Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Kamati yangu ya Katiba na Sheria. Naipongeza Kamati yangu ya Katiba na Sheria kwa ushauri wao mzuri walioutoa, naiomba Serikali ipokee mapendekezo yao na iyafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi katika Kamati yangu ya Katiba na Sheria tumeshauri bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria inapotolewa katika Bunge itolewe kwa muda muafaka ili iweze kufanya kazi maana vijijini huko mahakama za wilaya ni chache na mahakama za mwanzo nyingi zimechoka kwa kuwa ni za muda mrefu, zina nyufa. Tunaomba wawe wanapewa hilo fungu ili waweze kujenga mahakama maana wananchi wanatembea mwendo mrefu kwenda kwenye kesi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeshauri Majaji, Mahakimu wa ngazi za chini waweze kupewa mafunzo, waweze kufanya kazi zao kwa weledi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho tumeshauri, Mahakama Kuu hawana mashine maalum, watu wakienda pale wanakwenda kwa kupapaswa wakiwa wanaingia ndani, hiyo na yenyewe ni hatari, ni vizuri na wenyewe wawekewe mashine maalum wasiwe wanaingia hivihivi maana kwenye viwanja vya ndege, sehemu zingine hata na makanisani mahali pengine wana mashine za kuangalia wale watu wanaoingia mle ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho tumeshauri kwenye magereza, kuna wafungwa ambao wamekaa muda mrefu ambao wana wenzi wao, kama ni wanaume wameacha wake zao nje, kama ni wanawake wameacha waume zao nje, ni haki yao kutimiza tendo la ndoa. Tumeshauri mkakati ufanyike watengenezewe sehemu wawe wanakutana maana mtu kukaa miaka kama sita, saba mbegu za uzazi zinaweza zikaharibika, lakini kama wakitengenezewa sehemu ni vizuri na wenyewe wakaweza kukutana, tendo la ndoa ni haki yao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho tumeshauri katika Kamati yangu, upande wa mahakama, Majaji na Mawakili wanapaswa wapewe weledi wa hali ya juu sana, wapewe semina ili waweze kufanya kazi zao vizuri, pale Mawakili wanapotetea wateja wao waweze kutetea kwa umahiri sana, bila kuwapa kozi za maana wanaweza wakafanya mambo ndivyo sivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu ni hayo machache, nashukuru. (Makofi)