Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye kamati hizi kwa mwaka huu. Kabla sijaanza kuzungumza, juzi kuna propaganda imesemwa hapa na tunajua Bunge hili ni chombo cha wananchi na lina heshima kubwa. Sasa kama propaganda inaweza ikaja mpaka humu na ikaacha kujibiwa matokeo yake inaweza kuaminika na ikaleta uchafuzi. Ni bahati mbaya sana kwamba propaganda hiyo ilizungumzwa na kiongozi mwenyewe wa mhimili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Tarime hatujawahi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Heche subiri kidogo. Hayo maneno yalizungumzwa humu ndani na Kikanuni kama Mheshimiwa Mbunge ana shida na kilichozungumzwa na Kiti hapa, utaratibu uko kwenye Kanuni ya 5. Kwa hivyo, Mheshimiwa Heche endelea na mchango wako, usizungumzie yale ambayo Kiti kilisema kwa sababu Kanuni zetu zimeweka utaratibu. Kama kuna jambo lilizungumzwa na Kiti hapa Mbunge hakuridhika nalo Kanuni ya 5 inatoa maelekezo ya nini cha kufanya. Kwa hiyo naomba ujielekeze kwenye mchango wako na sio yale ambayo yalizungumzwa na Mheshimiwa Spika.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unilindie muda wangu huo mkubwa uliouchukua. Nazungumza kwa sababu tuko kwenye Kamati ya Nishati. Cha kwanza kama Mbunge wa Tarime nataka kusema hatujawahi kupewa pesa yoyote bure na mgodi, haijawahi kutokea. Pesa ambazo Halmashauri ya Tarime inapewa au iliyokusanya ni pesa zinazoitwa service levy. Service levy ipo kwa mujibu wa sheria; na kwa miaka mitatu tukizijumlisha ndiyo tumepata bilioni 9.3. (Makofi)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Heche kuna taarifa, ukae upokee taarifa hiyo. Mheshimiwa Dkt. Mollel.
T A A R I F A
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba fundisheni watu kuwa maana ya Wabunge wa Chama Tawala, mjiheshimu kama mnaoongoza nchi ili tujadiliane mambo ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pesa tulizopokea ni pesa za service levy ambazo ni kodi; na kodi ya service levy ina sheria yake ya matumizi. Sheria inasema unapokuwa umepokea pesa hizo 60 percent inakwenda kwenye development, 40 percent inakwenda kwenye uendeshaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tumepeta hizo pesa tukasema hatuwezi kupeleka 60 percent, tukapeleka development 80 percent, tofauti na wengine wote. Nataka nikutajie miradi michache tuliyofanya ili mjue Tarime ni Wilaya. Pesa za vijana na walemavu tumepeleka shilingi 1,219,000,000, TARURA tumepeleka milioni 700, madarasa kwenye vijiji… (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Kuna Taarifa Mheshimiwa Heche, Mheshimiwa Getere.
T A A R I F A
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, sijui kama ni kuhusu utaratibu au ni taarifa? Mimi nasema maendeleo tuliyoyafanya; madawati Tarime tumetengeneza 12,500 hakuna mtoto anakaa chini. Vituo vya afya tumetengeneza saba kwa miaka mitatu, vingine hamjaleta Madaktari, zahanati 24. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme kwa kifupi tu na mengine mengi. Kwa kumalizia CAG ametoa hati safi mara tatu mfululizo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inayoongozwa na CHADEMA, Tarime chini ya Mbunge Heche. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kwenye REA. Serikali ya CCM walisema wao ni Serikali ya wanyonge na kwenye wanyonge tulisema tuwapelekee maji na umeme. Kwenye maji wammeshindwa kwa sababu, Mheshimiwa Silinde alitoa hapa takwimu, sasa mimi nakuja kwenye umeme. REA Awamu ya Tatu iliyoanza mwaka 2017/2018, 2018/2019 tulipanga kupeleka umeme kwenye vijiji 3,559, leo tunavyozungumza vijiji vilivyopelekewa umeme ni 322 chini ya asilimia 90. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipanga kuunganishia wananchi laki moja na themanini…
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Heche kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Subira Mgalu.
MHE. JOHN W. HECHE: Tulieni dawa iingie.
T A A R I F A
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, anachangia. Kwanza grid extension au densification anaijua ambayo wao wanasema mabeberu, walikuwa wanawatukana mabeberu, yote grid extension inafadhiliwa na Norway ambao ni mabeberu anayoizungumza yeye pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulilenga kuunganishia umeme wananchi 180,766, waliounganishiwa hivi tunavyozungumza ni wananchi 7,300 peke yake chini ya asilimia tatu. Hizi pesa mfadhili wake ni nani? Financer wa pesa za REA na ninyi wote ni Wabunge, kama mnataka kurudi humu lazima muwe wakweli. Financer wa pesa za REA ni wananchi wenyewe wanaonunua mafuta, wanaonunua umeme na hizi pesa zilikuwa ring fenced. Sasa nataka watwambie, Mheshimiwa Waziri atwambie hapa, je, hizi pesa ndio wamechukua wakaenda kununua watu au wakaenda kujenga miradi mingine ambayo haikukusudiwa kufanyika? Kwa sababu, pesa za REA ziko ring fenced na zinaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo kama tumewaunganishia wananchi umeme asilimia 3.8 peke yake; na Mheshimiwa Waziri namsikitikia, kwa sababu ukihesabu vijiji, kuna vijiji tumeenda, mimi ni Mjumbe wa Kamati, umeme umepelekwa kijijini lakini umepita kwenye nyumba nne tu kijijini, nyumba nne peke yake; halafu wanahesabu tu vijiji, wanakimbia wanahesabu vijiji. Sasa kama leo ni miaka miwili ya REA Phase III wameunganisha vijiji 322 kati ya 3,500, wanafaa kuendelea kuongoza nchi hii? Wanafaa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye Stieglers Gorge. Kwanza kuna watu wanaimba humu Stieglers Gorge! Stieglers Gorge! Wamekuwa kama makasuku. Stieglers Gorge Gorge kupata umeme wake ni mwaka 2027…
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. JOHN W. HECHE: …kwa sababu, kuna wengine wanafikiri utawaka kesho umeme wa Stieglers Gorge.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Heche kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ally Keissy.
T A A R I F A
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niondoe, wanaimba vyovyote wanavyoimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme wa Stiegler’s ni bilioni 700; hivi tunavyozungumza pesa ambazo zimekwenda ni bilioni 26…
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. JOHN W. HECHE: …sasa kama umeme huu kujenga hili bwawa ni trilioni 7.1, trilioni 7.1 kwa bilioni 700 tunahitaji miaka 10 kujenga…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Heche kuna taarifa nyingine. Mheshimiwa Dokta Mollel.
T A A R I F A
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, unafanya, una-allow Kikao cha Bunge kiwe soko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi Stiegler’s Gorge pesa zilizotengwa ni 700 billion, pesa zilizokwenda ni bilioni 27. Kampuni iliyopewa tenda ya Arab Contractors ni kampuni inayohusika kujenga nyumba, haijawahi kujenga bwawa popote duniani, haijawahi. Kampuni hii imetafuta mtu wa kum-subcontract inayetaka kumpa 80 percent ya mradi, watu wanakataa wanaiambia nipe kazi yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii nchi ni ya kwetu…
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
MHE. JOHN W. HECHE: …na sisi tunasema...
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna source nyingi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Heche kuna Kanuni inavunjwa. Mheshimiwa Subira Mgalu, Kanuni inayovunjwa?
MBUNGE FULANI: Aitaje.
KUHUSU UTARATIBU
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie; na ilifaa utafute Hansard uone nilichosema. Kampuni ya Arab contractors, haina uzoefu wa kujenga mabwawa, nimesema hivyo. Nimerudia kusema na sitatoa neno langu, inatafuta ma-subcontractors wa kuingia kujenga bwawa. Ndicho nilichosema.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Angellah Kairuki, naomba ukae kwanza tumalize hili la utaratibu. Mheshimiwa Heche.
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI: Anadanganya.
MHE. JOHN WEGESA HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, siondoi neno langu hata moja.
MBUNGE FULANI: Iletwe Hansard.
NAIBU SPIKA: Naomba ukae.
Waheshimiwa Wabunge, nimetoa maelezo marefu, sikusudii kuyarudia. Kwa mujibu wa Kanuni ya 63 na hiyo Kanuni ya 64 Mheshimiwa Subira Mgalu nitakutaka utuletee mkataba. (Makofi/Vigelegele)
Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane. Mheshimiwa Heche, wakati huo naye atatuthibitishia, tukishapata huo uthibitisho kwamba nani anasema uongo? Kwa sababu hiyo, mchango unaohusu Stiegler’s Gorge na mjenzi aliyepata hiyo kazi kuhusu asilimia anazoweza kufanya kazi na uwezo wake wa kufanya kazi, mjadala huo hautaendelea mpaka hili jambo litakapokwisha. (Makofi)
Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Heche ataendelea na mchango wake ukiondoa hilo jambo la utendaji kazi wa mjenzi wa Stiegler’s Gorge na uwezo wake wa kazi. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisaidie Taifa kwa mambo mengine. Bomba la gesi ambalo tulikopa na tukajengea, mpaka sasa hivi utilization ni seven percent peke yake. Mtwara, alikuwa anazungumza hapa Mbunge wa Mtwara, tuna uwezo wa kupata umeme wa megawatt 300, Ruhunji tuna uwezo wa kupata Megawatt 350 na Kinyerezi III megawatt 350.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hizi pesa in total ambazo tungeweza kupeleka na tukapata umeme mwingi kweli kweli na wa haraka, kwa sababu umeme wa Stiegler’s Gorge ni mpaka 2027. Tunaweza tukapata umeme na wa haraka na wa bei nafuu, tumezichukua tunakwenda kuzi- dump sehemu ambazo hatuwezi kuzipata matokeo leo na tunakwenda kuharibu mazingira kweli kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, LNG.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)