Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia afya njema na kuweza kuendelea na shughuli zetu za Bunge kama kawaida. Pili, wakati wote sitaacha kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo langu la Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa maendeleo wa Taifa, naanza na viashiria vya uchumi kama vilivyoelezwa katika kitabu alichotusomea Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kwa mujibu wa takwimu ambazo tumezipata au Taarifa ya Fedha kupitia Shirika la Fedha Duniani (IMF) imezungumza kwamba uchumi wa dunia unakua kwa asilimia 3.9 na kwa upande wa Afrika Mashariki, Nchi yetu ya Tanzania na Rwanda ndizo zinazoongoza kwa uchumi wake kukua kwa asilimia 7.2 dhidi ya asilimia 7.1 ya mwaka uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua tu kwamba katika hili, mara nyingi wananchi wamekuwa wakituuliza sisi viongozi tunapopewa takwimu hizi za kukua kwa uchumi lakini mbona tukiangalia sisi wananchi hali kila siku inakuwa afadhali ya jana? Nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, pamoja na mipango mizuri aliyokuwa nayo ya kukua kwa uchumi lakini uchumi usikue kwenye makaratasi na makabrasha, uchumi ukue mpaka mifukoni kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu mfumuko wa bei kila siku unapanda. Kwa mfano, mwaka jana sukari kilo moja ilikuwa ni kati ya Sh.1,500 mpaka Sh.1,800 lakini sasa hivi mfumuko wa bei umependa ni Sh.2,600. Ukienda kwenye petroli kwa sisi watumiaji wa vyombo vya moto bei haishuki inaendelea kupaa. Jana bei imepanda tena kwa hapa Dodoma ni takribani Sh.2,445, bei inapanda. Sasa tunapoambiwa uchumi umekuwa hata sisi Wabunge inatushangaza. Naomba hii mipango ya Serikali ifike mpaka kwa wananchi nao waone kwamba kweli uchumi umekua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nalotaka kuzungumzia ni kuhusu hili sual la mikopo na madeni. Kwenye kitabu humu imeandikwa kwamba kuna mikopo tuliyoipata kutoka nje takribani shilingi trilioni 7.05. Kati ya hizo kuna deni la ndani na la nje, deni la nje ni takribani shilingi trilioni 1.35, lakini deni la ndani ni karibu trilioni 5.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe katika madeni haya, maneno yale tunayosema kwamba deni ni himilivu kwa kweli tunawadhuru na kuwafilisi wazabuni wanatoa huduma mbalimbali kwa Serikali. Kuna watu wanadai mpaka miaka mitano hawajalipwa, wamepeleka huduma mbalimbali katika sekta mbalimbali za Serikali. Naomba katika mipango yetu hii tuwalipe. Wengine wanapelekwa Mahakamani, wengine mali zao zinapigwa minada hali ya kuwa wameihudumia Serikali yetu. Kwa hiyo, naishauri Serikali iwalipe, kwanza asilimia kubwa ni maskini, wana-tender tu hizo za Serikali lakini wanafanya kazi katika mazingira magumu walipwe madeni yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo kwenye kitabu alichotusomewa Waziri hapa iko ukurasa wa 12. Nianze na ufuaji wa umeme wa maji (hydro-electric power). Tunashukuru Serikali juhudi inazofanya kila siku miradi kuja lakini miradi mingine inakuwa inaishia njiani. Huu mradi wa Stiegler’s Gorge, naishauri Serikali na kuiomba kwamba iwekeze fedha huu mradi ukamilike isije ikawa kama ule mradi wa gesi wa Mtwara ambao umeanza mpaka umefikia mwisho tunaambiwa watumiaji wa gesi ni asilimia 6 tena ambayo ni TANESCO peke yake hali ya kuwa gesi ni kitu kinachohitajika sana katika shughuli mbalimbali duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nishauri Serikali mradi wa Stiegler’s Gorge ufanikiwe kwa asilimia 100 ili hii Tanzania ya viwanda tunayoisema viwanda bila umeme haviwezi kwenda. Tunaanzisha reli ya Standard Gauge ambayo itakuwa ni treni inayotumia umeme kama umeme wetu utakuwa sio wa uhakika iko siku treni itakujaishia katikati ya mbuga ya wanyama ya Mikumi na hapo sasa abiria wajiandae kuliwa na simba. (Makofi)

Mheshimiwe Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali tunapoanzisha miradi tuihakikishe inakamilika kwa asilimia
100. Nashauri umeme uwe wa uhakika ili wawekezaji wa viwanda watakapokuja wasiwe na matatizo ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine katika huu umeme, bei ya umeme Tanzania ni kubwa kuliko nchi zote. Haya siyo maneno yangu hata Mheshimiwa Rais aliwahi kusema hivi na akaiomba TANESCO ipunguze bei ya umeme kusudi wananchi wetu waweze kutumia umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikupe mfano, Watanzania ndiyo tunaoongoza kwa matumizi ya kuni na mkaa chini ya Jangwa la Sahara. Unaposafiri kati ya mji mmoja kwenda mji mwingine ni Tanzania peke yake ndiyo utakuta pembeni kulia na kushoto mwa barabara kuna magunia ya mkaa na kuni. Tunataka tuondoe matumizi ya kuni na mkaa tutumie umeme na gesi ili tuweze kuokoa misitu yetu ambayo itatuletea mvua za uhakika na tuweze kupata umeme wa kutosha unaotokana na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la utalii. Kwenye utalii hapa naona kama tunafanya mchezo au tunafanya masihara kwa sababu haiingii akilini Tanzania tuna vivutio vingi sana vya utalii, tuna mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro, Mapango ya Amboni ya Tanga, Tongoni Ruins na mambo mengine ya kiutalii lakini hatutangazi, ndiyo tatizo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana hapa ilipitishwa bajeti ya shilingi bilioni 2 kama sikosei, mmoja wa Wabunge akatoa mfano Kenya wenzetu wanatumia shilingi bilioni 70 kwa matangazo. Ukiangalia hata matangazo katika ligi za Ulaya katika viwanja vya mipira wenzetu wengine wanatangaza lakini sisi Tanzania kuna tangazo moja ambalo lipo katika EPL, ligi ya Uingereza. Kwa nini tusitangaze katika Bundesliga ya Ujerumani, La Liga ya Spain na katika maeneo mengine ambayo yanakusanya watu wengi ili tukaweza kuingiza watalii wengi ambapo sekta ya utalii ni chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali yote duniani kama utasimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali tutangaze utalii wetu, tuna vyanzo vingi vya utalii lakini hatuvifanyii kazi.

Kuna mbuga pekee ya Saadan lakini haitangazwi kama inavyotakiwa kutangazwa. Nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama kweli tunataka mapato kwenye utalii tutumie fedha nyingi sana kwenye matangazo, matangazo ya biashara ndio yanayovutia wateja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye uvuvi bahari kuu. Kazi yetu kubwa kama Serikali ni kuanzisha operesheni na operesheni ile ilikuja mpaka ndani ya Bunge samaki wakaja wakapimwa kwa rula hapa canteen lakini tumeacha meli kubwa zinazovua katika bahari kuu. Wavuvi wadogo wadogo wa kwenye maziwa na bahari tunakamatana nao, nyavu zinakamatwa zinachomwa, nyumba za wavuvi zinachomwa moto na mashua zao zinachomwa moto na kupigwa mashoka, lakini tunaacha meli kubwa zinazovua katika bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano hai wa hili, miaka michache iliyopita palipatikana samaki wakawa wanaitwa samaki wa Magufuli. Sasa hebu fikiria ikiwa meli moja tu inaweza kuwa na tani 60,000 za samaki wakagaiwa magezani na taasisi mbalimbali za Serikali, je, meli zaidi ya 300 zinazovua sasa hivi tunavyozungumza kwenye bahari yetu na TRA hawachukui kodi hata shilingi moja tunapoteza kiasi gani? Kwa nini tuwakamate wavuvi wadogo hali ya kuwa kumbe bahari peke yake ni uchumi kama tutaisimamia vizuri itaweza kutuingizia mapato makubwa? (Makofi)

Mheshimiwe Mwenyekiti, kwenye Kamati yetu tumewahi kupata taarifa kwamba kuna shilingi bilioni 3 za feasibility study ambapo inatakiwa ikafanyike uchunguzi tu katika bahari kuu kuona tunawezaje kuwekeza kwenye bahari kuu tuweze kukusanya mapato. Kwa hiyo, naishauri Serikali kama tumeamua kufanya uvuvi katika bahari kuu tununue meli za uvuvi, ndege tulizonunua zimetosha sasa twende kwenye meli za uvuvi ili tuweze kukusanya mapato yanayotokana na bahari yetu. Japan, Singapore, Vietinum, Thaiwan na China ndiyo wanaonufaika na bahari yetu sisi wenyewe tunaenddelea kuwa maskini. Kwa hiyo, naishauri Serikali tununue meli za uvuvi tuanze kuvua katika bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulisema ni suala zima la bandari. Katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 50 -51 limezungumzwa suala la bandari na reli kwamba kutakuwa na ujenzi wa bandari ya Mwambani Tanga. Mimi naishauri Serikali bandari ile ya Mwambani ijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zitengwe ili tuweze kujenga bandari ile ambayo nayo itakuwa ni kichocheo cha uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho siisahau barabara ya Pangani. Barabara ya Pangani nayo itatuokoa kwanza kuokoa muda wa usafiri lakini pia wakazi wa Tanga watatumia muda mfupi sasa kutoka Tanga hadi Dar es Salaam kwa sababu barabara ya Pangani ni njia ya shortcut.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasema nashukuru.