Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adimu ili na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua. Naona Serikali yetu imejipanga vizuri, imechagua vipaumbele ambavyo vitasukuma gurudumu la maendeleo la nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kitabu hiki cha Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ukurasa wa 31 namba (xi), kwa ruhusa yako, naomba nisome anasema; “Aidha shughuli za kiuchumi pia zimeongezeka; vilevile, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji Mto Rufiji - MW 2100.” Hili ni jambo hili ni zuri sana kwa sababu nishati ndiyo dereva mkubwa wa maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi sana vya nishati, naomba aangalie huko. Ukichukua chanzo cha joto ardhi katika Rift Valley, Kenya ina potential ya kuwa na MW 1000 mpaka 1500, Tanzania tuna potential ya kuwa na MW 5000 kwa joto ardhi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri badala ya kuangalia tu kwenye maji na sehemu nyingine, aangalie kwenye joto ardhi ili tuweze kuwa na nishati ya kutosha kuweza kuendesha viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja upande wa udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, ukurasa wa 42 ameandika pale kwa ruhusa yako nasoma; “Kuhakikisha thamani halisi ya fedha inazingatiwa katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi za ujenzi kwa kuzingatia misingi ya Kanuni za Ununuzi wa Umma kama Force Account.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndiyo pana mgogoro. Inaonekana kwenye unit ya uzalishaji tuna kawaida ya kumuangalia Mhasibu, Mkaguzi wa Hesabu (Auditor) na General Manager, hatumwangalii mnunuzi na hapa ndiyo kuna hasara kubwa sana. Hatumwangalii mnunuzi kwa kumpa mafunzo ya kutosha na hatumwangalii kwa makini hasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano, sasa hivi Serikali imeamua kutoa fedha za kujenga Vituo vya Afya, Serikali ikatumia ujanja mzuri sana wakawaambia Halmashauri fungueni account tofauti, twende kwenye manunuzi tofauti, wakafungua Force Account, fedha imetumika vizuri sana, ina maana kuna tatizo kwenye ununuzi. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali angalieni kada (profession) ya ununuzi muifundishe na kuiangalia vizuri ili tusipoteze fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye ukurasa wa 46 kuhusu ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji, kwa mfano, reli na nishati. Wazo la kujenga Standard Gauge Railway ni zuri sana, litasaidia kwenye bandari yetu na biashara na nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia kwenye kitabu hiki, Mheshimiwa Waziri amesema reli hii inatoka Dar es Salaam kwenda Tabora, Tabora kwenda Mwanza, Tabora kwenda Kigoma na Isaka kwenda Rwanda. Naona Mheshimiwa Waziri amesahau ya Uvinza kwenda Msongati. Naomba tuiangalie sana reli hiyo, kwa sababu nchini Burundi kuna madini mengi sana, kuna nicol, platinum ambapo reli hiyo italeta biashara kubwa sana Tanzania. Kwa hiyo, naomba kama Burundi haina fedha, basi Serikali i-invite Burundi, m-negotiate naye ili reli hii ya kutoka Uvinza kwenda Msongati na kwenda Bujumbura ijengwe sambamba na hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika ujenzi wa reli kwa kuitumia bandari yetu ya Dar es Salaam, reli ya TAZARA tusiisahau, haihitaji kujengwa upya, inahitaji kuboreshwa tu ili sasa tuitumie vizuri bandari yetu ya Dar es Salaam. Tunapoiboresha reli ya TAZARA kwa kuipa umeme na kadhalika, tuangalie bandari kavu ya Inyala pale Mkoani Mbeya ili kutoka pale sasa tuiite Malawi tujenge pamoja reli ya kutoka Inyala kwenda Ziwa Nyasa kwenda Malawi kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge mwenzangu wa Mbeya Vijijini jana alisema nchi za Msumbiji, Namibia na Angola zinaboresha bandari zao kwa kuziangalia nchi ambazo ziko land locked za Zambia, Congo na Zimbabwe na sisi tunaangalia huko huko.
Kwa hiyo, naomba tunapojenga reli ya Standard Gauge tuboreshe reli ya TAZARA ili tuwe na reli tatu. Tutakuwa na bahati kuwa na aina tatu ya reli, tuna Standard Gauge, Metre Gauge na Cape Gauge. Kwa hiyo, mzigo wowote ule tunaweza kuumudu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, tunaponunua engine na mabehewa ya Standard Gauge, tununue mabehewa na engine ambazo ni adjustable ambazo zinaweza zikatumika kwenye reli ya Standard Gauge na kwenye reli ya Metre Gauge ya TAZARA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa compliment hiyo. You have made my day na leo ni birthday yangu, nina miaka 66, ahsante sana. (Kicheko/Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoiboresha reli ya TAZARA na Reli ya Kati, naomba tuangalie vilevile uwanja wa ndege wa Songwe. Nimeona kuna sehemu nyingi kuna viwanja vya ndege, tuangalie uwanja wa ndege wa Songwe ambao uko kimkakati sana kwa nchi za Kusini na Mikoa yote ya Kusini. Uwanja ule umekamilika, ni mzuri, lakini bado tu uzio, taa za kuongezea ndege, kumalizia na jengo la abiria. Naomba Mheshimiwa Waziri aangalie uwanja huu tuukamilishe ili uweze kuleta value for money kwa biashara za Mikoa ya Kusini na nchi za jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna mtandao mkubwa wa barabara ambao uko kwenye kitabu hiki. Naomba tunapojenga barabara hizi ambazo ni driver kwa uchumi wetu, tuiangalie sana barabara ya mchepuko ya kutoka Inyala kwenda kuingia kwenye barabara Kuu ya Tanzania - Zambia pale Mbalizi. Sasa hivi kwa barabara hii inapopita Mkoani Mbeya kuna congestion kubwa sana, kwa hiyo, kuna kupoteza muda mrefu sana. Naomba tuiangalie barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini nakushukuru sana kwa kunipa compliment ambayo you have made my day, naunga mkono hoja.