Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia maeneo machache…

SPIKA: Dakika 10.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, dakika 10? Ahsante sana kwa huo muda kwa sababu nilikuwa najaribu kuangalia dakika tano hizi.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kutoa mchango wangu katika sekta hizi tatu. Kwanza kabisa kabisa naomba nianze kuungana na Watanzania wenzangu kutoa pole sana kwa akinamama, akinababa na jamii ya Wananjombe kwa misiba mikubwa iliyotokea ya mauaji ya watoto wetu wasiokuwa na hatia. Natoa pole kwa sababu msiba huu ni mkubwa, ni msiba wa Kitaifa na hapa naomba nitoe ushauri kwamba, Serikali yetu ifanye kila jitihada inayowezekana ili wale waliohusika na mauaji yale waweze kupatikana.

Mheshimiwa Spika, mwaka fulani yalitokea mauaji ya wanawake Mkoa wa Mara, Serikali ilichukua hatua na mauaji yalikomeshwa. Mwaka fulani yalitokea mauaji ya maalbino, Serikali ilichukua hatua na mauaji yalikomeshwa. Hivi karibuni tuliona Rufiji mauaji yalikomeshwa na hivi karibuni tuliona watu wenye ulemavu wakifanyiwa ukatili, walikomeshwa, naomba na kule Njombe Serikali ichukue hatua za haraka, ili mambo haya yaishe.

Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Wajumbe wenzangu wa Kamati hizi mbili, Kamati ya UKIMWI na Kamati ya Huduma za Jamii, lakini pia niungane na wengine wote waliounga mkono hoja. Hapa nami naunga mkono hoja na kwa kuokoa muda naomba niishauri Serikali kwamba, Maoni ya Kamati ya Masuala ya UKIMWI, kama ambavyo tumeleta mapendekezo, yapokelewe na yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, tumezungumzia tozo ya kupata fedha kwa ajili ya kununua dawa za watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kwa ajili ya kufubaza. Tusiendelee kutegemea wafadhili kupitia fedha na maeneo mengine kwa sababu, kuna siku hawa wafadhili watasitisha na litakuwa ni janga kwa Taifa letu. Kwa sababu, tulishaanzisha Mfuko ni vizuri sasa Mfuko huu ukaboreshwa na Serikali ikaandaa utaratibu wa kuleta sheria na tukawa na tozo maalum.

Mheshimiwa Spika, pia, tumependekeza kwenye Kamati yetu ya UKIMWI kwamba, umri wa mtoto anayeweza kwenda kupima kwa hiyari bila kwenda na mzazi ufanyiwe marekebisho kulingana na wakati tulionao wa sasa. Badala ya kuwa miaka 18 mpaka kuendelea ianzie miaka 15 waweze kupima kwa sababu, taarifa ambazo Wizara imetuletea kupitia Kamati ya UKIMWI hali ni mbaya, watoto wetu kuanzia miaka 10 mpaka 15 mpaka 25 kila wananchi wanaopimwa asilimia 40 ni watoto wadogo. Kwa hiyo, naungana kabisa na Kamati kwamba, sasa Muswada uletwe hapa Bungeni tufanye marekebisho, sheria tuitunge ili sasa hata hawa watoto wadogo waweze kwenda kupima kwa hiyari kwa ajili ya kuwanusuru.

Mheshimiwa Spika, tumeleta mapendekezo, tunaishauri Serikali ilete sheria ya kuhakikisha suala la bima kwa wote linatungiwa sheria. Tumekwenda Rwanda, Kamati baadhi ya wajumbe walikwenda, wametuletea mrejesho; wenzetu katika suala la bima wako vizuri na sisi Tanzania tuige mfano wake, kuna wengine wamekwenda Ghana wametuletea mfano. Nami naomba nitoe mapendekezo hapa na niungane na Kamati kwamba, sheria ije sasa, ili wananchi wote wapate bima kwa ajili ya manufaa yetu na wewe mwenyewe juzi ulikuwa ukisisitiza, naomba niunge mkono hapo iletwe kwa ajili yetu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie sasa suala zima la ujenzi wa hospitali za rufaa, hospitali za mikoa, hospitali za wilaya na hata vituo vya afya. Hapa naomba nilete pongezi na shukrani nyingi sana kutoka kwa wananchi wa Mkoa wa Mara. Mkoa wa Mara tulikuwa tunajenga hospitali ya kwanza ya Mwalimu Nyerere Memorial Centre, hospitali hiyo ilijengwa kwa muda mrefu na ilikuwa haikamiliki, lakini kwa uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, sasa hivi hospitali inakwenda mbio na Serikali inatuletea fedha.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Waziri Mheshimiwa Ummy ameshatembea, ameshaona jitihada zinazoendelea na ameshapewa gharama na ili jengo liweze kuanza zinahitajika kiasi gani. Naomba nitoe ombi tena kwa niaba ya wananchi wa Mara, hebu Mheshimiwa Ummy au Serikali ituletee hizi fedha ili jengo liweze kukamilika hasa hili la mama na mtoto ili kituo kile cha Mwalimu Nyerere Memorial Centre kiweze kufanya kazi na kuwahudumia Wananchi wa mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Spika, tunaleta pongezi zetu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi tumepata fedha bilioni 1.0 kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Rorya; bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga Musoma Vijijini; bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga Tarime na maeneo mengine; lakini tumepata 400 kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Serengeti; na 400 kwa ajili ya kujenga hospitali Butiama. Ombi langu, hii Hospitali ya Butiama na hapa naomba wanisikilize vizuri, najua Mheshimiwa Waziri atakapokuwa aki-wind up atachangia; Hospitali ya Butiama naomba tuipe upekee wa utofauti kabisa. Hospitali ya Butiama ni hospitali ya kihistoria, ni hospitali ambayo Baba wa Taifa alikuwa anatibiwa hapo, ni hospitali ambayo Mama Maria Nyerere akiwa Kijijini Butiama akiugua ghafla ndiko anakotibiwa na ni hospitali ambayo kwa wilaya nzima ya Butiama ndio wilaya inayohudumua wananchi wote zaidi ya watu 200,000.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Butiama ina kituo kimoja tu cha afya kwa sababu, Mwalimu Nyerere alipokuwa Rais aliangalia Watanzania wote, aliwahudumia bila ubaguzi, hakujiangalia nyumbani kwake. Naomba katika misingi ya kumuenzi Baba wa Taifa hebu tuiboreshe Hospitali ya Butiama kwa sababu hata wageni wanaokuja kutembelea Kaburi la Baba wa Taifa wanaougua wanakwenda pale, lakini hata familia ya Baba wa Taifa yenyewe akina Makongoro na wenzake na hata Madaraka anayetulindia Makumbusho ya Baba wa Taifa akiumwa anatibiwa pale Hospitali ile ya Butiama haina hadhi ya kuendana na kazi aliyoifanya Baba wa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Serengeti wamechangishana fedha wamefika zaidi ya milioni 300 wakaanza kujenga hospitali, kama sio ya kwanza Kitaifa inaweza ikawa ya pili kwa mfano, ni hospitali kubwa na ni nzuri wananchi wamejitolea. Tunashukuru Serikali imetuletea shilingi milioni 400, naomba na hii hospitali hebu waiongezee na yenyewe ifike bilioni 1.5 kama ambavyo wamefanya kwingine.

Mheshimiwa Spika, nimesema mimi hapa leo ni shukrani maana maoni mengi kwenye Kamati yametolewa. Naomba nilete shukrani za wananchi wa Mkoa wa Mara, wametujengea na kuviboresha vituo vya afya 10, shilingi zaidi ya bilioni 6.0, tumepata katika mkoa wetu. Naleta shukrani za wananchi wa Mkoa wa Mara na hata kura zikipigwa leo Chama cha Mapinduzi na Rais wetu watapata ushindi wa asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, ombi letu na hapa nataka niongelee kwa Tanzania nzima ikiwemo Kongwa, Mbeya na maeneo mengine; suala la wafanyakazi au watumishi katika hivi vituo vya afya ambavyo vimeboreshwa; naomba Serikali tupeleke watumishi, kama hatukupeleka watumishi ni sawasawa na kufanya kazi bure. Hivi karibuni nimetembelea vituo vyote ambavyo vimepelekewa fedha, nimeenda kuona mafanikio na kusikiliza changamoto, nimejionea mwenyewe Kituo cha Nata nakitolea mfano, Daktari yuko mmoja peke yake wakati chumba cha theatre wanatakiwa wawepo Madaktari wanne; yeye ndio anashika mkasi, yeye ndiye anaandaa gloves, yeye ndiye anafanya kila kitu, yeye ndiye apige kaputi, Daktari mmoja!

Mheshimiwa Spika, aliniletea kilio akasema mama mnatuua, tumeboresha hospitali, tumejenga theatre, tumeweka vifaa tena vya kisasa, vingine tumekuta vimesimama havifanyi kazi kwa sababu, hata wa kuviwasha na kuendesha hiyo mitambo hawapo. Nimekuta baadhi ya mashine hata kujua pass word ikoje mtaalam anasema hajui. Kwa hiyo, nashauri kama alivyosema Waziri wa Utumishi asubuhi kwamba, kipaumbele ni kupeleka watumishi katika zahanati mpya na katika vituo vya afya. Hapa nashauri hivi vituo vya afya 350 walivyoviboresha Serikali yetu ya CCM, naomba na vyenyewe vipewe umuhimu wa kwanza kwa sababu, bila ya kufanya hivyo itakuwa ni sawasawa na kazi bure, wagonjwa watakwenda pale hakuna huduma, hakuna wataalam na kazi ambayo tumeifanya itaishia kwa kweli, kuwa sio nzuri.

Mheshimiwa Spika, naomba niongezee kwamba, kama ambavyo amesema mchangiaji Mheshimiwa Maige na Mkoa wa Mara pia ni miongoni mwa watu ambao wanafanya kazi sana. Sisi Mkoa wa Mara tunajenga majengo ya Serikali na huduma za jamii kwa kitu kinaitwa lisagha, yaani watu wa rika, umri wa kwangu tunapewa boma letu, umri wa mwingine wanapewa boma lao tunajenga kuanzia msingi mpaka lenta bila kutegemea msaada wa Serikali. Tumejenga maboma ya zahanati zaidi ya 100, tumejenga vituo vya afya zaidi ya 100, tumejenga sekondari zaidi ya 100… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, tunaomba hivi Serikali ikijaribu kutenga fedha kukamilisha haya majengo, ili kuunga mkono nguvu za wananchi ambao sasahivi wameishiwa, naleta ombi maalum; kengele ya kwanza hiyo…

SPIKA: Tayari muda wako umekwisha.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Hivi tayari?

WABUNGE FULANI: Ndiyo.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana na naomba kuwasilisha. (Makofi)