Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Temeke
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishukuru kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia kidogo katika bajeti ya Wizara hii ya Katiba na Sheria kwa niaba ya wananchi wa Temeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nioneshe masikitiko yangu makubwa kwa Bunge lenyewe kwa sababu Bunge limeunda Kamati na miongoni mwa Kamati ambazo limeziunda limeunda Kamati ya Sheria Ndogo. Kwa uelewa wa kawaida, Kamati ya Sheria Ndogo ilikuwa iwe Kamati pacha ya Katiba na Sheria. Kwa hiyo, ilikuwa tutegemee hapa wakati Kamati ya Katiba na Sheria inawasilisha pia kungekuwa na wasilisho kutoka Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu Kamati ya Sheria na Katiba imejikita katika sheria mama ambapo utekelezaji wa hizi sheria mama upo chini ya sheria ndogo ndogo ambazo ziko nyingi na hizo ndizo zinazowagusa Watanzania. Kwa kukosa nafasi ya kuzisemea sheria ndogo hizo katika Bunge hili si jambo zuri. Mwishoni unajiuliza hivi hii Kamati ya Sheria Ndogo yenyewe ikasemee wapi maana Kamati zote zimekuwa connected na Wizara na zinapata nafasi ya kuwasilisha hapa isipokuwa Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumza kwamba tunataka tutengeneze Taifa la kijani kwamba mwanamama Mtanzania aache kutumia mkaa atumie gesi unazungumzia sheria ndogo ndogo zitakazosimamia uagizaji wa gesi hiyo ili ipatikane kwa bei nafuu. Usipopata nafasi ya kuzisemea hapa unakwenda kuzisemea wapi ili uhakikishe kwamba hilo Taifa la kijani linakuja? Unaposema kwamba gharama ya ndege hapa nchini imekuwa kubwa unazungumzia uagizaji mbovu wa mafuta ya ndege ambapo waagizaji wanajiwekea bei zao wenyewe. Hapo unahitaji sheria ndogo kwa ajili ya kusimamia haya ili Mtanzania aweze kusafiri hapa ndani ya nchi kwa tiketi za bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Land Registration Act inampa mamlaka Waziri kuweka kanuni na sheria ndogo ndogo za kusimamia vibali vya makazi. Katika hili, pale Dar es Salaam pana changamoto sana na hasa jimboni kwangu. Vile vibali vya makazi vimeainisha kwamba watu wanaokaa mita 60 kutoka kwenye reli ya TAZARA hawastahili kupewa hivyo vibali vya makazi. Hapa wanasimamia Sheria Ndogo ya mwaka 1995 inayoongeza eneo la kuachwa wazi kutoka kwenye reli lakini hao watu ambao wananyimwa vibali hivyo wamekuwepo hapo kabla ya sheria hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wakazi pale kwenye Kata za Mtoni, Azimio, Tandika, Kilakala, Yombo Vituka na Sandali ambao toka mwaka 2002 nyumba zao zimewekwa alama ya ―X‖ na watu wa TAZARA wakisimamia hiyo sheria ya mwaka 1995 inayowataka wahame bila kulipwa wakati watu hao walikuwepo pale kwa muda mrefu. Tunapoacha kuzijadili hizi sheria ndogo tunawaacha Watanzania walio wengi kwenye matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri mkalitazama hili kwa kushirikiana na Wizara hii ili tuone haya mambo tunakwenda kuyashughulikia kwa namna gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipekee kabisa nimpongeze sana Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa namna ambavyo amewasilisha hotuba yake yenye mashiko, iliyojaa facts na imedhihirisha kama kweli imewasilishwa na Wakili msomi. Suala la watu wanaipokeaje, hilo si jukumu lake, yeye amewasilisha na ni ukweli utaendelea kubaki kuwa ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na hili suala mnaliita kiporo, suala la Katiba Mpya. Mchakato huu wa Katiba Mpya wakati unaanza kwanza harakati zake hazikuwa za muda mfupi, zilianza muda mrefu na hazikufanywa tu na wanasiasa zilifanywa na taasisi mbalimbali. Baadaye Serikali ya Awamu ya Nne iliona kwamba kweli kuna umuhimu wa kupata Katiba Mpya kwa sababu jambo hili mnakuwa mnatafuta muafaka wa kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato ulianza vizuri lakini ulikuja kuharibika kwenye Bunge la Katiba. Hatua za awali za ukusanyaji wa maoni zilikuwa ni nzuri kweli kweli lakini ilipofika kwenye Bunge la Katiba mchakato ule uliharibikia pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Taifa hili na Serikali hii ya Awamu ya Tano inatamani kuendeleza muafaka huo wa kitaifa kwamba hili Taifa lipate Katiba Mpya, ni vizuri mchakato huo ukarejewa kuanzia pale kwenye Bunge la Katiba na Mheshimiwa Rais ana mamlaka hayo. Kwa mujibu wa kifungu cha 28(2) cha Sheria Na. 83 ya 2011 maarufu kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inampa mamlaka hayo Mheshimiwa Rais kuweza kuliita tena Bunge la Katiba na kujadili mapendekezo yaliyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba. Kama kweli wote nia yetu ni moja tunakwama wapi? Ndugu zangu wana CCM jambo hili litawajenga ninyi. Mnapoanzisha mchakato, mkausimamia na ukafika mwisho mnajitengenezea heshima ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo likiishia kati mnawapa wasiwasi sana Watanzania. Jana tumepitisha hapa bajeti ya Wizara ya Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alisema anataka kulitoa jembe la mkono na kuliweka makumbusho, watu wanahoji, mmeshindwa kulitoa jembe la mkono kwenye bendera ya Chama cha Mapinduzi unawezaje kulitoa shambani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nia ni hiyo, watu waliofanya marketing wanajua, kile kinachopepea kwenye bendera kinapeleka ujumbe mzuri sana kwa wananchi. Kumbe tungeanza kwenye bendera ya Chama cha Mapinduzi kuondoa nyundo na jembe la mkono tukaweka computer na trekta ili kuonyesha kwamba kile tunachokihubiri ndicho tunachokisimamia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ishauri Serikali hii iuanzishe mchakato wa Katiba Mpya kuanzia kwenye Bunge la Katiba. Kuupeleka mbio mbio kweli tutafanikisha tutaileta Katiba lakini itakuwa si Katiba ambayo wananchi walikuwa wakiitarajia na hili haliwezi kutusaidia, tutakuwa tukiendelea kuimba Katiba Mpya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni huu mrundikano wa kesi. Mrundikano wa kesi mahakamani umekuwa ni mkubwa sana na work load kwa Majaji na Mahakimu ni mkubwa. Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa kwamba ni kesi 200 kwa Jaji, huo si mzigo mdogo, huo ni mzigo mkubwa sana. Inafika mahali labda shahidi hajatokea siku moja Jaji anakuambia mimi nina kesi nyingi msinisumbue, mimi ninaendelea tu. Sasa haya mambo ya kutafuta haki za watu huwezi kuyapeleka namna hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri tuone katika bajeti hii kwamba kuna vifungu vya kutosha kuweza kuongeza Majaji na Mahakimu ili kesi hizi ziweze kuisha. Kusema tu kwamba tunahitaji twende kwenye zero case bila kuwa na Mahakimu na Majaji wa kutosha maana yake utakwenda kulazimisha Majaji na Mahakimu waliopo wazimalize hizo kesi kwa namna yoyote ile na justice haitaki namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni uchakavu wa majengo. Majengo ya mahakama yanatia aibu kweli kweli. Kibaya zaidi nature ya hao wanaofanya kazi kwenye hayo majengo mabovu ni kuwa watu nadhifu. Tunawafedhehesha sana kuwarundika Majaji na Mahakimu kwenye vijumba vya hovyo, vyenye joto la ajabu na kwa unadhifu wao wamevaa tai na suti kubwa, kwa nini tunawatesa watu hawa?
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Wizara hii ikajipanga, iombe fedha ya kutosha kuhakikisha kwamba wanawatengenezea Majaji na Mahakimu majengo yenye heshima ya kuwa ofisi.