Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa sababu muda nitazungumzia masuala mawili tu na yote yanahusu mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza linahusu masuala ya kinidhamu ya Majaji. Tarehe 30 Novemba, 2014, Bunge hili lilipitisha Azimio kwamba Rais aunde Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza Majaji wa ESCROW. Majaji wawili ambao kwa ripoti maalum ya uchunguzi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge hili iliwakuta wamechukua mamilioni ya fedha kutoka kwa yule bwana wa ESCROW James Rugemalira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Majaji wawili Aloysius Mujulizi na Profesa Eudes Ruhangisa. Bunge lilipitisha Azimio, baadae Mheshimiwa Rais Kikwete alipozungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, tarehe12 Disemba mwaka huo alisema kwamba, suala la nidhamu ya uchunguzi wa Majaji hao linapelekwa kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama lianzie huko, halafu baadaye ndiyo liletwe kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapema mwaka jana na baadaye mwishoni mwa mwaka jana Mheshimiwa Jaji Mkuu aliviambia vyombo vya habari kwamba uchunguzi wa Majaji hawa wawili ulikuwa umeisha kamilika! Leo ni mwaka mmoja na nusu, tangu Azimio la Bunge, kuhusu Majaji wa ESCROW pamoja na wengine litolewe, taarifa iko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tafadhali Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujumuisha, utuambie Majaji waliochukua shilingi milioni mia nne, mia nne kutoka kwa Rugemalira na Bunge hili likapitisha Azimio kwamba washughulikiwe kwa mujibu wa Katiba, kitu gani kinatokea na huu ukimya ni wa nini?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la nidhamu ya Majaji ni suala muhimu sana, mahakama zetu zimechafuka, tunapenda kulalamika Mahakimu, Mahakimu, Mahakama zetu katika ngazi zote zimechafuka! Kitu cha ajabu kabisa ni kwamba tumekuwa tunachukua hatua dhidi ya Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo once in a long while, Majaji hawaguswi! Hatuna malaika wala watakatifu katika Mahakama Kuu, hatuna malaika wala watakatifu katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania, kitu cha ajabu ni kwamba mara ya mwisho na hii ni muhimu, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania amechukuliwa hatua ilikuwa mwaka 1991, Mheshimiwa Jaji Mwakibete alipoundiwa Tume ya Uchunguzi akaondolewa madarakani. Miaka zaidi ya 25 Mahakama ni rushwa tupu na kila mtu analalamika hapa! Lakini ikifika kuchukua hatua, kila mtu anaogopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa hili ambalo liko wazi kabisa la waliokutwa wamechukua mamilioni ushahidi wa nyaraka upo, tuambiwe imekuwaje? Tusinyamaziwe tafadhali, mahakama zetu kama tunakubali kwamba kutumbua majipu ya muda mrefu ni kitu muhimu, haya ya wazi haya, tusiyaache hilo la kwanza.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha pili ambacho kinasemwa sana ni hiki kinachoitwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi. Mara nyingi ninapoona watu ambao wanaonekana onekana kama wana akili hivi, kama wamesoma hivi, kama wanajua sheria hivi, halafu wanazungumza vitu vya ajabu kabisa, nakuwa nafedheheka sana.
Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa na Mahakama ya Mafisadi tangu mwaka 1984; kwa miaka 32 leo tuna Mahakama ya Mafisadi. Sasa haiitwi jina hilo inaitwa kwa kiswahili maarufu inaitwa Mahakama ya Wahujumu Uchumi. Ilianzishwa wakati wa crackdown ya Sokoine wa wahujumu uchumi na walanguzi. Mahakama Kuu inaposikiliza kesi zote za rushwa, Mahakama Kuu inaposikiliza kesi zote za kutakatisha fedha haramu, Mahakama Kuu inaposikiliza kesi zote za hujuma ya uchumi, makosa kwa mfano yanayohusiana na Sheria za Wanyamapori, Sheria za Dawa za Kulevya and so on and so forth, inakaa kama Mahakama ya Mafisadi, imeanzishwa kwa mujibu wa sheria. Sasa unashangaa watu wanaoonekana kama wanafahamu wanazungumza, tunampongeza Mheshimiwa Rais sana, ameamua kutuanzishia Mahakama ya Mafisadi nonsense!
Mheshimiwa Naibu Spika, nani aliyewaambia hakuna Mahakama ya Mafisadi? Kama mnataka kuibatiza tu semeni, halafu ukiuliza eehe! huo Muswada uko wapi? Aah tutaianzisha tu kama Division ya Mahakama Kuu, nonsense! Division ya Mahakama Kuu inahitaji Sheria, kuna Division ya Mahakama Kuu ya Ardhi, imeundwa kwa sheria. Division ya Mahakama Kuu ya Ajira Kazi, imeundwa kwa Sheria, Division ya Mahakama Kuu ya Biashara, imeundwa kwa sheria, hii Division ya Mahakama Kuu ya Mafisadi, sheria yake iko wapi? Hii ambayo mnasema mtaianzisha sijui mwezi Julai!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mambo haya, ambayo tunaambiwa tuna wataalam wa sheria wanaofahamu fahamu, why are they allowing these nonsense to go on. Kwa nini watu wenye utaalam wa sheria, madaktari hapa na wengine maprofesa, kwa nini wanaacha ujinga huu unaendelea kusambaa? Nafahamu na kwa sababu nimeshughulikia haya masuala kwa miaka mitano Bunge lililopita, kwamba kuna matatizo makubwa kuhusiana na uendeshaji wa kesi za ufisadi, nayafahamu, lakini kusema kwamba hakuna mahakama ya kuyashughulikia ni kuthibitisha ujinga tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunataka kupigana sawa sawa na tatizo la ufisadi, tuzungumze kuna tatizo gani katika Mahakama ya Economic and Organized Crimes Court iliyoanzishwa na Marehemu Sokoine mwaka 1984. Tusijifanye tunatengeneza mambo, hakuna kitu kipya hapa, Mahakama hii ipo for the past 32 years, ina matatizo yes, tuyazungumze hayo matatizo. Lakini tusizungumze as if hakuna kitu, tunaanzishiwa kitu kipya na Rais John Pombe Magufuli. Akizungumza Rais, namsamehe siyo mwanasheria, akizungumza Daktari wa Sheria nafedheheka sana kwa sababu anajua kama hajui anapaswa kujua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa vile muda hakuna, hivi umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu ni miaka mingapi? Hivi huyu Jaji Mkuu wa kwetu hajafikisha huo umri wa kustaafu? Wenzake wote aliokuwa nao darasa moja, Jaji Msofe, Jaji Masati, Dkt. Steven Bwana, walishastaafu miaka mingi, Jaji Mkuu wetu umri wake wa kustaafu ni lini? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.