Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niipongeze Kamati hii ya PAC ikiongozwa na Mama Kaboyoka kwa kadri ambavyo ilijikita kuchambua Taarifa Maalum za Ukaguzi. Maana kitabu hiki chote kina Taarifa Maalum za Ukaguzi. Kwa hiyo, naipongeza sana Kamati hii kwa sababu imefanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke wazi jambo hili kwamba watu wengi walihitaji kuingia kwenye Bunge, zaidi ya watu 5,000 tuliokuwa tunagombea nao kwenye Majimbo, lakini Mwenyezi Mungu aliweka kibali cha Waheshimiwa Wabunge 393 tu kuingia ndani ya Bunge hili. Kwa hiyo, sisi ni wateule yale ambayo tunapaswa kuyafanya kwa niaba ya wananchi lazima tuzingatie haki na ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie hapo hapo ambapo wengi wanataka kujua na wananchi wanataka kujua kwamba kwa nini trilioni 1.5 ilileta kizaa zaa kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Wengi hapa wanapotosha ukweli na umma unapotoshwa lakini kwa sababu sisi Kamati ya PAC ni Kamati makini na ina maadili ilisubiri ripoti halisi ambayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ameipitia akaileta kwetu. Kamati hii siyo ya twitter au instagram kwa hiyo tunataka tueleze kwa umma yale yaliyoonekana kwa CAG. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki wa CAG na bahati nzuri wanaopotosha tulikuwa nao ndani wakati Mheshimiwa Maida anauliza kwa CAG kwamba hebu tupe ufafanuzi wa shilingi trilioni 1.5 wapotoshaji tulikuwa nao ndani. Kwa mujibu wa Hansard Mkaguzi alisema hakuna hata shilingi iliyoliwa baada ya kufanya uhakiki, kwa hiyo, haya mambo ni ya upotoshaji. Ni vizuri tukajikita kueleza umma dosari na yale ambayo tunaweza kuishauri Serikali ili iweze kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, uhakika ni kwamba shilingi trilioni moja haijaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najiuliza sana, hivi nyakati hizi kwa Mheshimiwa Magufuli unaweza ukala shilingi trilioni moja kweli? Nilikuwa nashangaa, hivi hawamjui vizuri Mheshimiwa John, inaweza ikawa hawamjui Mheshimiwa John, lakini nataka kuwahakikishia kwamba sasa mali za Watanzania, miradi ya Watanzania inadhibitiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, misingi ya haki ilikuwa imeharibika na maandiko Matakatifu yanasema, misingi ya haki ikiharibika mwenye haki afanyeje? Kwa hiyo, yaweza kuwa wapotoshaji zamani walikuwa wenye haki lakini misingi ilipoharibika na wao waliharibika. Nataka kukuhakikishia kwamba misingi ya haki sasa inapangwa vizuri, inajegwa vizuri na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli kwa hiyo mambo yatakwenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye kifungu cha 3.1 ambacho kinahusu NSSF. Tumethibitishiwa na Ukaguzi Maalum, Kamati imepitia kwa kina tumeuona ubadhirifu mkubwa ulikuwa ukifanywa na NSSF kwa kununua viwanja ambavyo havina tija vingine hata tu kuhamisha umiliki kutoka kwa yule aliyenunuliwa haijafanyika na viwanja vingine vimevamiwa. Kamati yetu imependekeza vizuri sana na mimi nataka kuongezea uzito tu na haya yote yalifanywa na wanaopotosha wengine walikuwa viongozi kwenye Kamati hizo leo wanakuja wanageuka. Naomba sasa nipendekeze mambo ili Serikali ya Awamu ya Tano iweze kuchukua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, NSSF kama Serikali haitaunda Kamati Maalum ya kuchunguza na kuchukua hatua stahiki tutatia hasara mashirika haya ambayo tumeyaunganisha kwa sasa. Kwa hiyo, tuombe Serikali…
T A A R I F A
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga taarifa.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hii. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Taarifa.
TAARIFA
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei taarifa hiyo….
WABUNGE FULANI: Aaaaaa. (Kicheko)
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Kwa sababau aliyekuwa anaongea alikuwa mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba uovu na uozo uliofanywa na taasisi hii siyo wa kuvumiliwa. Kwa sababu inaonesha wazi kwamba kilikuwa ni kama kichaka cha upigaji...
MBUNGE FULANI: Kweli.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima iundwe Kamati itakayoweza kushughulikia watu hawa. Hawa watu wakipatikana wakusanywe wote wapelekwe huko kizuizini ili kuleta heshima ya nchi. Watanzania wanategemea Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii inapoendesha shughuli zake ilete faida ili impact ile iweze kuwasaidia wanachama wake lakini ilionekana kwamba ni kama kikundi ambacho kinaunda, miradi yote haijafanyiwa upembuzi yakinifu, miradi yote imebuniwa na watu wachache sana. Kwa hiyo, niombe sana jambo hili kwa kweli Serikali isilifumbie macho kwa sababu CAG ametuletea na sisi Kamati tumetoa mapendekezo yetu hapa. Tunaomba iundwe Kamati kwa haraka sana ili kuipa nguvu Kamati kwa yale ambayo imeyapendekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo Shirika letu la Maendeleo (NDC) liliingia uwekezaji na Kampuni ya IETL na kuunda kampuni ya TANCOAL. Ukaguzi huu Maalum umebaini mapungufu mengi sana hasa ya kimkataba. Mikataba ambayo iliingiwa ni mibovu na haiwezi kuisaidia Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, unaingia mkataba ardhi na madini uliyonayo hayakuingizwa kwenye mtaji. Kwa hiyo, ardhi na madini hayo yamekwenda bure, share yetu ni fedha taslimu bila kuanzia kwanza ardhi tuliyonayo, hii ni mikataba mibovu sana. Kama ambavyo tumeeleza kwenye taarifa yetu ya Kamati lazima tuhakikishe kwamba ndani ya miezi sita tuna review ili mkataba mmoja baada ya mkataba mwingine irekebishwe ili kuleta faida kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imekiukwa mikataba mingi sana. Kwa mfano, Kamati tumebaini kuna fedha nyingi zilikuwa zikilipwa bila kufuata mkataba jambo ambalo kwa kweli limeisababishia hasara Serikali. Kampuni hii haijawahi hata siku kuipa faida Serikali kwa kulipa gawio, kwa hiyo, kila siku inapata hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini NDC kama wabia tumegundua kwenye Menejimenti kuna udhaifu mkubwa sana, kwa hiyo, Menejimenti ni ya upande ule mwingine na Bodi ya Wakurugenzi ipo inaangalia bila kuyaangalia haya makandokando ambayo yanaitia hasara Serikali. Kwa hiyo, pamoja na mambo hayo tuangalie kama kuna mapungufu kwenye Shirika letu la Maendeleo kwa maana ya Menejimenti ibadilishwe na wachukuliwe hatua za kutosha. Kwa sababu huwezi kuwa na Shirika la Maendeleo ambalo haliangalii mbele. Tunaingia uwekezaji ambao hauleti faida kwa nchi, haiwezekani. Kwa kweli hatuwezi kukubaliana na kuendelea na jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana yale ambayo Kamati imeyabaini, yale ambayo tumeyapendekeza kwa Serikali, Serikali ichukue hatua mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)