Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hutuba ya Waziri Mkuu kwanza ni kupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyotusomea kitabu chake chenye mafungu kama tisa hivi. La pili, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa ziara anazifanya kusimamia Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi, Makamu wa Rais mama Samia anavyozunguka kuweka mambo sawa huko na Mheshimiwa Majaliwa na Mawaziri na wengine wote nawapongeza sana kwa mambo wanayoyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika sijui ni tano au ni kumi?

NAIBU SPIKA: dakika ni kumi.

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. La kwanza nitaanzia kwenye eneo la madini na naomba ku-declare interest kuwa mimi ni mchimbaji mdogo. Kwanza tumpongeze Mheshimiwa Rais na Makamu wake, Waziri wa Madini na Waziri aliyehamia kwenye uwekezaji kwa mkutano tuliofanya pale Dar es Salaam siku mbili, tunaipongeza sana Serikali kwa kuweza kuwasikiliza wadau wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la madini tuliahidi mambo mengi. Serikali yetu cha Chama cha Mapinduzi ni sikivu ilitoa kodi kwenye 27 tukaenda royalty sita kuongeza moja. Si jambo dogo ni jambo kubwa sana. Hapa sasa nataka kuiomba Wizara ya Madini na wachimbaji wadogo wadogo, tulikubali mbele ya Rais kwamba tutalipa kodi, tulikubali mbele ya Rais kwamba hatutatorosha madini, tulikubali mbele ya Rais kwamba lazima tukusanye kodi ili nchi iweze kuendeshwa. Niiombe Wizara ya Madini na Tume waache kuchekacheka na watu wanaoharibu dhamira nzuri ya wachimbaji wadogo. Tumekubaliana mtu akikamatwa na madini mahakamani tena uhujumu uchumi basi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo ndani ya Wizara hao wachimbaji wadogo wanasimamiwa na wafanyakazi wa Wizara ya Madini, hawa wafanyakazi wa madini ambao sio waadilifu waanze kuwachuja wasituletee matatizo. Sisi tumeshakubali kuchimba, tumeshakubali kulipa kodi, lakini unajikuta watu wanaunga, wanafanya jambo baya sana hili. Nimpongeze Waziri wa Madini juzi nilimuona Chunya, wale watu wameondoshwa, waondoshwe wengi, wapo watu wengi sana wanaoharibu kwenye sekta hii. Sekta hii ni nzuri, mwaka kesho wakati tunasomewa hotuba, sekta ya madini itakuwa imepanda mara dufu. Kwa hiyo msingi sisi tunachimba tunalipa kodi, lakini Wizara na Tume wasimamie watu wao. Kwa sababu kule ndani ndio watopandisha leseni anampa huyu na huyu, anageuza huku na huku, lakini kama hatuwezi kuipa umuhimu kama Rais alivyoipa umuhimu kodi hii ukusanyaji wake utakuwa shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale pale kwenye madini walikamatwa watu kwenye makinikia wakazuia michanga yao, sheria imekuja, kuna wenzetu ambao hawana matatizo ya kulipa kodi na kusafirisha michanga yao, kwa nini hawawapi ruhusa Serikali ikapata fedha yake? Wanakosa gani hawa? Mtu yupo tayari kulipa kodi, mtu hana tatizo ni mchimbaji, kuna watu wamewekeza katika nchi hii, kwa nini hawawaruhusu wakafuata taratibu kodi ile ikakusanywa? Nawaomba sana watu wa madini, hili eneo ni nyeti, lakini kuna watu wanafilisika, watu hawahudumiwi. Kwa hiyo, naomba kosa la mtoto mmoja lisimzuie mtoto mwingine kupata haki yake ya maisha. Kwa hiyo nawaomba sana watu madini, waende waangalie eneo hilo, wale watu ambao hawana shida wawaruhusu wasafirishe, walipe kodi, kwa nini wanarundika, wameweka mitaji, hali si nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliza niende katika suala la ardhi hapo hapo kwenye madini. Kwenye eneo la ardhi kumepimwa kuna madini lakini pale juu kuna mtu analima mahindi, siku ukienda kuchimba anakwambia sitaki, khaaa wewe unalima mahindi mimi nachimba dhahabu tofauti iko wapi? Niwaombe watu wa ardhi waende kule wawaelimishe hawa watu ambao wapo kwenye maeneo ya madini, nikishapewa ardhini kwa maana nimepewa leseni, mimi nitakuwa chini wewe utakuwa juu, msingi tujadiliane ili watu wote wawe wa moja. Hata hivyo, ukienda eneo la ardhini unakuta nao wameweka masharti yao, imeenda imerudi, wanachelewesha kuchangamsha uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maliasili na Utalii, mtu kapewa leseni ya madini pale vijimiti, kipori anasema ni hifadhi, hifadhi ipi? Wakati mali kubwa ya kuleta ushuru ipo wanaikatalia na hawaifanyii chochote? Hapo tusaidie Watanzania, wachimbaji wadogo wakusanye kodi hii msiweke vikwazo wakati sehemu hii haitumiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili naenda Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mwaka jana nilipambana na wao lakini mwaka huu nawapongeza sana, hongera sana kwa kazi wanayoifanya hasa hasa kwenye eneo la mifugo. Kwenye eneo la mifugo kulikuwa na shida sana sana tu, wafugaji wanatangatanga, wanaenda huku na huku wanafanya hivi, lakini naipongeza Wizara, juzi nimeona wamesaini mkataba wa kujenga viwanda vya nyama vingi na juzi nimeona wametangaza kule kwenye ranch, yale maeneo ya watu kupewa ranch, suala hili ni la muhimu na la
kupongeza, wapo Watanzania walikuwa wanakaa na vitalu hivi bila kulipa chachote Serikali haipati kodi. Sasa leo kwa sababu wamekuja na nia njema waisimamie, vitalu vipatikane, watu wachangie pato la Taifa, maziwa yapatikane, viwanda wanavyovijenga zaidi ya vitano, vipate malighafi. Katika hilo nampongeza Mheshimiwa Mpina, leo nampongeza na Mheshimiwa Ulega, nawapongeza sana wameenda vizuri, waweke utaratibu ili angalau makusanyo ya nchi yapatikane kila eneo yanapotakiwa kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lile la ranch kuna mwenzangu jana alisema Mheshimiwa Kamala sijui kama yupo, kwamba kuna wananchi walikuwepo, tunapotaka kuweka utaratibu watu wamekaa na ranchi miaka zaidi ya 15 Serikali haipati hata senti tano, acheni vitalu vigawiwe, Serikali ikusanye kodi, watu wafuge kwa uzuri ili maendeleo ya nchi yapatikane, sio cha mjomba, cha shangazi, mimi nasema wakaze kamba, tunataka kufuga, tunataka kufua, tunataka Tanzania uchumi uchangamke.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoka mifugo niende hapa kwenye Mambo ya Ndani, neno hili nalisema kwa mara ya nne, si zuri sana, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Mambo ya Ndani wafanyakazi wa nje waliopo humu nchini, vibali hivi kuna watu wana haki ya kupewa, kuna watu hawana haki ya kupewa. Wapo watu humu nikisema tunanuniana, lakini mimi ni mzee, sina shida, ukininunia mimi naenda kulala, kwa hiyo haisaidii kitu chochote. Yaani mtu ana miaka 20, leo hii wanafanya mpango kumpa uraia, Wizara ya Kazi na Mambo ya Ndani nasema suala hili tutaliweka hadharani hapa, mimi nakusanya vielelezo tu, mtu muda wake umekwisha, anatakiwa kutoka nchini, amekaa zaidi ya miaka 20, anafanya siasa, si Mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia kwa Mheshimiwa Jenista na Wizara ya Mambo ya Ndani nasema neno hili kwa mara ya mwisho, waende kwa huyu mtu, wampe vibali vya uraia, tutakutana hapa, sisi wote ni Watanzania. Kuna Mzee Raza jana kasema kuna kiwanda, kina watu zaidi ya 300, wanawaombea Engineers wawili wanakataa, watu 300 wote, hawatapata kazi? Huyu mtu anaitwa Vedigree anawalipa shilingi ngapi? Niko tayari kuweka vielelezo mezani nasema kwa mara ya tano leo ndani ya Bunge hili. Sasa wamwandalie uraia halafu tuone uraia huo ataupataje katika nchi hii, sababu si lazima watangaze. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa kengele ya pili.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulembo naomba ukae. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.

T A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliweke vizuri jambo hili kwa sababu nisipoliweka vizuri sidhani kama maneno yaliyotumiwa na Mheshimiwa Mbunge kama yapo sawasawa sana kwamba tunapewa shilingi ngapi kwa ajili ya suala hili. Hapana, si sawa, sidhani kama ana hakika kama kuna fedha yoyote imeingia kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba tu nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge Ofisi yangu jambo hili imeshalishughulikia na yeye anajua. Kwa hiyo masuala mengine ya mtu kuendelea kuomba kitu chochote, atafuata utaratibu na majibu ya kiutaratibu yatatolewa wakati utakapofika. Tukifika mahali Ofisi imeshachukua hatua na imeendelea kulishughulikia jambo lenyewe, halafu Mheshimiwa Mbunge anajenga hisia kwamba labda Ofisi ya Waziri Mkuu ina jambo fulani, nadhani si sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge na vinginevyo nitumie ile kanuni ya kumwomba aondoe hili jambo katika taarifa yake aliyoisema leo, ama tutumie kanuni nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimimu sana Mheshimiwa Bulembo na naomba nimpe hiyo taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulembo, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa watu wenye busara suala la hela nalifuta lakini mazingira ya rushwa siwezi kufuta.