Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye mada iliyoko Mezani. Kwanza naomba nizipongeze sana Kamati zote tatu, wamefanya kazi nzuri sana na kimsingi nakubaliana sana na mapendekezo ambayo wameyaweka. Kwa upande mwingine pia naomba niishukuru sana Serikali, nayo kwa upande wake imefanya kazi kubwa, imetimiza wajibu. Kwa mfano, katika Sekta ya Maendeleo ya Huduma za Jamii na Elimu, yako mambo mengi mazuri ambayo yemefanyika.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwa mfano kwa upande wa Afya jinsi ambavyo Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga Vituo vya Afya kwenye kila Kituo cha Afya ambacho kimependekezwa kwenye Halmashauri, vile vile kuna ujenzi wa Hospitali za Wilaya na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kwa ujumla nakubaliana na mapendekezo yalitolewa. Naomba tu niongezee kidogo kwenye maeneo ambayo nadhani ni muhimu Kamati hizi zingeweza kuyatazama na kuyawekea mkazo. Nilidhani ikiwezekana nimwombe sana Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii anisaidie katika ku-wind up, kuboresha azimio mojawapo linalohusu upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa sana kama ambavyo nimesema awali, lakini bado kuna maeneo ambayo tunahitaji kuongeza juhudi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya na elimu kwa mfano, tumefanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi waweze kujenga shule; na hapa nitazungumzia hasa Jimbo langu la Msalala kama mfano mmojawapo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 wakati tunafanya kampeni kwa kuzingatia Ilani yetu ya CCM, tuliwaambia wananchi kwamba tutajenga Zahanati kila kijiji na tutajenga Kituo cha Afya kila Kata na vilevile tutajenga shule kwenye maeneo yote ambayo hayakuwa na shule. Tuliwaambia wananchi kwamba mambo haya hatutayafanya sisi kama Serika peke yake na wao wananchi watashiriki; na tuliwaeleza kwamba wanapaswa kuinua maboma na Serikali itawashika mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wameitikia sana. Nilimsikia rafiki yangu Mheshimiwa Mwijage muda fulani anazungumza kwamba sisi kama Wabunge tende tukawahamasishe wananchi wetu kupiga propaganda ili waweze kuanzisha miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba kazi hiyo nimeshaianza. Hivi tunavyozungumza, tuna maboma 131 kwenye Jimbo la Msalala ambayo wananchi wameshaweka nguvu zao pale, mengine yana miaka mitatu, mengine yana mwaka mmoja na mengine yana miaka mingi kidogo. Tuna maboma zaidi ya 62 ya vyumba vya madarasa. Leo hii tunawahamasisha wananchi sasa waanze kuyajenga wenyewe hadi kuyakamilisha wakati walishakayakamilisha imebaki Serikali kuleta fedha za ukamilishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna maboma 40 ya Zahanati na katika mpango ule tulishawahamasisha wananchi wakanza kujenga Vituo vya Afya kwenye maeneo matatu. Kwa hiyo, kuna majengo makubwa matatu ambayo yanatosha OPD pamoja na vyumba vingine ikiwemo theater kwenye Kata tatu. Kwa hiyo, kwa ujumla tuna maboma ambayo thamani yake iliyobaki inayotakiwa kuyakamilisha ni shilingi bilioni 4,268.

Mheshimiwa Spika, wananchi wameshaweka nguvu zao pale na thamani ya fedha au nguvu ambazo wananchi wameweka pale ni zaidi ya shilingi bilioni 1,623. Kuna hatari kwamba maboma haya sasa yanaeleekea kuanza kubomoka na Serikali haijaleta fedha za ukamilishaji wakati matarajio ya wananchi yalikuwa kwamba wakishakuwa wamemaliza maboma haya, basi Serikali italeta fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo na Ustawi wa Jamii kama ilivyowasilisha Kamati kwenye lile azimio linalohusu kupeleka fedha, basi angalau kama unaona siyo lazima sana kwenye maeneo mengine, basi angalau lile azimio tuliboreshe tuseme kwamba Serikali ipeleke fedha za ukamilishaji wa maboma Jimbo la Msalala…

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Na Bukene.

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Na Bukene kama unaona kwingine haipendezi sana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hili suala la kupeleka fedha za miradi lifanyiwe haraka na liwe sehemu ya maazimio ambayo tungependa kuyaweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nizungumzie kwa upande wa elimu na tatizo la ajira. Katika maeneo ambayo tuna matatizo makubwa sana ni suala zima la ajira. Alisema Mheshimiwa Nkamia asubuhi na Waheshimiwa Wabunge wengine, suala la ajira kwa sasa ni janga. Tusipochukua hatua, ninaamini kabisa kwamba linaweza likaleta madhara makubwa kwenye jamii yetu na hata utangamano na ustahimilivu na usalama wa nchi.

Mheshimiwa Spika, ninavyoona tatizo liko katika mfumo wa elimu yetu. Tuna wahitimu wengi ambao wana- graduate kwa sasa hivi, zaidi ya graduates 600,000 kwenda juu, kuanzia level ya Form VI wale wanaokosa nafasi kuendelea na masomo hadi Vyuo Vikuu; wote hawa wanahitaji ajira kwenye sekta iliyo rasmi. Kwa mfumo huu tunaokwenda nao, naamini kabisa hatuwezi kutatua tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, tujaribu kujiuliza na nilitaka niwape changamoto Mawaziri wangu wawili hawa; Mheshimiwa Jenista Mhagama na hata Mheshimiwa Waziri wa Elimu, hivi katika intervention za Serikali zinazofanywa, hizi za kusaidia kukuza ajira, jiulize tu, tunaposema asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwenda kwa akina mama, vijana na walemavu, hivi kuna watu wangapi wenye elimu kuanzia Form VI wanaotumia fursa hiyo? Ukipiga hesabu ni kama hawapo. Wanaokwenda kwenye hizo fursa ni Darasa la Saba kwenda chini.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo elimu yote aliyoipata kuanzia Form VI kwenda juu hawaitumii kwenda kujishughulisha kujiajiri, wanawaachia wenzao wa chini zaidi na wao wanasubiri ajira za Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumetoa vitambulisho kwa wafanyabiashara, Mheshimiwa Rais ametoa karibia vitambulisho 100,000 sasa, hivi katika hao wafanyabiashara kuna wangapi ambao wamemaliza Form VI, ukiangalia utakuta ni hakuna. Kwa hiyo, hawa wote kuanzia Form VI kwenda vyuo wote wanasubiri ajira zilizo rasmi.

Mheshimiwa Spika, tuimarishe elimu ya ufundi (polytechnic colleges) ambayo mtu akimaliza pale, tena ikiwezekana hata mkopo tumpatie atoke na cherehani yake, aende ajiajiri, aanze kufanya kazi. Hii ya kumaliza wanagombea boom kule ambalo ndiyo mikopo ya Elimu ya Juu, halafu akimaliza anakaa anaanza kuomba ajira ambazo hazipo, ni tatizo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie mfumo wa elimu ili iweze kuwasaidia vijana wetu waweze kwenda kwenye ajira moja kwa moja badala ya kuwaandaa kuajiriwa kwenye nafasi za white collar jobs ambazo hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kujua kwamba muda unaelekea kwisha naomba nimalizei kusema naipongeza sana Serikali na Kamati zote tatu.

Mheshimiwa Spika, nimalizie sentensi kabla sijafunga kabisa, kuhusu suala la TARURA. Ni kweli, sasa hivi utengenezaji wa barabara za vijijini umepungua kuliko ilivyokuwa ukisimamiwa na Halmashauri. Kuna tatizo. Mojawapo ni fedha zinazopelekwa TARURA hazitoshi. Pia hili suala la ushirikishwaji; Madiwani ambao ndio wanaosimamia Halmashauri, wengi wao hawashiriki wala hawajui mipango ipi ambayo imewekwa na TARURA kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, nilidhani eneo hili ni vizuri likarekebishwa; mpango wa kuwaongezea fedha TARURA ufanyike na namna ya kuwashirikisha Madiwani ifanyike ili tuweze kufanikisha lengo la kuwa na TARURA na kuboresha barabara za vijjini.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja zote tatu. Nashukuru sana kwa nafasi uliyonipatia. (Makofi)