Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ilala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. MUSSA A. ZUNGU - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru lakini niwashukuru Wabunge wote na Mawaziri wa Kamati yetu ambao wamefanya kazi ambayo ilikuwa mimi ndiyo niifanye. Niwashukuru kwa majibu mazuri, sahihi na wamechukua muda mzuri kunipunguzia kazi yangu mimi hapa leo kwa mujibu wa kanuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza machache tu na la kwanza ni la kesi kuchelewa mambo ambayo hayakuzungumzwa humu ndani. Hivi karibuni Waheshimiwa wote mmeona kuwa Mheshimiwa Rais amechagua Majaji wapya wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ili ku- speed up kesi za watuhumiwa mbalimbali. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua yake hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tulishauri kwenye Kamati Waziri aanze sasa kutumia Mobile Court ambayo leo imezinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais. Mahakama hii itasaidia kwa haraka sana kupunguza msongamano wa mahabusu wenye kesi zile ndogo ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwa vile Waziri wa Mambo ya Nje hakuwepo ni suala nililozungumza sana kuhusu gharama za kodi za nyumba ambazo Serikali inagharamia sasa hivi. Nimezungumza kwenye speech yangu kwa takribani miaka kumi sasa tunatumia zaidi ya shilingi bilioni 216 kulipia kodi za mapango. Serikali sasa iingie kwenye utaratibu wa mortgage financing, utarabu ambao utapunguza gharama kubwa sana ya ujenzi kwani badala ya pesa kwenda huko zitafanya kazi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo ni jengo letu la Msumbiji. Sasa hivi tuna ghorofa tisa pale Msumbiji, tuna majengo New York na maeneo mengine ambayo ni mali ya Serikali ya Tanzania. Maeneo haya sasa yamesababisha hata maduhuli kuwa mengi kutokana na kodi ambayo tunaikusanya katika majengo hayo na katika nchi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo machache, niwashukuru Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge na wewe pamoja na Sekretarieti ambayo imesaidia Kamati yetu kutekeleza kazi kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako sasa lipokee taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na likubali maoni na mapendekezo yote ya Kamati kama yalivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.