Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia taarifa hizi za Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita sana kwenye Kamati ya Nishati na Madini lakini nataka nizungumzie sana kuhusiana na sekta ya madini. Kila mmoja wetu anajua kabisa kwamba sekta ya madini ni eneo muhimu sana na rasilimali kubwa sana katika Taifa hili. Tulitegemea kabisa katika Serikali hii Awamu ya Tano tulitegemea labda ingeweza kuchangia fedha nyingi sana katika pato la Taifa. Ukweli tu ni kwamba mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa bado uko chini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukijaribu kuangalia katika kipindi cha mwaka 2017/2018 tumeona sekta ya madini imechangia asilimia 4.8 lakini mwaka 2015 sekta ya madini ilichangia karibuni asilimia 5.8. Kwa hiyo, inaonyesha ni jinsi gani ambavyo sekta ya madini sasa hivi inazidi kushuka na haiwezi kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sababu nyingi za msingi zinazosababisha sekta ya madini iendelee kushuka. Tusitegemee miujiza kama sekta ya madini inaweza ikafikisha asilimia 10 kama ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano inavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017/2018, Serikali iliweza kutenga fedha za maendeleo na tukazipitisha ndani ya Bunge hili shilingi bilioni 20 lakini zilizokwenda kufanya kazi kwenye miradi walipeleka Sh.1,183,000,000, tusitegemee miujiza hapo. Mwaka 2018/2019 fedha za maendeleo zilitengwa Sh.19,621,000,000 na fedha ambazo zimekwenda sasa hivi kutekeleza miradi ya maendeleo kwa muda wa miezi sita ni Sh.100,000,000 peke yake, hapa tunategemea nini? Kama tuna dhamira ya kweli ya kuinua sekta ya madini katika Taifa hili miezi sita sekta ya madini imeweza kupata Sh.100,000,000 kati ya Sh.19,621,000,000, hapa tunategemea kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tusitegemee miujiza katika kuinua sekta ya madini na tusitegemee kabisa kama sekta hii ina uwezo wa kuchangia asilimia 10 ambayo mnazidi kuzungumza ndani ya Bunge hili. Hili jambo haliwezekani kwa sababu mnatenga fedha, tunafanya maigizo ndani ya Bunge halafu hampeleki fedha kwenda kutekeleza miradi hii. Kwa hiyo, tunategemea kwamba tutaendelea kushuka mwaka hadi mwaka kwa sababu hatuoni ni namna gani Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba sekta ya madini inakwenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo lingine, kuna taasisi inaitwa TEITI ambayo inasimamia uwazi na uwajibikaji katika sekta ya madini. Mwaka 2017/2018 taasisi hii iliweza kufanya ukaguzi wa taasisi mbalimbali kwenye sekta ya madini na baadaye ikatoa majibu. Kati ya taasisi 1,230 walikwenda kukagua taasisi 55 ambazo walikuta kuna upotevu wa fedha karibuni shilingi bilioni 30. Taasisi hii ilishindwa kukagua taasisi zote kwa sababu ilikosa fedha za kutendea kazi katika kipindi chote hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema hivi, kama hawawezi kutoa fedha kwenye maeneo muhimu kama eneo hili la TEITI tafsiri yake ni kwamba kuna ufisadi na kitu kinafichwa ndani yake ili tusiweze kutambua. Tunahitaji mashirika haya yote yaweze kukaguliwa katika kipindi kinachohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo lingine, uko mradi wa Tanzanite One pale Mererani. Ule mradi tulipata taarifa kwamba tayari Serikali inataka kubadilisha mkataba, iko kwenye mazungumzo na kampuni ambayo ni wabia na Serikali. Kilichotokea huwezi kuamini sasa ni mwaka wa tatu bado mazungumzo yanaendelea na pia Wizara ya Madini haina taarifa mazungumzo yale yamefikia wapi. Tunasikia tu kwamba Mheshimiwa Kabudi bado anafanya mazungumzo wakati miaka mitatu tunapoteza fedha na kodi. Ni mazungumzo gani ya miaka mitatu hayo? (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Frank Mwakajoka, kuna taarifa, Mheshimiwa Musukuma.

T A A R I F A

MHE. FRANK MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimesema siwezi kumjibu muhuni huyo namuacha tu.

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, usimuite Mbunge mwenzio muhuni, futa hilo neno halafu uendelee kuchangia.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nalifuta neno hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa nafikiria kwamba Serikali itafanya majadiliano kwa haraka ili kuhakikisha kwamba Mradi huu wa Tanzanite unainufaisha nchi lakini pia wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi katika mradi huu waweze kupata haki zao. Cha kushangaza ni kwamba mradi huu mpaka sasa umesimama sasa ni miaka mitatu, tunasikia tu Kabudi, Kabudi, Kabudi yuko kwenye mikataba, hivi Kabudi ndiyo Serikali? Tunataka kujua mikataba hii itatoa majibu lini na wananchi waweze …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, ni Mheshimiwa Profesa Kabudi.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Profesa Kabudi. (Makofi)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wanavyosikiliza tunavyozungumza Profesa Kabudi wanashangaa sana kwa sababu walikuwa na matarajio makubwa kwamba akipewa nafasi hii angeweza kuisaidia nchi sasa tunaona hali ni mbaya zaidi.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Frank, kuna taarifa nyingine, Mheshimiwa Kakunda.

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, akumbuke kwamba kwanza sisi huku tulikataa. Huku si tulisema hapanaaa, ndicho tulichokisema, huko wakasema ndiyo. Pamoja na hayo, Waziri wa Madini hajui majadiliano yanaendaje anayejua ni Kabudi, hivi kweli kuna usalama namna hii? Sisi kwenye Kamati yetu tunakutana na Mheshimiwa Waziri na tukisoma taarifa yake hapa inaeleza kabisa tumemuuliza kwenye kikao anasema hajui wanaendelea na mazungumzo, sasa sisi tunakuwa na wasiwasi. Kama kweli Serikali hii na viongozi ambao mmepewa madaraka mtakuwa hamna uchungu na maisha ya Watanzania na uchumi wa Taifa hili miaka mitatu mazungumzo yanafanyika ya kampuni moja tu na huyo mtu ni mbia, Profesa Kabudi inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunachotaka kusema ni kwamba lazima mjadala huu uishe mapema na Serikali ianze kupata fedha. Pia tunataka tujue wafanyakazi wa Tanzanite One ambao ni zaidi ya 400 hali zao zikoje na Serikali imejipanga namna gani namna ya kuwalipa wananchi wale kwa sababu wanadai madai yao kwenye mgodi ule. Sasa hivi hawana kazi, familia zinakufa, watoto wanakufa, wameshindwa kupeleka watoto shuleni mnasema mko kwenye majadiliano. Yaani mnajadili fedha kwa taratibu namna hiyo, uchumi mnaweza mkajadili kwa utaratibu namna hiyo? Kama ni hivyo Mheshimiwa Profesa Kabudi atakuwa ameshindwa na amefeli kwenye mjadala huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo lingine la mapunjo ya wafanyakazi kwenye Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira ambao jumla yao ni 800 ni miaka mingi imepita hawajalipwa. Mwaka 2015, Serikali imefanya majadiliano na kuhakiki madeni imekuta wanadai karibuni Sh.1,800,000,000, wafanyakazi wale wamefanya kazi miaka mingi lakini Serikali mpaka leo haijawalipa na hakuna mpango wowote wa kuwalipa kwa sababu hata bajeti ya mwaka jana hakukuwa na fedha zozote zilizotengwa kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi hawa. Tunaomba Waziri anavyokuja hapa aeleze ni lini wafanyakazi wa Mgodi wa Kiwira watalipwa fedha zao ili waweze kufuta jasho kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa miaka mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo lingine la makinikia. Watanzania bado wanajiuliza sana makontena 277 ambayo yalikuwa yamekamatwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam na wakasema yale makinikia yatakwenda kuuzwa na wakiyauza inawezekana kila mmoja Tanzania akapata Noah. Watanzania wamesubiri Noah hawajaziona. Mpaka sasa hivi Watanzania wamesubiri Noah hazionekani. Juzi watu wameanza kupunguza wanasema kama Serikali imeshindwa kuwapa Noah basi hata Balimi tatu tatu wataridhika. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya majadiliano yote ni Mheshimiwa Profesa Kabudi anaendesha majadiliano ya namna hii. Kwa hiyo, tunaona ni jinsi gani ambavyo Mheshimiwa Profesa Kabudi alivyoshindwa kabisa kuweka vizuri mambo haya na zile kontena sijui kama bado ziko bandarini au zimeshatambaa na maji, hatujui. Tunaomba kujua pia Waziri akifika hapa atueleze haya makontena yako wapi na ni lini tutapata Noah moja moja au Balimi tatu, ijulikane hiyo. Kwa hiyo, hakuna namna ni lazima tujue ni mali ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna fedha walisema wale Mabeberu wanaleta mpaka leo hizo fedha kishika uchumba hakionekani. Jamani hii nchi kweli kila siku tutakuwa tunadanganywa? Ndugu yangu Mheshimiwa Musukuma siku moja alichachamaa kwenye kikao baada ya kuona haoni Noah wala Balimi hazionekani lakini akawa hana namna yoyote. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)