuhamisha nyumba zilizokuwa chini ya Halmashauri kwenda Serikali Kuu umeacha watumishi katika Halmashauri ya Karagwe bila makazi, takribani kaya za Watumishi 60 hivi sasa hazina makazi kwa sababu Serikali Kuu imechukua nyumba ambazo zilikuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Je, Wizara haioni kwamba inabidi iwasaidie watumishi hawa kwa kuiomba NHC ishirikiane na
Halmashauri, Halmashauri tunaweza tukawapa eneo la kujenga nyumba nafuu kwa ajili ya watumishi hawa? Nashukuru
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Hata Wilaya ya Karagwe tuna vivutio vingi vya malikale likiwemo eneo ambalo Chief Rumanyika alikaa. Je, Wizara imeweka vivutio vya malikale hizi kwenye orodha ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja?
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayofanya. Nina swali kuhusu mradi wa Rwakajunju namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri awaambie akinamama wa Karagwe ni lini mradi wa Rwakajunju utatekelezwa ili kuwatua ndoo kichwani?
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kumekuwa na changamoto kubwa ya vijana ambao wanaajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi kuzungushwa pale wanapoenda kwenye Mifuko ya Pensheni kudai mafao yao ili waweze kuyatumia kama mitaji ya kujiajiri. Kwa mfano, kule Karagwe Kampuni ya Ujenzi ya Chico iliajiri vijana kwa utaratibu wa mikataba ya vibarua, mpaka hivi sasa wanazungushwa vijana hawa.
Je, Serikali inawasaidiaje vijana hawa kudai mafao
yao ili waweze kutumia hela hii kama mitaji ya kujiajiri?(Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mpango wa kupandisha watumishi madaraja wale wanaostahili lakini kuna changamoto ya wale watumishi ambao wanapandishwa madaraja mishahara huwa inachelewa ku-reflect lile daraja ambalo amepandishwa. Je, ni nini maelezo ya Serikali kuhusu suala hili?
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Pia katika Wilaya ya Karagwe kuna wahanga ambao wameathirika na wanyama waharibifu hasa tembo na viboko katika kata za Kihanga, Rugu, Nyakasimbi, Nyakabanga, Nyakakika na Bwelanyange, lakini pamoja na kushindwa kuwapa kifuta machozi wananchi hawa, pia vijiji katika hizi kata vinapakana na Pori la Akiba la Kimisi na Burigi na kuna asilimia ambayo inatakiwa kutoka kwenye mapato ya hifadhi kwenda kwenye vijiji ili kuwasaidia katika shughuli za maendeleo. Tumetuma madai katika Wizara kwa muda mrefu, lakini hatujawahi kupata hii fidia ili wananchi hawa nao wafaidike.
Je, ni lini Serikali itatoa kifuta machozi hicho pamoja na yale mapato? Ahsante.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kwenye taarifa ya habari ITV kulikuwa kuna kauli kwamba kuna uingizaji wa mbegu fake nchini. Kama kauli hii ina ukweli ni hatari sana kwani inamdhulumu mkulima ananunua mbegu akidhani ni mbegu yenye ubora lakini mbegu hii inakuwa ni feki matokeo yake anapanda havuni anachokitegemea.
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu kauli hii ambayo ilitoka ITV jana usiku kwenye taarifa ya habari? Nashukuru.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na kwamba wananchi wana haki ya kupata huduma ya watumishi, hasa walimu, wauguzi na watendaji wa vijiji na kata, pia jitihada nzuri ya Serikali inayoifanya ya kupeleka fedha za maendeleo vijijini inahitaji watumishi hawa waweze kusimamia miradi hii. Kwa upande wa Karagwe kuna shortage kubwa ya Walimu wasiopungua 850, kuna shortage kubwa ya wauguzi.
Je, nini tamko la Serikali, maana kila mwaka wa fedha Serikali inasema itapanga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuhakikisha tunakuwa na watumishi wa kutosha. Nini tamko la Serikali kuhusu hii shortage ya watumishi ya sasa hususan Wilaya ya Karagwe? Ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Changamoto za Jimbo la Bukene zinafanana na changamoto za Jimbo la Karagwe. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kuweka mpango wa kuweka lami barabara ya kuanzia Karagwe kwenda Benako - Ngara na barabara ya kuanzia Karagwe kwenda Murongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango hii mizuri ya Serikali wananchi wanaoishi katika barabara hizi wamesubiri fidia kwa muda mrefu, je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wa Karagwe wanaopakana na barabara ya Karagwe - Benako na Mugakorongo - Murongo? Ahsante.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kuna mgogoro kati ya Pori la Akiba la Kimisi na maeneo ya Rweizinga – Mguruka katika Kata ya Bwelanyange, mwaka jana Bunge liliielekeza Serikali iende katika hayo maeneo na kutatua migogoro hii, lakini mpaka hivi sasa Serikali haijafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua ni lini Mheshimiwa Waziri utaambatana na mimi ili tuende kwenye Kata ya Bwelanyange maeneo ya Rweizinga na Mguruka ili kushirikisha wananchi katika kuweka mipaka mipya kati ya pori la Akiba la Kimisi na Kata ya Bwelanyange? Nashukuru.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Karagwe tuna kituo cha ufundi stadi cha KVTC Kayanga. Serikali iliandaa mchoro wa kupanua hiki chuo kwa muda mrefu sasa miaka mingi. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kupanua hiki chuo cha KVTC Kayanga.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza, lakini kabla ya kuuliza maswali haya, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais na Serikali kwa utaratibu uliowekwa sasa wa kuhakikisha hakuna mwalimu anahama mpaka stahiki zake zinalipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo; naishukuru Serikali imeongeza annual increment kwa walimu lakini ni lini Serikali itawapandishia mishahara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa nini walimu wanachukua muda mrefu kupandishwa madaraja? Kuna walimu tangu mwaka 2012 mapaka hivi sasa walitakiwa wawe wamepandishwa zaidi ya mara tatu lakini mpaka sasa walimu hawa hawajapandishwa daraja hata mara moja. Je, ni nini majibu ya Serikali? Nashukuru. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, na pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana kaka yangu, Mheshimiwa Selemani Jafo na Dada Jenista Mhagama. Baada ya kufika Karagwe na kukuta wilaya ambayo ina watu takribani 360,000 ina Kituo cha Afya kimoja cha Serikali waliweka nguvu na Serikali sasa imetusaidia tumekamilisha hicho Kituo cha Afya cha Kayanga, nawashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, kwa vile Wilaya ya Karagwe ina Kituo cha Afya kimoja cha Serikali, na hivi sasa naishukuru TAMISEMI tunaenda kukamilisha Kituo cha Afya cha Nyakayanja, mnaonaje wakati mchakato wa kujenga Hospitali ya Wilaya unaendelea mtupe angalau vituo vya afya viwili ili ku-balance jiografia ya Karagwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa TAMISEMI na Wizara ya Afya wanafanya kazi nzuri, mnaonaje mkae na development partners kwa sababu Kamati ya Huduma za Jamii inaonesha kwamba kuna Wilaya 67 katika nchi yetu ambazo bado hazina Hospitali za Wilaya. Sasa kwa sababu Serikali inafanya kazi nzuri ya kutoa huduma mnaonaje mkae na development partners ili mtengeneze proposal ambayo itatusaidia kukamilisha ujenzi wa Hospitali 67 za Wilaya? Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuja na utaratibu mpya wa kutoa huduma hii kwa wananchi kupitia NSSF kwa kushirikiana na Azania Bank. Hii ni mara ya pili nauliza hili swali katika Bunge hili la Kumi na Moja kwa sababu ni jambo mahususi. Ili jamii yoyote iweze kutoka kwenye umasikini, lazima kuwe kuna kitu kinaitwa social safety net na huu mpango ulikuwa mzuri kwa sababu katika huduma hii wananchi wangenufaika na pensheni ya uzeeni, pensheni ya ulemavu, pensheni ya urithi, mafao ya uzazi, mafao ya mazishi, mafao ya matibabu na mikopo ya muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuiomba Serikali iwaambie wananchi wa Karagwe, je, tutegemee lini NSSF na Azania Bank watakuja Karagwe ili wale wananchi ambao walitoa ule mchango wa shilingi 20,000 wakasubiri huduma kwa muda mrefu, wategemee wataipata lini? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inaonaje kufanya pilot study kuanzia Karagwe na sehemu nyingine ili tuone namna ambayo tunaweza tukaleta social safety net along side, jitihada nzuri ya Serikali inayoendelea kutupeleka kwenye uchumi wa kati? Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyeki, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kirefu cha LUKU ni Lipia Umeme Kadri Utumiavyo. Kwenye ving’amuzi kwa nini Serikali isikae na watoa huduma ili mtumiaji alipie kadri anavyotumia badala ya kulipia kwa mwezi awe ametumia au hajatumia? Ahsante.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mimi nataka kujua kutoka Serikalini ni lini Walimu waliohamishwa kutoka shule za sekondari kwenda shule za msingi watalipwa stahiki zao. Kule Karagwe kuna walimu 131 mpaka hivi sasa wanasubiri stahiki zao. Serikali ilitoa shilingi milioni 52 na hela ambayo inayohitajika ni shilingi milioni 430. Sasa nataka kusikia kutoka Serikalini, walimu hawa mnawaambia nini? Ahsante sana.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwenye miji 17 ikiwemo Wilaya ya Karagwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwa vile Serikali imeshapata fedha ni lini Mradi wa Rwakajunju utaanza? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karagwe ina idadi ya watu wasiopungua 350,000 lakini tuna A Level moja tu ya Bugene Sekondari na haina maktaba hata moja, lakini pia ina upungufu wa madarasa yasiyopungua 17. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili yuko tayari kuambatana na mimi akajionee hali ilivyokuwa mbaya pale Bugene Sekondari? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za miundombinu katika hifadhi ya Serengeti zinafanana na changamoto za Hifadhi mpya ya Kimisi na Burigi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka miundombinu katika hifadhi mpya ya Kimisi na Burigi ili hifadhi hii iweze kuchangia mapato katika Halmashauri zetu za Wilaya zilizopo katika Mkoa wa Kagera pamoja na kuchangia pato la Taifa?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na mimi kwenda kwenye Kata za Bweranyange, Rugu, Nyakasimbi, Nyakabanga na Nyakakika ili kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji kwenye Kata hizi na Hifadhi? Ahsante sana.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Mheshimiwa Naibu Waziri anafanya kazi nzuri, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa butura ulikuwa unamsaidia sana mkulima wa kahawa Mkoa wa Kagera kupunguza ukali wa maisha wakati anasubiri kuvuna kahawa shambani. Je, Serikali imejipangaje kumsaidia huyu mkulima baada ya kuzuia uuzaji wa butura? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Special Seats (CCM)

Questions / Answers(29 / 0)

Supplementary Questions / Answers (40 / 0)

Contributions (54)

Profile

Hon. Aziza Sleyum Ally

Special Seats (CCM)

Profile

View All MP's