Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie japo machache kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati hii, pia Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii. Nimpongeze Mheshimiwa Mwenyekiti wangu kwa uwasilisho wake mzuri na pia kuipokea hii taarifa kwamba ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utaanza na shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kwa kazi nzuri anayoifanya ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Ndani ya miaka mitatu ameweza kufanya mambo ya ajabu mengi sana, sina sababu ya kuyataja, lakini miongoni mwa miradi hiyo ambayo anaifanya na sisi kama Kamati tumeona ina mafanikio ni suala la afya. Suala hili lilikuwa nyuma sana lakini Awamu ya Tano imepeleka pesa kwenye Wizara ya Afya au TAMISEMI kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali za Mikoa, Vituo vya Afya, pia Hospitali za Wilaya. Mpaka sasa kitu ambacho tumethibitisha Hospitali za Wilaya 67 na Vituo vya Afya 350 vimeshapelekewa pesa. Kwa hiyo, hayo ni mafaniko makubwa sana ambayo tumeyaona baada ya ziara zetu. Si hilo tu bali kuna ongezeko kubwa la madawa, Mheshimiwa Rais wetu ameweza kuongeza bajeti ya madawa na mafanikio yake yanaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata upande wa elimu, kwa ziara tulizotembelea sekta ya elimu kwa kweli kazi kubwa imefanyika. Nimpongeze sana Mheshimiwa Jafo amesimamia miradi yote pamoja na Naibu Mawaziri wake wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Spika, mambo haya yanaleta heshima kwa Serikali yetu, upo upungufu mdogo unaohitaji maboresho. Tuiombe Serikali itusaidie kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bajeti iongezeke TASAF, Awamu ya III. Fedha inayotolewa na Serikali ni kiasi kidogo sana, wafadhili ndiyo wanaochangia kwa kiasi kikubwa, iwapo wale wafadhili watajiondoa ina maana TASAF itakufa. Kazi wanayofanya TASAF Awamu ya III ni nzuri sana kama itaendelezwa kwa kupatiwa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni MKURABITA. Kwenye ziara za Mikoa yote tuliyokwenda MKURABITA imefanya kazi nzuri sana lakini wanachopungukiwa ni fedha kwani inayopelekwa ni kidogo sana. Kama MKURABITA itapewa fedha ya kutosha katika bajeti ina maana kazi itakayofanyika itawafafikia wananchi wote kwa sababu sasa hivi tayari wananchi wameshaelewa maana ya hatimiliki za kimila na kazi inafanyika vizuri, hata kwako Kongwa tuliwahi kupita na kuhakikisha kwamba Wagogo wote sasa wameshaelewa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, suala ligine ni TARURA. TARURA inafanya kazi nzuri sana kwenye maeneo yote ya Halmashauri lakini tatizo ni fedha, mahitaji ni mengi lakini fedha haitoshi. Kazi ya TARURA ni kufungua barabara za Wilaya, Vijiji na Mikoa hatimaye kuwa pamoja lakini hakuna fedha za kutosha.
Mheshimiwa Spika, niipongeze sana TAKUKURU kwa kazi nzuri inayoifanya. Sasa hivi heshima imerudi Wizara ya Afya, elimu na maofisini hakuna rushwa imepungua. Watu wanachukua rushwa lakini kwa uwoga, rushwa imepungua. Tatizo lao ni fedha ndogo wanayopewa, kwa hiyo, hawawezi kufika maeneo mengi kadri inavyotakiwa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kulichangia, Mjumbe mwenzangu wa Kamati aliyemaliza kuzungumza sasa hivi amesema kuhusu asilimia kumi ya Halmashauri. Kazi kubwa imefanyika katika Awamu ya Tano kuhusiana na asilimia hii kumi. Kwa nini nasema hivyo? Sisi wenyewe Wabunge humu ndani ni Wajumbe wa Halmashauri zetu, hizi bajeti zinapita kwetu. Sasa kama zinapita kwetu kwa nini tusizuie bajeti zao wakati wa Mabaraza ya kupitisha bajeti ya kila mwaka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutailaumu Serikali kwamba asilimia kumi watendaji wanachukua si kweli kabisa, udhaifu upo lakini na sisi kama Wabunge tunachangia kwa sababu ni Wajumbe wa Mabaraza, hususani wanawake wenzangu, Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum ni Wajumbe wa Mabaraza tupiganie tuhakikishe hii haki ambayo ni wanawake, vijana na walemavu bajeti zisipite pamoja na Wabunge wa Majimbo mtusaidie ninyi ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha. Kama ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha kwa nini msitambue kwamba asilimia kumi ni muhimu sana kwa maendeleo ya wanawake, vijana na walemavu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais…
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, taarifa huku.
SPIKA: Naomba tuvumiliane tu aongee, maana hata wanaotoa taarifa siwaoni.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, kushoto kwako.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuamua kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali. Naomba kweli kabisa Waheshimiwa Wabunge tupambane kwani asilimia kubwa ni wanawake na ndiyo wanaopambana Mheshimiwa Rais ametuokoa. Kwa hiyo, niombe Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wawatambue wajasiriamali kwa sababu kutokutoa vitambulisho hivyo ni kumvunja moyo Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, niombe Wabunge tuchangie jinsi gani ya kusimamia kuhakikisha wajasiriamali wanapata huduma kama ilivyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda unaniruhusu niombe, nimeona Serikali sasa hivi ina mabadiliko ya kuondoa Idara zingine TAMISEMI, kwa mfano, Serikali sasa hivi imeondoa masuala ya maji TAMISEMI, inategemea pia kuondoa Idara ya Kilimo, kwa nini nasema kilimo ibaki TAMISEMI? Wananchi wote wako TAMISEMI na TAMISEMI ni kwenye grass root, sasa unapomwondoa huyo Mkuu wa Idara aende Wizarani watu ambao anatakiwa kuwaongoza, kwa mfano Mkuu wa Mkoa wangu alitoa agizo kwamba Wakuu wote wa Idara wa Ugani hakuna kwenda likizo mwezi Novemba kwa sababu ya mvua na kilimo, alisema wote watakaokwenda atawasukuma ndani.
Mheshimiwa Spika, kitu ambacho ningeomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana, malizia hiyo sentensi.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hotuba ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, yote yaliyoandikwa na maoni yao yachukuliwe. Ahsante. (Makofi)