Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Najua kabisa dakika zangu ni chache, nina mambo machache sana ya kushauri kwa ajili ya mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natambua kabisa kwamba enzi za Mwalimu Nyerere alipotoa ile kauli mbiu ya Kilimo ni Uti wa Mgongo, alimaanisha kwamba binadamu huwezi kutembea bila uti wa mgongo na ukawa hai. Kwa maana hiyo kama tunafahamu kabisa kwamba kilimo ni uti wa mgongo, ningemshauri Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango yafuatayo na inatokana na kile ambacho nakiona kwenye kilimo kwa wakati huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mwalimu Nyerere aliposema Kilimo ni Uti wa Mgongo, alihakikisha katika maeneo mbalimbali anawasaidia wananchi kulima kisasa. Kwa mfano, natoka Pwani, alihakikisha Bonde la Ruvu linatoa mpunga wa kulisha karibu Dar es Salaam nzima na Tanzania kwa ujumla. Leo hii ukipita Kibaha ukafika Ruvu, utakuta lile bonde limegeuzwa kuwa viwanja vya kujenga nyumba. Nataka kujua hivi tumeshabadilisha lile shamba la Ruvu kuwa la ujenzi? Wakati Waziri ana windup atujulishe basi kama lile bonde ambalo tulikuwa tunapata mpunga na tunanunua chakula kwa bei nafuu kama limebadilishiwa matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye viwanda nimeona Pwani tunaongoza kwa viwanda, lakini kinachonishangaza pale Kibaha kuna matrekta, wananchi wa Tanzania ili tuweze kuondokana na kilimo cha jembe, tulitarajia kwamba Serikali itakuja na mpango angalau wa kuanzisha hata SACCOS wakopeshwe yale matrekta waweze kulima kilimo cha kisasa ili tuendane na ule mpango wa Rais wa Awamu ya Kwanza wa kauli ya mbiu ya kusema kwamba kilimo ni uti wa mgongo. Matrekta yale yanaoza pale Kibaha hayajulikani yatapaki kwa muda gani na wananchi wanalima kwa jembe la mkono na ni wa Kibaha pale pale. Hakuna maelezo yale matrekta yametengenezwa halafu yanaenda wapi, mwaka juzi yalikuwepo pale pale, mwaka jana yako pale pale lakini tuna Tanzania ya viwanda. Sasa ukianza kujiuliza nini maana ya Tanzania ya viwanda, kama ni Tanzania ya viwanda…
T A A R I F A . . .
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sikubaliani na hiyo taarifa kwa sababu mimi nimesema hivi, sasa hivi ni Tanzania ya viwanda na kile Kiwanda cha pale Kibaha hakijaanza enzi hizo za Wabunge walipokopa, yale matrekta yametengenezwa siku za karibuni, tunahitaji yatumike ili uti wa mgongo uwe ni kilimo. Hatuwezi kuwa na vijana ambao hawana kazi, Bonde la Ruvu limechukuliwa linajengwa nyumba, matrekta ambayo tulitarajia yagawiwe kwa wananchi yamepaki pale, halafu tuseme kuna Tanzania ya viwanda na kwamba tutawakwamua wananchi kwenye umaskini? Hicho ndicho nilichokuwa nakizungumzia.
T A A R I F A . . .
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kukubali ile taarifa, mimi naongelea mpango ambao una mambo mengi, kwake kwenyewe hata maji hamna, sasa tunataka mwananchi ajikwamue ili hizi rasilimali nyingine ziende mahali kwingine zikafanye kazi. Kwa hiyo, mtani wangu siwezi kumkubalia hilo. Mimi nilikuwa naelezea kwamba tuko vizuri katika kupanga mipango lakini katika kutekeleza lazima tuchukue hatua za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naongelea kuhusu PPP. Nafahamu kabisa kama tungetumia PPP ina maana tungeweza kubakiza akiba ya pesa tukafanya mambo mengine kulikoni kila kitu kufanya sisi kama Serikali. Tunachukulia mfano kwamba mpaka sasa hivi haijajulikana kama reli na Stiegler’s Gorge vinajengwa kwa pesa za ndani au kwa mkopo? Hata tunapoulizwa na wanachi tunashindwa kujibu kwa sababu, mara tuambiwe inajengwa kwa mkopo, mara tuambiwe inajengwa kwa pesa za ndani, kipi ni kipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda Mheshimiwa Dkt. Mpango ukija ku-windup utuambie kabisa hii miradi ya kimkakati inafanywa kwa pesa za ndani au kwa pesa za mkopo au kwa pesa za ndani pamoja na pesa za mkopo? Hilo tutaelewa ili tuweze kuwaelimisha wananchi kwamba jamani tunafanya hili kwa pesa za mkopo na kwa hili tunafanya kwa pesa za ndani. Hii itasaidia suala hili kueleweka kuliko kufanya propaganda kwamba tuna hela nyingi sana wakati wananchi wanaishi kwa shida, tuna hela nyingi sana wakati tungeweza kufanya kwa PPP tukaokoa hela.