Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbozi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba sasa na mimi niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la watumishi wa umma. Watumishi wa umma katika mpango huu naona kabisa kwamba wamesahaulika na kama si kipaumbele. Nimeangalia karibu kurasa nyingi sijaona mpango wa kuwaongeza watumishi wa umma mishahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo kwa kweli limetengeneza vidonda vikubwa sana mioyoni mwa watumishi wa umma katika Taifa letu. Watumishi wanalalamika tangu Serikali hii ya Awamu ya Tano iingie madarakani haijawahi kuwaza wala kufikiria kuwapandishia watumishi wa umma mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia kwa mfano kwenye kitabu hiki cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ukurasa wa 85 wanasema ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za sekondari na ujenzi wa mabweni.
Pia ukienda kwenye kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wanazungumzia ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya, nyumba takriban 306. Hata tukiwajengea maghorofa watumishi wa umma, kwa maana ya watumishi wa umma kwenye afya, idara ya elimu na kilimo, kama hawakuongezewa mishahara tutakuwa tunafanya kazi bure. Watumishi wengi wamekata tamaa, walimu wamekata tamaa na hali ni mbaya kwa sababu Serikali hii haijawahi hata mara moja kuwaongezea mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani inawezekana kuna tatizo aidha mmeshindwa kumshauri Rais afanye hivi au mnamuogopa. Sasa sijui, lakini kama mnamuogopa mtakuwa mmetenda dhambi sana kwa watumishi wa umma ambao tunawafanyisha kazi nzito lakini hali ni mbaya kuliko kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wapo watumishi waliostaafu wana miaka mingi hawajawahi kulipwa mafao yao lakini sioni kwenye mpango huu kama kuna jambo hilo ambalo limeeleza hawa watumishi wanalipwa lini. Watu wanastaafu na wengine wanafariki kwa sababu ya stress za maisha lakini mafao yao hawajalipwa. Nadhani sisi kama Taifa bila ya kujali itikadi za vyama vyetu kuna jambo sasa la kufikiria namna gani hawa watu wanaweza kulipwa ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni kuhusu mazao yote ya wakulima. Nimesoma kwenye hii hotuba ya Waziri amezungumza kwenye zile changamoto za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Bajeti wa mwaka 2017/2018, ukisoma changamoto namba sita, anasema changamoto ya masoko na bei ndogo za mazao kwa wakulima. Hii imeelezwa kama changamoto lakini nimekuja kuangalia nikadhani kwamba unapoeleza kama changamoto lazima utuambie kwamba sasa suluhisho la masoko itakuwa ni ipi ili wakulima wetu waweze kupatiwa bei nzuri ya mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo zao la kahawa hali ni mbaya bei ipo chini na mahindi hali ni mbaya. Wamezungumza baadhi ya Wabunge waliochangia humu ndani asubuhi, leo mkulima kwa mfano ukienda Mikoa ya Songwe, Mbeya, Ruvuma na Rukwa debe la mahindi linauzwa shilingi 2,500 na gunia moja linauzwa shilingi 15,000. Ili uweze kununua mfuko mmoja wa mbolea ya kupandia DAP ambao unauzwa shilingi 70,000 na ukisafirisha kutoka mjini kwenda kijijini kwenye mashamba ni shilingi 75,000, kwa hali kama hiyo unaona mkulima anauza bei ndogo mazao yake lakini wakati huo huo pembejeo zipo juu.
Sasa ndiyo hayo mambo ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango ulitakiwa utuambie namna gani mnaenda kushusha bei ya pembejeo kama mbolea lakini pia mnaenda kutafuta masoko ya mazao ya wakulima. Mazao yote nchi nzima, mahindi, kahawa, mbaazi ambayo ilikuwa shilingi 2,000 sasa hivi wanauza shilingi 80.
Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho ambalo ndiyo tulisema ni zao pekee lililokuwa limebaki angalau lilikuwa linatuingizia fedha za kigeni nyingi sana katika Taifa letu, leo korosho hali ni mbaya, wakulima wanalia na viongozi wanakuja na matamko wanasema kesho Serikali inaenda kununua korosho kama hazikununuliwa na wafanyabiashara. Sisi tunaomba mkanunue kweli kwa sababu mmeshaahidi kwa wananchi kwenda kununua. Soko huwezi ukatumia mabavu, soko lina principle zake siyo suala la kutumia mabavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba, kama alivyochangia ndugu yangu hapo, Mheshimiwa Kanyasu, leo asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania ni wakulima, mazao yote bei iko chini tafsiri yake ni kwamba hawa wakulima hata uwezo wa kununua bidhaa utakuwa ni mdogo sana na bidhaa zote zimepanda bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza hapa kuhusu vifaa vya ujenzi; saruji, bati, mafuta, hali ni mbaya, lakini mazao ndiyo kama hivyo hali imekuwa hivyo. Sasa hapa haitakiwi Wabunge walalamike halafu na Mheshimiwa Dkt. Mpango ambaye aliaminiwa na Rais na yeye analalamika kwenye hotuba yake ule ukurasa wa 35, analamika changamoto ya masoko, bei ndogo za mazao kwa wakulima, anatakiwa atuambie kwamba atafanya nini kutafuta masoko kwa wakulima, siyo suala la kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake kama Mheshimiwa Waziri analalamika anatakiwa apishe kiti hicho ampe mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi hiyo, mwenye uwezo wa kutafuta masoko ya wakulima. Kwa hiyo, nadhani hilo ndiyo jambo kubwa zaidi, atuambie kwamba utafanya nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa unalalamika kiongozi, Waziri, kwamba ni changamoto umeitaja, utuambie na way forward, utafanya nini kama changamoto ni soko, utatafutaje masoko sasa. Hapo hajatueleza vizuri, ameeleza changamoto page mbili lakini pale kwenye way forward, namna gani anakwenda kutatua hizo changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inapojirudia mara kwa mara maana yake imeshindwa kutatuliwa, ni malalamiko tayari hayo, kwa hiyo niseme tu kwamba hili ni vizuri akalipokea akaangalia namna ya kulifanyia kazi. Sisi kazi yetu kama Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali, ndiyo kazi yetu hiyo. Hayo masoko wakayatafute…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi natoa suggestion wakatafute masoko ya mazao ya wakulima, hiyo ndiyo solution ninayotoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nizungumzie kidogo suala la kuhusu hizi changamoto zilizoelezwa hapa. Nadhani kuna changamoto moja kubwa sana imesahaulika na hii changamoto Mheshimiwa Dkt. Mpango naomba akafanye utafiti na Serikali hii ya Awamu ya Tano ikafanye utafiti na hii changamoto isipofanyiwa kazi itaenda kulimaliza Taifa; hili suala la kufanya chaguzi za marudio, pesa nyingi tunapeleka kwenye chaguzi za marudio, sasa hii lazima tuitafutie ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mbunge alikuwa chama fulani anasema leo naamua kuhamia chama kingine na kuna mmoja nimemsikia asubuhi anazungumza anasema kwamba eti niliondoka huko sasa niko huru, niliondoka CHADEMA niko huru upande wa pili, lakini alizungumza kwamba mimi nimekimbia kwa sababu nilitaka nigombee Uenyekiti na Mbowe halafu nikaona Mbowe amekataa, sasa leo ameingia CCM, tuone kama atakwenda kugombea Uenyekiti na Rais Dkt. Magufuli, tuone, kama ninyi mnaruhusu namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunahitaji kwamba viongozi ukichaguliwa na wananchi umalize miaka yako mitano, hizi fedha za uchaguzi wa marudio ni fedha nyingi sana. Ni sehemu ya changamoto, angeiweka, kutumia fedha za Watanzania, fedha za wavuja jasho kwenda kwenye chaguzi za marudio, hizi fedha tungeweza kuwasaidia wakulima wetu, tungeweza kulipa mishahara kwa watumishi, tungeweza kufanya mazingira mazuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote kama mtu ulikuwa kwenye chama ambacho watu walikuamini na wakakuchagua kwenye chama hicho ukahamia Chama cha Mapinduzi, lazima hata uwezo wako wa kufikiri huweza kupungua, ndiyo unachokiona, ndiyo madhara yake hayo. Kuna sentensi moja ya Kizungu inasema an empty stomach is not a good advisor, kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba wakati mwingine tumbo likiwa wazi linaweza likakushauri vibaya, ngoja tuwaache tu mwisho wa siku…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.