Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji wa Hadhi ya Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika ili kuwa Hifadhi za Taifa. Nianze pia kwa kuwapongeza sana ndugu zetu wa TANAPA chini ya Kijaji ambao wanafanya kazi moja nzuri sana. Nawapongeza pia kwa kuwa na mahusiano mazuri na majirani zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao wamezungumzia habari ya migogoro pengine inaweza ikaongezeka kwa sababu watu wengine walikuwa wanapata kipato katika maeneo yale. Naomba niwatoe hofu kwanza katika zoezi hili zima ambalo litakwenda kufanyika baada ya Azimio kupita maana yake elimu itakuwa ni endelevu katika maeneo yale inavyofanyika kwa wananchi wengine wanaokaa jirani na Mapori ya Akiba. Wananchi wale huwa wanapewa elimu ya kuwa walinzi wa maeneo yale na kuelezwa faida watakazozipata kutokana na ule Mfuko wa Ujirani Mwema ambao wenzetu wa TANAPA wanawasaidia.

Mheshimiwa Spika, mbali na kuimarisha uhifadhi pia, watakuwa na zoezi hilo lingine la kuona kwamba, wanajivunia nchi yao kwa kuwa na rasilimali ambazo zinaongeza kipato, lakini pia katika suala zima la kuvutia watalii wanapokuwa wanakuja katika maeneo yale, wananchi walioko kule watakuwa na fursa pia, za kuweza kufanya mambo mengine, ikiwa ni pamoja na kuwa na bidhaa za kiutamaduni ambazo itakuwa ni manufaa kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba, tumekuwa na zoezi ambalo limekuwepo chini ya TANAPA wamelifadhili katika kupanga mpango wa matumizi ya ardhi katika maeneo yanayozunguka mapori. Nina imani na nina uhakika katika hili ambalo linakwenda kufanyika sasa watu wale pia, watapata huduma hiyo ya kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye yale maeneo, watapata fursa zote kama ambavyo wanapata wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ile hofu ya migogoro naomba tuiondoe kwa sababu, pia Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba, migogoro yote katika maeneo ya hifadhi, migogoro yote kwa wale wanaopakana na hifadhi inaondolewa. Kubwa ni kutoa elimu, pia kuwafanya wale wananchi wajitambue kwamba, zile ni rasilimali zao na ni sehemu ya ulinzi katika maeneo yale. Kwa hiyo, hayo wakiyajua yatakuwa hayana shida yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, napenda niseme jambo lingine katika wale watu wanaokaa katika maeneo yale, usalama utaongezeka. Tumekuwa wote tunajua unakwenda maeneo unasindikizwa na Polisi na uko ndani ya nchi yako. Usalama wa maeneo yale ulikuwa ni mdogo sana. Kwa hiyo, kwa kuyafanya kuwa hifadhi usalama utaimarishwa, lakini pia wananchi wenyewe watajiona wako salama ndani ya nchi yao. Ni maeneo ambayo kidogo yalikuwa na changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri nimefanya kazi Kagera na nilikuwa Muleba na Pori la Burigi linapakana katika maeneo hayo, kwa hiyo, maeneo yale hata ukienda kikazi ilikuwa unatakiwa uende na askari. Sasa unakwenda na askari mchana kwenye eneo lako, kwa hiyo, nina imani ulinzi utakwenda kuimarika. Kwa hiyo, tuwatoe hofu wananchi hasa wale waliokuwa wanafaidika na mapori haya. Nia ya Serikali na dhamira ni njema sana ni kuwawezesha pia wao kiuchumi katika kufungua fursa zingine ambazo zitawafanya wao pia waweze kufaidika na rasilimali iliyoko katika nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)