Parliament of Tanzania

Kamati mbili zawasilisha taarifa zake Bungeni

Kamati ya Kudumu Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imewasilisha taarifa yake Bungeni huku ikipendekeza kuchukuliwa kwa hatua kali kwa maduka binafsi ya dawa yanayokutwa na dawa za Serikali.


Akiwasilisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Peter Serukamba alisema Kamati imebaini kuwepo kwa wizi wa dawa ambazo zinakutwa kwenye maduka binafsi.


"Hali hii inawafanya wagonjwa wakienda hospitali wakose dawa na hivyo kuhatarisha maisha kwa wale wasio na uwezo,"alisema.


Aidha, alisema Kamati inapendekeza mipango iandaliwe ili kuwezesha mfumo wa ugawaji dawa uwe wa kielektroniki ili kupunguza malalamiko ya kuishiwa kwa dawa wakati dawa mbadala zipo.


Mhe. Serukamba alisema pia Kamati inaitaka Serikali kuhakikisha inaongeza bajeti katika Taasisi ya Saratani Ocean Road ili iweze kuwa na vifaa vingi na vya kisasa.


Mbali na mapendekezo hayo Kamati hiyo imetoa ushauri kwa Serikali katika masuala mbalimbali ili pamoja na mambo iweze kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.


Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi, Mhe.Dkt. Jasmine Tiisekwa akiwasilisha taarifa ya Kamati yake Bungeni ikiwemo elimi leo alisema Kamati yake inaishauri Serikali kuongeza Bajeti ya Jeshi la Polisi ili wanunue vitendea kazi vitakavyowasaidia kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya.


Kamati pia ilitaka kuimarishwa kwa Ulinzi hususan katika maeneo ya Bandari,viwanja vya ndege na mipaka ya nchi.


Aidha, kwa upande mwingine Mhe Tiiswekwa alisema kuwa kufuatia changamoto katika upatikanaji wa tiba za utengemao (Rehabilitation) wa warahibu (Addicts) za dawa za kulevya nchini ambapo kwa sasa zinapatikana katika mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar pekee Kamati imeishauri Serikali kwamba huduma hiyo ihuisihwe katika sera ya Afya ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hii nchi nzima.

“Kamati pia imeshauri Serikali iharakishe mapitio ya Sera ya Dawa za kulevya ya mwaka 2004 ili kunusuru Taifa na janga la dawa za kulevya,” alisema Mhe Tiiswekwa.

Aidha katika utendaji wake kwa kipindi hiki Mhe Tiiswekwa alisema Kamati pia ilibaini uwepo wa uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya Pombe za bei rahisi maruufu kama “viroba” na kuongezeka kwa tabia hatarishi zinazochangia ongezeko la Vijana katika matumizi ya Dawa za kulevya. Kutokana na hilo Kamati imeishauri Serikali kufungia kabisa uzalishaji na uuzwaji wa Pombe hizo ili kunusuru taifa.

Kwa upande mwingine Mhe Tiiswekwa alisema kuwa katika kufuatilia utekelezaji wa Majukumu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Kamati imebaini kuwa Tume hiyo inakabiliwa na ufinyu wa bajeti ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 90 ya Bajeti ya Tume inategemea fedha za Wafadhili wa nje hali inayopelekea kupunguza ufanisi wa Tume katika mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI.

“Kutokana na hilo Kamati imeishauri Serikali itoe kipaumbele katika mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kutenga bajeti ya kutosha kwa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania,” alieleza.

Katika hatua nyingingine Mhe Tiiswekwa alisema kuwa Kamati imebaini kuwa baadhi ya Asasi zisizo za Kiserikali zinazofanya kazi za Masuala ya UKIMWI kwa ufadhili wa watu wa nje, hutekeleza pia ajenda binafsi za wafadhili hao kama masharti ya ufadhili ambayo mara nyingi huenda kinyume na mila na destuti za Kitanzania. Kutokana na hilo Kamati imeishauri Serikali kuweka utaratibu maalum wa kufuatilia uendeshaji wa shughuli za Asasi zisizo za Kiserikali ili kuhakikisha kuwa zinafanya kazi kwa kuzingatia maadili, mila na desturi za kitanzania.


Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's