Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote waliowasilisha taarifa zao na hasa Mheshimiwa Jasson Rweikiza ambaye ni Mwenyekiti wangu wa Kamati. Pia niipongeze Serikali kwa ujumla wake kwa kazi kubwa ambayo imefanyika kwa kipindi hiki cha miaka mitatu. Najua kuna changamoto ambazo sisi inabidi tuzifanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, kwanza tulikuwa na upungufu mkubwa sana wa madarasa na vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali lakini Serikali kwa kujua hilo ilianza kupambana na changamoto hiyo. Changamoto kubwa ilikuwa ni majengo na sehemu kubwa majengo yamejengwa. Kwa hiyo, changamoto kubwa sasa ni upungufu wa wauguzi, walimu na kadhalika ambayo inaweza kutibika.
Mheshimiwa Spika, kwa huwa Serikali imesomesha kwenye vyuo vyetu vijana wengi kabisa na hawana shughuli na Serikali imewakopesha, kitu ambacho naishauri Serikali wapo ambao wapo tayari kujitolea, kwa nini Serikali isikubali vijana wale badala ya kukaa wakajitolea wakafanya kazi zile kupunguza upungufu wa wauguzi na walimu kwa miaka angalau miwili na shule zetu zote zingekuwa hamna upungufu sijui kuna kigugumizi gani? Pia wale ambao watafanya vizuri maana wanadaiwa na Serikali baadhi ya fedha zikapunguzwa kwenye mikopo yao ili waweze kufanya kazi kwa kujitolea na wengi wapo tayari. Naomba hilo Serikali ilichukue na ilifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni hili la TARURA. Tulipitisha wenyewe hapa Bungeni Muswada wa TARURA lakini leo tumeshaanza kugeuka kwa kuanza kusema Meneja wale waende wakaripoti kwenye Baraza la Madiwani. Nafikiri kikubwa tungeangalia changamoto lakini kazi inayofanyika ni kubwa, kama sisi Wabunge tutapitisha fedha kwa maana ya mgao, maana mgao uliopo sasa hivi ni 70 kwa 30, tukawaongozea TARURA kelele zitakuwa hazipo. Kama ilivyo TANROADS wanafanya kazi vizuri, ukiwaingiza kwa Madiwani au Wabunge inakuwa ni mfumo wa kisiasa, kila mmoja atataka barabara yake ijengwe hata kama ni kilomita 2 lakini unapowaachia huru, wanatoa tu taarifa kazi zitakwenda. Nafikiri tujikite zaidi kuona tunawaongezea ngapi ili kazi ifanyike kwa sababu sisi wenyewe tulipitisha kwa kuangalia changamoto nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, asubuhi niliuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na alinijibu vizuri sana. Nafikiri kuna haja Waziri wa Fedha mkawaongezea fedha wenzetu wa Wizara ya Michezo ili suala hili lipewe umuhimu. Kama nilivyosema asubuhi, sidhani hata baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa wana ulewa mzuri, michezo ya AFCON ni michezo ya Afrika nzima under 17 inafanyika Tanzania na hakuna matangazo ya kutosha ambayo yameshatolewa kuwapa watu uelewa waweze kuchangia pato la nchi ili fedha hizo siende kufanya kazi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumenunua ndege ndiyo ulikuwa wakati wa kutangaza wa ndege zile hata ikiwezekana Meneja wa Shirika la Ndege akasema kwamba kwa wale wataokwenda kuangalia michezo kutoka Iringa na sehemu nyingine watapata punguzo wakati wa mechi wakikata tiketi mapema, fedha zile zingeongezwa kwenye uchumi wetu. Rais wa FIFA atakuwepo hapa na kundi kubwa kabisa la watu kutoka nje ilikuwa ndiyo wakati mzuri wa kutangaza utalii wa nchi yetu na wao wakitoka hapa wangeweza kuwa Mabalozi wazuri wakatutangazia nchi yetu huko nje ili tuingize pato kwenye utalii. Nafikiri hili ni suala na Mheshimiwa Waziri wa Michezo na Waziri wa Maliasili kuangalia wanafanyaje ili kuhakikisha tunatangaza vizuri mashindano haya na kutuingizia pato kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa ni suala ambalo pia limezungumzwa na watu wengi. Mwaka jana tulikuwa na tatizo kubwa sana la mlundikano wa wanafunzi waliofaulu, ikabidi tuanze mchakamchaka kwa ajili ya kujenga madarasa, mwaka huu tatizo liko palepale. Nafikiri kuna tatizo labda kwenye takwimu au la wataalam wengine. Kwa sababu hivi leo watakaomaliza mwaka huu mwishoni idadi tunayo, kwa nini tunangoja kuja kuanza kufanya mchakamchaka wakati tunaweza tukatatua jambo hilo mapema? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kwamba kama ni kwenye bajeti liingizwe ama lishughulikiwe kwa njia yoyote lakini mapema siyo kama sasa hivi kuna wanafunzi ambao hawatakwenda shule wanasubiri mpaka mwezi wa pili, tatu, madarasa yajengwe ndipo waende, nafikiri hapo kuna tatizo. Niombe Mawaziri wafanye kazi kwa nguvu zote na kushirikiana badala ya kufanya kazi ya zimamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nisingependa kusema mambo mengi, niunge mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)