Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nianze kuwashukuru Wajumbe na Wenyeviti wa Kamati kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya ikiwemo kuleta mapendekezo mazuri katika kuboresha utendaji wa sekta ya afya na maendeleo ya jamiii. Kipekee niipongeze sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya Masuala ya UKIMWI. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme katika hatua hii tumepokea maoni na ushauri wa Kamati. Nataka kukiri mimi na Mheshimiwa Naibu Waziri tumekuwa tukipata ushirikiano mzuri sana, maoni mazuri sana kutoka kwa Kamati na ndiyo maana sekta ya afya inafanya vizuri sana nchini Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nitoe ufafanuzi katika maeneo makubwa manne. Eneo la kwanza ni kuhusu sekta ya maendeleo ya jamii, Kamati imeshauri kwamba katika kuimarisha uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali tuanzishe kanzi data ya NGOs. Tumeanzisha na tumeanza zoezi hili mwezi wa Juni, 2018 na tunataraji kwamba tutazindua katika Bunge lijalo la Aprili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la kuanzisha Kitengo cha Udhibiti Ubora wa NGO, tayari tunacho Kitengo cha Uratibu na Ufuatiliaji wa NGO lakini nataka kukiri tunahitaji kuongeza nguvu ili sasa kazi ya kufuatilia hela za NGO, kazi gani wamefanya na wanafanya tuweze kuzifahamu vizuri. Mwezi wa Oktoba, 2018 tumepitisha kanuni mpya kwa ajili ya kutaka uwazi na uwajibikaji wa mashirika ya NGO juu ya hela ambazo wanazipata. Kama tunavyofahamu NGO nyingi zinaomba fedha kwa kutumia majina ya Watanzania maskini. Kwa hiyo, tumepitisha kanuni tunataka watoe taarifa kila baada ya miezi sita hela hizo zimepatikana kiasi gani na zinatumika wapi na katika masuala mangapi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa upande wa sekta ya afya, tumepokea ushauri kuhusu kukamilisha mchakato wa kuanzisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Mimi na Naibu Waziri tumefarijika sana kwamba suala hili linaungwa mkono na Wabunge wote. Nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha Muswada, tunategemea utatupa nafasi Bunge la Bajeti, najua hatujadili sheria lakini tulete sheria hii muhimu kwa sababu Serikali ya Magufuli imefanya kazi kubwa katika kuboresha upatikanaji wa dawa, kujenga hospitali, kuboresha vituo vya afya pamoja na vifaa tiba. Kwa hiyo, ni kweli wananchi hawatapata huduma bora za afya kama hawana uwezo wa kifedha. Bima ya Afya itakuwa ndiyo suluhisho la kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la vifurushi tunalikamilisha, tumeanza na vifurushi mbalimbali, tunataka wananchi wajipimie wenyewe huduma za afya ambazo wanataka kuzipata. Kama unataka ufike mpaka Muhimbili utajipimia kufika Muhimbili na kama unataka ufike Dodoma Regional General Hospital utafika. Kwa hiyo, tunakamilisha na tumeanza kwa mfano kifurushi kwa ajili ya wakulima (Ushirika Afya) kwa ajili ya wakulima wa korosho na kwa Sh. 76,800 mkulima wa korosho anapata uhakika wa matibabu mwaka mzima. Tumeanza pia bima ya afya kwa ajili ya watoto (Toto Afya Card) kwa Sh.50,400. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ester Mmasi suala la Bima ya Afya ya Wanafunzi ni Sh.50,400 tu. Kwa hiyo, vyuo binafsi wanafanya wizi kama wanachukua Sh.100,000 ya Bima ya Afya ya Wanafunzi. Tutaweka utaratibu wanafunzi walipe moja kwa moja NHIF badala ya kulipa kupitia vyuo kwa sababu bima ni Sh.50,400. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo tumelipokea ni kwamba tufanye tathmini ya ustahamilivu ya Mfuko wa Bima ya Afya. Tumefanya tathmini kwa takwimu za mwaka 2016, nataka niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge tunaweza kutoa huduma za afya hadi mwaka 2029. Ila pale ambapo tutaongeza idadi kubwa ya wananchi kujiunga na bima ya afya, naamini mfuko utakuwa una ustahamilivu mzuri na hivyo kutoa huduma mbalimbali za afya.
Mheshimiwa Spika, suala la UKIMWI, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Ikupa amejibu baadhi ya hoja lakini nataka kukazia hoja moja ya Mheshimiwa Jacqueline Msongozi. Ile hoja ni muhimu sana kwa sababu tafiti zinaonyesha kwamba huduma za tohara kwa wanaume inakinga maambukizi ya VVU kwa hadi asilimia 60. Kwa hiyo, tusidharau wanaume kufanya tohara kwa wale ambao hawajafanyiwa tohara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa mikoa ya kipaumbele ya Iringa, Njombe, Tabora, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera, Singida, Kigoma, Mara na Morogoro huduma za tohara kinga ni bure.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, nakuongezea dakika mbili itaje mikoa taratibu, umeenda haraka hatujaisikia hii mikoa. (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, huduma za tohara ni bure katika Mikoa ya kipaumbele ambayo ni 17 na Mikoa hii inajumuisha Iringa, Njombe, Tabora, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera, Singida, Kigoma, Mara na Morogoro; Dodoma haipo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka tu kusisitiza kwamba ni tafiti za kitaalam zimeonyesha kwamba tohara kwa wanaume inaweza kuzuia maambukizi ya VVU hadi kwa asilimia 60. Kwa hiyo, tulitilie maanani suala hili.
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Msongozi ameongelea suala la kuambukiza saratani ya mlango wa kizazi. Saratani ya mlango wa kizazi inaambukizwa kutoka kwenye kirusi cha mwanaume kinaitwa Human Papilloma. Kwa hiyo, pale ambapo mtu ana mkono wa sweta inamuweka pia katika hali ya kuweza kuchochea mazingira ya kirusi kile cha Human Papilloma ambacho ndiyo kinasababisha saratani ya mlango wa kizazi. Kwa hiyo, nitoe rai kwa wanaume ambao hawajapata tohara waone suala hili kwamba ni la kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi tumeenda mbali, tumeanzisha Mpango wa Tohara kwa Watoto Wachanga kati ya siku 1 hadi siku 60. Lengo letu sasa ni kuhakikisha kwamba suala la tohara kinga linakuwa endelevu na tumeanza kutekeleza katika mikoa sita ya Njombe, Iringa, Tabora, Mbeya, Songwe na Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la tiba, Kamati imetushauri kutoa ruzuku kwa hospitali ikiwemo Jakaya Kikwete, MOI, MNH na Hospitali za Rufaa za Mikoa. Niseme sisi kama Serikali kwa mfano mwaka jana katika Hospitali ya Muhimbili tumepeleka shilingi bilioni 4.5 na mwaka huu tuna shilingi bilioni 5 lakini kwa JKCI tumeshawapatia shilingi bilioni 1.2.
Mheshimiwa Spika, katika hili, nisema tu kwamba sisi kama sekta ya afya tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuwezesha kufanya vizuri katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa. Nimemshangaa sana Mheshimiwa Sugu anaposema rufaa zimepungua kwa sababu watu wanaogopa kuandika rufaa.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe takwimu chache. Mwaka 2014, Hospitali ya Jakaya Kikwete ilikuwa inafanya upasuaji wa kifua wagonjwa 127. Kutokana na kazi nzuri ya Magufuli mwaka 2017 wamefanyia wagonjwa 275. Sasa tunataka tuwapeleke wapi kama huduma zinapatikana ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini suala la upasuaji wa moyo bila kupasua kifua mwaka 2018 uwezo wa Jakaya Kikwete ulikuwa ni wagonjwa 100 tu, mwaka 2017 tumefanyia wagonjwa 770. Sasa tunapeleka nje kwa sababu gani? Huduma zimeboreka na Mheshimiwa Sugu anatakiwa ku- appreciate kwamba tunafanya renal transplant na tunafanya upandikizaji wa vifaa vya kusikia kwa watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nitoe mfano wa mwisho, hospitali yetu ya Ocean Road, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais tumepata shilingi bilioni 9.4, tumenunua mitambo ya kisasa ya kutoa matibabu ya mionzi inaitwa LINAC. Kwa kipindi cha miezi mitatu, tumewafanyia wagonjwa 109 na kati ya hao wagonjwa 70 wote tungewapeleka India kwa kila mmoja shilingi milioni 50. Kwa hiyo, wenzetu mnatakiwa kukubali kwamba huduma za matibabu ya kibingwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli zimeboreka sana na ndiyo maana safari za India zimepungua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la fedha, Kamati inasema hatujapokea fedha za miradi ya maendeleo, nadhani tu ni takwimu lakini sisi hadi Desemba tumeshapokea shilingi bilioni 81 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo fedha za dawa na ndiyo maana hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutoa huduma za afya ngazi ya msingi na rufaa ni zaidi ya asilimia 90. Pia tumepokea fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali za Rufaa za Mikoa katika Mikoa mipya ya Simiyu, Katavi, Njombe, Songwe na Geita. Kwa hiyo, tumepata hela za miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalize kwa suala la viwanda vya dawa au uzalishaji wa ndani wa dawa. Suala hili ni la kipaumbele kwa Serikali na kwa Wizara ya Afya. Nafurahi kusema sasa hivi viwanda vinne vinajengwa na sekta binafsi. Tunacho Kiwanda cha Dawa Bahari, Kairuki Pharmaceutical naye anajenga kiwanda lakini pia Reginald Mengi naye anajenga kiwanda cha dawa na sasa hivi tumepata mwekezaji mwingine ambaye ataanza kujenga kiwanda cha dawa. Kwa hiyo, tunaamini kabla ya mwaka 2020 tutakuwa angalau tuna viwanda vinne vipya ambavyo vinazalisha dawa ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni la watumishi lakini naamini kaka yangu Mheshimiwa Mkuchika atalijibu lakini nakubaliana na maoni na ushauri wa Kamati kwamba sasa tuwekeze kuhakikisha vituo vya afya viliboreshwa vinafanya kazi na siyo kuwa na majengo ambayo yanaweza yakamalizwa kwa sababu ya popo. Kwa hiyo, kwenye hili, kipaumbele chetu sisi tunataka kutoka kwenye bora huduma twende kwenye ubora wa huduma. Kwa hiyo, suala la huduma bora za afya ndiyo kitakuwa kipaumbele chetu kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, niseme tena naishukuru na kuipongeza Kamati na kwa kweli Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ina watu vichwa sana na tunawashukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)