Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Nianze kwa kunukuu kifungu cha Biblia kinasema, nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao humo. Sehemu nyingine Biblia inasema Mungu ndiye anayetawala katika falme za wanadamu na yeye huamua kumpa mtu awaye yote amtakaye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge mwaka 2015 ulifanyika Uchaguzi Mkuu na kulikuwa na miamba miwili iliyokuwa inamenyana; alikuwepo Mheshimiwa Magufuli na Mheshimiwa Lowassa. Mimi nilikuwa Upinzani wakati huo; kwa kweli niwaambie Mheshimiwa Lowassa alipata umaarufu mkubwa sana hususani kwa wafugaji kwamba kwa kuwa yeye ni Mmasai anatokea Umasaini kwa wafugaji angekamata nchi hii wafugaji wangepata neema sana, lilimpa umaarufu mkubwa sana na hata huko nakotoka wafugaji walimwanini sana.
Mheshimiwa Spika, nataka niwambie kama kuna jambo ambalo Mheshimiwa Rais Magufuli amelifanya la kihistoria katika nchi hii ni jambo la kukubali kupitia upya GN ili wafugaji na wakulima wapate maeneo kwa ajili ya kulisha mifugo yao. Kwa wale ambao si wafugaji hawawezi kujua kwa sisi tunaotokea maeneo ya ufugaji, tunafahamu taabu ambayo wafugaji wanaipata katika nchi hii. (Makofi)
T A A R I F A
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naipokea taarifa hiyo, nilikuwa sijui, ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati nikiwa pale ng’ambo mwaka 2018, nilitoa shilingi kwa ajili ya kusimamisha zoezi la kuweka vigingi kwenye vijiji vilivyozunguka hifadhi mbalimbali ikiwemo hifadhi ya Serengeti. Wakati ule zoezi lilikuwa likiendelea kule Tarime kwenye vijiji vya kando kando ya hifadhi vikiwemo Vijiji vya Serengeti, Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Visarara, Bonchugu, Pakinyigoti, Miseke na kadhalika. Kama kuna wananchi wamefurahi baada ya tamko la Rais, ni Wananchi ambao wanazunguka maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, ukikumbuka, Hifadhi za Serengeti na hifadhi nyingine zilianzishwa kwa mujibu wa Sheria na GN na kilichokuwa kinatokea katika maeneo haya, walikuwa wanapanua mipaka na kwa kweli kulikuwa na confusion kati ya TAMISEMI na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwamba mipaka inawekwa kwenye vijiji, wananchi wanyang’anywa maeneo yao. Kwa kweli wananchi wamefarijika sana. Kwa hiyo, nina kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa hiki alichokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaambie, Tanzania tumepata neema ya kuwa na Rais ambaye pengine akiondoka madarakani ndio Watanzania watakuja wakumbuke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaambie, wakati nikiwa ng’ambo ile, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli alikuwa anatunyima usingizi kweli kweli. Ndiyo ukweli! Kwa sababu kule ng’ambo tulikuwa tumezoea ufisadi. Yaani ikitokea issue ya ufisadi, tunapiga kelele kweli kweli. Sasa jamaa amekuja amekaba hakuna cha ufisadi tena; na amekaba kweli kweli. Ukijulikana umefanya ufisadi anatumbua, hana mswalie Mtume, hata wao wanajua. Kwa hiyo, niwaambie tumepata Rais…
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Taarifa.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, wakati mwingine niseme ni maombi ya Watanzania, wewe ni shahidi.
T A A R I F A
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa yake, ni kweli, si tulikuwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba unilindie muda wangu. Kwa hiyo, ukweli ni hivi, 2010 Watanzania walikuwa wanaomba, yaani unajua inatakiwa tupate Rais wa kufanya maamuzi magumu.
Mheshimiwa Spika, unakumbuka ilifikia sehemu, sisi ambao tulikuwa huko duniani hatujaja humu, wananchi walikuwa wanasema, yaani tunatakiwa tupate Rais kichaa ili hii nchi inyooke. Nchi sasa hivi imenyooka. Nchi imenyooka Mura, wewe vipi? (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ngoja niwaambie, hivi kwa mfano, nani angeweza kuanzisha Bwawa kwenye Stiegler’s Gorge? Tuseme ukweli, nani? Yaani nchi za Ulaya hazitaki, Marekani haitaki, sijui nani hataki, nani? Huyu jamaa ana maamuzi magumu, tumuunge mkono. Umeme wa Stiegler’s Gorge ni kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Tutapata umeme kwa cheap price, wewe hutaki hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unajua wanasiasa wengi wanapenda kitu kinaitwa cheap politics. Mheshimiwa Dkt. Magufuli hapendi cheap politics anafanya hard politics. Hakuna ambaye angeweza kujenga reli, hakuna ambaye angenunua ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unajua wanasiasa wengi, hususan wa ng’ambo ile wangependa wajenge madarasa, vitu vidogo vidogo tu, lakini mambo mazito yenye kulinufaisha Taifa kwa miaka mingi, hakuna ambaye angethubutu kufanya. Kwa hiyo, ukiona tumehamia upande huu, tumeona mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ile hoja yako ya miaka saba, ile tumpe Magufuli hata miaka saba aendelee. Hivi…
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wanaoafiki!
WABUNGE FULANI: Ndiyoooooo.
SPIKA: Hapana, hiyo futa kwenye Hansard. Endelea Mheshimiwa. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naona wamekaa kimya, wanaelewa ndiyo ukweli.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nilitka niongelee ni jambo la cultural tourism. Cultural tourism kwa maeneo ya Serengeti inakuwa affected na single entry. Naomba kupendekeza kupitia Kamati ya Maliasili na Utalii, ongezeni jambo la single entry, is a big challenge kwa watu wetu. Watalii wanaishia hifadhini. Watalii wanatakiwa wakifika hifadhini, waende kutembea kwenye vijiji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)