Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia. Kwanza naomba niwapongeze Wenyeviti wote wawili kwa taarifa zao nzuri, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyojitabisha kwa ajili ya Watanzania, anafanya kazi usiku na mchana ili kuwaletea maendeleo Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusu reli ya SGR, reli hii inakwenda sambamba na viwanda pamoja na kilimo, vitu vyote vinashabihiana. Naomba kushauri wakati tunaendelea na ujenzi wa reli, tuweze kulima mazao ya biashara lakini niishukuru Serikali kwa jinsi ilivyokuja na mpango wa kilimo wa mchikichi. Katika Mkoa wa Kigoma tukiwekeza katika kilimo cha mchikichi na huku reli ikiwa inajengwa, wakati reli ya SGR inakamilika, mazao yale ya mchikichi yatakuwa tayari yanaanza kustawi na kuvunwa na kupelekwa sokoni. Kwa hiyo, kupitia reli hiyo tutaweza kusafirisha mawese kupeleka katika viwanda. Hivyo, naipongeza Serikali kwa kwenda sambamba na mambo ya ujenzi wa miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niishukuru Serikali kwa kutoa pesa kwa ajili ya kujenga barabara kutoka Kankoko – Kibondo – Kasulu - Buhigwe naipongeza sana Serikali kwa kuweza kuliona hilo. Naomba wakati barabara hiyo imejengwa iweze kujengwa border post kwa ajili ya kusafirisha mizigo inayotoka Burundi kuja Tanzania ili waweze kufanya biashara kwa kushirikiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma umepakana na nchi jirani ya Kongo pamoja na Burundi na sisi Kigoma tunalima mahindi, maharage, mpunga pamoja na mihogo. Kwa hiyo border katika Mkoa wa Kigoma kwa maana ya Wilaya zote nne zimepakana na nchi jirani; ukienda Kakonko imepakana na Burundi, ukija Buhigwe imepakana na Burundi, lakini ukija Kigoma Vijijini nayo imepakana na nchi ya DRC. Kwa hiyo tunaomba boader iweze kujengwa ili wananchi wa pande zote mbili, wananchi wa Tanzania pamoja na wananchi wa kutoka Burundi na Kongo waweze kufanya biashara kwa kushirikiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri, reli ya SGR iweze kuanzia Kigoma kabla ya kwenda Kigali kwa sababu mizigo mingi inatokea Burundi na Kongo na inapitia Kigoma. Kwa hiyo, naomba kabla ya kwenda kujenga Kigali, ianzie Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo linawasumbua sana wananchi wa Mkoa wa Kigoma. Mara nyingi watu wa Uhamiaji wamekuwa wakiwasumbua wafanyabiashara kwa kuweka vikwazo mbalimbali kwamba siyo Watanzania kitu ambacho kinawakatisha tamaa wananchi wakati mwingine wanashindwa kufanya biashara kwa uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba watu wa Uhamiaji waliangalie suala hili wasiwazuie wananchi kufanya biashara ila wawaelimishe waweze kujua ni jinsi gani wale watu ambao wapo mipakani wanaweza kufanya biashara kwa kushirikiana na nchi jirani. Tukiendelea kuwasumbua wananchi ambao wanatokea mipakani tutaendelea kupoteza mapato. Serikali haitaingiza mapato kwa sababu wananchi hawatatumia border watatumia vichochoro kwa ajili ya kuingiza biashara zao sokoni. Kwa hiyo, tutakuwa tumepoteza mapato kwa sababu ya kusumbuliwa na watu wa Uhamiaji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)