Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nami kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hizi tatu; kwa maana ya Mambo ya Ndani, Ulinzi na Usalama, pamoja na Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kikao chake alichofanya tarehe 22 pale Dar es Salaam, kuitisha wachimbaji wadogo na kusikiliza kero zao. Ni jambo zuri na kwa kweli wachimbaji wote Tanzania nzima wamempongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri na Naibu Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na Wizara ya Mambo ya Ndani. Ukurasa wa 11, Kamati imezungumzia kuhusu migogoro mbalimbali baina ya wananchi pamoja na Jeshi la Polisi na Magereza. Naomba nizungumzie kuhusu suala la migogoro ya wananchi pamoja Magereza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Ilagala tunalo Gereza, lakini ni miaka mingi sana wananchi wa Ilagala wamekuwa wakipiga kelele kwamba Gereza limehodhi maeneo yao na Ofisi ya DC pamoja na Mkurugenzi waliunda Kamati na ikabaini kwamba ni kweli Gereza lilihodhi maeneo ya wananchi bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua nia njema ya Serikali na Wizara kwamba wanahitaji Magereza wawe na maeneo kwa ajili ya kulima kutosheleza chakula cha wafungwa; lakini kwa kuwa Magereza wamechukua karibu ekari 10,000 na kitu, tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa, awaambie wananchi wa Ilagala: Je, wameamua ni ekari ngapi zitarejeshwa kwa wananchi ili na wananchi wapate maeneo ya kulima?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, nitajikita sana kwenye suala la madini. Nimeona hapa Sekta ya Madini inachangia asilimia 4.8 tu kwenye Pato la Taifa. Hii ilinishawishi niingie kwenye mtandao kuangalia kwenye East Africa nchi nyingine zinafanyaje especially kwa wachimbaji wadogo? Nikaangalia kwa mfano, wenzetu Kenya wanazungumzia tu kwenye Kijiji cha Usiri. Kijiji hiki ile revenue per year kwenye local economy tu, kinaingiza Dola za Kimarekani 1.9 million.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha hivyo, Migori District, kwenye madini ya dhahabu tu; nataka tu kutoa mfano, madini ya dhahabu tu, Migori wanaingiza 37 Million USD per year. Ukienda Rwanda ambayo ni nchi ndogo sana, unaona kwamba wachimbaji ambao wamewa-formalized pamoja wanaingiza 39.5 million per year, lakini wanakwambia kwa mwaka mzima kusafirisha madini nje kwenye nchi ya Rwanda ni sawasawa na asilimia 20 inaingiza mapato ya Serikali ya Rwanda kwa maana ya hii foreign exchange. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka nizungumzie suala la madini. Tuliwasikia wachimbaji wakati wanaongea na Rais, walimwomba Mheshimiwa Rais Wizara ya Madini isijikite tu kwenye masuala ya dhahabu, tanzanite na gemstones, wajikite vilevile kwenye industry minerals kama vile gypsum, chokaa na madini mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi, kwa sababu gani? Wachimbaji hawa wanaochimba madini ya ujenzi, Serikali kupitia Wizara ya Madini wangeweza kuwaangalia vizuri, kuwasimamia ili wajiunge wawe na utaratibu mzuri, Serikali ingepata mapato mengi sana kwenye madini ya ujenzi, tofauti kama wanavyong’ang’ania dhahabu na madini mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia hivyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hata ile withholding tax ile 5%, mimi nipo kwenye Kamati ya Bajeti, tuliomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kuitoa ile kuishusha iende mpaka 3%. Naona Kamati kwenye ukurasa wa 32 nao wamependekeza hivyo hivyo, withholding tax itoke 5% iende mpaka 3%.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Mheshimiwa Rais wakati anaongea na wachimbaji alionesha kwamba anaridhia na alitoa tamko kwamba Wizara ya Fedha na Wizara ya Madini ikae chini na ione namna gani ya kupunguza hii withholding tax pamoja na tozo nyingine mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, madini ya chokaa yana namna mbili; tuna namna ile kwamba madini yameshakuwa processed kwa maana ya ile lime powder ambayo unaweza ukauza hapa hapa nchini, lakini tuna ile limestones ambayo tunasafirisha nje. Sasa ukienda ukurasa wa 33, mimi naungana kabisa na Kamati kwamba Wizara itoe vibali vya kusafirisha madini nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema madini yasitoke nje, madini yanatofautiana. Tanzanite sawa utai- process hapa utaipeleka nje lakini limestone tunasafirisha. Mimi ni mdau, tunasafirisha ikiwa imepondwapondwa kama kokoto, tunapeleka kwa tons tunazisafirisha nje kwa maana ya Kongo, Burundi, Rwanda na nchi nyingine. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hebu haya mapendekezo ya ukurasa wa 33 tunaomba ayafanyie kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wachimbaji wadogo wanachajiwa ekari moja Sh.80,000/=. Ni mchimbaji gani anaweza? Unakuta mchimbaji ana-own ekari 30, anatakiwa alipie Sh.80,000/= kwa ekari. Naona Kamati nayo imetoa mapendekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la NEMC, wachimbaji wadogo wanatakiwa walipe shilingi milioni moja na nusu, wachimbaji wakubwa ndiyo shilingi milioni 4.5. Sasa namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atoe tamko zuri ili tuweze kuelewa Serikali yetu na kama Rais wetu alivyo na nia njema katika kuhakikisha hii Sekta ya Madini inakua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia NEMC; wachimbaji wa chokaa wao wanachoma kwa kutumia kuni, sasa hivi wanajipanga kuchukua makaa ya mawe ambayo wanayatoa Mpanda. Wananunua tani moja shilingi 145,000 na kule Mpanda hawaruhusiwi kununua tani moja mpaka waanzie tani tano. Kwa hiyo, unakuta shilingi 145,000 mara hiyo tani tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema hivi, wachimbaji wa chokaa mfuko mmoja wa chokaa ambayo imeshakuwa processed wanailipa Halmashauri shilingi 500 kwa mfuko. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, hilo aliangalie. Wanailipa Wizara ya Madini, kwa maana ya Ofisi ile ya Madini shilingi 150.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wanaomba angalau hiyo shilingi 500 kwa mfuko iteremke mpaka kwenye shilingi 250 ili waweze kukidhi na angalau Serikali muweze kupata mapato zaidi kuliko kuweka kiwango kikubwa ambacho mnawasababishia watafute njia za panya kutorosha chokaa zao badala ya kuilipa Serikali na Serikali iweze kupata mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naishukuru sana Serikali, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwajali wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzania. (Makofi)