Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Nianze kwa kutoa masikitiko yangu makubwa; kwanza nitoe pole nyingi sana kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa mauaji ya kikatili ya watoto ambayo yametokea. Kihistoria kabisa kwa Mkoa wa Njombe, Mkoa wa Njombe unajulikana ni mkoa wa amani na kwa miaka mingi hatujawahi kusikia vitu kama hivyo. Kwa kweli naomba sana, kutokana na kauli ya Mheshimiwa Waziri, kwamba wamejipanga vizuri kuweza kukomesha jambo hili. Naomba nitoe wito kwa wananchi watoe ushirikiano wa kutosha, kufikia watu wote ambao walikuwa na mipango ya kutaka kuchafua Mkoa wetu wa Njombe, mkoa ambao ni wa amani, ambapo tunawakaribisha wawekezaji waje kuendeleza mkoa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa ya Kamati ya Ulinzi, Mambo ya nje na Usalama; niseme tu naiunga mkono kwa sababu mimi ni mjumbe pia na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, hasa wa Mambo ya Ndani kwa namna alivyotoka kwenye uninja na kwenda kuwa kamanda. Waziri Kangi Lugola, anafanya kazi nzuri na Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri na vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Tuviunge mkono, tuweze kushirikiana nao ili kusudi wafanye kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwa upande wa Nishati, niipongeze sana taarifa ya Kamati. Katika ukurasa wa 11 wamezungumzia maoni ya aina tatu; kuna suala la upelekaji wa fedha za mradi, kuna suala la vijiji vinavyorukwa na tatu kuna suala la kufungwa mashine umba zile transformer ambazo hazikidhi viwango. Kwa kweli Waziri wa Nishati na Naibu wake wanafanya kazi nzuri sana na pia ni wasikivu. Hata hivyo, nataka kusema pamoja na hiyo Wabunge tunapotoa ushauri tunataka wafanye vizuri zaidi ili ikifika mwaka 2020 basi tuwe na vijiji hivi vilivyolengwa kupatiwa umeme viwe vimepata; maana ukikuta mpinzani anakusifia, basi wala ujue kabisa huyu anakukebehi, lakini ukikuta, wa CCM anakusifia basi ana maana kweli umefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana, katika changamoto ambazo zimeelezwa na Kamati, kitu kikubwa watumishi wa REA wanapokwenda vijijini, hawapiti kwa viongozi wa vijiji. Kwa hiyo unakuta wanaleta orodha ya vijiji lakini unakuta vijiji vinaandikwa ni vijiji lakini halisi ni vitongoji. Sasa vitu kama hivi ni kwa sababu hawafiki pale; halafu pili wananchi wanashindwa kujua taarifa ya ratiba ya mradi. Kwa mfano, ukichukulia Wilaya ya Wanging’ombe; nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri amefika, ameona kabisa kasi ya utekelezaji wa mradi ule si nzuri. Tuna miaka miwili lakini ni vijiji saba tu na vitongoji ndivyo vimewashwa umeme, kati ya vijiji 38 vilivyolengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kushauri kwamba zile changamoto ambazo zinafanya utekelezaji uwe hauendani na kasi Wizara izichukue na kuzifanyia kazi na pia hii changamoto ya vijiji na vitongoji kuwa kuchanganywa ni kwa sababu tu hawaendi kwa viongozi wa vijiji, basi naomba jambo hili lirekebishwe ili kusudi tutakapokuja kwenye REA phase III, awamu ya pili, turekebishe yale maeneo ambayo yamerukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika REA Phase III unakuta vijiji vile ambavyo vilikuwa na umeme tangu awamu ya kwanza hawajanufaika na hii ya kulipa Sh.27,000. Kwa hiyo ili wanufaike na Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi naomba kwamba katika mzunguko wa pili hata vile vijiji ambavyo vilikuwa vimepata umeme kidogo, basi nao waingizwe kwenye mradi wa REA ili nao wanufaike na hii tozo ya Sh.27,000; kwa sababu hayo ndiyo niliyoona kuwa ni malalamiko ya wananchi wengi kule vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nikubaliane na hoja za Kamati. (Makofi)