Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nitambue michango yote iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Idadi ya Wabunge waliochangia ni 18 na kwa nafuu ya muda sitawataja majina. Pia nitambue michango mizuri iliyotolewa na Waheshimiwa Mawaziri wote na katika baadhi ya hoja ambazo tayari Waheshimiwa Mawaziri wameshazijibu, sitakwenda huko tena kwa sababu ninaamini kama ni ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge basi utakuwa umechukuliwa na Waheshimiwa Mawaziri na pengine wataufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo limezungumzwa kwa kina pengine napenda kulisisitiza sana ni kuomba Kiti chako kwamba hizi semina kwa Waheshimiwa Wabunge ni muhimu sana ili kila mmoja wetu aweze kutambua mipaka ya kuchangia hususan inapohusu mihimili hii mitatu inayounda Serikali. Kwa sababu ipo michango mingi ambayo imezungumzia kuhusu Mahakama na inatambulika kabisa kwamba Mahakimu au Majaji wana kinga na malalamiko yoyote dhidi ya Hakimu/Jaji mamlaka yake ya juu ni kukatia rufaa kutokana na maamuzi ambayo yametolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge walitambue hilo na pengine tutumie fursa ya uelewa wetu kuwaambia wananchi wetu umuhimu wa kuheshimu mihimili hii yote mitatu lakini hususan kabisa mhimili wa Mahakama ambao ndiyo umepewa mamlaka yote ya utoaji haki kwa mujibu wa Ibara ya 107 ya Katiba. Kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge watambue kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Jaji Mkuu lakini pia watendaji wa Mahakama wamefanya kazi nzuri sana kuboresha mifumo ya utoaji haki hapa nchini. Natambua hilo kwa kuwa mimi ni miongoni mwa vijana ambao tumekulia kule, najua hali ilivyokuwa huko nyuma na hali ilivyo sasa kwa kweli Mahakama imefanya kazi kubwa sana, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo yamezungumzwa kuhusu mamlaka ya utoaji haki na masuala ya dhamana. Niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwamba ni vyema wakajikita kabisa katika kusoma vizuri Ibara ya 26 ya Katiba ambayo inamtaka kila Mtanzania kutii Katiba na sheria zetu za nchi ambazo zinatuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema tukaitambua mipaka ya utoaji haki na ni vizuri tukajikita kutafuta wataalam watusaidie katika maeneo ambapo tunaamini kabisa hatukutendewa haki. Ukisoma vizuri Katiba na sheria za nchi yetu zimetoa maelekezo mazuri kabisa ni namna gani ambapo mtu anapaswa kukata rufaa lakini ni namna gani ambapo Mahakama inapaswa kutoa dhamana na masuala mengine yote ambayo yamezungumzwa kwa kina hapa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama nilivyosema Wabunge 18 ndiyo waliozungumza mambo mbalimbali na kwa kuwa tayari mengine yameshajibiwa na Waheshimiwa Mawaziri na tunaamini mengine yamechukuliwa vizuri na Waheshimiwa Mawaziri, naomba nijikite tu kwenye baadhi ya masuala machache ya muhimu ili kuongeza msisitizo katika maeneo hayo. Kwa ujumla utendaji wa Wizara na taasisi zinazosimamiwa na Kamati yangu ya Katiba na Sheria ni wa kuridhisha sana ukiacha baadhi ya changamoto ambazo tayari Serikali imeshaanza kuzitafutia ufumbuzi. Hivyo, Kamati inaipongeza na kuishukuru Serikali kwa ushauri wao mzuri uliofanikisha utekelezaji wa shughuli za Kamati. Maeneo ambayo Kamati imebaini kuwa na changamoto, imetoa mapendekezo yake kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi kama yanavyoainishwa katika Sehemu ya Tatu ya taarifa ya Kamati kuanzia ukurasa wa 39 mpaka 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya maeneo hayo yaliyobainishwa na kutolewa mapendekezo ni pamoja na Serikali iongeze usimamizi na uratibu wa masuala ya watu wenye ulemavu nchini na itangaze rasmi Wajumbe wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu. Jambo hili tayari Naibu Waziri wa Vijana ameshalizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo lingine mwingine ni Serikali ianzishe pia Mfuko wa Masuala ya Wenye Ulemavu na kuanzisha fungu dogo la kibajeti kwa kulitengea fedha kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020. Ushauri huu pia umezingatia maoni ya wadau wengi wa kundi hili muhimu katika jamii ambao wamechangia yetu kupitia vikao mbalimbali vya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo lingine ni Serikali pia iongeze usimamizi wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa lengo la kuimarisha SACCOS zilizopo na kudhibiti SACCOS hewa za vijana ambazo hukopeshwa na kupokea fedha za Serikali. Pia Ofisi ya Waziri Mkuu iwe na ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambao ndiyo wenye dhamana ya Halmashauri kwa lengo la kuhakikisha kila Halmashauri inawajibika na kuratibu fedha zinazotolewa na Mfuko wa Vijana na kusimamia marejesho yake kwa wakati. Maoni na mapendekezo ya Kamati ni kama ambavyo imefafanuliwa katika taarifa yangu ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza kwa kina shughuli zilizotekelezwa na Kamati kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2018 hadi Januari, 2019, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kukubali maoni na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii ili yawe maazimio ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.